Gideon alitulia kwenye kochi lililokuwa sebuleni kwake katika jumba lake la kifahari lililokuwa Masaki jijini Dar es Salaam. Alikuwa akimwangalia mke wake, Juliana Marcel jinsi alivyokuwa amekongoroka na kubaki mifupa mitupu. Alitia huruma pale alipokuwa amekaa, hakuwa mwanamke mrembo tena, uzuri wake ulipotea kabisa machoni mwa Gideon.
Mwanamke huyo aliyesifika kwa urembo kipindi cha nyuma, alichakaa, hakuwa kama Juliana yule aliyepita ambaye aliwatingisha wanaume kutokana na uzuri wake.
Gideon alikumbuka jinsi Juliana alivyokuwa kipindi cha nyuma, kipindi walichokuwa wakisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kipindi ambacho wanaume wote walikuwa wakivutiwa naye. Alikuwa na urembo wa ajabu, aliwavutia wanaume wengi lakini mwisho wa siku, aliwakataa wenye magari na pesa zao, akamkubalia yeye, mtoto wa mama ambaye hakuwahi hata kumiliki milioni moja mfukoni.
Leo hii, miaka kumi baada ya kumuoa na kuzaa naye mtoto mmoja aliyeitwa Jesca, Juliana hakuwa yule wa miaka ile, alichoka, uzuri wake wote ukapotea na kubaki mifupa mitupu. Kila mara Gideon alipokuwa akimwangalia, alitamani kulia, alitamani kumwambia kwamba hakumpenda tena, wakati mwingine alitamani kumpa talaka lakini kwa sababu alikuwa Mkristo, alishindwa kujua afanye nini.
“Kwenye shida na furaha, uzima na ugonjwa nitakuwa na wewe,” aliyakumbuka vilivyo maneno aliyosema mbele ya mchungaji, mbele ya kanisa zima kwamba kamwe asingeweza kumwacha mwanamke huyo.
Leo hii hakutaka kukumbuka tena, asingeweza kuendelea kuishi na mwanamke huyo, wakati mwingine alitamani kumuua, alitamani kwenda jikoni, akachukue kisu na kumchomachoma. Hakuwa na mapenzi naye tena, kisa tu alikuwa amechoka, kisa tu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Saratani ya Damu.
“Mume wangu!” aliita Juliana huku akimwangalia Gideon.
“Unasemaje?” aliitikia Gideon kishari, kwa jinsi alivyomchoka mkewe, hakutaka hata kuisikia sauti yake.
Juliana akanyamaza, moyo wake ulichoma, kipindi hicho kilikuwa ni cha jaribu kubwa maishani mwake. Gideon aliyemzoea hakuwepo, tabasamu pana alilokuwa akimpa kipindi cha nyuma halikuwepo tena, kile kicheko alichokuwa akikiona usoni mwake kilipotea, kwa kifupi, Gideon huyu hakuwa yule wa zamani, hakuwa yule ambaye alizoea kumwangalia na kumwambia ni jinsi gani alikuwa akimpenda.
“Ninakufa mume wangu! Kansa inaendelea kusambaa mwilini mwangu,” alisema Juliana kwa sauti ndogo kabisa.
“Kwa hiyo?” aliuliza Gideon.
Wakati mwingine alihisi kwamba mtu aliyekuwa akizungumza naye hakuwa Gideon yule wa nyuma, alihisi kulikuwa na msichana aliyekuja na kumchukua Gideon wake na kumwachia Gideon mwingine, asiyeeleweka, Gideon aliyekuwa na hasira na asiyetamani kumuona mbele ya macho yake.
Juliana akasimama kutoka kwenye kiti, akamsogelea pale alipokuwa na kukaa karibu yake. Gideon akakunja sura zaidi, hakutaka kabisa kumuona mwanamke huyo akikaa karibu naye kama vile na ndiyo maana hata muda wa kulala alikuwa radhi kulala sebuleni, ang’atwe na mbu lakini si kuona akilala na mke wake, Juliana.
“Unanipenda?” aliuliza Juliana huku akimwangalia mume wake huyo.
“Maswali gani hayo?”
“Nimekuuliza!”
“Ili?”
“Nijue?”
“Hivi wewe mwanamke mbona hutaki kunielewa? Mbona hutaki kunisikiliza?” aliuliza Gideon huku akimwangalia Juliana kwa macho yaliyojaa chuki.
“Gideon! Unanipenda?” aliuliza Juliana.
“Naomba uniache! Niache nipumzike. Nimekuachia chumba ukalale kule ili nilale sebuleni, cha ajabu, usiku sana, muda kama huu unakuja sebuleni, kufanya nini? Au unataka kulala sebuleni ili nikalale chumbani?” aliuliza Gideon kwa hasira.
“Nimekukumbuka mume wangu! Nimekumbuka tabasamu lako, nimekumbuka joto lako, naomba unikumbatie, hata kwa dakika moja tu, nakuomba mume wangu,” alisema Juliana kwa sauti ndogo kabisa, tena yenye kubembeleza.
“Nikukumbatie wewe?” aliuliza Gideon.
“Ndiyo!”
“Unanichekesha sana. Naanzaje kwa mfano?”
Moyo wa Juliana ukachoma, akahisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake, hakutegemea kusikia maneno kama hayo yakitoka mdomoni mwa mume wake. Alimkumbuka, alihitaji faraja, alijua kwamba alikuwa akipitia katika kipindi kigumu, alitakiwa kubembelezwa, alitakiwa kufarijiwa na kutiwa moyo sana lakini kwa mume wake huyo, hilo lilionekana kuwa kama ndoto. Angeanzaje kumkumbatia?
“Unalala sebuleni au chumbani?” aliuliza Gideon.
“Popote utakapolala! Siwezi kulala peke yangu tena! Gideon mume wangu! Kumbuka tulivyokuwa, kumbuka ulivyoahidi mbele ya kanisa, shida na raha, ugonjwa na afya! Umesahau yote hayo mume wangu?’ aliuliza Juliana huku akimwangalia Gideon.
“Clock is ticking…” (muda unakwenda tu)
“Gideon! Pleasee..” (tafadhali, Gideon..)
Gideon akasimama, kwake, maneno yote aliyokuwa akiambiwa na mkewe hayakuonekana kuwa na maana kabisa, hayakumuingia hata kidogo moyoni mwake. Alimchukia Juliana, hakumpenda, alikuwa radhi kulala na mbwa lakini si kulala na mtu kama Juliana.
Alibadilika, hakuwa mzuri, hakuwa na mvuto, kila alipomwangalia, alionekana kuwa kama kituko. Bosi yeye, milionea, eti alale na mtu kama Juliana! Ili iweje? Thamani ya mwanamke huyo ilipotea moyoni mwake, mapenzi yakapotea, chuki ikaingia moyoni mwake.
Kila alipomwangalia, alitamani kumuua, alitamani kumchukua na kwenda kumtelekeza mahali fulani lakini si kuendelea kukaa ndani ya nyumba yake, yaani kila alipokuwa akiamka, amkute chumbani humo. Alimchukia kupita kawaida.
“Kuna siku nitamuua tu! Nitakuja kumuwekea sumu kwenye maji,” alisema Gideon huku akipiga hatua kuelekea chumbani, hakuyajali machozi ya Juliana, jinsi alivyokuwa akilia, kwake alimuona kama muigizaji wa Bongo Muvi ambaye alikuwa kwenye filamu kali ya majonzi.
Huo ndiyo ulikuwa msimamo wake, alimchukua mkewe, yuleyule mwanamke ambaye kipindi cha nyuma alimwambia kwamba alimpenda kwa moyo wote, alimpenda hata zaidi ya alivyokuwa akiwapenda wazazi wake.
Kansa ikabadilisha kila kitu, ikayaondoa mapenzi aliyokuwa nayo na kupandikiza chuki moyoni mwake. Hakukuwa na jingine alilokuwa akilifikiria zaidi ya kumuua mwanamke huyo ambaye bado alikuwa akiteseka kila siku.
2004, UDSM, Dar es Salaam
“Gideon! Unampenda kweli Juliana?” alisikika jamaa mmoja akiuliza.
“Nampenda sana! Nakiri kwamba nitampenda maisha yangu yote, niwe naye kwanza, nitamthamini na kumlinda,” alisema Gideon huku akimwangalia rafiki yake huyo aliyeonekana kushangaa, tangu awaone watu wakipenda, hakuwahi kumuona mtu akipenda kama alivyokuwa Gideon.
“Ila si unajua mtoto wa kishua, halafu watu wengi wamemfuata na magari, pesa, sasa wewe majalala utampata kweli?’ aliuliza rafiki yake huyo aliyeitwa Amos.
“Kwa nini nishindwe? Nitashindwaje sasa? Nitampata tu! Mapenzi si pesa, mapenzi hayatengenezwi benki kaka! Hutengenezwa moyoni,” alisema Gideon huku akionekana kuwa na uhakika juu ya kile alichokuwa akikizungumza.
“Kama una uhakika! Haina shida.”
Gideon alichanganyikiwa, hakukuwa na kitu kilichokuwa kikimuumiza moyo wake kama kumuona msichana Juliana akiwa anamkataa kila alipokuwa akimfuata.
Moyo wake ulikuwa na kiu kubwa, alikuwa kwenye presha kubwa, hakukuwa na msichana aliyeuteka moyo wake vilivyo kama ilivyokuwa Juliana. Alimpenda, kila alipokuwa akilala, mtu wa mwisho kumfikiria alikuwa msichana huyo na alipoamka asubuhi, ndiye alikuwa mtu wa kwanza kumuweka kichwani mwake.
Alilewa, hakuelewa kitu, alihitaji mapenzi, alijua kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakipenda mno lakini kila alipokuwa akijiangalia, jinsi moyo wake ulivyokuwa kwa msichana huyo, alijiona akishika namba moja.
Aliwahi kumfuata Juliana na kumwambia ukweli kwamba alikuwa akimpenda na hakuwa akijiweza. Msichana huyo, kama kawaida yake akamkataa Gideon na kumwambia kwamba aokoke, aachane na maisha ya mapenzi na aukabidhi moyo wake kwa Yesu kristo.
Hakuumia sana moyoni kwa kuwa alikataliwa kwa staili ambayo hakuwahi kuifikiria kabla. Hakutaka kukata tamaa, maneno hayo hayakumrudisha nyuma, bali yalimtia nguvu ya kusonga mbele. Akajifanya msumbufu, kila alipokuwa akimuona Juliana, alimfuata na kuanza kumchombeza.
“Nimesema sitaki! Nimekwambia uokoke, ndivyo Biblia inavyosema,” alisema Juliana huku akimwangalia mwanaume huyo.
“Sawa. Lakini Biblia hiyohiyo inaagiza upendo. Halafu wewe hunipendi, sasa hiyo Biblia ya wapi Jully?” aliuliza Gideon huku akimwangalia msichana huyo katikati ya macho yake.
“Naomba unielewe!”
“Lakini hujanijibu swali langu Jully!”
“Hakuna kujibu swali. Biblia haimaanishi huo upendo unaozungumzia wewe. Naomba uniache,” alisema Juliana huku akionekana kuchukia.
“Daah! Unaniumiza Jully!”
“Hivi wewe mwanaume hutaki kunielewa?”
“Nataka ila nawewe mbona hutaki kunielewa?” aliuliza Gideon kwa sauti ya upole na yenye kubembeleza.
Kila alichokuwa akikizungumza Juliana, Gideon aliingizia maneno yake. Juliana alichukia, kila alipomwangalia mwanaume huyo, moyo wake ulishikwa na hasira kiasi kwamba alitamani hata kumpiga vibao.
Akasimama na kuondoka zake kwa hasira.
Gideon akabaki mahali hapohapo, akamwangalia Juliana jinsi alivyokuwa akiondoka, moyo wake ulimuuma mno, alitamani kumfuata, kumsimamisha na kumwambia amsikilize tena.
Hakukoma, haukuwa mwisho, akapiga moyo konde na kuamini kwamba kuna siku angeweza kumpata msichana huyo. Akawaambia marafiki zake, ugumu wake kumuingiza Juliana mkononi mwake.
Wenzake wakamwambia kwamba kwa staili aliyokuwa akienda asingeweza kumpata, ilimbidi atumie mbinu nyingine zaidi.
“Ipi?” aliuliza Gideon huku akiwa na shauku ya kutaka kufahamu.
“Jifanye kuwa malaika wa nuru!”
“Mmh! Kivipi?”
“Jifanye umezama katika wokovu! Yeye si ndiyo anataka maisha hayo! Fanya hivyo!” alisema Amos.
Hakuwa na jinsi, ulikuwa mtihani mkubwa kwake lakini alitakiwa kuhakikisha anaufanya na kufanikiwa na kumnasa msichana huyo mrembo.
Baada ya siku mbili, akamfuata msichana huyo kwa mara nyingine, alipoanza kuzungumza naye, Juliana alishangaa, hakuamini kama kweli maneno hayo yanatoka kwa mwanaume huyo.
Aliongea kiustaarabu sana, kila alipokuwa akizungumza, alilitaja jina la Yesu, alipobadilisha, basi alitamka jina la ibada tu. Juliana alihisi kama mwanaume huyo alikuwa akiigiza lakini kila alipomwangalia, alionekana kubadilika.
“Juliana! Naomba umsahau Gideon yule wa nyuma. Amekufa! Huyu ni Gideon mpya aliyezaliwa mara ya pili. Ningependa uje kushiriki ibada kanisani kwetu kama hutojali,” alisema Gideon huku akiachia tabasamu pana.
“Kanisa gani?”
“Living Water. Nakuomba uje Juliana uuone utukufu wa Mungu!” alisema Gideon.
“Nitaangalia.”
“Nashukuru!” aliseema Gideon.
Gideon akaondoka huku akiwa na matumaini makubwa ya kumpata msichana huyo mrembo, alimfikiria sana kichwani mwake na kila muda alikuwa akiliandika jina lake kwenye karatasi, alimpenda kwa moyo wake wote.
Juliana alikuwa na wasiwasi, hakumwamini sana Gideon, hata kitendo cha kumwambia kwamba aliamua kuyabadilisha maisha yake na kumkabidhi Mungu bado ilimpa hofu mno.
Aliona haikuwa rahisi kwa mtu kubadilika kwa kipindi kifupi namna hiyo, alihisi kwamba inawezekana mwanaume huyo aliamua kutumia nafasi hiyo ili kumnasa kiulaini kwani kwa kipindi kirefu alikuwa amemsumbua.
Mawazo hayo yalipotea baada ya kukumbuka sura ya Gideon, jinsi alivyokuwa akizungumza naye, alionekana kama mtu aliyemaanisha kile alichokuwa akimwambia. Moyo wake ukagawanyika pande mbili, moja ilimuamini lakini upande mmoja haukumuamini kabisa.
“Ngoja nimpe nafasi ya kwenda huko kanisani, kama amebadilika au hajabadilika nitajua tu,” alisema Juliana.
Jumapili ya siku iliyofuata wakatangulizana kanisani. Gideon alifurahi, hakuamini kama suala hilo lingewezekana kwa haraka namna hiyo. Alitamani kumwambia ukweli kwa mara nyingine kwamba alikuwa akimpenda lakini hakuona kama kulikuwa na uharaka wa kufanya hivyo.
INAENDELEA
,Simulizi: Juliana Sehemu Ya Pili (02)
4 days ago
Alichokitaka ni kuweka ukaribu mkubwa, aonekane kuwa mtu muhimu katika maisha ya msichana huyo. Hilo liliwezekana, kwenda kanisani pamoja, kusoma Biblia pamoja kukawafanya kuwa karibu.
Kila kona wakawa wawili, alipokuwa Gideon ilikuwa ni rahisi kumuona Juliana, na kama hakuwa naye basi hakuwa mbali kutoka hapo alipokuwa.
Hilo liliendelea kwa miezi mitatu mfululizo, Gideon hakutaka kujifanya kuwa na presha, alitaka kufanya mambo kiuhakika na mwisho wa siku kumuingiza msichana huyo katika kumi na nane zake.
“Ataingia tu! Hapa ni mwendo wa kujifanya nimezama kiroho mpaka nimchukue. Huyu binti nina mipango naye sana tu ila naye shetani ananiwekea kauzibe tu,” alisema Gideon huku akikenua.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yao ya kila siku, ukaribu ukaongezeka kiasi kwamba Juliana akaanza kujisikia hali ya tofauti moyoni mwake. Moyo wake ukaanza kuhisi mapenzi, akaanza kumuona Gideon kuwa mtu muhimu katika maisha yake kupita kawaida.
Hakuwa mtu wa kumpigia simu, japokuwa walikuwa na ukaribu lakini alitaka mwanaume huyo awe anampigia simu kitu ambacho hakikuwa tatizo lolote lile.
Mambo yakabadilika, badala ya Gideon kumpigia sana simu sasa ikawa zamu yake.
Kila mara ilikuwa ni lazima ampigie simu mwanaume huyo. Alikuwa akizungumza naye na muda mwingi alikuwa akichekacheka. Aliichukia hali iliyokuwa ikijitokeza moyoni mwake, alitamani kuiondoa lakini alishindwa kabisa, alikikataza kichwa chake kumfikiria Gideon lakini hilo lilionekana kuwa jambo gumu mno.
Moyo wake ukafa na kuoza, akawa hasikii kitu chochote kile. Walikuwa wakizungumza mambo ya kawaida kwenye simu, safari ya Waisrael kutoka Misri kwenda Kanaani, Jinsi Daniel alivyonusurika kuliwa na simba kwenye shimo kubwa, Yesu alivyolisha watu elfu tano kwa mikate na samaki lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele, mambo yakabadilika na hatimaye kuanza kupiga stori za kina Ommy Dimpoz na Harmorapa, shoo zao, upinzani mkubwa wa Kiba na Diamond, na mwisho wa siku kabisa kuanza kuelezea hisi kali zilizokuwa mioyoni mwao.
“Hapana Juliana. Hatutakiwi kuzungumzia mapenzi lakini,” alisema Gideon, tayari akajiona kuwa mshindi, alijiona kufanikiwa kumuingiza msichana huyo katika mikono yake, naye akaanza kumletea mapozi.
“Gideon! Pleaseee…you are hurting me, you love is killing me,” (Gideon! Tafadhali..unaniumiza, penzi lako linaniua) alisema Juliana, Gideon hakuamini masikio yake.
“Juliana!”
“Abee!”
“Ni wewe kweli au?” aliuliza Gideon.
“Kwa nini unauliza!”
“Umebadilika! Yesu hapendi, si unajua hilo?”
“Najua lakini…Gideon naomba nikuone! Naomba nikuone!”
“Haina shida. Ila niahidi kitu kimoja!”
“kipi?”
“Hatutozungumzia kuhusu mapenzi. Nataka niingie kwenye mfungo wa mwezi mzima kuyaombea masomo yetu,” alisema Gideon.
“Sawa,” aliitikia Juliana kwa sauti ya upole.
ITAENDELEA
Tags:
CHOMBEZO