ADILI NA NDUGUZE
Nduguze kuwa Manyani
Baada ya Adili kutoswa, nahodha alishtuka akauliza nini kilichotumbukia baharini kwa kishindo kikubwa. Kusikia vile ndugu zake walianza kujiliza uongo kuwa ndugu yao amepotea. Nahodha alikwenda kutazama akaona Adili hayuko. Aliamuru kutua tanga na kuteremsha mashua. Lakini sasa dhoruba kali ilianza, na chombo kilichokuwa katika mrama mkubwa, kwa mawimbi makubwa ya upepo na umande, kilipakia maji, omo na tezi, na kulia na kushoto. Giza kuu lilinyemelea roho za mabaharia. Palikuwa hapatiliki nanga. Kwa hivi tamaa ya kumuokoa Adili ilikatika.
Nahodha alipotaka kujua Adili alivyopotea, ndugu zake walimwambia kuwa ndugu yao aliamka akaenda msalani. Ghafula walisikia anguko kubwa majini. Watu wote jahazini walisikitika kupotelewa na Adili. Ndugu zake walilizana kitambo wakanyamaza. Kilio cha kujisingizia hakina machozi wala matanga.
Hasidi na Mwivu walichukua sanduku la Adili wakalifungua. Walitoa majohari yote wakagawana mafungu mawili usiku ule ule. Sasa ugomvi kati yao ulianza juu ya yule msichana mzuri aliyekuwa chomboni. Hasidi alitaka kumwoa, na Mwivu kadhalika alitaka kumwoa. Asiyefurahia heri ya mwenziwe, shari yake kumghadhibikia. Walimsahau ndugu yao aliyepotea dakika chache zilizopita kama aliyekufa miaka kumi iliyopita. Walikuwa na mioyo migumu iliyoje!
Mwelekevu, yule msichana mzuri, alikuwa hana tabasamu. Uzuri wake ulisawazika kwa machozi ya njia mbili usoni. Huzuni ilimshika vibaya, lakini alikuwa imara kutetea heshima yake. Aliwaambia wale ndugu wawili wasigombane bure. Hakuwa tayari kuolewa na yeyote kati yao. Na kabla ya sauti ya maneno aliyosema haijaishilia masikioni mwao, alijitosa baharini akatoweka vile vile.
Hasidi na Mwivu hawakujua la kutenda. Atakaye makaa ya mgomba hapati kitu ila jivu tupu. Ndugu hawa wawili walimtosa ndugu yao kwa tamaa ya kupata msichana , lakini walipata aibu tupu. Walikaa kitako wamefedheheka, walipokuwa katika hali hiyo na jahazi inakwenda mbio, Huria na Adili walitua ghafula kama ndege chomboni.
Marejeo ya Adili yalishangaza watu chomboni. Macho ya ndugu zake yalisutana. Kwa kutahamaki walimkumbatia wakajifanya kumfariji. Walisema hatari yake ilitisha, na msiba wao ulikuwa mkubwa. Watu wengine wote chomboni waligeuza macho yao kando waliposikia uongo wa ndugu zake. Walakini Adili aliwashukuru akisema bahari haiweki amana ya kitu kieleacho, kwa kuwa alielea aliokoka.
Kwa hasira kubwa Huria alinena, "kama mngalijua hatari ya kumtosa mtu baharini, au mngalikuwa na fikira za msiba, msingalijaribu kumtumbukiza ndugu yenu baharini alipolala. Wauaji ninyi hamstahili kuishi," aliwashika shingoni pamoja na mkono wa kushoto akawabana kwa nguvu ya ajabu. Mkono wake wa kulia uliinua ngumi juu tayari kuwaangukia kwa uzito mwingi. Ndimi vinywani na mboni machoni mwao zilitoka kwa hofu wakataka kuombewa.
Damu nzito kuliko maji. Hasidi na Mwivu walikuwa damu kwa Adili . Hakuvumilia kuona hilaki yao akamwomba Huria kuwasamehe. Walimtosa tu, hawakumwua. Huria alibisha kuwa walistahili kifo. Jaribu la jinai lilitosha kuhalalisha adhabu ya kifo ujinini. Adili alitaradhia kuwa jaribu la jinai halikutosha kuhalalisha kifo duniani. Kama walikufa kwa sababu yake angalikuwa mnyama wa mwitu mbele ya macho ya watu. Huria aliposikia maneno hayo alinena sheria ya wanadamu ilitatiza. Kwa sababu hiyo walikuwa hatarini milele. Walakini alikubali kuwasamehe kwa sharti ya kuwageuza wanyama. Aliwalaani watoke katika umbo la uanadamu. Mara ile ndugu zake walikuwa manyani.
Kisha Huria aliwakabili watu waliokuwa chomboni akasema. Adili alikuwa rafiki yake mkubwa. Alimjali na kumheshimu juu ya marafiki zake wote. Alipata upendo wake kwa sababu alikuwa salihi na mstahiki wa kuajabiwa na dunia nzima. Ataonana naye mara kwa mara. Mtu yeyote akifitini ataona nguvu ya mkono na uwezo wa ulimi wake. Atampatiliza kama alivyofanya kwa waovu wale wawili. Wajihadhari wapate kujiokoa kwa sababu alikusudia kutimiza alivyosema. Aliwaonya pia watakapofika kwao wasiseme habari ile. Mtu yeyote atakayejaribu kunong'ona habari ile atakoma kusema milele.
Aliagana na Adili akasema, "Funga manyani haya kwa kamba . Ukifika Jannibu utayafunga kwa minyororo viunoni mbalimbali. Utayatia chumbani na kila moja lifungwe peke yake. Kila usiku wa manane utachukua kiboko ukafungue kila nyani ulipige mpaka lizimie. Utayapa posho na kuyaadhibu hivi daima. Kama amri hii haikutiiwa utaadhibiwa wewe." Alipokuwa akitoa amri hii alijibadilisha sura za ajabu kila dakika moja. Watu wote jahazini walishikwa na mshangao mkubwa kwa mabadiliko yake ya mfululizo, wakatosheka kuwa aliweza kubadili kitu chochote katika umbo alilotaka.
Adili aliyageukia manyani akauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea. Manyani yaliziba nyuso kwa viganja vya mikono yao kwa aibu.
Tags:
RIWAYA