ADILI NA NDUGUZE
Mji wa mawe
Adili alikwenda mpaka ulikokuwa ukuta alioona. Kimo cha ukuta wenyewe kilikaribia futi arobaini. Juu ulikuwa na upana wa futi kama ishirini. Wote ulikuwa wa mawe yaliyowekwa kwa imara na ustadi. Mivule , mikangazi, mibuyu na miti mingine ya magogo manene iliota juu yake. Miti yote iligeuka mawe, lakini rangi ya majani yake ilikuwa ya kijani. Maki ya ukuta wote ilikuwa futi ishirini. Duara kubwa sana ilikuwa katikati ya ukuta huo. Katika duara hiyo ulikuwako mji uliokuwa na majengo mazuri sana . Milango mia moja ilikuwa ukutani, na kila mlango ulitengana na mwingine kwa umbali wa maili hamsini. Milango yote ilikuwa ya chuma kilichokuwa na maki ya futi saba. Ulikuwa mji mzuri na wenye ngome bora duniani.
Milango yake ilikuwa wazi. Adili alipotaka kuingia ndani aliona mtu amesimama mlangoni. Kichaka kikubwa sana cha funguo kilikuwa mkononi mwake. Adili alidhani mtu yule alikuwa bawabu. Alikwenda karibu yake akamwamkia. Hakujibu neno. Alimwamkia mara ya pili na ya tatu lakini hakujibu hata kidogo. Adili alishangazwa na adabu ya mtu aliyemwamkia.
Alidhani hakuelewa lugha yake. Lugha ni pingamizi kubwa kwa watu duniani. Kwa hivi alimwamkia kwa ishara. Hili liliposhindwa kufaulu alimsogelea akamshika begani. "Bwana umelala nini?" Hakujibu wala hakutikisika. Alizidi kumtazama na kumshika mwilini. Alipofanya hivyo aliona kwamba alikuwa si mtu ila jiwe lililokuwa halina maisha. Ugunduzi huu ulitia mzizimo wa hofu katika moyo wa Adili lakini alijikaza. Adili alikuwa si mtu wa kukata tamaa. Tamaa kwake ilikuwa gurudumu la maisha naye alijua namna yakuitawala. Mzizimo wa hofu iliyotambaa moyoni mwake uliyeyushwa na udadisi wake mkubwa.
Aliondoka aliposimama akaingia ndani kidogo. Huko aliona mtu mwingine amesimama barabarani. Alimkaribia akamtazama. Lilikuwa jiwe vilevile. Alizungukazunguka barabarani. Kila alipokwenda alitazama huku na huko. Mabarabara yote yalikuwa yamejaa watu waliosimama, Lakini wote walikuwa mawe matupu. Alipofika sokoni aliona umati mkubwa wa watu. Baadhi yao walikuwa wamekaa kitako na wengine walikuwa wamesimama wima. Mbele ya watu waliokaa palikuwa na vikapu vya nafaka iliyogeuka changarawe, unga uliokuwa vumbi, matunda yaliyobadilikia komango, na vitu vingine vya biashara vilivyogeuzwa mawe. Vyote vilikuwa katika hali iliyokuwa haifai kwa chakula. Sababu iliyoweza kueleza mabadiliko yale ilikuwa bado kuonekana. Kwa hivi, Adili aliazimu kuitafuta kwa kila hali. Adili alikuwa na uchunguzo uliomwongoza katika ugunduzi mkubwa.
Alipoondoka sokoni aliona nyumba moja kubwa barabarani . Milango yake ilikuwa wazi. Hili lilikuwa duka la tajiri mkubwa. Alipoingia ndani aliona mwenyewe amelala juu ya kitanda cha dhahabu. Kitanda chenyewe kilitandikwa nguo nzuri na matakia ya zari teule. Mbele yake palikuwa na kabati lililokuwa na kimo cha futi kumi na upana wa futi tano. Tajiri mwenyewe alikuwa mgumu na baridi kama jiwe; na vitu vyake vyote kadhalika. Adili alitazama kabatini akaona mifuko imepangwa safu. Alishika mfuko mmoja lakini kitambaa chake chote kilikuwa vumbi. Vitu vilivyokuwa katika mifuko hiyo ilikuwa sarafu ya dhahabu tupu. Hii haikubadilika mawe wala vumbi. Alijaribu kuchukua dhahabu, lakini hakuweza kama alivyopenda. Moyo wake uliingiwa na fikira kwamba kama angalikuja na ndugu zake wangaliweza kuchukua dhahabu ya kutosha.
Alipotaka kutoka nje aliona makabati yaliyotiwa nguo za hariri na sufu. Nguo hizo zilikuwa za rangi mbalimbali na za almaria bora. Aliponyoosha mkono wake kuzishika zilikuwa vumbi kama vitambaa vya mifuko ya dhahabu. Alitoka akaingia duka jingine. Huko aliona mali nyingi sana kuliko alizoona katika duka la kwanza. Ah, maskini! Mali ilipatikana lakini haikuwa na wachukuzi. Watu waliokuwa na njaa na jahazi yao iliyotaka shehena walikuwa wamesimama kando kwa zembe. Jahazi ilifika nchi ya dafina ya ajabu, lakini mabaharia wake hawakushuka pwani kuipakia. Kula uhondo kwataka matendo. Asiye matendo hula uvundo.
Adili alikuwa kama chura kilichofurahia mvua lakini kilikuwa hakina mtungi wa kuwekea maji. Alitamani kuwa na nguvu za ndovu ili achukue dhahabu ya kutosha lakini haikuwezekana. Basi aliingia hapa akatoka. Alikwenda pale akaondoka na fikira ya mwujiza alioona.
Kila barabara aliyopita ilikuwa na watu, ng'ombe , farasi, nyumbu, punda na mbwa , lakini wote walikuwa mawe matupu. Hofu kubwa ilitambaa moyoni mwake kuwa naye asijegeuzwa jiwe. Lakini alijifariji kuwa labda ilikuwako sababu ya mji ule, wanyama na vitu vyake kuwa mawe, na kuwa lile lilikuwa fundisho kwake. Wazo hili lilimpa nguvu akaendelea kupeleleza. Alipoingia katika maduka ya masonara aliona wenyewe wamegeuka mawe. Mikono yao ilikuwa imeshika vito vilivyokwisha tengenezwa. Vito vingine vilikuwa ndani ya mikebe. Alipoona vile alitupa mbali dhahabu aliyokuwanayo kwanza akarukia vito kwa pupa . Lakini mara moja alisimama kwa mshangao. Alijiona amekaliwa na uzito wa vitu alivyopapia. Juu ya uzito huo hakuweza kuongeza hata pini moja ya shaba. Vitu vilivyobaki vilimtazama kama vilivyokuwa vikimsimanga kwa choyo yake. Tamaa ya mali ni kubwa. Mioyo mingi haitoshwi na mali. Walakini, kwa kweli fikira ya mali isiyo kadiri ni mzigo usiochukulika.
Alipotoka pale aliingia katika maduka ya majohari. Huko aliona wenyewe wamekaa vitini. Mbele ya kila tajiri lilikuwako bweta. Mabweta hayo yalijaa yakuti, almasi, fususu, lulu, feruzi na majohari mengine. Matajiri wote walikuwa mawe. Alitupa chini vito vilivyotengenezwa akachagua yakuti; aliacha yakuti akashika almasi; alikataa almasi akatwaa fususi; alitaka lulu badala ya fususi na feruzi kwa majohari mengine.
Alikuwa hana nguvu ya kuchukulia majohari yote. Kiasi cha majohari aliyoweza kuchukua hakikupunguza wingi alioukuta. Majonzi yalimjia akasikitika juu ya ndugu zake kwa kukosa kufuatana naye. Ndugu zake walikuwa na miguu ya kwendea bali hawakuitumia; walikuwa na nguvu za kuchukulia tunu zilizotosha kwa utajiri wao lakini hawakuwapo. Hili lilimwonyesha Adili kuwa maumbile yalikuwa si bahili. Yalikuwa karimu katika kugawa vipawa. Lakini zaidi ya nusu ya hasara za wanadamu hutokea kwa sababu wenyewe hawataki kutumia vipawa vyote walivyopewa. Basi alichukua alichoweza akaendelea mbele. Moyo wake ulijaa majuto juu ya ndugu zake aliopenda kushiriki nao furaha ya ugunduzi, fahari ya usitawi wa utukufu wa matendo bora.
Alipozunguka nyuma ya maduka alitokea kulikokuwa na nyumba moja kubwa kabisa. Nyumba yenyewe ilikuwa na milango mingi. Miongoni mwa milango hiyo mmoja ulikuwa mkubwa sana. Kwanza hakufaham kwa nini mwenyewe alipata gharama kubwa juu ya milango mingi kama ile. Kisha aliona kuwa gharama yake ilikuwa na maana kwa mtu mwenye akili. Si nyumbani tu lakini hata katika jambo lolote hadhari hukataza mtu kujitia ndani yake kama halina milango ya kuingilia na kutokea. Milango ya nyumba ile ilitosha kwa salama. Baada ya kuwaza hivyo alipita kwa mlango mkubwa uliokuwa wazi akaona mabawabu na askari waliokuwa na sura za kuogofya. Lakini walikuwa mawe.
Ndani kulikuwa na uwanja mkubwa uliozungukwa na viti pande zote. Aliendelea mbele kidogo akatokea katika halmashauri kuu. Juu ya nusu ya halmashauri hiyo palijengwa ulingo. Ulingo wenyewe ulikuwa umejengwa kwa ustadi mwingi. Juu yake palizunguka watu aliodhania kuwa mawaziri, makadhi, mashehe, wanajimu, washauri na madiwani wengine. Kati yao palikuwa na kiti cha dhahabu kilichotonewa kwa majohari mbalimbali. Juu ya kiti hicho alikaa mfalme aliyevaa lebasi za fua zilizokuwa hazitamaniki kwa kumetameta. Kichwani mwake alivaa taji. Taji hilo lilipangiliwa kwa majohari ali ali. Kwa mng'ao mkubwa wa majohari mfalme mwenyewe alikuwa hatazamiki. Alipopanda juu ya ulingo kutazama aliona kuwa hadhara yote ilikuwa mawe matupu.
Alishuka chini akaingia katika halmashauri nyingine. Hiyo kadhalika ilikuwa sawasawa na ile ya mfalme ila ilikuwa na madiwani wanawake watupu. Baadhi ya madiwani walikuwa wamesimama mbele ya malkia na mikono yao vifuani, na wengine walikuwa wamepiga magoti chini yake kwa unyenyekevu. Walakini halmashauri hiyo ilikuwa na mapambo bora kuliko ile ya kwanza. Ilikuwa na meza ya pembe na viti vya mpingo. Juu ya meza palikuwa na bilauli za johari memetevu. Halmashauri nzima ilikuwa imejaa wanawake waliokuwa na uzuri wa sifa kubwa sana. Malkia mwenyewe alikuwa amekaa kitako kati yao. Mabibi wote walikuwa mawe matupu. Utulivu wa akili ya Adili ulichafuka. Alitupa chini majohari yote yaliyokuwa katika miliki yake. Moyo wake ulisimama juu ya bilauli zilizokuwa mezani. Alichukua zilizotosha kuwa mzigo wake akaondoka pale kabla moyo haujarogwa na uzuri wa mabibi waliogeuka mawe.
Tags:
RIWAYA