NIACHE NILIE -01 😓😓😓

Msimuliaji: Esther

Mpenzi msomaji, kabla sijaanza kusimulia kisa cha kusikitisha kilichotokea katika maisha yangu, napenda kukuambia kwamba dunia ina mambo mengi mabaya na mazuri ambayo nilipokuwa mdogo sikuweza kufikiri kama yapo.

Nasema hivyo kwa sababu nilikuwa nasoma na kusikia habari za watu waliokumbwa na mikasa ya kutisha, lakini sikudhani kama siku moja nami ningepatwa na masaibu hayo.

Kabla sijaanza kusimulia mkasa ulionikuta napenda kukuelezea historia fupi ya maisha yangu kisha uungane nami katika kisa cha kuhuzunisha kilichonikuta.

Kwa jina naitwa Emiliana Ernest. Nilizaliwa mwaka 1990, katika familia yetu, mimi ni mtoto pekee kwa wazazi wangu.

Kwa mujibu wa mama, awali maisha yetu yalikuwa ya amani na upendo kwani baba na mama walikuwa wananipenda na kunilea kwa upendo wa dhati.

Kama inavyofahamika watu hususan wanandoa hawawezi kuishi bila kukutana na vikwazo, mama alisema yeye na baba ambaye sikumfahamu waliingia kwenye mgogoro uliosababisha watengane ambapo kila mmoja alikwenda kuishi kivyake.

Mama yangu aliyekuwa mjasiriamali aliendelea na biashara zake na baba aliyekuwa akifanya kazi ya umakanika aliendelea na kazi yake.

Wakati mama anaendelea na maisha yake, aliolewa na mwanaume mwingine na baba naye alioa. Hivyo kwa upande wa mama nina ndugu wanne.

Kwa baba nina ndugu watatu na mimi ni wanne. Baada ya kutengana kwa wazazi wangu, nilienda kuishi na bibi yangu mzaa mama, Martha Wawaya Chuwa huko Rungwe mkoani Mbeya.

Niliishi na bibi yangu hadi alipoamua kurudi Moshi katika Kijiji cha Uru alikozaliwa, bibi alinipa mapenzi ya hali ya juu.

Waswahili husema ng’ombe wa maskini hazai na akizaa huzaa dume, wakati nikiwa namtegemea bibi kwa kila kitu kwa bahati mbaya bibi aliugua na kufariki dunia.

Kifo cha bibi lilikuwa pigo kubwa sana kwangu kwani alifariki na kuniacha nikiwa binti wa miaka tisa, hakika nilipata pigo ambalo sitalisahau mpaka nitakapoondoka hapa duniani.

Kufuatia kifo cha bibi, sikuwa na jinsi nilikubaliana na hali halisi iliyotokea. Tulimzika bibi yangu. Na tangu hapo maisha yangu yakaanza kuwa magumu. Kwani nilianza kuishi mikononi mwa watu ambao sikuwa nimewazoea.

Baadaye nilienda kuishi kwa babu yangu ambaye ni kaka yake marehemu bibi yangu aliyekuwa akiishi katika Kijiji cha Uru Kitandu. Kutokana kumzoea sana marehemu bibi, ilinichukuwa muda mrefu kuyazoea mazingira mengine.

Hata hivyo, kule nyumbani kwa babu sikupungukiwa kitu chochote, nilikula, kununuliwa nguo na mahitaji mengine na maisha yalikwenda kama kawaida.

Baada ya kukaa kwa babu kwa muda, wazazi wangu walinifuata ambapo tulikaa kikao cha pamoja. Katika kikao hicho babu alikuwa mzungumzaji mkuu.

Nakumbuka babu aliniita na kusema: “Emiliana, hawa ni wazazi wako, huyu ni baba yako na huyu ni mama yako.”

Nilifurahi sana kukutana na wazazi wangu ambao walitengana nikiwa mdogo sana, hata wao walifurahi kuniona.

Babu alipotoa kauli hiyo, aliniambia kwamba kwa kuwa wazazi wangu waliachana nikiwa mdogo sikumfahamu baba yangu ndipo alinitambulisha kwake.

Baada ya kunitambulisha alisema: “Emiliana wazazi wako wamekuja kukuchukua, sasa ni uamuzi wako kuchagua wapi ukaishi, kwa mama au kwa baba yako?”

Kufuatia kauli ya babu, niliduwaa ndipo nilimuuliza babu: “Babu unasema nichague niende nikaishi na mzazi yupi wakati wote ni wazazi wangu?”

Babu alinifahamisha kwamba walikuwa hawaishi pamoja ndiyo maana aliniuliza nichague ningeenda kuishi kwa nani!

Ukweli ni kwamba nilikuwa sijawahi kuishi na mzazi hata mmoja nikiwa nina akili za kikubwa, hivyo sikujua mapenzi ya baba wala ya mama.

Nilimjibu babu kwamba nitaenda, kuishi na baba yangu. Basi babu akampa masharti baba kwamba akitaka kunichukua alete mbuzi mmoja.

Baba alikubali kufanya hivyo, muda wa chakula ulikuwa umefika tukala ndipo baba aliaga kwamba anarudi Arusha alikokuwa akiishi kwa ajili ya kufanya utaratibu wa kurudi tena Moshi akiwa na mbuzi.

Nilimsindikiza baba hadi kituo cha mabasi ambapo tuliagana akaelekea Arusha, kitendo cha kukutana na mzazi wangu huyo ambaye nilikuwa simfahamu kilinipa raha sana!

Baada ya muda si mrefu, baba alikuja kunichukua Moshi ambapo aliongozana na mama mmoja, pia alikuwa na mbuzi aliyeagizwa na babu.

Tulipomaliza kusabahiana, baba alimtambulisha yule mwanamke aliyeongozana naye kwamba ni dada yake aliyeitwa Elizabeth Martini Tairo.

Nilifurahi sana kwani kwa upande wa baba sikumfahamu hata ndugu mmoja, licha ya awali kusalimiana naye, kwa furaha ya kukutana na shangazi yangu nilimsalimia tena.

Baada ya muda baba alimkabidhi babu mbuzi wake ambapo alifurahi sana kisha kwa amani alimruhusu baba kuondoka nami.

Chakula kilipokuwa tayari, tulikula ndipo niliingia chumbani nikafungasha nguo na vitu vingine vilivyonihusu tayari kwa safari ya Arusha.

Muda wa kuondoka ulipowadia, tuliiaga familia ya babu ambapo walitusindikiza hadi kituoni ambapo tulipata usafiri wa kuelekea Moshi mjini, kwa ujumla siku hiyo nilifurahi sana.

Tulipofika Moshi mjini baba aliniita na kuniambia;

“Mwanangu nakupenda sana na si unajua kuwa mimi ni baba yako?” Nikamjibu; “Ndiyo wewe ni baba yangu na pia hata mimi nakupenda sana.”

Akaniambia yeye anakwenda Arusha hivyo nibaki pale Moshi mjini kwa shangazi yangu angekuja kunichukua baada ya siku mbili, sikuwa na kipingamizi nilikubaliana naye.

Licha ya kumjibu hivyo, furaha na amani niliyokuwanayo ilitoweka nikajikuta nabubujikwa machozi.

Baba na shangazi walinisihi ninyamaze lakini niliendelea kulia kisha nilimuuliza baba, mbona wakati ananichukua kwa babu alisema tunakwenda kuishi kwake Arusha iweje aniache Moshi kwa shangazi!



Kufuatia swali langu, hakuwa na jibu zaidi ya kuniambia; “Nenda tu mwanangu kesho kutwa nitakuja kukuchukua.”

Alipotoa kauli hiyo nikanyamaza na kumsindikiza kwenda kupanda basi kisha akaondoka kuelekea Arusha, mimi na shangazi tukarudi nyumbani huku moyoni nikiwa sina raha!

Baada ya kufika nyumbani kwa shangazi aliniambia maneno haya: “Hapa ndiyo umefika, utakaa hapa na kusoma hapa hapa.”

Nilikubali kwani sikuwa na jinsi, hata kama ningekataa ningeenda wapi kwa sababu sikuwa na nauli ya kurudi kijijini kwa babu yangu.

Shangazi alinionyesha chumba ambacho ningekitumia kulala, baada ya kuingia nilianza kulia na kujiuliza kwa nini baba alinidanganya kwamba tunaenda kuishi kwake Arusha kisha kuniacha dada yake.

Ingawa bado nilikuwa mdogo, jambo hilo lilinihuzunisha sana lakini sikuwa na la kufanya zaidi ya kuanza maisha mapya pale kwa shangazi ambaye siku hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kumuona.

Shangazi yangu alikuwa ni mwalimu wa shule ya msingi iitwayo Mwereni iliyopo Moshi hivyo alienda kuniandikisha darasa la kwanza. Nilianza masomo rasmi nikiwa na umri wa miaka tisa.

Shauku ya kuwa na baba ilinitoka, sikumuwaza tena badala yake nilimzoea sana shangazi ambaye nilimuona kama mama yangu mzazi.

Awali shangazi alinipenda sana lakini nikiwa darasa la nne upendo ulitoweka akaanza kunifanyia visa ambavyo vilinifanya nimkumbuke baba yangu.

Shangazi aliendelea kunifanyia visa ambavyo nilivivumilia hadi nilipofika darasa la sita ndipo kitovu changu ambacho kilikuwa kikinisumbua tangu utotoni kikaanza kuniuma tena.

Kufuatia tatizo hilo, nilianza kuzimia ovyo hali ambayo ilimpa wakati mgumu shangazi yangu. Alipoona sikuwa na dalili za kupata nafuu aliamua kunipeleka Arusha kwa Mmasai mmoja kwa ajili ya matibabu.

Nilipofikishwa kwa mtaalam huyo wa tiba asili wa mambo yalikuwa hivi;

Masai : Wewe ni mtoto wa ngapi kwenu?

Jibu : Ni mtoto wa kwanza kwa wazazi wangu

Masai: Tatizo ni nini?

Jibu: Kitovu kinanisumbua sana na pia wakati wa baridi huwa kinavimba chenyewe. Basi alichukua dawa na kunichua na nyingine akanipa kwa ajili ya kunywa nyumbani.

Baada ya kutoka kwa yule Mmasai, shangazi alinipeleka kwa baba ambapo nilimueleza juu ya tatizo la kuumwa kwangu, akanipa pole.

Hata hivyo, nilipotaka kumweleza kuhusu mateso niliyokuwa nayapata kutoka kwa shangazi niliogopa, kulipokucha tulimuaga ambapo aliahidi kuja kunisalimia Moshi.

Nilipofika Moshi niliendelea kutumia dawa huku nikienda shuleni kama kawaida, tulipofunga shule baba alimpigia simu shangazi na kumweleza alihitaji niende nikamsalimie Arusha ningerejea Moshi shule zitakapofunguliwa.

Kitendo cha baba kunihitaji niende Arusha kilinifurahisha sana na nilifurahi zaidi baada ya shangazi kukubaliana naye kwamba niende huko.

Baada ya siku mbili niliondoka Moshi kuelekea Arusha ambapo baba alinipokea vizuri alinitambulisha kwa mkewe na wadogo zangu, licha ya kukaa huko kwa mwezi mmoja sikudiriki kumweleza baba kuhusu mateso niliyokuwa nayapata kwa shangazi.

Jambo la kuhuzunisha ni kwamba, tangu mwaka 1999 nilipoanza kuishi na shangazi sikuwahi kumuona mama yangu tuliyeachana naye Moshi kijijini kwa babu.

Niliendelea kuishi na shangazi yangu na kupata kumonio ya kwanza na kipaimara nikiwa kwake, wakati huo nilikuwa naabudu katika Kanisa Katoliki.

Nikiwa kwa baba yangu, maisha yaliendelea vizuri kwani nilipata mapenzi ya wazazi kwani mama mdogo alinipenda na kunijali kama alivyofanya kwa watoto wake.

Likizo ilipoisha amani ilitoweka ghafla kwani nilijua narudi tena kwa shangazi yangu kuendelea kutuseka, siku hiyo nilipoteza uchangamfu niliokuwanao.

Usiku tulipomaliza kula, tukiwa tumeketi sebuleni baba aliniita na kusema: “Mwanangu hautarudi tena Moshi utabaki na utasoma hapa hapa.

Kauli ya baba ilinifanya niruke kwa furaha kisha nilimshukuru kwa uamuzi huo, ambapo alisema nisijali kwa hilo.

Baada ya kufungua shule na kupita siku kadhaa bila kuniona, shangazi alimpigia simu baba na kuhoji sababu za kutorudi Moshi ambapo mazungumzo baina yao yalikuwa kama ifuatavyo:

Shangazi: Kaka mbona simuoni Emmy na shule zimefunguliwa?

Baba : Mtoto nimemwambia lakini amegoma.

Shangazi: Kwa nini agome tuseme mtoto anakuzidi akili?

Baba: Nimeogopa.

Shangazi: Kwa nini uogope kuna tatizo gani?

Baba: Mwanao ameongea jambo la kutisha.

Shangazi: Jambo gani na linahusu nini?

Baba: Mtoto amesema kuliko arudi kwako ni bora afe.

Shangazi: Kweli Emmy ametamka hivyo?

Baba: Ndiyo.

Shangazi: Haya bwana sina la kusema, akakata simu.

Shangazi yangu aliendelea kuyatafakari maneno yale. Na hivyo ilimlazimu kufunga safari na kunifuata Arusha kwa baba lakini baba na mama waliniambia hata akija mjibu hivyo hivyo.

Waliponiambia hivyo, sikuwajibu chochote na maisha yaliendelea hadi shangazi alipoamua kuja ambapo alinikuta mimi na mama mdogo kwani baba alikuwa kazini.

Akiwa amesimama nje alimuuliza mama mdogo nilikuwa wapi? Wakati huo nilikuwa napika jikoni.

Shangazi : Vipi wifi.

Mama mdogo: Safi wifi, karibu.

Shangazi : Asante lakini siingii ndani.

Mama mdogo: Kwa nini wifi?

Shangazi: Emmy yuko wapi?

Mama mdogo: Yupo.

Walipokuwa wakiendelea kuongea nilitoka jikoni na nilimkuta shangazi kasimama huku mama kasimama mlangoni, kwa kweli kitendo hicho sikukifurahia kwani alipaswa kumpatia kiti.

Shangazi aliponiona alinisalimia kwa kusema: Hujambo mwanangu?

Nilimwambia sijambo kisha nilimwamkia ambapo aliitikia salamu yangu na kuniuliza mbona sijarudi kwake wakati shule zilikuwa zimefunguliwa!

Nilinyamaza kimya, mama mdogo aliwahi kumjibu kwamba mtoto amesema kuliko arudi kwako ni bora afe tumzike hapa. Shangazi akageuka na kuniambia ni kweli Emmy? Nimekufanya nini au nimekukosea nini? Nilizidi kunyamaza bila kujibu lolote lile zaidi nilizidi kuona machozi yakinitoka kwani sikuwahi kuyatamka yale maneno aliyoambiwa.

Nilitamani kumwambia ukweli kuwa yale maneno niliambiwa akija niyatamke lakini sikuweza, nilibaki nimenyamaza tu huku nikiendelea kumwangalia shangazi yangu.

Shangazi alipoondoka, nililia sana ndipo mama mdogo alinifuata na kuniambia kwa nini shangazi yangu aliponiuliza nilikaa kimya?

Akaniambia; “Mjinga wewe, pumbavu kabisa.”

Nilizidi kulia kwa yale maneno waliyomtamkia shangazi yangu. Baba aliporudi salamu aliyopewa na mama mdogo ilikuwa: “Huyu mtoto wako ni mpumbavu na mjinga,” baba akauliza kwani kuna tatizo gani? Mama akamwambia, “dada yako Eliza amekuja hapa na alipofika alimhoji mwanao kuhusu kutorudi Moshi lakini huyu mpuuzi hakujibu kama tulivyomwambia.”

Baba akajibu; “Muache atajua na upumbavu wake.” Nilijua baba atanitetea na kuwa upande wangu lakini haikuwa hivyo. Tangu hapo maisha yalianza kubadilika.

Baba sikumuelewa, nilianza kumuuliza habari za shule lakini aliniambia toa ujinga wako hapa. Muda wa shule ulifika sikwenda. Ndipo nilipoona giza la utata machoni mwangu na katika maisha yangu.

Upendo ulipotea, baba hakunipenda tena nilichukiwa kupita kiasi na hata wale ndugu zangu hawakunipenda tena. Maisha yaliendelea kubadilika na kuwa magumu. Muda wa kwenda shule ulizidi kwenda na mimi bado nikawa nyumbani tu. Baadaye baba alikwenda kunitafutia nafasi katika Shule ya Msingi Ngarenaro. Alipata nafasi na kuniandikisha hapo. Nilianza kwenda shule kwa shida na kwa manyanyaso makali mno. Shule waliyonipeleka walituruhusu kusuka nywele, hivyo na mimi nilianza kusuka na ndugu yangu pia alikuwa akisuka tangu mwanzo, yaani tangu nilipoenda kwa baba nilimkuta akisuka.

Nilienda shule na kusoma bila uhamisho kutoka katika shule niliyotokea. Walimu wakawa wakali ambapo mwalimu mkuu siku moja aliniuliza;

“Mbona unasoma bila uhamisho? Mwambie mzazi wako alete uhamisho kutoka shule uliyotokea.” Nikasema sawa mwalimu nitafanya hivyo. Niliendelea na darasa la sita. Nilipofika nyumbani nilimweleza baba. Baba akaniambia, “toa upuuzi wako hapa pumbavu kabisa toka mbele yangu.”

Nilikosa amani kwani sikusikilizwa tena na wazazi wangu, amani ilizidi kupotea ndani yangu, furaha haikuwepo tena giza la utata lilizidi kuwa kali kwangu. Nilisoma kwa shida bila maelewano kuwa na maelewano na wazazi wangu.

Hata nilipopata matatizo nilisita kuwaeleza kwani nilisha chukiwa pale nyumbani, muda ulizidi kwenda na baada ya mwezi wa saba kupita visa vilianza.



Ilikuwa hivi:-

Baba alianza kuninyima kukaa na watoto wake ambao ni ndugu zangu na kuwaeleza kuwa mimi ni mchawi na uchawi huo nilifundishwa na bibi yangu ambaye ni mama wa mama yangu.

Nilitengwa na kunyimwa kutembea na wadogo zangu kwa madai kwamba ningewaroga. Baada ya muda wakaniambia ninyoe zile nywele nilizokuwa nikisuka na kuambiwa, “kwa nini wewe uje juzi tu nywele zako zikue kuliko za ndugu yako? Nyoa.” Nikaenda kunyoa na nikaambiwa nikishanyoa nilete zile nywele sikujua walipozipeleka, nikaanza kuishi maisha ya shida nilishindwa kuongea yaani nikawa bubu kwa wiki moja. Baadaye nilinyimwa kwenda shule na hata kanisani sikwenda tena nikawa nakaa nyumbani tu. Wakitoka wananifungia, nje hadi watakaporudi. Nilimwambia baba mbona mnanikataza kutoka na nyie na kila mnapoondoka mnanifungia nje ya geti? Baba alinijibu, “tumwachie mchawi nyumba? Na pia hatuwezi kuongozana na mchawi njia moja.” Nilikuwa wakulia kila siku amani, upendo, furaha viliondoka moyoni mwangu. Baada ya wiki moja niliweza kuongea na nikaanza kwenda shuleni hakika maisha yalikuwa magumu sana.

SOMA HAPA MAKALA ZA MAFANIKIO 

INAENDELEA 

Post a Comment

Previous Post Next Post