GEORGE; NATAMANI NIFE LAKINI BADO SIJAITWA BABA 01

 
Wakati nakutana naye alikua katoka kuachana na mwanaume wake, alikua na ujauzito wa miezi miwili tu. Alinielezea matatizo yake na kweli niliamua kumchukua, tukawa tunaishi naye kama mke na mume. Nilimhudumia kwa kila kitu, akanitambulisha kwao, kwakua yule mwanaume alikua kamkataa na kumuambia atoe mimba yake basi nilimchukulia mwanae kama mwanangu.

Baada ya kujifungua nilienda kwao kumtolea mahari, nikamtafutia mtaji kwa kukopa kazini na kumfungulia Duka zuri tu la vyombo vya nyumbani. Mwanzo mambo yalikua mazuri tu, lakini baadaye alibadilika, akawa hataki kusikia kuhusu kufunga ndoa na kila nikimuuliza mambo ya dukani akawa anakasirika tu.

Mwanzo nilikua namfuata dukani, tunafunga na kurudi wote, lakini akanipiga marufuku kufika dukani kwa madai kuwa namharibia kwa wateja wake, hali hiyo ilinikesa sana na kila nilipokua nikienda basi aliishia kunitukana, kunifanyia vituko na kuongea maneno mabaya mabaya.

Alikua ananinunia bila sababu huku akilalamika kuwa namdahlilisha kwakua tu naenda dukani kwake bila idhini yake, aliniambia namnyanyasa kwakua nimempa mtaji hivyo akasema kama siwezi kuacha kwenda dukani basi ni bora kuachana. Kwakua nilikua nampenda sikuona sababu ya kuachana naye. Niliacha kwenda dukani, pesa nikawa siioni, mwanzo tulikua tunakaa na kupanga vitu lakini akawa kila kitu anafanya mwenyewe.

Nyumbani mimi ndiyo nilikua nahudumia kila kitu, akawa hajali tena kuhusu familia, kumbuka ana mtoto ambaye nilimchukulia kama mtoto wetu lakini alikua hata kumnunulia nguo hawezi. Mimi nilichukua mkopo hivyo nikawa nakatwa mshaara kila mwezi na Biashara anasimamia yeye, malengo ilikua ni Biashara ikianza kutengeneza faida basi anisadie majukumu ya nyumbani lakini haikua hivyo.

Duka lilizidi kupanuka, nilikua naona kabisa anauza vitu, yaani naona kama linakua kubwa lakini nikimuuliza kuhusu pesa ananiambia kama vipi tuachane yeye kachoka kuulizwa ulizwa kama mtoto.
“Si ulinipa milioni kumi, basi mimi naweza kukurudishia pesa yako kila mtu ashike njia yake, siwezi kusimamiwa simamiwa kama mtoto!” Aliniambia huku akijifanya kukasirika. Hapo basi ananuna hata mwezi mzima huku akimpigia simu kila mtu kuwa ninamnyanyasa, namsumbua na nataka kumfukuza kwakua tu nilimfungulia duka.

Nilikua nakasirika sana lakini kwakua nilikua nampenda basi nilivumilia. Alikua haachi pesa ya chakula, wakati huo nilishachukua mikopo mpaka napata laki moja na nusu kwa mwezi kwani mahitaji ya nyumbani yalikua makubwa, haachi kitu lakini akirudi anatumia mpaka kugawa kwa marafiki zake na ndugu zake, nikiongea anakua mkali huku akilalamika kuwa siwapendi ndugu zake.

Kwa hela hiyo nililazimika kulipia kodi, kununua chakula, kumnunulia mtoto nguo na kumpa kila kitu lakini bado alikua hanithamini. Hata binti wa kazi aliyekua akikaa na mtoto wake nilikua namlipa mimi nikimuambia anasema yeye hana pesa. Nakumbuka kuna siku alinijibu kwa dharau mpaka nikatamani kumpiga, nilimuambia kuhusu mshara wa binti wa kazi akaniambia.

“Kama unafanya kazi huwezi kupata elfu hamsini ya kumlipa mfanyakazi si bora ubaki nyumbani mimi nitakulipa hiyo hela, Mwanaume unajiita mwanaume halafu unafanya kazi ambayo huwezi kupata elfu hamsini!” Nilikasirika sana bila kudhamiria nikajikuta namtandika makofi, hapo ndipo kila kitu kilibadilika, alienda Polisi na kunichukulia RB.

Nilikuja kukamatwa na nilikaa ndani siku tatu bila dhamana, nilipokuja kufuatilia nikuwa alikua akitembea na mkuu wa kituo, Asikari wa pale ndiyo waliniambia huku wakishangaa kuwa yule mwanamke ni mke wa mtu kwani mbali na kutembea na mkuu wa kituo lakini alikua na wanaume wengi tu anawahcnganya na wengi walikua ni maaskari.

Nilikaa Polisi mapaka Mama yake mzazi alipokuja kuniwekea dhamana, lakini niliporudi nyumbani nilikuta ameondoka na kumuacha mtoto kwa Mama yake huku yeye na hiyo ndiyo sababu Mama yake alikuja kuniwekea dhamana ili tu nityoke na kukaa na mtoto! Alienda kuishi na mwanaume mwingine ambaye alikua ni mume wa mtu. Kwakua mtoto wake alikua kanizoea sana na kila mtu akijua kuwa mimi ndiyo Baba yake nilienda kumchukua na maisha yaliendelea.

Hakukaa sana kwa huyo mwanaume, kama mwezi mmoja hivi alirudi, hakuniambia kama anarudi, hakuomba msamaha nilimkuta tu ndani, baada ya kama siku mbili hivi alianza kuumwa, aliumwa sana nilipompeleka hospitalini ndipo iligundulika kuwa ametoa mimba ambayo nilikua na uhakika kuwa si yangu kwani zaidi ya mwaka alikua hajaniruhusu kuugusa mwili wake.

Nilimhudumia mpaka alipopona, lakini hata hakujali kuniomba msamaha wala kuongea na mimi kwa upole, hapana, alikua na hasira zake, alikua akiongea kana kwamba mimi ndiyo nilimsababishia yeye kuwa vile. Kila siku alikua ni mtu wa kunilalamikia, akiongea na watu anaongea kana kwamba mimi namnyanyasa, nampiga, namtukana lakini tofauti na siku ile nilikua sijawahi kumpiga wala kumtukana pamoja na kunifanyia vituko vingi.

Pamoja na kwamba hakuomba msamaha lakini nilimsamehe, siku moja niliamua kumtoa out nikiamini kuwa labda kuna kitu nilikua nimemkosea ndiyo maana alikua akinifanyia vituko. Nakumbuka nilimpeleka kwenye Baa moja maarufu hivi, nilimuona kama mke wangu hivyo nilitaka kumtoa out nikidhani labda kwakua nimekua bize sana na kazi kuna mambo nakosea.

Mimi nakunywa pombe na mara moja moja nikiwa sijabanwa na majukumu. Tulifika na kukaa, niliagiza nilichokua nikiagiza lakini kama dakika 20 hivi niliona vinywaji vinaanza kumiminika kwenye meza yetu, nilishangaa nikamuuliza mhudumu ni nani kaagiza ndipo yeye alinijibu kwa hasira, yaani aliona kama vile ninamdhalilisha wka kuuliza vile. 
“Kunywa unataka kujua ili iweje? Mtu mwenyewe pesa za mawazo kwani ukinunuliwa kuna shida gani?”  

Nilijisikia vibaya nikawa sina amani, nikawa naangalia angalia kuona ni nani alikua anaagiza, niliona meza ya jamaa mmoja aliyekua anaagiza kwani nilipomgeukia ni kama alikua anaongea na mhudumu na alinichekea kinafiki kama vile ananiambia “Kuywa tu ushalipiwa huku!”

Mhudumu alipokuja tena kutuletea vinuywaji nilimuambia kuwa sitaki.
“Muambie tunashukuru lakini tuko sawa, mrudishie vinjwaji vyake!” Lakini cha ajabu mpenzi wangu alinyanyuka kwa hasira na kuondoka kwa madai kuwa namdhalilisha.
“Unanidhalilisha kwa wanaume zangu wamaana, yaani mijitu mingine haina hata shukurani! Ujinga mtupu!”

Baada ya kama dakika mbili hivi nami nilitoka, kufika nnje sikumkuta, nilijaribu kumpigia simu yake lakini ilikua haipokelewi na mwisho ikazimwa, sikua na namna zadi ya kurudi nyumbani kuona kama ameshafika lakini hakufika. Nikaanza kuhangaika kumtafuta kwa marafiki zake mpaka kumpigia Mama yake ila hakuna aliyemuona. Hakurudi mpaka asubuhi alipokuja na kuniambia kuwa anataka tuachane na kila mtu ashike hamsini zake.

Niliona kama utani ila siku ileile vitu vilikuja kuchukuliwa, akamchukua na mtoto na hapo ndipo nilimuona yule mwanaume wa jana yake aliyekua anatununulia vinywaji alikua alikuja kumchukua na gari. Nilikasirika na kuona kama nimedhalilishwa hivyo sikumuomba msamaha wala kutaka kuongea naye chochote. Aliondoka na mtoto wake, ingawa niliumia sana lakini sikua na namna.

Nilikaa kama wiki mbili hivi nikiamini kuwa atarudi lakini hakurudi, nilifika dukani na kukuta makufuli, kuulizia nikaambiwa kuwa alishachukua kila kitu na hawajui ameenda wapi. Nilienda mpaka nyumbani kwao kujaribu kuongea na Mama yake lakini safari hii ilionekana kama yupo pamoja na mwanae haktaka hata kuongea na mimi!

“Mama Amekasirika, umekuja umetolea Dada mahari lakini hutaki kumuoa, ameona ni bora achukue mahari nyingine.” Aliniambia mdogo wake, mpaka wakati huo nilikua sijajua nimekosea wapi wala nifanye nini, niliumia sana nilipogundua kuwa kuna mwanaume alikua akiishi naye, mbaya zaidi nikuwa, alikua kahamishia duka langu sehemu nyingine na huko ndipo alikua akiishi na huyo mwanaume.

Kilichoniuma zaidi ni mambo aliyokua kaongea kwa ndugu zake, aliwaambia kuwa mimi nilimnyima kufanya kazi, hata duka ambalo nilichukua mkopo kumfungulia alikua kajibana na huyo mwanaume ambaye alienda kuishi naye ndiyo alimuongezea mtaji. Aliwaambia kuwa simpendi mtoto wake, kuwa ile mara ya kwanza tuligombana nikampiga na alinipeleka Polisi kwakua nilimtishia kumuua. Aliwaambia kuwa suala la Ndoa ni kitu ambacho ananiambia kila siku lakini mimi sitaki, hivyo ameamua kuondoka kwani anaona akiishi na mimi basi nisipomuua yeye nitamuua mtoto wake.

Nilijaribu kumtafuta ili angalau aniambie nilikua nimemkosea nini lakini hakunipa jibu, aliniambia tu hanitaki nimuache na maisha yake. Kilikua ni kipindi kugumu sana kwangu, nilikua nampenda yule mwanamke, alikua ni kila kitu changu, kibaya zaidi ni kininyang’anya mtoto na nilipojaribu kumdai alitangaza kwa kila mtu kuwa yule hakua ni mtoto wangu mimi sina uwezo wa kumpa mimba mwanamke na ndiyo sbabau ya kuniacha.

Iliniuma sana kwani ilinidhalilisha sana, nikawa mtu wa kukaa ndani, nikawa mtu wa pombe yaani nakunywa pombe mpaka nasahau nyumbani ni wapi? Mwaka mzima nilikua nasumbuka kumuomba msamaha, nilikua nahangaika kila siku kwenda kwake, ananitukana yeye na mwanaume wake lakini sikujali, nilikua nampenda mpaka ndugu zangu waliingilia kati na kuja kunichukua baada ya kufukuzwa kazi kutokana na pombe na kutokwenda kazini.

Miaka minne niliyoishi naye nilikua sijawahi kumsaliti wala kumfanyia kitu chochote kibaya, nilimuona kama mke wangu ingawa suala la ndoa kila siku alikua akinipiga chenga. Hali yangu ilikua mbaya sana, nilikua sioni sababu ya kuishi hasa alivyotangaza kwa kila mtu kuwa yule mtoto alikua si mtoto wangu na mimi sina nguvu za kiume siwezi kumpa mwanamke ujauzito.

Ingawa nilimpenda sana mtoto wake lakini hata mimi nilikua na hamu sana ya kuwa na mtoto wangu, lakini katika miaka yote hiyo minne alikua hajawahi kubeba ujauzito wangu hivyo yale maneno yaliniumiza na kuna wakati nilijikuta naamini kuwa nina matatizo siwezi kumpa mwanamke ujauzito, ingawa sala la nguvu za kiume nilijua kabisa kuwa ni uongo ila ishu ya mtoto iliniumiza sana.

Nilikaa kwa ndugu zangu kama miezi sita, nikawa vizuri kabisa, kwa bahati nzuri nilipata kazi sehemu nyingine kwenye kampuni moja kubwa na cheo kikubwa kabisa. Maisha yaliendelea, ingawa ilikua ngumu kwangu lakibni nilimsahau kabisa Salma, sikua na mahusiano mengine kwani nilikua siamini tena wanawake.

Pale ofisini nilikua na Dada mmoja ambaye alikua ni rafiki yangu sana, hakua mpenzi wangu lakini tulikua na ukaribu sana na kwa kiasi kikubwa yeye ndiyo alinisaidia kumsahau Salma. Siku moja alikuja ofisini kwangu huku akicheka, hakuonekana kukasirika bali alionekana kama vile haamini.
“Kumbe umeoa ndugu yangu hutuambii?” Aliniuliza, huku akinikabidhi simu yake.
“Mke wako naye mtata, sasa ndiyo vitisho vyote hivyo vya nini?” Aliendelea kuongea, alikua anaongea kama utani, mimi nilishtuka kidogo kwani baada ya kuipokea ile simu moja kwa moja niliona namba ya X wangu, Salma (Sio jina lake halisi).

Ni namba ambayo ilikua haijawahi kutoka kichwani kwangu, nilikua naikumbuka na mara nyingi sana nilikua nikishika simu yangu, naiangalia nasubiria labda atapiga au kutuma meseji ila hakufanya hivyo.
“Achana na mume wangu, humjui nitakufanya kitu kibaya. Kila mwanaume unamchekea tu, unajionana hilo tako lako unafikiri unamtisha nani, Nimeshakuambia George ni wakwangu hawezi kuwa na mwanamke mwingine zaidi yangu!”

MAMBO NI MAPYA KABISA; Unadhani Salma anataka nini? Vipi George atafanya nini? Usijali 

ITAENDELEA…. 

Post a Comment

Previous Post Next Post