TROPEA - Mji wa wafu SEHEMU YA 01



"Mume wangu Bingo, tayari tumefikisha miezi mitatu tangu mimi na wewe tufunge pingu za maisha. Ukweli nafurahia sana uwepo wako katika maisha yangu, na vile vile najivunia kuwa na mwanaume mzuri mkamilifu muaminifu, ukweli uko sawa kwangu lakini licha ya kwamba maisha yetu ya ndoa kuwa yenye furaha na amani ila kuna suala moja ambalo huwa linanitatiza akilini mwangu na nashindwa kulielewa kabisa, hivyo basi naamini leo utanipa ufumbuzi ili niweze kulielewe. Nakupenda Bingo tena zaidi ya sana, kwahiyo nakuomba unambie ukweli, usinifiche mimi ni mkeo", ilikuwa sauti ya mwanadada aitwaye Millander. Sauti hiyo ilisikika akimbembeleza mumewe wa kuitwa Bingo ili aseme ukweli wa siri nzito inayoendelea juu yake. 

"Ukweli upi unao utakaa mke wangu!?" Bingo aliuliza kwa mashaka.

Millander akashusha pumzi kidogo kisha akaongeza kusema "Usiku huwa unakwenda wapi?.." 

"Ahahahahaha", Bingo akacheka kwa madaha baada kusikia swali hilo la mkewe, mara baada kukatisha kicheko chake akajibu. 
"Ipo siku utajua ukweli tu, wewe ondoa shaka".

"Kwanini usiniambie leo?..", aliongeza kuhoji Millander, lakini moyo wa Bingo bado ukawa mgumu kusema ukweli juu ya Siri yake. 

Hivyo hali hiyo ikazidi kuwa endelevu, usiku mmoja Millander aliamua kumfuatilia akidhania anaweza kujua ukweli, ila kutokana na giza nene na woga alio nao ukapelekea kurudi nyumbani pasipo kujua mwisho wa Bingo unakuwa upi, na kila alipo rudi alinukia harufu ya ubani sambamba na kutapaa damu sehemu mbali mbali za mwili wake.    

Kitendo cha Bingo kuendelea kuficha ukweli, kilimfanya Millander kupoteza furaha kabisa. Alipoa, ile hali ya kufurahia ndoa ilitoweka kabisa ila hakutaka kukata tamaa, ndipo siku nyingine aliweza kusema maneno yale yale aliyowahi kumwambia siku kadhaa zilizo pita. 

Hapo Bingo hakuona haja ya kuendelea kuficha tena, hivyo kabla hajaanza kufungua siri hiyo alikohoa kwanza kidogo kisha akasema "Millander mke wangu, kwanza asante sana kwa kutambua umuhimu wa ndoa yetu na vile vile kuniweka mimi kipaumbele katika maisha yako"

kwisha kusema hayo, alinyanyuka akaketi kisha mgongo wake akauegesha kwenye wigo wa kitanda asubuhi ile ya mapema wakati huo Millander naye alikaa sawa kutega sikio lake. 

"Katika maisha yangu kuna mitihani mikubwa sana nimepitia, katika mtihani huo nikakumbana na changamoto ngumu ambayo moja ni ile iliyonipeleka TROPEA mji wa ajabu sana, mji uishio wafu mji ambao kuishi ni tabu hasa kwa wale wanadamu wenye hali ya kawaida yaani namanisha waliotunukiwa uhai. Nia na madhumuni iliyonipelekea huko ni kufuaata dawa ya kumtibia mama yangu mzazi ambaye kwa kipindi kirefu sana alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya hapa na pale. Mama yangu alisumbuliwa na miguu kuvimba na kutoa maji, mara nyingine kumtokea hali ya kushindwa kula chakula na kupoteza fahamu mara kwa mara. Hayo ni magonjwa ambayo yalimtesa sana hadi kupelekea kudhoofika huku kila dawa zikishindwa kutatua matatizo hayo. Ikafikia hatua akawa amekata tamaa ya kuendelea kuishi ulimwenguni akabaki kungojea siku ile ambayo Mungu atamtuma malaika mtoa roho aje kuchukua roho yake kwa sababu alijiona hana tena thamani ya kuendelea kuishi. Matatizo hayo yalimfanya baba kumkimbia na kisha kuoa mwanamke mwingine ilihali ndugu baadhi nao wakionyesha kumtenga baada kuona hana dalili yoyote ya kupona"

Alisema Bingo, mkasa ambao ulimtoa machozi pindi alipo ukumbuka kwani ni zamani kidogo tangu mambo hayo yapite. Millander alipomuona mumewe amedondosha chozi alimgusa bega akamtuliza munkari kwa kumpa pole. Bingo aliyafuta machozi yake kisha akaendelea kueleza mkasa huo ambao ulimpelekea kufika Tropea mji ambao huishi wafu, mbali na kwenda kuchukua dawa katika mji huo vile vile Millander alitaka kujua ni sababu ipi inayomfanya Bingo kila siku usiku wa manane kuamka na kuelekea makaburini ilihali pindi anaporudi hunukia harufu ya ubani huku sehemu mbali mbali za mwili wake zikiwa zimetapaa damu.
"Yote hayo yalijiri nikiwa na miaka 18 pekee", aliongeza kusema Bingo sambamba na kuanza kusimulia mkasa huo. 
   
          ***********

"Tumepoteza pesa nyingi, tumelala tongo macho kutafuta tiba yake lakini hakuna mafanikio yoyote. Nasema hivi mimi nimenyoosha mikono niacheni na maisha yangu", sauti ya baba yake mkubwa Bingo ilisikika. 

Maneno hayo aliyanena saa za jioni akiwa amelewa chakari, alipaza sauti juu ikiwa kama kutuma ujumbe mlangoni kwa mama Bingo ambaye hali yake ni mahututi bin taabani. Maneno hayo yalipenya vyema kwenye masikio ya mama huyo hakika alisikitika sana, aliumia moyoni mwake lakini hakuwa na lakufanya zaidi ya kulia na maumivu yake. Sio huyo tu, bali hata ndugu wengine mbali mbali nao walijitoa kumsaidia mama Bingo. Ndipo jioni moja kijana Bingo aliamua kufunga safari kuelekea kule alipohamia baba yake, mzee Abacha. 

Ikawa siku nzuri kwake sababu alimkuta baba yake akiwa nje akipiga zogo na mkewe wa pili. Safari hiyo ya Bingo ni kwa niaba ya kumpa taarifa baba yake juu ya hali ya mama yake inavyo zidi kuwa mbaya ikiwa yeye hatoi ushirikiano wowote ule lakini licha ya Bingo kueleza hali hiyo, ghafla alijikuta akiambulia matusi na masimango kutoka kwa baba yake. 
"Sipo tayari kupoteza muda wangu kuhudumia mgonjwa asiyepona mimi, tena ondoka upesi mbele yangu kabla sijakufanya kitu chochote kibaya", alisema kwa hasira mzee Abacha.

Maneno hayo yalimuumiza sana Bingo. 
"Baba lakini tambua yule ni mkeo, vile vile ni binadamu mwenzako. Hebu jaribu kuwa na moyo wa huruma, kigezo cha kuoa kisikufanye ukamsahau mama yangu." kwa sauti ya chini iliyojaa huzuni ndani yake Bingo alisema.

"Unanifundisha maisha?", aliuliza mzee Abacha, swali ambalo lilimfanya Bingo kukaa kimya huku uso wake akiwa ameinamisha chini wakati huo huo akitafakari jibu la kumrudishia mzee wake lakini kabla hajasema chochote mzee Abacha akaongeza kusema. "Potea machoni mwangu Bingo, na nenda ukamwambie mama yako mimi sipo tayari kusaidia chochote juu yake hapo nilipofika basi inatosha" . Hapo Bingo hakuwa na namna nyingine tena zaidi ya kuondoka. 

Akiwa njiani aliwaza sana, hali ya mama yake ilikuwa tete, jambo hilo lilimfanya kutafakari ni namna gani atapambana kuokoa uhai wake. 

Kutokana na mtihani huo aliotunukiwa wa kususiwa mama yake ikabidi afanye kazi kwa bidii, alifanya vibarua vya kulima, alikata mkaa, Maisha hayo yalikuwa endelevu kwa kijana Bingo, msimu wa kilimo ulikuwa faida kwake, aliweza kufanya kazi kwa bidii alitumia nguvu nyingi sana kulima bila kuchoka, alifanya hivyo huku akizingatia kununua mazao ya chukula na kisha kuyahifadhi ndani ili msimu wa njaa hapo kijijini Ngaza wasije wakapata tabu. Kwa misimu kadha wa kadha, kijiji hicho kilikumbwa na janga la njaa, hivyo wasi wasi wa kurejea janga hilo ukamfanya Bingo kujituma ipasavyo hasa hasa akizingatia kuwa hawakuwa na mashamba kijijini hapo, kwani mara baada baba yake kuoa mwanamke mwingine aliuza mashamba yote ambayo alikuwa akiyatumia na mama yake kisha akanunua mashamba mengine kijiji cha pili alicho weka makazi mapya. 

Siku zilisonga miezi ikasogea miaka nayo ikajongea, asubuhi moja yapata saa kumi na mbili wakati Bingo anajiandaa kuelekea shambani kumalizia kibarua alichopata siku kadhaa nyuma alisikia sauti ya mama yake ikimuita, sauti ambayo ilisikika kwa chini kabisa kiasi kwamba ilimshtua Bingo. Haraka sana alitupa jembe chini akarudi ndani kumsikiliza huku moyoni akiwa na hofu dhofu lihali. 

"Bingo mwanangu", aliita mama Bingo kwa tabu sana sambamba na kukohoa mara mbili mfululizo. 

"Naam! nipo hapa mwanao", huku akimtuliza aliitikia Bingo. 

"Najua unavyo hangaika kila siku. Naumizwa sana na suala hilo lakini natumaini ipo siku Mungu atakukumbuka nakupenda sana Bingo wangu" Bingo aliachia tabasamu mara baada kuyasikia maneno hayo ya mama yake, na mara baada kukatisha tabasamu hilo akasema. 

"Wala usiwe na hofu mama yangu, mimi ni mwanao, tena mwanao pekee kwahiyo nitapambana mpaka tone la mwisho kuhakikisha wewe unafurahia maisha japo upo katika hali hiyo, na vile vile......", kabla Bingo hajamaliza kusema alichotoka kuongea mara ghafla nje ilisikika sauti kali ikisema. 
"Bingo toka ndani mwanahidhaya mkubwa mkubwa wewe." alishtuka Bingo, upesi alinyanyuka akatoka ndani akaenda kumsikiliza mtu huyo. 

"Habari za asubuhi Bi Mboni, shikamoo" 

"Sina haja ya salamu yako Bingo, ninachotaka hapa ni pesa yangu maana naona kazi imekushinda" Bi Mboni hakutaka kabisa salamu ya Bingo zaidi aliongea maneno hayo kwa jazba.

Hapo ndipo kijana Bingo alipoanza shughuli ya kujitetea, ila bado Bi Mboni kikongwe huyo mwenye uso mkavu aliendelea kumbana Bingo kwa kumuuliza maswali tofauti tofauti kuhusu kucheleweshewa kazi yake baada ya yote alisema "Usinichezee bwana mdogo, kama pesa yangu ulichukua basi maliza kazi yangu la sivyo nitakupoteza kwenye uso huu wa Dunia" kwisha kusema hayo Bi Mboni akaondoka zake. 

               ******

Millander alishtuka baada kuisikia kauli hiyo. Simulizi ambayo alikuwa akisimulia na mumewe ili msisimua sana na kutamani kujua ni kipi kilichoendelea. 

"Enhee ikawaje sasa", kwa shauku kubwa akauliza. Bingo akashusha pumzi ndefu kwanza kisha akaendelea kusimulia. 
"Vitisho vya Bi Mboni viliniogopesha sana, na zaidi kutokana na historia yake kijijini, ndio sababu kuu ya kuhofia, hivyo basi siku hiyo nililima sana, kuanzia asubuhi mpaka saa moja usiku, haikuwa kawaida yangu kufanya kazi mpaka muda huo ila ilinilazimu, hata nilipo rejea nyumbani ajabu kijiji chote kilikuwa kimepoa ndege na wanyama mwitu wakipata nafasi ya kuzurura huku na kule huku sauti za wadudu nazo zikipaza vyema kabisa kwenye masikio yangu. Mimi sikujali, jembe begani panga mkononi nilizipiga hatua za haraka haraka kurudi nyumbani lakini kabla sijafika. Mara ghafla mbele yangu alitokea mtu ambaye siku mfahamu wala kuwahi kumuona mahali popote pale. Ajabu mtu huyo yeye alinifahamu, alikuwa ni Ajuza japo kulikuwa giza lakini nilimtambua kwa sababu alikuwa na mkongojo mkononi mwake "

"Wewe ni nani mbona mimi sikufahamu, na umetoka wapi pia unataka nini.?" nilimuuliza maswali hayo haraka haraka wakati huku nikiwa na woga. Lakini badala Ajuza yule anijibu, cha kustaajabisha aliangua kicheko wakati huo sauti yake ikijirudia mara mbili mbili, vile vile sauti iliyo sikika haikuwa yake ilisikika sauti ya kiume nzito. 

Niliogopa sana, nikataka kukimbia lakini miguu yangu ikawa mizito. Hapo sasa ikabidi nipige mayowe kuomba msaada kwa wanakijiji ili waje kunisaidia, kweli wanakijiji wakafungua milango ya nyumba zao lakini maajabu yakawa bado yanaendelea kwani wanakijiji waliotoka katika majumba yao hawakuwa binadamu, dhahiri shahili kwa macho yangu niliwaona wakitoka damu midomoni mwao huku wakijongea mahali nilipo simama kwa mwendo wa kusafa. 

USIKOSE SEHEMU IJAYO YA HADITHI HII YA KUSISIMUA.. 

Post a Comment

Previous Post Next Post