ILIPOTOKA...
Ni hadithi inayohusu maisha ya msichana Anne na nguvu za giza. Mwanamke mrembo, Anne amefikishwa mbele ya mahakama kwa kosa la kumuua mama yake kwa kumchoma kisu. Kesi yake inakuwa nzito, huku hakimu ambaye alisoma naye akitaka kumtetea kwa kumuweka huru, mwenyewe anasema kwamba anastahili kufa.
Baada ya hapo mahakamani, maisha yaliyopita ya mwanamke huyo yanaanza kuonekana katika simulizi hii. Alipokuwa mdogo, mama yake alipanga kumrithisha umalkia wa uchawi hivyo hakutakiwa kufanya mapenzi na mtu yeyote yule vinginevyo mwanaume atakayejaribu kufanya naye mapenzi atakufa.
Mwalimu wake anapombaka ofisini, anakufa hapohapo, anapofanya mapenzi na mpenzi wake, Dioniz, naye anakufa. Mbali na hao, pia kulikuwa na mwalimu wake, Catherine, naye anakufa.
Maisha yamebadilika, anaua bila kupenda, uchawi unamwendesha Anne. Huku akiwa ameua sana, anakutana na nguvu za Mungu hivyo kuamua kuokoka.
Hiyo hamsaidii kumuepusha na kesi ya mauaji, anachukuliwa na kupelekwa sero akisubiri kesi inayomkabili kwa kumuua Dioniz na walimu wake.
Mara baada ya kuokoka, mama yake anakasirika hivyo kuamua kumfuata hukohuko sero kwa lengo kumuua kwa mikono yake, kisa tu aliamua kuokoka.
SONGA NAYO....
“Ndiyo ni mama yangu lakini there is nothing I can do to help”(Hakuna ninachoweza kufanya kusaidia!) Alitamka Anne huku akitupa mikono yake huku na kule kwa hasira, alionyesha ni kiasi gani alimchukia mama yake, shetani alimwingia na kujikuta akilia machozi kwa hasira, madereva walishangaa.
“Kwanini mmemleta hapa lakini?” Anne alimfokea dereva teksi.
“Amesema yeye ni mama yako na kwa sababu ni mgonjwa tukashindwa kumwacha ukizingatia sisi tunakufahamu!”
“Asanteni sana ndugu zangu lakini ninasikitika mimi siwezi kumpokea huyu mama!”
“Lakini ni mama yako kweli?”
“Ndiyo lakini……!”
“Lakini dada hata kama alikukosea huyu ni mama yako tafadhali tunakuomba umpokee!”
“Nasema haiwezekani!” Anne aliongea akiwa ametoa macho kumwangalia dereva.
“Kwanini?”
“Mimi ninajua kwanini sitaki kumpokea nyinyi hamuwezi kuelewa ni bora mniache niendelee na uamuzi wangu!”
Mama yake Anne, Isabella alikuwa ndani ya gari hajiwezi mwili wake ukiwa umevimba kwa sababu ya kupigwa, ingawa hakueleza ni kwa sababu gani sungusungu walimpiga Anne alijua ilikuwa ni sababu ya uchawi wake na ni hilo hilo ndilo lililomfanya asiwasiliane na mama yake kwa miaka karibu kumi.
“Sasa dada tutafanya nini na huyu mama yako?”
“Kwa kweli mimi sijui labda mmrudishe mlipomchukua!” Alisema Anne bila huruma, ni kweli alikuwa mama yake lakini alimuogopa.
“Na pesa yetu atatulipa nani?”
“Kama ni pesa nitawalipa lakini sipo tayari hata kidogo kumpokea!”
“Basi tulipe hizo pesa zetu sisi tuondoke!”
“Nisubirini!” Alisema Anne na kuondoka kuingia ndani na aliporudi alikuwa na noti ya shilingi mia tano mkononi mwake na kumkabidhi dereva.
Cha kushangaza baada ya dereva kuipokea pesa hiyo alifungua mlango na kuanza kumshusha mama yake Anne kutoka ndani ya gari, alipomfikisha chini alimuamuru kijana aliyekuwa naye aingie ndani ya gari na walianza kuondoka kwa kasi.
“Mama yako huyo hapo chini bwana, hatuwezi kuzunguka nae tuache kufanya biashara utajua mwenyewe la kufanya naye ili mradi amekwishafika kwako!” Alisema dereva wakati gari lake likiondoka.
Anne alimwangalia mama yake na roho ikamuuma kupita kiasi kweli Isabella alikuwa mama yake kabisa, lakini mambo ambayo mama yake alimfanyia katika maisha yake hakuyafurahia hata kidogo kwa sababu hiyo hakuwa tayari kumkaribisha ndani.
Alijua kufanya hivyo lingekuwa kosa kubwa kwani ni lazima mama yake angesababisha madhara makubwa sana kwa familia yake hasa kwa watoto wake wakiwemo mapacha Patrick na Nancy waliokuwa na umri wa mwaka mmoja tu wakati huo.
“Nisaidie mwanangu!” Isabella alilia akimwangalia mwanae Anne usoni, alishangaa kuona mtoto wake hakuwa na huruma kiasi kile lakini kwa aliyomtendea hakuhitaji kumlaumu.
“Mama siwezi kukusaidia sababu tabia na mwenendo wako ni mbaya sana! Hebu nieleze kwanini umechapwa kiasi hiki?”
“Wanadai mimi mchawi!”
“Wanadai?”
“Ndiyo!”
“Yaani hata mimi unaniambia hivyo wakati kila kitu nakielewa cha muhimu mama uache tabia hiyo! Si unaona matatizo yake?”
“Nimekwishaacha mwanangu na ninaomba tu unipokee nyumbani kwako unitibu mpaka nipone!”
“Hapana mama siwezi kufanya hivyo mume wangu hatakubali hata kidogo kwani anaifaha....!” Kabla hajamaliza sentensi yake Anne alisikia mlio wa gari ikitokea upande wake wa kulia alipogeuka lilikuwa gari la Huggins! Alishangaa ni kwanini mume wake alirudi nyumbani muda huo kitu ambacho hakikuwa kawaida yake.
“Vipi honey mbona umerudi saa hizi tena?”
“Nimepigiwa simu kuwa hapa nyumbani kuna mgeni tena ni mgonjwa na umekataa kumpokea!” Alijibu Huggins baada ya kuteremka kwenye gari.
“Ndiyo ni huyu mama yangu! Sitaki kabisa aingie ndani kwetu!”
Huggins aliinama na kumwangalia mama mkwe wake aliyekuwa amelala chini huruma ilimshika moyoni mwake, alijua kilichomfanya mke wake asikubali mama yake aingie ndani!
Aliuogopa uchawi wa mama yake lakini yeye Huggins hakuwa na hofu kwani alijua ile ilikuwa ndiyo nafasi nzuri ya kumbadilisha mama yake na Anne na kumfanya aachane na matumizi ya nguzu za giza!
“Anne mruhusu tu mama aingine ndani tafadhali nakuomba!”
“Haiwezekani! Sitaki! Sitaki Huggins, mimi namfahamu mama!”
“Mwache mama Anne! Yasahau ya zamani wewe sasa unaifahamu nuru lazima uwe tayari kutoa msamaha!” Alisema
Huggins lakini badala ya Anne kukubali alianza kulia machozi.
Huggins aliendelea kumbembeleza mke wake mpaka akakubali na wote wawili walisaidiana kumbeba Isabella na kumwingiza ndani ya nyumba yao na dakika chache baadaye Huggins alitoka na kwenda kumtafuta daktari aliyekuja nyumbani na kuanza kumpa Isabella matibabu.
Baada ya huduma hiyo Huggins aliondoka kurejea kazini kwake na kumwacha mke wake akimhudumia mama mkwe wake kwa chakula, Anne aliyafanya yote hayo akiwa na hofu kubwa, watoto wake wakubwa Frank na William walimuuliza maswali mengi wakitaka kujua Isabella alikuwa nani.
“Ni bibi yenu ndiye mama yangu mzazi!”
Watoto wake walifurahi sana kumwona bibi mzaa mama yao.
******
Ilimchukua Isabella miezi miwili mpaka kurejea katika hali yake ya kawaida na katika muda huo wote Huggins na Anne waliendelea kumpasha mama yaojuu ya Mungu ili ageuke na kuyaacha mambo yake mabaya! Kwa juujuu Isabella aliwakubalia lakini ndani ya moyo wake roho ya uchawi iliendelea kumtawala na pamoja na wema wote aliofanyiwa mpango wake wa kumuua mwanae bado uliendelea.
******
Baada ya Huggins na Anne kuwa wamekaa na mama yao kwa miezi sita bila matatizo, akiwa amewahakikishia kuwa tabia ya uchawi aliiacha, wote walimkubali na kuyasahau ya zamani.
Anne alimsamehe kabisa mama yake ikawa ni familia yenye furaha tena,mama aliishi kwa raha na alikuwa kipenzi kikubwa cha wajukuu zake, ilikuwa si rahisi kuamini Isabella aliwahi kuwa mshirikina.
Kasoro pekee aliyokuwa nayo mama yao ni kutokwenda kanisani! Hakuweza kwenda kanisani kwa sababu siku aliyojaribu kufanya hivyo alipoukaribia mlango wa kanisa alianguka chini akageuza macho na kuanza kutoa mapovu mdomoni.
Kwa siku tano mfululizo Isabella alikuwa kama mwendawazimu akiongea peke yake na kuokota makopo, alitulia baada ya kufanyiwa maombi na wachungaji lakini tangu siku hiyo hakuthubutu kuingia tena kanisani, si kanisani tu bali hata nyumbani hakushiriki ibada yoyote kila mahali lilipotajwa jina la Mungu yeye hakuthubutu kusimama, kila mtu aliamini Isabella bado alikuwa na mapepo.
Huggins na Anne pamoja na watoto wao walimwamini Isabella lakini kumbe hakufaa kuaminiwa, kwani roho yake bado ilijaa uchawi na nia ya kuua! Isabella alichukizwa sana na kitendo cha mwanae aliyetegemewa kuwa mrithi wake wa mzimu wa Lutego kujiunga na Ukristo kitu ambacho hakutakiwa kukifanya.
Hapakuwa na mtu mwingine wa kuurithi mzimu wake isipokuwa Anne peke yake na kila siku iliyokwenda kwa Mungu Isabella alitamani sana Anne aanguke na kurejea katika imani yao lakini haikuwa hivyo.
Hatimaye siku moja baada ya Isabella kuwa amevumilia sana alifikia uamuzi wa kumwita mwanae kwa maongezi siku hiyo Huggins hakuwepo nyumbani.
“Anne nimejaribu sana kuvumilia lakini nimeshindwa na ninaomba niseme wazi nia yangu ya kuja hapa ilikuwa kukuua lakini nilipofika hapa kwa msaada ulionipa niliamua kughairi!”
Moyo wa Anne ulilipuka na kujikuta akikubwa na hofu kubwa,
lakini alijikaza hakutaka kuonyesha udhaifu wa wazi.
“Asante mama!”
“Sipendi hata kidogo kukua mwanangu, lakini wanachama wa Lutego wote walichukizwa sana na kitendo chako cha kuingia katika Ukristo na wote wanahitaji kunywa damu yako, siku zote nimejaribu kujitahidi sana kukutetea lakini siku zote imeshindikana, juzi nilipoongea nao walisema ili wakuache hai ni lazima uache dini yako na urejee na kuwa malkia nitakapokufa!”
“Mama kumbe bado unahudhuria sherehe zenu usiku?” Anne aliuliza kwa mshangao hakuamini kabisa kama mama yake katika siku zote alizokaa nao alikuwa akitoka usiku na kwenda kwenye vikao vya wachawi!
“Hilo usijali kitu cha muhimu wewe eleza unakubali kuacha dini yako au hapana!”
“Mama hiyo haiwezekani tena!”
“Kweli? Shauri yako yatakupata makubwa!”
“Mama lolote na liwe!”
Maongezi yao hayakuendelea tena, yaliishia hapo hapo Isabella alionyesha hasira kali.
Jioni ya siku hiyo Huggins aliporejea kutoka kazini kwake hakuwa mtu mwenye furaha kama siku zilizotangulia, alionekana mnyonge na mwenye mawazo mengi, kwa sababu hiyo Anne alishindwa hata kumweleza kilichotokea siku hiyo nyumbani kati yake na mama yake na alipomchunguza mume wake vizuri usoni aligundua Huggins alikuwa akilia! Anne alishtuka na kumsogelea.
“Vipi tena baba?”
“Nina matatizo makubwa sana mke wangu!”
“Matatizo gani tena?”
“Nimepunguzwa kazi ofisini!”
“Umepunguzwa kazini kwa sababu gani?”
“Hata mimi sijui ila wafanyakazi kama kumi hivi tumepewa barua za kupunguzwa kazi na tutalipwa mafao yetu baadaye!”
“Mh! Unasema kweli au unatania baba Patrick!”
“Kweli ndiyo maana unaona nina hali hii nashidwa kuelewa maisha yetu yatakuwaje!” Alisema Huggins na kuendelea kulia huku mkewe akimbembeleza na kumpa moyo!
“Usilie darling hayo ni majaribu tu, si ajabu Mungu amekutayarishia sehemu nyingine nzuri zaidi!”
“Kweli?” Aliuliza kwa mshangao Huggins ilikuwa si rahisi hata kidogo kuyaamini maneno ya mkewe kwani kutokea kwa jambo hilo kulimaanisha mwisho wa kila kitu!Mwisho wa raha zote na mwisho wa furaha iliyokuwa katika maisha yao.
*****
Wakati Huggins anasimamishwa kazi ulikuwa ni mwezi wa kumi na mbili katikati na hayo yaliyotokea yalikuwa ni jaribu makubwa katika maisha yao, yalihitaji mtu imara kusimama.
Huggins akawa haendi tena kazini akawa mtu wa kushinda nyumbani na familia yake na usiku ulipoingia alilala, hiyo ndiyo ikawa ratiba yake ya kila siku kwa mtu aliyezoea kazi yalikuwa ni mateso makubwa! Watoto wake walimsumbua sana wakimuuliza maswali ni kwanini alikuwa haendi kazini tena, hakuwa na jibu la kuwapa ila maswali hayo yaliuumiza moyo wake sana.
******
Shule zilipofunguliwa Huggins hakuwa na pesa ya ada ya watoto wake kwani mafao yao hayakuwa tayari! Watoto walimsumbua kwa maswali wakitaka kujua ni kwanini walikuwa hawaendi shule wakati wenzao walikuwa wakisoma!
Watoto hakuwakujua tatizo lilikuwa ni ada, Huggins hakuwa na akiba yoyote, akaunti yake haikuwa na pesa, pesa yote aliitumia kununulia shamba sehemu za Nyegezi mwezi mmoja kabla ya kupunguzwa kazi! Alishindwa kuelewa angepata wapi pesa za kulipa ada ya watoto wake.
Ni usumbufu wa maswali ya watoto wake yaliyomfanya asiwe anashinda nyumbani na kurudi usiku watoto wakiwa wamelala ni mke wake aliyempa ushauri wa kuuza gari lao ili wapate pesa za kulipa ada ya watoto ! Huggins hakuwa mbishi mbele ya mke wake ilibidi aliuze gari lao na pesa iliyopatikana aliwalipia watoto wake ada katika shule ya kimataifa, waliyokuwa wakisoma na sehemu nyingine alilipa pango la nyumba yao lililokuwa limekwisha.
Watoto walianza kwenda shule lakini bado waliendelea kumsumbua baba yao na maswali zaidi, kila jumapili walimuuliza gari lilikuwa wapi waende kanisani kuna wakati walikataa kwenda kanisani kwa kutumia daladala wakitaka gari la baba roho ya Huggins ilizidi kuuma zaidi, alitamani yaliyokuwa yakitokea yawe ndoto lakini uliendelea kubaki ukweli.
Watu wengi kanisani waliyaelewa matatizo yake na walimpa pole wakifikiri ingesaidia lakini ndiyo alizidi kumfanya achanganyikiwe zaidi mwisho alianza kuona aibu mbele ya waumini wenzake taratibu akaanza kupunguza safari zake za kwenda kanisani mke wake peke yake na watoto wakawa wanahudhuria misa kila Jumapili, Anne alimshauri Huggins arejee kanisani lakini haikuwezekana.
Kitendo hicho cha Huggins kilimfanya mke wake awe analia machozi na alilia zaidi siku Huggins aliporudi nyumbani akiwa amelewa pombe chakari, hakuwahi kumwona Huggins akiwa amelewa katika maisha yao ya ndoa hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza na alijua wazi kuwa mumewe alikuwa amevurugikiwa.
“Huggins umeanza kunywa pombe?”
“Ni lazima nipumzishe mawazo mke wangu nitachanganyikiwa!”
“Upumzishe mawazo kwa pombe badala ya kufunga na kuomba?”
Huggins hakunywa pombe tu bali alianza pia tabia ya kuwa anampiga mke wake na kusumbua watoto! Ilibidi Anne apeleke taarifa hizo kwa wazazi wake na Huggins ambao pia walijaribu kumshauri mtoto wao bila mafanikio tabia ya Huggins ilizidi kuwa mbaya.
Huggins alipoteza imani kwa Mungu katika muda mfupi tangu alipopunguzwa kazi, alishindwa kuelewa hayo yalikuwa majaribu ambayo ilikuwa ni lazima ayapitie, akawa mlevi kupindukia na watu wengi walishangazwa na mabadiliko hayo na kuna wakati akawa analala katika baa na kurudi asubuhi.
Hali hiyo ilimvunja moyo sana Anne naye pia akawa haendi kanisani tena, imani katika familia yao ikapotea na uwepo wa Mungu ukaisha! Mama yake Anne aliifurahia hali hiyo kwa sababu jina la Mungu likawa halitajwi tena katika familia yao, shetani akatawala kila kona ya nyumba! Kwake huo ndio ulikuwa wakati mwafaka wa kufanya kazi yake iliyomleta mjini.
******
“Mwanangu Anne hili sasa ni ombi la mwisho, jana tulikuwa kwenye kikao cha Lutego, wazee wametaka damu yako na nilipokataa sana walisema wanataka damu ya watoto wako wawili!”
‘MAMAAAA! UNANITAFUTA NINI? NINAAMINI NI WEWE UMENIHARIBIA NDOA YANGU NA UCHAWI WAKO!”
“Unasemaje?”
“Tena nasema ondoka kwangu leo hii nitakuitia polisi!”
“Unanifukuza Anne?”
“Ndio mama na ninajuta kukukaribisha hapa nyumbani!”
“Naondoka lakini cha moto utakiona!”
Siku hiyo hiyo mama yake alikusanya mizigo yake na kuondoka, ilikuwa yapata saa tisa za jioni na Huggins aliporejea saa sita usiku Anne alimsimulia kila kitu kilichotokea na kumwambia mama yake alikuwa ameondoka kurejea Kisiwani Kome.
“Heri mama yako ameondoka labda ndiye anayenitia mikosi hii?” Alisema Huggins.
Waliongea mengi baadaye walipitiwa na usingizi, masaa matatu baadaye walizinduliwa na kelele ndani ya chumba chao walipofungua macho kulikuwa na mwanga mkali kupita kiasi, wote waliogopa na miili yao ilitetemeka.
“Baba Patrick nini?”
“Hata mimi sijui!”
Hali hiyo ilidumu kwa dakika ishirini ilipotulia walikwenda kwenye chumba cha watoto na kujikuta wakilia walipowakuta watoto wao wawili Frank na William wakiwa wamening’iniza vichwa pembeni mwa vitanda vyao damu zikiwatoka puani na mdomoni! Walikuwa wamekufa.
“MAMAAAAA KWELI UMEUA WANANGUUUU!” Anne alipiga kelele.
“Ni mama aliyewaua?” Huggins aliuliza.
Je nini kitatokea?
Tuonane siku ya Jumatano mahali hapa.
TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 10
Songa nayo
KWA kawaida wazazi wengi huwa na upendeleo fulani kwa baadhi ya watoto wao, mzazi anaweza kuwa na watoto kumi lakini akawa anampenda zaidi mtoto mmoja au wawili kati yao pamoja na kuwa wote ni watoto wake, katika familia nyingine hali hufikia mpaka watoto wengine kuelewa kabisa kuwa mtoto fulani ni kipenzi cha baba au mama na wengine sio!
Hivyo ndivyo pia ilivyokuwa kwa Huggins, alikuwa na watoto wanne lakini kati ya watoto hao aliwapenda sana Frank na William, hawakuwa watoto wake tu bali marafiki zake wakubwa, ingawa umri wao ulikuwa mdogo ni wao waliomwambia aache tabia mbaya ya kunywa pombe kwa wingi na kurudi nyumbani usiku na wakati mwingine kumsumbua mama yao.
Ni watoto hao kipenzi wa Huggins, ndiyo walikuwa wakining’inia darini damu zilichuruzika sakafuni.
“Patrick na Nancy wako wapi?” Huggins alimuuliza mke wake.
“Wako kitandani wamelala!”
“Hawajashtuka?”
Wangeshtuka wangelia!”
Aliendelea kujibu Anne huku akilia.
****
Ghafla bila kutegemea kibunga kikubwa na cha ajabu kiliibuka nje ya nyumba yao.
“Anne ni nini hiki lakini, nini kimetupata jamani? Mbona mimi sielewi”
“Huggins huyu ni mama tu hakuna mwingine na anafanya hivi kwa sababu ninamemwasi na kujiunga na Ukristo!”
“Kweli ni mama yako?” aliuliza tena Huggins kwa mshangao.
“Nakuambia hakuna mwingine huyu ni mama tu na nguvu zake za giza na ndiye kawaua watoto wetu Frank na William!”
“Hivi kweli Frank na William wamekufa ehe?”
“Nina hakika watoto wetu wamekufa Huggins!” Aliitikia Anne huku akilia.
Pamoja na yote aliyoyaona kwa macho yake bado Huggins hakuamini kama kweli watoto wake walikuwa wamekufa, alichofanya ni kutafuta kitu cha kukanyagia ili apande juu na kuhakikisha kama kweli Frank na William walikuwa wamekufa au la!
Alipata kiti kirefu na kukisogeza karibu na mahali mwili wa Frank ulipokuwa ukining’inia lakini kabla hajapanda ili kuangalia alisikia sauti ya kutisha ikitokea dirishani kwao.
“Anne mwanangu ni mpaka ukubali cha dini yako ndipo tutaacha kuiteketeza familia yako na sasa bado wewe, mpaka tutainywa damu yako na usithubutu kuyasema mambo haya kwa watu!”
Walipoisikiliza vizuri sauti hiyo waliigundua ilikuwa ni sauti ya Isabella mama yake Anne, ni sauti hiyo ndiyo iliyomfanya Huggins aamini maneno aliyoyasikia kwa mke wako.
“Uchawi wa mama yako ndiyo umeua watoto wangu Frank na William?” alisema Huggins huku akimsogelea Anne.
Katika hali ya kushangaza ambayo Anne hakuitegemea kabisa alishtukia mumewe akimkaba na kuanza kumpiga vibao, ngumi na mateke bila huruma.
“Huggins kwanini unanipiga?”
“Utanieleza kwanini wewe na mama yako mmewaua watoto wangu!”
Anne alijaribu kadri ya uwezo wake kujitoa mikononi kwa Huggins lakini alishindwa kabisa, aliendelea kulia akiomba msaada wa majirani kwa sababu ya mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha hakuna jirani hata mmoja aliyeisikia sauti yake na kumfanya Huggins aendelee kutoa kipigo kwa mkewe bila huruma. Kilio cha Anne kiliwaamsha Nancy na Patrick na kuwafanya nao waanze kulia na kuzidisha kelele.
“Yaani uchawi wenu ndiyo umeua watoto wangu wapendwa? Wewe na mama yako mtawala watoto hawa nyama!” Huggins alisema kwa hasira.
“Siyo hivyo mume wangu ni mama pake yake, mimi nisingeweza kuwaua watoto niliowazaa mwenyewe! Niliwapenda mno Frank na William hata wewe unajua!
“Haiwezekani, umewatoa wanangu sadaka kwani mimi sijui wachawi mnavyofanya!”
Radi ilipiga kila mahali lakini Huggins hakuogopa, alitembea gizani huku mvua ikinyesha na kuyachukua machozi yote yaliyotiririka kutoka machoni pake, moyo wake uliuma mno!
****
Anne alibaki pake yake ndani akiwa amelala sakafuni hajiwezi kwa kipigo alichopewa, damu nyingi ilimtoka puani na kuilowanisha blauzi yake, Huggins alimuumiza sana na hakuamini kama ni yeye aliyemfanyia ukatili huo.
Hali ndani ya chumba chake ilitisha, giza lilitanda kila mahali sababu umeme ulikatika muda mfupi baada ya mvua kuanza kunyesha, kila wakati picha ya watoto wake wakining’inia darini ilipomwijia kichwani alipiga kelele kwa woga.
Baadaye ilimbidi anyanyuke na kupapasa mezani kwake ambako alichukua kiberiti akawasha mshumaa akachukua pamba ambazo alizitumia kuziba pua ili damu isiendelee kutoka zaidi, alipomaliza kazi hiyo aliuzima mshumaa kwa sababu hakutaka kuiona miili ya watoto wake ikining’inia darini.
****
Kama saa mbili hivi asubuhi Anne alisikia mlango wa mbele ya nyumba yake ukigongwa, alifikiri labda ni Huggins alikuwa amerudi kwa sababu tangu alipoondoka usiku wa manane mvua ikinyesha hakurudi tena.
Alinyanyuka na kujikongoja hadi mlangoni ambako alifungua mlango, tofauti na alivyofikiria mtu aliyekuwa mlangoni hakuwa Huggins bali akinamama wawili wa nyumba za jirani.
“Mama Patrick vipi tena mbona damu nyingi kiasi hiki zimechuruzika nje? Kuna nini humu ndani? Mmechinja mbuzi nini?” aliuliza mmoja wa majirani hao kwa utani.
Badala ya Anne kujibu swali hilo aliangua kilio! Kitendo hicho ndicho kilichowashtua majirani hao na kuwafanya waanze kudadisi.
“Mama Patrick nini? Hebu tueleze tafadhali? Una tatizo gani?”
“Ni mambo makubwa mno na sijui nianzie wapi kuyaeleza!”
“Nini?”
“Ingieni wenyewe humo ndani mkaangalie!”
Bila kusita majirani wale walimpita Anne pembeni na kuingia ndani walifuata michirizi ya damu hadi sebuleni hawakuona kitu!
“Mbona hatuoni kitu?” Mama Mariam alisema kwa sauti.
“Angalieni darini!” Anne alipaza sauti iliyochanganyika na kilio.
Kauli hiyo ya Anne iliwafanya majirani wale wanyanyue shingo zao kuangalia juu, alichosikia Anne kutoka ndani ya nyumba kilikuwa ni kilio huku akinamama hao wakikimbia kurudi nje, walimpita Anne na kusimama.
“Anne watoto wako wamepatwa na nini?”
“Nimewaeleza ni stori ndefu sana!”
“Na mumeo yupo wapi!”
“Aliondoka usiku kwenye safari!”
“Ni nini hasa kilichotokea mpaka watoto wakatundikwa darini?”
“Majambazi walituvamia” Anne alidanganya.
****
Hapakuwa na jambo la kufanya zaidi ya majirani kwenda kutoa taarifa polisi, kila mtu aliyeona miili hiyo darini alilazimika kumuuliza Anne juu ya kilichotokea lakini jibu lake lilikuwa majambazi.
Polisi walipokuja wakiambatana na daktari waliishusha miili ya Frank na William darini na kuibeba miili ya marehemu kwenda nayo Hospitali ya Sekotoure ambako ulifanyika upasuaji kuichunguza vizuri miili hiyo.
Baada ya kuchunguza kufanyika miili ilihifadhiwa chumba cha maiti wakati majibu yakisubiriwa, wazazi wa Huggins walishapata taarifa na walikuwa miongoni mwa watu waliofurika hospitali kutaka kujua ukweli.
Siku iliyofuata majibu yalitoka na yalionyesha kulichoua watoto kilikuwa ni kupasukakwa mishipa kichwani lakini kitaalamu haikuweleweka ni kitu gani kilichowapandisha darini ingawa Anne alielewa.
Baada ya majibu hayo majirani wakiongozwa na baba ya Huggins mzee Martin William waliruhusiwa kuchukua miili ya marehemu kwenda kuzika.
****
vifo vya Frank na William viliwachanganya akili sana wazazi wa Huggins, walishindwa kuamini kama ni majambazi kweli walioua watoto ila walilazimika kukubali kilichosemwa na Anne, walichukua Patrick na Nancy na kuwahamishia nyumbani kwao.
“Hivi baba yao yupo wapi?” mzee Martin aliuliza.
“Aliondoka usiku!
“Kwenda wapi?”
“Hakuniaga!”
“Hakukuaga kwanini? Je wakati anaondoka watoto walishafariki au la!”
“Walishafariki!”
“Sasa kwanini aliamua kuondoka?”
Anne alikosa jibu na kubaki kimya na baadaye aliangua kilio.
“Baba acheni kwanza kuniuliza maswali hivi sasa mimi bado nimechanganyikiwa!”
lilikuwa ni ombo la msingi na baba wa Huggins alielewa alikuwa amevuka mpaka kuuliza maswali kwa mtu aliyefiwa.
“Samahani sana mwanangu ni sababu ya uchungu!”
Baadaye Anne alihitajika kituo cha polisi kutoa maelezo juu ya tukio hilo bado msimamo wake uliendelea kuwa huo huo kuwa alivamiwa na majambazi usiku walikuja kulipa kisasi.
****
Mazishi hayakufanyika siku hiyo sababu Huggins hakuwepo na watu wote waliamini Huggins alikuwa safarini, ilibidi mazishi yaahirishwe hadi siku iliyofuata ambayo Anne alidanganya kuwa mume wake angeweza kurudi kutoka safarini.
Kulipokucha asubuhi watu walianza kukusanyika msibani, kijana mmoja aliwashangaza waombolezaji alipoleta taarifa kuwa alimwona Huggins asubuhi hiyo akiwa amefunga taulo kiunoni akipiga mswaki nyumbani kwa mwanamke mmoja aliyejishughulisha na biashara ya kuuza pombe za kienyeji aina ya gongo.
“Hakyanani nimemwona Huggins nyumbani kwa Delila!”
Alisisitiza kijana huyo.
“Nani labda umemfananisha!”
“Nina uhakika nimemwona kama hamuamini nendeni mkahakikishe!”
“Kweli?” baba yake Huggins mzee Martin aliuliza kwa mshangao ilibidi vijana watano wa mtaani waamriwe kwenda kuhakikisha, waliporudi dakika kumi na tano baadaye jibu lao liliwashangaza wazee na kuanza kuhisi vifo vya watoto wao havikuwa vya kawaida.
“Tumemkuta nyumbani akiwa amelewa vibaya mno, tukampa taarifa za vifo vya watoto wake lakini amekataa kuja!”
“Mna hakika mliyemwona kweli ni Huggins?” aliuliza baba yake na Huggins Mzee Martin.
“Ndiyo baba ni yeye!”
“Haya twendeni nikahakikishe mwenyewe sasa hivi!” Alisema mzee Martin na vijana kama ishirini hizi waliongozana nae hadi nyumbani kwa Delila, Huggins alipomwona baba yake alianza kulia.
“Mwanangu vipi?”
“Baba mke wangu na mama yake wamewaua watoto wangu!”
“Akinanan?”
“Mke wangu na mama yake!”
“Wamewauaje?”
“Kichawi na simtaki tena yule mwanamke ni mchawi nimemwambia awale nyama!”
“Mh! Huggins unayosema ni kweli?
“Ni kweli baba!”
“Siamini hata kidogo twende kwenye msiba wa watoto!”
“Baba niache tafadhali niache baba!” Huggins alikataa katakata pamoja na kubembelezwa na baba yake kwa masaa matatu!
****
Taarifa za kugoma kwa Huggins zilisambaa mioyoni mwa majirani ikabidi watu wengi wajae nyumbani kwa Delila wakijaribu kumshawishi Huggins akubali.
Taarifa hizo kuliwaudhi sana wakazi wa mtaa huo ambao mara nyingi walifiwa na watoto wao kimazingara na kujikuta wakimbebesha Anne lawama zote juu ya vifo vilivyotokea mtaani hapo, akimama waliokaa nae ndani walitoka nje na kumwacha chumbani peke yake na maiti mbili za watoto wake.
“Anajifanya mlokole kumbe ni mchawi!” Sauti hiyo ilimuumiza sana moyo Anne.
“Hatuwezi kuzika maiti ya mtu aliyeua watoto wake mwenyewe!” alisema kiongozi wa mtaa.
Maneno hayo yaliwafanya wananchi waanze kusambaa kurudi majumbani kwao baba na mama yake Huggins walishindwa kuondoka na kumwacha Anne peke yake na maiti.
“Mama hebu tueleze ukweli nini kimetokea?”
Anne aliendelea kulia machozi huku akizidi kuzikumbatia maiti za watoto wake zilizokuwa pembeni yake.
“Baba ninawapenda sana watoto wangu nisingewaua!”
“Sasa ni nini kimewaua?”
“Ni mama yangu, alitaka damu za wajukuu zake ili zikanywewe na wachawi wenzake siyo mimi wazazi wangu naonewa bure!”
Ilibidi Anne achukue sana kuwaeleza wazazi wa Huggins juu ya mzimu na jinsi ulivyorithiwa kutoka kwa mwanamke mmoja hadi mwingine na pia alieleza jinsi ambavyo mama yake alimlazimisha yeye kuacha Ukristo ili awe mrithi wake atakapokufa.
“Mwanangu kama ndio hivyo hatuwezi kukusaidia shauri yako, utabaki na miili ya watoto wako utawala nyama!” Alisema baba yake Huggins kwa hasira.
“Baba!” aliita Anne lakini mzee Martin hakujibu kitu alimnyanyua mke wake na wote walianza kutoka nje ya nyumba.
“Mama!” Anne aligeuka na kuanza kumwita mama yake Huggins lakini naye pia hakuitika wote walitoka nje na kuingia ndani ya gari lao na kuondoka, mbele walikatisha nyumbani kwa Delila na kumkuta mtoto wao akiwa amelewa chakali, Huggins alipomwona mama yake alianza kulia tena kwa uchungu akiita majina ya watoto wake.
“Mama, amewaua watoto wangu!”
“Pole sana mwanangu Mungu anayafahamu yote haya na atakupa faraja!”
walimbembeleza kuondoka naye lakini alikataa alichofanya ni kuwaomba wamtunzie watoto wake.
****
Mawingu yalikusanyika angani jioni ya siku ya jumapili baadaye mvua yenye radi kubwa ilianza kunyesha na kusababisha giza kila mahali, umeme ulikatika tena na kufanya kuwa kiza kabisa!
Katika hali kama hiyo Anne alikuwa ndani ya nyumba yake katikati ya maiti mbili za watoto wake katikati ya maiti mbili za watoto wake machozi ya uchungu yaliendelea kumbubujika, watu wote walishamkimbia mpaka wakati huo alikuwa haamini hata kidogo kama dunia ilikuwa imemgeukia kiasi kile, yote hayo kwa sababu ya mama yake, aliwatingisha watoto wake akifikiri yaliyotokea yalikuwa ndoto na labda wangeweza kurejewa na fahamu, ukweli haukubadilika.
Asubuhi siku iliyofuata pia hakuna mtu aliyefika nyumbani kwake, Anne aliendelea kukaa peke yake na maiti za watoto wake akilia, hakuna mtu aliyefika kumpa pole, alitamani Patrick na Nancy wangekuwepo kumfariji lakini bibi na babu yao waliwachukua!
Alikaa hivyo hivyo kwa siku ya nne na maiti zilianza kutoa harufu.
Je nini kitaendelea?
Je Anne ataweza kupigana vipi na hali hii tena akiwa peke yake?
Tags:
RIWAYA