HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 05-----06


Mwanamke Anne amefikishwa mbele ya mahakama kwa kosa la kumuua mama yake kwa kumchoma kisu. Tukio hilo linawashtua watu wengi na siku ya hukumu yake, watu wanakusanyika kwa wingi mahakamani.
Anne anabaki akilia tu, ndani ya mahakama hiyo, kuna watoto wake wake mapacha, msichana aliitwa Nancy na wa kiume aliitwa Patrick.
Hakimu ambaye alikuwa akisimamia kesi hiyo aitwaye Raphael Mpoki anamuonea huruma Anne, hataki kumuhumu kifo na hivyo kumuuliza alitaka amfanyie nini, cha ajabu, Anne anasema kwamba anachokitaka ni kufa tu na ni kweli alimuua mama yake.
Mahakama inashtuka, wakili aliyekuwa akimsaidia aitwaye Lydia naye anashtuka, haamini kama mteja wake aliyetumia nguvu nyingi kumsimamia anakihitaji kifo kwa gharama yoyote ile.
Kwa uchungu mkubwa moyoni mwake, tena huku akiwa analia kama mtoto, Anne anaanza kusimulia kilichotokea maishani mwake na sababu iliyosababisha kumuua mama yake, historia ambayo ilibadilisha kila kitu.
Historia ya maisha yake inaanzia shule, huku akiwa hajui kama amepewa uchawi, mama yake anamtahadharisha kwamba hatakiwi kufanya mapenzi na mwanaume yeyote yule kwani akifanya hivyo mwanaume huyo atakufa.
Mtu wa kwanza kabisa kufa alikuwa mwalimu wake, Lutambi. Anapoitwa na kuhojiwa, anakataa katakata. Haikuishia hapo, anajikuta akimuua mtu wa pili ambaye ni mwanafunzi handome aitwae Dioniz.
Hajui ni nini anachotakiwa kukifanya, akili yake imechanganyikiwa.
SONGA NAYO...
Kifo cha Dioniz kiliwasikitisha watu wengi sana, alikuwa kipenzi cha wanafunzi wengi shuleni kwao na si kwa wanafunzi peke yao bali hata walimu wake!
Lilikuwa ni pigo kwa kila mmoja wao na hakuna mtu aliyekuwa tayari kuamini Dioniz hakuwepo duniani! Wengi waliamini Dioniz alikuwa hai ila alikuwa ametoweka kwenda kusikojulikana na si ajabu Ulaya.
Wanafunzi wa Nsumba hawakuchoka kumtafuta, msako uliendelea usiku na mchana! Polisi nao walilazimika kuleta mbwa wa kunusa lakini hakuna mbwa hata mmoja aliyefanikiwa kuwapeleka kwenye shimo la maji machafu kulikokuwa na miili ya watu wawili.
Kwa siku saba Dioniz aliendelea kutafutwa bila mafanikio yoyote na hakuna mtu aliyehisi mahali alikokuwa wengi walijifariji kwa kusema Dioniz aliondoka shuleni kurejea nyumbani kwao kwa sababu katika kipindi hicho kulikuwa na tatizo ya ada ya shule kwa wanafunzi wengi! Lakini kwanini aondoke usiku? Wengi waliendelea kujiuliza bila majibu na walipofuatilia ofisini waligundua kuwa hakuwa na tatizo la ada ya shule.
***
Katika Shule ya Ngaza aliyosoma Anne hali ilikuwa mbaya pia, Emmaculata aliyekuwa mpenzi wa Dioniz kabla ya Anne kuyaingilia kati mapenzi yao alikuwa bado akimlilia Dioniz, aliamini kabisa Anne alifahamu vizuri mahali alikokuwa. Mara kwa mara alisisitiza upelelezi uzidi kufanyika na Anne abanwe ili aeleze.
Emmaculata hakuamini maneno kuwa Dioniz alipotea, wasiwasi wake mkubwa ulikuwa kuuawa na maiti yake kufukiwa ardhini lakini alipolitoa wazo hilo kwa watu walimbeza na kumpuuzia! Alitamani amuulize Anne lakini alishindwa kufanya hivyo, aliamini asilimia mia moja Anne alikuwa mchawi na angeweza kumfanyia lolote hata kumuua kabisa.
****
Ilikuwa ni siku ya pili Anne akiwa mwenye mawazo mengi juu ya mauaji aliyokuwa ameyafanya! Muda mwingi alikuwa akilia na kumlaumu mama yake, hakupenda kuwa jinsi alivyokuwa alitaka awe na uhusiano na mvulana kama walivyokuwa wasichana wengine, lakini kila mvulana aliyekutaka naye alikufa! Jambo hilo lilimsikitisha sana.
Ni siku hiyo hiyo saa 11:30 jioni taarifa zilipelekwa ofisini kwa mwalimu mkuu msaidizi kuwa mwalimu Catherine hakuwepo kazini kwa siku mbili! Mkuu wa shule msaidizi alituma watu kuangalia kama alikuwepo nyumbani kwake.
“Hatujamkuta, tumekuta mlango wa nyumba yake umefungwa!”
Walimjibu mkuu wa shule msaidizi waliporejea.
“Hakuna mtu yeyote anayeishi naye?”
“Anaishi peke yake ila Mkuyuni kuna mchumba wake!”
“Basi nendeni hukohuko Mkuyuni kwa mchumba wake mkamwangalie si ajabu anaweza kuwa mgonjwa!”
Waliporudi baada ya masaa mawili jibu lilikuwa lilelile kuwa mwalimu Catherine hakuwepo Mkuyuni, mkuu wa shule alipojaribu kudadisi kama alimuaga mtu yeyote hakuna aliyekiri! Alipotafutwa mtu aliyekuwa naye mara ya mwisho jibu lake liliwapa utata!
“Ile siku ya mahafali mimi nilikuwa naye zamu lakini ilipotimu saa kumi na moja alfajiri aliondoka kurudi kwake, sikumwona tena nikafikiri labda amesafiri.
“Uliripoti mahali popote?”
“Ndiyo nilimwambia Wadeni!”
Watu walizidi kuchanganyikiwa walishindwa kuelewa ni nini kilikuwa kimetokea katika shule ya Ngaza, watu wawili kupotea kwa wakati mmoja halikuwa jambo la kawaida.
Habari za kupotea kwa mwalimu zilipoanza kuongelewa shuleni zilimtia Anne simanzi kubwa na kukiongeza kilio chake! Uongozi wa shule ulilazimika kutoa taarifa hiyo kwa polisi ambao mpaka wakati huo walikuwa bado wakiendelea na upelelezi wa kupotea kwa Dio.
****
“Itabidi huyu binti tuondoke naye ili atusaidie katika upelelezi wa suala hili tuna wasiwasi atakuwa anafahamu kitu fulani kuhusu kupotea kwa yule kijana!” mmoja wa maaskari alishauri baada ya Anne kuitwa ofisini kwa mahojiano zaidi.
Anne aliyasikia maneno hayo moja kwa moja hakutaka kabisa kupelekwa kituo cha polisi kama ilivyotokea mara ya kwanza mwalimu Lutambi alipokufa!
“Hiyo ni kazi yenu sisi hatuwezi kuwaingilia hata kidogo!’ Mwalimu Mkuu msaidizi alisema.
“Mfunge pingu upesi tuondoke naye sasa hivi, kituoni atasema tu alipo Dio!”
Bila kuchelewa mmoja wa maaskari aliyekuwepo ndani alinyanyuka na kumtia pingu mikononi Anne aliyekuwa akilia muda wote wa mahojiano na alizidi kusisitiza kuwa hakufahamu mahali alikokuwa Dioniz.
‘Utasema tu ukifika kituoni wewe si ndiye uliyekuwa nae mara ya mwisho!”
“Ndiyo lakini........!” Anne alishindwa kumalizia sentensi yake, kwikwi za kulia zilizidi kumkaba shingoni!
Anne alitolewa ofisini na kuanza kusukumwa na polisi akipelekwa kwenye gari la polisi lililokuwa limeegeshwa katikati ya uwanja wa mbele ya shule, wanafunzi waliokuwa mabwenini walimshuhudia Anne akisukumwa, kelele zaidi zilisikika kutoka ndani ya bweni liitwalo Machame! Bweni alilolala Emmaculata.
“Ni huyo huyo ndiye anafahamu alipo Dio! Mchukueni mchawi mkubwa huyo!”Alipiga kelele kwa nguvu Emmaculata.
Sauti ya Emmaculata ilipomfikia Anne pamoja na kwamba kweli alihusika na kupotea kwa Dio na mwalimu alijisikia vibaya sana moyoni mwake na kujikuta akimchukia Emma kwa mara nyingine.
Anne aliumia kujisikia muuaji, vifo cha Dioniz na mwalimu vilimuuma sana moyoni mwake, hakupenda Dioniz afe na zaidi ya yote mahali alipoficha maiti yake ndipo palipomsikitisha zaidi, Dio alikuwa kijana mzuri mno kutumbukizwa katika shimo la maji machafu tena ya chooni!
Ilikuwa si rahisi kwa mtu yeyote kufikiria kuwa miili wa Dio na mwalimu ilikuwa ndani ya shimo palepale shuleni! Anne alijua isingejulikana lakini bado aliamini kwake ilikuwa si rahisi kulisahau tukio hilo, siku zote za maisha yake angekuwa mtumwa wa siri hiyo jambo aliloliona ni mateso makubwa kwake lakini aliahidi kukaa nalo moyoni hadi kaburini!
Dakika tano baadaye gari liliegeshwa kituo cha polisi na Anne aliteremshwa na kupelekwa moja kwa moja hadi chumba cha upelelezi kilichokuwa na giza nene! Waipoingia, taa ziliwasha na Anne alisukumwa kwa nguvu na kuingia ndani ambako alikalishwa chini, hasira zilimkaba lakini alishindwa kumnyoshea askari kidole chake cha sumu akijua kufanya hivyo kungesababisha aaminike kuwa muuaji.
“Binti kama umefika hapa jiandae kueleza ukweli! Hapa si mchezo dada yangu, ukidanganya tu hutoki salama hebu pumzika kwanza ndio tuanze mahojiano yetu!” Alisema mmoja wa maaskari.
Anne alikaa chini kwa kama dakika ishirini hivi akiwa mwenye wasiwasi mkubwa, muda wote huo alishuhudia vifaa mbalimbali vikiingizwa chumbani yakiwemo mawe mawili makubwa! Aligundua yalikuwa maalum kwa ajili ya kumtesa ili aseme ukweli lakini aliuahidi moyo wake kutofanya hivyo!
“Dada wakati umefika sasa hebu nieleze wazi Dioniz yupo wapi?”
“Dioniz?”
“Ndiyo!”
“Tuliachana naye nje ya ukumbi siku ya mahafali!”
“Nje ya ukumbi? Unanitania siyo? Unaviona vifaa vyote hivi?”
“Ndiyo!”
‘Ni vifaa vya mateso kwa ajili yako usiposema ukweli tu nitavitumia!”
“Hata kama mtanitesa na kuniua kabisa sitakuwa na jibu jingine zaidi ya kusema sikumwona Dioniz, baada ya kuachana naye nilikuwa na mvulana mmoja aliyeitwa Benedict!”
“Una hakika?”
“Asilimia mia moja!”
“Unanidanganya mimi subiri sasa!”
Baada ya kusema hayo afande alichukua kinyundo kidogo na kuanza kumgonga nacho Anne kwenye visigino na magotini! Anne alilia kwa maumivu makali aliyoyapata!
“Jamani mtaniua bure mi sijui kitu chochote!”
“Utasema tu!”
Mateso yaliendelea hadi usiku lakini Anne hakuwahi kukubali kufahamu mahali alipokuwa Dio!
Mwili wake wote ulivimba kila sehemu, ndani ya nafsi yake alijua wazi kuwa kweli alihusika na vifo vya watu hao wawili lakini hakuwa tayari kutoboa siri hiyo kwani alijua huo ndio ungekuwa mwisho wa maisha yake kitu ambacho hakupenda kabisa kitokee! Alikuwa tayari kufa lakini si kutamka mahali mwili wa Dioniz ulipokuwa!
Ilipotimu saa nne ya usiku bila kusema kitu maafande walikusanya vifaa vyao vya mateso na kuondoka wakimwacha Anne amelala sakafuni, lawama zote za mateso yale Anne alimtupia mama yake.
****
Asubuhi siku iliyofuata majira ya saa tano idadi kubwa ya wanafunzi kutoka Shule za Ngaza na Nsumba walifurika kituo cha polisi cha kati mjini Mwanza, waliruhusiwa kwenda kituoni kumsalimia Anne, habari za kupotea kwa Dioniz na mlinzi wa shule ya Ngaza zilikuwa zimesambaa sana Mwanza mjini na katika vitongoji vyake kiasi kwamba watu wengi walitamani kumwona kwa macho Anne aliyetuhumiwa kuhusika na kupotea kwa Dioniz na pia kifo cha mwalimu Lutambi.
Kituoni haikuwa rahisi kwa wanafunzi kumwona Anne moja kwa moja mahabusu alikokuwa lakini walimwomba mkuu wa kituo awaruhusu kuongea na wanafunzi mwenzao walikubaliwa na mkuu wa kituo aliwaagiza maaskari wawili wamtoe Anne mahabusu ili asalimiane na wanafunzi wenzake.
Wanafunzi walitulia wakisubiri Anne atolewe mahabusu, dakika tatu baadaye walimwona mtu aliyevimba uso na viungo vya mwili akitoka katika chumba fulani kilichokuwa karibu na kaunta ya polisi, alipojaribu kutembea peke yake alishindwa na kuanguka chini.
Wanafunzi walipoangalia vizuri waligundua kuwa msichana yule alikuwa ni Anne! Wengi hasa ambao hawakuifahamu siri ya mauaji hayo walidondosha machozi.
Maaskari walimbeba hadi nje ambako alikalishwa kwenye msingi wa kituo! Aliponyanyua uso wake kuwaangalia wanafunzi wenzake Anne alilia machozi! Alitia huruma alikuwa amevimba mno usoni kutokana na kipigo wakati wa kuhojiwa.
“Pole Anne! lakini kweli unajua alipo huyo mwanafunzi wa Nsumba?”
“Hapana Angelina!”
“Mwalimu Catherine je?”
“Hata yeye sijamwona kabisa wananionea bure!”
Emmaculata aliyekuwa miongoni mwa wanafunzi waliokuwa kituoni na aliyasikia maneno hayo na kulazimika kusogea mbele ambako alianza kumzodoa!
“Unaonewa nini wakati huo ndio mchezo wako? Unajua kila kitu huna sababu ya kulia!”
Anne aligeuka kwa huruma na kumwangalia Emmaculata msichana waliyesoma naye darasa moja shuleni kwao na waliwahi kuwa marafiki kabla Dioniz hajajitokeza, hasira kali ilimshika Anne akajikuta akisahau kuwa kidole chake cha shahada kilikuwa ni sumu kali kuliko hata Thiodani!
“Wewe Emmaculata weweeeee!” Anne alimsonta Emmaculata kwa kidole chake huku akiwa amevimba kwa hasira.
Katika hali ambayo wanafunzi wengi hawakuitegemea Emmaculata alianguka chini kama mzoga na kuanza kufuka moshi mwili mzima! Wanafunzi wote walishangaa na wengine walianza kukimbia, Anne aligundua alikuwa amefanya kosa ambalo lingepelekea watu kuamini kuwa kweli alikuwa na nguvu za miujiza ya kichawi zenye uwezo wa kuondoa maisha!
“Hee! Kumbe kweli mchawi?” Ilisikia sauti ikitoka katika kundi la wanafunzi.
Anne alijilaumu kwa kitendo hicho na bila kuchelewa aliwaomba wanafunzi wamshikilie mkono na kumsogeza hadi mahali alipolala Emmaculata akitoka moshi na povu mdomoni kama mtu mwenye kifafa akitupa miguu huku na kule kama mtu aliyekuwa akitokwa na roho.
Anne alipomfikia alimsogezea Emmaculata mdomo karibu na sikio na bila mtu yeyote kuona alimpulizia kiasi kidogo cha pumzi sikioni.
****
Dioniz alikuwa ni mtoto wa tano na wa mwisho katika familia yao na ni yeye pekee aliyekuwa mtoto wa kiume na familia yake ilimtegemea yeye zaidi kuwa mrithi wa mali zote alizokuwa nazo baba yake, wazazi wake walimpa kila kitu alichokitaka na walihakikisha anapata elimu bora ili aweze kuziendesha vizuri shughuli za baba yake akiwa mtu mzima.
Taarifa za kupotea kwa Dioniz ziliwachanganya sana akili wazazi wake, presha ya mama yake ilipanda na kumwangusha chini akazirai, kwa siku saba mama huyo alikaa hospitali akisumbuliwa na ugonjwa mbaya wa kiharusi na alipooza upande mmoja wa mwili wake kwa sababu ya ugonjwa huo.
Walitumia kila uwezo waliokuwa nao kumtafuta Dioniz lakini hawakufanikiwa, walipiga simu kwa kila ndugu lakini hakuna aliyejitokeza na kusema Dioniz alikuwa kwake! Wazazi na ndugu wote walichanganyikiwa na waliposikia taarifa za Anne na hisia zilizokuwepo juu yake walitaka sana wamwone ili awaeleze kama kuna kitu chochote Dioniz alimweleza kabla ya kupotea.
Walipokwenda shule walimkuta Anne amekwishaondoka kwenda kwao Sengerema kwa mapumziko baada ya kutoka mahabusu, haikuwa gharama kubwa sana kwao kusafiri kwenda mpaka kisiwani Kome wilayani Sengerema ambako Anne na wazazi wake waliishi!
Majibu ya mama yake na Anne, Isabella yaliwasikitisha sana wazazi wa Dioniz, yeye alijua wazi kilichokuwa kikiendelea na alijua wasingeweza kufanya lolote.
“Mtoto wenu hajapotea isipokuwa kafa na maiti yake hamtaiona milele! Kwa sababu alimlazimisha mwanangu kufanya naye mapenzi na kuna mwalimu mmoja wa shule hiyohiyo aliwahi kumlazimisha nae akafa kifo kibaya! Sisi sio watu wa kuchezea” Alisema Isabella huku akifoka.
“Nini?” Aliuliza kwa ukali Regnald baba mzazi wa Dioniz.
“Umeshasikia! Na ninawaomba muondoke hapa nyumbani!”
“Mama acha kuwafukuza hao watu bado wanauchungu na mtoto wao!”
“Mimi hiyo sijui!”
“Binti ni kweli yanayosemwa na mama yako?”
“Hata mimi mwenyewe sijui kinachoendelea, huwa inanitokea tu ila mama anaelewa zaidi! Nilimpenda mno Dioniz nisingemuua ilikuwa bahati mbaya” Anne alijibu huku machozi yakimtoka.
Wazazi wa Dioniz waliondoka huku wakilia walipofika mjini Mwanza walichofanya ni kuitafuta familia ya marehemu mwalimu Lutambi na familia ya mwalimu Catherine ambao pia walikuwa na uchungu na kifo cha ndugu yao.
Siku hiyo hiyo usiku kilifanyika kikao na wote walikubaliana kutumia kila walichokuwa nacho kuhakikisha wanapambana na familia ya akina Anne!
“Tutatumia kila tulichonacho kuhakikisha kuwa tunalipiza kisasi, mimi nitakwenda Kigoma, wewe utakwenda Bagamoyo na wewe utakwenda Sumbawanga!” Mzee Regnald aligawa majukumu kwa watu wa familia zote.
Je nini kitaendelea?
Je watu hao wataweza kupambana na Anne na mama yake?
Je ni nini hatima ya kila kitu?


HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 6
MTUNZI: ERIC JAMES SHIGONGO
Mwanamke Anne amefikishwa mbele ya mahakama kwa kosa la kumuua mama yake kwa kumchoma kisu. Tukio hilo linawashtua watu wengi na siku ya hukumu yake, watu wanakusanyika kwa wingi mahakamani.
Anne anabaki akilia tu, ndani ya mahakama hiyo, kuna watoto wake wake mapacha, msichana aliitwa Nancy na wa kiume aliitwa Patrick.
Hakimu ambaye alikuwa akisimamia kesi hiyo aitwaye Raphael Mpoki anamuonea huruma Anne, hataki kumuhumu kifo na hivyo kumuuliza alitaka amfanyie nini, cha ajabu, Anne anasema kwamba anachokitaka ni kufa tu na ni kweli alimuua mama yake.
Mahakama inashtuka, wakili aliyekuwa akimsaidia aitwaye Lydia naye anashtuka, haamini kama mteja wake aliyetumia nguvu nyingi kumsimamia anakihitaji kifo kwa gharama yoyote ile.
Kwa uchungu mkubwa moyoni mwake, tena huku akiwa analia kama mtoto, Anne anaanza kusimulia kilichotokea maishani mwake na sababu iliyosababisha kumuua mama yake, historia ambayo ilibadilisha kila kitu.
Historia ya maisha yake inaanzia shule, huku akiwa hajui kama amepewa uchawi, mama yake anamtahadharisha kwamba hatakiwi kufanya mapenzi na mwanaume yeyote yule kwani akifanya hivyo mwanaume huyo atakufa.
Mtu wa kwanza kabisa kufa alikuwa mwalimu wake, Lutambi.
SONGA NAYO...
Kidole cha shahada cha Anne kilikuwa tishio na gumzo kubwa midomoni mwa wanafunzi wote shuleni kwao, kitendo cha Emmaculata kuanguka chini baada ya kusontwa kiliwashangaza wengi na kuwafanya waamini kweli Anne alikuwa na nguvu za kichawi!
Wote waliamini isingekuwa Huggins Martin mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nsumba na rafiki mkubwa wa Dioniz kumwombea Emmaculata angekufa!
‘Bila yule mwanafunzi wa Nsumba kuwepo Emmaculata angekuwa marehemu!”
Huggins alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliookoka katika shule yake, yeye ndiye alikuwa kiongozi wa umoja wa Kikristo wa wanafunzi Tanzania(UKWATA) katika shule yao. Huggins alimcha Mungu na alimfanya awe kila kitu katika maisha yake!
****
Huggins alikuwepo kituo cha polisi wakati Anne alipomsonta Emmaculata na kidole chake cha shahada na kwa maneno aliyokuwa ameyasikia juu ya Anne, Huggins alikigundua nini lilikuwa tatizo lake aligundua alikuwa na mapepo mabaya.
Huggins alimshuhudia Anne akihangaika kwa dakika kama tatu bila Emmaculata kushtuka, ndipo alipomsogelea karibu zaidi na kumgusa begani!
“Anne yupo Mungu mwenye nguvu zaidi ya hizo ulizonazo!”
Anne aliduwaa bila kujua ni nini cha kufanya na hakuyaelewa vizuri maneno yaliyosema na Huggins, alimfahamu kijana huyo kama rafiki wa Dio lakini hakukielewa alichokisikia kutoka mdomoni kwake
“Unasemaje?”
“Nakuambia yupo mwenye nguvu kuliko hizo unazotumia!”
“Nani huyo?”
“Mungu wa mbinguni, unahitaji msaada wake!”
Anne alitingisha kichwa kuashiria kuwa alikubaliana na kilichosemwa.
Bila kuchelewa Huggins alinyanyua mkono wake wa kuume na kumwekea Emmaculata aliyekuwa amelala chini kwenye paji lake la uso.
“TOKA KATIKA JINA LA YESU! UKASHIDWE NA UKALEGEE PEPO MCHAFU! MWACHIE KATIKA JIIIIIIINA LA YESU!NASEMA MWACHE HURU!” Huggins alikemea.
Askari mmoja alilazimika kumchukua Anne kwa haraka na kumrudisha mahabusu ambako alifungiwa tena rumande, nyuma yake Huggins aliendelea kumwombea Emmaculata, lakini kabla hajamaliza maombi yake gari la polisi lilifika na Emmaculata akapakiwa ndani ya gari harakaharaka tayari kwa kwenda Hospitali ya Seko Toure kwa matibabu.
Huggins alipanda nyuma ya gari hilo pamoja na wanafunzi wengine wa Shule ya Ngaza waliosoma na Anne pamoja na Emmaculata, njiani aliendelea kumwomba Mungu afungue miujiza, mita chache baadaye kabla hawajafika hospitali walishangaa mwili wa Emmaculata ulipoanza kufuka moshi ambao ulijaa nyuma ya gari na kuonekana kama vile gari lilitaka kushika moto! Ilimlazimu dereva asimamishe gari na kurudi hadi nyuma kuangalia ni nini kilikuwa kimetokea.
“Vipi?”
“Anatoa moshi!”
“Moshi!”
“Ndiyo!”
“Unatoka wapi?”
“Mwilini kwake!”
Dakika tatu baadaye Emmaculata alijitingisha na baada ya kunyanyuka alikaa kitako huku akiwashangaa watu walikuwa ndani ya gari!
“Mnanipeleka wapi?”
“Hospitali!”
“Kufanya nini?”
“Kutibiwa si unaumwa!”
“Naumwa nini?”
“Umeanguka ghafla!”
“Wapi?”
“Kituoni!”
“Ilikuwaje nikaanguka?” Alizidi kuuliza Emmaculata na ililazimu Huggins amsimulie kila kitu kilichotokea, wanafunzi wenzake ndani ya gari walikuwa wakilia, Emmaculata alisikitika sana na kujikuta akilia pia.
“Kwa hiyo basi hakuna haja ya kwenda hospitali tena au?” Aliuliza dereva wa gari la polisi!
“Ahsante Huggins kwa msaada wako kwani bila wewe nisingekuwa hai, Anne alishaniua tayari!”
“Hapana siyo mimi niliyefanya kazi hii ila ni yeye aishie ndani yangu!” Alijibu Huggins.
Walipofika kituo cha polisi Huggins alitaka kuonana na Anne pengine kuliko wanafunzi wengine wote, alijua kabisa Anne alihitaji msaada mkubwa sana kutoka kwake na alikuwa na uwezo wa kumsaidia, alijua wazi Anne alikuwa na mapepo yaliyomsumbua na kumpa mateso maishani.
“Jamani naomba mniruhusu nimwone Anne, ananihitaji sana!” Alisema Huggins kwa sauti kubwa mbele ya maaskari na sauti hiyo ilipenya moja kwa moja hadi ndani ya mahabusu na kumfanya Anne anyanyuke kutoka sehemu aliyokuwa amekaa na kutembea hadi mlangoni ambako alichungulia nje na kumwona Huggins akiwabembeleza maaskari wamruhusu aonane naye!
“Mpaka saa tisa kamili jioni wakati wa kuleta chakula sawa?” Afande alimwambia Huggins ikabidi akubali kusubiri.
Huggins hakutaka kuondoka kituoni kurudi shuleni bila kuonana na Anne, alipotoka nje aliagana na wanafunzi wa Ngaza na wakaondoka kurudi shuleni, Huggins aliamua kusubiri mpaka muda wa mahabusu kuletewa chakula ufike ili aonane na Anne, alitaka kumsaidia na kumwondoa katika mateso aliyokuwa nayo.
****
Muda wa mahabusu kuletewa chakula ulipofika Huggins aliisogelea kaunta ya polisi na kuwaeleza nia yake ya kuonana na Anne.
“Wewe bado upo hapa tu?”
“Ni lazima nimwone!”
“Ni lazima?”
“Hapana ni ombi!”
“Kama ni ombi sawa! Hebu njoo huku ndani uongee naye hapahapa kwenye nondo!”
Huggins alizunguka hadi upande wa pili wa kaunta ambako alipelekwa hadi kwenye mlango wa mahabusu ya wanawake.
“Anneee!” Afande mmoja wa kike aliita na Anne akajitokeza na kuja hadi mlangoni!
“Ninaitwa Huggins nafikiri unanikumbuka vizuri, ni rafiki wa Dioniz na nimeshaligundua tatizo lako, kama ukitoka ndani nitakuja shuleni kufanya maombi na wewe! Kwa sasa chukua hiki kitambaa changu cha mkononi nimekifanyia maombi kitakusaidia!”
“Wewe kijana usimpe kitu chochote huyo huruhusiwi kabisa kufanya hivyo, unataka akitumie kujinyonga? Wee msichana hebu mrudishie haraka hicho kitambaa chake, halafu wewe uondoke tayari umekwishaharibu mambo!” Alifoka afande huyo wa kike.
Bila ubishi Huggins aliingiza kitambaa chake mfukoni na kuanza kutembea kurudi nyuma hatimaye kutoka kabisa nje ya kituo ambako alinyoosha moja kwa moja hadi stendi ya mabasi na kupanda basi la kwenda Nyegezi ambako alitembea kwa miguu hadi shuleni kwao!
Wiki moja baadaye Huggins alisikia Anne aliachiwa baada ya Afisa elimu kushinikiza, lakini Huggins alipokwenda shuleni kwao kumtafuta alipewa taarifa kuwa baada tu ya kutoka aliondoka kurudi nyumbani kwao kupumzika baada ya wanafunzi kuonekana kumtenga.
****
Ndugu na wazazi wa Dioniz, mwalimu Catherine na mwalimu Lutambi walisafiri kwenda sehemu mbalimbali kama walizokubaliana, mwingine alikwenda Sumbawanga, mwingine Kigoma na mwingine Bagamoyo!
Nia yao ikiwa ni kutafuta namna ya kulipiza kisasi kwa familia ya Anne kwa kitendo walichofanyiwa, umoja waliokuwa wameuunda ulikuwa na nia mbaya ya kisasi tena kwa gharama yoyote!
Waliporejea baada ya wiki kila mtu alikuwa na burungutu lake la madawa, zilikuwepo dawa za radhi kuvunjwa njia panda! Palikuwa na dawa za kutupa baharini! Kulikuwa na dawa za kuoga kufukiza n.k! Zote zikiwa na lengo la kuiteketeza kabisa familia ya Anne na wazazi wake!
Kazi ilivyokuwa mbele yao ni kuzitumia dawa hizo ili kutimiza azma yao waligawana majukumu zaidi, na kuondoka na dawa zao tayari kwa kuzitumia usiku wakiwa wamekubaliana kukutana siku iliyofuata, hali ya mzee Edward haikuwa nzuri hivyo alishindwa kuzitumia dawa zake usiku huo nakuwapa wanachama wenzake wazitumie.
“Tukutane tena kesho tujue tumefikia wapi na kazi hii kila mtu atimize wajibu wake usiku huuhuu sawa jamani, ninataka kesho nisikie Anne na mama yake wamekufa sawa?”
“Sawa!” aliitikia mchumba wa Catherine, Laurian.
****
Saa moja kamili siku iliyofuata mzee Edward alikuwa nyumbani kwake akiwasubiri wenzake wafike na kumpa ripoti, lakini hakumwona hata mtu mmoja akitokea! Aliingia wasiwasi, usiku wa siku hiyo hakulala kwa mawazo.
Siku iliyofuata wakati akijaribu kwenda majumbani kwao kuulizia nini kilichotokea alishangaa kukutana na mchumba wa mwalimu Catherine akiwa uchi mtaani huku akiongea peke yake, mzee Edward alishtuka sana na kushindwa kuelewa nini kilichokuwa kimempata lakini hakutaka kusimama, alinyoosha moja kwa moja kwenda nyumbani kwa mzee Lutambi.
Kabla hajafika alishangaa kuona makundi makubwa ya watu! Nyumbani kwa Mzee Lutambi kulionyesha kuwa na msiba! Alishindwa kuelewa kulikuwa na nini.
Alifika na kuulizia, jibu alilolipata lilimchanganya sana akili Bi Nyanda shangazi wa marehemu Mwalimu Lutambi aliyekuwa mmoja wa wanachama alikutwa mtaani akiwa uchi wa mnyama damu zikimtoka puani na mdomoni haikufahamika ni nani alimuua.
Hakuna aliyehisi ni majambazi kwa sababu pembeni ya mwili wake kulikutwa dawa nyeusi, hirizi nyeupe na nyekundu na mwili wake ulijaa chale kubwakubwa! Wengi walidai alikufa katika mazingira ya kishirikina!
Mzee Edward alielewa ni nini kiliwapata! Walizidiwa nguvu na dawa za Anne na mama yake.
Miujiza mingi ilijitokeza chumbani kwake usiku, mara kwa mara alisikia sauti ikimwita nje na akiwa hajui hili wala lile ghafla alishtukia mlango na madirisha yote ya nyumba yake yakifunguka na kitu kama kimbunga kikubwa kikaingia ndani! Hali ilitisha mno ikabidi afumbe macho, alipofumbua macho yake alishangaa kukuta mkewe hayupo! Alisikia sauti ya mkewe akilia nje katika shamba lao la migomba.
Mzee Edward alijaribu kutoka nje kujaribu kufuatilia lakini alishindwa kuwafikia, sauti ya mkewe ilizidi kutokomea mbali zaidi migombani!
“Ni heri basi nife na kumfuata mwanangu Dio!”
****
Mzee Edward hakumwona tena mkewe na kwa wiki mbili nzima alimtafuta kila mahali kwa msaada wa majirani na polisi bila mafanikio! Kila mtu alijua mkewe alichukuliwa msukule, waganga kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania walijitokeza ili kujaribu kumrudisha Dioniz na mama yake bila mafanikio yoyote, alitumia kiasi kikubwa cha pesa na alikuwa tayari kutumia pesa zaidi katika kuhakikisha mkewe anapatikana.
“Nimegundua Anne na mama yake si watu wa kulipizwa kisasi kwa uchawi ila kuwafuata mchana mchana na bastola na kuwaua kikatili, hawawezi kuniharibia maisha yangu kiasi hiki, hawezi kunitesa kiasi hiki!” Alijisemea mzee Edward na kunyanyuka sebuleni alipokuwa amekaa peke yake na kwenda chumbani ambako alijitupa kitandani.
Alikuwa amepania kuwa siku iliyofuata aondoke kwenda kisiwani Kome na kulipiza kisasi kwa mkono wake mwenyewe, hakutaka tena kutumia madawa ya kienyeji tena! Alikuwa na hasira kali iliyomfanya atetemeke mwili mzima, kila alipowakumbuka mke na mtoto wake roho ilimuuma sana na aliona hapakuwa na uwezo wa kulipiza kisasi zaidi ya kufanya mambo kwa mkono wake mwenyewe.
Siku iliyofuata asubuhi alichukua bastola yake na kuiweka kiunoni akavaa suruali na koti juu, akatoka nje na kuelekea stendi ya mabasi ya kwenda Sengerema, alitamani sana afike Kome dakika hiyohiyo na kuimaliza kazi iliyokuwa mbele yake!
Hakuwa na kazi nyingine zaidi ya kuwaua Anne na mama yake, alikuwa amedhamiria na alikuwa tayari kwenda kufia gerezani! Hakuamini kama maisha yake yangeweza kuharibika kiasi hicho! Bila mwanae Dioniz na mke wake mzee Edward alikosa maana ya yeye kuishi.
“Lazima niue!”
****
Ilikuwa ni katikati ya usiku Anne na mama yake pamoja na watu wengine wengi walikuwa chini ya mti mkubwa wa mbuyu ilikuwa ni kama sherehe watu wakila na kunywa pombe! Watu wote waliokuwa uwanjani pale walikuwa uchi wa mnyama.
Chini ya mbuyu kulikuwa na kiti kilichokaliwa na aliyekuwa malkia wa sherehe hiyo, huyo alikuwa Isabella mama yake Anne, pembeni yake alikaa msichana mdogo mzuri na mrembo huyo alikuwa Anne, mama yake alikuwa akimwomba Anne msamaha kwa mambo aliyoyafanya katika maisha yake na alimtaka arithi mzimu aliokuwa nao yeye.
“Mwanangu huwezi kukwepa jukumu hili hata siku moja! Mimi nilikataa kama wewe lakini nililazimika kukubali hivyo tafadhali sana usikatae utakufa!”
“Kwanini nife?”
“Hautakiwi kukataa wadhifa huu, baada ya mimi kufa ni wewe utakayerithi!”
“Pale ilihitajika damu ya watu wawili ndiyo maana ukajikuta unaua!”
“Mama sitaki kuua tena, niliumia sana alipokufa Dioniz!”
“Dioniz hajafa yupo hapahapa anahifadhiwa ila katika ulimwengu mwingine, watu wengi hawawezi kumwona ila sisi peke yetu! Bado unampenda Dioniz?”
“Sana mama! Yupo hapa kweli?”
“Ndiyo!” Aliitikia mama yake na kumwita bibi kizee mmoja aliyekuwa akipita karibu na eneo hilo!
“Hebu mlete Dioniz hapa!”
Yule bibi kizee aliyekuwa uchi aliondoka akikimbia mbio kwenda nyuma ya mbuyu mkubwa, Anne alisikia mbuyu ukitingishika kama ulitaka kudondoka!
Aliporejea bibi kizee alikuwa na kijana mrefu, akiwa na mavazi aliyovaa siku ya graduation, Anne hakuamini na kunyanyuka mbio akimkimbilia alipomwangalia kweli alikuwa ni yeye!
‘Oh! My God, Dio....is that you!”(Oh! Mungu wangu Dio ni wewe!) Alisema Anne akimkimbilia Dioniz lakini badala ya Dioniz kuchangamka alikuwa ameinamisha kichwa chake chini na hakutaka kuangalia mbele.
“Dio! Dio! Dio!” Anne alizidi kuita!
“Huyu hawezi kuongea tena amekwishakatwa ulimi!” Alisema mama yake Anne.
Je nini kitaendelea?
Je huo ndiyo mwisho wa kila kitu?

Post a Comment

Previous Post Next Post