MFALME RAI 05

ADILI NA NDUGUZE 

Mgawo Mwingine

Katika kueleza msiba wao, ndugu zake Adili walisema walipoondoka Janibu walikwenda Gube. Walianza kuuza bidhaa zao huko. Ngozi iliyonunuliwa Janibu kwa shilingi moja iliuzwa kwa shilingi kumi, na ile ya shilingi mbili kwa shilingi ishirini. Walipata faida kubwa sana. Baadaye walinunua viatu kwa bei ya shilingi kumi jozi moja. Viatu hivyo vingalifika Janibu vingaliuzwa kwa shilingi arobaini kila jozi. Walipotoka Gube walikwenda mji wa Gharibu wakafanya biashara kubwa kuliko ya mara ya kwanza. Walishindwa kujua hesabu ya fedha waliyoipata, walisifu uzuri wa miji waliyokwenda, usitawi wa biashara na faida iliyopatikana huko.

Mtu kushindwa kujua pato lake mwenyewe huonyesha uchache wa uangalifu. Lakini Adili hakusema neno juu ya hili. Ulikuwa si wakati wa kusema makosa. Ndugu zake walitaka huruma wakati ule siyo kulaumiwa.

Kisha waliendelea kusema kuwa msiba wao ulikuwa hausemeki. Walipoona wamepata mali nyingi hawakufurahi kukaa ugenini tena. Iliwatokea dhahiri kuwa mtu huchuma juani akala kivulini. Kwa kila mtu kwao ni kivulini na ugenini ni juani. Fikira hii ilipowatopea walifanya safari ya kurudi kwao. Basi walijipakia chomboni. Kwa muda wa siku tatu safari yao ilikuwa njema, lakini siku ya nne bahari ilichafuka. Mvua ilianza na giza lisilopenywa na nuru lilifunika bahari. Mchana ulikuwa kama usiku. Palitokea radi na umeme. Dhoruba kali iliandama nyuma. Mawimbi makubwa kama milima katika bahari isiyopimika kina yaliwakabili. Jahazi yao ilipeperushwa kama jani mwambani ikavunjika. Shehena ya mali ilikuwa chomboni ilitota. Fikira ya mali yao haikuwajia. Waliomba wokovu wa maisha yao tu. Kwa msaada wa mbao chache zilizopatikana katika chombo kilichovunjika, walielea baharini mchana na usiku kwa muda wa siku sita.

Siku ya saba, walipokuwa karibu kukata tamaa, jahazi ilipita karibu yao. Mabaharia wa jahazi hiyo waliwaokoa. Jahazi iliyowaokoa ilikuwa na safari ya kwenda nchi nyingine. Iliwapasa kuwa katika safari zile na kufanya kazi bila ijara chomboni. Waliposhuka katika kila bandari waliyofika waliomba chakula katika baadhi ya miji walipewa chakula, lakini katika miji mingine hawakupata kitu. Kwa hivi, waliuza nguo walizovaa wapate fedha ya kununulia chakula. Uchi wao uliweza kungojea nguo, lakini njaa yao haikuweza kungoja chakula. Walipata robo tatu za mashaka ya dunia toka siku waliyokufa maji mpaka siku waliyofika kwao. Laiti wasingalipatwa na bahati mbaya wangalirudi Janibu na utajiri mkubwa.

Ndugu zake walikuwa masogoro katika kusema. Walijifunza sana kutumia ulimi na midomo. Adili alivutwa na maneno yao siku zote. Hakujua kama tumaini lake juu ya ndugu zake lilikuwa kazi bure. Walikuwa waovu katika kila inchi ya miili yao. Baada ya kuwasikiliza aliwapa pole. Alisema kuwa mali hufidia roho lakini roho haifidiwi na kitu. Salama ya maisha yao ilikuwa bora kuliko faida iliyopotea. Umaskini umetengana hatua moja tu na utajiri. Kwa kuwa vitu vile vimekaribiana sana, wako watu katika dunia waliopata kuonja uchungu wa umaskini na ladha ya utajiri. Madhali ndugu zake wameonja uchungu wa umaskini, aliwakuza moyo kutazamia ladha ya utajiri wakati ujao.

Siku ya pili Adili aliwachukua ndugu zake kwa kadhi. Alipofika aliomba mali yake igawanywe mafungu matatu sawasawa kati yao. Alifanya hivyo kwa kuwaambia mali ile pia ilitokana na baba yao. Kila mtu alichukua fungu lake akafungua duka. Adili aliomba dua kuwa ndugu zake na yeye wote wabarikiwe. Aliwaonya wenziwe hatari ya uvivu na hasara ya ulevi. Aliwapa chakula na haja nyingine za lazima bure siku zote. Walikaa nyumbani mwake raha mustarehe. Mara kwa mara walipokuwa pamoja, Adili aliambiwa sifa za nchi ngeni. Ndugu zake walikumbuka mali yao na usitawi wa biashara walioona. Walimvuta Adili kusafiri pamoja nao tena kwa sababu faida za safari, yaani kufarijika katika hamu, kujua namna ya kuendesha maisha, kupata elimu mpya, kuelewa tabia za watu mbalimbali, kukutana na marafiki wa kweli kushinda ndugu, na mtu mwenye bahati mbaya kwao huweza kupata bahati njema ugenini.

Adili aliyageukia manyani akauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea. Manyani yaliziba nyuso kwa viganja vya mikono yao kwa aibu. 

Post a Comment

Previous Post Next Post