TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 11------12


Saa 12:45 asubuhi ya siku ya Jumatano ikiwa tayari ni siku ya tano tangu Anne asusiwe watoto na majirani zake pamoja na ndugu wote baada ya kuaminika kuwa aliwaua mwenyewe kichawi, alikuwa ndani nyumba yake akilia, mume wake hakuwepo alimkimbia baada tu ya watoto wake kufariki katika mazingira ya kutatanisha.
“Hivi kweli Isabella ni mama yangu mzazi? Hivi ningekuwa mtoto wake kweli angenifanyia ukatili huu? Hapana si mama yangu na mimi nitamuua, ni lazima afe, kama siyo leo kesho na kama si kweli wiki ijayo lakini ni lazima Isabella afe tu!” Alisema Anne huku akilia.
Harufu ilisambaa mtaa mzima na kuwaghasi watu wengine, baadhi ya majirani walitamani kwenda kumsaidia Anne lakini waliogopa kwa kitisho walichokipata kutoka kwa uongozi wa mtaa kuwa yeyote ambaye angejitokeza na kwenda nyumbani kwa Anne kumsaidia pia angetengwa!
Kauli hiyo ilizidi kuwafanya majirani wote wabaki ndani ya nyumba zao kama vile hakukutokea kitu mtaani kwao. Taarifa za mateso hayo ya Anne ziliwafikia waumini wa kanisa la Praise And Worship ambalo Anne na Huggins walisali kabla ya kuasi na kuacha kwenda kanisani, habari hizo za Anne kufiwa ziliwasikitisha sana waumini wenzake.
Kuna hata waliolia kanisani habari hiyo ilipotangazwa, kanisa zima waliazimia kwenda kumsaidia Anne katika mateso yake.
“Pamoja na kwamba ameasi kuja kanisani lakini bado ni ndugu yetu tu katika bwana ni wengi waliasi na baadaye kurudi tena kanisani, ni lazima tumsaidie Anne!” Alisema mchungaji Aaron Mugabiro aliyekuwa kiongozi wa dhehebu hilo na waumini wote waliitikia Ameni!
Hawakutaka kupoteza muda taratibu zote ziliandaliwa, mabasi mawili yalikodishwa pamoja gari dogo aina ya Landcruiser pickup lililokuwa mali ya mmoja wa waumini yalipeleka waumini kwenda nyumbani kwa Anne!
Ukimya uliokuwepo nyumbani hapo wakati wanaingia uliwashangaza waumini wote hapakuwa na dalili yoyote ya kuwepo mtu, milango yote ya nyumba ilifungwa na hapakuwa na kelele yoyote, mchungaji aliteremka katika gari lake aina ya Musso na kwenda mlangoni kuanza kugonga lakini hakuna mtu aliyeitikia.
“Labda walisafirisha?”
“Hapana nilivyosikia mimi Anne alikuwepo hapa na maiti za watoto wake!” Alijibu muumini mwingine.
“Sasa atakuwa wapi?”
“Sifahamu!”
Karibu kila muumini aliyekuwepo mbele ya nyumba ya Anne aliziba pua yake, sababu ya harufu kali iliyokuwepo mahali pale, iliyowafanya waendelee kuamini ni lazima maiti za watoto wa Anne zilikuwemo ndani!
“Huyu huku nyumba!” Ilikuwa ni sauti ya mmoja wa waumii aliyezunguka nyuma ya nyumba waumini wote walitembea harakaharaka hadi nyuma ya nyumba wakiongozwa na mchungaji Aaron!
Anne alikuwepo nyuma akichimba shimo ardhini, shimo lilishafika kiunoni mwake na alikuwa akilia machozi, alitia huruma sana.
Anne alishajua kulikuwa na watu nyumba yake lakini hakuonyesha kujali, aliendelea kuchimba huku akilia machozi, alionekana kama mtu aliyekata tamaa kabisa, mchungaji alimfuata na kumgusa begani lakini hakugeuka, aliweka jembe lake chini na kukaa ndani ya shimo akilia.
“Mwanangu Anne unafanya nini hapa?” Mchungaji aliuliza.
“Ni..na…chi…mba…kaburi….la…watoto..wa..ngu!” Aliongea Anne huku kwikwi ya kulia imemkaba!
Jibu hilo la Anne liliwafanya waumini wote waliokuwepo waanze kulia na hata mchungaji Aaron alishindwa kuvumilia akamwaga machozi.
“Acha mwanangu nyanyuka na utoke shimoni, maombi yako Mungu ameyasikia!”
Anne alijitahidi na kusimama waumini wakamsaidia kutoka shimoni akasimama nje ya kaburi na kusadiwa kuingia ndani ya nyumba yake ambako harufu ilizidi na kuwafanya hata baadhi ya waumini kushindwa kuvumilia kakaa ndani ya kutoka nje!
Miili ya watoto wake ilikuwa imelazwa kitandani chumbani ikiwa imevimba na kuharibika vibaya, hakuna mtu aliyekuwa tayari kuamini kama binadamu wanaweza kufanya binadamu mwenzao kitendo cha kinyama kiasi kile!
“Huu si ubinadamu hata kidogo na kwanini hukuja kwetu kututaarifu?”
“Niliogopa!”
‘Uliogopa nini mwanangu?”
‘Nilijua msingenisaidia kabisa!”
“Kwanini?”
”Sababu niliacha kuja kanisani!”
Baadaye wakati waumini wengine waliondoka kwenda makaburini kuchimba makaburini, mchungaji alipata nafasi ya kumhoji Anne suala lililopelekea mpaka majirani zake wagome kuzika watoto wake! Annne alisimulia kila kitu mpaka kilichopelekea mume wake kukimbia nyumbani kwake na kuhamia nyumbani kwa kahaba, mchungaji alipigwa na butwaa!
“Kwa hiyo kila mtu anaamini kuwa wewe ndio umeshirikiana na mama yako kuwaua watoto wako siyo?”
“Ni kweli mchungaji lakini jambo hilo si kweli hata kidogo, ila mama yangu amefanya hivyo yeye peke yake, kama njia ya kunishinikiza mimi nikubali kurudi tena katika ushirikina kitu ambacho sipo tayari kukifanya ingawa hivi sasa nipo nje ya kanisa!”
“Unajua kwanini lakini mama yako amefanikiwa kuua watoto wako?”
“Hapana mchungaji!”
“Kwa sababu wewe na mumeo mliacha kumtumaini Mungu! Kwanini unafikiri hakulifanya hili siku za nyuma?”Anne alikaa kimya kwa sababu alijua kilichosemwa na mchungaji kilikuwa kweli tupu!
“Unasikia?”
”Nimekuelewa mchungaji!”
Baadaye watu waliokwenda makaburini kuchimba kaburi walirejea na kutoa taarifa kazi hiyo ilikuwa tayari, mchungaji na watu wengine kama watano hivi waliingia ndani wakiwa wamevaa mipira mikononi na kusafisha miili ya Frank na William ilikuwa ni kazi ngumu lakini ulikuwa ni wajibu wao.
Baada ya hapo kazi hiyo ibada fupi ilifanyika na miili ikachukuliwa kwenda makaburini kwa mazishi ambako mchungaji Aaron pia aliongoza ibada! Muda wote huo Anne alikuwa akilia, maisha yake tangu utotoni yalikuwa ni ya mateso mengi na kutengwa na jamii, hali iliyosababishwa na mama yake.
“Sasa tunamwomba mama wa marehemu hawa aje mbele aweke mchanga kama ishara ya kuwaaga wapendwa wake!”
Anne alishikwa mikono na akinamama wawili waliomwongoza hadi kaburini lakini kabla hajaweka mchanga alilegea na kuanguka chini, alikuwa amezimia, ilibidi ndoo ya maji iletwe haraka na kumwagia maji ili azinduke lakini haikuwa hivyo, ikabidi apakiwe katika gari na kurudishwa nyumbani akiacha mazishi yakiendelea, nyumbani pia alimwagiwa maji lakini hakuzinduka ikabidi achukuliwa na kupelekwa hospitali ya TMC iliyokuwa karibu na nyumbani kwao ambako alipewa matibabu ya kuzimia ikiwemo kuongezewa maji na kuzinduka masaa mawili baadaye.
Alipozinduka kwa mara ya kwanza alifikiria yupo makaburini, hakujua mara moja kuwa alikuwepo hospitali.
“Nipeni mchanga! Nipeni mchanga niwaage watoto wangu!” Watu wote waliokuwa karibu yake wakiwemo manesi walisikitishwa sana na kitendo hicho na walimhurumia sana Anne.
“Hapa ni wapi?” Aliuliza fahamu zilipomrudia kichwani.
“Hapa ni Hospitali ya TMC!”
“Nimekukuja hapa saa ngapi?”
“Ulizimia makaburini!”
“Kweli haya nirudisheni makaburini upesi!”
“Makaburini wameshatoka labda tukupeleke nyumbani!”
”Hapana nataka makaburini nataka niyaone makaburi ya watoto wangu!”
Mchungaji Aaron na waumini wengine waliokuwepo hospitali walijaribu kumshauri waende nyumbani kwanza lakini Anne alikataa na kuendelea kusisitiza apelekwe makaburini, hapakuwepo na njia ya kulikataa hilo ikabidi watoke hospitali na kumpakia hadi makaburini.
“Watoto wako tumewalaza kwenye kaburi hili!”
Anne alianguka juu ya kaburi hilo na kuanza kulia akiita majina ya watoto wake.
“Frank na William kweli mmekwenda? Kweli mmeniacha? Kwa sababu yenu mimi nitamuua mama yangu!”
“Acha Anne acha usiseme hivyo tafadhali mwachie Mungu kila kitu!”
“Mchungaji inauma sana!”
Walimnyanyua kutoka kaburini na kumwomba waondoke, Anne hakutaka kuendelea kukataa huku akilia alitembea hadi kwenye gari nakupanda, alikuwa amekonda sana sababu ya kulia na kutokula.
“Mchungaji sijui jinsi ya kukushukuru wema na waumini wa kanisa, Mungu atanilipia ila mmenisaidia katika wakati mgumu sana!”
****
Walipofika nyumbani walikuta waumini wengi wakiendelea na shughuli za msiba, wengine wakipika chakula na wengine wakipasua kuni na wanakwaya wakiimba nyimbo mbalimbali za kumsifu Mungu, ilikuwa ni faraja kubwa sana kwa Anne, majirani walikuwa wamemtenga walishangazwa sana na kitendo kile, wengi walipita na kuchungulia na kutokuamini kama hatimaye watoto wa Anne walikuwa wamezikwa, wao pia walishukuru kwa kitendo hicho kwani walikuwa na mateso makali sana ya harufu nyakazi za usiku.
****
Mchungaji Aaron na waumini wengine walikaa na Anne wiki moja wakimfariji siku ya nane nao walilazimika kumwaga ili warudi nyumbani kwao na kuendelea na shughuli zao, siku zote alizokaa nao zilikuwa za faraja kubwa kwa Anne mpaka wakati huo alishindwa kuelewa bila waumini hao mwisho wa tatizo lake lingekuwa nini? Ndiyo angezika halafu baadaye kingefuata nini, hakuwa na jibu la moja kwa moja.
Shukrani zake kwa mchungaji na waumini wengine wote zilikuwa kubwa mno na hakujua jinsi ya kuzielezea kwa maneno, asingependa sana Frank na William waendelee kuishi naye lakini isingewezekana ilikuwa ni lazima sasa apambane na maisha peke yake!
Katika siku zote waumini waliokaa kwake, hakuwahi kumwona Huggins akija nyumbani pale wale wazazi wake na watoto wake wawili Patrick na Nancy roho ilimuuma sana kujikuta katika hali hiyo, angependa kumbadilisha na kuirejesha tena katika wakati wa zamani alipokuwa na maisha bora lakini aliona kama ilikuwa si rahisi kabisa jambo hilo kutokea.
Hapakuwa na njia ya kuwazuia waumini wasiondoke, ilibidi waondoke na kumwacha Anne peke yake, nyumba kubwa aliyoishi ilimtisha sana na ilimfanya asikie ukiwa zaidi.
Siku hiyo alilala peke yake ndani na siku hiyo hiyo majira kama ya saa tisa hivi usiku alisikia dirisha la chumba alikokuwa amelala likigongwa alishtuka sana ana hakufahamu ni nani aliyekuwa akigonga usiku huo, baadaye alisikia sauti ya kiume ikiita dirishani, alipoisikiza vizuri sauti ile ilikuwa ni sauti ya Huggins, furaha kubwa ilimrejea moyoni na kujua kipenzi chake alikuwa amerejea kwake, hakutaka kuchelewa alisimama na kutembea hadi dirishani na kufungua.
Alipofungua alishangaa kukutana na sura ya mama yake! Mwili wake ulitetemeka alikataa kufungua dirisha lakini alishindwa
“Karibu mama!”
“Unamkaribisha nani? Na bado nimekwishachukua watoto wawili sasa nimebakiza kuwajia hao wawili ulionao ndio utaelewa kuwa mimi nimekasirika mpaka utakapokubali kuwa upande wangu ndipo nitakapokuacha, umeuniudhi sana!” Mama yake alisema maneno hayo kabla Anne hajajibu kitu alishtukia kitu kama maji yenye harufu kali yakimwangika kuingia ndani na kumlowanisha mwili mzima!
“Huo tayari ni mkosi watu watakuona kama mavi kuanzia leo!” Mama yake alisema na kupotelea katikati ya migomba.
Anne alirudi na kuanguka kitandani kwao na kuanza kulia alishindwa kuelewa ni kwanini mama yake alikuwa akimfanyia unyama ule!
“Watoto wangu hawaui nitawapeleka kwa mchungaji Aaron na halafu mimi nianze kazi ya kumtafuta mama hadi nimuue tu!”Asubuhi kulipokucha Anne alitoka ndani baada tu ya kunywa chai na kuanza kutembea kwenda nyumbani kwa wazazi wake na Huggins kabla hajafika alipita kwanza nyumbani kwa Delila kumwona Huggins!
Aligonga mlango na mlango ulifunguliwa na Huggins mwenyewe.
“Wewe mchawi umefuata nini hapa? Tokaa vinginevyo nitakua!” Alisema Huggins.
“Huggins wewe ni baba wa watoto wangu acha kusema maneno hayo!”
“Toka hapa kwanini umeua watoto wangu?”
“Sio mimi Huggins nimekwisha kueleza juu ya jambo hilo!”
Huggins alimwacha Anne mlangoni na kuingia ndani alipotoka alikuwa na panga mkononi na kuanza kumkimbiza Anne, watu waliokuwa wakiangalia walishangilia na kumzomea Anne! Kweli Anne aliamini mama yake alikuwa amempaka mkosi, kila alipopita watu walipishana nae hawakutaka akae karibu yao, harufu ya mwili wake haikuwa nzuri.
“NITAMUUA MAMA!” Alisema kwa sauti alipofika nyumbani kwa wakwe zake walishangaa kwa harufu aliyokuwa nayo. Siku iliypfuatia, akaamua kuwapeleka watoto wake kwa mchungaji Aaron.
Kwa mwaka mzima aliishi mbali na watoto wake na hakuona jambo lolote lililowapata Patrick na Nancy alimshukuru Mungu mama yake hakuja tena usiku.
****
Januari 23 saa tisa ya usiku ikiwa ni miezi miwili tangu watoto wake wafariki alizinduliwa usingizini na sauti ya mtu akiongea dirishani ilikuwa ni sauti ya mama yake.
“Kwa sababu umewaweka watoto wako kwa mchungaji sasa nitakupa adhabu nyingine, itabidi kila siku maisha yako yote!”
Dakika mbili tu tangu asikie sauti hiyo alishangaa kusikia nguo zake za ndani zikilowa damu ilikuwa ikitoka kama maji!
“Mungu wangu!” Alisema Anne kwa mshangao, hakuamini kama hali hiyo ingeendelea siku zote lakini alishangaa alipomaliza miezi sita ikivuja damu usiku na mchana wakati mwingine alilazimika hata kwenda kuongezewa damu na kupewa vidonge vya kuongezwa damu, nyumba yake ilijaa makopo ya vidonge vya Fero B’ alivyopewa hospitali kuongeza damu! Aliishi kwa mateso, inzi walimfuata kila alikokwenda, watu hawakumkaribia, kila mara alishindwa kukaa kitini sababu kila alipokaa alilowanisha kiti alichopewa katika daladala alisimama hata kama kulikuwa na viti.
Hakuweza kumudu kununua ‘Always’ badala yake akawa anatumia taulo lakini nazo zilioza pia, yalikuwa mateso makubwa sana kwa Anne alilia na kumwomba Mungu amsaidie, hasira ya kumuua mama yake ilipanda kila siku.
Je nini kitaendelea?


HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 12
MTUNZI: ERIC JAMES SHIGONGO
Anne alizidi kukimbia huku akilia machozi, Huggins alizidi kumfuata nyuma yake, akimpiga na ubapa wa panga! Watu wote walioshuhudia walizidi kupiga kelele wakishangilia kitendo kile na wengine walizomea!
Taarifa za Huggins kuhama nyumbani kwake na kutoshiriki katika mazishi ya watoto wake kwa kile kilichoaminika kuwa ni mkewe kuwatoa sadaka watoto wake mwenyewe wafe kichawi!
Wengi walimchukia Anne, hakuna mtu hata mmoja aliyekuwa tayari kumsaidia Anne akipigwa na Huggins, hata alipoangushwa chini na kuanza kuchaniwa nguo watu wote walishangilia na kupiga mayowe.
“Ua mchawi huyo! Ua mchawi huyo!” Wananchi walipiga kelele.
Huggins alizidi kushusha kipigo kwa Anne huku watu wakizidi kushangilia, mwisho kabisa Huggins alilinyanyua panga lake na kumkata nalo Anne begani, damu nyingi sana ilimtoka, watu walipoona kitendo kile waliogopa na kuanza kukimbia kuondoka eneo lile, baadaye Huggins naye aliondoka.
Anne alijitahidi akanyanyuka lakini alishindwa kwa sababu alikuwa nusu uchi, watu waliendelea kukusanyika wakimshangaa, baadhi ya akinamama walimhurumia lakini wengine walimlaani kwa kitendo chake cha kuwaua watoto.
Baaaye alishtukia akifunikwa na khanga mwili mzima! Alishangaa ni mtu gani mwenye huruma, alinyanyua uso kuangalia juu, aliitambua sura yake!
“Anne vipi?”Aliuliza
“Mume wangu kanipiga dada!”
“Kwanini?”
“Wewe ni nani na unaishi wapi hujayasikia yaliyonipata?”
“Mimi naitwa Victoria kama utakumbua tulisoma wote Ngaza!”
Aliposema hivyo kweli Anne alikumbuka msichana huyo alikuwa miongoni mwa wasichana waliosoma katika shule ya wasichana ya Ngaza, ila Anne alikuwa mbele yake, msichana yule alimsaidia Anne kusimama wima.
“Twende nikusindikize hospitali!”
“Lakini nilikuwa nakwenda ukweni kwangu kuwafuata watoto wangu, baba mkwe aliwachukua!”
“Hapana huwezi kwenda katika hali hii ya kuvuja damu twende kwanza polisi ukatoe taarifa kisha twende hospitali ukatibiwe, baada ya hapo ndipo utaweza kwenda ukweni kwako!”
“Twende tukatoe taarifa wapi?”
“Polisi!”
“Hapana Vicky siwezi kwenda polisi!”
“Kwanini?”
“Sitaki kumshitaki mume wangu, Huggins ni baba wa watoto wangu, akifungwa watoto wangu watakuja kuniuliza!”
“Mh!” Vicky aliguna.
“Kama ni hospitali twende lakini polisi sitakwenda, nisaidie kunifikisha basi!”
“Hospitali hawawezi kukutibu bila PF3!”
“Hilo nalifahamu lakini wee twende tu!”
Walianza kutembea taratibu kuelekea hospitali ambako pia hapakuwa mbali sana na mahali tukio hilo lilipotokea, watoto wengi waliwafuta nyuma wakati wakitembea na watu wengine wakubwa walizidi kuwashangaa.
****
“Binti kimetokea nini?”Daktari aliuliza.
“Nimeangukia kisu jikoni!”
“Pole sana na hayo majeraha usoni je?”
“Ni jengo la jiko limebomoka ndiyo likasababisha niangukie kisu!’
“Aisee pole tena!” Daktari alimpa pole Anne.
“Itabidi tukushone kiasi cha nyuzi zisizopungua kumi na tano, sababu umeumia sana, itakugharimu shilingi elfu kumi na tano na baada ya hapo tutakuandikia sindano za PPF tano na chanjo ya pepopunda sawa, kwa hiyo gharama na matibabu yote itakuwa shilingi eflu ishirini na moja na mia tano!”
“Daktari mie sina pesa kabisa!” Alisema Anne huku akilia.
“Mimi nitalipa!” Vicky alisema na palepale alianza kufungua mkoba wake kutoa pesa!
“Subiri kwanza basi utalipia pale dirishani kwa keshia!”
Baada ya kulipia Vicky alirudi kwenye benchi na kukaa akimsubiri Anne amalize kuhudumiwa muda wa dakika thelathini baadaye, Anne alitoka chumba cha upasuaji akiwa amefungwa bandeji kubwa begani! Alishachomwa tayari sindano za PPF na Pepopunda.
****
Walipotoka hospitali, Anne alimuomba Vicky waongozane kwenda ukweni kwake kuwachukua watoto, Vicky alikubali na walikwenda hadi nyumbani kwa mzee Martin.
Walipowasili nyumba ilikuwa kimya kama vile hapakuwa na watu, Anne aligonga na mlango ukafunguliwa na mama yake Huggins!
“Karibuni sana!”
“Ahsante shikamoo mama” wote wawili waliitikia na baada ya salamu wote waliingia ndani ambako walikaa vitini na muda mfupi mzee Martin aliungana nao na wote wakamwamkia!
“Vipi binti zangu?”
“Baba nimekuja kuwafuata watoto, hawatakiwi kabisa leo kulala hapa, najua kitakachowapata!” Alisema Anne akikumbuka kitisho kilichotolewa na mama yake.
“Nini kitawapata?”
“Watakufa?”
“Watakufa vipi?”
“Mama amesema anawafuata!”
“Sasa unataka kuwapeleka wapi kwenye usalama kuliko hapa nyumbani?”
“Nataka niwapeleke kwa mchungaji Aron akakae nao, leo mama anakuja kuwadhuru watoto wangu!”
“Hilo mwanangu haliwezekani, watoto hawaondoki hapa, baba yao amekataa kabisa!” mama yake Huggins aliweka mgomo.
“Hapana mama nipeni watoto wangu, niondoke nao!”
“Haiwezekani labda tumwite baba yao aje hapa umuombe!”
“Sitaki kuonana na Huggins kabisa, kwani ni yeye aliyenifanyia hivi!”
“Sawa na pole sana lakini sisi hatuwezi kuacha uondoke na watoto bila yeye kukubali!”
Wakati maongezi yakiendelea, Patrick na Nancy waliokuwa wakicheza chini walimfuata Anne na kusimama mbele yake! Ikabidi Anne awapakate miguuni pake, alijisikia vizuri kuwa na watoto wake tena! Hakutaka kabisa kutenganishwa nao! Aliwapenda na hakutaka wapatwe na matatizo yaliyosemwa na mama yake!
“Baba siwezi kuwaacha watoto wangu!” Alisema Anne huku akiwawekea watoto wake matiti mdomoni ili wanyonye! Watoto walionyesha furaha.
“Mimi naondoka!”
“Tafadhali waache watoto!” Baba yake Huggins alisema kwa sauti.
“Hapana baba ni lazima niondoke nao
Ulitokea mzozo mkubwa sana wa kunyang’anyana watoto hatimaye Anne alinyang’anywa Patrick na Nancy walilia kupita kiasi wakimlilia mama yao.
“Ondoka hapa vinginevyo nitakuitia polisi”
“Siondoki nipeni watoto wangu upesi!” alisema Anne huku akilia machozi.
“We binti!” Mzee Martin alimwita Vicky!”
“Naam mzee!”
“Hebu mwondoe huyu mchawi hapa sisi hatuwezi kumpa watoto akawaue, ondokeni kabla sijawaita wezi!”
Vicky aliogopa na kujikuta akimwomba Anne waondoke, Anne alikataa lakini Vicky alimbembeleza hatimaye alikubali na wote walianza kuondoka, watoto wakimlilia mama yao lakini mzee Martin na mkewe hawakujali walizidi kumfokea Anne kwa maneno machungu yaliyomuumiza moyo.
****
Kwa msaada wa Vicky huku akilia machozi Anne alikwenda hadi nyumbani kwake , baada ya kufika Vicky aliaga na kuondoka kwenda nyumbani kwake, aliishi kwenye majengo ya shule ya Isamilo ambako alifanya kazi kama mwalimu!
“Ahsante kwa msaada wako Vicky!” alisema Anne akitoa shukrani.
****
Saa tatu usiku Anne akiwa amelala kitandani kwake alisikia sauti ya watoto wakilia nje ya nyumba yake, alishituka zaidi kusikia mlango ukigongwa! Aliogopa kwenda kuufungua lakini baadaye aliposikia sauti ya watu wakiongea na kuitambua sauti ya mama mkwe wake alinyanyuka harakaharaka kwenda mlangoni.
Alisikiliza kwa muda na kugundua kweli waliokuwa nje walikuwa wakwe zake pamoja na watoto wake, ingawa aliogopa na hakujua kilichowaleta alifungua mlango, alishangaa kukuta Huggins na Delila pia wapo.
“Karibuni ndani!”
“Unamkaribisha nani ndani? Nani aingie nyumbani kwa mchawi” Delila alisema kwa nyodo.
“Jamani ingieni ndani!”
“Sisi ndani hatuingii, tangu umeondoka watoto wanalia tu na hawataki kula sijui umewaroga, sasa dawa ya mchawi ni kumpa mtoto alee! Tumekuletea watoto wako ili uwaue vizuri!”
Baada ya kusema hayo tu waliwabwaga watoto chini na kuondoka, Anne alimshukuru Mungu na alichofanya pale kikawa ni kuwachukua watoto wake na kuanza safari ya kwenda nyumbani kwa mchungaji.
Hapakuwa mbali sana ulikuwa kama umbali wa robo kilometa hivi, alipofika aligonga na kufunguliwa.
“Nimewaleta watoto wangu mkae nao hapa nyumbani!”
“Mchungaji na mke wake hawakutaka kuuliza kwanini bali waliwapokea watoto wale na kuagana na Anne, watoto walilia lakini hapakuwa na njia ilibidi wabaki kwa usalama wa maisha yao, Anne alikuwa na uhakika pale walikuwa salama kuliko nyumbani kwake.
Aliporudi nyumbani aliendelea kulia akimfikiria mama yake na jinsi alivyomtesa tangu utotoni! Alikosa raha ya maisha na thamani ya kuwa na mama mzazi.
Mpaka saa tisa ya usiku Anne alikuwa bado yupo macho, bila kupata hata lepe la usingizi, ghafla alishitukia kimbunga kikubwa nje na mwanga mkali ukafuata, alilifananisha tukio hilo na tukio la siku Frank au Henry, jina alilopewa na babu yake baada ya kuzaliwa na William walipokufa!
“Ahaa! Umejifanya mjanja siyo, umewahamisha watoto eh! Sasa ni kazi kwako! Nakuambia tangu sasa utalowanisha hizo nguo zako hadi mwisho wa uhai wako!”
Baada ya sauti hiyo tu, Anne alishitukia kitu kama maji mengi yakitoka sehemu zake za siri na nguo zake za ndani zililowa, alifikiri ni mkojo lakini hali ilipotulia na kuangalia vizuri aligundua haukuwa mkojo bali damu nzito iliyotiririka kushuka chini miguuni kwake!
“Hili ni pigo jingine lakini ni heri hali hii kuliko watoto wangu kufa na ugomvi wangu na mama hautakwisha mpaka nimwondoe duniani!” aliwaza Anne.
****
Asubuhi kulipokucha nguo zote alizovaa zililowa damu, damu iliyokuwa ikimtoka ilikuwa nyingi mno kiasi cha kushindwa kuvaa ‘pedi’ ili kuzuia isilowanishe nguo zake alilazimika kuchukua taulo ya kuogea na kulikunja akaivaa katika ya miguu yake lakini nalo muda mfupi tu lililowa!
Pamoja na shida hiyo Anne alijitahidi kutembea hadi nyumbani kwa Mchungaji kuwaangalia watoto wake, aliwakuta wakinyweshwa uji aliwabeba na kuanza kuwanyonyesha.
Walimweleza kila kitu kilichotokea usiku, kimbunga na mwanga mkali huku sauti za watu wakiwataka Nancy na Patrick, Anne alielewa kilichoendelea.
“Ilibidi mimi na mchungaji tuanze maombi ndipo hali ikatulia!” Mke wa mchungaji alisema.
*****
Hayo ndiyo yakawa maisha ya Anne kila siku ilikuwa ni lazima aende kwa mchungaji kuwanyonyesha watoto wake, damu iliendelea kumtoka kila siku, kila alikokwenda kwa sababu ya harufu alifuatwa na inzi wengi, harufu hiyo ilimfanya atengwe na watu, kila alipokaa watu walimkimbia!
“Aliishiwa damu mara tano katika kipindi cha miezi sita, safari zote alilazwa hospitali na kuongezwa damu chupa kadhaa! Madaktari walijaribu kumpa tiba lakini haikusaidia, ikabidi ajaribu tiba za jadi lakini nazo hazikusaidia, maisha yalimtesa na hakuona haja ya kuendelea kuishi alitamani kufa lakini aliwahurumia watoto wake Patrick na Nancy alijua bila yeye wangepata taabu kubwa maishani.
“NITAMUUA MAMA HAWEZI KUNITESA HIVI” Anne aliwaza na siku hiyohiyo alichukua kalamu na karatasi kumwandikia mama yake barua akimweleza kuwa aliamua kuuacha Ukristo na kurudi tena katika uchawi ili awe mrithi wa mzimu wa Lutego.
Mama yake alipoipokea barua hiyo alifurahi mno na kuisoma usiku mbele ya wanachama wenzake, walipiga makofi na kushangilia wakajua Anne alikuwa amenyooka.
“Hivyo nitakwenda mimi na wengine wawili na tutakwenda kama binadamu wa kawaida!”
“Lini?” wanachama wengine waliuliza!
“Kesho asubuhi!”
****
Ulikuwa mchana wa joto kali, Anne alikuwa amechoka sasa alidhamiria kumwondoa mama yake duniani! Hakuwa na kitu kingine cha kufanya, mateso aliyopata yalitosha kabisa hakutaka mengine zaidi, akiwa katika mawazo hayo ghafla alishitukia mlango wa nyumba yake ukigongwa, alikwenda moja kwa moja kufungua mlango, alikutana na sura ya mama yake na bibi vizee wengine wawili, alipowaangalia aliwafahamu walikuwa bibi vizee wa kijijini kwao.
Hasira ilimkaba Anne kooni lakini hakutaka kuionyesha, aliazimia kuwaua wote watatu
****
Anne alikuwa akitetemeka kwa hasira, tayari alishamchoma mama yake kwa kisu kifuani tena kwenye titi la mkono wa kushoto na alipohakikisha kuwa amekufa alikichomoa na kutembea hadi chumba cha pili ambako bibi kizee mwingine muumini wa Ushirikina aliyeongozana na mama yake alilala, huko nako aliikamilisha kazi yake kwa kukizamisha kisu kilekile kifuani kwa bibi yule naye akaaga dunia.
Alikuwa amebakiza mtu mmoja tu ili alikamilishe zoezi zima, bibi kizee wa tatu aliyelala katika chumba kilichokuwa mkono wa kulia pembeni mwa chumba chake cha kulala, ni huyo ndiye aliyekuwa amesimama mbele yake!
Tofauti na mama yake pamoja na bibi kizee mwingine aliyekwishawaua, bibi kizee huyo alikuwa macho amesimama katikati ya chumba huku tunguli mbili kubwa zikiwa mikononi mwake! Anne alitetemeka hali iliyokuwepo ilikuwa ni tofauti kabisa na picha aliyoitegemea, kwa hasira aliyokuwa nayo moyoni hakusita wala kuiruhusu hofu imtawale.
“Nakuua! Amini usiamini wewe bibi kizee pamoja na uchawi wako mimi nakuua uwafuate wenzako kwanini mmenitesa kiasi hiki?”
“Mimi huwezi kuniua, utajiua mwenyewe tu!”
“Nakuambia wazi utakufa!”
“Huwezi na jaribu uone!”
Akiwa na hasira kali na uchungu pamoja na nia ya kuua ambayo hakutaka kabisa izuiliwe, Anne aliruka juu huku kisu chake chenye ncha kali kikiwa mkononi, lengo lake likiwa kumchoma bibi kizee shingoni lakini kabla hajamfikia bibi alizirusha tunguli zake juu na zilipodondoka chini zilipasuka!
Moshi mkubwa ulikifunika chumba na kumfanya Anne ashindwe kuona mbele baadaye mwanga mkubwa ulimulika kila kona ya chumba, Anne aliona kitu kama moto ukiwaka chumbani lakini cha kushangaza hakuhisi maumivu wala kuungua.
Anne aliendelea kuzunguka chumbani akimtafuta bibi kizee lakini hakufanikiwa kumpata sehemu yoyote ya chumba! Ghafla alihisi kuanza kulewa na kupoteza fahamu na hatimaye akajikuta akianguka sakafuni, hakuelewa tena kilichoendelea na alipozinduka alishangaa kujikuta akiwa amelala nje ya nyumba yake akiwa uchi wa mnyama! Alishindwa kuelewa nini kilitokea mpaka akajikuta nje!
Je nini kitaendelea?
Je Anne ataweza kuwaua wengine?
Je watoto wake watabaki salama?
 

Post a Comment

Previous Post Next Post