*SIKUACHI BABY EP 10* MWISHOOOO_ *MWISHOOOOOOO*


“Unasemaje dokta?” nilimuuliza huku nikiwa kama sijamsikia vizuri, wakati huo nilikuwa nimeyakodoa macho yangu kwa mshangao mkubwa sana.
“Nasikitika kukuambia kuwa Samira amefariki dunia,” alirudia kuniambia tena maneno ambayo yalinichanganya sana, sikutaka kuyaamini hata kidogo.
Nilianza kuhisi joto kali likinitawala mwilini na haikuchukua sekunde jasho likaanza kunitoka, hofu ilikuwa imenitawala kwa wakati huo.
“Pole sana,” aliniambia dokta lakini sikuweza kumjibu, akili yangu haikuwa sawa baada ya kusikia kuwa Samira alikuwa amefariki dunia.
Hali ya usalama wa maisha yangu haikuwa shwari, kasi ya mapigo yangu ya moyo yalikuwa yakinienda mbio, nilizidi kuwa katika hofu kubwa sana baada ya kumfikiria mume wa Samira endapo kama angeweza kuzipata taarifa hizi za kifo cha mke wake ambaye alifia mikononi mwangu ni nini ambacho angeweza kuamua kukifanya? hii ilikuwa ni moja kati ya kesi kubwa mno iliyokuwa ikinikabili.
Baada ya daktari yule kuniona nipo katika hali hiyo ya mawazo ilibidi aniite ofisi kwake ili aweze kuzungumza vizuri na mimi.
“Kwahiyo dokta hakuna njia yoyote ya kuyaokoa maisha yake?” nilijikuta nikimuuliza dokta swali ambalo lilimshangaza, akabaki akinitazama kwa mshangao, wakati huo tulikuwa ndani ya ofisi yake.
“Niambie dokta hakuna uwezekano wa kuurudisha uhai wake?”nilimuuliza tena kwa kujiamini.
“Mbona sikuelewi kijana,” aliniambia dokta.
“Hunielewi kivipi dokta?”
“Tangu lini umewahi kusikia mtu aliyefariki dunia akapona au akarudishiwa uhai?” aliniuliza yule daktari swali ambalo lilinirudisha katika fahamu zangu, nilizidi kuchanganyikiwa baada ya kusikia maneno hayo ya daktari.
“Mbona hii kesi ni kubwa sasa,” nilijisemea maneno haya ambayo nilihisi nayasikia peke yangu lakini kumbe haikuwa hivyo niliyatamka kwa sauti kubwa na yule daktari aliyasikia.
“Kesi! Kesi kivipi?” aliniuliza.
“Hapana, hapana dokta hakuna kitu,” nilimjibu.
“Hivi ulisema huyu ni mke wako wa ndoa?”
“Ndiyo.”
“Lakini kwanini mliamua kuchukua maamuzi haya au hamkupenda kuwa na mtoto?”
“Hapana ni mipango tu lakini kwa wakati huu hatukupanga kuzaa,” nilimjibu daktari kwa kumdanganya baada ya kuona anazidi kunidadisi undani wa maisha yangu.
“Pole sana kwa kumpoteza mkeo.”
“Asante,” nilijibu.
Nilipomfikiria mume wa Samira akili yangu ilizidi kutawaliwa na mawazo sana, nilifahamu hakukuwa na usalama tena wa maisha yangu na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kufunzwa kwa tabia yangu ya kutembea na wanawake wengi niliyokuwa naona ufahari kuwa nao.
Nilikumbuka maneno ya Mama yangu aliyokuwa akinipigia kelele kila siku kuhusu kuoa, hakupendezwa na aina ya maisha niliyokuwa nikiishi japo mtaani nilisifika kuwa na tabia ya upole sanjari na heshima lakini siri na mwenendo mzima wa maisha yangu hakukuwa na mtu ambaye alifahamu.
Kama katika maisha yako hayajawahi kukusibu kama yaliyowahi kunisibu mimi katika maisha yangu basi muombe sana Mwenyezi Mungu yasije yakakusibu maana utatamani ufe kabla ya kukisubiri kifo chako ambacho ni halali yako kabisa.
Kifo cha Samira kilizidi kunipasua kichwa mno.
****
Siku hiyo nilirudi nyumbani mapema sana huku nikionekana kuwa mnyonge, haikuwa kawaida yangu kuwahi kurudi nyumbani. Bianka msichana niliyekuwa nikiishi naye kama mke wangu wa ndoa aliponiona aligundua tofauti yangu.
“Kuna nini Metu?” aliniuliza.
“Hakuna kitu,” nilimjibu.
“Sio kweli Metu embu acha kunificha kitu kuna nini kimetokea mbona umewahi kurudi nyumbani?”
“Sipo sawa.”
“Haupo sawa kivipi?”
“Basi tu sipo sawa.”
“Umemgonga mtu na pikipiki?”
“Hapana.”
“Hapana nini sasa si useme mpenzi lakini?” aliniuliza Bianka.
“Unajua Bianka kuna kitu……..” nilianza kumueleza Bianka ukweli ambao nilikuwa nimemficha siku zote lakini kabla sijaanza kuziunganisha sentensi zangu mara simu yangu ikawa inaita, niliitoa mfukoni na kuitazama, mpigaji alikuwa ni Diana msichana ambaye niliwahi kumtongoza miezi miwili iliyopita, alinikubalia na tayari nilikuwa nimeshafanya naye mapenzi, sikutaka kuipokea simu hiyo, niliikata.
“Mbona umekata simu?” aliniuliza Bianka huku akionekana kushangazwa na kitendo hicho.
“Hana umuhimu zaidi ya mazungumzo yetu,” nilimwambia.
“Sawa embu endelea kunielezea nini kimetokea?” aliniuliza Bianka lakini kabla sijaanza kumuelezea mara ujumbe mfupi uliingia katika simu yangu. Niliufungua na kuusoma.
“KAMA TULIVYOZUNGUMZA HAKIKISHA MNAPANGA MIPANGO YA MAZISHI MAPEMA MJE KUUCHUKUA MWILI WA MAREHEMU MOCHWARI.”
Niliusoma ujumbe huo aliyonitumia yule daktari, nilishindwa kuendelea kumueleza ukweli Bianka, nguvu za mwili ziliniishia, nikajikuta nadondoka chini na kupoteza fahamu.

Nilipata fahamu nikajikuta nimelala chini sakafuni, nilijihisi kuwa mzito mno na kichwa kilikuwa kikiniuma kwa wakati huo. Nilisahau kuwa ni nini kilichokuwa kimetokea mpaka kikasababisha mimi kuwa katika hali hiyo.
Niliyaangaza macho yangu huku na kule nikitegemea kuyashuhudia mazingira tofauti lakini hakukuwa na utofauti wowote ule niliyouona. Nilikuwa bado nipo ndani ya chumba changu, nilimtazama Bianka ambaye alikuwa ameketi kitandani huku akiwa amejiinamia.
Nilipokuwa nikiendelea kumtazama Bianka ghafla! nilipokelewa na sauti ya kilio cha kwikwi, alikuwa akilia.
Nilikurupuka kutoka pale chini nilipokuwa nimelala kisha nikamfuata na kuketi pembeni yake.
“Kuna nini?” nilimuuliza lakini hakuweza kunijibu lolote, aliendelea kulia mfululizo, nikazidi kubaki nimeyakodoa macho yangu kodo! Huku nisifahamu lolote lililokuwa limetokea.
“Kuna nini Bianka?” nilimuuliza tena huku nikijipapasa mifukoni mwangu kutafuta simu, sikuwa na simu kwa wakati huo, nikataka kumuuliza Bianka lakini kabla sijaamua kumuuliza mara akanitupia simu yangu.
“Soma meseji zako,” aliniambia kisha akaendelea kulia, nilipoichukua simu yangu na kuiangalia nilikutana na meseji nyingi za wanawake pamoja na meseji ya daktari aliyokuwa akinisisitizia niwahi kupanga mipango ya mazishi ili niweze kwenda kuuchukua mwili wa marehemu Samira mochwari.
Sikutaka kuamini kwa kile nilichokiona, Bianka aliweza kuzisoma meseji zangu zote na ndizo zilizosababisha mpaka akawa katika hali ile ya kilio.
Nilikumbuka mara ya mwisho niliupokea ujumbe wa yule daktari uliyonishtua mno na mpaka kufikia hapo sikukumbuka kitu kingine chochote kilichoendelea.
“Ina maana kumbe nilipoteza fahamu?” nilijiuliza swali lililonipa jibu la ndiyo.
Kitendo cha Bianka kuzisoma meseji zangu kiliweza kuyafichua maovu yangu yote pamoja na siri niliyokuwa nimeificha , hakukuwa na kitu kipya tena ambacho ningeweza kumueleza akanielewa.
“Diana ni nani yako na huyo Rose, Jack, Cleopatra na Recho ni nani zako?” aliniuliza aliponyamaza na kuyafuta machozi yake, akanitazama kwa macho yaliyohitaji kuona namueleza ukweli.
Kwa kweli nilishindwa kutoa majibu ya haraka kwasababu hao wasichana wote nilikuwa katika mahusiano nao ya kimapenzi.
“Unashindwa kunijibu kwasababu unajua kuwa wote hao ni wanawake zako hivi Metu kwanini huridhiki kwanini unanifanyia haya yote lakini?”
“Nisikilize Bianka.”
“Nikusikilize nini Metu wakati kila kitu nimeshakifahamu, yani umesahau jinsi mama yangu alivyonifukuza nyumbani kwasababu yako, Metu nimebeba huu ujauzito wako lakini bado ulikuwa unanilazimisha niutoe kumbe ulikuwa na maana yako.”
“Hapana usiseme hivyo.”
“Hapana nini Metu wewe ni Malaya.”
“Unaniita mimi Malaya Bianka?”
“Ndiyo unatembea na kila mwanamke.”
“Kwanini unashindwa kunisikiliza, unataka nitumie neno gani ili uweze kunielewa.”
“Umeniharibia maisha yangu Metu, umenipotezea muda wangu, sijui hata ni wapi natakiwa kuanzia tena,” aliniambia kisha akaanza kulia, nilianza kumbembeleza huku nikizidi kumsihi anipe nafasi ya kumueleza jambo muhimu.
“Unataka kuniambia nini?”
“Naomba unisamehe sana.”
“Unafikiri nitaweza kukusamehe kirahisi kweli?”
“Najua utaweza ila mpaka hapa nilipofikia sina budi kukuomba msamaha na pia kumuomba msamaha Mungu wangu anisamehe.”
“Una maanisha nini?” aliniuliza.
Nilianza kumsimulia kila kitu kilichokuwa kimetokea katika maisha yangu, sikutaka kumficha kitu nilimsimulia historia ya wanawake wote niliyowahi kuwa nao kimapenzi mpaka ikafikia hatua nikapata pigo la kufiwa na mmoja wao mikononi mwangu, ilikuwa ni katika harakati za kujaribu kuutoa ujauzito wake ili tufiche siri kwa mume wake.
“Nahisi kuwa mwenye kesi ya kujibu mbele za Mungu,” nilimwambia Bianka.
Alianza kuonekana kunihurumia baada ya kumsimulia matukio yote niliyoyafanya ya kutembea na wasichana lukuki katika maisha yangu, alisahau yote niliyokuwa nimemfanyia katika maisha yake na sasa alikuwa upande wangu, alinihurumia sana baada ya kusikia kuwa Samira alikuwa amekufa na mpaka kufikia wakati huo nilikuwa sijui ni nini nilichokuwa natakiwa kufanya.
Hakukuwa na wazo lingine lililonijia kichwani zaidi ya kutoroka, nilipanga kutoroka ili niweze kuyakimbia matatizo yaliyokuwa yamenitokea, Bianka ndiye msichana aliyekuwa bega kwa bega na mimi katika kuhakikisha lengo langu hilo linatimia mbali na makosa yote niliyokuwa nimemfanyia katika maisha yake lakini aliamua kunisamehe na kuacha ibaki kuwa historia, hakuta kuona nikipoteza maisha mbele yake baada ya mume wa Samira kunikamata.
Siku hiyo iliyofuata ndiyo nilipanga ndiyo nitoroke na mkoa ambao nilipanga kwenda ulikuwa ni mkoa wa Mwanza, niliamini kwa kukimbilia huko ndipo ungeweza kuwa usalama wa maisha yangu.
****
Siku iliyofuata ikawadia, asubuhi na mapema nilikuwa tayari kwa safari ya kwenda mjini Mwanza, sikukumbuka kumuaga Mama yangu mzazi wala rafiki yangu yoyote. Naweza kusema nilikuwa nikiikimbia maiti ya Samira pamoja na mume wake ambaye niliamini alikuwa akinitafuta kwa udi na uvumba.
Kipindi ambapo nilikuwa kwenye daladala kuelekea Ubungo Terminal, tulipofika maeneo ya Buguruni daladala nililokuwa nimepanda ghafla! lilipata ajali mbaya sana, liligongana na uso kwa uso na lori.
****
Nilichokuja kusimuliwa wakati nilipokuwa nimelazwa hospitalini ni idadi ya vifo vya abiria kumi katika ajali hiyo mbaya iliyoniacha na ulemavu wa maisha, nilikuwa nimekatwa miguu yangu yote miwili.”
Hii ndiyo sababu ya ulemavu wangu huu niliyokuwa nao kwa sasa, najua utajiuliza maswali mengi sana kuhusu Samira na Bianka ilikuwaje na ni nini kiliendelea baada hapo lakini ukweli ni kwamba Samira alikuwa amefariki dunia na ukweli baadae ulikuja kufichuka lakini kwa msaada wa yule daktari aliweza kunisaidia kutengeneza kesi ya kifo cha Samira ambayo ilinisaidia nisifikiriwe vibaya na jamii hususani mume wake Samira.
Licha ya mambo yote yaliyokuwa yametokea pamoja na ulemavu wangu lakini Bianka hakunicha, alizidi kuwa na mimi kila siku.
Mama yangu aliumia sana baada ya kuniona nimekuwa kilema, alijua fika nisingeweza tena kuitimiza ndoto yake ya kuona siku moja nikioa na kumletea mjukuu.
Bianka aliweza kuyafuta machozi ya Mama yangu, alikubaliana na yote yaliyokuwa yametokea na mwisho tuliamua kufunga ndoa.
Baada ya miezi tisa ya ujauzito wake kupita hatimaye alifanikiwa kujifungua mtoto wa kiume ambaye niliamua kumuita jina la Amedeus, jina hili lilikuwa ni la Baba yangu, niliamua kumuita jina hilo mwanangu kama ishara ya kumuenzi kwani tayari alikuwa ameshatangulia mbele za haki.
Siwezi tena kufanya kazi yangu ya udereva wa bodaboda, nimekuwa ni mtu wa kusubiri kila siku kuletewa chakula na mke wangu ambaye kwa sasa anafanya kazi kama muhudumu wa baa. Japo najua adha wanazokutana nazo wahudumu wa baa lakini nashindwa kumkataza mke wangu asifanye hiyo kazi kwasababu mwisho wa siku ndiyo inayonilisha mimi pamoja na mwanangu.

MWISHO........ 

Post a Comment

Previous Post Next Post