MFALME RAI 08


ADILI NA NDUGUZE 


Mrithi wa Mji wa Mawe

Baada ya kwenda mbele hatua chache Adili aliona mlango mdogo. Kizingitini pake palikuwa na ngazi iliyoongoza juu. Alipopanda vidato vichache aliona dalili za mtu au watu walioishi mle. Kwanza alikuwa akipanda kwa kusitasita, lakini sasa dalili zile zilimvuta akafululiza kupanda. Aliendelea mpaka orofani. Alifuata zilikoongoza dalili mpaka akafika kulikokuwa na chumba kidogo. Mlango wake ulikuwa wazi, kwa hivi aliingia ndani. Huko aliona pazia la hariri lililotariziwa kwa vito vya dhahabu, lulu na yakuti linaning'inia mbele yake. Fusui hizo zilimeremeta kama nyota. Dalili alizoona ziliendelea nyuma ya pazia hilo. Alijipa moyo mkuu akafunua pazia. Alipofanya hivyo macho yake yaliona mlango wa tarabe.

Mlango huo ulikuwa mzuri sana. Mbao zake zilikuwa za mpingo, nazo zilinakshiwa kwa johari na pembe. Mtu yoyote angaliona mlango huo angalistaajabu sana. Adili alibisha hodi akaingia katika chumba kikubwa. Chumba chenyewe kilikuwa kimepambwa vizuri sana. Katikati yake palikuwa na meza na kiti. Msichana wa fahari alikuwa amekaa kitako pale juu ya kiti. Usoni mwake ulikuwa umetukuka. Kwa uzuri uliokuwa haumithiliki. Bila shaka yeye alikuwa malkia wa wazuri katika dunia nzima. Libasi alizovaa zilikuwa nzuri na za thamani kubwa sana. Katika miji yote mingine aliyopata kufika katika safari zake, Adili alikuwa bado kukutana na mtu yeyote mwingine aliyevaa libasi nzuri kama zile.

Kama uzuri ulio peponi wamejaaliwa malaika; karibu uzuri wote ulio duniani alijaaliwa msichana huyo. Uzuri wake ulikuwa haulingani kwa uzuri na mwanamke mwingine yeyote aliyesifiwa kuwa mzuri katika zamani zake. Msichana mwenyewe alikuwa anasoma kitabu kitakatifu. Matamko yake yalikuwa kama mafuatano ya muziki. Moyo wa Adili ulitekwa na mapenzi ya tamasha hiyo. Akili yake ilipotea na nuru ya macho yake ilizimika kitambo. Ile ilikuwa mara ya kwanza mshale wa mapenzi kupenya moyoni mwake. Ulipenya katikati ya moyo wake. Haukuacha nafasi ya mapenzi ya mwanamke mwingine. Licha ya Adili hata mtu mwingine aliyekuwa hajui mapenzi angalikutana na mwanamke huyo moyo wake ungalitekwa pia.

Akili ya Adili iliporudi alimwamkia mwenyeji wake. Mwenyeji aliyeamkiwa hakuitikia tu, lakini alitaja jina la aliyemwamkia vile vile akamkaribisha kwa furaha. Adili alimwuliza alilijuaje lina lake, yeye alikuwa nani na miujiza gani iliyopita pale hata viumbe wa mji mzima wakageuka mawe. Bila ya kusema neno msichana aliondoka akaenda kuchukua kiti. Alikiweka karibu yake akamwomba Adili kukaa kitako. Mwendo aliotumia katika kwenda na kurudi wakati wa kuchukua kiti ulichukua pumzi zote za Adili. Alikwenda kwa hatua za kupendeza , na mikono yake ilipunga kama upepo. Uzuri wake wa fahari ulikuwa na madaha makubwa. Chumba chake kilikuwa kama mahali pa faraja panapotafutwa na wanadamu.

Miguu ya msichana

Na mwendo aliokwenda,

Adili alipoona

Moyowe ulimshinda.

Alikuwa na miguu

Mfano wa charahani,

Wala ulimwengu huu

Hajatokea kifani.

Alipendeza hatua

Wakati alipokwenda,

Chini viatu vyalia

Mithali kama kinanda.

Alikwenda kwa madaha

Mwanamke mwenye enzi,

Yaliyompa furaha

Kila mwenye kubarizi. 

Post a Comment

Previous Post Next Post