MFALME RAI 04

ADILI NA NDUGUZE 

Ndugu Zake

Katika kisa cha kwanza Adili alisema manyani yale mawili yalikuwa ndugu zake. Baba yao alikuwa mmoja na mama yao mmoja. Baba yao aliitwa Faraja. Faraja alikuwa mtoto wa pacha. Wakati wa kuzaliwa pacha huyo mtoto mmoja alikufa pakabaki mmoja. Huyu aliyebaki aliitwa faraja kwa sababu aliwafariji wazazi wake katika msiba wa ndugu yake. Alipokuwa wazazi wake walimwoza mke, yaani mama yao. Mama yao alichukua mimba ya kwanza akazaa mwana aliyeitwa Hasidi. Alichukua mimba ya pili akazaa mwana vile vile aliyeitwa Mwivu. Alichukua mimba ya tatu akazaa mwana tena aliyeiywa Adili. Walilelelewa mpaka wakawa watu wazima wenye vichwa vilivyofunzwa lakini mioyo iliyosahauliwa. Busara kubwa kichwani haina faida kama moyoni hamna chembe ya wema.

Baba yao alipokufa aliacha shamba zuri, duka kubwa, mifugo mbalimbali na nakidi shilingi hamsini elfu. Walimzika kama desturi wakafanya matanga. Siku arobaini zilipopita, Adili alikaribisha matajiri na watu maarufu wa janibu karamuni. Karamu ilipokwisha Adili alitamka kuwa maisha ni safari, na dunia ni matembezi kwa wanadamu. Maskani yao ya milele yako peponi. Hapana mtu ambaye atabaki duniani. Baba yake amekufa akiacha mali nyingi. Alichelea kuwa walikuwako watu waliomdai au walioweka amana kwake. Alitaka kila mtu apate kulipwa ili aindoe lawama la baba yake ulimwenguni. Baada ya kusema hivyo kimya kikubwa kilitokea. Watu walinyamaza kama waliokuwa wamenyang'anywa ndimi zao.

Halafu walijibu kwa umoja kuwa hawakuweza kuuza pepo kwa dunia. Walikuwa wacha Mungu na wafuasi wa haki. Walifahamu halali na haramu. Jambo moja katika mambo waliyokimbia kabisa lilikuwa mali ya yatima. Walimfahamisha Adili kuwa mali ya baba yake ilikuwa imebaki mikononi mwa watu. Bila shaka watu hao watamlipa. Hapakuwa na mtu hata mmoja miongoni mwao aliyedai kitu kwa marehemu. Walithibitisha kuwa walimsikia mara nyingi baba yake Adili akisema kuwa alichelea sana deni. Katika uhai wake alizoea kuomba asife na deni. Tabia ya baba yake ilikuwa kamili. Kila karadha aliyochukua alilipa kabla ya kudaiwa. Alipokopesha kitu kwa mtu hakudai kwa fadhaa. Wadeni wake walimlipa pole pole. Mtu aliyekuwa hana njia ya kulipia alisamehewa.

Adili aliwashukuru kwa kuhudhuria karamuni na kwa kumpa hakika ya ukamilifu wa baba yake. Wageni walipokuwa wanakwenda zao waliambiana njiani, "Mwana wa mhunzi asiposana huvukuta. Adili atakuwa mwema kama baba yake."

Sasa Adili aliwaambia ndugu zake kuwa kwa ushahidi uliotolewa alitosheka kuwa baba yao alikuwa hadaiwi na mtu. Urithi walioachiwa ulikuwa mkubwa sana. Warithi walikuwa watoto watatu tu. Aliuliza kama ndugu zake walipenda urithi ule ugawiwe kila mtu achukue sehemu yake, au uachwe kama ulivyokuwa ili watumie shirika. Ndugu zake walitaka urithi ugawiwe kati yao.

Adili alikwenda kumwita kadhi. Kadhi alipokuja aligawa urithi wao katika mafungu matatu. Mafungu yote yalikuwa sawasawa kwa thamani. Kila mmoja alipata fungu lake. Adili alichukua shamba na duka. Mali nyingine walipewa ndugu zake.

Basi Adili alifungua duka lake. Alinunua bidhaa akatia dukani mpaka likajaa tele. Alikaa kitako akafanya biashara. Ndugu zake walinunua marobota ya ngozi na bidhaa nyingine wakafanya safari ya kwenda nchi ngeni kufanya biashara. Siku ya kuagana nao, Adili aliomba Mungu awabariki ndugu zake ugenini, naye ampe riziki yake kwao. Alifanya biashara kwa muda wa mwaka mmoja. Hakuacha kuhesabu kitu alichonunua wala alichouza. Vitu vyote, kilichoingia ndani na kilichotoka nje , vilitiwa daftarini kwa uangalifu. Mali bila ya daftari hupotea bila habari. Adili alikuwa macho sana juu ya neno hili. Aliweka hesabu ya kila siku na ya kila mwezi. Mwisho wa mwaka alipolinganisha faida na hasara aliona amepata mali kama ile iliyoachwa na baba yake. Hakika mtu anayehesabu mapato na matumizi yake hafi maskini.

Siku moja Adili alikuwa amekaa dukani pake. Ulikuwa wakati wa baridi. Alikuwa amejifunika mablanketi mawili. Moja lilikuwa la sufu na jingine la pamba. Aliona ghafla watu wawili wanakuja dukani. Walikuwa hawana kitu. Kila mmoja alivaa kanzu mbovu bila ya nguo nyingine ndani. Midomo yao ilibabuka kwa baridi. Alipotambua kuwa walikuwa ndugu zake, moyo wake uliwaka moto kwa huzuni. Watu aliowapenda walikuwa katika hali mbaya sana. Aliondoka kitini akaenda kuwakumbatia. Mitiririko ya machozi ya moto ilitoka machoni mwake. Hakuweza kujizuia kulia kwa sababu ya mapenzi makubwa aliyokuwa nayo juu ya ndugu zake. Mapenzi yake yalitoneshwa na hali mbaya waliyokuwa nayo.

Adili Alikuwa tayari siku zote kugawana na mtu yeyote tonge moja la chakula lililokuwa mikononi mwake. Alipoona ndugu zake katika matambaa hakuweza kuhimili. Uchi wao ulikuwa uchi wake. Alivua mablanketi yake mwenyewe akampa kila mmoja lake.

Maji ya moto yalitengenezwa akawapeleka msalani kuoga. Kisha alitoa sandukuni vikoi viwili, fulana mbili, kanzu mbili, jozi mbili za viatu na kofia mbili akawapa. Vitu hivyo vilikuwa vizuri na thamani yake ilikuwa kubwa sana. Baada ya kuvaa nguo walikaribishwa sebuleni. Wakati ule hali yao ilikuwa bado dhaifu sana kwa uchovu na njaa. Chakula kililetwa katika sinia moja ya dhahabu iliyonakshiwa kwa fususi. Walitafadhalishwa kula chakula wakala mpaka wakashiba.

Adili aliyageukia manyani akauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea. Manyani yaliziba nyuso kwa viganja vya mikono yao kwa aibu. 

Post a Comment

Previous Post Next Post