MFALME RAI 03

ADILI NA NDUGUZE

Adili Mbele ya Rai

Uso wa Ikibali ulikuwa na haya na moyo wake ulijaa hisani. Alikuwa tayari kutumika kama alivyotakiwa na mfalme, lakini alichelea kuwa haini kama siri aliyotoa ilikuwa maangamizi ya Adili. Alijuta ulimi wake haukuwa na nadhari. Hapana roho mbinguni wala duniani isiyopatwa na majuto. Tuna busara nyingi sana baada kuliko kabla ya neno kufanyika. Kama taratibu ya msaada haikufaulu, Ikibali hakupenda kumkabili Adili. Wakati ule ule hakuweza kughairi dhima yake. Ugomvi baina ya hiari na dhima ulianza moyoni mwake. Mambo haya mawili hayatimiziki mara moja. Hapana mtu awezaye kwenda njia mbili wakati mmoja. Kwa hivi, Ikibali alitii mahitaji ya dhima yake akaenda janibu.

Adili alipoona Ikibali amerudi alishtuka. Alisema moyoni mwake ataokolewa katika uovu aliolazimishwa lakini hakuupenda kuutenda. Baada ya hayo alimuuliza Ikibali neno lililomrudisha ghafla Janibu. Ikibali alijibu asingalirudi ghafla vile, lakini katika jitihada yake ya kutenda wema ametenda nuksani. Alikuwa hana udhuru wa kujitetea katika lawama lake. Ulimi wake mwenyewe umemponza. Aliungama alipofika Janibu mara ya kwanza alishawishika kumpeleleza Adili siku tatu. Kila usiku alipokwenda kuadhibu manyani, yeye alimfuata nyuma. Aliporudi nyumbani kulala, yeye alitangulia mbele. Mambo aliyotenda kwa manyani yalikuwa ajabu kwake. Hakupata kuuliza sababu yake. Aliporejea Ughaibu alizungumza habari zile kwa mfalme. Mfalme aliposikia alimrudisha janibu kumchukua Adili na manyani yake.

Adili alikuwa mwema na msamehevu. Alibaini kama Ikibali alilaumika kwa kufichua siri, kadhalika yeye mwenyewe alilaumika kwa ukatili. Tafakuri ilimwonyesha Adili kuwa ukali wa mbwa utokana na msasi. Mbwa wa msasi mkali ni wakali pia. Rai alikuwa mfalme mwadilifu. Ilijuzu Ikibali, mjumbe wake, kuwa mchunguzi hodari. Mambo yaliyogunduliwa yalikuwa kweli. Mambo yenyewe hayakumpendeza Adili mwenyewe, licha ya mfalme na mjumbe wake. Kipawa kimoja katika vipawa bora kwa mwanadamu ni ujuzi wa maovu. Adili alibarikiwa kipawa hiki. Alishukuru kuwa siri iliyogunduliwa imefika katika masikio ya mfalme. Adili mwenyewe alitaka ijulikane, lakini alichelea kuwa haini kwa mfadhili wake. Madhali imefichuka alikuwa tayari kuithibitisha.

Adili alijiandaa kwa safari ya kuitika mwito wa mfalme. Farasi watatu walitandikwa matandiko mazuri. Yeye alipanda farasi mmoja na mmoja kwa kila nyani. Ikibali alipanda farasi wake mwenyewe. Farasi wa Adili na yule wa Ikibali walikwenda sambamba njiani. Nyuma yao yaliandama manyani juu ya farasi. Kila mtu aliyeona manyani yamepanda farasi alistaajabu. Mnyama kupandwa na mnyama ilikuwa upeo wa miujiza kwa watu. Vinywa vya umati wa watu vilikuwa wazi kwa kivumo cha Lo salala! Wakati umefika wa mawe kusema, miti kujibu na wanyama kuwa watu! Ikibali aligeuza uso wake kwa Adili akasema kwa ucheshi. "Mbwa wanatubwekea kama walionusa mtara wa windo." Adili alikubali kwa kuinamisha kichwa akatabasamu, walisafiri hivi mpaka Ughaibu. Baada ya kutua Adili alipelekwa mbele ya mfalme na manyani yale.

Manyani yalipomwona mfalme yalifanya ishara mbili. Kwanza yaliinua juu mikono yao kama yaliyokuwa yakiomba, pili yalilialia kama yaliyodhurumiwa. Ishara ya kwanza ilionyesha ombi la msaada, na ile ya pili ilionyesha mashtaka. Licha ya Rai, hata mimi na wewe tungalifasiri hivi kama tungalikuwa katika baraza hiyo. Mfalme alipoona vile alitaka kujua kwa Adili sababu ya kuadhibiwa, kulishwa na kunasihiwa manyani yale kila usiku. Katika sababu zake alionywa kusema kweli tu. Adili alijibu kuwa waungwana hawasemi uongo. Atasema kweli, na manyanai yatakuwa mashahidi. Maneno yake yakiwa uongo, yatakanushwa na manyani kwa mguno, lakini yakiwa kweli, manyani yatayathibitisha kwa kuziba nyuso kwa viganja vya mikono yao. Sasa kisa baada ya kisa juu ya manyani kilisimuliwa. 

Post a Comment

Previous Post Next Post