Ilikuwa ni saa kumi na mbili kasorobo na hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa ameingia ndani ya nyumba ya Anne asubuhi ile, alichofanya baada ya kuzinduka ni kukiokota kisu chake kilichokuwa pembeni na kujikongoja taratibu kuingia ndani ambako alizunguka akamtafuta bibi kizee yule lakini hakumuona mahali popote! Alishindwa kuelewa mahali alipokuwa lakini alihisi ni lazima aliondoka kichawi.
Alipoingia katika chumba alicholala mama yake aliikuta maiti ikiwa imelala sakafuni ikiwa imezungukwa na damu nyingi iliyoganda, huruma ilimshika Anne! Alikuwa amemuua mama yake aliyemzaa.
“Shauri yake si alinianza mwenyewe, kanitesa sana!” Alisema Anne kwa hasira huku akilia alijua wazi alilolifanya lilikuwa kosa.
“Sikuwa tayari Nancy na Patrick wafe halafu mama aendelee kuishi! Ni heri mimi niendelee kuteseka na hii damu mpaka mwisho wa maisha yangu lakini mama afe na sijutii nilichokifanya!” Aliendelea kusema peke yake Anne.
Ghafla kumbukumbu za tangu utoto wake zilimwijia, alikumbuka jinsi mama yake alivyompenda, alishindwa kuelewa ni kitu gani kilitokea kiasi cha kumfanya mama yake ampe mateso makubwa kiasi kile!Yaliyompata shuleni yalimuumiza zaidi moyo wake, alipokumbuka kifo cha Dio mvulana wa kwanza kumpenda hasira yake ilizidi kumpanda zaidi.
“Kwa kweli aliyonifanyia mama ulistahili kifo! Hakuna mtu angeweza” Alipaza sauti Anne.
Alitoka chumbani na kwenda moja kwa moja hadi chumba alicholala bibi kizee mwingine aliyemuua, hakuamini alipokuta maiti ya bibi kizee aliyemuua haipo! Alishindwa kuelewa ilikuwa wapi na ghafla alisikia sauti ikitoka darini lakini hakumuona mtu aliyekuwa akiongea, ilikuwa sauti nzito na ya kutisha.
“Tunakuachia mzoga wa mama yako sisi tunaondoka zetu! Usingeweza kutuua kwani sisi si damu yako!”
Baada ya sauti hiyo Anne alishuhudia kimbunga kikubwa kikiitingisha nyumba yake na paa la juu ya chumba alichokuwa amesimama liliezuliwa mabati kama matano yakatupwa pembeni Anne akauona mwanga kutoka nje.
“Bahati yao!” Anne alitamka akijua bibi vizee wengine walikuwa wameondoka kichawi.
Anne alikuwa amebaki na maiti ya mama yake, alianza kufikiria ni kitu gani angefanya na maiti hiyo na alikuwa na uhakika kabisa hapakuwa na mtu yeyote aliyefahamu nini kilichotokea ndani ya nyumba yake na hakutaka mtu yeyote aelewe.
Alijua wazi kuwa hakuna mtu angekuwa kumsaidia kuzika mwili wa mama yake na alijua ni lazima watu wangehoji kilichomuua, akili ilimzunguka kichwani kwani hakutaka kubaki na maiti ndani kama ilivyotokea kwa watoto wake.
“Nafunga mlango na ninatoka kwenda kwa mchungaji Aaron kuwanyonyesha watoto wangu, simwambii mtu yeyote juu ya jambo hili, nikirudi usiku nitaibeba maiti kwenda kuitupa barabarani halafu nitatangaza mama yangu amepotea!” aliwaza Anne.
Alichofanya baada ya mawazo hayo ni kuingia ndani ya nyumba yake na kuvaa nguo safi, akachukua taulo nyingine nzito akaikunja na kuvaa katikati ya miguu yake ili kuzuia damu iliyokuwa ikitoka isimchafue zaidi.
**********
Ali funga mlango wa nyumba yake na kuondoka taratibu kwenda nyumbani kwa mchungaji Aaron kunyonyesha watoto wake ndani ya moyo wake alijawa na huzuni, moyo wake ulikuwa mzito kupita kiasi kwa sababu ulibeba siri kubwa ya mauaji.
Pamoja na kuua na maiti kuwa ndani Anne alikuwa ameamua kuonyesha ushujaa, hakutaka kuonyesha dalili yoyote juu ya mauaji aliyoyafanya.
“Anne, una matatizo gani leo?” Mke wa mchungaji alimuuliza Anne baada ya kugundua tofauti katika tabia yake.
“Hapana mama mchungaji najisikia kichwa kinauma sana, nafikiri ni sababu ya mawazo!”
“Mh! Lakini nahisi kuna tatizo linalokusumbua!”
“Hapana mama na lingekuwepo lazima ningekueleza!”
Muda wote akiwanyonyesha watoto wake mawazo yake yalikuwa chumbani ilipolala maiti ya mama yake ni hicho ndicho kilifanya mke wa mchungaji agundue! Alipomaliza kuwanyonyesha watoto aliwakabidhi kwa mama mchungaji akawabusu usoni na kuaga kurudi nyumbani kwake.
Njiani wazo jipya lilimwijia, hakuelewa wazo hilo lilianzia wapi, ghafla alijikuta akitamani kupita nyumbani kwa Delila ili aonane na Huggins! Aliogopa kwenda alipoyakumbuka mambo aliyofanyiwa na Huggins mara ya mwisho, kwa sababu moyoni mwake bado alijisikia kumpenda Huggins alijipa moyo na kuamua kupita tena ingawa moyo wake ulijaa hofu.
Alijipa moyo na kuanza kutembea kuelekea nyumbani kwa Delila lakini alipokaribia akiwa umbali kama wa mita mia moja na hamsini alishangazwa na umati wa watu uliokuwepo, kulikuwa na magari mengi sana yaliyoegeshwa mbele ya nyumba ya Delila!
Alipoangalia vizuri alilitambua gari la baba yake na Huggins! Moyo uliruka ghafla na ghafla aliona wanawake wengi wakijishughulisha na kusomba maji huku wengine wakipasua kuni.
Anne alishindwa kuelewa kilichokuwa kimetokea nyumbani kwa Delila mpaka kuwa na idadi kubwa kiasi kile ya watu, wazo lililomwijia kwanza kichwani mwake lilikuwa ni harusi! Alihisi uwezekano wa Huggins kufunga ndoa na Delila kama njia ya kumkomoa na kumuumiza moyo.
Alijaribu kusikiliza sauti ya muziki ambayo aliamini ingekuwa ishara ya harusi hakusikia lakini alipotulia zaidi alisikia sauti ya vilio vya watu! Moyo wake ulishituka ikabidi asogee karibu zaidi.
Aliposimama katikati ya uwanja wa nyumba ya Delila kilio kiliongezeka, watu walizidi kulia kuliko hata mwanzo, maneno yenye kumuumiza yalitamkwa katikati ya vilio vya akina mama na alilisikia jina lake likitajwa akilalamikiwa kusababisha kifo cha Huggins.
“Bila Anne kuwaua watoto wake Huggins asingeondoka nyumbani kwake kuja kwa huyu malaya na hivyo asingekufa!”
Maneno hayo yalizidi kumchanganya akili Anne na alishindwa kuamini kama Huggins alikuwa amekufa! Afe vipi wakati alionekana mzima siku aliyomkimbiza na kumkata panga!
“Haiwezekani! Huggins haweza kufa” alisema Anne akitembea kuelekea jikoni walikokuwa akina mama wengi alipowakaribia alishangaa kuona wanawake wote wakianza kusambaa na wengine kumkimbia, Anne alijisikia vibaya.
Anne alikumbuka kilichokuwa kikiendelea watu waliogopa kuongea naye sababu ya vitu viwili, cha kwanza ni amri iliyotolewa na uongozi wa mtaa lakini cha pili kilikuwa ni mkosi aliomwagiwa na mama yake dirishani mara tu baada ya mazishi ya watoto wake!
Alijaribu kuwasogelea akinamama lakini walizidi kumkimbia, kabla hajaondoka eneo hilo vijana watatu walimfuata wakamkatama na kuanza kumvuta kwa nguvu kumwondoa nyumbani pale.
“Jamani mnieleze tu kimetokea nini?”
“Mumeo Huggins amekufa!”
“Haiwezekani amekufa vipi mume wangu wakati alikuwa mzima?”
“Amenyweshwa sumu na Delila inaaminika alikuwa akimpa dawa ya mapenzi, hakujua kumbe ilikuwa sumu hivi sasa Delila ametoroka!”
“Sasa kwanini mnanitoa kwenye msiba wa mume wangu?”
“Haiwezekani wazee wamesema hawataki kukuona msibani sababu wewe ni mchawi!” Vijana wale walipomfikisha barabarani tu walimwacha na kuondoka zao kurudi nyumbani kwa Delila
Anne alilala barabarani akilia alikuwa akimlilia Huggins, alimpenda na aliamini ni matatizo yake Anne ndiyo yaliyochangia sana kifo cha mumewe, alimlaumu mama yake kwa kila kitu.
“Tena afadhali nimemuua !” alisema Anne huku akisimama, machozi yalikuwa yakimmwagika mfululizo.
****
Muda mfupi baadaye akiwa amesimama barabarani alishuhudia sanduku likibebwa na kuingizwa katika moja ya magari, watu wengi walipanda kwenye magari na msafara mrefu ulianza kuondoka nyumbani kwa Delila.
Ilivyoonekana ndugu wa Huggins walikwenda nyumbani kwa Delila kuichukua maiti ya Huggins kuirudisha nyumbani kwa baba yake kwa ajili ya mazishi!
Gari lenye jeneza lilipopita karibu yake Anne alianza kulikimbilia jambo hilo lilionyesha ni kiasi gani Anne alimpenda mumewe pamoja na kutengana! Baadhi ya akina mama ndani ya gari walimuonea huruma na kumwomba dereva asimamishe gari ili Anne apande lakini dereva alikataa na kuendelea na safari, Anne aliendelea kulifukuza gari hilo bila kuchoka.
“Hivi huyu dada ni kichaa?” Aliuliza mmoja wa wanawake aliyekuwa ndani ya moja ya magari.
“Kichaa? Hapana huyu ni mke wa marehemu!”
“Sasa ni kwanini hapandi kwenye gari badala yake anakimbia kwa miguu?”
“ Ametengwa na kijiji baada ya kuua watoto wake wawili na ni yeye anayedaiwa kusababisha Huggins afe, wazazi wa marehemu hawataki hata kumwona kwenye mazishi!”
Mbele zaidi Anne alichoka na kuanguka chini, magari yalipita yakimwacha amelala chini, hakuna aliyeonyesha kumjali baadaye alinyanyuka na kuanza kutembea taratibu kuelekea nyumbani kwao na Huggins, alipania kuhudhuria mazishi ingawa alijua asingeruhusiwa.
Alipofika nyumbani kwao na Huggins alishangaa kukuta hakuna gari hata moja, ikabidi awaulize watu waliokuwepo na kuambiwa mwili wa Huggins ulisafirishwa kwenda Musoma kwa mazishi, Anne aliishiwa nguvu na kukaa chini na kuendelea kulia, hakuliona kosa lake mpaka azuiliwe kuuona mwili wa marehemu mume wake mara ya mwisho!Kwa mara nyingine tena alimlaumua marehemu mama yake.
****
Alifika nyumbani kwake saa nne ya usiku akiwa na wazo moja tu la kuuchukua mwili wa marehemu mama yake na kwenda kuutupa njia panda ili kupoteza ushahidi kuwa ni yeye aliyefanya mauaji!
Je nini kitaendelea?
Tukutane siku ya Jumamosi mahali hapa
HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 14
MTUNZI: ERIC JAMES SHIGONGO
Ilikuwa ni siku ya Februari 14, Siku ya Wapendano au Valentine Day kama ilivyojulikana na watu wengi, siku ambayo kabla ya Anne na Huggins kuingia katika migogoro yao ya ndoa, walisherehekea kushinda hata walivyofanya kwa Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya.
Ni siku waliyoonyeshana upendo mkubwa sana kati yao, walikwenda sehemu ambayo hawakuwahi kufika kabla na kula chakula pamoja, kucheza muziki na walipigana mabusu mbele ya watoto wao, ilikuwa ni siku nzuri na ya furaha kwa familia yao.
Valentine ya siku hiyo ilikuwa tofauti sana na miaka ya nyuma, Huggins hakuwepo tena na si kuwepo nyumbani tu bali alikuwa amekufa, watoto wake wawili Frank na William nao pia walikuwa kaburini na Patrick na Nancy watoto wake waliobaki aliwahifadhi kwa mchungaji Aaron ili kuwaepusha na nguvu za kichawi.
Anne alikuwa peke yake ndani ya nyumba kubwa ambayo awali aliishi na familia yake yenye furaha, ukubwa wa nyumba yake ndiyo uliifanya itishe zaidi na ilikuwa kimya, alitamani hali ingekuwa tofauti.
Alikuwa amekaa mbele ya maiti ya mama yake mzazi akilia machozi, maisha yake yalikuwa yamebadilika tena na kumrudisha alikotokea, kwenye maumivu na mateso makali ya maisha, yote hayo kwa sababu ya mama yake.
Anne alimlaumu mama yake aliyekuwa amemuua kwa mkono wake mwenyewe kwa yote yaliyotokea, kila alipoiona maiti ya mama yake mbele yake hasira ilizidi kuongezeka, alitamani achukue tena kisu achome mama yake ingawa tayari alishakufa, alihisi akili yake haikuwa sawa, alihisi kuchanganyikiwa na kuwa mwehu!
“Ni lazima nitoe hii maiti hapa ndani nikaitupe barabarani, baadaye nitoe taarifa polisi nikijifanya mama yangu amepotea, polisi wakimtafuta lazima wataikuta maiti yake imetupwa hapo kila mtu ataamini mama ameuawa na majambazi!” Alisema Anne moyoni mwake.
Moyoni mwake aliogopa na alihisi kutetemeka mwili lakini pamoja na hali hiyo hakuwa na la kufanya ili kujiepushia matatizo ilikuwa ni lazima aiondoe maiti ya mama yake ndani.
“Vinginevyo kama ikikutwa humu ndani mambo yataniharibikia!” Aliwaza Anna.
Alipoangalia saa yake ya ukutani ilimwonyesha tayari ilikuwa saa tano kasoro dakika kumi na sita! Anne alinyanyuka na kutembea kinyonge hadi chumbani kwake ambako aliwasha taa na kuchukua suruali na koti jeusi lililotumiwa na marehemu mume wake, Huggins na kuvaa wakati akitoka chumbani alipitia kofia kubwa nyeusi iliyokuwa ukutani nayo pia akaivaa, alisimama mbele ya kioo na kugundua ni kiasi gani alikuwa amebadilika.
“I’m going for the last mission!”(ninakwenda kwa shughuli ya mwisho) Alijisemea mwenyewe moyoni mwake.
Alinyoosha moja kwa moja hadi chumbani ilikokuwa maiti ya mama yake mama yake alikuwa mnene sana na Anne alijua maiti yake ingekuwa nzito lakini hakuhitaji msaada wa mtu mwingine, alijipa moyo na bila kujua zilikotokea nguvu nyingi mwilini mwake aliunyanyua mwili wa mama yake na kuuweka begani, akatoka nao nje ya nyumba yake ambako aliuweka chini na kukimbia nje kuangalia usalama kwani hakutaka mtu yeyote hasa majirani waigundue kazi aliyokuwa akiifanya usiku huo.
Alipohakikisha hapakuwa na mtu yeyote akipita Anne alirudi mbio hadi uwani ambako aliubeba mwili wa mama yake begani kwa mara nyingine na kuanza kutoka nao nje, ambako aliingia katikati ya migomba na kuanza kutembea kuelekea darajani, hakutaka kutumia barabara kwa kuhofia angeweza kukutana na watu ambao wangetaka kujua nini alichobeba.
Usiku ulikuwa wa giza nene na manyunyu ya mvua yaliendelea kudondoka taratibu, siku hiyo ya Valentine ilionekana ya kutisha sana lakini Anne hakuogopa alikuwa ameamua kutimiza kazi yake kikamilifu.
Kutoka nyumbani kwake hadi darajani ulikuwa umbali wa mita kama mia tatu hivi, ulikuwa ni umbali mrefu sana kwa uzito wa mzigo ambao Anne alikuwa nao begani kwake ukizingatia alikuwa msichana, kwa mara mbili mfululizo alilazimika kuishusha chini maiti ya mama yake alipolemewa sana na uzito.
Ghafla alishtukia radi ya ajabu ikianza kupiga katikati ya migomba, mwanga mkali ulionekana kila sehemu aliyopita, alijua ni nini kilitaka kutokea! Ni wazi ulikuwa uchawi wa mzimu wa Lutego, Anne aliogopa sana na kujikuta akishindwa kuendelea na safari yake na kuitupa maiti ya mama yake chini.
Alianza kukimbia haraka kurudi alikotokea sauti nene na nzito ilimfuata nyuma yake, ilikuwa ni kama sauti ya binadamu lakini hakuwa binadamu wa kawaida!
“Umemuua Malkia wetu ni lazima na wewe ufe, tena kifo cha mateso!” Iliendelea kusema sauti hiyo na kumtisha zaidi Anne.
Radi ilizidi kupiga na muungurumo uliongezeka ghafla mvua kubwa tena ya mawe iliyoambatana na upepo ilianza kunyesha, Anne alishindwa kuelewa mvua ile ilitokea wapi kwa sababu hapakuwa na mawingu mazito na makubwa jioni ya siku hiyo, hakuwa na uhakika wa kufika salama nyumbani kwake.
“Ni heri mniue mimi niliyewakosea kuliko kuwaua watoto wangu wasio na hatia!” Alipiga kelele Anne huku akikimbia katikati ya migomba, mawazo yake yote yakiwa kwa watoto wake, alijua ni lazima naye angekufa kabla ya kufika nyumbani, alijua yote yaliyokuwa yakitokea yalifanywa na bibi vizee waliotoroka mauaji yake.
****
Gongo ilikuwa ni pombe haramu na ilipigwa vita kila siku iliyokwenda kwa Mungu, lakini pamoja na vita hiyo bado watu waliendelea kuitumia, ilionekana kama hapakuwa na njia yoyote ya kuwafanya wananchi wasinywe pombe hiyo.
Bernard au Bernie Killer kama alivyojulikana na wengi maeneo ya Isamilo mjini Mwanza alikuwa ndiye mpikaji maarufu wa pombe hiyo na alishafungwa mara mbili mfululizo kwa kosa la kujishughulisha na pombe haramu ya gongo lakini hata alipotoka gerezani hakukoma, bado aliendelea kupika gongo kazi iliyomfanya aishi na hata kusomesha watoto wake!
Alifanya kazi hiyo usiku wa manane wakati watu wote wamelala, alifanya hivyo ili kujiepusha na maaskari na alifanyia katikati ya migomba, alifanya kazi hiyo yeye na mke wake pamoja na vijana wengine wanne waliowaajiri.
Usiku wa siku hiyo ya Valentine, Bernard na mke wake pamoja na wafanyakazi wao walikuwa katikati ya migomba wakiendelea na kazi ya kupika gongo, walishangaa kuona mtu aliyevaa nguo nyeusi akitokea upande wa kulia katikati ya migomba! Wote walishtuka na kufikiri labda ni polisi waliokuwa katika msako wa wapika gongo, waliingiwa na hofu na kulala chini pembeni ya mtambo wao.
Mtu huyo alionekana amebeba kitu mabegani kwake na alipita eneo walilokuwa bila kufanikiwa kuwaona, mbele aliutupa mzigo huo chini na kuanza kukimbia kurudi alikotoka na hapo hapo mvua kubwa ilianza kunyesha na radi ilitanda kila mahali, hali ilibadilika ghafla.
“Sijui ametupa nini?”Bernard alimwambia mke wake.
“Hata mimi sijui, isije kuwa ni pesa?”
“Acha nikaangalie, vijana twendeni lisije kuwa bomu halafu linilipukie peke yangu!” Alisema Bernard huku akiwaita vibarua wake na wote waliongozana kwenda mahali ulipotupwa mzigo ule.
“Mh! Huyu siyo mtu kweli?” Alisema Bernard!
“Tumfunue mzee!”
“Mfunueni!” Bernad aliwaruhusu vijana wake na kweli walifunua mwili ule na Bernard akaumulika kwa tochi.
“Masikini huyu si ni mama yake na yule jirani yetu Anne, tena alikuja juzi tu kuhani msiba wake kimempata nini?” Alisema Bernard kwa sauti ya chinichini!
“Ni yeye kweli au umemfananisha!”
“Ni yeye namfahamu vizuri sana huyu mama ni mama mkwe wake na marehemu Huggins aliyefariki jana!”
“Sasa tufanye nini?”
“Hata mimi sijui ila najaribu kufikiria ni nani aliyemtupa hapa?” Alizidi kuuliza Bernard na baadaye kuanza kumulika pembeni ni huko ndiko alikokiona kiatu kimoja!
“Mh! Hiki kiatu mbona ni cha Anne? Ina maana Anne ndiye ametupa maiti ya mama yake hapa, haiwezekani hii ni njama ya kumwigiza matatani binti wa watu, hebu tufungashe vifaa vyetu tuondoke eneo hili tayari limekwishaingiwa na gundu polisi wanaweza kufika hapa wakati wowote!”
Walianza kufungua mitambo yao na kuifunga tayari kwa kuondoka kila mmoja wao alikuwa na hofu, lilikuwa tukio la kwanza katika historia ya kazi yao ya kupika gongo waliyoifanya kwa miaka kumi na tano.
Kabla hawajaanza kuondoka eneo hilo walishtukia mtu akitokea katikati ya migomba huku akinyata, mtu huyo alikuwa na tochi yenye mwanga mkali mkononi mwake na alimulika kila mahali kuzunguka eneo ilipolala maiti.
“Huyu si ndiye aliyekimbia au?” Alionong’ona Bernard akiongea na mmoja wa wafanyakazi wake.
“Ni yeye alivaa nguo nyeusi hivihivi!”
“Hebu tulieni mimi nimchunguze vizuri ni nani hasa?” Alisema Bernard na kuweka mizigo yake chini, akaanza kutembea kwa tumbo kuelekea nyuma ya mahali ilipolala maiti.
“Masikini sijui kile kiatu kipo wapi jamani, kitaniponza ni lazima watajua ni mimi ndiye nimemuua mama!” Alisikika akisema mtu huyo, Bernard aliitambua sauti ile, haikuwa sauti ngeni masikioni mwake ingawa hakuweza kuitambua mara moja ni ya nani.
“Hiki hapa!! Yes, afadhali, kisingepatikana ningefanya nini mie?” Sauti ile ilimfikia tena Bernard na kumpa jibu la uhakika, ilikuwa ni sauti ya Anne asilimia mia moja.
Bila kugundua kuwa palikuwa na mtu akimchunguza Anne alianza kutimua mbio kwa kutumia tochi yake na kutokomea katikati ya migomba na kupotea.
“Ni Anne amemuua mama yake!” Alisema Bernard mwili wake ukitetemeka.
“Nani?” Mkewe aliuliza kwa mshangao.
“Ni Anne!”
“Kweli?”
“Ndiyo na ni lazima suala hili niitaarifu polisi!” Alisema Bernard!
*****
Alipofika nyumbani kwake Anne aliingia moja kwa moja hadi ndani na kujitupa kitandani, nguo zake zote zililowa na maji lakini hakujali, alianguka hivyo hivyo na kuyalowanisha mashuka yote alikuwa amechoka kupita kiasi, kazi aliyokuwa amefanya ilikuwa ngumu sana.
Aliendelea kuwa na uhakika hapakuwa mtu aliyemwona akitimiza azma yake, aliamini zoezi zima lilikuwa limekwenda kama alivyopanga! Kilichokuwa kimebaki mbele yake wakati huo ni kwenda kituo cha polisi na kutoa taarifa juu ya kupotea kwa mama yake mzazi.
Hakutaka kupoteza muda zaidi, bila kuchelewa ingawa ilikuwa ni usiku wa manane alitoka na kuanza kutembea akielekea kituo cha polisi, Anne hakuogopa kitu kwani ilikuwa ni lazima atoe taarifa polisi ili kuficha ukweli wa tukio zima.
Alipofika kituoni kabla hajaingia ndani, mlangoni alikutana na Bernard aliyeshuhudia Anne akilia na machozi.
“Vipi jirani?”Bernard aliuliza.
“Mama yangu amepotea tangu jana na nimemtafuta bila mafanikio au umemwona mahali?”
“Hapana sijamwona, pole sana kwa hiyo umekuja kutoa taarifa siyo?” Alisema Bernard ingawa alifahamu kila kitu na alishatoa taarifa polisi!
“Ndiyo!”
“Sawa basi mimi naondoka polisi watakusaidia!”
Alipoingia ndani kabla hajasema kitu chochote Anne alishtukia anapigwa pingu mikononi.
“Vipi jamani mbona mnanifunga pingu?”
“Muuaji mkubwa wee!”
“Nimemuua nani?”
“Umemuua mama yako halafu unajifanya mjanja!” Alisema Askari na kumpiga Anne kwa rungu kichwani damu ilianza kumtoka.
“Mimi nimemuua mama yangu kwa makosa gani?”
Alizidi kujitetea Anne lakini hakuna mtu aliyemsikiliza.
“Mpakieni ndani ya gari mwende naye nyumbani kwake mkapekue haraka!” Mkuu wa kituo aliamuru na Anne alianza kuvutwa na kutupwa ndani ya gari, Anne alishindwa kuelewa ni nani aliiitoa taarifa hiyo polisi, aliamini kwa hali ilivyokuwa ndani ya nyumba yake hapakuwa na jinsi ya kujitetea juu ya mauaji ya mama yake kwani damu zilikuwa bado zimo vyumbani na alishindwa kuelewa ni maelezo gani angeyatoa juu ya damu hizo, ili aaminike kuwa hakumuua mtu.
“Sijui niseme nilichinja kuku! Lakini pia hawataamini!” aliwaza Anne.
Walipofika nyumbani kwake waliingia moja kwa moja hadi ndani na kuanza kupekua nyumba nzima, wote hawakuamini walipopambana na damu iliyogandamana sakafuni katika baadhi ya vyumba vya nyumba yake.
“Hii damu ni ya nini?”
“Kuku!”
“Kuku? Unatufanya sisi watoto, hebu sema ukweli!”
Alisema mmoja wa maaskari na kuanza kumshushia mvua ya virungu Anne kichwani mpaka akaanguka chini na kupoteza fahamu, alipozinduka damu nyingi zilikuwa zikimtoka mwili na baadaye aliendelea kupewa mateso makali sana ili aeleze ukweli.
Je nini kitaendelea?
Je Anne ataweza kusema ukweli?
Itaendelea Jumatatu.
Tags:
RIWAYA