NIACHE NILIE --02

7 days ago

Manyanyaso yaliongezeka

Nilitengewa vyombo vyangu vya chakula, kikombe changu sahani na kijiko. Nilitengwa nisilale na ndugu zangu nililazwa sebuleni peke yangu na kupewa shuka yangu ya pekee. Kila chakula kilipopakuliwa nilipeleka sahani yangu ili niwekewe chakula na hata chai ilipokuwa tayari nilipeleka kikombe pia. Sikuruhusiwa kukaa mezani na wenzangu, nilikaa chini saa ya chakula. Niliendelea kupata usumbufu shuleni lakini sikuweza kumueleza baba yangu kwani nilishamuogopa nilinyamaza tu. Siku moja nikiwa natoka shuleni nilikutana na mama yangu mdogo aitwaye Mary Mwakalinga alinikaribisha nyumbani kwake wakati tunaelekea ndani nilimwambia haya;

Emmy: Mama mdogo acha tu niende nitakuja kukutembelea siku nyingine.

Mary: Hapana twende mara moja.

Emmy: Hapana mama mdogo nitakuja kesho.

Basi niliachana naye nikaelekea nyumbani kwetu kesho yake nilienda shule na nilipotoka nilielekea kwa mama mdogo tena kwani nilimueleza kuwa nitaenda kwake na bahati nzuri nilimkuta.

Emmy: Shikamoo mama mdogo.

Mary: Marahaba, za tangu jana?

Emmy: Nzuri tu.

Mary: Ulikuja lini Arusha?

Emmy: Tangu likizoya mwezi wa sita

Mary: Habari nyingine…

Emmy: Mama mdogo tangu nimekuja kwa baba nimekuwa nikifanyiwa vitendo vya ajabu na vyakikatili sana.

Mary: Vitendo gani tena? Yule si baba yako?

Emmy: Ni kweli, lakini sijui amekuaje na isitoshe nimekuwa nikiota ndoto mbaya na za kutisha.

Mary: Hebu nieleze.

Emmy: Nililala siku moja nikamwota bibi yangu yule ambaye nilikuwa nikiishi naye na niliota akiwa amevaa vazi jekundu kifuani mwake lile vazi limeipigwa liki lakini kwenye hiyo liki kuna mkato yaani liki imekata kosa. Hadi sasa sijaelezwa ile ndoto ilinimaanishia nini. Na siku iliyofuata niliota katika kile chumba nilichokuwa na lala kuna mtu ambaye amekaa chumba kizima yaani mtu anayetisha jitu ambalo halieleweki na halina kichwa. Lakini nilishtuka usingizini, na niliposhtuka nikaamka na kukaa. Nilipokaa na kuwa macho bado nilizidi kuliona lile jitu na nilipopiga kelele sauti haikutoka. Nilikaa na kuanza kulia ingawa sauti haikutoka. Pumzi ilizidi kuwa ngumu kuipata nilizidi kulia bila msaada wowote kupata.

Baada ya hapo nilimaliza maelezo kwa mama yangu mdogo. Mama mdogo akaniambia basi tuombe, tuliomba na kuvunja kila aina ya nguvu za shetani. Na tulipomaliza maombi mama mdogo akanipa zawadi ya kanga peya mbili nikamuuliza ni nani kanipa akaniambia ni mama yako mkubwa yule wa Mbeya ndiye aliyekutumia na alizituma muda mrefu. Namshukuru Mungu kwa kukuona. Nikazipokea kisha niliagana naye na kuondoka uku nikimwambia tutaonana kesho. Nilianza safari kuelekea nyumbani na nilipofika nilimkuta mama mdogo ambaye kwangu ni mama wa kambo akiwa anaendelea na shughuli zake za kushona masweta kisha akaniuliza nimepitia wapi? Nikamwambia hamna mama, akaniambia, “unafikiri nilivyokuuliza mi mjinga?” Nikamwambia sijapitia mahali popote mama, mazungumzo yalizidi kuwa mengi na akiendelea kunibadilikia yaani akiendelea kuwa mkali kwangu nilizidi kukosa raha na amani ndani yangu.

Mama: Nakuuliza kwa mara ya mwisho, ulienda wapi?

Emmy: Kimya

Mama: Sema ukweli, nikusamehe. Nilizidi kuwa kimya sikumjibu lolote lile. Aliamka pale alipokuwa ameketi na kusimama na alinipokonya mfuko niliokuwa nimeubeba ambao ulikuwa ni zile kanga nilizopewa na mama yangu mdogo ambaye ni mdogo wa mama yangu mzazi. Alipochukua ule mfuko akaangalia ndani na kuziona zile kanga, kisha akaniangalia usoni, akaniambia, “nilikuuliza umepitia wapi ukawa kimya na je hizi kanga umezitoa wapi?” Nikamwambia, “nilipotoka shule nilikutana na mama yangu mdogo na ndiye aliyenipa hizi kanga alipokuwa ananipa sikuingia hata ndani alinipa na mimi nikaondoka.” Akasema, “unanifanya mimi mjinga?” Nikamwambia hapana mama, basi akaniambia ngoja baba yako arudi ndiyo utaweza kujieleza kwa sasa naona huwezi kujieleza.

Niliingia ndani na kuvua nguo za shule, na nilipotoka, nje nilienda kuchukua vyombo vya kuosha na wakati, nachukua vyombo akanikataza nisivichukue. Nilipata uchungu na kuanza kulia huku nikiendelea kumkumbuka marehemu bibi yangu. Bado maisha kwangu yalizidi kuwa magumu na ya utata zaidi.

Nilitamani sana kwenda kwa mama yangu mzazi lakini sikupafahamu kabisa. Ingawa kwa mama mdogo ambaye ni mdogo wa mama yangu nilishamfahamu lakini ilikuwa bado ni ngumu kwangu kwani wazazi niliokuwa naishi nao walishaanza kunifuatilia kila kona. Basi baba alirudi kutoka kazini na kitendo cha kumuona tu moyo uliuma gafla. Nilimpokea na kumsalimia, aliingia ndani nami niliendelea na kazi zangu. Majira ya usiku tulipata chakula cha na baada ya kumaliza kula mama akamuelezea baba kuhusu ile safari niliyopita kwa mama mdogo na kumwambia kuhusu zile kanga nilizopewa. Baba akaniuliza, “hizo kanga za kichawi ulizozileta ndani kwangu ziko wapi wewe shetani?” Nikamwambia baba si za kichawi, kama unavyosema akaniambia, “wakati naongea usiwe unanijibu hata siku moja, shetani mkubwa wewe.” Nilizidi, kuumia zaidi kwani yule ni baba yangu mzazi ambaye angetakiwa awe mtetezi wangu wa karibu sana kwangu lakini alizidi kuwa adui kwangu. 

Niliingia chumbani na kwenda kuzileta kanga hizo na baada ya kuzileta alimkabidhi mama naye akaelekea kwenye mti wa mparachichi uliokuwa karibu sana na mlangoni na kuziweka juu. Baba akaniuliza, “nani alikupa ruhusa ya kwenda kwa mama yako mdogo?” Nikamjibu hakuna aliyeniambia. Akaendelea kusema, “kama hamna nini kilikupeleka huko?” Nilipoona maswali yamekuwa mengi niliomba msamaha na kukiri kuwa nimekosea na kumwahidi sintarudia tena. Baba hakuweza kunisikiliza hata kidogo na sapoti nyingi za hasira ziliindelea kutolewa na mkewe. Baba alianza kunishambulia bila huruma alinipiga sana huku nikimuomba msamaha lakini hakunisikiliza hata kidogo kwa sababu sikuwa na wakunitetea. 

Nilitamani kukimbia lakini sikuweza huku mama akisema hawezi kumtetea mchawi. Nilizidi kuumia kwa lile neno. Baba hakuweza kunihurumia mwanaye alizidi kunipiga ingawa nilitia sana lakini bado kilio changu hakusikia hata kidogo. Alinipiga sana lakini cha ajabu sikuyasikia maumivu hata kidogo alipokuwa akinipa kipigo japo nilikuwa nalia. Naweza kusema hamu yake yakuendelea kunipiga ilimwisha, basi akaniacha na kuniambia, “rudia tena uwone nitakacho kufanya ewee mchawi, umenielewa?” Nilikubaliana naye lakini moyo uliniuma sana.

****

“Ni bora nisingekuwa na mzazi kuliko haya yanayonipata” nilikuwa nawaza moyoni huku nikuvuta sura au taswira ya marehemu bibi yangu ambaye niliishi naye kwa upendo wa hali ya juu. Mawazo ya kujiua yalinijia moyoni mwangu nikaanza kutafuta sumu ili ninywe nitoweke juu ya huu ulimwengu. Nilifikia uamuzi huo baada ya kukosa furaha ya maisha ya kuishi na wazazi wangu na ghafla nilianza kumchukia baba yangu ikawa kila nilipomuona moyo wangu ulizidi kukosa amani zaidi.

 Wadogo zangu nao walianza kunibeza huku wakinicheka na kuniambia, “dada gani wewe baba alikupiga jana hatukuiti dada tena, baba amesema atakukomesha, kwanza mama yetu ametuambia kuwa wewe ni mchawi, usitembee na sisi wala usile na sisi tena usilale na sisi, kumbe wewe mchawi aaa.” 

Niliumia sana na nilizidi kulia huku nikijuta kuzaliwa, nilizidi kukosa amani ndani ya moyo wangu, nilikonda kadiri siku zilivyozidi kwenda. Mbali na kutaka kujinyonga pia nilitamani heri ningekuwa yatima huenda watu wema wangejitolea kunilea kupewa mapenzi ya dhati.

Kulipokucha ndipo nilipoanza kusikia maumivu ya kipigo cha usiku nilichopigwa na baba yangu. Cha ajabu wakati ananipiga hadi anamaliza kunipiga sikusikia chochote ila asubuhi ilifika wakati nikashindwa kukaa pia mwili ulikuwa umevimba na majeraha yalionekana zaidi mwilini mwangu. 

Hakuna aliyeongea na mimi wala kunipa pole zaidi ya kunicheza na kuendelea kunibeza hali iliyosababisha nianze kulia kwa uchungu huku nikimuwaza mama yangu mzazi ingawa sikufahamu alipokuwa anaishi. Siku zilizidi kwenda hamu ya kuishi ikiendelea kutoweka ndani yangu, mawazo mabaya yakizidi kukimbilia kwenye ufahamu wangu, akili, ikizidi kuchoka. 

Siku msahau muumba wangu nilizidi, kumwomba Mungu anisaidie na kuniepusha na ugumu wa maisha niliokuwa nikipitia. Nilihisi giza la utata katika maisha yangu kwani tangu marehemu bibi yangu kufariki sikupata kuishi maisha ya furaha tena na wala amani sikuipata. Maisha yaliendelea kuwa magumu kwangu nakupelekea niwe binti wakulia tu kila kukicha. Niliichukia familia ya baba yangu yote sikutamani hata kuwaona. Sikuwa na lakufanya kwani bado nilikuwa nikiishi nao. Kweli ni bora kukosa kila kitu katika ulimwengu huu kuliko kukosa amani na furaha na upendo katika maisha. 

Nilihisi nitaishi maisha ya amani na ningepata furaha kwa wazazi wangu na pale nilitarajia ningeonyeshwa upendo wa dhati lakini hali ilikuwa tofauti kama nilivyokuwa nikiwaza katika ufahamu wangu na kujikuta kila kitu kwangu nikikiona kibaya hata kile kizuri sikukithamini hata kidogo. Ndipo niligundua kuwa hakuna anayejua thamani ya maisha yangu kwa hapa duniani zaidi yake Mungu aliyeniumba. Kutokana na mateso makali niliyokuwa nayapata kutoka kwa baba kilipelekea niwe na hali ya kuwachukia wanaume wote kwani nilijua wanatabia kama ya mzazi wangu na kufikiri hata nikitoka kwa baba na kwenda mahali pengine mambo yataendelea kuwa yaleyale. Nilikatazwa kwendwa kanisani kwa madai kuwa mimi mchawi na kupewa kazi ya kuwa mlinzi wa nyumbani. 

Kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwangu kwani hatima ya maisha yangu sikujua itaishia wapi. Siku moja nilimuomba baba niende kanisani lakini alikataa katu katu lakini mama mdogo aliahidi kunipeleka. Kweli baada ya muda mama alianza kunipeleka kanisani na kuanza kufanyiwa maombi. Nilisali katika kanisa moja lililopo Ngulelo mkoani Arusha. Nilihudhuria kanisani kwa muda mrefu huku nikiendelea kufanyiwa maombi kanisani hapo.

Siku moja niliitwa na mchungaji wa kanisa hilo kwa ajili ya mazungumzo zaidi na yalikuwa marefu lakini yaliniumiza kwa upande mwingine.

Mchungaji: Emmy hujambo?

Emmy: Sijambo mchungaji Bwana Yesu asifiwe.

Mchungaji: Ameni.

Mchungaji: Nimekuita kuna mazungumzo kati yangi mimi na wewe.

Nilinyamaza na kujiandaa kuyasikiliza mazungumzo aliyoniitia.

Moyo ulianza kukosa amani hata kabla ya mazungumzo yenyewe, moyo ulianza kuzungukwa na machozi ya uchungu.

Ilikuwa hivi:

Mchungaji: Emmy tumechoka kukuombea wewe na ujue tumefika mwisho hakuna mtu ambaye atapiga magoti tena na kusema anakuombea wewe. Kwani wewe hausikii na ukitaka kuendelea kuishi hapa na kusali katika kanisa langu naomba ukafanye haya nitakayo kwambia. Nikamwambia sawa mchungaji.

Aliniambia kuwa;

“Kuna kitu umechimbia pale mlangoni kwa baba yako sasa nahitaji uende ukakifukue hapo, sawa?” Nilimwambia mchungaji sijafanya kitu kama hicho lakini yeye aliendelea kusisitiza kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu anajua anachofanya na Mungu anamuonyesha mengi. Nikamwambia tena mchungaji sijachimbia chochote na maneno hayo ni mageni kwangu. Lakini yeye aliendelea kusisitiza kuwa anachokisema ni kweli na kama sitaki niseme. 

Nilinyamaza kimya sikuwa na lakuongea, nilisikia uchungu na moyo ulizidi kuniuma kwa yale mazungumzo. Akaniambia; “nakupa siku tatu tu uwe umeshachimbua hivyo vitu sawa?” Nilinyamaza. Akanimbia nisipochimba atawatuma watumishi wake waje wachimbe hapo nyumbani. Nilinyamaza kimya huku machozi yakinitoka na nilipata uchungu sana moyoni. Baaya kukataa akaniambia niondoke nami nilisimama na kuondoka nikiwa nimeongozana na mama mdogo. Tuliondoka na kuelekea nyumbani, wakati tunaelekea nyumbani mama mdogo aliniambia; “kumbe umechimbia uchawi wako nyumbani kwangu ndiyo maana nashindwa kuishi kwa amani na familia yangu.” Katika mazungumzo yangu na mchungaji nilimwambia kuwa wakati baba ananunua kiwanja sikuwepo na kipindi anajenga nilikuwa sijafika na wakati wanahamia mimi sikuwepo. 

Lakini mchungaji hakuniambia chochote kile kuhusu jambo hilo zaidi yakuniambia nienda kuchimba hicho alichoniambia nimekichimbia nyumbani kwetu. Tulipofika nyumbani mama mdogo alinigeuzia kibao kisha akawa mkali na kunitaka nikachimbue uchawi wangu niliouchimbia nyumbani kwake. Nilimwambia hakuna nilichochimbia na mchunguaji sijui maneno hayo ameyatoa wapi mpaka wanilazimishe kuchimbua vitu ambavyo sijaviweka na wala sivijui. 

Mama mdogo alisema mtumishi wa Mungu si mwongo hata kidogo hivyo ninachotakiwa nienda kuchimba huo ushetani wangu. Mchungaji alisema kitu hicho nilikichimbia mlangoni upande wa kusohoto pembeni ya korido kidogo. Basi mama mdogo aliingia jikoni na alipotoka alitoka na panga, akanikabidhi na kuniambia nichimbe vitu hivyo nami nilijikuta naliaa kwa uchungu kwani alinilazimisha nifanye hivyo haraka kabla watumishi wa Mungu hawajafika maana nitapata shida sana. 

Aliendelea, kunilazimisha nichimbe ile sehemu niliyoambiwa. Baada ya kuona kipigo kimeanza nilianza kuchimba ile sehemu niliyoambiwa na mama mdogo. Nilianza kuchimba mpaka nilipofika kwenye msingi wa ile nyumba na kukutana na kimfuko cheusi kilichofungwa vifundo vitatu na kilikuwa ni kirefu.

**** 

Post a Comment

Previous Post Next Post