MFALME RAI 13

ADILI NA NDUGUZE


Adhabu ya Kwanza.

Baada ya kutoweka kwa Huria. Adili alikwenda ngamani kumtazama Mwerekevu. Hakuona mtu. Alipouliza aliambiwa alijitosa baharini ndugu zake walipomkalifu kumuoa. Adili hakuweza kujizuia, akaanguka chini kwa huzuni. Moyo wake ulifumwa kwa msiba akalia kama mtoto mdogo.

Uzuri aliotetea kwa thamani ya maisha yake ulipotea. Aliona wokovu wake haukumfaidia. Bahati ilikuwa mbaya na katili sana kwake. Alifikiri kwamba yeye peke yake ndiye aliyepatwa na ajali mbaya kama ile tangu kuumbwa kwa dunia. Adili aliwaza hivyo, haijulikani mtu mwingine angewazaje.

Kulipokucha chombo chao kilitia nanga Janibu. Matajiri walipanda chomboni wakaamkiana na Adili. Walizungumza mambo mengi, lakini hapakuwa na mtu hata mmoja aliyeuliza habari za ndugu zake. Hili lilimshangaza akamaizi kuwa walio aili walikuwa hawana nafasi katika kumbukumbu za dunia.

Alishuka pamoja na manyani yake akaenda zake nyumbani kwake. Baada ya kuyaweka chumbani alijishughulisha na kupakuwa mali yake. Hakuwahi kutafuta minyororo ya manyani siku ile, na usiku alisahau kuyapiga akalala. Saa saba usiku Huria alitokea na hasira imemjaa tele. Alisema kuwa alikuwa jini. Neno la jini halirudi. Kwa kukosa kutii amri yake adhabu ya kwanza ilimpasa Adili.

Kabla Adili hajajibu neno, mikono yake miwili ilikuwa katika mkono wa kushoto wa Huria. Hakuweza kuponyoka. Kwa mkono wa kulia Huria alimpiga Adili kibao mpaka akazimia. Ndipo alipokwenda yalipokuwa manyani akiyapiga kiboko vile vile mpaka yakakaribia kufa.

Alimrudia Adili aliyekuwa anaanza kupata fahamu akasema, “Twaa kiboko hiki, utayapiga manyani haya kesho usiku kama nilivyofanya. Siku moja ikipita bila kuyapiga, kiboko hiki kitaishia mwilini mwako.” Macheche ya moto yalitoka kinywani mwake alipokuwa akiamuru hili, na mara neno la mwisho lilipotamkwa alitoweka.

Siku iliyofuata Adili alikwenda kwa sonara akatengeneza minyororo miwili ya dhahabu. Aliileta nyumbani mwake akaifunga viunoni mwa manyani yake. Usiku alipokwenda kuyapiga na kuyaposha machozi yalimlengalenga machoni.

Katika ini alifumwa na mshale, na moyoni mwake michomo ya maumivu makali. Hakupendelea kuadhibu wanyama waliokuwa kwanza ndugu zake. Huruma yake ilikuwa lakini ilikalifiwa na amri.

Huria alijua huruma ya Adili na kuwa alimkalifu sana. Lakini ndugu zake walikuwa waovu, katili, hiani na wauwaji wa kutisha. Walikosa fikra wakawa duni Kama wanyama wa porini. Adhabu kali kwa waovu ilikuwa ndiyo ulinzi peke yake ya wema. Jini ililiona hivyo, haijulikani mtu angalionaje.

Siku nyingi zilipita, Adili alidhani labda adhabu ya Huria ilikwisha. Siku moja hakuyapiga manyani yake. Loh salale! Dhahama gani? Alijuta kuzaliwa akatamani ardhi ipasuke ajitie ndani yake. Alipigwa kiboko siku hiyo kuliko siku ya kwanza. Mwili wote ulienea makato ya kiboko akavuja damu mpaka akazirai.

Aliteremsha mavazi aliyovaa mpaka kiunoni akaonesha makovu ya mapigo ya Huria. Wepesi wa maumbile wa kuondoa alama haukuweza kufuta makovu ya Adili. Yalijionyesha wazi wazi mwilini mwake.

Toka siku ile na baadaye, hakusahau maumivu ya mapigo yale. Kwa muda wa miaka kumi hapakupita tena hata siku moja aliyoacha kuyapiga manyani yake. Kwa huruma yake kila baada ya kuyapiga aliyanasihi akilia:-

“Nala sumu ndugu zangu
msambe naona tamu,
Takalifu kubwa kwangu,
Kuadhibu yangu damu,
Sina raha ndugu zangu,
Neno hili kwangu gumu.”

Mwisho wa ushahidi, Adili aliyageukia manyani akauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea.
Manyani yalijiziba nyuso kwa viganja vya mikono yao kwa aibu 

Post a Comment

Previous Post Next Post