MFALME RAI 11

ADILI NA NDUGUZE 

Wokovu wa Adili

Adili alipotupwa alizama kama jiwe katika kilindi cha bahari ambacho urefu wake haukutambulikana. Viwambo vya masikio yake vililia akadhani maji yalipenya sikio hata sikio, na mianzi ya pua yake ilijaa maji yaliyozuia pumzi. Macho yake yalipofumbuka vimemeta kama nyota mbinguni vilionekana katika maji, vimemeta hivyo vilifanywa na mtikiso wa mwili wake. Kutumbukia baharini usiku wa giza ni hatari ya kutisha sana.

Kasi ya kutupwa ilipokoma alijitatamua akakata vifungo vya kamba iliyokatizwa mwilini mwake. Sasa mikono na miguu yake ilianza kufanya kazi. Nusu ya nguvu yake ilikuwa imetumika, lakini matumaini yake yalikuwa kamili. Adili alikuwa si mkata tamaa, na kabla pumzi yake haijakwisha alikusudia kuebuka. Jaribu lake lilikutana na fanaka, maana kabla moyo wake haujakoma alijiona anaelea juu ya bahari. Aliinua kichwa juu ya maji akahema kwa nguvu kama gari moshi. Kulipopambazuka alikuwa katika bahari iliyoghadhibika kwa dhoruba kali, na hali yake ilikuwa taabani. Kutazama hatari usoni kunavunja moyo wa mtu lakini alijikaza kiume.

Mara ile palikuja ndege aliyekuwa na umbo la kutisha akamwopoa Adili majini. Kama koleo, miguu ya ndege ilimshika kwapani akaruka naye. Fikiri wewe mwenyewe hofu aliyokuwa nayo Adili. Binafsi yake alijiona ameokoka kuliwa na papa akawa chakula cha tai. Ndege mwenyewe alipaa juu mpaka Adili alipotelewa na fahamu. Fahamu yake ilipomrudia alijiona katika nyumba kubwa sana iliyokuwa nzuri ajabu. Wasichana warembo na walio changamka walikuwa watumishi katika nyumba hiyo . Miongoni mwao palikuwa na bibi mmoja aliyejipambanua kama malkia, huyo alikaa juu ya kiti cha enzi kilichopambwa na majohari mbalimbali. Rangi ya mavazi yake ilikuwa fua, na kichwani alivaa taji lililopigisha moyo mshindo kwa uzuri.Yule ndege alikuwapo, lakini mara ile alijigeuza msichana wa utanashati mkubwa. Msichana mwenyewe alikuwa yule aliyezama ardhini, baada ya kuokolewa na Adili, alipokuwa katika umbo la tandu na kushambuliwa na nyoka jabalini.

Malkia alimwuliza msichana mtu aliyemwokoa baharini alikuwa nani, na kwa nini aliletwa mbele yake.

Msichana alieleza kuwa mtu yule alikuwa mfadhili wake mkubwa. Zamani maisha yake yalipokuwa katika hatari ya nyoka alipata wokovu kwake. Alimwokoa na kumleta mbele yake kwa sababu aliahidi kulipa fadhili yake.

Kusikia vile, Malkia alisimama akampa mkono Adili aliyeupokea huku amepiga magoti chini. Malkia alimwinua akamkaribisha kuketi kitini akisema, "Starehe, mwanangu. Hali yako ni hali yetu".

Kisha msichana alimwuliza Adili kama aliweza kumtambua yeye alikuwa nani. Adili alijibu kuwa hakuweza.

Msichana alieleza kuwa yeye alikuwa tandu katika jabali fulani zamani akakaribia kuuwawa na nyoka, lakini aliokolewa.

Adili alikubali kuwa alikumbuka kuona tandu jeupe, nyoka mweusi, na msichana aliyezama ardhini.

Tandu lilikuwa yule msichana. Naye alikuwa Huria binti Kisasi. Kisasi alikuwa mfalme wa Majini. Aliyekaa kitini alikuwa mama yake. Jina lake lilikuwa Mjeledi, Malkia wa Majini. Nyoka aliyepigana naye Huria alikuwa waziri wa Ngazi. Alijulikana kwa jina la Hunde. Hunde alikuwa kiumbe cha mwisho katika wanaume waliokuwa na sura mbaya. Siku moja katika matembezi Huria alikutana na Hunde. Alikuwa hatazamiki kwa ubaya, licha ya yeye kumtazama mtu. Pale pale Hunde aliingiwa na shauku kubwa juu ya Huria. Wanawake hukutana na mikasa mingi mibaya duniani. Mioyo yao hulemewa na haja zisizokubalika; masikio yao hutiwa uziwi kwa maombi ya haraka; na miili yao ni mawindo ya jeuri daima.

Hunde alikwenda kwa Kisasi kumposa Huria. Kisasi alijibu Hunde alikuwa ni sufu kwa binti yake ijapokuwa alikuwa waziri wa Ngazi, na kwamba asingalithubutu mbele yake haja kama ile. Tangu siku ile alikomeshwa tamaa ya kuposa mabinti wafalme. Aliudhika akatisha kumwonyesha Huria uwezo wake. Na tangu alipotisha hivyo hakumpa nafasi hata ya uzi kupenya tundu la sindano.

Kila mahali Huria alipopita , Hunde alifuata nyayo zake mpaka aligundua alikokuwa. Iliendelea hivyo mpaka Kisasi akapigana naye. Alishindwa akakimbia. Huria alipotaka kutembea alijigeuza umbo la mnyama. Kila alipojigeuza na yeye alijigeuza vile vile akanusa harufu yake kama mbwa. Alipojigeuza panya, yeye alikuwa paka, alipojifanya paka, yeye alijigeuza chui; na alipokuwa chui, yeye akawa simba. Kila alipoingia yeye alipajua kwa kufuata nyayo zake. Wanaume wana inda mbaya ufisadi unapowapofusha.

Siku aliyojigeuza tandu , yeye alikuwa nyoka akamfukuza. Alipochoka kukimbia alimkamata. Kabla hajamhasiri, Adili alimpiga jiwe akafa. Alijigeuza mtu akaonekana na Adili kwa macho yake. Kabla ya kujizamisha chini aliahidi kulipa wema kwa Adili.

Huria aliomba dua siku zote ya kuweza kutimiza ahadi yake kwa Adili. Siku aliyotoswa baharini na ndugu zake alikuja upesi kumwokoa katika hatari. Ilipasa wazazi wake, Mfalme na Malkia wa Majini kumkirimu mfadhili wake.

Alimwambia mama yake kwa deni alilowiwa na Adili lilikuwa kubwa sana. Hakudai lilipwe lote lakini lipunguzwe kama lilivyowezekana.

Mjeledi alimwambia Adili kuwa wema wake haukuoza. Kwa kumwokoa Huria aliwatendea wazazi wake fadhili na heshima kubwa nchi ya Majini. Ilikuwa zamu yao kumkirimu walivyoweza sasa.

Adili aliyenyamaza kwa muda mrefu alijibu, "Deni langu limekwisha lipwa lote. Niliokoa maisha ya binti yako, naye ameokoa yangu. Hapana deni tena kati yetu."

Malkia wa Majini alitabasamu akasema, "Usiseme kikembe mwanangu. Wema wako ulikuwa asilia, nawe ulitangulia kuutenda; wa binti yangu ulikuwa wa kuigiza, naye ameutenda nyuma. Asili na uigaji ni vitu mbalimbali. Havilinganiki wala havitalinganika milele."

Adili alipelekwa katika hazina ya majini iliyokusanya utajiri wote wa ulimwengu. Johari ndogo katika hazina hiyo ilikuwa na uzito usiochukulika kwa Adili. Alipochaguzwa kuchukua alichopenda hakuweza kuchagua kitu chochote.

Malkia alisikitika akasema, "Haidhuru!" Alishika simu akauliza" Naweza kusema na mfalme wa majini?"

Jibu lilikuja , " Naam, Kisasi huyu! Nani mwenzangu?" " Mjeledi , Malkia wa majini ndiye asemaye. Adili amechaguzwa apendacho katika hazina yetu, lakini ameshindwa kuchukua hata kitu cha uzito wa sindano moja. Wanadamu hawajaweza kutumia uwezo waliopewa kama Majini. Nataka msaada wako."

" Vema. Mlete hapa," kengele iliishilia.

Adili alikwenda katika halmashauri ya Majini. Alipofika mfalme alikuwa amekaa kitini kwa juu kuelekea hadhara kubwa ya mawaziri. Joho la mfalme lilikuwa la rangi ya fua, na kichwani alivaa taji la zari. Mawaziri walivaa majoho meusi, na vichwa vyao vilikuwa wazi. Hadhara nzima ilisimama Adili alipotokeza . Ilipokaa kitako tena alipewa kitabu cha hawala ya hazina ya majini. Kwa kila hawala iliyoandikwa na kutiwa sahihi ilipochomwa Adili aliweza kupata alichotaka katika hazina ya majini. Alifurahi kwa zawadi ile. Ilikuwa nyepesi kuwekeka, rahisi kutumika, nayo si nzito kuchukulika. Alimshukuru mfalme wa majini akarudi kwa Huria.

Adili aliyageukia Manyani akauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea . Manyani yaliziba nyuso zao kwa viganja vya mikono yao kwa aibu. 

Post a Comment

Previous Post Next Post