ADILI NA NDUGUZE
HARUSI
Adili alipolala mtingisho mkubwa ulitokea chumbani mwake sakafu ikapasuka. Kuzinduka uso wake ulikutana na uso wa Huria. Wa kwanza ulijaa matumaini, wa pili ulituna kwa hasira. Nyuso zao zilisomana. Kila uso ulijaribu kuzua mzungu wake.
Adili alivunja amri aliyopewa mara tatu. Alionekana alizoea kuhalifu. Kukomeshwa mazoea yake alipasa kugeuzwa nyani kama ndugu zake. Walakini, kabla ya hili kuwa Huria alitaka kusikia kama Adili alikuwa na udhuru wa kujitetea.
Adili hakusema, lakini tabasamu ya mvuto mwingi ilikuwa ikicheza usoni mwake. Alichukua barua ya Rai akampa Huria. Huria aliposoma barua hakuweza kufanya alilokusudia. Alitoweka akaenda ujinini kumshauri baba yake.
Barua ya Rai ilipowekwa mbele ya Kisasi, kuopolewa kwa ndugu zake Adili kuliridhiwa. Huria alimwuliza Mfalme wa majini labda haja ya Mfalme wa wanadamu isingakubaliwa ingalikuwaje. Baba alieleza.
Mfalme wa wanadamu aliweza kufanya dhara aliyotaka kwa majini. Alikuwa mwanadamu. Mwanadamu alikuwa bora kuliko jini. Majini katika Jua, Mwezi, Mushtara, Zebaki, Zuhura, Mirihi, Sumbla, Zohali, Sarateni, Kausi na Utaridi hayakuweza kushindana na watu katika ardhi.
Majini yaliweza kugeuza watu katika umbo lolote, lakini watu waliweza kufunga majini yote katika chupa moja. Magereza yao yalikuwa mabaya sana. Kama mtu asingalikuwa mzembe mwenyewe, busara ya jini ingalikuwa busara yake. Alipasa kuheshimiwa kama alitaradhia heshima yake.
Mara ile Huria alirudi kwa Adili akatangaza kuwa haja ya Rai ilifaulu. Mfalme wa majini alikubali ndugu zake kuwa watu tena.
Aliyabadili manyani akasema, “Tokeni katika uhayawani mrudi katika utu.” Walikuwa watu tena, wakajiangusha miguuni mwa ndugu yao kuomba radhi. Adili alimshukuru Huria, na punde wakaagana.
Asubuhi watumishi walimwona bwana wao na watu wawili. Waliwatambua kuwa walikuwa ndugu zake. Walipouliza kuwa walikuwa wapi kwa muda mrefu, bwana alijibu kuwa walikuwa manyani yaliyoonekana jana yakila naye. Walifurahi kumuona bwana wao si mkichaa, wakamwombea azidishiwe furaha katika maisha yake.
Baada ya kustaftahi aliwavika ndugu zake nguo ali ali, akapanda nao farasi kwenda Ughaibuni. Liwali Adili alipofika Ughaibu na habari kuwa manyani yake yalikuwa watu tena palikuwa na furaha kubwa sana. Jitihadi na kufaulu kwa Rai kuliandikwa katika kumbukumbu za dunia. Hasidi na Mvivu walipoletwa barazani kila mtu aliajabia sura zao. Walikuwa wazuri ajabu.
Mfalme wa Ughaibu alimsifu Adili kuwa alikuwa sababu kubwa ya wokovu kwa ndugu zake katika dhima ya wanyama.
Mateso yaliyompata yalishinda uvumilivu wa mtu. Alivumilia mateso mengi kwa ajili yao. Alikuwa mwanamume barabara na fahari ya Ughaibu. Nchi yake ilimsifu hivi, haijulikani nchi yangu au yako ingalimsifiaje mtu wa namna ile.
Alipogeuka kwa ndugu zake Adili, Rai alionya kama wavivu wajitahidi kuwa hodari, ilikuwa kinyume hodari kuwa mvivu. Kama waovu walitaka kuwa wema, ilichukiza wema kuwa waovu. Kama masikini walitafuta utajiri, ilikuwa ujinga matajiri kufuja walichokuwa nacho. Kama mbegu kidogo iliongezwa mchanga, ilikuwa uharabu mtu kuua ndugu yake. Pia ilikuwa aibu kubwa sana kwa wazuri kutenda maovu.
Wakamilifu walikuwa na nafasi kubwa duniani kuliko wapungufu. Maonyo ya Mfalme yalikuwa mwanana, lakini yalishinda mioyo ya watu waliokusudiwa kuonywa.
Walimshukuru wakaahidi kuwa walikoma kutenda dhara kwa ndugu yao, na kwa kitu chochote kilichokuwa na maisha. Ahadi hii haikuvunjwa.
Mawe huwa dhahabu,
au johari na chuma.
Na mtu anapotubu,
dhambi yake kukoma.
Nidhani zake thawabu,
na heshima ya daima.
Adili alipanda farasi akarudi Janibu na ndugu zake. Njiani alikutana na mabibi watatu waliopanda farasi vile vile.
Mabibi wenyewe walikuwa wazuri na watanashati sana. Wa kwanza alikuwa Mwelekevu aliyeokolewa na Mrefu. Macho ya Adili na ya Mwelekevu yalipokutana mioyo ya giza ilijaa nuru tena. Wote wawili walishuka chini wakaamkiana.
Aha, ilikuwa furaha kubwa iliyoje! Mioyo miwili ya mapenzi iliyopoteana ilikutana tena. Neno halikuwezekana kusemeka. Walitazamana wakachekana. Walishikana mikono wakabusiana. Walikuwa katika siku bora ya maisha yao.
Adili alipomwambia Mwelekevu kuwa wavulana wawili watanashati aliokuwa nao walikuwa ndugu zake, Mwelekevu kadhalika alisema kuwa wasichana wawili warembo aliofuatana nao walikuwa marafiki zake.
Watu wote wanne walishuka chini wakaamkiana vile vile. Kisha wote walipanda farasi wao wakashika njia kuelekea Janibu.
Walipofika palifanywa harusi tatu siku moja. Siku hiyo ilikuwa kubwa kuliko yoyote iliyopita Janibu....MWISHOOOOO
Tags:
RIWAYA