Mzee Edward alinyoosha bastola yake lakini kabla hajafyatua alishtukia macho yake yakiingia giza, hakuwaona tena na aliamini walipotea kimazingara. Yeye mwenyewe alitetemeka hakutaka tena kubaki kisiwani Kome aliamua kurejea Mwanza mara moja!
Lililomtokea lilikuwa jambo la kutisha sana, alikata tamaa ya kuwapata mke wake na mwanae.
******
Ulikuwa ni usiku wa kutisha sana Anne hakuamini alichokuwa akikiona mahali pale, alikuwa bado hajaamini kama mtu aliyemwona alikuwa ni Dioniz! Kabla hajakaa vizuri alimwona mtu kama mwalimu Catherine akiwa na shoka mikononi akipasua kuni! Alipozungusha macho yake upande wa pili alimwona mwanamke mmoja na alipomwangalia vizuri aligundua alikuwa na mama yake na Dioniz.
“Huyu mama naye kaja huku lini?” Alijiuliza Anne lakini hakupata jibu.
Alikimbia kwenda mahali alipokuwa amesimama Dioniz na kumkumbatia wakaanguka nae hadi chini huku akimmwagia mabusu mfululizo.
“Dioniz nakupenda!” Alisema Anne.
“Anne usitumie maneno hayo hapa si mahali pake! Utaiudhi mizimu yetu”
“Sawa mama lakini ninampenda Dioniz na kwanini ulimuua? Je hatuwezi kumrudisha tena duniani?”
“Hiyo haiwezekani tena mwanangu mtu akishafika huku hawezi kurudi duniani tena, sisi pekee yetu ndio tunaweza kufanya hivyo!”
“Lakini kwa ninavyompenda Dioniz mama ni heri na mimi nibaki hukuhuku niishi naye!”
“Haiwezekani mwanangu anakoishi Dioniz wewe huwezi kukaa kabisa kuna mateso makubwa mno!”
“Nitavumilia mama!”
Muda mfupi baadaye Dioniz, mwalimu Lutambi na mwalimu Catherine pamoja na watu wengine ambao hakuwafahamu wakatolewa eneo lile na kuzungushwa nyuma ya mbuyu ambako bibi mmoja alipiga kelele akiomba ardhi ifunguke na wote walidumbukizwa ndani ya shimo lililotokea chini ya mbuyu na kupotelea ardhini Anne alimlilia Dioniz.
Baada ya tukio hilo la kutisha mama yake alimpiga Anne usoni kwa unyoya wa Jogoo, mazingira yakabadilika wakawa wamerejea katika dunia ya kawaida ambayo Anne aliizoea! Anne aliwaona watu wakitembea kuelekea mahali yeye na mama yake walikokuwa wamesimama wakiwa uchi.
“Mama wale watu watatuona!”
“Wao hawaoni ila sisi ndio tunawaona!”
“Kweli?”
“Kama huamini tukikaribia tuwatishie kwa kuwachoma na miti machoni, kama wakishtuka basi wanaona lakini kama hawaoni basi hawatafumba wala kushtuka!”
Ili kuhakikisha maneno ya mama yake, Anne alipowakaribia alinyanyua kipande cha mwiba na kuanza kuwatisha kama anawachoma machoni lakini watu wale hawakufumba macho wala kushtuka! Anne akaamini kuwa kweli walikuwa hawawaoni akacheka.
Njiani waliendelea kupishana na watu lakini wote waliokutana nao hawakuwaona kwa macho, walipofika nyumbani mama yake aligeuka na kuugusa mlango kwa matako, mlango ukafunguka bila hata kuguswa na mtu! Wote wakaingia ndani na kujitupa kitandani.
*****
Asubuhi kulipokucha Anne alikuwa mwenye mawazo mengi sana juu ya tabia ya mama yake, ni usiku wa siku hiyo ndiyo aligundua kumbe mama yake alikuwa mchawi. Kilichomsumbua zaidi akilini Anne ni vipi Dioniz na mwalimu Catherine walitoka katika shimo la maji machafu ya chooni alikowadumbukiza na kwenda hadi kwao.
Anne na mama yake waliendelea kwenda kwenye sherehe za kichawi kila siku usiku, akiwa katika matayarisho ya kurithishwa Kiti cha Umalkia mara bada ya mama yake kufariki. Hatimaye Anne alizoea na kukubali kuwa mchawi! Alifundishwa kitu na mama yake.
****
Pamoja na waganga wote aliokwenda kwao kumweleza kuwa mtoto wake Dioniz alifariki dunia kichawi bado mzee Edward hakuamini na aliendelea kuwasisitiza polisi wamtafute mwanae na pia mke wake, aliamini Anne na mama yake walikuwa wachawi.
Kitendo cha yeye kuona giza alipotaka kuwashambulia kwa risasi kijijini kwao ndicho kilimfanya aamini Anne na mama yake walikuwa wachawi lakini pamoja na hayo bado aliendelea kuwashinikiza polisi wamtafute Dioniz mpaka apatikane.
Kwa shinikizo hilo msako wa polisi ulikuwa bado ukiendelea tena kwa nguvu kuliko mwanzo lakini Dio hakupatikana, mzee Edward na polisi na hata watu wengine walikata tamaa na kuendelea na maisha yao mambo yote wakimwachia Mungu.
“Yaani mke wangu na mwanangu hawapo tena? Mungu anajua na yeye ndiye atanilipia!”
****
Baadaye Anne alirejea shuleni kuendelea na masomo, shule nzima ilimtenga si wanafunzi tu bali hata walimu pia walimwogopa, hakuna mwalimu ayediriki kumchapa Anne hata kama alikosea kitu! Ni msichana mmoja tu katika shule hiyo aliyetokea kumzoea Anne na kuwa rafiki yake.
Msichana huyo aliitwa Grace mwenyeji wa Morogoro, yeye na Anne walikuwa marafiki wakubwa sana, walisoma pamoja, walikula pamoja na pia kucheza pamoja, wanafunzi wengine katika Shule ya Ngaza walimshangaa Grace na kuna wakati walihisi labda yeye pia alikuwa mchawi.
Kila siku iliyopita Grace alimshauri Anne juu ya kujiunga na UKWATA, Anne alitamani sana kuingia katika umoja huo kusali kitu ambacho hakuwa kukifanya katika maisha yake, lakini aliogopa vitisho alivyopewa na mama yake kuwa siku yoyote ambayo angeingia kanisani angekufa sababu mizimu yao ilizuia!
Siku zote aliendelea kumkatalia Grace bila kumwambia sababu, kila siku iliyokwenda kwa Mungu aliendelea kuteseka na siri aliyokuwa nayo moyoni mwake, hakuwa na mtu wa kumwambia jambo lililomsumbua ingawa moyo wake siku zote ulitamani kufanya hivyo.
“Ipo siku nitaenaweza kusema jambo hili kwa mtu yeyote!” aliwaza Anne.
****
Juni 26 Mkutano Mkubwa wa UKWATA ulipangwa kufanyika katika shule ya sekondari ya Ngaza, Grace ndiye alikuwa muandaaji wa mkutano huo kwa sababu yeye ndiye alikuwa mwenyekiti wa UKWATA katika shule yao, shule zote za sekondari mjini Mwanza zilitegemewa kutuma wawakilishi kwenye mkutano huo.
Kijana Huggins alikuwa miongoni mwa watu waliotegemewa kuhudhuria mkutano huo na na kutoa mahubiri kwa wanafunzi wenzake, hilo lilikuwa moja ya malengo ya Huggins lakini lengo la pili la Huggins lilikuwa ni kumtafuta Anne, msichana aliyetamani kumwona siku zote. Alitaka amwone ili amsadie matatizo yake.
“Safari hii ni lazima nimwone tu!” Aliwaza Huggins.
Kila siku Grace aliendelea kumshawishi Anne pia ahudhurie mkutano huo, maneno ya Grace na yalimwigia lakini bado aliogopa kuingia kanisani!
“Tuna kijana mmoja aitwaye Huggins ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Nsumba, atakuwepo na atakuwa mahubiri maalum tafadhali njoo usikie habari zake!”
“Huggins?”
“Ndiyo kwani unamfahamu?”
Kabla Anne hajajibu swali hilo kumbukumbu zake zilimrudisha moja kwa moja hadi kituo cha polisi, siku aliyomsonta Emmaculata kwa kidole akaanguka chini,ni Huggins aliyemnusuru baada ya kumwombea maombi maalam!
Kwa siku nyingi sana Anne pia alitamani kukutana na kijana huyo aliposikia alikuwa anakuja hisia za kutaka kumwona zilianza kumwingia tena upya.
“Kweli atakuja au unamwongelea Huggins mwingine?”
“Hapana ni Huggins yuleyule mmoja si ni mrefu mwenye sura nzuri hivi?”
“Sawasawa kabisa Grace!”
“Basi atakuwa hapa 26!”
Walipoachana siku hiyo Anne aliendelea kumfikiria Huggins, sura yake ilimchanganya akili, yeye na Dioniz hawakuwa na tofauti sana! Lakini alipofikiria kasoro aliyokuwa nayo mwilini mwake alisita kwani hakutaka kuua tena!
“Akija nitaonana naye lakini siyo kanisani kwao!”
****
Mkutano ulijaa idadi kubwa sana ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali zilizopo mjini Mwanza, ilikuwa ni furaha kupita kiasi, wanafunzi waliimba, wanafunzi walifanya maombi na mambo mengine mengi ya kufurahisha, Huggins alimtafuta Anne bila mafanikio yoyote, Anne alikuwa amejificha hakutaka kabisa kuwa karibu na mkutano ule, aliigopa mizimu yao, kila aliposikia nyimbo za mapambio zikiimbwa alijisikia kupandisha mashetani.
Ndani ya roho ya Huggins aliendelea kusikia sauti ikimweleza amtafute Anne kwani alijisikia kumsaidia, ndipo alipofikia uamuzi wa kumtafuta Grace na kumuuliza.
“Tena nilikuwa naongea naye jana tu ni rafiki yangu sana!”
“Sasa nitafanye nini ili nimpate?”
“Subiri baadaye kidogo tukimaliza mahubiri nitakwenda nikamwite sawa?”
Muda wa mahubiri ulipowadia wanafunzi walitulia kumsikiliza Huggins akihubiri, Anne alikuwa umbali wa kama mita mia nne hivi kutoka mkutanoni akiwa ameinama chini ya mti na vitabu vyake, alikuwa akiusikia mwili wake ukiwaka moto!
Anne alishindwa kuelewa kabisa moto ule uliomuunguza ulitoka wapi, aliungua kama alikuwa ndani ya pipa la maji ya moto! Alikimbia bafuni kujimwagia maji lakini maji ya bafuni hayakutosha na kujikuta akichomoka uchi kuelekea ziwani ambako alijitupa majini na kuanza kuogelea lakini bado maji ya ziwani hayakuupoza mwili wake!
Watu walimwona akikimbia kuelekea ziwani akiwa uchi walimtaarifu mwalimu wa nidhamu ambaye alitoka akiongozana na walinzi pamoja na baadhi ya wanafunzi hadi ziwani ambako walimkuta Anne ndani ya maji akilia kwa maumivu.
“Moto! Moto! Moto! Unaniunguza!” Alimwambia mwalimu.
“Moto upo wapi?”
“Mwilini mwangu mwalimu nisaidieeeeeeeeee!” Anne alipiga kelele kwa maumivu.
Walimkamata na kumtoa majini na kuanza kuongozana naye kwenda bwenini mwalimu mmoja wa kike alitoa khanga aliyokuwa amejifunga na kumfunga Anne kiunoni, kabla hawajafika bwenini upepo ulielekea upande wao na sauti ya kipaza sauti ilisikika vizuri masikioni mwao.
“BABA WA MBINGUNI SHUSHA MOTO! MOTO! MOTO! MOTO !MOTO WA MBINGUNI UMETEKETEZE SHETANI!” Ilikuwa ni sauti ya Huggins.
Kadri moto ulivyozidi kutajwa katika kipaza sauti ndivyo Anne alivyozidi kujirusha huku na kule akidai moto ulimuunguza, walipoingia bwenini sauti iliacha kutaja neno moto na palepale Anne alitulia.
Wakati bado wanajadiliana kitu cha kufanya Huggins alianza tena kupaza sauti yake akimwomba Mungu ashushe moto kumteketeza shetani, Anne alianza kupiga kelele tena.
“Mh!”Mwalimu aliguna.
“Mbona kila mhubiri anapotaja moto ndio Anne anadai kuungua?”
“Hata mimi nashangaa!”
Wakiwa bado wanatafakari hilo ghafla macho ya Anne yalianza kutoka nje na mapovu mengi pia yalitoka mdomoni watu wote waliogopa.
“Jamani mimi nafikiri huyu msichana ana mapepo!”
“Hata mimi!”
Mwalimu, walinzi na wanafunzi waliokuwepo walikubaliana kumpeleka Anne moja kwa moja kwenye mkutano huo!
“Hapana msinipeleke!”
“Kwanini?”
“Nitakufa kabisa!”
“Huwezi kufa huko ndiko utapata msaada!”
“Mama! Mama! Msinipeleke huko!” Alilia Anne
Baadaye alichomoka nakuanza kukimbia kuelekea ziwani, walipomfuata hawakumuwahi walimkuta ameshaingia majini na alizidi kuogelea kuelekea kwenye maji yenye kina kirefu zaidi, wanafunzi walizidi kuogelea kumfuata majini, kabla hawajamfikia Anne alizama majini na alipoibuka hakuwa yeye bali nyoka mkubwa aina ya chatu mwenye vichwa viwili! Wanafunzi na waalimu walikimbia na kutoka majini! Taarifa zilipelekwa kwa Huggins naye alishuka hadi ziwani kila mtu aliamini lile lilikuwa ni pepo.
Bila kuchelewa Huggins alishuka jukwaani na kuongozana na wanafunzi wengine hadi ziwani, mkononi alikuwa na Biblia yake, alipofika alishangaa kuona nyoka mkubwa majini!
“Mh! Huyu alikuwa mtu?”
“Ndiyo ni mwanafunzi mmoja anasoma hapahapa!”
“Anaitwa nani?”
“Anaitwa Anne!”
Alilikumbuka jina lakini hakusema kitu na bila kuchelewa alianza kuteremka kuingia majini, watu wote walimshangaa, alizidi kumsogelea yule nyoka huku akiwa amenyanyua mikono yake juu!
Nyoka alizidi kuvimba kama vile alitaka kumrukia Huggins amuume, watu wote waliokuwepo ziwani waliingiwa na hofu kubwa mioyoni mwao, walijua Huggins angeumwa na nyoka na kufa!
“Toka katika jina la …..!” Aliamuru Huggins huku bado hakukutoka kitu. Na watu wote walikuwa kimya kusikiliza.
“Nakuamuru katika jina la Yesu toka, mwachie kiumbe wa Mungu shetani wewe mwachie nenda nyikani na usirudi tena!” Alizidi kukemea Huggins.
Ghafla katika hali ambayo haikutegemewa na wengi nyoka yule alizama majini na alipoibuka hakuwa nyoka tena bali Anne, akilia machozi, watu wote walipigwa na butwaa.
“Ahsante baba kwa sababu umemweka mtumishi wako huru!” Huggins alisema akiwa amenyanyua mikono yake juu.
“Nisaidie Huggins nimeteseka kiasi kikubwa!”
“Siyo mimi ila ni yeye aishie ndani yangu atakusaidia, upo tayari kutubu?”
“Ndiyo!”
Hapohapo majini alimwangoza Anne Sala ya Toba, alipomaliza wote waliondoka kuelekea juu mahali kulipokuwa na mkutano awali ambako Anne alipandishwa jukwaani na kuanza kutoa ushuhuda juu ya mambo aliyowahi kuyafanya.
“Mama yangu alinifanya mimi mchawi bila kutaka, nasikitika nilisababisha kifo cha mwalimu Lutambi, Dioniz na mwalimu Catherine!” Aliposema tu maneno hayo wanafunzi wa Nsumba waliomfahamu Dioniz walianza kulia machozi.
“Haijalishi alifanya nini, Mungu amemweka huru na sasa yeye ni safi! Haleluya!!
“Ameeni!” Watu wote waliitikia kwa sauti kuu!
Kumbe katika watu waliokuwepo katika mkutano huo wapelelezi wawili walijichanganya, aliposhuka tu jukwaani Anne alifikia mikononi mwa polisi na kutiwa pingu mikono yote miwili.
“Tuonyeshe mahali ulipozika miili ya watu uliowaua umetusumbua sana!”Askari mmoja alimshambulia Anne na kumzaba vibao.
Je nini kitaendelea?
Je Anne ataonyesha mahali watu hao walipo?
HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 8
MTUNZI: ERIC JAMES SHIGONGO
Minong’ono ilitawala kila mahali watu wakijadiliana juu ya kitu ambacho Anne alikisema jukwaani kama ushuhuda wa maisha yake yaliyopita! Watu hawakuamini kama kweli Anne na jinsi alivyokuwa mzuri alikuwa mchawi na ndiye aliyemuua Dio na mwalimu wao Catherine.
Mkutano haukuendelea tena palepale ulivunjika na Anne huku akifuatwa na kundi kubwa la watu aliongozwa na maaskari kupelekwa kituo cha polisi ambako ilibidi aandikishe maelezo yake juu ya nguvu aliyokuwa nayo ndani ya mwili wake iliyomwezesha kuwaua Dioniz na watu wengine akiwemo mwalimu Lutambi na Catherine!
Kwa kila mtu aliyesikia tukio hilo na mpaka walimu wa shule ya Ngaza, ilikuwa si rahisi kuamini kuwa msichana mdogo na mwenye sura ya kuvutia kama Anne alikuwa na nguvu ya kichawi na za hatari kiasi kile, hata askari wa kike WP Jacqulline aliyekuwa akichukua maelezo ya Anne alitetemeka.
“Bila msaada wa maombi ya leo mimi ndiye nilikuwa nimetayarishwa kuwa mrithi wa mama yangu katika uchawi!”
‘Mrithi wa nani?”
“Ni habari ndefu sana ila fahamu tu kuwa kuna mzimu uitwao Lutego, upo katika ukoo wetu ni huu ambao hutumika kutulinda sisi watu na ukoo wote wa mzee Kamanzi! Mzimu huu hukaa ndani ya mwanamke mmoja katika ukoo!”
“Kwa hivi sasa anao nani?”
“Anao mama yangu na baada ya kufa yeye mzimu huo ungeniingia mimi na tangu siku hiyo ningekuwa na uwezo mkubwa mno kichawi na ni mimi ndiye ningekuwa malkia wa wachawi kanda ya ziwa!”
Maelezo hayo ya Anne yalizidi kumtisha WP Jacqulline na maaskari wengine na kuwafanya wawe na wasiwasi zaidi, kwa hofu hiyo hakuna hata askari mmoja aliyethubutu kumpiga Anne, askari aliyemzaba kibao baada ya kumtia pingu kwenye mkutano aliingiwa na wasiwasi mkubwa maisha yake, ikabidi amfuate Anne kumwomba msamaha.
“Nisamehe sana dada yangu!” Alisema baada ya kupiga magoti chini.
“Usiwe na wasiwasi Afande hayo ni ya zamani, hivi sasa mimi ni kiumbe kipya kabisa! Sina tena mambo hayo nimeokolewa na kuwa huru!” Alijibu Anne.
****
Baada ya maelezo hayo Anne alichukuliwa na maaskari na kupelekwa kwenye chumba cha mkuu wa kituo ambako pia alitoa maelezo yaliyomtisha sana mkuu huyo, bila kuchelewa alitoa idadi ya maaskari wapatao sita na gari la kunyonya maji machafu kwenda kuona kama kweli miili ile ilikuwa ndani ya shimo alilodai Anne au la!
“Binti kweli una hakika miili hiyo ipo ndani ya shimo manaake usitupotezee muda wetu bure!”
“Afande hauamini basi twende ukaone!”Anne alisema kwa ujasiri ingawa moyoni mwake alishindwa kuwa na uhakika zaidi kama kweli miili wangeikuta ndani ya shimo la maji machafu au la! Kitendo cha kuwaona akina Dioniz na mwalimu Catherine kisiwani Kome katika moja ya sherehe zao za kichawi zilizofanyika usiku kilimfanya akose uhakika!
“Sina uhakika lakini acha twende tukaone, kama haipo sijui nitawaeleza nini!” Aliwaza Anne.
****
Habari juu ya tukio la mwanafunzi na kukiri kuua watu kichawi na kutumbukiza maiti zao katika shimo la maji machafu zilivuma sana katika maeneo yote ya kuzunguka shule ya Ngaza na hatimaye yalifika shule ya sekondari ya Nsumba, wanafunzi walipopata taarifa kuwa gari la polisi lilikuwa likinyonya maji katika shimo hilo ili kuzitoa hizo wengi walimiminika shuleni hapo kushuhudia tukio hilo la ajabu.
Pamoja na kuwepo na watu wengine idadi kubwa ya watu waliokuwepo walikuwa ni wanafunzi wa shule ya sekondari ya Nsumba, waliokuwa wakilia machozi kumlilia Dioniz rafiki yao mpendwa.
Gari la majitaka lililomilikiwa na jeshi la polisi liliendelea kunyonya maji yote yaliyokuwemo ndani ya shimo hilo ili kuona kama kweli miili ya Dioniz na mwalimu Catherine ilikuwemo ndani ya shimo hilo kama alivyodai Anne.
Watu mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali ya habari walikuwepo kushuhudia tukio hilo, walimpiga Anne picha nyingi zisizo na idadi na alijua wazi kuwa magazeti ya siku iliyofuata yangejaa picha na habari zake kwa kichwa cha habari ambacho wangetaka wenyewe.
Anne hakuona aibu wala kujuta moyoni mwake kuitwa mchawi! Hiyo ni kwa sababu hakuwa hivyo tena hayo yote kwake yalikuwa mapito, hiyo ilikuwa historia yeye wakati huo alijisikia ni mtu mpya na mwenye mtazamo wa kimungu zaidi kuliko dunia.
Wanafunzi wa Nsumba wenye hasira walimkuta Huggins akiwa pale na aliwasimulia kila kilichotokea na kuwaomba wawe wavumilivu mpaka mwisho wa tukio hilo, alihofia wangeweza kufanya jambo lolote kwa hasira ya kumpoteza Dioniz.
Maneno ya Huggins hayakusaidia lolote kwani badala ya wanafunzi kuwa wavumilivu waliendelea kumshambulia Anne kwa maneno makali huku wengine wakimmwagia mchanga machoni na kumwita mchawi, wanafunzi wa Ngaza pamoja na polisi walijaribu kuzuia lakini haikuwezekana.
“Tuue wote basi, ulimuua Dio unashindwa nini kutumaliza na sisi kabisa?”
Anne alizidi kulia machozi, Huggins alimhurumia na akamsogelea na kuanza kumfuta machozi yake machoni.
“Jamani! Jamani! Jamani!” Huggins alipiga kelele Huggins akiwaomba wanafunzi wenzake wamsikilize na kweli walitulia ili kusikia alichotaka kusema.
Pamoja na Huggins kuwa kiongozi wa UKWATA katika shule ya Nsumba pia alikuwa kiranja mkuu hivyo wanafunzi walimheshimu sana.
“Wanafunzi wenzangu nawaombeni sana tafadhali msimsumbue Anne kwani hana makosa, yaliyotokea yote si kwa mapenzi yake, tafadhali msimwagie mchanga wala kumwita mchawi, kwa taarifa yenu ndugu zangu hivi sasa Anne ni mpendwa mwenzetu amekwishaamua kumpokea kristo na kufanya ngome yake yaliyotokea nyuma katika maisha yake hayajalishi tena, hebu tushangilie!” Alisema Huggins lakini idadi ya watu walishangilia haikuwa kubwa sana wengi walionekana kutaka kuendelea kummwagia mchanga na kumpiga Anne.
Muda wote Anne alikuwa akilia machozi, alizidi kumlaumu mama yake kwa alichomfanyia, alijilaumu kuzaliwa katika ukoo wa wachawi, katika maisha yake hakutaka kuua lakini tayari alishafanya hivyo bila mapenzi yake mwenyewe!
“Kwa kweli simpendi mama ila nimemsamehe kwa sababu hivi sasa nimeokoka!” Aliwaza Anne.
Wakati hayo yote yakiendelea mpira mkubwa wa gari la maji taka ulikuwa ndani ya shimo ukiendelea kunyonya maji machafu, watu wote walikaa kusubiri maji yaishe ili waone kama kweli maiti zilikuwepo chini.
Dakika ishirini na tano baadaye kazi hiyo ilimalizika na wafanyakazi wawili wa gari hilo walichungulia ndani ya shimo kukagua, macho yao yalipambana na tope zito, hawakuona kitu chochote kile!
Baada ya majadiliano na uongozi wa shule uamuzi ulifikiwa kuwa shimo hilo libomolewe ili maaskari waingie ndani kuangalia vizuri ndani ya tope ili kuona kama kweli kulikuwa na kitu chochote kimejificha humo.
Ilikuwa ni lazima waangalie ndani ili kujua kama kweli yaliyosemwa na Anne yalikuwa kweli au la, Anne alikuwa pale na pingu zake mikononi akishuhudia choo kikipigwa nyundo na kubomolewa, ilipomalizika kazi hiyo maaskari wawili waliovaa mavazi maalum waliingia ndani ya shimo na kwa kutumia chepeo walianza kulichambua tope lililokuwepo chini wakiangalia.
Ghafla chepeo la mmoja wao liligonga kwenye kitu kigumu kilichokuwa ndani ya matope, alipokibinua kilikuwa ni kipande kikubwa cha mgomba, kilichofungwa khanga na alipoivuta khanga aligundua ilifungwa kwenye jiwe kubwa lililokuwepo pembeni.
Muda mfupi baadaye askari huyo huyo alipambana na kipande kingine cha mgomba kilichofungwa kwenye jiwe, alizidi kushangaa!
Walipomaliza kazi hiyo hapakuwa na kitu kingine zaidi ya mgomba ndani ya tope hilo, Maaskari wote walishangaa na kuitoa migomba ile nje!
‘Tumekutana na migomba hii tu hakuna kitu kingine chochote ndani ya shimo hili!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Binti uliwatupa wapi mbona hatuwaoni?”
“Niliwadumbukiza humo humo ndani ya shimo! Sijui maiti zao zimepotelea wapi ila hiyo nguo ilikuwa ya mwalimu Catherine!”
Waalimu na wanafunzi wote waliokuwepo pale waliitambua nguo ile, ilikuwa ya mwalimu Catherine na alipenda sana kuivaa baada ya saa za kazi.
Maaskari walizidi kuchanganyikiwa lakini watu wa kanda ya ziwa waliokuwepo eneo lile walielewa migomba ile ilimaanisha kitu gani kuwepo ndani ya shimo hilo, miili yote ya watu waliochukuliwa msukule ilibadilika kuwa migomba.
****
Pamoja na kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuwa kweli Anne aliwaua Dioniz, mwalimu Lutambia na mwalimu Catherine, tendo pekee la kukiri mauaji kilitosha kabisa kumfanya awekwe mahabusu! Huggins alijitahidi kuwaomba askari wasifanye hivyo lakini haikuwezekana kuwazuia walidai hata kama alitubu kwenye mkutano wa dini kisheria alikuwa bado ana kesi ya kujibu na kama ingethibitika alifanya mauaji hayo angehukumiwa kifungo cha maisha.
“Jamani si mmwachie tu kwa sababu ametubu!”
“Hapana hiyo haiwezekani hata kidogo ni lazima akae mahabusu mpaka upelelezi ukamilike!”
Huggins badala ya kufurahia alilia machozi, wanafunzi wenzake walishangaa kuona akimtetea Anne mtu aliyemuua Dio rafiki yao kipenzi.
“Ebwanae na wewe usilete ulokole wako hapa hebu twende zetu shule upesi si umwache akafie lupango, wewe inakuuma nini? Mbona Dio alikufa” Alifoka kijana mmoja.
“Hapana jamani, Anne amekwishatubu hayo ina maana amekwishasamehewa mbinguni na duniani!”
“Mbinguni na wapi?”
“Duniani!”
“Mbinguni sawa lakini duniani, anajidanganya ni lazima akanyee ndoo tu!” alijibu mwanafunzi mwingine.
****
Mkutano wa wanachama wa Lutego ulikuwa umekutana kwa dharura kuliongelea suala la Anne kukiri kuua watu kichawi na kuokoka, jambo ambalo hakutakiwa kabisa kulifanya hata kama angekuwa amewekewa kisu shingoni, hilo lilikuwa mwiko kwa wanachama wote wa chama hicho! Kuamua kwake kumpokea Yesu Kristo lilikuwa kero kubwa sana kwa mama yake na wanachama wenzake ambao hatimaye walidhamiria kunywa damu yake kupunguza hasira zao!
Uamuzi huo kwa maana nyingine ulimaanisha kifo cha Anne, ilikuwa ni lazima afe na damu yake inywewe na wanachama.
“Mtoto huyu kanikosea sana na nitaamuru watu wanywe damu yake sasa hivi kwanini kaenda kuniadhirisha kiasi hicho?” Aliwaza mama yake Anne.
Kikao kizima kilikuwa kimya watu wote wakifikiria ni nani angemrithi malkia kama mtu aliyetegemewa kufanya hivyo alikuwa ameamua kukiasi chama chao na kujiunga na Ukristo!
“Ni lazima Anne afe!” Alipiga kelele mama yake na vibibi vizee vyote viligeuka kumwangalia kwa mshtuko mkubwa! Ilikuwa ni mara ya kwanza kumwona mama yake Anne akiwa katika hali hiyo hawakujua nini kingempata Anne huko alikokuwa.
“Nileteeni damu ya mtoto mchanga hapa upesi!” Haikuchukua hata sekunde mbili damu ikaletwa katika kikombe cheupe.
“Haya nileteeni kipande cha kamba aliyojinyongea mwanamke!” haikuchukua muda mrefu kamba hiyo ikaletwa!
“Naomba mniletee kipande cha sanda ya zeruzeru pamoja na mchanga kutoka kwenye kaburi la mwendawazimu!”
Vitu vyote hivyo alikabidhiwa, alichukua sanda, kamba na kuvichoma moto na majivu yake aliyamwaga katika kikombe cha damu ya mtoto na vyote kwa pamoja alivinywa.
Aliposhusha kikombe mwili wake ulikuwa ukifuka moshi jambo kuwa alikuwa na hasira kubwa sana.
“Nisikilizeni kwa makini leo nimekasirika kupita kiasi na nafikiri nimesikia mambo ambayo Anne ameyafanya huko shuleni kwao, ametusaliti vibaya mno hivyo nimeamua afe hukohuko mahabusu aliko na ninakwenda mwenyewe ninafikiri hatanisumbua, hivyo nitarudi sasa hivi nisubirini”
Baada ya kusema hayo kiti alichokalia kilibaki tupu akawa amepotea ghafla katika kimbunga kilichotokea.
****
Mpaka saa tisa hivi usiku Huggins alikuwa hajapata usingizi, mawazo yake yalikuwa kwa Anne aliyekuwa mahabusu akiteseka, alijishangaa ni kwanini alikuwa amevutiwa kiasi hicho na msichana huyo, kwa mara ya kwanza katika kipindi kirefu alihisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kikitokea ndani ya moyo wake.
Huggins alihisi kumpenda Anne, alimhurumia kwa mateso aliyokuwa akiyapata ingawa tayari alishaokoka na kubadilishwa! Usiku huo alikuwa katikati ya maombi akimwomba Mungu amlinde Anne huko mahabusu alikokuwa.
Anne naye mpaka muda huohuo alikuwa akifanya maombi ya toba, alikuwa akitubu dhambi za kuua alizofanya na kumwomba Mungu amtie nguvu zaidi ili aweze kupambana na mzimu wa Lutego ambao alijua kwa vyovyote ungetumwa kwake.
Ghafla akiwa katikati ya maombi hayo alishtukia anasikia kishindo kikubwa sana nje ya mahabusu, wafungwa wote walikuwa wamelala usingizi katika sakafu iliyolowa maji na mikojo! Ni yeye tu aliyesikia.
Baada ya hapo aliendelea kusikia vishindo vikiendelea nje ya mahabusu, Anne alijua ni nini kilikuwa kikitokea nje, alijua huyo alikuwa mama yake na yeye alizidisha maombi akimwomba Mungu ampe ulinzi zaidi, alijua wazi bila ulinzi wa Mungu siku hiyo ndiyo ingekuwa mwisho wake.
Ghafla alianza kusikia sauti ya bundi wengi wakilia nje na sauti ya mtu akiita jina lake ilisikika pia, sauti hiyo ilikuwa ya mama yake alijua alikuwa amekuja kumdhuru kwa sababu ya msimamo wake, Anne alizidi kumwomba Mungu amsaidie katika janga lililokuwa mbele yake.
Baadaye sauti za bundi zilitulia lakini vishindo viliendelea kuwepo mpaka mwanga wa jua ulianza kutokea kwenye kidirisha kidogo kilichokuwa juu ya mahabusu, ilionyesha kuwa tayari kulikuwa kumekucha.
Majira aliyoyakadiria kuwa saa kumi na mbili na nusu hivi alisikia sauti za watu wakipiga kelele nje ya mahabusu.
“Jamani mwanga! Mwanga! Mwanga! Huyu hapa mwanga! Amekuja kuloga kituo cha polisi!” Anne aliisikia sauti hiyo na kujua kilichotokea, mama yake alikuwa ameshikwa wanga kituoni.
Kelele ziliendelea na alianza kusikia kilio cha mama yake na watu wakimpiga, muda mfupi baadaye katika hali ambayo hakuitegemea Anne alishtukia mlango wa mahabusu ukifunguliwa na mama yake akitupwa ndani, alikuwa uchi wa mnyama akiwa amevalia mavazi ya kutisha ya kichawi Anne alipiga kelele kuomba msaada!
“Kuniingiza humu wamenirahisishia kazi!” mama yake alitamka huku akicheka.
Je nini kitaendelea?
Je Anne ataweza kuuawa humo?
Tags:
RIWAYA