*SIKUACHI BABY * (9)


Nilibaki nimeduwaa kwa muda huku nisijue ni nini nilitakiwa kufanya kwa wakati huo, simu mbili nilizozipokea ziliniweka katika wakati mgumu mno.
Sauti ya yule mwanaume aliyejitambulisha kuwa ni mume wake na Samira ilianza kujirudia kichwani mwangu, nilikumbuka kila kitu alichonieleza kwa wakati ule.
Taarifa ya Bianka aliyoniambia kuwa ni mjamzito nayo ikazidi kuniweka katika wakati wa mawazo, sikutaka kuamini kama kweli alibeba ujauzito wangu katika kipindi kile, nilianza kujuta kwa kosa kubwa nililokuwa nimelifanya, nilijiona kuwa mzembe sana kwa kukubali kufanya mapenzi bila kutumia kinga. Hilo lilikuwa ni kosa kubwa sana. Nilijilaumu mno.
****
“Unaujazito wangu kweli?”
“Ndiyo.”
“Umeingiaje tena?”
“Ina maana umesahau ulivyokuwa unafanya mapenzi na mimi.”
“Hapana sijamaanisha hivyo mbona sasa hukuniambia kama uko katika siku zako za hatari?”
“Tumeshafanya kosa mpenzi sasa mimi nitafanyaje?”
“Unanipa wakati mgumu sana.”
“Wakati mgumu kivipi inamaana kumbe ulikuwa huna malengo na mimi?”
“Hapana.”
“Ila?”
“Mwenyewe unaona hali ya maisha yangu, kazi yangu ya bodaboda nayo haitabiriki hivi nitaweza kweli kumlea huyo mtoto?”
“Hivyohivyo Metu tutamlea kwani wewe unatakaje?”
“Tuitoe hiyo mimba.”
“Unasemaje?”
“Mpenzi wangu nakuomba tuitoe hiyo mimba na kama tatizo ni mtoto tutazaa kwa wakati mwingine tukishakuwa tayari.”
“Metu mimi siwezi kushiriki hiyo dhambi, siwezi Metu.”
“Huwezi nini mpenzi wangu naomba unisaidie katika hili, nakuahidi sitokuacha katika maisha yako, siwezi kukuacha nisaidie mpenzi wangu.”
“Metu mimi sipo tayari kufanya hivyo.”
“Haupo tayari kivipi Bianka inamaana kumbe hunipendi?”
“Nakupenda sana lakini embu nionee huruma.”
“Kama unanipenda basi nisikilize, kubali kuitoa hiyo mimba kama tatizo ni pesa mimi nitakutafutia ya kutolea.”
“Metu nielewe siwezi halafu Mama tayari ameshajua,” aliniambia Bianka maneno yaliyozidi kuniweka katika wakati wa mawazo.
Nilijaribu kutumia kila mbinu za kuweza kumshawishi akubali kuitoa mimba lakini ilishindikana, mwisho aliamua kuniambia ukweli kuhusu Mama yake kuwa tayari alishafahamu kila kitu na hivyo isingewezekana kuitoa.
Hakukuwa na siku ambayo naweza kusema nilikuwa katika wakati mgumu kama siku hiyo, kila nilivyokuwa nikimtazama Bianka nilihisi kuchanganyikiwa.
****
Baada ya mume wake Samira kunipigia simu na kunipa vitisho vikali kwa kweli nilishindwa kuendelea na zoezi langu la kila siku katika kumpeleka ofisini kwake na kumrudisha, nilishindwa mpaka kumpigia simu.
Nilihofia mambo mengi sana ambayo angeweza kunifanyia mwanaume huyo aliyeonekana kuwa na hasira sana.
Niliyakumbuka maneno ya Samira aliyoniambia kuwa alikuwa hana mume katika maisha yake, nikashindwa kuelewa ni nini kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia kwani nilishaanza kupata vitisho vya kuuliwa na kisa alikuwa ni yeye.
Sikutaka kuamini kama tayari nilikuwa nimeshaingia katika mchezo mchafu wa mapenzi ambao ungeweza kusababisha kifo changu.
Baada ya kupita siku tatu tangu tukio hilo lilipoweza kutokea Samira aliweza kunipigia simu.
“Kwanini ulinidanganya?” nilimuuliza.
“Nisamehe Metusela mpenzi wangu,” alinijibu kwa sauti iliyoambatana na kilio.
“Nikusamehe nini wakati unajua ulichokifanya.”
“Naomba unisamehe Metu ila sina jinsi ya kufanya mimi nakupenda wewe.”
“Utapenda wangapi na huyo mume wako?”
“Simpendi.”
“Humpendi kivipi embu acha kuniletea matatizo,” nilimwambia kisha nikakata simu.
****
Kichwa changu bado kilitawaliwa na mawazo sana, niliendelea kumfikiria Bianka ambaye mpaka kufikia wakati huo sikujua ni nini nilitakiwa kukifanya.
“Nini ulichoamua?”
“Mama yangu anataka akufahamu Metu.”
“Umemueleza kuhusu mimi?”
“Ndiyo.”
“Usijali nitaenda kujitambulisha ila bado mapema sana,” nilimwambia.
Nilichokuwa nikikiwaza kwa wakati huo ni kutafuta njia ya ziada ya kuweza kumshawishi Bianka mpaka akubali kuitoa mimba yake ili niishi maisha ya amani, sikupanga kuzaa naye katika maisha yangu.

Hakukuwa na kitu kilichokuwa kikiniumiza kichwa kama ujauzito wa Bianka, sikutamani kumuona akiwa na ujauzito wangu, nilipanga kufanya kila niwezalo mpaka akubali kuutoa na huo ndiyo ungekuwa mwisho wa mapenzi yetu.
Kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha yangu hakikwenda sawa na sababu kubwa ilikuwa ni ujauzito huo uliyozidi kuniweka katika wakati wa mawazo.
Baada ya kuniambia kuwa Mama yake alihitaji kuniona, sikutaka kukataa, niliamua kwenda nyumbani kwao na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa Mama yake kunifahamu.
“Umeingia choo cha kike,” aliniambia Amani baada ya kumueleza kuhusu ujauzito aliyokuwa nao Bianka.
“Nimechanganyikiwa sijui hata nifanyaje,” nilimwambia.
“Mama yake anasemaje kwani?”
“Alitaka kunifahamu ila alichoniambia kimezidi kunipa wakati mgumu sana.”
“Amekuambia nini?”
“Anataka nimuoe Bianka.”
“Sasa umeamuaje?”
“Sasa nitajibu nini zaidi ya kumdanganya, nimemdanganya kuwa nitamuoa lakini tusubiri kwanza mpaka ajifungue.”
“Hapo hauna jinsi ya kufanya itabidi ukubali kumuoa.”
“Siwezi kukubali kizembe kiasi hicho.”
“Sasa utafanya nini?”
“Nitajua cha kufanya lakini siwezi kumuoa Bianka kwanza hakuwa katika akili yangu kabisa imetokea bahati mbaya ameushika ujauzito wangu,” nilimjibu Amani.
Nilianza kuona mambo yanazidi kuwa magumu kila siku, ujauzito wa Bianka ulizidi kunifanya nikose amani ya maisha.
****
Samira aliendelea kunisumbua, kila siku alikuwa akinipigia simu na alihitaji kuonana na mimi ili tuweze kuzungumza juu ya tukio lile lililotokea la mume wake kunipigia simu na kunipa vitisho.
“Najua umekasirika mpenzi ila naomba unipe nafasi ya kuzungumza na wewe nikuelezee.”
“Siwezi kukupa hiyo nafasi, wewe ni mke wa mtu Samira.”
“Kwanini unanifanyia hivyo lakini?”
“Naomba ukae mbali na maisha yangu,” nilimjibu.
Aliendelea kunisumbua sana, hakutaka kuona nikikatisha mawasiliano naye japo alikiri mwenyewe kuwa alinidanganya, aliniambia kuwa alifanya hivyo kwa kuwa hakuwa na jinsi ya kufanya lakini hakuacha kuniambia ananipenda. Hilo likazidi kunishangaza.
“Mume wako kwani anafanya kazi gani?” nilimuuliza baada ya kuona usumbufu umezidi.
“Ni mwanajeshi,” alinijibu.
Nilishikwa a butwaa! Na baada ya kusikia hivyo, sikutaka kuamini kama nilishiriki kufanya mapenzi na mke wa Mwanajeshi.
****
Niliendelea na kazi yangu ya bodaboda huku nikijitahidi kujiweka mbali na Samira, sikutaka kupata matatizo mengine ambayo yangeweza kunikuta, lile la Bianka lilinitosha na sikutaka hata Mama yangu aweze kufahamu.
Licha ya mambo yote aliyonieleza Samira juu ya mume wake ambaye alikuwa ni mwanajeshi pamoja na muda wake mwingi ambao aliutumia kukaa kambini, hakuacha kuniambia alinipenda na alikuwa yupo radhi kufanya lolote ili aweze kunipata, hakutaka nimuache kirahisi kiasi kile.
“Naomba usiache Metusela.”
“Mume wako akijua bado naendelea na mchezo huu atanitoa roho.”
“Usiogope wewe kubali kwanza halafu mimi nitakwambia nitafanya nini?”
“Nikubali nini na utafanya nini?”
“Kubali kwamba hauniachi.”
“Halafu?”
“Wewe kubali.”
“Sikuachi.”
“Nafurahi kusikia hivyo mpenzi ila kuna kitu nitafanya kwa ajili ya mapenzi yetu ili mume wangu asijue kinachoendelea.”
“Utafanya nini?”
“Nitakuwa nikiwasiliana na wewe kwa siri na kila tutakapomaliza kuchat nitahakikisha nafuta meseji zote, hatojua kitu.”
“Una uhakika?”
“Ndiyo mpenzi tatizo lako wewe unaogopa sana.”
“Lazima niogope umeshaniambia mume wako ni mwanajeshi unafikiria nini kingine kama sio kuuliwa.”
“Hawezi kukuua mtu mimi nakupenda wewe halafu muda mwingi huo yupo kambini, akirudi tutaendelea kula raha zetu,” aliniambia Samira nilipokuwa nikizungumza naye kwenye simu.
Nilijikuta nikilainika taratibu na kurudia kuwa na mahusiano na Samira ya kisirisiri, naweza kusema nilichanganywa na uzuri wake na ndiyo uliyonifanya nikubali kirahisi kuendelea kuwa naye. Nilijitoa muhanga wa kimapenzi.

Moyo wangu bado uliendelea kuumia sana baada ya kumfikiria Bianka, alikuwa ni msichana wangu ambaye nilipanga kumtumia kingono kisha na kumuacha, sikupanga kuzaa naye lakini kwa wakati huo alikuwa tayari ana ujauzito wangu. Nilitamani kuona siku moja Bianka akikubali kuutoa ujauzito huo lakini hilo hakutaka kulikubali.
“Kwahiyo umekataa kuutoa huo ujauzito?”
“Ndiyo siwezi Metu kuua kiumbe kisichokuwa na hatia.”
“Bianka kwani ugumu uko wapi, tunatoa na kama tatizo ni mtoto tutazaa mwingine.”
“Metu wewe unaongea kwasababu hii hali haipo kwako, lakini jaribu kuwa na roho ya huruma hata kidogo mbona unakuwa katili kiasi hicho?”
“Nampenda sana huyo mtoto ndiyo maana nakwambia ufanye hivyo, sitaki kuja kumtesa.”
“Mimi siwezi Metu kwanza naogopa kufa.”
“Huwezi kufa mpenzi nikubalie,” nilimwambia kwa sauti ya kumbembeleza lakini hakuweza kukubali.
Niliendelea kumbembeleza akubali kuutoa ujauzito mpaka pale siku moja ambapo Mama yake aliamua kunisusia, hakutaka kuendelea kuishi na Bianka. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuishi na Bianka bila ndoa, yalikuwa ni maisha ambayo sikuyatarajia kwa wakati huo, sikuwa na jinsi ya kufanya kwa kile kilichokuwa kimetokea, nilikubaliana na kila kitu.
Nilishindwa kumueleza Mama yangu ukweli wa mambo yote yaliyokuwa yametokea, niliamini kama ningeweza kumueleza angenichukia sana kwa kitendo kile cha kususiwa mwanamke na kuanza kuishi naye.
****
Niliendelea kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Samira huku kila kitu kilichokuwa kikiendelea kati yetu kiliendelea kuwa kama siri. Nilizidi kushiriki kufanya naye mapenzi lakini pia sikuacha kuwa makini kujihami na mume wake ambaye alikuwa ni Mwanajeshi.
Penzi la Samira lilinichanganya mno, wazo la mume wake lilianza kuniondoka kichwani, nilianza kumdharau baada ya kuendelea kulifaidi penzi la mke wake bila ya madhara yoyote.
Alikuwa akinipa pesa nyingi sana na pesa hizo nilizitumia na Bianka, hakufamu lolote kuhusu maisha ya msichana huyo niliyekuwa naishi naye nyumba moja.
“Ni hakikishie usalama wangu,” nilimwambia Samira siku moja majira ya jioni tulipotoka kufanya mapenzi katika moja Lodge iliyokuwepo maeneo ya Tandika.
“Usalama upo ila kama nilivyokwambia naomba usiwatangazie watu kuhusu mahusiano yangu na wewe, mume wangu akijua kuwa bado naendelea na wewe itakuwa ni hatari kwetu,” aliniambia.
Dereva bodaboda mwenzangu Amani hakuacha kunishauri juu ya kuachana na Samira, kila siku alirudia kuniambia maneno hayohayo kuwa niachane na aina ya mapenzi ambayo mwisho wa siku yangeweza kuniletea matatizo makubwa katika maisha yangu.
“Kwanini usitulie na Bianka maana mpaka sasa ana ujauzito wako na unaishi naye,” aliniambia Amani tulipokuwa kijiweni.
“Bianka sio chaguo langu,” nilimjibu.
“Hutakiwi kusema hivyo kumbuka tayari ana damu yako,”aliniambia.
“Laiti ungejua natamani hata kesho huo ujauzito wake utoke maana nishamchoka” nilimwambia.
“Metusela badilika mshikaji wangu hayo maisha unayoishi siyo kabisa, rudi kwenye mstari.”
“Hayo mahubiri unayonihubiria hata sikuelewi kwani nikitembea naye kuna ubaya gani au kuna kitu unachopungukiwa?”
“Usicheze na mke wa mwanajeshi, utafanywa kitu kibaya.”
“Hawezi kunifanya lolote kwanza ni mchumba tu huo uwanajeshi wake mimi haunitishi lolote,” nilijibu huku nikijiamini.
****
Kama wasemavyo wahenga kuwa siku zote mbio za sakafuni huishia ukingoni hii ndiyo iliyonitokea. Katika kipindi ambacho nilikuwa nikitembea na Samira kwa siri siri, alikuja kupata ujauzito wangu.
Nilichanganyikiwa baada ya Samira kunieleza kuhusu ujauzito huo aliyokuwa nao, kwa upande wake hakutaka kuamini kama kweli alikuwa ni mjamzito, aliogopa mno na hakujua ni nini ambacho angeweza kumwambia mume wake ambaye tayari alishamfumania na kumkanya.
Hakukuwa na wazo lingine lililonijia kichwani na kumshauri zaidi ya kumwambia alitakiwa autoe ujauzito huo ambao ungeweza kuleta madhara makubwa hapo baadae, aliweza kukubaliana nalo.
Hatimaye mipango ya kisirisiri ya kuutoa ujauzito wa Samira ilianza kufanyika, nilipokuwa hospitalini nilikuwa nikimuomba Mungu muda wote tukio lile liweze kufanyika salama. Majibu ya daktari aliyokuja kunieleza baada ya kufanikiwa kuutoa ujauzito wa Samira yaliniweka katika hali ya sintofahamu.
“Imekuaje dokta?” nilimuuliza mara baada ya kumuona akitoka Theatre kwa wakati huo.
“Nimefanikiwa kuutoa lakini amepoteza damu nyingi sana,” alinijibu dokta.
“Kwahiyo tunafanyaje?”
“Hakuna cha kufanya tena?”
“Kivipi?”
“Nasikitika kukuambia kuwa Samira amefariki dunia,” aliniambia daktari.

ITAENDELEA.. 

Post a Comment

Previous Post Next Post