TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 17----18


Miezi sita kabla ya hukumu hiyo mchungaji Aaron na mkewe walipata uhamisho kwenda nchini Kenya katika jiji la Nairobi ambako mchungaji Aaron alitegemea kuongezea elimu zaidi ya mambo ya dini, alitakiwa kusoma Digrii ya kwanza ya Teolojia katika chuo kikuu cha Nairobi Theological University
Yalikuwa ni masomo ya miaka mitatu kamili, yeye na mke wake walisikitika sana kuwaacha Patrick na Nancy ambao tayari walishaanza kuwahesabu ni watoto wao, lakini kikubwa kilichowaumiza zaidi kilikuwa ni Anne aliyekuwa gerezani, hawakujua wangemwona tena lini kwani waliamini angehukumiwa kifo na si ajabu kunyongwa bila wao kuwepo.
Taarifa za kwenda Nairobi zilikuja ghafla mno kiasi kwamba hawakupata kabisa nafasi ya kwenda gerezani kumuaga Anne! Kitu kikubwa walichokifanya ni kumtafuta Suzanne, msichana aliyekwenda nyumbani kwao mara kwa mara kuwaona Patrick na Nancy, akidai walikuwa ni watoto wa dada yake yaani yeye na Anne walikuwa watoto wa baba mkubwa na mdogo.
Suzanne aliwaeleza kuwa alikuwa ameolewa hapohapo mjini Mwanza maeneo ya Capripoint, iliwachukua siku kama tatu kumtafuta Suzanne kwa sababu hakuwahi kuwaachia namba yake ya simu, siku ya nne wakiwa wamekata tamaa kabisa wakifikiria kuwapeleka Patrick na Nancy Ustawi wa Jamii, walifanikiwa kumpata baada ya kumuulizia kwa jina la mume wake Anorld aliyekuwa mfanyabiashara maarufu mjini Mwanza.
Suzanne alikuwa ni miongoni mwa watu waliofanikiwa kimaisha kwani kulikuwa na nyumba kubwa na magari kadhaa ndani ya ngome yake! Nyumba yake ilipambwa vizuri na kila aina ya samani zilizofanya ivutie kupita kiasi. kifupi Suzanne na mumewe walikuwa na pesa!
Tatizo pekee alilokuwa nalo Suzanne ni bahati mbaya ya kutozaa watoto! Akiwa kidato cha tatu bahati alipata ujauzito uliotaka kuhatarisha maisha na masomo yake, ilibidi yeye na mvulana aliyempa mimba washirikiane kutafuta mitaani daktari wa kuitoa, kazi hiyo ilifanyika lakini bahati mbaya haikufanyika vizuri kwani mabaki mengine ya mimba hiyo ya miezi mitatu hayakutoka, yalibaki ndani ya mfuko wa uzazi hivyo kusababisha mfuko wa uzazi kuoza.
Ili kuokoa maisha ya Suzanne madaktari walilazimika kumfanyia operesheni na kuutoa mfuko wake wa uzazi uliooza! Suzanne akawa amepoteza uwezo wake wa kuzaa.
Kwa uzuri wa sura Suzanne alikuwa ni mwanamke mzuri wa kumvutia kila mtu aliyemwangalia, alipata bahati ya kusoma hadi chuo kikuu na kuhitimu digrii mbili za uchumi, elimu hiyo ilimwezesha kupata kazi nzuri sana katika shirika lililojishughulisha na uchimbaji wa visima kanda ya ziwa, Hesawa na Suzanne ndiye alikuwa bosi katika shirika hilo lililofadhiliwa na wazungu.
Ni kweli Suzanne na Anne walikuwa ndugu, baba zao walikuwa ni mtu na mdogo wake. Suzanne akiwa Mwanza alisikia habari za Anne na matatizo aliyoyapata, alisikitika sana kusikia alikuwa gerezani na alianza juhudi za kuwatafuta Patrick na Nancy ili aishi nao nyumbani kwake kwani alikuwa na kila kitu isipokuwa watoto!
Mchungaji Aaron na mkewe hawakuwa tayari kwa jambo hilo, sababu hata wao waliwapenda sana watoto hao hivyo walimkatalia Suzanne kuwachukua, lakini walipotakiwa kwenda kusoma Nairobi hawakuwa na chaguo jingine zaidi ya kumtafuta tena Suzanne ili awachukue watoto na kuishi nao.
“Ninakwenda kusoma kwa muda wa miaka mitatu!”
“Wapi?”
“Hapa jirani tu Kenya!”
“Aisee hongera sana!”
Suzanne alifurahi mno kukabidhiwa watoto, aliowatamani kuwa nao kila siku, kitu cha kwanza alichokifanya baada ya kuwachukua Patrick na Nancy ni kuwahamisha kutoka shule ya Nyakabungo waliyosoma na kuwapeleka shule ya kimataifa ya Green Garden iliyokuwa maarufu kwa watoto wa watu wenye uwezo, wakawa wanafuatwa asubuhi na gari la shule na kurudishwa nyumbani jioni na walipewa chakula cha kutumia na walinunuliwa nguo mpya!
Hata mume wake Suzanne nae pia aliwapenda sana Patrick na Nancy na alitamani wangekuwa watoto wake! Alilifahamu tatizo la mke wake kutokuwa na uwezo wa kuzaa mtoto lakini alimpenda Suzanne na hakuwa tayari kumwacha Suzanne kwa sababu hiyo.
Siku zote Anorld alitamani kuwa na mrithi wa mali zake na alimtamani sana Patrick, alitamani sana kuwa na mtoto kama yeye lakini alijua isingewezekana tena na hakutaka kabisa kuzaa nje ya ndoa yake, Anorld alikuwa mwanaume mwaminifu pengine kuliko wanaume wote mjini Mwanza ingawa alikuwa na mali nyingi.
Nyumbani kwa Suzanne Patrick na Nancy walipewa kila kitu na mwisho wa wiki ilikuwa ni lazima wapelekwe kisiwa cha Saa nane kuogelea! Maisha yalibadilika na kuwa ya raha, pamoja na hayo bado hawakumsahau mama yao kila siku walimfikiria na kabla ya kwenda kulala ilikuwa ni lazima wapige magoti na kumuombea.
Waliamini muda si mrefu mama yao angetoka gerezani na kuwachukua kwenda kuishi nao pamoja, walikuwa tayari kuacha kila kitu ili mradi wawe na mama yao hata kama wangetakiwa kulala chini na kulala bila kula kwao ilikuwa sawa kwa sababu walimpenda sana mama yao!
Watu wengine ambao Patrick na Nancy hawakuwa tayari kabisa kuwasahau walikuwa ni mchungaji Aaron na mkewe, waliokuwa tayari chuoni Nairobi, kila siku waliukumbuka wema wao na walimweleza hata Suzanne na mumewe jinsi familia hiyo ilivyompenda Mungu! Walijaribu pia kumshauri Suzanne na mumewe wamgeukia Mungu na kumtegemea yeye katika maisha yao.
*****
Mchungaji Aaron na mkewe wako wapi na wewe Suzanne umekuja lini?”
“Mimi dada? Mbona nipo hapa Mwanza muda mrefu tu shikamoo kwanza!”
“Marahaba! Kweli?”
“Ndiyo!”
“Na hawa watoto wangu ulikutana nao wapi na vipi na Mchungaji Aaron na mkewe wako wapi?”
“Mchungaji Aaron na mkewe hivi sasa hawapo wamekwenda Nairobi kimasomo, kabla ya kuondoka sababu nilishakwenda kwao kujitambulisha mimi ni nduguyo walikuja hapa kuniomba nikae na watoto mpaka utakapotoka gerezani,kwa hivi sasa ninao kwa miezi sita sasa, wanasoma vizuri na ninaishi nao kama watoto wa ndugu yangu!”
“Ahsante sana hivi sasa una watoto wangapi Suzanne?”
“Sijajaliwa bado!”
“Kweli?”
‘Ndiyo!”
“Usijali lakini! Watoto hutoka kwa Mungu!”
“Mbona una hali hii Anne? Mbona nguo zako zimelowa sana?” Aliuliza Suzanne akimwangalia Anne kwenye sketi yake aliyovaa.
“Ni mama!Ni mama aliyenifanyia kitu hiki kibaya kila siku ninapata hedhi, kwa muda wa miaka karibu kumi sasa!”
“Mungu wangu kweli? Ulishakwenda hospitali?”
“Ndiyo lakini siponi haya ni mambo ya Lutego, ili nipone ninahitaji kuombewa na mchungaji au mtumishi yeyote wa Mungu!”
“Usijali mama Ipo siku utapona tu na sisi pia tutaendelea kukuombea!” Nancy alimwambia mama yake.
“Suzanne nitunzie vizuri watoto wangu Mungu atakubariki!”
“Mama usiwe na wasiwasi anti ni mtu mzuri sana anatupatia kila kitu!” Patrick aliongea kabla Suzanne hajasema neno
“Nakushukuru sana Suz….!”Kabla Anne hajamaliza alivutwa kwa nyuma na kuanza kupelekwa moja kwa moja hadi kwenye gari la kupakia wafungwa kwenda mahabusu.
“Kwaherini mwanangu, ninawapenda sana ipo siku tu tutakuwa pamoja!”
“Hakuna shida tunakupenda mama na tunakuombea na tunasubiri urudi!”
Baadaye wote walilishuhudia gari likipakia wafungwa na mahabusu likaanza safari ya kuondoka mahakamani kwenda gerezani Butimba, Patrick na Nancy walibaki wakilia machozi kwa ajili ya mama yao, walimpenda sana Anne na walitaka sana kuwa naye maishani mwao!
Gari lilipopotea machoni pao, Suzanne alifungua mlango wa gari lake na Patrick na Nancy waliingia ndani safari ya kuelekea nyumbani ilianza!Njia nzima Patrick na Nancy walilia machozi wakilitaja jina la mama yao! Katika maisha yao hawakuwa na kumbukumbu za kuishi na mama yao kwani alipotiwa nguvuni walikuwa na umri wa miaka miwili.
*****
Jioni ya siku hiyo Patrick na Nancy wakiwa wamelala usingizi, maongezi mazito na ya hatari yaliendelea chumbani kwa Suzanne na mume wake maongezi ambayo hawakutaka kabisa watoto wayasikie.
“Najua unataka sana watoto Anorld lakini mimi uwezo wa kuzaa sina, unataka sana mrithi wa mali zetu lakini sina la kufanya kusaidia!”
“Sasa tutafanya nini mke wangu? Natamani kuwa na mtoto kama Patrick ili angalau nikifa aweze kurithi mali zetu!”
“Lakini si Patrick yupo hapa na dada yake pia, hawa wanaweza kuwa watoto wetu au unaonaje?”
“Mama yao je? Mimi nataka watoto wangu mwenyewe!”
“Sasa tutawapate wapi?”
Suala la watoto lilimsumbua sana Anorld, siku zote alikuwa mtu mwenye mawazo juu ya jambo hilo na alishindwa angelitatua vipi! Mara nyingi alimshawashi mke wake Suzanne angalau wanunue mtoto wa wizi na kujifanya ni wao lakini Suzanne aliukataa mpango huo.
Usiku huo walivutana sana juu ya suala la watoto mpaka wakafikia mahali wakashindwa kuelewana, baada ya majadiliano walifikia uamuzi wa kuwachukua Patrick na Nancy moja kwa moja wawe kama watoto wao wa kuzaa.
“Nauliza mama yao je?”Anorld aliuliza tena.
“Mama yao pamoja na kuwa ni ndugu yangu,furaha katika ndoa yetu ni watoto, hivyo hakuna njia nyingine zaidi kama unakubali tuhakikishe Anne anafia huko huko gerezani, hatoki na haonani na watoto wake tena sisi ndio tutakuwa wazazi wao!”
“Tutalifanyaje hilo?”
“Tutamuua huko huko gerezani!”
“Tutawezaje kumuua mtu gerezani na ulinzi wote ulipo kule?”
Wote wawili walikaa kimya kwa muda wakijaribu kutafakari ni kipi kingefanyika ili kuhakikisha Anne anakufa gerezani, na Suzanne na Anorld wanawachukua watoto wake, Suzanne alikuwa ndugu kabisa wa Anne lakini alikuwa ameamua kumuua ndugu yake ili amnyang’anye watoto wake wazuri waliompenda.
“Hilo la tutamuuaje hebu tuliache kwanza tulale kesho tutakuwa tumeshalifikiria vizuri!”
*****
Asubuhi kulipokucha Suzanne aliwaamsha watoto na kuwatayarisha kwa kwenda shule, hiyo ndiyo ilikuwa kawaida yake kila siku, hakuonyesha dalili yoyote ya maongezi yaliyofanyika kati yake na mumewe usiku, alikuwa na furaha na mapenzi kwa Patrick na Nancy kama kawaida na alizidi kuwatamani watoto wale maradufu.
“Nimeshajua cha kufanya Anne atakufa kirahisi sana, tutatafuta msichana yeyote mteja wa madawa ya kulevya, tutampa pesa ili afanye kosa lolote na afungwe akiwa gerezani tutamwambia amtafute Anne mpaka ampate, akishampata tutampa sindano ya sumu ya ‘Heart stopper’amchome usiku akiwa amelala na kufa, hakuna mtu atakayegundua!”
Aliwaza Suzanne bila kujali mtu aliyekuwa akipanga kumuua alikuwa ndugu yake kabisa.
“Mimi sijali ni lazima afe na Anorld akija jioni nitamweleza mpango wangu!” Aliendelea kuwaza Suzanne.
Jioni mumewe aliporudi kutoka kazini watoto wakiwa wamelala Suzanne alimweleza mpango wake aliokuwa ameupanga, Anorld alicheka sana.
“Mbona unacheka?”
“Nimeamini kweli wewe ni komandoo!”
“Kwanini?”
“Una mawazo kama yangu!”
“Na wewe ulikuwa unawaza hivyo?”
“Ndiyo na tayari nimeshampata msichana wa kufanya hiyo kazi, anaitwa Zena atafanya vurugu yoyote ile leo na akitiwa ndani tutapigiwa simu!”
“Kweli?” Suzanne alieleza bila huruma.
“Wewe subiri alisema baada ya vurugu zake kwenye ukumbi wa disko wa Deluxe kesho lazima atapelekwa polisi, atatupigia simu!”
Waliongea mengi juu ya Patrick na Nancy lakini baadaye walipitiwa na usingizi na kulala fofofo! Walizinduka saa 12 asubuhi kengele ya simu pembeni mwa kitanda chao ilipoita, Anorld alinyoosha mkono akainyanyua na kuiweka sikioni.
“Ndiyo! Anorld hapa, nani mwenzangu?”
“Mh! Kituo cha polisi kati hapa?”
“Kuna nini tena ndugu yangu?”
“Kuna dada mmoja kakamatwa baada ya kupigana na polisi na kumchania shati lake Deluxe!”
“Haya nakuja sasa hivi!” Alijibu Anorld alishafahamu msichana huyo ni nani na ni kwanini alikuwa akiitwa kituoni!
“Suzanne! Suzanne! Suzanne!” Alimwita mkewe aliyeonekana kuwa katikati ya usingizi mzito.
“Vi...pi?”
“Tayari! Kazi imekwishaanza kutekelezeka!”
“Kweli?Umejuaje?”
“Nimepigiwa simu sasa hivi na polisi amka twende!”
Wote wawili walijiandaa na kutoka nje ambako walichukua gari na kukimbia haraka hadi kituoni ambako walipata nafasi ya kuongea na Zena!
“Naingia kazini hiyo milioni yangu niikute!”
“Usiwe na wasiwasi tutakuwa tumekuja kukutembelea gerezani kila Jumapili, ukishampata tu utuambie tutatumia ujanja wetu wote kukuletea hiyo sindano ya kumchoma nayo! Sawa?”
“Hakuna tatizo kabisa kaka Anorld kazi nitaifanya vizuri na kwa uangalifu!” Zena aliwaondolea wasiwasi.
Baadaye waliondoka haraka kurudi nyumbani kwenda kuwatayarisha Patrick na Nancy kwenda shule! Watoto hawakuwa na habari kabisa juu ya mpango uliokuwa unaendelea juu ya kumuua mama yao! Walijua kila kitu kiliendelea vizuri.
“Anti lini tutakwenda kumuona mama gerezani?”
“Jumapili!” Alijibu Suzanne akijua ni siku hiyo ndiyo yeye na mumewe wangekwenda kumwona Zena gerezani Butimba!
“Kweli?”
“Ndiyo!”
Gari la shule lilipokuja liliwachukua watoto na kuwapeleka shuleni, Suzanne na mumewe nao muda mfupi baadaye waliondoka kwenda kazini kwao.
****
Kijua kilikuwa kikichoma hali ya Mwanza siku hiyo ya Jumapili ilikuwa ya joto kidogo, ilikuwa rahisi kuifanananisha na Morogoro, siku hiyo Anorld, Suzanne, Patrick na Nancy waliondoka kuelekea gerezani Butimba ndani ya gari dogo la Anorld aina ya Cadillac! Watoto waliamini walikuwa wakienda gerezani kumwona mama yao kumbe Anorld na mkewe walikuwa na mpango tofauti kabisa vichwani mwao, walikuwa wakienda kumwona Zena na kumuuliza kama alifanikiwa kumpata Anne gerezani ili wakamilishe mpango wa kumuua.
Kitu cha kwanza kilichofanyika baada ya kufika gerezani Butimba kilichowashangaza pia watoto ni kuitwa kwa mwanamke mwingine badala ya mama yao ambaye hawakumtambua na Anorld kwenda kuongea naye pembeni kwa muda mrefu!
“Anti mbona mama humwiti? Muda wa kuona ndugu si utakwisha?” Patrick alimuuliza Suzanne lakini hakujibiwa kitu.
****
“Vipi Zena umefanikiwa kumpata?” Anorld alimuuliza Zena!
“Hapana tangu niingie hapa nimemtafuta lakini sijampata , nimejaribu hata kuulizia jina lake lakini sijampata si anaitwa Anne?”
“Aisee, basi subiri hapahapa kwani mwanamke atakayetoka sasa hivi kuongea na sisi ndiye huyo! Akija nitakuita nikutambulishe nikidai wewe ni dada yangu ili iwe rahisi wewe kuzoeana naye! Sitaongea na wewe tena ila Jumapili ijayo nitakuletea sindano ya sumu ndani ya ugali ambao hutatakiwa kuula kabisa! Cha kufanya kuanzia leo jaribu kumzoea sana ili nikileta sindano ukamilishe kazi!”
“Hiyo wewe usijali nionyeshe kwanza huyo marehemu mtarajiwa mwenyewe! Alisema Zena aliyeonyesha sura ya mtumiaji halisi wa madawa ya kulevya na pombe kali!”
Anorld aliondoka na kujiunga tena na familia yake, akamwacha Zena akiwa amesimama peke yake akisubiri kutambulishwa kwa Anne!’
“Anko mbona mama hatoki?”
“Subirini nilikuwa nasalimiana na anti yenu mwingine!”
“Mbona na sisi hatusalimiani nae?” Watoto walizidi kudadisi.
“Atakuja sasa hivi!” Alisema Anorld na kuondoka kwenda kuandikisha jina la Anne ili wamwone, haikuchukua muda Anne akatoka, watoto wake walimkimbilia na kumkumbatia kwa furaha! Kama ilivyokuwa kawaida yake Inzi wengi walikuwa nyuma yake na harufu mbaya ilisikika mara tu alipofika baadhi ya watu walianza kuhama eneo hilo!
Nguo zake zote zililowa na kugandamana na damu! Anne alisikitisha, pamoja na hali hiyo watoto wake hawakudiriki kumwacha walimkumbatia mpaka wakaangushana naye chini! Watu wote walishangaa na Anne alicheka kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu!
Hali ilipotulia waliketi chini na kusalimiana, Anne aliendelea kumshukuru sana Suzanne kwa wema aliokuwa akimfanyia kwa kuwalea watoto wake waliongea pia mengi juu ya maisha katika siku zilizopita kati yao!
“Huyu ndiye shemeji yako anaitwa Anorld ni mfanyabiashara hapa mjini!”
“Aisee nafurahi kukufahamu shemeji, huyu ni ndugu yangu kabisa ishi naye vizuri!”
“Hakuna tatizo shemeji pole na matatizo yaliyokupata!”
“Ulisema hujabarikiwa mtoto?” Anne aliuliza tena.
“Bado lakini Patrick na Nancy wanatufariji sana, tunajisikia vizuri kuishi nao nyumbani kwetu na tunasubiri umalize muda wako ili tuungane wote nyumbani kwetu!”
“Ahsanteni sana na kwa sababu kifungo kinahesabiwa usiku na mchana siku mbili tofauti nitakaa hapa kama miaka mitatu hivi!”
“Siyo muda mrefu utatoka tu!” Patrick alimwambia mama yake, Anne alishangazwa na busara iliyokuwemo ndani ya mtoto wake! Alikuwa ni marehemu mume wake tupu.
Waliongea kwa karibu saa nzima, wakamkabidhi zawadi walizomletea na kuondoka zao, Patrick na Nancy walisikitika kumwacha mama yao tena, lakini hivyo ndiyo ilivyokuwa.
****
Jumapili iliyofuata Anorld alinunua chupa ya sumu ya ‘heart stopper’ sumu kali ya kusimamisha moyo, aliinyonya na kuiweka ndani ya bomba la sindano, mkewe alipiga ugali mzuri na sindano hiyo ikazamishwa katikati ya ugali huo uliopozwa ili kuzuia bomba lisiyeyuke!
Anorld aliwasha gari na kwenda moja kwa moja hadi gerezani ambako alifanya mpango getini na kutoa kitu kidogo kwa maaskari akamkabidhi Zena chakula kile bila kukaguliwa.
“Humo ndani ndiyo ipo hiyo sindano baada ya kumchoma nayo, atakauka! Hapohapo usichelewe kimbia chooni ulitupe bomba la sindano! Si tayari mmeshazoeana?”
“Tayari na tunalala pamoja!”
“Fanya kweli basi!”
“Usiwe na wasiwasi tayarisha pesa yangu tu!”
Je nini kitaendelea?


HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 18
MTUNZI: ERIC JAMES SHIGONGO
“Utajiri bila watoto ni hasara, kumbe basi kipi bora? Watoto au mali?” Hilo ndilo swali alililojiuliza Anorld kila siku kichwani mwake! Alikuwa na kila kitu, mke mzuri mwenye mguu wa kuvutia, mwanya, rangi nzuri ya ngozi alikuwa mzuri pengine kuliko wanawake wote duniani.
Anorld alipata kila starehe iliyopo chini ya jua, kila mwaka wakati wa sikukuu za Krismasi ilikuwa ni lazima yeye na mke wake waende Canada kupumzika na kurudi mwanzoni mwa mwaka mpya! Kwao safari za visiwa kama Shelisheli, Comoro, Zanzibar kwenda kupumzika lilikuwa jambo dogo na la kawaida! Waliweza kufanya hivyo mara tano au sita kwa mwaka! Pesa ilikuwepo kilichotakiwa ni namna gani itumike.
Kifupi Suzanne na mume wake walikuwa na kila kitu kasoro kitu kimoja tu! Nacho ni mtoto, Suzanne kutokuwa na uwezo wa kuzaa ndio kuliwafanya wakose raha kidogo ya maisha katika ndoa yao pamoja na kuwa na kila kitu!
Mrithi wa mali ndiye alikuwa tatizo sababu wote walifahamu ilikuwa ni lazima siku moja wafe! Nani angebaki mrithi wa mali yao? Hilo ndilo swali liliwaumiza vichwa vyao kila siku, hivyo kuja kwa Patrick na Nancy katika maisha yao kulionekana kutoa jibu la tatizo hilo!
uzuri wa watoto hao uliwachanganya sana akili Suzanne na Anorld, Patrick na Nancy walikuwa watoto wazuri mno na hiyo ilitokana na mchanganyiko wa damu ya marehemu baba yao Huggins, walitamani watoto wale wawe wao! Roho ya dhuluma ilishawaingia mioyoni mwao, dhuluma ya watoto, viumbe hai, binadamu! Ilikuwa ni dhuluma kubwa lakini Suzanne na Anorld walikuwa wamedhamiria kuifanya bila uoga.
Ilikuwa si rahisi kuwapata watoto hao kama mama yao angetoka gerezani baada ya miaka mitano! Hivyo ili wawapate njia pekee ilikuwa ni kumwondoa Anne duniani akiwa hukohuko gerezani, walifahamu pengine baada ya Anne kufa wazazi wa marehemu Huggins au ndugu zake wengine wangeweza kujitokeza na kudai kuwachukua watoto, ni hilo pekee ndilo liliwatia hofu lakini walijua jinsi ya kulishughulikia.
“Pesa haishindwi kitu ni lazima watoto hawa wawe wetu, isitoshe sisi ni kama tumewasaidia katika maisha ni watoto wenye bahati kubwa sana hawa! Utajiri wote huu tuwaachie?’ Aliongea Anorld kwa uchungu!”
“Kwa kweli tumewasaidia!” Suzanne aliitikia.
Wakati maongezi hayo yakiendelea chumbani kwao Suzanne na Anorld waliaamini kabisa kuwa Patrick na Nancy walikuwa wamelala usingizi! Haikuwa hivyo kwani Patrick alikuwa macho akiendelea kumlilia mama yake, aliyoyaona gerezani siku hiyo yalimtia simanzi kubwa sana moyoni mwake.
Hali ya mama yake ilivyokuwa, alivyotoa harufu, alivyofuatwa na Inzi wengi kila alikokwenda, alivyokonda ilimuumiza sana moyo na kumfanya akose kabisa usingizi!Dada yake Nancy alikuwa tayari usingizini lakini Patrick hakupata hata lepe la usingizi mawazo yalikuwa mengi mno kichwani mwake, alishindwa kuelewa ingekuwaje siku ambayo mama yake angetoka gerezani. Aliamini hiyo ndiyo ingekuwa siku ya furaha kuliko zote maishani mwake.
Ghafla akiwa katika mawazo hayo alisikia maneno kutoka katika chumba cha Suzanne na Anorld hakuyaamini masikio yake ikabidi asikilize tena kwa makini zaidi lakini maongezi yaliendelea kubaki yaleyale!
“Watoto hawa watakuwa wetu tu! Si Anne anakufa usiku huuhuu! Ile sindano atakayochomwa itamkausha kama samaki!”
“Masikini Anne lakini inaniuma sana ndugu yangu kufa! Sina jinsi ya kuzuia hili lisitokee kwa sababu ninawataka sana Patrick na Nancy!”
Moyo wa Patrick uliruka mapigo mawili mfululizo, alisikia kama moyo wake unataka kusimama kufanya kazi.
“Ha! Mama yangu anakufa? Anakufa kwa nini?” Alijiuliza Patrick na kumwamsha dada yake aliyekuwa amelala fofofo!’
“Nancy!Nancy!Nancy! Tafadhali amka upesi!” Aliongea taratibu huku akimtingisha dada yake.
“Nini tena Patrick?”
“Amka usikilize wanavyoongea anko na anti Suzanne!’
“Wanaongea kitu gani?”
“Wasikilize tu!” Patrick alimwambia dada yake.
Wote wawili walisimama na kusogea dirishani na kuanza kusikiliza jinsi Anord na Suzanne walivyokuwa wakirufahia kifo cha Anne usiku huo, kifo cha sindano ya sumu aina ya Heartstopper ambayo Anne angechomwa na Zena usiku huo gerezani.
Wote wawili walimkumbuka dada zena waliyemwana gerezani siku hiyo, Nancy alishindwa kujizuia na kuanza kulia machozi tena kwa sauti ya juu, sauti hiyo iliwafikia Anorld na Nancy chumbani kwao na kutoka mbio kukimbilia chumbani kwa akina Nancy.
“Usithubutu kuwaonyesha kuwa tumeyasikia maongezi yao umenisikia?”Patrick alimwambia dada yake kabla hajafungua mlango kuruhusu Anorld na Suzanne waingie ndani.
“Vipi watoto wangu?” Suzanne aliuliza.
“Hakuna kitu ni Nancy alikuwa anaota ndoto ya kutisha!” Patrick alijibu wakati dada yake akiwa amelala kitandani na kujifunika na shuka hadi kichwani.
“Nancy!Nancy!Nancy! Vipi mwanangu?”
‘Mh!Mh!” Nancy aliguna na kuendelea kulia machozi chini ya shuka hakutaka kujifunua, alitii alichoambiwa na kaka yake. Baadaye Anorld na Suzanne waliondoka kurejea chumbani kwao ambako waliingia kitandani na kulala.
“Sijui wamesikia maongezi yetu hawa?” Anorld aliuliza.
“Ah! Wapi, haiwezekani!”
****
Nancy na Patrick hawakulala tena, waliendelea kulia wakimlilia mama yao! Walijua mama yao angekufa usiku huohuo kwa kuchomwa na sindano ya sumu, walijua wasingekuwa na mama tena duniani kuanzia asubuhi iliyofuata, walikuwa yatima tayari, walipoamka macho yao yalikuwa yamevimbiana kwa sababu ya kulia. Siku hiyo hawakujiweka tayari kwa shule kama ilivyokuwa kawaida yao jambo lililowapa Anorld na Suzanne wasiwasi kidogo.
“Mbona macho yenu yamevimba kiasi hiki?”
“Sababu ya kulia!”
“Kwanini mlie sana watoto wangu wazuri?”
“Kumbukumbu ya jana, mama alituumiza sana moyo!” Alijibu Patrick.
“Vaeni basi mwende shule sasa hivi au?”
“Mimi sijisikii hata kidogo kwenda shule anti, labda Nancy ajiandae!” Alijibu tena Patrick.
Nancy alipoulizwa naye alikataa walishapanga kutokwenda shule siku hiyo,walitaka kutoroka kwenda gerezani kuangalia kama kweli mama yao alikuwa amekufa.
“Haya chukueni hii pesa mtanununua soda mnywe sawa? Sisi tunakwenda kazini!” Alisema Suzanne na kuwakabidhi Patrick na Nancy noti ya shilingi 500.
“Ahsante anti!’ Aliitikia Nancy baada ya kuipokea noti hiyo mkononi mwake.
Suzanne na Anorld waliingia ndani ya gari na kuondoka kwenda kazini, nyuma Patrick na Nancy hawakutaka hata kupoteza dakika moja walichofanya ni kuvaa viatu na kuchomoka hadi nje ambako kabla ya kutoka mlinzi aliwauliza walikuwa wakienda wapi.
“Tunakwenda dukani kununua miswaki!”
“Ok! Nendeni basi lakini msichelewe kurudi!”
“Sawa babu!” Patrick aliitikia.
Walipofika nje walitembea hadi kituo cha daladala cha Nera ambako walipanda basi lililowapeleka hadi kitu cha mabasi ya kwenda Butimba karibu na kampuni ya Kauma, asubuhi hiyo walikuta basi moja likiwa limeegeshwa kituoni, wao ndio walikuwa abiria wa kwanza kupanda basi hilo na kusubiri abiria wengine walioanza kuingia mmoja baada ya mwingine mpaka likajaa na kuanza kuondoka.
Njiani Patrick na Nancy waliendelea kulia machozi wakimlilia mama yao, waliamini kabisa kuwa tayari Anne alikuwa maiti! Kwa maongezi waliyoyasikia kutoka chumbani kwa suzanne na Anorld ilikuwa si rahi si kuamini kuwa mama yao angekuwa hai.
“Sindano ya sumu! Yaani wamemuua mama yetu kwa sindano ya sumu? Huu ni unyama, kama walitutaka sisi ni kwanini wasingeongea tu na mama badala ya kumuua?’ Kwani mama angekataa kusema watuchukue, wakati hata uwezo wa kututunza kama mama angetoka gerezani hangekuwa nao?” Aliendelea kuwaza Patrick.
Watu wote ndani ya basi walishangazwa na kitendo cha watoto hao wawili kuendelea kulia , mzee mmoja alitaka kufahamu nini kilikuwa chanzo.
“watoto mbona mnalia tangu tuondoke kituoni?’
“Mama yetu amekufa!”
“Amekufa wapi?”
“Gerezani Butimba?’
“Nani amewapa taarifa hizo?”
Patrick na Nancy walishindwa kujibu swali hilo na kujikuta wakiendelea kulia machozi tu.
“Nielezeni basi?”Mzee yule aliendelea kuwabembeleza waseme lakini hawakufanya hivyo!
Gari lilipofika gerezani Butimba Patrick na Nancy waliteremka na kunyoosha hadi gerezani lengo lao likiwa ni kufahamu kama kweli mama yao alikuwa amekufa au la! Watu wa kwanzakukutana nao walikuwa ni maaskari walinzi wa gereza.
“Nyie watoto mnakwenda wapi asubuhi hii?’
“Tumekuja kumwona mama yetu!”
“Mama yenu nani?”
“Anne!”
“Ni mfungwa wa mahabusu!”
“Amefungwa miaka mitano!”
“Leo siyo siku ya kuona wafungwa, njooni jumamosi au Jumapili siyo leo mnasikia?”
“Hapana tunataka kumwona mama yetu, tunataka kujua yupo hai au amekufa!”
“Kwani mmeambiwa amekufa?”
“Ndiyo tunafahamu amechomwa sindano ya sumu!”
“Sindano ya sumu nani kamchoma?”
“Mfungwa mwenzake anaitwa Zena! ”
“Nyie watoto mbona siwaelewi, mnaongea jambo kubwa sana hilo hebu jaribuni kunieleza vizuri!” Askari huyo aliwachukua na kuwapeleka pembeni ambako walianza kumsimulia kila kitu kilichotokea na jinsi walivyosikia sauti ya Suzanne na Anorld wakiongea, pia jinsi sindano hiyo ilivyoingizwa gerezani ndani ya ugali.
“Mh! Jambo hilo linawezekana kweli?” Alihoji askari wakati bado akijaribu kutafakari jambo hilo lango la gereza lilifunguliwa na maiti ya mtu ikiwa imefungwa ndani ya shuka jeupe ilipitishwa mbele yao na kupakiwa ndani ya gari.
“Haya maafande waliochanguliwa kwenda kuzika maiti hii pandeni haraka ndani ya gari tuondoke!” aliamuru askari magereza mmoja mwenye V tatu begani. Maaskari kama kumi hivi walipanda ndani ya garini haraka tayari kwa kuondoka.
Tayari Patrick na Nancy walikuwa na uhakika kabisa kuwa maiti iliyopakiwa ndani ya gari ilikuwa ni mama yao,walianguka chini na kuanza kulia machozi, wakiliita jina la mama yao na kuwatupia lawama Suzanne na Anorld kwa kitendo chao cha kinyama!
Kelele hizo ziliwafanya maaskari wangine zaidi washtuke na kulazimika kuwafuata Patrick na Nancy na kuwadadisi zaidi, maelezo yao yalitosha kuwafanya maaskari waamini kweli aliyekufa alikuwa ni mama yao.
“Wapandisheni ndani ya gari wakalione kaburi la mama yao ili kama wakitaka kuwapeleka ndugu zao wawapeleke baadaye!” Alisema dereva.
Patrick na Nancy walipandishwa ndani ya gari na safari ya kwenda eneo la Mkolani nje kidogo ya mji wa Mwanza kwa mazishi ilianza, njia nzima waliendelea kulia, katika maisha yao hawakuwahi kuishi na mama yao kwa muda mrefu lakini walimpenda na alikuwa kila kitu kwao.
Walimtegemea baada ya miaka michache tu baadaye angekuwa huru pamoja nao lakini sasa maisha ya kipenzi chao yalikuwa yamekatishwa kinyama na Anorld na Suzanne sababu tu ya kutaka kumdhulumu watoto alizaa mwenyewe!
“Huu ni ukatili na Mungu atawalipia anti na anko!” Nancy alisema kwa uchungu.
“Na sitaki tena kurudi nyumbani kwao ninakwenda mwenyewe nitakako! Nitakuwa hata chokoraa lakini sipo tayari kurudi kwao tena wauaji wakubwa wale!” Alifoka Patrick.
Walipofika makaburini shimo lilishachimbwa tayari na bila hata kuruhusiwa kutoa heshima zao za mwisho au kuiona sura ya mama yao kwa mara ya mwisho, maiti ilitupwa shimoni na kuanguka kama mzigo! Shimo likaanza kufukiwa na udongo, Patrick na dada yake walilia hadi sauti zao kukauka lakini hawakuubadili ukweli kuwa mama yao alikuwa amekufa.
Baada ya mazishi walipakiwa ndani ya gari na safari ya kurudi gerezani ilianza tena ambako waliachiwa na kuingia mitaani, hawakurudi tena nyumbani kwa Anorld na Suzanne kama walivyokuwa wameamua, waliwaona ni wauaji ambao wangeweza kuwachinja hata wao wenyewe.
****
Jioni ya siku hiyo Suzanne aliwahi kurudi kutoka kazini kabla ya Anorld na dakika kama ishirini tu tangu aingie ndani ya nyumba yake, maaskari watatu walibisha hodi mlangoni aliwakaribisha sebuleni lakini hawakukakaa sana kabla hawajamwambia shida yao.
“Mama sisi ni maafisa wa polisi na hivi tunavyoongea na wewe upo chini ya ulinzi unahitajika kituoni mara moja!”
“Nimefanya nini?” Aliuliza Suzanne.
“utaelezwa hukohuko, mumeo yupo wapi?”
“Yupo kazini bado hajarudi!”
“Tutamfuata baadaye!”
“Labda nimjulishe arudi upesi?”
“Hapana!” Alijibu askari mmoja na kumpiga pingu za mikononi Suzanne akaanza kusukumwa kumtoa nje ya nyumba yake!
Alipelekwa moja kwa moja hadi kituo cha polisi ambako alifahamishwa wazi kuwa yeye na mumewe walikuwa wakituhumiwa kuingiza sumu gerezani na kusababisha kifo cha mfungwa mmoja!
Ndugu na marafiki waliofika baadaye polisi kutaka kujua sababu ya kukamatwa kwa Suzanne waliporudi majumbani kwao walimpigia simu Anorld ambaye alishapata taarifa na kujificha eneo la Nyamanoro kwa rafiki yake na kumjulisha sababu ya kukamatwa kwa mkewe na sababu iliyopelekea hilo!
“Nendeni kwanza mkaangalie nyumbani kama wale watoto wapo?” Anorld alishauri.
“Sawa!” Alijibu Jesca dada yake Anorld na bila kuchelewa alichukua gari la mama yake na kwenda nalo moja kwa moja hadi nyumbani kwa Anorld.
Alipofika nyumbani kwa kaka yake ilikuwa tayari yapata saa sita na nusu ya usiku na kukutana na mlinzi wa nyumba hiyo.
“Vipi babu akina Patrick na Nancy wamerudi?”
“Hata mimi nashangaa sijui wapo wapi siyo kawaida yao hata siku moja kukaa nje hadi saa hizi za usiku, sijui nao wamekamatwa?” Alihoji mlinzi.
“Hapana! Sijui mahali walipo! askari wamekuja tena?” Jesca aliuza.
“Nafikiri kila baada ya dakika kumi hivi wanafika na ninaona ni heri uondoke sababu wakikukuta hapa halafu itakuwa taabu!”
*****
Jesca aliondoka kurejea nyumbani ambako alimpigia tena simu Anorld na kumtaarifu hali halisi ilivyokuwa.
“Ninajua wazi hao ni Patrick na Nancy tu hakuna mwingine na nitawatafuta usiku huu huu hadi niwapate! Wamenichomea polisi watanitambua watoto hawa!” Alisema Anorld na baada ya kukata simu alimpigia msaidizi wake ambaye alitayarisha magari madogo kumi kwa ajili ya msako wa kuwatafuta watoto usiku huo.
“Je kama wamelala nyumbani kwa mtu?”
“Hawana ndugu yeyote hapa jijini na jua watakuwa wamelala sehemu fulani mitaani na ninafikiri maeneo ya hukohuko Butimba, mkikosa huko jaribuni kwenye makaburi ya Mkolani ambako wafungwa huzikwa kwa uchungu walionao ni lazima watakuwa wamelala juu ya kaburi la mama yao!”
*****
Usiku huohuo wa baridi kali huku manyunyu ya mvua yakidondoka, Patrick na Nancy walilala juu ya kaburi waliloamini ni la mama yao! Walikuwa bado wakimlilia mama yao kwa uchungu sana na kukilaani kitendo cha Suzanne na Anorld.
Hawakuwa na ufahamu wa jambo lolote lililoendelea mjini Mwanza kwa wakati huo, wala hawakuwa na hisia za kusakwa ili wauawe.
Patrick na Nancy wakiwa hawana hili wala lile mara ghafla walisikia muungurumo wa gari na kuona mwanga mkali wa taa za gari ukikatisha kutoka barabarani kuelekea makaburini kila mmoja wao alishtuka.
“Mh!nini tena? Lakini hawa wanaweza kuwa majambazi au watu wamekuja kufanya uchawi wao makaburini!”
“Sasa tufanye nini?” Nancy alimuuliza kaka yake wakati gari likizi kukaribia zaidi!
“Njooni huku tujifiche!” Patrick alisema huku akimvuta dada yake kuelekea Kwenye nyasi ndefu zilizokuwepo jirani yao wakiwa katika nyasi hizo walishuhudia gari likiegeshwa na watu watano kushuka, pamoja na kuwa giza walipojaribu kuziangalia sura za watu wale waliitambua sura ya mtu mmoja na hata sauti ilikuwa ya Anorld!Moyo wa Patrick ulilipuka, watu wote walikuwa na bunduki mikononi!
“Tafuteni kaburi la leo! Watakuwa wamelala hapohapo!” iliamrisha sauti ya Anorld.
Tochi zilimulika kila mahali hatimaye wakalifikia kaburi la siku hiyo.
“Hili hapa!” Alipiga kelele mtu mmoja!”
“Wapo?”
“Hawapo? Ila kuna miguu ya watoto hii hapa juu! Inavyoonekana walikuwa hapa muda si mrefu!”
“Inaeelekea wapi?”
“Porini!”
“Fuatilieni huko huko porini na mkivipata hivyo vitoto ueni kabisa ili kupoteza ushahidi, maana hivyo vitajidai vishahidi maana ndivyo vilisikia maneno yangu!” Aliamuru Anorld.
“Sawa bosi!”
****
mauaji yalivyotokea gerezani:
Usiku wa manane Anne akiwa amelala fofofo, Zena aliyekuwa pembeni yake alipohakikisha kuwa asingeweza kushtuka alinyanyuka na kwenda hadi chooni ambako alilificha sufuria lililokuwa na ugali darini, alilichukua na kushuka nalo hadi chini ambako alianza kuusambaza ugali na kulitoa bomba la sindano.
“Yes! Kazi imekamilika mwisho wa maisha yake umefika! NI lazima nimuue nikachukue pesa yangu” alisema Zena.
Aliliangalia bomba la sindano na kuona lilikuwa limejaa vizuri sumu ambayo ingeukausha mwili wa Anne kama alivyokuwa ameambiwa na Anorld.
“Mimi sijali kuondoa maisha ya mende kama Anne ili mradi nimepewa pesa!” Alinong’ona Zena.
Je nini kiliendelea?
Je Nancy na Patrick walipatikana?

Post a Comment

Previous Post Next Post