MFALME RAI 02

Adili na Nduguze:- Shaaban Robert

Siri inafichuka

Ikibali alitakiwa na Maarifa kwenda Janibu kuchunguza kodi. Ikibali alikuwa mshauri katika halmashauri ya Ughaibu na mshauri wa mfalme. Alichaguliwa kwa kazi hii kwa sababu alikuwa na maarifa ya kuchukuana na watu. Kwa maarifa haya aliweza kupata mradi wake siku zote bila ya kuamsha uadui wa watu juu yake. Ughaibu ilikuwa teuzi katika wasimamizi wake na katika madaraka yao. Uteuzi wake ulikuwa na maana kwa sababu ukamilifu wa mtu duniani ni tabia njema. Mbali ya sifa nyingine, kila mtu bora alitakiwa kuonyesha ubora wake kwa kuchukuana na watu. Ikibali alikuwa mkamilifu wa tabia akaaminiwa na Rai, Maarifa, halmashauri na watu wadogo.

Siku ya pili, saa moja asubuhi, Ikibali alikwenda janibu. Mwendo wa saa sita kwa farasi ulikuwa kati ya Ughaibu na Janibu. Adhuhuri ilipokaribia Ikibali alikuwa amefika katika viunga vya mji aliokusudia. Huko alitua akapeleka taarifa kwa Adili, Liwali wa janibu kuwa amewasili. Adili alipopata habari alikwenda akamlaki mgeni wake nje ya mji kwa furaha. Baada ya kumlaki aliingia naye mjini. Saa saba mchana Ikibali alifika nyumbani kwa mwenyeji wake akapokewa kwa taadhima. Alikula chakula cha mchana na mudir wa Janibu, na saa nane akazuru idara zao. Hulka ya ikibali ilipendeza watu waliopata kukutana naye. Kicheko kilikuwa midomoni mwake na shukrani katika pumzo zake. Hulka njema sawa na mali. Fundisho hili linakwenda duniani mpaka sasa.

Jioni Ikibali na Adili walipokuwa peke yao mazungumzo juu ya kodi yalianza. Hapakuonekana upungufu wowote. Hesabu haikuwa kamili tu, lakini ilionyesha ziada vile vile. Ikibali alihakikishwa kuonyeshwa ziada hii asubuhi. Sababu ya kuchelewa ilihusiana na makusanyo ya ziada. Kama Adili hakutanguliwa na Ikibali siku moja, Adili alikusudia kupeleka hesabu yake Ughaibu siku ya pili. Ikibali alifikiri habari hizi njema zilitosha kutuliza wasiwasi wa mfalme. Kwa hivi, aliazimu kurudi Ughaibu kesho yake. Adili alitaka kutajamali na Ikibali. Hamu yake ilikuwa kubwa sana. Kama haja hii haikumkalifu Ikibali, Adili aliomba sana jamala ya kutafaraji naye kwa muda wa siku tatu. Kwa kuwa waungwana hawanyimani neno lisilokalifu Ikibali alikubali kuahirisha marejeo yake.

Sasa Adili na mgeni wake waliingia sebuleni. Sebule hiyo ilikuwa imesakifiwa na marmar za rangi tatu, yaani, nyeupe, nyekundu na samawati. Dari yake iliikizwa vizuri sana. Ilisaki sawasawa juu ya kuta nne zilizopakwa sherezi ya manjano. Katikati ya dari hii ilining'inia chini karabai moja iliyozungukwa na matovu ya almasi. Kuta mbili katika hizi nne zilikuwa na madirisha mazuri. Katikati ya sakafu palitandikwa mazulia ya thamani kubwa. Juu ya mazulia hayo palikuwa na meza moja ya mkangazi na viti viwili vya henzirani. Vyakula na vinywaji mbalimbali viliandaliwa juu ya meza. Walikaa kitako hapo kwa kuelekeana wakala chakula cha usiku. Baada ya kula na kunywa walizungumza mpaka wakati wa kulala.

Malazi ya Ikibali yalifanywa katika chumba kilichokuwa na sakafu ya marmar nyeupe tupu. Dari ilipakwa sherezi ya samawati na kuta zilikuwa na sherezi ya zari. Kila ukuta ulikuwa na dirisha la kioo kilichosimama juu ya mihimili ya johari. Vitanda viwili vya pembe vilivyokuwa na viwambo vya ngozi na matandiko ya pamba vilitandikwa humo.. Mihimili ya vyandarua ilikuwa ya dhahabu. Siku ile Adili alilala katika chumba kimoja na mgeni wake. Baada ya kupanda vitandani wote wawili walinyamaza kimya. Kila mtu alidhani mwenzake amelala, lakini wote wawili walikuwa macho. Ikibali alikuwa akisanifu mashairi, kama ilivyokwisha semwa kuwa alikuwa mshairi mashuhuri. Alipoendelea hivyo mpaka usiku wa manane alimwona Adili ameondoka ghafula kitandani. Chumbani lilikuwamo bweta. Adili aliokwisha vaa nguo zake aliliendea bweta akalifungua. Alitoa mjeledi na mshumaa. Mshumaa ulipowashwa nuru kubwa sana ilitokea. Sasa Adili alifungua mlango wa chumbani akatoka nje. Hakujua kama Ikibali alikuwa macho.

Ikibali alishangaa usanifu wake ukachafula. Hakujua Adili alikusudia kwenda wapi na mjeledi usiku ule. Alijua kwamba ilikuwa si murua kunyemelea mambo ya watu, lakini alijua pia kwamba ilikuwa wajibu kujiweka tayari kusaidia katika haki. Kwa sababu ya msaada aliona haifai kulala kama mvivu nafasi ya kutenda wajibu wake ilipotokea. Wazo hili lilimwondoa kitandani akatoka nje.. Alimfuata Adili nyuma polepole. Karibu ya nyumba moja ndogo Ikibali alisimama kando. Adili alifululiza mpaka mlangoni. Aliufungua akaingia ndani. Alipotoka nje alikuwa na sinia moja. Siniani mlikuwa na sahani za chakula na birika la maji. Alijibandika begani sinia akaenda zake. Ikibali alimfuata nyuma vile vile.

Adili alipofika nyumba nyingine, kubwa kuliko ya kwanza, alifungua mlango akaingia ndani. Nyuma yake mlango ulifungwa kwa nguvu. Ikibali alinyata mpaka mlangoni akasimama kimya. Alichungulia ndani katika ufa wa mlango akaona ukumbi. Katikati ya ukumbi palikuwa na kitanda kizuri na meza moja. Manyani mawili yaliyofungwa viunoni minyororo ya dhahabu yalikuwa yamelala kitandani. Adili aliweka sinia juu ya meza. Nyani moja lilipofunguliwa lilirukaruka likalialia kinyonge. Adili alilikamata akalifunga miguu ya mbele na ya nyuma kwa kamba. Alipolitupa chini alishika mjeledi kwa mkono wa kulia akalipiga mpaka likazirai. Nyani jingine lilipigwa likazirai vile vile. Manyani yalipozinduka yalinasihiwa. Adili aliapa kuwa hakufurahi kuyaadhibu, na kwamba alitazamia faraja yao kutokea karibu.

Sasa manyani yalichukuliwa mezani kula chakula kwa vijiko na nyuma. Yaliposhiba yalinyweshwa maji. Midomo yao ilifutwa kwa leso za hariri. Kisha yalifungwa minyororo kama yalivyokuwa. Mambo haya yalipotendeka Ikibali alikuwa amesimama kimya anachungulia. Adili Alipokusanya vyombo ili atoke nje, Ikibali alitangulia kuondoka mlangoni. Alikwenda mpaka kitandani pake akajilaza kimya kama aliyekuwa hajui lililotokea. Kitambo kidogo Adili alirudi akaweka mjeledi na mshumaa bwetani. Hakushuku neno, na baada ya kuvua nguo zake alilala tena. Lakini tangu wakati ule mpaka asubuhi, Ikibali hakupata usingizi kwa mawazo mbalimbali. Kila njia ya fikra aliyokwenda haikumfikisha katika tafsiri ya mwujiza ule. Adili Alikuwa mtu wa maana. Hakutazamiwa kufanya ukatili kwa wanyama.

Mwenyeji na mgeni waliondoka vitandani. Baada ya kuoga na kuvaa walikwenda sebuleni kustaftahi. Walipokwisha walikwenda mazizini kutazama wanyama waliokusanywa. Siku ile moyo wa Ikibali ulikuwa mzito kwa mawazo, lakini hakuuliza neno juu ya siri aliyogundua. Ilikaa moyoni mwake mwenyewe. Siku ya pili , usiku wa manane vile vile, Adili alifanya tena mambo aliyofanya jana. Siku ya tatu mambo yalikuwa yaleyale. Katika muda huu wote Ikibali hakuacha siku hata moja kumfuata na kutazama matendo yake. Siku ya nne alipewa hesabu aliyojia akarudi ughaibu. Kwa kesha ya siku tatu hakuweza kuongoza vema farasi kwa usingizi. Laiti asingalikuwa mzoefu wa kupanda farasi angalitupwa chini njiani amelala.

Alipofika Ughaibu alitoa habari za ujumbe wake. Alitaka sana kuficha siri ya manyani ya Adili na adhabu yao, lakini hakuweza. Alifikiri kama Adili aliyaadhibu kwa ukatili tu asingalijisumbua kuyafuga, kuyalisha na kuyanasihi. Mtu hawezi kutunza kitu asichokijali. Zaidi ya umahiri, werevu na usuluhifu, Ikibali aliweza kufahamu upande wa pili wa neno. Aliona dhahiri kuwa Adili hakupenda adhabu ile kuendelea. Kama aliitenda kwa kulazimishwa alikuwa na haki ya kusaidiwa. Yamkini mfalme aliweza kumsaidia. Kwa sababu hii alitoa siri aliyokuwa nayo. Rai aliposikia nywele zake zilisimama kichwani, na damu yake ikasisimka mwilini. Ikibali alitumwa tena Janibu kumleta Adili pamoja na manyani yake mbele ya mfalme. 

Post a Comment

Previous Post Next Post