ADILI NA NDUGUZE
Tandu na Nyoka
Moyo hauhimili mshawasha wa mfululizo. Hasa mshawasha wenyewe ukitokana na mtu unayempenda au tamaa ya utajiri. Moyo wa Adili ulikuwa na mapenzi makubwa juu ya ndugu zake. Aliwapenda kama pumzi ya maisha yake mwenyewe. Aliposikia maneno yao alisema haikuwezekana katika maisha yake kukataa haja iliyotakiwa na ndugu zake. Alikubali kusafiri pamoja nao walikopenda.
Fedha ya kuchanga kwa ajili ya safari iliyokusudiwa ilikisiwa. Mafungu matatu sawasawa yalitakiwa. Fungu la kila mtu lilipokusanywa jumla kubwa sana ya fedha ilipatikana. Walinunua ngozi na bidhaa nyingine. Halafu walikwenda bandarini wakaajiri jahazi kubwa. Walipakia mali yao na vyakula mbalimbali. Siku ya pili walipakia chomboni wakasafiri.
Adili alisumbuka safarini kwa sababu ilikuwa mara yake ya kwanza kusafiri baharini. Baada ya safari ya siku tatu walifika bandarini. Bandari yenyewe ilikuwa ya kwanza katika bandari walizokusudia kwenda. Walishuka wakafanya biashara. Kwa faida iliyopatikana pale, Adili alisadiki maneno yaliyosemwa na ndugu zake. Waliondoka pale wakaenda mji wa pili. Huko walifanya biashara vile vile wakapata tija kubwa kuliko ya kwanza. Walikwenda mji wa tatu wakauza bidhaa zao kwa faida kubwa pia. Kabla ya kufika miji yote waliyokusudia kwenda, waliona wamekwisha rudisha thamani ya mali yao, na faida iliyopatikana ilikuwa kubwa sana. Nusu moja ya mali waliyokuwa nayo ilikuwa imeuzwa. Palibaki nusu ya pili kuuzwa. Walikwenda miji mingine.
Baada ya safari siku moja walifika jabalini. Nahodha aliamuru kutua tanga na kutia nanga. Kisha mabaharia walitakiwa washuke jabalini kutafuta maji kwa sababu jahazini mlikuwa hamna maji hata tone moja. Pipa la maji jahazini lililotosha kwa mwezi mmoja lilitoboka. Maji yake yalivuja bila ya kujulikana na mtu. Mabaharia wote walishuka wakatafuta maji chini ya jabali. Adili alipanda juu ya jabali. Huko aliona tandu linakimbia. Rangi yake ilipendeza sana. Iling'ara kama kioo. Nyuma yake lilifuatwa mbio na nyoka aliyetisha kabisa. Nyoka alipolifikia aliliuma kichwani. Kisha alilibana jiweni. Tandu lilitoa mlio wa kusikitisha. Kwa mlio ule Adili alijua kuwa tandu lilikuwa hatarini. Mara ile moyo wake uliingiwa na huruma. Hakuweza kuvumilia. Aliokota jiwe liliokaribia uzito wa ratili moja akamtupia nyoka. Jiwe lilimpiga nyoka kichwani. Ilikuwa shabaha nzuri sana. Kichwa chote kilipondeka kwa pigo moja akafa mara ile.
Ghafula tandu lilijigeuza mwanadamu, yaani, msichana mzuri. Uso wake ulivuta macho ya Adili kwa haiba yake kubwa. Mbele ya wanawake mia moja wazuri, msichana huyo angalitokea, wote wangalijichukia wenyewe kwa kujiona hawakulingana nae kwa uzuri. Tazamo la mwanamume yeyote lingalivutwa kama angalitokewa na msichana huyo. Alikwenda kwa Adili akampa mkono. Alimshukuru kwa wema aliomtendea. Adili aliombewa dua na msichana apate himaya mbili. Himaya ya dunia na himaya ya ahera. Ya kwanza imfae katika maisha yake, na ya pili imwokoe siku ambayo mtu hatafaliwa na kitu kingine ila wema aliotenda. Kama alivyookolewa msichana aliahidi kutenda neno lolote jema kwa Adili katika wakati ujao.
Baada ya hayo msichana alielekeza kidole chake cha shahada chini. Mara moja ardhi ilipasuka akaingia ndani yake. alipokwisha jitia ndani ardhi ilijifunga sawia. Msichana hakuonekana tena. Adili alifahamu kuwa alikuwa si mwanadamu ila jini. Kitambo kidogo aliona nyoka aliyemwua anawaka moto. Mara moja alikuwa majivu matupu. Kufumba kope na kufumbua mahali palipokuwa na majivu palitokea chemchemi ya maji safi. Mambo haya yalikuwa mwujiza mkubwa sana kwa Adili. Alirudi kwa wenziwe na habari za ugunduzi wa maji. Adili alishangiliwa sana kwa ugunduzi wake. Walipkwisha chota maji ya kutosha walilala. Asubuhi walitweka wakasafiri baharini mchana na usiku kwa muda wa siku thelathini. Walikuwa hawaoni bara wala kisiwa. Maji yao yalikwisha tena.
Nahodha alipotangaza chomboni kuwa maji yamekwisha mabaharia waliomba chombo kielekezwe upande wa bara. Lakini nahodha aliapa kuwa hakujua upi ulikuwa upande wa bara toka mahali walikokuwako. Aliposema hivyo mioyo yao ilihuzunika machozi yakawatoka machoni njia mbili mbili. Walikuwa hawana neno la kutenda ila kuomba hifadhi ya Mungu. Siku ile walilala na kihoro. Kulipokucha waliona jabali refu sana baharini. Walianza kufurahi tena.
Tanga liligeuzwa wakaenda jabalini. Walipolikaribia walitua. Kisha walishuka chomboni wakapanda jabalini kutafuta maji. Hali zao zilikuwa dhaifu kwa kiu. Walitafuta hiku na huko lakini hawakuona maji. Adili alipanda juu zaidi. Huko alitazama upande wa pili wa jabali akaona kwa mbali sana akaona ukuta umezunguka. Ilipata mwendo wa robo saa toka jabalini mpaka ulikokuwa ukuta. Aliwaita wenziwe waliokuwa chini ya jabali.
Walipokuja aliwaonyesha ukuta alioona. Alidhani ndani yake ulikuwako mji mkubwa ambako maji na vitu vingine viliweza kupatikana. Basi aliwashauri wenziwe kwenda kule. Wenziwe wote walikataa kwenda. Walichelea kuwa mji wenyewe usije kuwa wa watu wabaya. Wakikamatwa utakuwa mwisho wa maisha yao. Kwa vile walivyokuwa katika hatari ya kiu, hawakuweza kujasiri katika hatari nyingine kwa tamaa ya maji. Walikataa kwenda wakajitolea wenyewe kufa kwa kiu, Lakini Adili hakukubali. Moyo wake ulikuwa imara sana. Alitaka kujaribu kujiokoa kwanza kabla ya kujitolea kushindwa. Ilikuwa idhilali kwake kujilegeza mbele ya shida iliyowezekana kushindwa. Kwa hivi, alisema kuwa hakua na mamlaka juu ya mabaharia wote, lakini alitaka kwenda na ndugu zake. Lo, ndugu zake waliruka wakakataa kufuatana naye. Walionywa na Adili kuwa mwanadamu ameumbwa kwa heri na shari, na hasa kwa heri.
Ilikuwa hasara iliyoje kutazamia shari tu katika maisha! Juu ya onyo hili ndugu zake hawakuwa tayari kwenda naye. Basi aliwaomba wamngoje jabalini. Walipokubali kufanya hivyo alikwenda zake peke yake kujaribu bahati yake.
Adili aliyageukia manyani akauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea. Manyani yaliziba nyuso kwa viganja vya mikono yao kwa aibu.
Tags:
RIWAYA