Anne alikuwa chini akiwa amepoteza fahamu kwa kipigo alichokipata lakini hakuna mtu aliyekuwa na muda wa kuchukua maji na kummwagia ili azinduke, polisi walimchukua hivyohivyo na kwa harakaharaka walimpakia ndani ya gari lao akiwa na pingu zake mkononi kwenda naye kituoni, walishakuwa na uhakika asilimia mia moja kuwa Anne ndiye alimuua mama yake mzazi na kwenda kumtupa porini.
Alipofikishwa kituoni alipelekwa moja kwa moja hadi mahabusu ambako lango lilifunguliwa na kutupwa ndani na kuwaangukia mahabusu wengine waliokuwemo ndani.
Alilala chini akiwa hajitambui lakini kwa ubaridi uliokuwepo sakafuni uliotokana na mikojo ya mahabusu Anne alirejewa na fahamu zake saa sita ya usiku na kujikuta yupo kwenye chumba kidogo chenye giza! Aliangalia huku na kule ndani ya chumba hicho na kushindwa kuelewa mahali alipokuwa.
Alihisi yupo katikati ya watu na aliposikiliza vizuri alisikia watu wakihema na kukoroma pembeni yake, alizidi kuingiwa na hofu na kuchanganyikiwa alishindwa kuelewa ni mahali gani alipokuwa, moyo wake ulizidi kwenda mbio, hakuwa na kumbukumbu juu ya tukio lolote lililotokea mpaka kumfanya awe pale.
Alipojigusa usoni juu ya jicho lake la kulia mkono wake ulikutana na uvimbe mkubwa! Ghafla kumbukumbu zilimiminika kichwani mwake juu ya kipigo kibaya alichokipata kutoka kwa polisi na pia aliyakumbuka mauaji ya mama yake aliyoyafanya siku hiyo.
“Hivi hapa nipo wapi hasa? Au Nipo mochwari nini? Labda polisi walifikiri nimekufa wakaniweka chumba cha maiti?” Aliwaza Anne lakini sauti za watu wakikoroma zilimfanya aelewe mahali pale hapakuwa kama alivyopafikiria!
Alipata nguvu na kunyanyuka akaanza kujikongoja kutembea mahali kulikoonekana kuwa na mwanga kidogo, alihisi kuwakanyaga watu waliolala sakafuni, alitembea hadi getini, ambako alimkuta mwanamke mmoja amesimama wima akiimba wimbo wa dini ulioonekana kuwa pambio.
“Dada shikamoo!”
“Marahaba mdogo wangu hujambo?”
“Sijambo! Hivi hapa ni wapi?” Anne aliuliza.
“Mdogo wangu hapa hupafahamu?”
“Ndiyo dada!”
“Hapa ni mahabusu!”
“Dada nimeletwa hapa saa ngapi?”
“Usiku lakini umefanya nini mdogo wangu?”
“Sijafanya kitu dada wananionea!”
“Hapana haiwezekani ukaletwa hapa hivihivi!”
“Kwani wewe imekuwaje mpaka ukaingia humu?”
“Nimeua watoto wangu mwenyewe!”
“Umeua watoto wako? Kwanini?”
“Kwa bahati mbaya nilikuwa napika mboga jikoni wakati huohuo nikawa napaka dawa ya kunguni kwenye magodoro sijui ile dawa iliingia vipi katika mboga watoto wangu watatu walipokula wote wakafa, ikagundulika ni sumu ndiyo iliwaua nikakamatwa ndiyo maana nipo hapa! Sasa niambie na wewe kitu gani kimekupata mdogo wangu?”
“Dada ni siri nakueleza wewe tu, kwa kweli nimemuua mama yangu mzazi!”
“Mdogo wangu kimetokea nini mpaka ukafikia hatua hiyo? Nini kilikuudhi?”
“Mama yangu alinitesa sana tena kwa muda mrefu, aliwaua watoto wangu wawili, alisababisha kifo cha mume wangu na bado alitaka kuwaua watoto wangu wawili waliobaki! Nilipokataa akanipiga mimi na ugonjwa wa kupatwa na hedhi kila siku, nikawa nanuka na watu wakanitenga, hapakuwa na njia nyingine yoyote ya kumzuia asiendelee kunitesa zaidi ya kumuondoa duniani, sikufichi dada nimeua lakini mahakamani sitakubali jambo hilo, najua nitanyongwa! Kifo cha mama yangu hakinisikitishi hata kidogo mama alistahili kufa, kitu kimoja tu kinanitia huzuni nacho ni watoto wangu nimewaacha wakiwa na miaka miwili tu nani atawalea?” Alimaliza Anne na kuanza kulia.
“Usilie pole sana mdogo wangu hebu nielezee umemuuaje mama yako?”
“Anne alieleza kila kitu kilivyotokea, alimchoma mama yake kisu na kwenda kutupa mwili wake porini ambako hakuelewa ni nani alimwona na kutoa taarifa polisi hatimaye akakamatwa, alimweleza pia mateso mengine mengi yaliyompata maishani mwake ambayo yalisababishwa na mama yake.
“Lakini kesi hiyo unaweza kushinda tena kirahisi kabisa!”
“Inawezekanaje dada wakati mimi nimeua?”
“Mimi ni mwanasheria, hakuna ushahidi wa kutosha kukubana!”
“Mbona damu wameikuta ndani?”
“Hiyo siyo sababu damu inaweza kuwa ya ng’ombe, mbuzi au hata kunguni!”
“Nitashinda vipi kesi hii?”
“Omba Mungu mimi nitoke hapa mahabusu, ndugu wananishughulikia nikitoka naweza kukusaidia bure ili ushinde!”
“Kweli?”
“Ndiyo wala usiwe na wasiwasi, hii siyo kesi kabisa, mimi pia nitashinda kwa sababu sikuua kwa kukusudia, nisingeweza kuua watoto wangu mwenyewe niliowapenda!”
“Unaitwa nani?” Anne alimuuliza dada yule.
“Mimi naitwa Lydia Ishengoma ni mwanasheria mashuhuri sana hapa mjini, wewe unaitwa nani?”
“Mimi naitwa Anne nakuomba sana ukitoka hapa kabla yangu nisaidie dada yangu, watoto wangu! Watoto wangu nawapenda sana nimewaacha wadogo mno watateseka!” Anne alianza kulia tena.
“Usilie binti utatoka tu ingawa inaweza kukuchukua muda mrefu kidogo lakini mwisho ni lazima uwe huru!”
Waliongea mengi hadi mwanga wa asubuhi ulipoanza kuonekana na baadaye ndugu wengi walianza kuja kufuatilia masuala ya ndugu zao, maaskari waliwaita baadhi ya mahabusu mmoja baada ya mwingine wakawa wanatoka nje na wengine walipelekwa mahakamani, mahabusu wote walitoka wakabaki Anne na Lydia peke yao.
“Nyie wauaji hamuwezi kutoka kaeni humo ndani msubiri kupelekwa Butimba!” Alisema askari mmoja wa kike.
Mpaka saa nne asubuhi ilipotimu Anne na Lydia walikuwa bado wako mahabusu, wahalifu wengine zaidi walizidi kuongezwa katika chumba hicho kidogo. Ghafla Anne akiwa katikati ya mawazo alisikia sauti ya watoto wakilia na aliposikiliza vizuri aligundua zilikuwa ni sauti ya watoto wake! Alisimama wima na kuchungulia kaunta, huko aliwaona mchungaji Aaron na mkewe wakiwa wamewabeba Patrick na Nancy mikononi, watoto wakilia kwa sauti ya juu!
“Jamani watoto wangu! Watoto wangu jamani” Anne alianza kupiga kelele, aliumia kuwaona watoto wake wakilia, alijua asingeishi nao tena maishani mwake alijua ilikuwa ni lazima anyongwe.
“Kelele!” Askari mmoja aliongea kwa sauti akimuamuru Anne anyamaze.
“Nawataka watoto wangu jamani, nataka niwaage kwa mara ya mwisho!” Alisema Anne.
“Umeambiwa unakwenda kufa?” Alijibu askari
“Ningejua nisingemuua mama, lakini kama nisingemuua ni lazima angewaua watoto wangu, ni heri mimi nikateseka gerezani lakini Patrick na Nancy wawe salama!” Anne aliwaza.
Alipotupa tena macho yake kaunta aliwashuhudia polisi wakiwasukuma mchungaji Aaron na mkewe kuwatoa nje ya kituo, aliendelea kuwaona watoto wake wakilia na roho ilimuuma sana! Aliwahurumia watoto wake na alijua kwa yeye kupelekwa gerezani wangeishi kama yatima duniani kwa sababu baba yao alikuwa amekufa!
*****
Muda mfupi baadaye Anne na Lydia walitolewa mahabusu na kuanza kusukumwa kwenda nje ambako gari lilikuwa tayari kuwapeleka gerezani Butimba, alipofika nje Anne alitupa macho kulia kwake na kuwaona mchungaji Aaron na mkewe wakiwa na watoto wake mikononi!
Alishindwa kuvumilia na kujikuta akitimua mbio kuwafuata akiwa na pingu zake mikononi, askari aliyekuwa akiwalinda alifikiri Anne anatoroka, bila kuchelewa alilenga bunduki yake tayari kumfyatulia risasi, lakini kabla hajaachia hata risasi moja alimwona Anne akisimama mbele ya watu wawili wenye watoto.
“Nisogezeeni watoto wangu niwabusu!” Anne alisema kwa sauti kubwa iliyomfikia askari aliyenyosha bundiki yake kwa lengo la kumpiga Anne.
“Ana bahati vinginevyo ningemmalizia mbali!” Alisema askari huyo aliyeonekana si mwepesi kutumia bunduki.
Watoto walisogezwa karibu yake na Anne alianza kuwamwagia mabusu kibao usoni kwao.
“Watoto wangu Patrick na Nancy bakini salama nawapenda na nimemuua bibi yenu kwa sababu ya kuwalinda nyinyi,bibi yenu alitaka kuwaua bila hatia!” Alisema Anne na kuwafanya mchungaji na mke wake ambao hawakuwa na habari juu ya mauaji aliyoyafanya washangae.
“Anne umemuua mama yako?” Mchungaji Aaron aliuliza kabla Anne hajajibu swali hilo maaskari walimvamia na kuanza kumpiga kwa virungu kichwani akaanguka chini tena.
“Nyanyuka twende muuaji wewe!” Alifoka mmoja wa maaskari.
“Mchungaji nitunzieni watoto wangu, ninajua sitatoka gerezani leo wala kesho, wafundisheni kumcha Mungu na mara kwa mara waelezeni kuwa mimi mama yao nipo ili wasinisahau, waleteni gerezani mara kwa mara kuniona!” Anne alisema maneno huku virungu vingi vikizidi kumwangukia chini alipolala.
Baada ya kusema hayo alijikongoja na kunyanyuka ardhini alipoanguka ni kweli aliwatia huruma watu wote waliokuwepo kituoni, uso wake wote ulivimba, na nguo zake zote zilijaa damu, ilikuwa si rahisi hata kidogo kuamini kuwa mwanamke yule alikuwa Anne!
****
Alivutwa na kupelekwa moja kwa moja hadi kwenye gari, ambako alitupwa sehemu ya nyuma na kumkuta wakili Lydia Ishengoma akiwa amekaa!
“Anne tulia watakuumiza hawa hawana huruma!” Wakili alisema.
Anne alinyanyuka na kuanza kuwapungia mchungaji na mke wake waliokuwa bado wamesimama mahali alipowaacha wakiwa watoto wakilia mikononi mwao, mlango wa gari kubwa aina ya Scania walilopanda ulifungwa baada ya kuingia askari mwenye bunduki mikononi.
“Una bahati wewe! Pale nilishaamua kukumiminia risasi kwani nilijua unatoroka, mshukuru Mungu wako!” Askari yule alisema na gari lilianza kuondoka kutoka kituo cha polisi.
Kutoka mjini Mwanza hadi gereza la Butimba ilikuwa ni mwendo wa kama kilometa kumi na tano lakini iliwachukua muda wa saa nzima kwa sababu ya ubovu wa barabara za Mwanza mjini! Walipofikishwa gerezani wote walishushwa na kuingizwa ndani ya gereza walipekuliwa na kuingizwa chumba maalum cha mahabusu wa mauaji ambako walikaa wawili tu.
****
Miaka miwili tu baada ya kuingia gerezani wakili Lydia Ishengoma aliachiwa kutoka gerezani ilipogundulika hakuua kwa kukusudia, kazi yake ya kwanza kama alivyoahidi alipotoka gerezani ilikuwa ni kumtetea Anne! Akijua shida alizokuwa nazo gerezani hasa tatizo la upungufu wa damu ambalo Anne alilolipata mara kwa mara wakili Lyidia alianzisha harakati za kumtetea Anne mahakamani.
Siku wakili Lydia aliyoondoka gerezani Anne alilia kama mtu aliyefiwa na ndugu yake kwa sababu hakuwa na rafiki mwingine yeyote zaidi yake, mahabusu wengine wote walimtenga kwa sababu ya harufu aliyotoa kutokana na hedhi ya kila siku, ni wakili Lydia peke yake katika gereza zima aliyemvumilia, alishindwa kuelewa maisha yake yangeendeleaje baada ya hapo, lilikuwa pigo kubwa!
Huo ndio ukawa mwanzo wa Anne kuingia gerezani, ambako alikaa kwa muda wa miaka kumi akipelekwa mahakamani mara moja kila mwezi ambako kesi yake iliendelea kutajwa na baadaye kuanza kusikilizwa! Alishangaa siku aliyomkuta wakili Lydia amevaa mavazi ya Uwakili akimtetea mahakahami, Anne aliamini ipo siku angekuwa huru.
Anne aliendelea kusota gerezani, nguo alizokuwa nazo zilichakaa damu ziliendelea kumtoka mfululizo, jambo hilo lilimkera sana, alinuka na inzi wengi walimfuata kila alikokwenda! Hali hiyo ilisababisha mahabusu wenzake wamfukuze katika kila chumba alichopangiwa kulala, mwisho akawa analala barazani kwenye baridi na mbu wengi.
Yalikuwa ni mateso makali mno, lakini lawama zote hizo alimtupia mama yake mzazi aliyempa ugonjwa huo wa ajabu.
“Mama alistahili kufa, na sijui ni kwanini alinizaa, inakuwaje mtoto umzae mwenyewe halafu umtese kiasi hiki? Na ninasema siku nikinyongwa huko kuzimu nikimkuta mama ni lazima nimuue tena!” Alilia Anne.
****
Kama alivyowaomba mchungaji Aaron na mke wake walilazimika kuwapeleka Nancy na Patrick gerezani kumwona mama yao kila mwezi, walikuwa ni watoto wazuri waliokuwa na kulelewa katika familia ya Kikristo, walimpenda mama yao pamoja na kuwa alikuwa gerezani. Patrick alifanana sana na marehemu baba yake Huggins lakini Nancy alimfanana Anne kwa kila kitu.
“Mama usijali ipo siku utatoka tu gerezani, tunakupenda mama, wewe ni mama yetu hata kama ni mfungwa!” Hayo ndiyo yalikuwa maneno ya watoto wake walipotimiza umri wa miaka minane.
Katika umri huo walikwisha kuwa watoto wakubwa wenye kuyafahamu mema na mabaya, walikwenda mahakamani kila siku ya kesi ya mama yao ilipofika, ni kama walikulia mahakamani wazee wa mahakahama na Mahakimu wote waliwafahamu Patrick na Nancy!
Je nini kitaendelea?
HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 16
MTUNZI: ERIC JAMES SHIGONGO
MIAKA KUMI BAADA YA KUINGIA GEREZANI
Kesi ilikuwa imepamba moto wakili Lydia Ishegoma alikuwa amedhamiria kumtoa Anne gerezani, kila mara alimtembelea na kufanya naye mahojiano.
“Haupo ushahidi wa kukufunga Anne!”
“Lakini niliua mheshimiwa!”
“Pamoja na hayo lakini nitahakikisha unatoka gerezani kwa sababu uliyofanyiwa na mama yako yalikuwa ya kukulazimisha ufanye ulichokifanya!”
“Nitashukuru kama nitatoka gerezani naomba ujifahidi sana na Mungu atakusaidia, watoto wangu ndio wanaonifanya nihuzunike sana!”
“Kwani kwa hivi sasa wanaishi na nani?”
“Wanaishi na Mchungaji wa kanisa letu, niliwapeleka kwake kabla ya kukamatwa!”
“Hebu nieleze vizuri, unafikiri kuna mtu yeyote aliyekuona wakati ukiibeba maiti ya mama yako kwenda kuitupa?”
“Hapana ilikuwa ni usiku mno na watu wengi walikuwa wamelala isitoshe ilikuwepo dalili ya mvua kubwa kunyesha!”
“Sasa nani aliwaeleza polisi?”
“Hata mimi nashangaa!”
“Kuna watu waliofahamu kuwa wewe na mama yako mlikuwa hamuelewani?”
“Hapa mjini hapana, lakini kijijini kwetu Kome wapo watu wanaoelewa jambo hili!”
“Je, kuna watu walielewa kuwa mama yako alikuja hapa mjini?”
“Ndiyo lakini sio wengi!”
“Baada ya kufanya kitendo hicho ulipiga kelele kuita watu kuwaeleza kuwa mama yako amepotea?”
“Hapana ila nilikwenda moja kwa moja kituo cha polisi kutoa taarifa”
“Na huko ndiko ulikamatwa?”
“Ndiyo!”
“Unahisi nani anaweza kuwa alitoa taarifa polisi?”
“Kwa kweli sifahamu na si rahisi kuelewa na nilishangaa polisi walijuaje”
“Uliushika maiti ya mama yako kwa mikono yako?”
“Ndiyo, kwani vipi?”
“Ilipopimwa haikuonyesha alama za vidole!”
“Labda kwa sababu mvua ilinyesha sana usiku ule!”
“Anne!” Aliita wakili Lydia.
“Naam mheshimiwa!”
“Nitahakikisha unashinda kesi hii!”
“Nitashindaje mheshimiwa wakati niliua?”
“Hiyo kazi niachie mimi! Wamepanga siku ya hukumu iwe Januari 21, leo ni tarehe ngapi?”
“Ni tarehe 15, bado wiki moja tu ninyongwe! Dada Lydia utanisaidia kuwalea watoto wangu?”
“Anne nimekuambia huwezi kunyongwa, kwani hakuna ushahidi wa kutosha kukutia hatiani, mtu mwingine yeyote angeweza kumuua mama yako na kwenda kumtupa porini!”
****
Sifa ya Anne kuwa mwanamke muuaji ilisambaa kwa kasi mjini Mwanza na vitongoji vyake, kwa kitendo cha kumuua mama yake mzazi aliyemleta duniani Anne alionekana ni mwanamke mwenye roho mbaya pengine kuliko binadamu wote! Alilaaniwa na kila mtu na watu wote walitamani ahukumiwe kifo na kunyongwa!
Ni kweli Anne aliua hata yeye hilo alilikubali lakini hakuwa na mtu hata mmoja aliyeufahamu ukweli ni kwanini alifikia uamuzi wa kumuua mama yake aliyemzaa. Alitamani kuueleza ukweli Ulimwengu mzima ili asafishe jina lake lakini hakuwa na nafasi ya kuongea na watu wote! Mtu pekee aliyeufahamu ukweli alikuwa ni wakili wake.
Siku ya Januari 21, 1998 mamia ya watu walifurika mahakama kuu ya Mjini Mwanza kuisikiliza kesi ya Anne, alipoteremshwa tu kutoka katika gari lililombeba kutoka gerezani Butimba akiwa na mahabusu wengine, watu waliokuwa nje ya mahakama walianza kunong’onezana na wengine kusema kwa sauti bila hata uoga kuwa Anne alistahili kifo.
“Mnyongeni tu! Hafai kuishi huyu kwanini amuue mama yake kinyama kiasi kile?” Alisema mama mmoja wakati Anne akipitishwa, maaskari waliokuwa wakimlinda walicheka lakini maneno yale yalimuumiza sana moyo Anne na kumfanya atokwe na machozi, alimhurumia mama yule kwa sababu hakuujua ukweli.
Alitembea kwa shida akiwa amefungwa pingu mikononi na miguuni, nguo zake zilikuwa chafu kupita kiasi na mwili wake ulijaa ukurutu na ulikuwa mweusi kwa sababu ya kutokuoga, alionekana muuaji kuliko wauaji wengine wote waliotangulia.
Anne alitupa macho yake pembeni na kuwaona watoto wawili wakilia huku wakijaribu kujitoa mikononi mwa mwanamke aliyewashikilia, Anne alipomwangalia mwanamke huyo alimkumbuka, alikuwa ni mdogo wake yaani mtoto wa baba yake mdogo, Suzzane na alipotupa macho yake kuwaangalia watoto hao aliwatambua, walikuwa ni Nancy na Patrick watoto wake.
“Watoto wangu! Watoto wangu! Wale pale!” alipiga kelele Anne huku akijaribu kugeuka na kuanza kutembea kuelekea mahali walipokuwa Patrick na Nancy watoto wake mapacha waliobaki, waliosababisha amuue mama yake mzazi ili kuokoa maisha yao.
“Mama! Mama! Mama! ninakupenda mama, pole mama!” Alisema Patrick.
“Niachie! Niachie! Niachie niende kwa mama yangu!” Alilia Nancy huku akimuuma mama yake mdogo mkono ili amwachie lakini aliendelea kumshikilia kwa nguvu asimponyoke.
Anne aliumia sana moyoni mwake kushuhudia kitendo kile cha watoto wake, alitamani kuwasogelea watoto wake lakini alishindwa kwani kabla hajasogea umbali mrefu maaskari walimshika na kumbeba juu akatupwa katika mahabusu ndogo iliyokuwepo karibu na mahakama hiyo, ilikuwa ni mahabusu chafu iliyonuka mikojo na kinyesi.
“Ipo siku mama yangu atakuwa huru na nitamsaidia!” Alisema Patrick.
Katika maisha yao Nancy na Patrick hawakuwahi kuishi na mama yao, kwani kwa mara ya kwanza alipokamatwa walikuwa na umri wa miaka miwili na mpaka siku hiyo alikuwa amekaa gerezani miaka kumi, tayari walikuwa na umri wa miaka kumi na mbili! Lakini pamoja na kutokuishi na mama yao bado walimpenda na waliamini siku moja angekuwa huru na kurejea tena kwao.
****
Muda wa mahakama kuanza kazi uliwadia na watu walianza kuingia mahakamani na kuchukua viti vyao. Patrick, Nancy na mama yao mdogo nao waliingia na kuketi, wote walikuwa wakilia machozi ya uchungu ni kwa sababu walijua siku hiyo ndiyo ilikuwa siku ya hukumu ya mama yao na lolote lingeweza kutokea, kifo ama maisha.
Watu wengi walishindwa kuingia mahakamani kwa sababu ya ufinyu wa nafasi iliyokuwepo na kusimama nje ya mahakama na wengine kukaa chini ya miti wakisubiri mahakama ianze. Mawakili wote walikuwa ndani.
Kesi ya Anne ilipangwa kuwa ya kwanza, Anne alitolewa mahabusu na kuingizwa moja kwa moja hadi mahakamani, alipoingia tu hali ya hewa ndani ya chumba cha mahakama ilibadilika! Inzi waliongezeka na harufu mbaya ilitanda, watu walishindwa kuelewa hali hiyo ilitokana na nini lakini inzi walivyozidi kumfuata Anne wengi walianza kuhisi huenda alikuwa amejisaidia ndani ya nguo zake.
Jaji Raphael Mpoki aliyekuwa maarufu kwa kuhukumu watu miaka mingi katika historia ya Tanzania tena bila huruma alipoketi kitini minong’ono yote iliyokuwepo ndani ya mahakama ilikwisha na mahakama ilianza bila kupoteza hata dakika moja.
Karani wa mahakama alisimama na kuanza kutaja namba ya kesi na baadaye muendesha mashtaka alisimama na kusoma historia nzima ya kesi na baadaye kumwomba Jaji Mpoki amhuhuku Anne kwa sababu ulikuwepo ushahidi wa kutosha kuonyesha ni kweli alimuua mama yake kwa kumchoma visu.
Anne alisimama kizimbani akilia akiwa amewaangalia watoto wake Patrick na Nancy ambao pia waliendelea kulia, roho yake ilimuuma sana kujua ni lazima angehukumiwa kifo na kuwaacha watoto wake wakiteseka peke yao duniani, kuna wakati alijilaumu ni kwanini alimuua mama yake lakini alipokumbuka kuwa mama yake alitaka kuwaua watoto wake alisita kujilaumu na kuona alichokifanya kilikuwa sahihi.
Mahakama iliendelea kuwa kimya wakati mwendesha mashtaka akiendelea kumueleza Jaji Raphael Mpoki sababu za kuitaka mahakama imhukumu mshtakiwa kunyongwa.
“Mheshimiwa Jaji ushahidi wa kutosha upo na hivyo naiomba mahakama yako Tukufu imhukumu mshtakiwa kifo ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo!”
****
Jaji Mpoki aliinamisha kichwa chake chini na kuanza kutafakari hiyo ndiyo ilikuwa kawaida yake kabla hajamhukumu mtu kifo! Watu wote walijua baada ya kunyanyuka pale ni lazima angemhukumu Anne kunyongwa.
“Anne!” Jaji Mpoki aliita baada ya kunyanyua kichwa chake lakini Anne hakuitika aliendelea kulia machozi akiwa amewaangalia watoto wake waliokuwa wakilia kwa sauti na kusababisha kelele mahakamani.
“Wanangu Patrick na Nancy leo nakufa kwa ajili yenu!” Badala ya kumwitikia hakimu Anne aliwaita watoto wake.
“Hapana mama usife, bado tunakuhitaji sana usituache!” Patrick alipiga kelele mahakamani na kuchomoka mikononi mwa mama yake mdogo akakimbia na kumfuata mama yake lakini kabla hajakifikia kizimba alikamatwa mkono na askari na kuanza kuvutwa kupelekwa mahali alipokuwa amekaa.
“Anne tafadhali nijibu nakuita!” Jaji Mpoki aliita tena
“Na.a..am mhe...sh..i..mi..wa ja..ji!”
“Sema Anne, sema usiogope unataka nikufanye nini? Kwani maisha yako hivi sasa yapo mikononi mwangu!” Aliuliza Jaji Mpoki, wakili Lydia Ishengoma alijua nini alichomaanisha Jaji Mpoki kwa kuuliza swali hilo kwani haikuwa kawaida yake kuuliza maswali wakati wa hukumu na ilipotokea akauliza swali hilo alikuwa ameingiwa na huruma na kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kumwachia huru mshtakiwa.
Wakili Lydia alitegemea Anne angeomba msamaha na alijua wazi angeachiwa huru! Moyoni alijawa na furaha kupindukia alijua ushindi ulikuwa umewadia, hakutaka kabisa Anne ahukumiwe kifo kwa sababu aliua kwa kulazimishwa na mazingira.
“Mheshimiwa Jaji ninajua mimi ni muuaji na ninastahili kifo na siwezi kukataa ninakuruhusu unihukumu kifo nife lakini.....!” Anne alianza kuongea, mahakama nzima ilikuwa kimya kumsikiliza yeye, wakili Lydia alishangaa ni kwanini Anne alianza kujitetea kwa kauli hiyo lakini moyoni mwake alijua ingebadilika.
Baadaye Anne aliendelea“.... ni kweli niliua lakini mheshimiwa Jaji naomba niseme maneno yafuatayo kwa watu waliokuwepo hapa mahakamani ili wapate kuelewa ni kwanini nifanya hivyo! Ni wengi wananyongwa na ni wengi wameua lakini kwa kweli hawakutakiwa kufanya hivyo, mimi si muuaji ila nililazimika kuua kwa sababu sikuwa na njia yoyote ya kuwalinda watoto wangu! Mama yangu aliyenizaa na kunileta duniani alitaka kuwaua wanangu ingawa tayari alikwishaua watoto wangu wengine wawili William na Henry”
Mahakama ilikuwa kimya watu wote wakisikiliza maneno ya Anne aliyoyaongea huku akilia.
“Nilipokataa kumpa watoto wangu alinipiga na ugonjwa wa kupata hedhi kila siku na hivi mnavyoniona hapa niliposimama nguo zangu zote zimelowa na nimekuwa katika hali hii kwa muda wa miaka kumi na moja!”
Anne alieleza kila kitu na kila mtu mahakamani alishikwa na huzuni wengi walinong’ona taratibu wakidai hata wao wasingeweza kuvumilia mateso aliyofanyiwa Anne! Wengi walimwaga machozi na hata Jaji mwenyewe alishindwa kujizuia na kujikuta akilia mbele za watu.
“Nimemaliza mheshimiwa naomba unihukumu kifo ili ninyongwe nimfuate huko mama huko aliko na nikimkuta ni lazima nimuue tena kwa sababu amenitesa sana na mara kwa mara najiuliza ni kwanini alinizaa!” Alimaliza Anne huku akilia.
Watu wote walikaa kimya kumsubiri Jaji Mpoki atoe hukumu yake, walipomwangalia alikuwa akijifuta machozi kwa kitambaa chake na alipomaliza kufanya hivyo alimwangalia Anne kwa huruma.
“Uta....kwenda jela mia...ka mitano!” Jaji Mpoki alijikuta akitoa hukumu ambayo hakuna mtu mahakamani aliitegemea na maaskari walimuongoza Anne kumtoa mahakamani, aliondoka huku akilia na alisindikizwa na vilio vya watoto wake.
“Msiwe na wasiwasi muda si mrefu nitakuwa pamoja na nyinyi watoto wangu!” Anne aliwaaambia watoto wake kabla hajatolewa ndani ya mahakama.
Wakili Lydia aliruka na kushangilia kwa furaha alijua miaka mitano haikuwa mingi na ilikuwa bora kuliko kunyongwa, aliwakumbatia Patrick na Nancy pamoja na mama yao mdogo, kila mtu alikuwa na furaha.
“Masikini kumbe msichana huyu ameteseka kiasi hiki?”
“Aisee kwa aliyofanyiwa alikuwa na haki ya kuua!” Walisikika wakiongea watu waliotoka mahakamani.
Wakili Lydia,Patrick, Nancy na mama yao mdogo walisimama nje ya mahakama wakisubiri Anne atolewe na kupakiwa ndani ya gari kwa safari ya kwenda gerezani, machozi yalishapungua usoni na nyuso zao zilionyesha furaha.
“Mnasoma?” Wakili aliuliza.
“Ndiyo!” Patrick na Nancy waliitikia.
“Darasa la ngapi?”
“Darasa la sita!”
“Mlishika nafasi ya ngapi darasani?”
“Mimi nilishika nafasi ya pili dada yangu akashika nafasi ya kwanza!”
“Ah! Hongereni sana, wewe unataka kuwa nani ukiwa mkubwa?” Wakili alimuuliza Patrick.
“Ninataka kuwa Mchungaji! Lakini dada yangu anapenda kuwa mwanasheria!”
“Kweli?” Wakili alimuuliza Nancy
“Ndiyo mama!”
Walikaa mahakamani mpaka saa saba mchana mahakama ilipokwisha na walishuhudia Anne akitolewa mahabusu na kupakiwa ndani ya lori kubwa lililokuwa maalum kwa ajili ya kubeba mahabusu kuwarudisha gerezani.
Alikuwa amekonda sana na nguo kama sketi aliyovaa ilionekana kulowa kwa damu! Inzi wengi walimfuata, Patrick na Nancy waliumia mioyo yao kumwona mama yao katika hali hiyo na walitamani mambo yangekuwa tofauti.
Pia mambo waliyoyasikia mahakamani siku hiyo yaliwaumiza moyo, waliumia kujua mama yao aliua lakini walifarijika kujua aliua kwa sababu ya kuwatetea wao! Huo ulikuwa upendo mkubwa mno kwa mama kuuonyesha, mama yao alikuwa amekubali kuteseka gerezani kwa sababu yao! Jambo hilo liliwafurahisha sana.
“Tutaoanana watoto wangu! Miaka mitano si mingi kama nitabaki gereza la hapa Butimba tafadhali mje kunitembelea mara kwa mara lakini kama nikihamishwa basi tutaonana Mungu akipenda!”
“Sawa mama, tunakupenda mama!”
“Mchungaji Aaron na mkewe wako wapi? Na wewe Suzzane umekuja lini?”
Alipouliza swali hilo Patrick na Nancy walianza kulia machozi tena.
Je nini kitaendelea?
Je Anne ataweza kushinda kesi hiyo?
Tags:
RIWAYA