HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 03----04


Mwanamke Anne amefikishwa mbele ya mahakama kwa kosa la kumuua mama yake kwa kumchoma kisu. Tukio hilo linawashtua watu wengi na siku ya hukumu yake, watu wanakusanyika kwa wingi mahakamani.
Anne anabaki akilia tu, ndani ya mahakama hiyo, kuna watoto wake wake mapacha, msichana aliitwa Nancy na wa kiume aliitwa Patrick.
Hakimu ambaye alikuwa akisimamia kesi hiyo aitwaye Raphael Mpoki anamuonea huruma Anne, hataki kumuhumu kifo na hivyo kumuuliza alitaka amfanyie nini, cha ajabu, Anne anasema kwamba anachokitaka ni kufa tu na ni kweli alimuua mama yake.
Mahakama inashtuka, wakili aliyekuwa akimsaidia aitwaye Lydia naye anashtuka, haamini kama mteja wake aliyetumia nguvu nyingi kumsimamia anakihitaji kifo kwa gharama yoyote ile.
Kwa uchungu mkubwa moyoni mwake, tena huku akiwa analia kama mtoto, Anne anaanza kusimulia kilichotokea maishani mwake na sababu iliyosababisha kumuua mama yake, historia ambayo ilibadilisha kila kitu.
Historia ya maisha yake inaanzia shule, huku akiwa hajui kama amepewa uchawi, mama yake anamtahadharisha kwamba hatakiwi kufanya mapenzi na mwanaume yeyote yule kwani akifanya hivyo mwanaume huyo atakufa.
Hajui kwa nini lakini anachokiahidi ni kutofanya mapenzi na mwanaume yeyote. Huku maisha ya shule yakiendelea, mwalimu wake mkuu, Lutambi anatokea kumtamani. Anapandwa na muhemko na hivyo kutaka kufanya naye mapenzi.
Anne anakataa kwa kumwambia mwalimu kwamba atakufa. Mwalimu Lutambi anabisha, anajiona mwanaume wa shoka, anamvamia Anne na kuanza kumbaka. Anapomaliza, ghafla anaanguka chini na kuanza kuhangaika, mwisho wa siku, anafariki dunia.
SONGA NAYO...
Pamoja na udhaifu wa kufanya mapenzi na wanafunzi mwalimu Lutambi alikuwa kipenzi kikubwa cha wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ngaza, hakuwa mkali kwao na alipenda sana kuendeleza taaluma, ni katika kipindi chake cha utawala ndiyo Shule ya Ngaza ilifanya vizuri zaidi kiasi cha wanafunzi kumi hadi ishirini kufaulu kwenda kidato cha tano!
Mwalimu Lutambi hakuwa kipenzi cha wanafunzi peke yake bali pia waalimu wenzake katika shule hiyo, aliishi nao vizuri na alijitahidi kuwatafutia nafasi mbalimbali za masomo ni katika kipindi cha utawala wake, waalimu watano kutoka shule hiyo walipata nafasi ya kuendelea na masomo ya chuo kikuu kuchukua digrii ya kwanza ya elimu!
Hivyo kifo chake cha ghafla kiliwashtua watu wengi, karibu kila mtu shuleni alilia, hakuna aliyejizuia! Familia yake ilichanganyikiwa na mkewe ambaye ndiye alikuwa amejifungua mtoto wao wa kwanza alilia mpaka kupoteza fahamu.
“Mume wangu alikuwa mzima tangu asubuhi wala hakuwa na homa, imekuwaje afe ghafla kiasi hiki?” alilia mwanamke huyo aliyejulikana kwa jina la Rosemary!
Wengi walishindwa kukieleza vizuri kifo cha mwalimu Lutambi na walimu walijiuliza maswali mengi bila majibu maafisa elimu wa mkoa na wilaya walipokuja, nao walichanganyikiwa kwa sababu kuliko na wiki kama moja tu mbele kabla mkutano wa wakuu wa shule haujafanyika.
Anne alikuwa katika wakati mgumu sana, wakati huo tayari alikuwa bwenini akiwa amejifunika na shuka akilia kwa sababu ya maumivu makali aliyokuwa nayo sehemu zake za siri! Mwalimu Lutambi alimjeruhi vibaya mno kiasi kwamba alishindwa hata kusimama wima.
“Hebu nendeni mkamwite Anne bwenini ili aje atueleze alichokishuhudia kabla ya kifo cha mwalimu!” mwalimu mkuu msaidizi aliwaamuru wanafunzi waliokuwa nje ya ofisi yake wakilia na wanafunzi watatu wa kidato cha pili waliondoka wakikimbia kuelekea bwenini ambako walimkuta Anne akiwa kitandani kwake.
“Unaitwa na mkuu wa shule msaidizi”
“Nikafanye nini jamani mimi naumwa?”
“Hata sisi hatujui!”
“Sawa basi nakuja!”
Baada ya kujibiwa wanafunzi waliondoka tena mbio kurudi ofisini ambako waliwakuta walimu wote wamekusanyika wakimsubiri Anne.
Anne aliteremka polepole kitandani kwake na kuanza kuchechemea akielekea ofisini kwa mwalimu, macho yake yalikuwa mekundu kwa sababu ya kulia, alielewa ni kwanini alikuwa anaitwa, alijua walimu walihisi alielewa chanzo cha kifo cha mwalimu Lutambi! Ingawa kweli alifahamu sababu ya kifo lakini hakuwa tayari kuitoa!
Anne alikuwa tayari kufa kwa maumivu ya kubakwa aliyokuwa nayo kuliko kudiriki kufungua mdomo wake kusema maneno aliyoambiwa na mama yake ambayo aliamini ndiyo yalikuwa chanzo cha kifo cha mwalimu, alishindwa kuelewa angelifafanua vipi jambo hilo wakati hata yeye mwenyewe hakuielewa siri ya maneno aliyoambiwa na mama yake.
Kabla hajaingia ofisini alikutana na mwalimu wake wa Biolojia aliyeitwa mwalimu Kassanda, mwalimu aliyeonyesha kushangazwa na mwendo wa Anne.
“Anne vipi mbona unachechemea?”
“Nilijikwaa jana na tayari nina mitoki miwili mapajani hiyo ndiyo inanisumbua!” Anne aliuficha ukweli, hakuwa tayari kusema kitu chochote ambacho kingepelekea kugundulika kwa kilichotokea ofisini.
Kwa taabu alipanda ngazi na kuingia ofisini ambako aliwakuta walimu wote wamekaa duara wakimsubiri, walikuwepo pia maafisa elimu wa wilaya na mkoa, dada mkuu na kaka mkuu, kiti cha Anne kiliwekwa katikati ya walimu wote baada ya salamu walianza kumuuliza maswali wakitaka kujua kilichotokea kabla mwalimu hajaanguka chini na kufa!
“Anne hebu tuambie kilichotokea nafikiri wewe ndiye ulikuwa ukimpikia chai siyo?”
“Ndi….o…mwali….mu!” Anne alijibu kwa shida na alishindwa kuendelea.
“Kilitokea nini mpaka mwalimu akafa?” Afisa elimu alidaka kwa swali.
Badala ya kujibu swali hilo Anne alianza kulia tena walimu wote alijaribu kumbembeleza bila mafanikio, nusu saa baadaye akiwa bado yupo ofisini alitulia na walimu waliendelea kumdadisi ili aeleze kilichojitokeza.
“Hata mimi sijui!”Alijibu jibu la mkato.
“Ndiyo hujui, lakini kilitokea nini kabla?”
“Baada tu ya kumpa chai kabla hata hajainywa alianguka chini akaanza kutokwa damu puani na masikioni, macho yakamtoka na ulimi wake pia ukaning’inia nje, nilishtuka sana nikaanza kupiga kelele nikiomba msaada ndipo mwalimu Malima alipokuja na kumkuta mkuu wa shule ameanguka chini amekufa!
“Uliweka kitu kingine kwenye chai?” Afisa elimu alihoji tena.
“Hakuna kitu zaidi ya sukari na majani mkuu!”
“Kweli?”
“Ndiyo mwalimu!”
Kila kona ya shule ya Ngaza ilifunikwa na vilio, wanafunzi walilia na kugalagala chini wakimlilia mwalimu wao Lutambi, kifo chake kilikuwa cha ghafla sana na kilisababisha mshtuko mkubwa mno miongoni mwao! Jina la mwalimu Lutambi lilitajwa kila sehemu katika vilio vya wanafunzi wake.
Hali hiyo ilimsikitisha sana Anne ambaye pia alishindwa kuelewa ni nini hasa kilimpata mwalimu Lutambi mpaka kufa kifo cha aina ile tena baada ya kumbaka!
“Mwanangu Anne usije ukafanya tendo hilo mtu utakayefanya naye atakufa!” Maneno ya mama yake yalimwijia kichwani.
Pamoja na kuyakumbuka maneno hayo bado alishindwa kuelewa ni kitu gani kilichomuua mwalimu Lutambi, kifo chake pamoja na kwamba alimbaka kilimfanya amwonee huruma mwalimu kwa yaliyompata! Anne alilia akimtupia mama yake lawama nyingi.
****
Ndugu wa marehemu mwalimu Lutambi walishinikiza mwili wake ufanyiwe uchunguzi kabla ya kuzikwa na pia chai iliyokuwa mezani kwake kabla ya kifo ilichukuliwa na kupelekwa kwa mkemia mkuu Dar es Salaam ili kufanyiwa uchunguzi kwani kulikuwa na hisia pengine Anne alimnywesha mwalimu Lutambi sumu! Aliitwa kituo cha polisi kutoa maelezo yake na ilibidi kwa siku nne atiwe ndani ili kuisaidia polisi katika upelelezi wake.
Majibu ya uchunguzi wa mwili marehemu yalipotoka yalionyesha mwalimu Lutambi alikufa kwa ugonjwa wa shinikizo la damu! Ni majibu hayo ndiyo yaliyomweka huru Anne kutoka mahabusu ingawa ndugu wa marehemu hawakuridhika na majibu hayo.
Mazishi ya mwalimu huyo kipenzi cha wanafunzi yalifanyika katika Makaburi ya Nyegezi mjini Mwanza na wanafunzi wa shule zote za jirani ya Ngaza walihudhuria mazishi yake na kufanya idadi ya watu waliokuwepo mazishini kuwa wengi mno.
Anne alijisikia vibaya kila alipoona watu wakilia machozi makaburini, alijua wazi ni yeye aliyesababisha machozi ya watu wote kumwagika alijisikia muuaji ingawa hakufahamu aliua vipi? Hata yeye hakufahamu ilivyotokea ingawa aliamini wazi mama yake alifahamu chanzo cha kifo hicho!
Mwezi mmoja tu baada ya mazishi mwalimu majibu kutoka kwa mkemia mkuu nayo yalirudi na kuonyesha chai aliyokunywa marehemu siku ya tukio pia haikuwa na sumu yoyote kama ilivyodhaniwa! Na wanafunzi waliokuwa wameanza kumchukia Anne wakifikiri alimpa sumu mwalimu wao walifurahi kupata majibu yao na uhusiano wao na Anne aliyetengwa na wanafunzi wenzake ulianza kurejea.
Lakini pamoja na hali hiyo ndani ya nafsi yake Anne hapakuwa na amani hata kidogo, aliendelea kujisikia muuaji kwani alijua wazi kuwa kifo cha mwalimu kilimhusu.
“Nikienda likizo ni lazima mama anieleze ni kwanini mwalimu alikufa na ni kwanini aliniambia nisifanye mapenzi, nitafanyeje mimi wakati mwili wangu unahitaji? Sitakubali nataka kujua!”
****
Miongoni mwa watu ambao hawakuamini kuwa kifo cha mwalimu Lutambi kilisababishwa na shinikizo la damu alikuwa ni kaka yake marehemu, Leonard huyu aliamini sana uchawi na ushirikina, baada ya mazishi alilazimika kusafiri hadi sehemu za milima huko Sumbawanga, kwa mganga mmoja wa kienyeji ili kufahamu vizuri chanzo cha kifo cha mdogo wake na jibu alilopewa na mganga wake maarufu mzee Kipili lilimtia hasira kubwa hasa baada ya kuonyeshwa picha ya Anne katika beseni la maji na kuambiwa ni yeye ndiye alimuua mwalimu si kwa sumu bali kwa uchawi wa kabila la Wazinza.
“Msichana huyo ni malkia mtarajiwa na hatakiwi kufanya mapenzi na mtu mpaka atakapoolewa na ikitokea akifanya hivyo mwanaume atakayefanya naye atakufa! Nduguyo alimbaka msichana huyo ndiyo maana akafa!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
Baada ya kutoka hapo Leonard alikwenda tena kwa waganga wengine watatu na jibu liliendelea kuwa hilohilo na kuamua kurejea nyumbani Mwanza akiwa na hasira zake kifuani.
Jambo la kwanza alilolifanya baada ya kufika Mwanza ni kuwataarifu ndugu zake juu ya majibu aliyoyapata na kila mtu alisikitika sana, hasa mke wa marehemu na jioni ya siku hiyo hiyo Leonard aliivamia Shule ya Ngaza akiwa na panga mkononi na kufanya fujo kwa lengo la kumshambulia Anne na kumuua lakini walinzi wa shule walifanikiwa kumzuia kabla hajafika bwenini kwa Anne na kumuondoa shuleni.
“Weweeeeeee! Unataka uniue mimi nimekukosea nini?” Anne alisema huku akimsonta na kidole.
“Usitembee kabisa mitaani, siku yoyote nitakayokuona nje ya ngome hii nitakumaliza! Huwezi kumuua ndugu yangu hivihivi mchawi mkubwa wewe!” Alifoka Leonard huku wanafunzi wakiwa wamejaa na kushangaa.
Baada ya kufoka Leonard aliondoka zake, kilichosikitisha zaidi siku iliyofuata taarifa zilikuja shuleni wengi walisikitika mzee yule aligongwa na treni na kufa!
Baada ya siku hiyo hisia zilianza kusambaa kuwa Anne pamoja na uzuri wake alikuwa mchawi na akawa anaogopa hata kutoka shuleni kwa vitisho vya ndugu wengine wa marehemu mwalimu Lutambi.
****
Shule ilipofungwa gari la shule lilimchukua hadi kituo cha mabasi ambako alipanda basi la kwenda Sengerema, nyumbani kwao alimsimulia mama yake kila kitu.
“Mama hali ni mbaya sana shuleni!”
“Kwanini mwanangu!”
“Watu wawili wameshakufa kwa sababu yangu!”
“Kwanini ulifanya mapenzi na mtu?”
“Nilifanya lakini si kwa ridhaa yangu mwalimu wangu alinibaka na palepale alikufa! Wa pili ni ndugu yake yeye alikuja shuleni na panga kwa lengo la kutaka kuniua kesho yake tulisikia kuwa aligongwa na treni akafa!”
Anne alieleza kila kitu juu ya yaliyompata na kutaka kujua kutoka kwa mama yake kilichokuwa kikiendelea.
“Siwezi kukueleza kitu hivi sasa mwanangu utafahamu baadaye mimi nikifa ila bado nasema hutakiwi kufanya tendo la ndoa na mtu yeyote yule mpaka baada ya mimi kufa na wewe kuolewa na hutakiwi kumnyoshea mtu kidole, ukifanya hivyo tu mtu huyo atakufa!”
“Mama nini lakini? Hebu tafadhali nieleze kinachoendela nataka kufahamu siwezi kuendelea kuishi hivi!” Anne alijikuta akifoka.
“Hapana Anne nikikueleza sasa hivi nitakufa mimi, sitaki kabisa kutoboa siri hii!”
Anne alilia machozi kwani alitaka sana kufahamu jambo lililokuwa likiendelea mwilini mwake na alikumbuka kumwonyesha kidole kaka yake marehemu mwalimu Lutambi!
“Ndiyo sababu alikufa, jamani mimi nitaishije katika hali hii?”
****
Baada ya likizo yake Anne alirejea tena shuleni na kuendelea na masomo, wanafunzi wenzake walishirikiana naye vizuri ingawa kuna baadhi bado walimwogopa kwa madai alikuwa mchawi ingawa hapakuwa na mtu aliyekuwa na uhakika na jambo hilo.
Pamoja na hayo bado Anne aliendelea kuwavutia na wanaume wengi walioendelea kumsumbua wakimtaka mapenzi kila siku, hata walimu wake hawakumwogopa, hakuna aliyekuwa tayari kuamini kuwa Anne ndiye alimuua mwalimu Lutambi!
Wavulana wengi waliokuja shuleni kuwatembelea wasichana wao walipomwona Anne walishtuliwa sana na uzuri wake na kujikuta wakianza kumfukuzia kwa nguvu na wakati mwingine walipoleta zawadi kwa wapenzi wao na yeye walimletea kama njia ya kumsogeza karibu.
Mmoja wa wavulana waliovutiwa sana na uzuri wa Anne alikuwa Dioniz Edward , huyu alikuwa ni mmoja wa vijana waliojaliwa sura nzuri sana duniani kiasi kwamba wanafunzi wenzake wa Shule ya Nsumba alikokuwa kiranja mkuu walimbandika jina la School HB, wakiamaanisha yeye ndiye alikuwa mzuri kuliko wavulana wote shuleni kwao!
Dioniz alikuwa mpenzi wa Emmaculata, msichana aliyesoma darasa moja na Anne, mara kwa mara alikwenda shule ya Sekondari ya Ngaza kumtembelea msichana Emmaculata ambaye pia alikuwa mrembo kupindukia, ingawa si kama Anne! Kama ni urefu wote walikuwa warefu na kama ni miguu mizuri wote walikuwa nayo na kama ni mianya wote walikuwa nayo!
“Emma kwa kweli ninampenda sana msichana huyu!”
Mwanzoni Emmaculata alifikiri labda alichoambiwa na Dioniz kilikuwa ni utani, lakini alishangaa mwezi mmoja baadaye alipowakuta Anne na Dioniz wamesimama peke yao ufukweni, siku hiyo Dioniz alikuja shuleni bila kumtaarifu Emmaculata na kwenda ufukweni kutanua na Anne!
Emmaculata alilia na kuanza kumvuta Dioniz lakini haikuwezekana kumshawishi kwani alishalewa penzi la Anne! Dioniz alikataa kuondoka.
“It is too late Emma, at the moment I’m in love with Anne!”(Umechelewa Emma kwa sasa hivi nina mapenzi kwa Anne!)
“Kweli Dioniz?”
“Ndiyo!”
“Hebu njoo basi kwanza nikueleza kitu!”
Dioniz aliitikia mwito huo na kumfuata Emmaculata pembeni alipokuwa amesimama huku Anne akitabasamu pembeni!
“Huyu msichana ni mchawi utakufa Dio!”
“I’don’t care, jambo hilo nimelisikia sana lakini najua huo ni uongo mnampakazia ili asifukuziwe!”
“Dio!”
“Nini?”
“Achana naye huyo binti!”
“Haiwezekani tena Emma niache nifanye kitu ambacho moyo wangu unataka!”
Kwa hasira Emma alimfuata Anne na kuanza kumfokea matusi makubwa akimwita mchawi aliyetumia madawa kuvuruga mapenzi ya watu!
“We Emma usinitukane tafadhali!”
“Nini? Fanya unachotaka!”
Anne alipotaka kumsonta Emma kwa kidole chake aliyakumbuka maneno ya mama yake “Siku zote usimsonte mtu yeyote kidole ukifanya hivyo atakufa!”
Baada ya siku hiyo Anne na Emmaculata walinuniana kwa sababu ya Dio! Na mwili wa Anne ulizidi kusisimka na kumfanya atamani kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Dio hasa alipowasikia wanafunzi wenzake wakiliongelea tendo hilo bwenini, alitamani sana kuwa na mpenzi lakini aliogopa kuua tena kama ilivyotokea kwa mwalimu Lutambi Lakini baadaye alilazimika kumkubali Dio
“Dio nimekubali lakini mimi na wewe hatutafanya tendo la ndoa ila tutafanya mapenzi ya kiwokovu, tutaongea kubadilishana mawazo lakini siyo ngono!”
“Unaogopa Ukimwi sana eeh!”
“Sanaaaaa, sitaki kufanya mapenzi kabla ya wakati!”
“Mimi bora tu niwe na wewe darling!”
Walikumbatiana na kupigana mabusu! Walipoachiana Dioniz alikuwa akiumwa kichwa ghafla lakini baadaye kilitulia, alipomwambia Anne kuhusu maumivu hayo aliielewa sababu.
Uhusiano wao ulidumu kwa muda mrefu sana na mara kwa mara Dioniz alimtembelea Anne shuleni, Anne pia alifanya hivyohivyo! Katika uhusiano wao hata siku moja hawakuwahi kufanya tendo la ndoa ingawa mara nyingi Dioniz alijaribu kumwomba Anne wafanye hivyo.
****
Ilikuwa ni siku ya mawingu na ngurumo nyingi angani lakini ni siku ambayo muziki mzito ulitanda kila mahali ndani ya ukumbi wa shule ya Ngaza, ilikuwa ni siku ya furaha, wanafunzi wakifurahia wenzao kumaliza kidato cha nne! Wakati huo Anne alikuwa kidato cha tatu akiwa na mwaka mmoja mbele kumaliza masomo yake ya sekondari.
Wavulana kutoka shule za sekondari ya wavulana Nsumba pamoja na Bwiru walikuwa shuleni hapa kucheza muziki na wasichana wa shule hiyo ya wasichana tupu, mmoja wa wanafunzi wa Nsumba waliokuokuwepo shuleni alikuwa ni Dioniz, aliyekuwa amemkumbatia Anne wakicheza bluzi pamoja, wote wawili walilingana urefu! Katika kucheza alimng’atang’ata Anne shingo na kumsemea sikioni jambo lililomfanya Anne ashindwe kuvumilia na kumfanya aanze kumtamani Dioniz.
“Labda leo itakuwa siku tofauti acha tu nijaribu lakini nampenda sana Dioniz nisingependa kumuua!” Anne alijipa moyo.
“Anne kwanini leo tusifanye kumbuka tumevumiliana sana?”
“Kufanya nini Dio?”
“Kwani wewe hujui?”
Ingawa alitamani kufanya hivyo Anne alijifanya kugoma, kitu pekee kilichomtisha kilikuwa ni kumbukumbu za kifo cha mwalimu Lutambi lakini baadaye alikubali.
****
Ilikuwa ni saa sita kamili ya usiku disko lilikuwa limepamba moto Dio na Anne walipotoka nje ya ukumbi na kwenda gizani bustanini ambako waliendelea kutomasa miili yao! Ilikuwa ni siku ya kwanza kwa Anne kusikia raha kama vile akiguswa na mwanaume aliyempenda.
“Lakini kichwa kinaniuma sana!” Dio alisema.
Muda mfupi baadaye Anne ilizidiwa mahaba na kujikuta akilala ardhini na Dionizi alimfuata bila kuchelewa na wote wawili walijikuta akili zao zikipepea angani! Akili za Anne zilirejea aliposhtukia matone ya damu yakimlowanisha begani! Alipomwangalia vizuri Dioniz aliuona ulimi wake ukiwa nje na macho yake yalikuwa yamemtoka! Picha ya marehemu mwalimu Lutambi ilimwijia akilini akajua Dio kafa!
Aliusukuma mwili wa Dio pembeni na kuanza kuutingisha akimwita jina lake lakini alikuwa ametulia.
“Dio! Dio! Dio! Dio!” Anne aliita mara nyingi lakini Dioniz hakutingishika na damu nyingi zilizidi kutoka puani na mdomoni!
“Dioniz umekufa!” Alisema Anne huku akilia mwili wake wote ulitetemeka kwa hofu.
“Sijui nitawaweleza nini wanafunzi wenzake! Ni lazima nitafute njia ya kuuficha ukweli huu kabla haujajulikana!” Aliwaza Anne kisha kuangalia huku na kule!
Baada ya mawazo hayo alitoka mbio hadi bwenini na kulivua shati lake lililokuwa na damu na kuvaa tisheti nyingine iliyokuwa na madoa ya damu aliichoma moto na bila kuchelewa alianza kutembea kuelekea tena bustanini alikomuacha Dioniz.
Alipofikiria kuhusu kuchimbia shimo ili aifukie maiti alishindwa kwa sababu hakuwa na jembe wala koleo, alipoangaza pembeni aliliona shimo la maji ya chooni na kukimbia hadi lilipokuwa na kulifungua.
“Hili linafaa!” Alijisemea mwenyewe moyoni mwake na kurudi hadi maiti ya Dio ilipokuwa na kuanza kuivuta hadi pembeni mwa shimo lile lengo lake likiwa ni kuidumbukiza lakini aligundua isingezama bila kufungwa na kitu kizito, alikimbia hadi jikoni ambako alichukua kamba mbili ndefu akaja na kuifunga na kuidumbukiza shimoni, alipomaliza kazi hiyo alifunika vizuri na kuondoka taratibu kuelekea ukumbini ambako aliendelea kucheza muziki huku akilia machozi.
Je nini kitaendelea?


HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 4
MTUNZI: ERIC JAMES SHIGONGO
Mwanamke Anne amefikishwa mbele ya mahakama kwa kosa la kumuua mama yake kwa kumchoma kisu. Tukio hilo linawashtua watu wengi na siku ya hukumu yake, watu wanakusanyika kwa wingi mahakamani.
Anne anabaki akilia tu, ndani ya mahakama hiyo, kuna watoto wake wake mapacha, msichana aliitwa Nancy na wa kiume aliitwa Patrick.
Hakimu ambaye alikuwa akisimamia kesi hiyo aitwaye Raphael Mpoki anamuonea huruma Anne, hataki kumuhumu kifo na hivyo kumuuliza alitaka amfanyie nini, cha ajabu, Anne anasema kwamba anachokitaka ni kufa tu na ni kweli alimuua mama yake.
Mahakama inashtuka, wakili aliyekuwa akimsaidia aitwaye Lydia naye anashtuka, haamini kama mteja wake aliyetumia nguvu nyingi kumsimamia anakihitaji kifo kwa gharama yoyote ile.
Kwa uchungu mkubwa moyoni mwake, tena huku akiwa analia kama mtoto, Anne anaanza kusimulia kilichotokea maishani mwake na sababu iliyosababisha kumuua mama yake, historia ambayo ilibadilisha kila kitu.
Historia ya maisha yake inaanzia shule, huku akiwa hajui kama amepewa uchawi, mama yake anamtahadharisha kwamba hatakiwi kufanya mapenzi na mwanaume yeyote yule kwani akifanya hivyo mwanaume huyo atakufa.
Mtu wa kwanza kabisa kufa alikuwa mwalimu wake, Lutambi. Anapoitwa na kuhojiwa, anakataa katakata. HAikuishia hapo, anajikuta akimuua mtu wa pili ambaye ni mwanafunzi handome aitwae Dioniz.
Hajui ni nini anachotakiwa kukifanya, akili yake imechanganyikiwa.
SONGA NAYO...
Anne alikuwa mwenye mawazo mengi, machozi yalizidi kumtoka alishindwa kuelewa nini kilikuwa kikitokea katika maisha yake.
“Tayari mtu wa pili amekufa sababu yangu, hivi nini hasa kilichomo mwilini mwangu? Ni mkosi gani nilionao mimi masikini?” alizidi kuwaza Anne.
Anne alijaribu kucheza muziki lakini haukuchezeka, mwisho aliamua kukaa kitini na kuendelea kufikiria jinsi ambavyo angekabiliana na tatizo lililokuwa mbele yake, alijua muda si mrefu Dioniz angetafutwa na wanafunzi wenzake kabla hawajaondoka shuleni na kwa sababu yeye alionekana naye kwa mara ya mwisho ni lazima angetakiwa kueleza mahali alikokuwa. Mawazo hayo yalimfanya Anne ashindwe kuvumilia na kujikuta akilia machozi.
Alipojaribu kumkumbuka Dioniz na kifo chake roho ilimuuma sana, Dioniz kijana mwenye sura nzuri alikuwa ndani ya shimo la maji machafu kutoka chooni, alipowaza hilo roho ilimuuma zaidi! Alijiona ni mkosaji mkubwa mbele ya Mungu!
“Yaani katika umri huu mdogo tayari nimekwishafanya mauaji ya watu wawili?!” aliwaza Anne na kuendelea kulia.
“Dada twende tukacheze!” Mvulana mmoja alisimama mbele ya Anne na kumwomba wakacheze wote.
“Mimi?”
“Ndiyo!”
“Sijisikii vizuri kwani hali yangu si njema nimebanwa sana na mafua”
“Kweli?!”
“Niwie radhi kaka yangu!” Anne alimjibu kijana mmoja wa Shule ya Sekondari ya Nsumba aliyetaka kucheza naye Blues ya Michael Bolton iitwayo “Soul Provider!”
“Hakuna tatizo dada yangu! Nakumbuka nilikuona na HB! Yupo wapi?”
“HB ndiye nani kaka yangu?”
“Dioniz, sisi shuleni humwita HB kwa sababu ya uzuri wa sura yake!”
Moyo wa Anne ulidunda kwa nguvu kufuatia swali hilo, aliuhisi ukichomoka na kuuacha mwili wake, hofu kubwa ilimkumba kwani alijua baadaye angetakiwa kueleza mahali alipokuwa Dioniz! Alikaa kimya akiwa amemkodolea macho mvulana aliyemuuliza.
“Dada sijui kama umesikia swali langu?”
“Umeulizaje kweli kaka yangu? Maana hapa ndani muziki umepamba moto na una sauti kubwa sana!”
“Nilikuuliza kuwa Dioniz umemwacha wapi? Maana mara ya mwisho ulikuwa naye!”
“Ah! Dioniz!...Ah!... Tuliachana naye kitambo na yeye akarudi hapa ndani, mimi nikaenda bwenini labda jaribu kupitapita hapa ukumbini utamuona!” Alijibu Anne huku akitetemeka!
“Ok wewe si ni Anne lakini?”
“Ndiyo!”
“Aisee kwanza nimefurahi sana kukutana na wewe ana kwa ana mimi naitwa Benedict, nasoma darasa moja na Dioniz na lengo langu kuja hapa Nganza lilikuwa ni kukutafuta wewe, lakini bahati mbaya Dioniz ameniwahi kuonana na wewe lakini hakijaharibika kitu! Kwanza kabisa wewe Anne ni mzuri!”
“Ahsante sana Benedict lakini hata wewe ni mzuri pia!”
“Ahsante sana, je, unaweza kuniruhusu nikae na wewe kidogo!”
“Unasemajeee?”
“Hakuna matatizo yoyote kaa tuu!”
Walijaribu kuongea mambo tofauti kuhusu masomo na sherehe nzima iliyokuwa ikiendelea lakini baadaye Benedict alimwekea Anne mkono begani.
“Anne ninakupenda na tafadhali kubali kuwa na mimi na siyo Dio, ninakupenda sana Anne tafadhali usiniangushe!”
“Mungu wangu mwingine tena huyu, nitafanya nini mie? Ee Mungu ni kwanini uliniumba na uzuri huu, halafu nikawa na kasoro hii, nitaendelea kuua watu hadi lini?” Aliwaza Anne na badala ya kufurahi Anne alianza kulia machozi mbele ya Benedict moyo wake ulikuwa bado haujatulia, kifo kilichompata Dio kilikuwa bado kikimsumbua akilini.
“Vipi mbona unalia?”
“Naomba uniache kaka!”
“Haiwezekani Anne ni vizuri unipe jibu zuri kabla sijarudi shuleni!”
“Siwezi kuwa na uhusiano na wewe kimapenzi!”
“Kwanini?”
“Usiniulize kwanini! Kama kweli unajipenda, achana na mimi kabisa na ufuate mambo yako!”Alijibu Anne kwa ukali na kuanza kunyanyuka kuelekea nje ambako Benedict aliendelea kumfuata huku akimbembeleza akubali.
“Najua ni kwa sababu umekutana na Dio mwenye sura nzuri kuliko mimi ndiyo maana unakataa lakini Dio atakuchezea tu ana wasichana wengi sana, mimi nataka kukuoa kabisa kama tutaelewana!”al
isema Benedict.
Juhudi za Benedict kumbembeleza Anne ili akubali ziligonga mwamba akaamua kurudi zake ukumbini, Anne naye alikwenda bwenini ambako alipanda kitandani na kuendelea kulia machozi, alishindwa kuelewa nini kingefuata.
Saa moja baadae alishitukia muziki umezimwa Bwaloni, aliponyanyuka na kuchungulia dirishani aliona wanafunzi wenzake wakitoka ukumbini huku wakishangilia na kufurahi, dakika kama mbili hivi baadaye wanafunzi wenzake wakaanza kuingia bwenini.
“Hakyanani ya leo ilikuwa kiboko, sijawahi kuona disco kali kama la leo hili!”
“Hata mimi!” wasichana wawili waliolala vitanda vya chini ya Anne sababu kitanda chao kilikuwa cha deki, waliongea huku wakivua nguo zao tayari kwa kwenda kuoga! Anne alikuwa amejifunika shuka hadi kichwani.
“Hivi viatu si vya Anne!”
“Ndiyo, yupo wapi?”
“Alitoka na yule handsome wa Nsumba naona leo mambo yake safi, aangalie tu asije naye akamuua kama alivyomuua mwalimu wetu Lutambi maana mimi yule huwa simwelewi hata kidogo!” mmoja wa wanafunzi wale alijikuta akitamka maneno yaliyomfikia Anne moja kwa moja chini ya shuka lake na kumuumiza moyo zaidi! Alihisi ni lazima alichokifanya kingejulikana.
Msichana mmoja alinyanyua uso wake kuangalia juu ya kitanda na alishangaa sana kugundua kuwa Anne alikuwepo kitandani!”
“Ha! kumbe yupo sijui kasikia?” alimnong’oneza mwenzake!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Lakini hajasikia hebu jaribu kumwita uone kama bado yupo macho!” Alishauri mmoja wa wasichana wale na mwenzake alijaribu kumwita Anne kwa jina lakini Anne hakuitika, alisikia kila kitu lakini aliamua kukaa kimya huku akiendelea kulia!
Machozi yaliendelea kumwagika na kulowanisha mashuka yake, baadaye wasichana wale waliondoka kwenda bafuni kuoga na wengine wengi waliendelea kuingia bwenini wakilisifu disco la siku hiyo!
Anne alipoangalia saa yake tayari ilionyesha saa tisa na nusu ya usiku! Na nje alisikia kelele za wanafunzi wa Nsumba wakimuulizia Dioniz.
“Yuko wapi?”
“Hata sisi hatujui lakini alikuwa na msichana mmoja wa hapa Nganza simkumbuki kwa jina!”
Hofu kubwa iliujaa moyo wake na alizidi kutetemeka, alilala macho yakiwa yameangalia nje ambako aliwaona wanafunzi wakizunguka huku na kule kumtafuta Dioniz bila mafanikio, moyo wake ulidunda kwa nguvu na aliendelea kutetemeka!
“Labda katangulia shuleni?”
“Kwa usafiri gani?”
“Huwezi kujua labda alipata lifti ya mtu yeyote, si mnajua tena Dioniz ni mtu wa usingizi hata muziki huwa hachezi labda aliboreka akaamua kutangulia shuleni cha msingi twendeni tukaangalie kwanza!”
Walimu na wanafunzi waliojitokeza kumtafuta Dioniz walikubaliana akaangaliwe kwanza shuleni kwao, wengi waliamini ni lazima angekuwa shuleni.
Anne aliyasikia vizuri majadiliano yao kutoka kitandani kwake, kauli ya kuamini kuwa alikuwa shule ilimpa ahueni moyoni, baadae alilisikia gari la Shule ya Nsumba likiondoka na moyo wake ukatulia.
Kupotea kwa Dioniz kulikuwa gumzo shuleni Nganza usiku huo, wanafunzi wengi walimfuata Anne kitandani kwake na kumuuliza mahali alikokwenda na Dio usiku lakini jibu lake liliendelea kuwa “Niliachana nae!”
****
Siku iliyofuata ilikuwa ni siku ya Jumapili na kwa sababu ya kuchelewa kulala wanafunzi wengi walichelewa kuamka pia, lakini kwa Anne ilikuwa tofauti aliwahi sana kuamka kabla jua halijachomoza na kwenda moja kwa moja bustanini, kwenye shimo la maji machafu kuangalia kama kulikuwa na dalili yoyote iliyoonyesha kuwa mtu alidumbukizwa ndani ya shimo hilo!
Anne aligundua alama za viatu vyake na mkwaruzo iliyojitokeza wakati akiuburuza mwili wa Dioniz kuupeleka shimoni.
“Hii itaniletea matatizo!” aliwaza Anne na kwa haraka bila kuchelewa alikata tawi la mti na kuanza kufuta alama zote ardhini, alipomaliza aliamua kuchungulia shimoni ili kuona kama mwili wa Dioniz ulikuwa ukielea juu juu!
Kabla hajaufunua vizuri mfuniko wa shimo la maji machafu, ghafla alisikia sauti ikiita jina lake kwa nyuma, alipogeuka alikuwa ni mwalimu wake wa somo la Biolojia, mwalimu Catherine!”
“Unafanya nini hapo asubuhi hii?”
“Ah! Ah! Ah! Unajua... mwalimu!...”
“Nini unachofanya hapo kwenye shimo!?”
Anne alikosa kitu cha kujibu na aligundua wazi kuwa siri yake ilikuwa imeanikwa ni lazima mwalimu wangetaka kujua kilichokuwa ndani ya shimo hilo. Mwalimu alizidi kumsogelea.
“Kuna nini humu shimoni?”
“Hakuna kitu mwalimu!”
“Hebu funua nione?”
Anne aliogopa kufanya hivyo, alihofia mwili wa Dioniz ungeonekana hakutaka hata mwalimu Catherine afunue hakutaka kabisa siri yake ijulikane!
“Hutaki kufunua siyo? Basi nafunua mwenyewe!”
“Hapana mwalimu, tafadhali usifunue hilo shimo”
“Kwanini?”
“Usifunue tu acha mwalimu utapata matatizo.”
“Matatizo gani?”
Mwalimu hakulijali onyo hilo la Anne na kuushika mfuniko wa shimo na kuanza kufunua.
Bila kuchelewa Anne alinyanyua mkono wake wa kulia na kumsonta mwalimu kwa kidole, polepole mwalimu alilegea na kuanguka juu ya sakafu ya shimo akiwa taabani huku mapovu yakimtoka mdomoni na puani.
“Mwalimu unaona sasa, mimi nilikuambia usifunue hilo shimo wewe ukang’ang’ania!”
“Sasa mimi ningefanya nini?” alisema Anne huku akiusogelea mwili wa mwalimu uliokuwa juu!
Anne aliangaza macho huku na kule na kugundua hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa karibu yake, wazo lilimwijia haraka kichwani na alisikia sauti ikimwambia “Na yeye mdumbukize shimoni!”
Anne alilikimbilia jiwe kubwa lililokuwa karibu na kulisogeza karibu kabisa na shimo, alimvua mwalimu khanga alizokuwa amejifunga kiunoni na kulifunga vizuri jiwe lile, kisha akalifunga kiunoni kwa mwalimu Catherine na kwa nguvu za ajabu ambazo hakujua alizipata wapi alimnyanyua mwalimu na kumpitisha katika tundu la shimo lile kisha akalidumbukiza jiwe pamoja naye, mwalimu alizama taratibu akipenya katikati ya maji machafu hadi kupotea kabisa!
Anne bila kupenda alimuua mwalimu Catherine kwa sababu tu alitaka kuificha siri ya mauaji ya Dio! Aliomba Mungu kusiwe na mtu mwingine yeyote aliyeshuhudia akimzamisha mwalimu Catherine shimoni.
“Kama kuna mtu kaona basi nimekwisha kabisa!”
Aliangaza huku na kule lakini hakuona mtu yeyote, mara ghafla jogoo likawika na alikimbia haraka kwenda bwenini ambako aliingia bafuni na kuanza kuoga, alipoyafikiria yote yaliyokuwa yakitokea katika maisha yake alimlaumu sana mama yake.
Alishindwa kuelewa ni nguvu gani iliyokuwa ndani ya mwili wake iliyofanya hata aue kikatili kiasi kile! Hakuamini zilikuwa ni nguvu za uchawi kwa sababu hakuwahi kufundishwa mahali popote! Maji yakiendelea kutiririka na kumlowanisha na kufanya atetemeke ovyo!
Akiwa wima kabla hata kuoga ghafla alishitukia mlango wa bafuni ukigongwa alipofungua walikuwa ni wanafunzi wenzake.
“Anne unaitwa ofisini kwa Mwalimu Mkuu haraka!
“Sawa!”alijua tayari mambo yamekwishaharibika na alihisi kuna mtu alimuona asubuhi ile akimdumbukiza mwalimu Catherine shimoni, mwili wake wote ulitetemeka alitoka mbio bafuni na kuanza kukimbia kuelekea kilipokuwa kitanda chake!
“Hey! Anne mbona unatembea bila nguo!”
“Ha! nimesahau taulo langu bafuni!”Alijibu Anne na kuanza kukimbia tena kurejea bafuni ambako alichukua taulo lake na kulivaa.
Alinyoosha moja kwa moja hadi kitandani kwake ambako alivaa nguo safi na kutoka kuelekea ofisini kwa Mwalimu Mkuu ambako alikuta walimu wote wamekaa wakimsubiri, mkutano ule ulimkumbusha siku alipokufa mwalimu Lutambi. Mmoja wa waalimu alikuwa kutoka Nsumba na alikuwa na watu wengine wawili ambao hakuwafahamu kabisa!
“Mbona unatetemeka Anne!” Mwalimu Mkuu aliuliza.
“Baridi mwalimu, nilikuwa naoga!”
“Baada ya jibu hilo Anne aliwageukia walimu na kuwaamkia.
“Msichana mwenyewe ndiye huyu hapa!” Mwalimu Mkuu alisema.
“Sawa!” Alijibu mwalimu kutoka Nganza
“Kwani kuna nini mwalimu!” Anne aliwauliza. Alijifanya kushangaa ingawa alifahamu kabisa ni kwa nini aliitwa ingawa hakuwa na uhakika ni suala la Diozin au la mwalimu Catherine.
“Eti binti ni wewe ndiye uliyekuwa na Dioniz jana usiku? Ulitoka naye nje?”
Je, nini kitatokea?
Je, mwalimu Catherine na Dioniz watagundulika shimoni?

Post a Comment

Previous Post Next Post