HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 01---02

  
MTUNZI: ERIC JAMES SHIGONGO
Nashukuru sana kwa kuwa kila siku mnaendelea kuongezeka ndani ya ukurasa huu, na ninashukuru kwa kuwa wengi wenu mnafuatilia simulizi zangu katika magazeti ya Kampuni ya Global Publishers.
Leo, ninakwenda kuanza simulizi hii ambayo nilikwishawahi kuitoa gazetini miaka ya nyuma. Wengi mliipenda na ninadhani litakuwa jambo zuri kuirudia mahali hapa. Ungana nami, kwenye ushauri, nishauri, kwenye maoni, niambie na hata kwenya makosa, niambie pia ili niweze kujirekebisha.
ANZA NAYO...
Hali ya hewa ilikuwa tulivu ingawa kulikuwa na kijua kilichochoma kwa mbali na kufanya hali ya Mwanza iwe na joto kiasi.
Anne alisimama kizimbani mbele ya jaji wa Mahakama ya Rufaa Raphael Mpoki, siku hiyo ya Januari 21, 1998 ilikuwa siku ya hukumu yake na wengi wa watu waliohudhuria mahakamani walitegemea kwa kosa alilolifanya Anne ni lazima angenyongwa.
Miongoni mwa watu waliokuwepo makahamani walikuwa watoto wake wawili, wa kike Nancy na wa kiume aliyetwa Patrick, walikuwa watoto wazuri tena mapacha na siku tano kabla ya siku hiyo walitimiza miaka kumi na mbili lakini miaka waliyoishi na mama yao katika maisha ilikuwa ni miwili tu!
Patrick na Nancy walikosa mapenzi ya mama yao na si mama tu bali pia baba yao aliyefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha wakiwa na umri wa mwaka mmoja, yeye hawakumwona kabisa zaidi ya kuiona sura yake katika picha.
Mpaka siku hiyo Anne alikuwa amekaa mahabusu kwa takribani miaka kumi na siku thelathini na saba kamili na aliwaacha watoto wake wakiwa na miaka miwili tu! Patrick na Nancy walikuwa kama watoto wa yatima wakilelewa na mama yao mdogo, Suzanne.
Walimhurumia sana mama yao kwa sababu alikuwa amekondeana sana alivaa nguo chafu na mwili wake ulijaa vipele na ukurutu lakini pamoja na hali hiyo ya uchafu bado alionekana ni mwanamke mwenye sura nzuri na sura yake ilifanana sana na ya mtoto wake wa kike Nancy!
Tofauti pekee kati yao ilikuwa ni rangi ya ngozi zao, Nancy alikuwa mweupe zaidi ya mama yake kwa sababu baba yake Huggins alikuwa Mmarekani mweusi mwenye mchanganyiko wa damu ya kizungu ila mama yake ndiye alikuwa raia wa Sierra Leone aliyehamia Marekani miaka mingi kabla.
Anne alipowaangalia watoto wake wawili waliokuwa wamekaa miguuni kwa mama yao mdogo akiwa amewakumbatia, alilia machozi alisikia uchungu moyoni mwake kufahamu kuwa ni siku hiyo ndiyo ilikuwa ya mwisho kwake kuwaona watoto wake!
“Patrick and Nancy today I’m dying for you!”(Patrick na Nancy leo nakufa kwa ajili yenu!)
“No! Mom don’t die! Please mom we need you mom dont go!”(Hapana mama usife, tafadhali bado tunakuhitaji sana usituache) mtoto mdogo Patrick alipiga kelele mahakamani na kuchomoka mikononi kwa mama yake mdogo na kukimbia akimfuata mama yake.
Kabla hajakifikia kizimba alishikwa mkono na askari na kuanza kuvutwa akirudishwa mahali alipokaa mama yake mdogo. Mawakili waliokuwa wakiendelea na mabishano ya kisheria ndani ya mahakama na hata jaji mwenyewe walikerwa sana na kelele za mtoto Patrick aliyekuwa akilia, ikabidi hakimu aagize Patrick na Nancy pamoja na mama yao mdogo watolewe nje ya mahakama haraka ili kuruhusu mahakama iendelee na kazi yake!
“Hatutaki! Hatutaki! Hatutaki! Tuachieni tumwone mama yetu mara ya mwisho!”Patrick na Nancy walilia wakati askari akiwavuta kuwatoa nje ya mahakama.
****
Hali ilipotulia mahakama iliendelea na kazi yake kama kawaida.
“Mheshimiwa Jaji siamini hata kidogo kuwa mshtakiwa alimuua mama yake kwa sababu marehemu alikutwa nje ya nyumba yake iliyo umbali wa mita elfu moja kutoka nyumbani kwa mshtakiwa, akiwa amechomwa visu, kimoja shingoni na kingine kwenye titi la kushoto. Mheshimiwa jaji kufanyika kwa kitendo hicho haimaanishi kuwa mshtakiwa ndiye aliyefanya na hakuna ushahidi wa kutosha kulithibitisha jambo hilo uliokwishatolewa mbele ya mahakama yako tukufu!”
Mahakama ilikuwa kimya ikimsikiliza wakili Lydia Ishegoma aliyekuwa akimtetea Anne mahakamani, alikuwa ameifanya kazi hiyo kwa miaka kumi na siku hiyo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho! Aliamua kumtetea Anne kwa sababu walisoma wote na aliyefanyiwa na mama yake mzazi yalimsikitisha sana kiasi cha kusema hata yeye asingeweza kuvumilia.
“Mheshimiwa Jaji mtu yeyote angeweza kufanya hivyo na kisha kuutupa mwili wa marehemu nje ya nyumba yake na isitoshe visu vyote vilipopimwa na wataalam wa vidole haikuonyesha alama za vidole vya aina yoyote! Jambo linalonifanya niamini muuaji alikuwa mtaalam wa kazi hiyo kuliko anavyoonekana mshtakiwa! Hivyo naiomba mahakama yako tukufu imwachie mshtakiwa huru kwa sababu ameteseka kwa muda mrefu na ni mama wa watoto wawili ambao baba yao alikufa miaka mingi!” Alimaliza wakili Lydia kutoka chama cha mawakili wanawake nchini Tanzania.
Maneno ya wakili Lydia yalionekana kumwingia jaji akilini na ndani ya moyo wake, alijikuta akiingiwa na huruma kwa sababu alishaisikia historia ya jambo lililopelekea Anne kumuua mama yake mzazi!
Alitaka sana kumwachia Anne huru lakini alishindwa atumie kifungu gani cha sheria wakati ushahidi uliokwishatolewa mahakamani uliyoonyesha wazi kuwa Anne ndiye alimuua mama yake.
Huku moyo wake ukiwa umejaa huzuni Jaji Raphael aliigonga meza iliyokuwa mbele yake kuashiria kuwa mahakama ilikuwa inapumzika kwa muda wa dakika tano na alitoka mahakamani kupitia mlango wa nyuma na alikwenda moja kwa moja hadi ofisini kwake ambako aliendelea kuwaza mambo mengi juu ya Anne.
Watu wote ndani ya mahakama baada ya Jaji kuondoka waliendelea na minong’ono kimya kimya wakimwongelea Anne aliyekuwa ndani ya kizimba akilia! Kilichomfanya Anne alie si kingine bali ni watoto wake.
“Bila Patrick na Nancy wala nisingejali kifo changu kwani kufa ni kulala! Aliwaza Isabella.
****
Mwili wake wote ulinuka na alihisi nguo zake kulowana! Inzi wengi walimzunguka na aliwapiga kwa mkono wake kuwafukuza. Anne alijua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea, kwani mwaka mmoja kabla ya kutiwa mahabusu alipatwa na ugonjwa wa ajabu, ugonjwa uliomtesa na kumpa fedheha kubwa katika jamii iliyomzunguka, ni ugonjwa huo ndio uliomfanya mumewe na baba wa watoto wake Huggins William kijana wa kimarekani kumwacha na kuanza kuishi na mwanamke mwingine aliyeitwa Delilla.
Ni mwanamke huyo ndiye aliyempa sumu Huggins, mwanaume ambaye Anne alimpenda na kumuua! Mpaka siku hiyo ya hukumu bado Anne aliamini bila kupatwa na ugonjwa huo, Huggins asingemkimbia kwenda kwa Delilla na asingekufa.
“Mimi naona nilichomfanyia mama ni sawa tu! Kwani alichonifanyia yeye mimi yaani niwe namiminika hedhi kila siku kwa miaka kumi! Mama alistahili kifo na kama kuna maisha baada ya kunyongwa kwangu huko ahera ninakokwenda ni lazima nimuue tena! Alinifanyia ubaya mkubwa mno na ninashangaa kwanini Jaji hanihukumu ili nife, acha nihukumiwe nife niende zangu, nina thamani gani hapa duniani mie ni bora kifo!”Aliendelea kwanza Anne.
****
Dakika tano baadaye Jaji alirejea tena mahakamani na mahakama iliendelea.
“Anne!” Jaji aliita kwa huruma lakini Anne alikaa kimya bila kujibu kitu, watu mahakamani walishangaa kuona jaji Raphael Mpoki akiongea kwa upole kiasi kile siku hiyo kwani alikuwa ni jaji aliyeaminika kuwa mkali kupita majaji wote nchini Tanzania.
“Anne!”Jaji aliita tena safari hii akitabasamu, watu wote wakajua ushindi ulikuwa ni wa Anne.
“Naa..m mhe…shimi…wa!” alijibu Anne huku akilia.
“Usilie binti tafadhali niambie kwanini nisikuhukumu kifo kwa mauaji ya kikatili uliyoyafanya kwa mama yako kwa sababu kila aina ya ushahidi kuwa ulifanya tendo hilo!”Jaji alimwambia Anne huku akimwangalia kwa huruma!
Watu wote mahakamani walikaa kimya wakisubiri jibu la Anne, hata watoto wake ambao tayari walisharudishwa ndani ya mahakama pia walikuwa wakisubiri jibu la mama yao, walitaka dunia ibadilike na mama yao asihukumiwe kifo wala kifungo cha maisha, walitaka aachiwe huru ili waonje na kufaidi upendo wa mama! Walikuwa wemechoka kujisikia yatima na kushinda kutwa nzima wakiangalia picha za mama na baba yao!
Anne alijaribu kufungua mdomo ili aongee kitu lakini maneno hayakutoka kwa sababu ya kwikwi iliyokuwa imekaba kooni!
“Sema Anne, sema usiogope ongea na mimi unataka nikufanye nini maisha yako yapo mikononi mwangu?” Alisema jaji Raphael Mpoki lengo lake likiwa ni kumshawishi Anne aombe kuachiwa huru ni hicho tu alichokuwa akisubiri ili amuachie aende zake.
“Mhesh..imi...wa Ja..ji!” Anne alijikaza na kujikuta akiongea ingawa kwa shida na watu wote walikaa kimya kumsikiliza.
“Ndiyo nastahili kifo na ninaomba unihukumu kifo, ninaomba unihukumu kunyongwa lakini kabla sijafa naomba niseme maneno yafuatayo kwa watu waliopo hapa mahakamani! Ndugu zangu ni wengi wananyongwa na ni wengi wameua lakini hawakutakiwa kufanya hivyo , mimi si muuaji ila nililazimika kuua kwa sababu sikuwa na njia yoyote ya kuwalinda watoto wangu, kwa sababu mama yangu aliyenizaa mimi na kunileta duniani alitaka kuwaua wanangu ingawa tayari alikwishawaua watoto wangu wengine wawili, William na Henry!”
Mahakama ilikuwa kimya watu wote wakisikiliza kwa makini maneno ya Anne aliyoyaongea huku akilia.
“Nilipokataa kumpa watoto wangu akaniroga na kunipa ugonjwa wa kupata hedhi kila siku na hivi mnavyoniona hapa niliposimama nguo zangu zote zimeloa na nimekuwa katika hali hii kwa muda wa miaka kumi na moja! Macho yangu ni meupe kwa sababu nimepoteza damu nyingi na sili chakula kizuri gerezani! Na yote haya alinifanyia mama yangu mwenyewe ambaye bila yeye mimi nisingeifahamu dunia, mlitegemea nifanye nini wakati alitaka kuniulia watoto wangu Patrick na Nancy? Ni yeye aliyesababisha kifo cha mume wangu na kuniharibia maisha yangu kwa kweli ilibidi nimuue mama yangu ili kuokoa maisha ya watoto wangu NA SINA LA KUFANYA MHESHIMIWA JAJI NAOMBA UNIHUKUMU KIFO ILI NINYONGWE NIMFUATE MAMA HUKO ALIKO NA NIKIMKUTA NI LAZIMA NIMUUE TENA KWA SABABU AMENITESA SANA NA MARA KWA MARA NAJIULIZA NI KWANINI ALINIZAA!”
Maneno hayo ya Anne yalimfanya wakili wake aliyejua siku hiyo ushindi ulikuwa wao apigwe na butwaa na kujikuta akiziba mdomo wake kwa mikono yake yote miwili, kwa utetezi aliokuwa ametoa alifahamu wazi Anne angeachiwa huru lakini maneno aliyoyatoa Anne pale mahakamani yalimfanya wakili wake atokwe na machozi!
“ANNE WHAAAAT!”(Anne nini?) wakili wa Anne ajikuta akipiga kelele.
“Sorry Lydia I want to die! I’m very sorry for wasting your ten years time trying to defend me in court but God will pay you for me!”(Samahani Lydia nataka kufa, nasikitika kwa kukupotezea muda wako wa miaka kumi ukijaribu kunitetea mahakamani lakini Mungu atakulipia!)
Kwa historia aliyoitoa Anne watu wote mahakamani walijikuta wakimwanga machozi kumlilia Anne, maneno yake yaliwachoma watu wengi, waligundua alifanyiwa unyama mkubwa ambao binadamu yeyote mwenye akili ya kawaida asingeweza kuuvumilia, hata jaji Mpoki pia alikuwa akijifuta machozi kwa sababu ya kulia, maaskari pia walishindwa kuvumilia na kujikuta wakitokwa na machozi.
“Nimesikitishwa sana na historia aliyoitoa na sina la kufanya zaidi ya …………….!” Jaji Raphael Mpoki alijikuta akishindwa kuvumilia na kuangua kilio mbele ya watu wengi waliokuwa mahakamani, watoto wa Anne na mama yao mdogo pia waliendelea kulia machozi, mahakama nzima ilijaa vilio na maaskari walijaribu kunyamazisha mahakama bila mafanikio.
Je nini kitaendelea?
Je Anne atahukumiwa kifungo cha gerezani au atanyongwa?
Je nini kilitokea katika maisha ya mwanamke huyu?
Kuna mambo mengi ya kusisimua, tukutane Ijumaa mahali hapa. 


HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 2
MTUNZI: ERIC JAMES SHIGONGO
Mwanamke Anne amefikishwa mbele ya mahakama kwa kosa la kumuua mama yake kwa kumchoma kisu. Tukio hilo linawashtua watu wengi na siku ya hukumu yake, watu wanakusanyika kwa wingi mahakamani.
Anne anabaki akilia tu, ndani ya mahakama hiyo, kuna watoto wake wake mapacha, msichana aliitwa Nancy na wa kiume aliitwa Patrick. Hakimu ambaye alikuwa akisimamia kesi hiyo aitwaye Raphael Mpoki anamuonea huruma Anne, hataki kumuhumu kifo na hivyo kumuuliza alitaka amfanyie nini, cha ajabu, Anne anasema kwamba anachokitaka ni kufa tu na ni kweli alimuua mama yake.
Mahakama inashtuka, wakili aliyekuwa akimsaidia aitwaye Lydia naye anashtuka, haamini kama mteja wake aliyetumia nguvu nyingi kumsimamia anakihitaji kifo kwa gharama yoyote ile.
Kwa uchungu mkubwa moyoni mwake, tena huku akiwa analia kama mtoto, Anne anaanza kusimulia kilichotokea maishani mwake na sababu iliyosababisha kumuua mama yake, historia ambayo ilibadilisha kila kitu.
SONGA NAYO...
1972, kisiwani Kome:
Kabila la Wazinza ni miongoni mwa makabila madogomadogo mkoani Mwanza, watu wa kabila hili hasa huishi wilayani Sengerema na makao yao makuu yakiwa kisiwani Kome na maeneo ya Nyakalilo wilayani humo. Wazinza ndilo kabila la asili wilayani Sengerema ndiyo maana eneo lote baada ya kuvuka tu kwenye kivuko cha Kamanga huitwa UZINZA!
Makabila mengine kama Wasukuma, Wakerewe, Wajita ni wahamiaji tu katika maeneo hayo ili kutafuta maisha baada ya kusikia maeneo hayo yalikuwa na rutuba ya kutosha!
Ukoo wa mzee Kamanzi ulikuwa mkubwa sana katika jamii ya Wazinza na ni ukoo ulioheshimiwa na kuogopwa na kila mtu ndani ya kabila hilo kwani uliaminika kuumiliki mzimu hatari ulioitwa Lutego! Mzimu huo uliua watu, ulimaliza koo mbalimbali na watu waliojaribu kwa namna moja au nyingine kupingana na ukoo huo.
Mtu yeyote aliyefanya maudhi katika ukoo wa Kamanzi alitumiwa mzimu wa Lutego uliwaua ndugu zake wote katika ukoo wake tena mmoja baada ya mwingine mpaka kuumaliza kabisa ukoo huo, katika Nyumba iliyotupiwa mzimu huo viumbe vyote vyenye damu kuanzia watu, mbuzi, kuku hadi sisimizi vilikufa!
Ukoo wa Kamanzi ulitisha! Hakuna mtu aliyethubutu kuigusa familia yoyote katika ukoo huo, mzimu wa Lutego uliokuwepo katika familia hiyo kwa miaka karibu mia tano iliyopita, ukihama kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine.
Ni mwanamke mmoja tu katika ukoo aliyeteuliwa kuishi na mzimu huo ndani ya mwili wake, huyo walimwita Malkia au Maha! Na huyo Maha alipokufa alimwachia mtoto wake yeyote wa kike katika familia yake ambaye mzimu ulimwingia naye alikaa na mzimu huo mpaka mwisho wa uhai wake na alipokaribia kufa alimrithisha mtoto wake mzimu huo.
Mzimu huo ulirithishwa kwa mtu mwingine kwa kumpa hirizi ya chuma ambayo ilitoka yenyewe mwilini kwa Maha aliyekufa kabla ya kuzikwa! Hirizi hiyo alilishwa mtoto aliyechaguliwa kuurithi mzimu huo siku chache baada ya mazishi tena usiku wa manane katika sherehe kubwa iliyofanyika katikati ya ziwa Victoria na watu wengi walioamini uchawi walihudhuria, ilikuwa ni lazima watoto wawili mapacha watolewe kafara kabla Maha hajameza hirizi.
Mrithi wa mzimu huo katikati ya miaka ya sitini na sabini alikuwa Bi Isabella Katikilo, mama huyu aliabudiwa sana na ukoo mzima na alikuwa mwanamke mzuri ambaye ilikuwa si rahisi hata kidogo kufahamu kwamba alitembea mwilini na mzimu uliowaua watu!
Baadaye mama huyo aliolewa na bwana Innocent Mataruma na kuzaa naye mtoto mmoja wa kike wakampa jina la Bibi Anna ambalo baadaye lilikuja kubadilishwa na sista mmoja huko Kome aliyemwita mtoto huyo Anne! Mtoto huyo alikuwa mtoto mzuri na aliyemvutia karibu kila mtu aliyemwona na wengi walipenda kumbeba mtoto huyo.
Wana ukoo walioijua siri ya Isabella Katikilo walimsikitikia mtoto huyo kuzaliwa katika ukoo huo kwani walijua ni yeye ndiye angeurithi mzimu wa Lutego!
Shuleni akiwa na umri wa miaka saba Anne alionyesha uwezo mkubwa sana katika masomo yake, tangu darasa la kwanza hadi la saba alishika namba moja kila siku katika masomo yake, kila mtu aliamini Anne angekuja kuwa mtu mkubwa katika maisha yake!
Alipofaulu mtihani wake wa darasa la saba na kuingia kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Ngaza iliyopo mjini Mwanza, hakuna mtu aliyeshangazwa na matokeo hayo kwani hilo lilikuwa ni tegemeo la watu wengi.
Uzuri wa sura yake shuleni ulifanya wanafunzi wengi kumbadika jina la ‘Miss Ngaza’. Alikuwa mrefu, alikuwa na miguu ya kuvutia na alikuwa na umbile zuri la kuvutia kwa nyuma! Kila mtu alimtamani Anne si walimu tu bali hata wanafunzi wa shule jirani ya Nsumba iliyokuwa ya wavulana tupu!
Magari ya matajiri wa Mwanza mjini kila siku ya kutembelea wanafunzi ilipofika, walifurika wakimtaka msichana huyo, lakini hakuna aliyefaulu kuiona nguo ya ndani ya Anne, wasichana wenzake walimshangaa kwanini kwa uzuri aliokuwa nao hakuwa na mpenzi ambaye angemtunza badala ya kuendelea kupata shida ndogondogo shuleni!
“Kwanini usimkubali tu hata Huggins?” Dina rafiki mkubwa wa Anne alimwambia kila siku iliyokwenda kwa Mungu.
“Siwezi Dina, ningependa kuwa na mpenzi lakini siwezi kufanya hivyo!”
“Kwanini lakini?”
“Siwezi kukueleza hata siku moja hiyo ni siri yangu mimi mwenyewe!”
Anne alihitaji sana kuwa na mpenzi lakini maneno aliyoambiwa na mama yake kabla hajaondoka nyumbani yalimtisha!
“Mwanangu Anne usijaribu kufanya mapenzi na mwanaume yoyote katika maisha yako kabla hujanirithi mimi, wewe ndiye mrithi wangu ni lazima uyatayarishe makazi ya nanihii sawa?”
“Makazi ya nani mama?”
“Utakuja kufahamu baadaye ila usijitie najisi bure na siku utakayofanya hivyo mwanaume utakayefanya naye atakufa kifo kibaya sana mbele ya macho yako!” Yalikuwa ni maneno ya mama yake yaliyomtisha mno Anne na kumfanya awaogope wanaume.
Ndiyo aliogopa lakini alipofikisha umri wa miaka 17 akiwa kidato cha tatu mwili wake ulianza kumlazimisha afanye tendo hilo na kujiliwaza.
****
“Anne tangu leo nimekuchagua utakuwa unanipikia chai hapa ofisini kwangu!” ilikuwa ni sauti ya mwalimu mkuu wa shule ya wasichana ya Ngaza aliyeitwa Joseph Lutambi!.
“Sawa mwalimu nakushukuru sana na nitakuwa mwaminifu!” Alijibu Anne.
Hiyo ndiyo ilikuwa tabia ya mwalimu Lutambi, kila mwaka alibadilisha msichana wa kumpikia chai, alimchukua huyu na baada ya kufanya naye mapenzi alimfukuza ofisini kwake na kuchagua tena msichana mwingine! Ofisi yake ilikuwa ni kama nyumba ya wageni ya chapuchapu na ilikuwa na kitanda ambacho yeye alidai ni cha kujipumzisha nyakati za mchana, ukweli ni kwamba hakikuwepo kwa ajili ya kazi hiyo bali kazi ya kufanyia ngono na wanafunzi kila walipomtayarishia chai mwalimu Mkuu ofisini kwake.
Siku zote alimtamani Anne sifa zake alizipata kuwa hakuwa na uhusiano na mvulana yoyote na iliaminika alikuwa bikira!
“Nitamuanza mimi, mimi dume bwana!”
****
Ilikuwa siku ya Ijumaa mchana wakati wa mapumziko ya chakula cha mchana mwalimu Lutambi alimwita Anne ofisini kwake, mvua kubwa sana ilikuwa ikinyesha kiasi kwamba Anne alilowa wakati akikimbia ofisini kwa Mwalimu.
Alipoingia tu ofisini mwalimu alifunga mlango nyuma ya Isabella na kudumbukiza funguo mfukoni mwake.
“Anne leo nataka ufanye kama ambavyo wenzako waliopitia ofisi hii wamekuwa wakifanya!”
“Kwa vipi mwalimu?”
“Ni lazima tulale!”
“Tulale una maana gani mwalimu!”
Kabla mwalimu Lutambi aliyekuwa mrefu na aliyejaza misuli mingi hajajibu swali hilo alimkamata Isabella na kumtupia kitandani!
Akampanua miguu yake kwa nguvu! Mvua kubwa tena ya mawe ilikuwa kinyesha kiasi kwamba sauti ya Anne haikufika nje ya ofisi iliyokuwa imefungwa vilivyo!
“Mwalimu niachie mimi sitaki mchezo huo!”
“Hutaki nini? Wenzako wote wamewezaje uwe wewe?”
“Mwalimu kwangu mimi ni mwiko utapata matatizo!”
“Matatizo gani? Acha yaje tutakabiliana nayo mimi najulikana hadi wizarani siogopi kitu!”
“Siyo hivyo utakufa!”
“Nitakufa? Ataniua nani na mimi ni jiwe!”
“Mwalimu utakufa!”
Ilikuwa kukurakakara kitandani hatimaye mwalimu alifanikiwa kumwingilia Isabella kwa nguvu, alikuwa amembaka msichana yule mdogo na kumharibu.
“Anne kumbe ulikuwa bado?”
Anne hakujibu kitu aliendelea kulia, ghafla mwalimu Lutambi alianguka chini mbele ya Anne, macho yakamtoka na ulimi ukatoka nje urefu wa mkono wa binadamu na kuning’inia chini na mwili wake ulikakamaa ghafla, damu nyingi zikimtoka masikioni, puani na mdomoni, alikuwa amekufa!
Anne alinyanyuka kitandani akiwa katika maumivu makali na damu zikimtoka sehemu za siri alikuwa akilia machozi.
“Unaona sasa mwalimu nilikuambia uache hukunisikiliza!” alisema Anne kwa huzuni.
Je nini kitatokea?
Je Anne atahukumiwa kifo?
Fuatana na mtunzi mahiri wa simulizi hii ya kusikitisha na kusisimua siku ya Jumapili asubuhi. 

Post a Comment

Previous Post Next Post