TROPEA - Mji wa wafu. SEHEMU YA 02

ILIPOISHIA....... 

.....kweli wanakijiji wakafungua milango ya nyumba zao lakini maajabu yakawa bado yanaendelea kwani wanakijiji waliotoka katika majumba yao hawakuwa binadamu, dhahiri shahili kwa macho yangu niliwaona wakitoka damu midomoni mwao huku wakijongea mahali nilipo simama kwa mwendo wa kusafa. 

ENDELEA NAYO....... 

Nilizidi kuogopa, kijasho chembamba kikanichwea wakati huo yule Ajuza aliendelea kuangua kicheko japo sauti yake haikutanabaisha na muonekano aliokuwa nao. Punde si punde kicheko kile kilipotea na wale wanakijiji nao walipotea kimaajabu nikabaki sasa mimi na yule Ajuza ambapo aliniambia "Bingo najua tabu unazozipata wewe na mama yako lakini tambua msaada umepatikana endapo kama utakubaliana na masharti nitakayo kwambia". 

Maneno hayo ya Ajuza yalimshtua Bingo, kwa hamaki kubwa akamuuliza 

"Masharti gani na huo msaada unahusu nini?.." 

"Ahahah aha", kwa mara nyingine tena Ajuza huyo wa ajabu aliangua kicheko, baada ya kukatisha cheko lake akasema "Dawa ipo, dawa ambayo itamrudisha mama yako katika hali yake ya kawaida, lakini kuipata kwake dawa hiyo inahitaji moyo ili kufika huko ilipo..". 

"Ipo wapi?..", alirudi kuhoji Bingo. 

"Ipo Tropea! Mji uishio wafu itakulazimu ufe ili kufika huko" alijibu Ajuza, maneno hayo yalisikika kwa kujirudia mara mbili mbili mithili ya mwangwi. 

"Nife? Halafu nikisha kufa?..", kwa mashaka Bingo aliuza tena, lakini kabla Ajuza hajajibu swali hilo, ghafla Bingo alisikia sauti ikimuita. Sauti hiyo ilipaza mara nne, mara ya tano Bingo aliitika kitendo ambacho kilimpelekea kutoka usingizini. Alistaajabu sana kujikuta yupo kitandani. "Mungu wangu, kumbe ni ndoto? Inamaana gani ndoto hii?.., akiwa na wingi wa hofu alijiuliza wakati huo mapigo ya moyo wake yakienda kasi mithili ya saa mbovu. 

Nje sauti ile bado iliendelea kumuita, alinyanyuka akakutoka kitandani, akavaa nguo haraka haraka kisha akatii wito. Alipofika mlangoni alikutana na uso wa Bi Mboni. Bibi yule ambaye alipata kumuota kwenye ndoto. Hali hiyo ilimfanya Bingo kuinamisha uso wake chini kitendo ambacho kilimtia shaka Bi Mboni. Bibi huyo alitambua fika maisha ya kijana Bingo, hivyo kinywa chake hakikuwa kizito kumuuliza kinacho msibu. 

" Hakuna shaka bibi", alijibu Bingo huku uso wake kwa mbali akiachia tabasamu hafifu lenye kitu fulani ndani yake.

"Mama anaendeleaje?..", aliongeza kusema Bi. Mboni. 

"Hivyo hivyo tunamshukuru Mungu"

"Sawa, mguu huu ni wako bwana Bingo" aliongezea kusema Bi. Mboni.  

Bingo akakunjia mikono yake kwenye kifua akatega masikio yake vyema kumsikiliza kikongwe huyo anakipi cha kumwambia asubuhi hiyo. 

"Ndio nipe maisha" 

"Nina sehemu yapata nusu tu nataka unilimie, nimetumiwa pesa na mwanangu kwahiyo nimeona bora niweke kibarua ili anisaidie. Nimeona wewe ndio mtu sahihi kabisa", Bingo alifurahi kusikia habari hiyo, hayo ndio yalikuwa maisha yake. 

"Na ningependa kesho uanze kwa maana siku yoyote mvua inaweza kunyesha", aliendelea kusema Bi Mboni. 

"Hilo ondoa shaka, umefika hapa kwa Bingo Alwatan kiboko wa ardhi. Kesho kutwa nakukabidhi shamba lako", alijibu Bingo huku akijiamini.

Bibi huyo hakuwa na la ziada, aliondoka zake huku akimsisitiza kijana Bingo kufika shambani kwake pasipo kukosa. Baada ya hayo alirejea chumbuni kwake, aliketi kitandani sambamba na kushusha pumzi ndefu huku ubongo wake ukijaribu kuikumbuka ndoto ile aliyoota. Hakika ni ndoto ambayo ilimuacha mdomo wazi na kushindwa kufahamu ndoto ile inamaana gani.

Siku hiyo ilikuwa ni siku ya tofauti kwake, aliumiza kichwa juu ya kuwaza ile ndoto ya ajabu. Alishindwa kutambua inamaana gani jambo ambalo lilimfanya kushusha pumzi mara kwa mara huku akisitisha kulima nakisha kupumzika kwa dakika kadhaa ilihali kichwa chake akikipa majukumu ya kuidadavua ndoto ile. 

"Ipo Tropea! Mji uishio wafu itakulazimu ufe ili kufika huko", maneno yale ya Ajuza aliyemtokea kwenye ndoto yalijirudia kichwani kwa Bingo, ndipo kwa mara nyingine tena akaishusha pumzi yake kisha akaendelea kulima ingawa kichwa chake bado hakikuwa sawa lakini wakati yupo kwenye hali hiyo, mara ghafla alisikia sauti ikimuita. Sauti hiyo iliyokuwa ikimuita ilitokea nyuma yake, ni sauti ambayo ilimshtua sana kwani aliifahamu fika sauti hiyo kabla hata hajageuka kule ilipokuwa ikitokea.  

"Bingo Bingo Bingo, habari yako", ilisema sauti hiyo, Bingo akiwa na hali ya taharuki aligeuka nyuma yake ili ajue kama ndio yeye mtu anayemdhania ingawa mtu huyo miaka kadhaa imepita tangu afariki. Ajabu alikutana na mtu tofauti na yule aliyemfikiria, ni mwanadada mrembo mwenye umbile refu na mweupe mithili ya muarabu, nywere zake za singa wakati huo huo kifuani alikuwa amevaa mikufu ya dhahabu na mkononi akiwa na bangili. alikuwa mrembo ambaye alionyesha tabasamu muda wote. 

Bingo alizidi kutaharuki, upesi alitupa jembe chini huku akionyesha kumuogopa mrembo huyo. 

"Wewe ni nani?", aliuliza Bingo kwa sauti ya woga, hasa hasa akiamini kabisa msichana mrembo wa namna hiyo ni nadra kuonekana vijijini, mawazo yake yaliamini kuwa mwanadada huyo sio binadamu wa kawaida. 

"Ahahahahha", alicheka mwandada huyo wakati huo huo akimsogelea Bingo kijana aliyeonekana kuhaha kwa woga. Alipomkaribia alimtazama usoni, akaachia tabasamu bashasha na akasema "Bingo, naitwa Roya, tukutane Tropea", alipokwisha kusema hayo mwadada huyo aliyejitambulisha kwa jina Roya alipotea ikasalia vumbi. 

Bingo alipiga mayowe akatimua mbio huku akipaza sauti ya kuomba msaada. Alipofika mbali na mahali pale alipotokewa na Mwanadada Roya, alisimama. Ghafla akaanza kuiamini ndoto ile aliyoitoa kuwa inaukweli ndani yake. Maneno ya Roya yalimfanya kuamini kwamba ipo siku atafika Tropea mji uishio wafu, jambo ambalo lilimpelekea Bingo kupata tumbo joto hasa hasa baada kukumbuka kuwa kwenye ndoto Ajuza alimueleza kuwa ili kufika katika mji huo inamlazimu afe kwanza.

Suala hilo la kufa lilimchanganya kabisa Bingo kiasi kwamba akaanza kujiona ni mfu aliye hai, mbali na lile tukio la kutokewa na Roya vile vile siku kadhaa mbele alitokewa na mtu mwingine wa ajabu ambaye alionekana sehemu mbali mbali za mwili wake akiwa anaumbile la nyoka ingawa miguu yake ikiwa kwato za mbuzi. 

Mtu au kiumbe hicho cha ajabu, alikutana naye saa ile ile ya jioni akiwa ametoka porini kukagua mitego yake. Wakati yupo njiani anarudi nyumbani huku akifurahi kupata kitoweo, ghafla aliguswa bega lake la kushoto. Upesi akageuka, alishtuka kumuona mwenye umbile hilo la kutisha. Aliogopa, akiwa na wingi wa hofu alimkodolea macho mtu huyo ambaye naye muda huo aliangua kicheko. Cheko la kutisha ambalo lilienda sambamba na mwangwi, punde si punde mtu huyo au kiumbe hicho kikatoweka ikasikika kisha sauti nene ikapasa ikisema "Bingo Bingo njoo Tropeaaaaa", sauti hiyo ikamaliza kicheko kizito.   

Alipagawa Bingo, ile imani ya kujiona mfu aliye hai iliendelea kuota mizizi ambayo ilionyesha kukomaa haswa. 

Maisha hayo ya kukumbana na mauza uza ya kukutana na watu wa ajabu ajabu katu hayakuweza kupotea, alizidi kuandamwa na mauza uza hayo mpaka kupelekea kuonekana kituko kwa wanakijiji kwao. 

Jioni moja vijana wa kijiji walimjadili "Jamani hivi siku hizi Bingo mnamuelewa kweli?..", sauti ya kijana mmoja aliwauliza vijana wenzake wakiwa kijiweni saa ya jioni. Zogo hilo lilikwenda sambamba na chai ya tangawizi pamoja na vitumbua. Hakika kijiwe hicho kilionekana kuchangamka haswa. 

"Hapana hata simuelewi kiukweli, yaani Bingo amekuwa kama mwendawazimu kila mara utamuona anakimbia kimbia. Mara anasema anaona watu wa ajabu ajabu. Hivi yupo sawa kweli yule jamaa?" Kijana wa pili alidakia. 

Muda huo huo kijana watatu naye alisema "Bingo ni kijana mwenzetu ni mwanakijiji mwenzetu kinachotakiwa sisi kama kumfuata tumuulize ni kipi kinacho msibu mpaka kupelekea aonekane kituko hapa kijijini" 

"Kabisa, wewe umesema jamboy zuri lakini mbali na hilo la kumdadisi ili kujua kinacho msibu, vile vile inatakiwa tumchangie pesa ili tumtafutie shamba. Bingo kawa kama punda hapa kijijini, amekuwa mtu wa kulima vibarua tu wakati kuna wanakijiji humu wanamiliki mashamba mengi kiwango kwamba mengine hawayafanyii kazi" Aliunga mkono na kisha naye kusema ya moyoni kijana huyo wa nne.   

"Hala hala mti na macho", sauti iliyoambatana na kikohozi cha kubanja kilisikika. Punde akatokea mzee mmoja wa makamo kilingeni hapo. Mzee huyo aliitwa Ndelo. Mzee huyo aliketi kwenye benchi, akahitaji kupatiwa chai ili apashe koo jioni hiyo. Alipopewa akanywa kwa kupuliza kisha akakiweka chini kikombe.  
"Nimeyasikia maongezi yenu, lakini niwahakikishie mnajitafutia matatizo endapo kama mtalifanya hilo mlilo lipanga" Alisema mzee Ndelo.

Maneno hayo yaliwashtua sana vijana hao, mioyo yao ikawa na shauku kuu ya kutaka kujua anamaanisha nini kusema maneno hayo. 

Mzee huyo alikunywa chai kwa mara nyingine tena, safari hiyo akasindikiza na kitumbua. Akatafuna akameza kisha akaendelea kusema "Kuna siri kubwa katika familia ile, hivi hamjiulizi kwanini mzee Abacha ameamua kumkimbia mkewe na mwanaye? Mbali na mzee Abacha, hamuoni ndugu nao walipuuzia jambo hilo? Endapo mtayatafakari maswali haya, basi mtaacha kufanya mnacho kifikiria juu ya Bingo" 

"Umetuacha njia panda mzee wetu, tafadhali tuambie ukweli ili tujue" Aliongea kijana mmoja. Punde si punde kijana wa pili akasema. 
"Habari tuliyoisikia ni kwamba mzee Abacha aliamua kumtelekeza mkewe baada kuona ugonjwa alio nao hatopona kamwe" 

"Si kweli" Mzee Ndelo alikataa jambo hilo. 

"Nyie bado vijana wadogo hamjui chochote, na kinacho waponza ni kujifanya mnakijua kitu. Kiujumla hamtaki kukaa na wazee ili mfahamishwe mambo msiyo yajua. Mimi mzee nayajua mwanzo mpaka mwisho matatizo aliyonayo mama Bingo.. Anaitwa Seya, ndilo jina lake baada kuolewa na Abacha walikaa kwa kipindi kirefu pasipo kupata mtoto. Jambo hilo Abacha hakufurahishwa nalo hali iliyopelekea amani kati yao kupotea kabisa " Aliongeza kusema mzee Ndelo, maneno hayo aliyaongea kwa msisitizo mkubwa.

Akapasha koo kwa chai ya tangawizi iliyokuwa ikinogesha zogo kijiweni hapo. Punde si punde akaendelea kuelezea kisa hicho cha miaka mingi iliyopita. Enzi hizo ya ujana baina ya Seya mama Bingo pamoja na Abacha baba yake Bingo. 
         
                 *********

Ndoa ilikuwa ndoano kwa Seya mara tu alipojikuta hana uwezo wa kuzaa yaani tasa, jambo hilo lilipelekea ndoa yao kuzaa migogoro ya hapa na pale ingawaje kwa mara kadhaa mzee Ndelo aliingilia kati kuitatua. Siku moja Seya aliamua kufunga safari kuelekea nyumbani kwao kuomba mawazo kipi afanye ili aweze kuimarisha ndoa yake ambayo ilionekana kujaa migogoro. 

"Ni heri umekuja binti yangu, nafikiri tatizo lako litakwisha haraka sana iwezekanavyo", Jabar, baba yake Seya aliongea baada binti yake kumueleza shida yake. 

"Nisaidie baba yangu, nipo katika wakati mgumu mimi" Alisema Seya kwa sauti iliyo ambatana na kilio. 

"Nimesha kwambia ondoa hofu, mizimu ya ukoo itakusaidia mwanangu" Mzee Jabar akaendelea kumtoa wasi wasi binti yake kisha akamshika mkono wakaelekea kwenye mti mkubwa wa tambiko. Mti mwenye mizimu ya ukoo wao, mizimu ambayo ukieleza shida mbali mbali hutatuliwa. Seya alieongea shida yake chini ya mti huo. Alipohitimisha, ghafla anga likabadilika. Giza totoro likatanda mahali hapo sambamba na miale ya radi pamoja na ngurumo nzito. Seya aliogopa sana kuona kitendo hicho, lakini baba yake alimtoa wasiwasi ikiwa muda huo huo kicheko kizito kilisikika, cheko la kutisha ambalo lilijirudia mara mbili mbili. Punde cheko hilo likatoweka, ikiwa muda huo huo mbele yake Seya kikatokea kibuyu kidogo kilicho pambwa shanga mbali mbali. 

"Seyaaaa..!! Chukua kibuyu hicho" Sauti nzito ya kiume ikamwambia Seya. Kwa hofu na woga, Seya akakichukua. Mara baada kukitwaa mkononi, vicheko vya ajabu vikasikika kwa mara nyingine tena. Punde vikapotea kisha sauti ile ile ikaendelea kusema.

"Seya, ndani ya kibuyu hicho kuna damu. Ondoka nacho mpaka nyumbani kwako, hakikisha hakidondoki chini wala kuonwa na mtu yoyote yule. Ifikapo saa nane usiku, kunywa damu hiyo iliyomo ndani ya kibuyu hicho. Hali yoyote itakayo kutokea kubaliana nayo, vile vile hupaswi kupinga pindi utakapo hitajika kufanya jambo fulani. Sawa sawa?.. " Seya aliitikia kwa woga wakati huo huo sauti hiyo ilitoweka, mwanga uliokuwa umefichwa ukarejea ikiwa ile miale ya radi na ngurumo nazo zikitoweka. Hali ikawa kama hapo awali. Baada ya hayo Seya aliambatana na baba yake kutoka pale kwenye mti wa mzimu ya ukoo wao, mizimu ya Abdi. Hatua kadhaa mbele waliagana, mzee Jabar alirejea nyumbani kwake ikiwa Seya naye alirejea nyumbani kwake kijiji cha pili. Alitembea kwa madaha huku matumaini ya kupata kile alicho kihitaji yalimjaa tele. 

Ule muda ulipo wadia aliamka na kufanya vile mizimu ilivyo mwambia wakati huo mumewe akiwa yupo katika dimbwi zito la usingizi kiasi kwamba hakujua ni kitu gani ambacho mkewe anakifanya usiku huo. Baada kuinywa damu ile, ghafla tumbo likaanza kumuuma, hali ambayo ilidumu kwa takribani dakika kumi na tano. Alisafa akigugumia maumivu, punde si punde akadondoka chini akapoteza fahamu. Akiwa katika hali hiyo, alistaajabu yupo katika ulimwengu mwingine wakati huo kwa mbali zilisikika sauti za nafsi zikilalama.. 

NINI KILICHOJIRI HAPO? TUKUTANE SEHEMU YA TATU YA SIMULIZI YETU YA KUSISIMUA. 

Post a Comment

Previous Post Next Post