Kama ilivyo kawaida ya gereza lolote chakula huwa kidogo na mara nyingi hakifai wala hakiwezi kulinganishwa na chakula cha nyumbani na kwa kawaida wafungwa hula mara moja kwa siku, hivyo siku zote huwa ni watu wenye njaa!
Akiwa na bomba la sindano mkononi Zena alianza kupiga hatua kuelekea mahali alipolala Anne, alikuwa amedhamiria kuyakatisha maisha yake kwa sababu ya pesa! Hatua kama tano mbele aliikumbuka sufuria la ugali aliloliacha chini, aligeuka kuliangalia na kukuta liko palepale.
“Hili sufuria na ugali wake litaniletea taabu wacha nilirudishe kwanza darini ndiyo nije niendelee na kazi yangu!” Aliwaza Zena na kumwangalia Anne aliyekuwa amelala sakafuni akiendelea kukoroma taratibu.
Bila kuchelewa wala kusita Zena alikata kona akiwa na bomba lake mkononi kulifuata sufuria la ugali, alilibeba na kuanza kutembea kuelekea nalo chooni! Mbele kidogo hisia za ajabu zilimwijia, mate yakaanza kumdondoka! Alijisikia njaa ya ajabu, hakuwa kusikia njaa namna hiyo katika maisha yake, aliutamani ugali aliokuwa ameubeba na kujikuta akiyapuuzia maneno aliyoambiwa na Anorld kuwa asiutie mdomoni ugali huo.
Aliuangalia ugali ule na kuzidi kuutamani mdomo wake ulitaka sana aule lakini akili yake ilishindana sana na mawazo hayo. Zena alijikuta njia panda bila kujua la kufanya, ghafla alijikuta akiliweka bomba la sindano chini na pamoja na kuwepo harufu kali chooni alianza kuula ugali huo kwa juujuu bila kuingia ndani ambako bomba la sindano lilifukiwa kabla hajalitoa.
“Hata kama ni sumu huku juu haiwezi kuwa imefika ni lazima itakuwa humohumo ndani lilipokuwa bomba!” Alijipa moyo Zena na kuendelea kula ugali huo lakini dakika tano baadaye alianza kusikia kizunguzungu na baadaye macho yake yalianza kuona kiza, misuli ikaanza kukamaa na kubana kama ambavyo hutokea kwa mcheza mpira, maumivu ya misuli yalikuwa makali mno kabla hajaanza kulia alianguka chini na kupoteza fahamu hakujua tena kilichoendelea.
Saa kumi na moja alfajiri Anne alizinduka usingizini na kuanza kumwamsha mfungwa aliyelala jirani yake akidhani ni Zena.
“Mimi sio Zena!”
“Zena yuko wapi?”
“Aliondoka usiku wakati wewe umelala na hakurudi tena sijui yuko wapi?”
Kabla hawajaendelea sana na maongezi yao mara walisikia kelele za mtu kutoka chooni, wote wawili walishtuka wakanyanyuka na kukaa.
“Jamani!Jamani!Jamani! Mtu kafia chooni!” Alipiga kelele mtu huyo akikimbia kutoka chooni kwenda katika ukumbi waliolala wafungwa.
Baada ya kusikia kelele hiyo wafungwa wote walinyanyuka sakafuni walikokuwa wamelala na kuanza kumfuata mwanamke aliyekuwa akipiga kelele ili kumuuliza vizuri juu ya jambo alilokuwa akilisema.
“Yuko wapi huyo mtu aliyekufa?” Anne aliuliza hakuwa na wasiwasi kuwa mtu huyo angeweza kuwa Zena.
“Yupo chooni ingieni wenyewe mkaone!”
Anne aliongoza kundi la wafungwa kuingia ndani ya choo, hakuyaamini macho yake kukuta aliyenguka chini ni Zena!
Bomba la sindano na sufuria la ugali vikiwa pembeni mwake, hakuamini kama alikuwa amekufa palepale alipiga magoti chini na kuanza kumtingisha akimwita jina lakini Zena hakushtuka alipogusa moyo wake pia ulikuwa umesimama kabisa ni hapo ndipo alipoamini Zena alikuwa amekufa!
Kila mfungwa alihisi Zena alikuwa amejiua mwenyewe kwa kujichoma sindano ya madawa ya kulevya lakini walipoliangalia bomba la sindano lilikuwa limejaa dawa mpaka juu jambo lililoonyesha wazi kuwa alikuwa bado hajajichoma kwa sindano ile.
Anne aliangua kilio, alilia mpaka akaanguka chini na kuzimia! Ikabidi wafugwa wenzake wamtoe nje na kummwagia maji ndipo akazinduka tena, alikuwa akimlilia rafiki yake mpendwa Zena waliyekutana naye hapohapo gerezani.
Hakuwa na habari hata kidogo juu ya jambo ambalo Zena alipanga kumfanyia usiku wa siku hiyo, bila Zena kuula ugali ni lazima yeye Anne ndiye angekuwa marehemu wakati huo! Aliendelea kumlilia Zena mpaka mkuu wa gereza alipokuja na kuamuru mwili wa Zena uondolewe chooni na kupelekwa zahanati ambako ulihifadhiwa.
Pia ugali na bomba la sindano vilivyokutwa pembeni kwa Zena viliondolewa na kuhifadhiwa kwa uchunguzi asubuhi ya siku hiyo, kila mtu alichanganyikiwa na kifo cha Zena, mkuu wa gereza na daktari wa gereza walishindwa kuelewa ni dawa gani iliyokuwa ndani ya bomba la sindano alilokutwa nalo Zena na walishindwa kuelewa alilipata wapi akiwa kama mfungwa.
Kulipokucha asubuhi bomba la sindano pamoja na ugali vilichukuliwa na kupelekwa moja kwa moja hadi hospitali ya Bugando ambako vyote vilifanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa bomba la sindano pamoja na ugali vilikuwa na sumu aina ya ‘Heartstopper’ ambayo kazi yake ni kuusimamisha moyo kufanya kazi!
Kila mtu aliamini Zena alikuwa ameamua kujiua mwenyewe kwa sumu hiyo mbaya, hakuna mtu hata mmoja aliyehisi kuwa sumu ile iliingizwa gerezani kwa lengo la kumuua Anne na si Zena.
Nani aliingiza sumu ile gerezani ndilo lilibaki kuwa swali la kila mtu, mkuu wa gereza alichanganyikiw
a na kuamuru kufuatilia ni nani aliyeingia ugali ule ndani ya gereza. Kwa sababu ya umaarufu wa Anorld haikuchukua muda mrefu kugundua kuwa ni yeye ndiye aliyeleta chakula hicho.
Mkuu wa gereza alitoa taarifa hiyo polisi ambao bila kuchelewa walianza msako wa kumtafuta Anorld kama mtuhumiwa namba moja wa mauaji hayo! Polisi walipokwenda kwake hawakumkuta na kulazimika kumkamata mke wake Suzanne na kumweka mahabusu wakati msako wa kumtafuta Anorld ukiendelea.
Mipango ya mazishi kwa taratibu za gereza ilianza kuandaliwa ili mwili wa Zena uzikwe lakini mara tu baada ya maiti yake kupakiwa ndani ya gari watoto wawili mapacha Patrick na Nancy waliwasili gerezani, habari waliyoitoa kuwa waliwasikia Anorld na mkewe wakipanga jinsi ya kumuua mama yao ili wamdhulumu watoto wake ilizidi kuwahakikishia kuwa ni Anorld na Suzanne ndiyo waliofanya mauaji hayo.
*****
Msako wa Patrick na Nancy porini:
“Fuatilieni hukohuko porini na mkivipata hivyo vitoto viueni kabisa ili kupoteza ushahidi, maana hivyo ndivyo vitajidai ni mashahidi mahakamani sababu ndivyo vilisikia maneno yangu!” Aliamuru Anorld.
Maneno hayo yalimfikia Patrick moja kwa moja mahali alipokuwa amejificha, hofu kubwa ilimwingia moyoni mwake alijua mwisho wao ulikuwa umefika kama tu wangeingia mikononi mwa watu waliokuwa wakiwatafuta. Alishindwa kuelewa ni kwanini Anorld na mama yao mdogo Suzanne walikuwa wameamua kuwageuka kiasi hicho.
Hawakuwa na mahali pa kukimbilia walijua kwa vyovyote vile wangekamatwa tu! Kwani miale ya kurunzi za majambazi ilimulika kila mahali, mahali walipolala katikati ya nyasi hapakuwa mbali sana na makaburi na kama wangejaribu kusimama wima ni lazima wangeonekana.
Nancy alijua pia kuwa yeye na kaka yake walikuwa katikati ya hatari, walikuwa katikati ya kifo na maisha! Kama mtoto wa kike hakuna alichokijua zaidi ya kulia na kuzidi kumkumbatia kaka yake akimuuliza kipi wangefanya ili kujiokoa.
“Patrick! Patrick!Patrick!” Aliita lakini kaka yake hakumwitikia.
Alianza kumtingisha lakini Patrick hakuonekana kushtuka wala kujibu kitu chochote!Alikuwa kimya kabisa na mwili wake ulikuwa wa baridi kupita kiasi, Nancy alishindwa kuelewa ni nini kilimpata kaka yake, alishindwa kuyazuia machozi yalianza kumiminika huku tochi zikimulika kuelekea mahali walipokuwa wamejificha.
“Patrick!Patrick!Amka twende, mbona umekaa kimya?” Alizidi kusema Nancy lakini Patrick hakushtuka wala kuongea kitu chochote alionekana kama mtu aliyekufa na Nancy alishindwa kuelewa alikuwa hai au la!
“Patrick usife kaka yangu! Usiniache peke yangu ninakuhitaji tutoroke pamoja! Bila baba, bila mama, bila wewe nitaishije mimi?” Alisema Nancy huku akibubujikwa na machozi.
Tochi zilizidi kumulika katikati ya nyasi walipojificha, hofu ilizidi kumwingia Nancy na mwili wake ulikufa ganzi kabisa, alijikuta akiwa tayari kwa kifo au lolote ambalo lingetokea.
“Nasikia minong’ono sehemu hizi sijui viko wapi? Mara mbili nimesikia sauti ikiita Patrick!Patrick sijui tuko wapi hutu tutoto!” Alisema mmoja wa majambazi.
“Mulika sehemu ambako umesikia minong’ono inatokea! Ni lazima hawa watoto wauawe!” Anorld alizidi kuamuru na majambazi walizidi kuzikanyaga nyasi ndefu katika kuwatafuta Patrick na Nancy.
Patrick aliendelea kuwa kimya na Nancy aliendelea kutetemeka mwili mzima, dakika chache baadaye wazo lilimwijia kichwani mwake akaamua kusogea mbele, kwa sababu hakuwa na uwezo wa kumbeba kaka yake aliamua kumvuta katikati ya nyasi ni kelele za nyasi zilizowashtua majambazi mpaka wakagundua mahali walipokuwa wamejificha.
“Hivi huku!” Alipiga kelele mmoja wa majambazi baada ya kusikia mlio wa kitu kikivutwa katikati ya nyasi na majambazi wote walikimbia kuelekea eneo hilo na tochi zao.
*****
Ilikuwa ni saa tisa alasiri siku hiyo baada ya kazi ya kupasua kuni, Anne na wafungwa wenzake walikaa ndani ya gereza wengine wakiimba nyimbo za kumsifu Mungu, mpaka wakati huo Anne alikuwa bado akilia machozi sababu ya kifo cha Zena, alikuwa bado hajauelewa ukweli, mara ghafla askari magereza wa kike alisimama mlangoni.
“Kuna mfungwa anaitwa Anne humu ndani?” Aliuliza askari huyo.
“Ndiyo! Ni mimi afande!” Anne aliitikia.
“Unaitwa ofisini kwa mkuu wa gereza mara moja!”
Anne alisimama na kuanza kukimbia kutoka nje ya gereza na kwenda moja kwa moja hadi ofisini kwa mkuu wa gereza. Mkuu wa gereza alikuwa mzee wa makamo kati ya miaka 45-50, mweusi na kichwa chake kilijaa mvi nyingi, alikuwa ni mwenyeji wa Kigoma na sura yake ilitisha kidogo.
Hakuna mtu aliyemuogopesha Anne katika maisha yake kama mkuu huyo wa gereza! Hakutaka hata kumwona na kwa kuitwa kwake ofisini siku hiyo alijua wazi kulikuwa na tatizo kubwa sana ambalo kwa vyovyote lingepelekea kuongezwa kifungo, ilikuwa si kawaida kwa mfungwa kuitwa ofisini kwa mkuu wa gereza.
“Sijui nimekosa nini tena mie? Sijui wamebadilisha tena kifungo changu?” Anne alijiuliza maswali mengi kabla hajafika ofisini kwa mkuu wa gereza.
“Unaitwa nani?”
“Mimi?”
“Wewe ndiyo!”
“Ninaitwa Anne!”
“Unatakiwa kuhama gereza hili na utapelekwa gereza la Keko jijini Dar es Salaam! Hivyo utaondoka hapa Butimba kesho asubuhi!” Mkuu wa gereza alisema.
Anne alikaa chini na kuanza kulia machozi akimwomba Mkuu wa gereza abadilishe uamuzi huo kwa sababu alikuwa na watoto ambao wangependa kumwona mara kwa mara.
“Mungu wangu watoto wangu watanionaje huko Dar es Salaam baba? Nihurumie tafadhali” Alisema Anne, hakujua jambo lolote lililokuwa likiendelea nje ya gereza juu ya watoto wake.
Je, nini kitatokea?
Anne atakubaliwa kubaki gerezani Butimba?
Na je huko porini Patrick kafa au yupo hai?
Na je watakamatwa?
HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 20
MTUNZI: ERIC JAMES SHIGONGO
Suzanne aliwekwa maabusu kwa karibu masaa mawili akihojiwa mahali alipokuwa mumewe Anorld, mahojiano hayo yaliambatana na mateso makali akilazimishwa kusema ukweli, Alivumilia kwa muda lakini baadae alishindwa na kutoboa mahali ambako alifikiri mumewe angeweza kuwa amejificha.
Kilichofanywa na polisi ni kumchukua ndani ya gari hadi nyumbani kwa dada yake ambako waliwachukua watu watatu akiwemo dada yake na Anorld na kwenda kufanya nao mahojiano kituoni, nao waliteswa sana mpaka kufikia mpaka wakataja kila kitu kilichoendelea.
“Wamekwenda kuwatafuta wale watoto ili wawaue kwa sababu wanaamini ni wao ndio waliowaeleza nyinyi juu ya mpango wa kumuua mama yao!” Dada yake Anorld aliyasema maneno hayo mbele ya Suzanne baada ya kubanwa mikono na koleo!
“Wewe uliufahamu vipi mpango huo?”
“Nilimsikia kaka akisema kwa hasira baada ya kusikia mmemkamata mke wake, alisema ni lazima Patrick na Nancy wafe kwani ndio waliotoboa siri hiyo nilipomuuliza juu ya siri hiyo alinieleza kila kitu!”
“Kwa hiyo wamekwenda kuwatafuta wapi?”
“Taarifa nilizonazo wamekwenda katika makundi mawili, moja linazunguka mitaani na jingine limekwenda makaburini ambako mwili wa marehemu umezikwa wanaamini watoto hao watakuwa huko!”
“Yeye Anorld amekwenda na kundi gani?”
“Amekwenda na kundi lililokwenda makaburini!”
“Ok ahsante!” Alijibu mkuu wa kituo na kuwaamuru maaskari waliokuwa karibu kuwaweka Suzanne na watu wengine waliowakamata mahabusu!
“Tunaondoka kwenda makaburini Sawa, fanyeni hivyo haraka!” Aliendelea kusema Mkuu wa kituo cha Polisi cha kati mjini Mwanza.
“Sawa Afande!” Waliitikia Maaskari wote.
Mkuu wa kituo na Maaskari wengine kumi na tano waliingia ndani ya magari matatu ya polisi na safari ya kwenda makaburini kumsaka Anorld na kundi lake lilianza.
Walipolikaribia eneo la makaburini Mkuu wa kituo alisimamisha gari lake na kushuka.
“Vijana tumekaribia eneo lenyewe, tafadhali wekeni silaha zenu tayari na taa za magari yote zizimwe!”
“Sawa afande!”
“Si mnayafahamu makaburi yenyewe?”
“Ndiyo tunayafahamu!”
“Ok!”
Baada ya kusema maneno hayo safari iliendelea kuelekea makaburini, taa za magari zikiwa zimezimwa na magari yakiendeshwa kwa mwendo wa taratibu ili sauti ya miungurumo yake isisikike, mita kama mia nne hivi kutoka makaburini magari yote yalisimamishwa na maaskari wote wakashuka na bunduki zao mikononi.
“Magari yote yabaki hapa na maaskari watano wazunguke upande huu na wengine watano wapite upande huu na tutakaobaki twende moja kwa moja, nafikiri kama wapo hapa tutawakamata sababu tutakuwa tumewaweka kati!”
“Ni lazima tuwakamate kabla hawajawaua watoto! Askari mwingine aliitikia na wote walisonga mbele.
******
Makaburini
Tochi zilizidi kumulika kila upande wa msitu wa nyasi ambamo Patrick na Nancy walijificha, majambazi waliwatafuta ili wawaue watoto wale wasio na hatia, Anorld huku akitetemeka kwa hasira alizidi kuamrisha juhudi za kuwatafuta ziongezeke! Nancy aliisikia sauti ya Anorld na kuzidi kuogopa, alizidi kulala juu ya mwili wa kaka yake bila kujua la kufanya.
Alijua ni lazima wangekamatwa na kwa uhakika hata yeye angekufa kama alivyokuwa kaka yake! Aliamini asilimia mia moja Patrick hakuwa hai! Roho ilimuuma sana na kujikuta akitokwa machozi ya huzuni.
Alishindwa kuelewa kama Anorld aliyewatunza na kuwalea akiwapa kila kitu ndiye aliyekuwa akiwatafuta ili awaue, lilikuwa si rahisi kulikubali na mpaka wakati huo Nancy alikuwa haamini juu ya mambo yaliyomtokea, alifikiri ilikuwa ni ndoto.
Patrick alikuwa bado amelala akiwa kimya kabisa kama mfu. Nancy alijua tayari kaka yake alikuwa maiti, hivyo alikuwa amebaki peke yake duniani ilikuwa ni lazima apambane na maisha mwenyewe na akujua angeyaanza vipi mapambano hayo! Alipoliwaza hilo ndio alizidi kububujikwa na machozi zaidi, hakujua maisha yangeendeleaje baada ya siku hiyo bila kaka yake na pacha wake Patrick.
Hakuwa na mama, hakuwa na baba na kwa historia aliyopewa ndugu zake wawili walifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha ni bibi yao aliyedaiwa kufanya uchawi kuwaua na alipotaka kuwaua wao Patrick na Nancy kwa uchawi huo huo mama yao Anne aliamua kumuua kabla hajatekeleza nia yake ni jambo hilo ndilo lilimfanya aingie gerezani.
Wakati akiyawaza hayo huku akilia, tochi zilizidi kuelekea mahali alipokuwa, mwili wake wote ulikufa ganzi na hakujua angefanya nini kuokoa maisha yake kwa sababu ndugu yake tayari alishakufa!
“Vitoto hivi vipo wapi jamani?” Aliuliza mmoja wa majambazi
“Vipo maeneo haya haya tu!” jambazi mwingine alijibu.
Ghafla lilimwijia wazo kichwani mwake akiwa katika kutafuta kujiokoa, alianza kumvuta kaka yake katikati ya nyasi kutafuta mahali pengine pa kujificha, ni kelele ya nyasi ndiyo iiyowashtua majambazi na kujikuta mmoja wao akipiga kelele.
“Jamani wale watoto hawa hapa!” Alipiga kelele mmoja wa majambazi na kelele hiyo ilisababisha majambazi wengine wote wakimbilie eneo hilo, kwa hofu bila kufikiria mara mbili Nancy alijikuta akinyanyuka na kuanza kukimbia katikati ya nyasi akiwa ameinama.
Risasi kama tano hivi zilimfuata nyuma yake lakini bahati ya Mungu zote zilimkosa! Akazidi kutokomea katikati ya nyasi, ni milio hiyo ya risasi ndiyo iliyowafanya maaskari waliokuwa karibu na eneo hilo waweke tayari silaha zao, ilikuwa ni milio ya bunduki aina ya SMG wakati wao walikuwa na bunduki aina ya RPG! Walijua wazi kuwa milio ile haikuwa ya bunduki za zao.
Majambazi wakiongozana na Anold walizidi kumkimbiza Nancy porini, lakini mbele kidogo Nancy alijikuta akitumbukia ndani ya shimo refu lililoonekana kuwa ni kaburi ambalo halikutumika, shimo hilo lilikuwa katikati ya nyasi nyingi kiasi kwamba majambazi hawakufanikiwa kumwona alipotumbukia.
“Kakimbilia wapi?”
“Sijui!”
“Lakini si vilikuwa vitoto viwili?”
“Ndiyo lakini kitafuteni tu ndiyo hicho kimoja kimalizeni kwanza halafu tukitafute kingine, sawa?” Anorld aliendelea kutoa amri.
“Hakionekani tena!” Alijibu mmoja wa majambazi.
Nancy aliyasikia maneno hayo akiwa ndani ya shimo lenye urefu kama futi 5 hivi yalizidi kumuogofya. Alitetemeka sababu ya hofu na baridi kali iliyokuwepo, alizidi kulia machozi na hali ya kukata tamaa iliutawala moyo wake, hakujua ni kitu gani kingeendelea dakika chake baadae! Kwa mara nyingine alimkumbuka mama yake
Alipomfikiria Patrick na mahali alipomwacha roho ndiyo ilizidi kumuuma zaidi, alitamani kutoka shimoni ili nae auawe kama alivyokufa kaka yake, lakini alishindwa kutoka shimoni kwa sababu hapakuwa na mahali popote pa kushika kama msaada wa yeye kutoka nje.
Kilichofuata Nancy akiwa shimoni ni milio mingi ya risasi, alishindwa kuelewa ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Alisikia sauti za watu wakilia na vishindo vya watu wakikimbia huku na kule vilisikika, Nancy hakupata jibu la kilichokuwa kikiendelea juu ya shimo hilo! Alihisi kulikuwa na mapigano makali sana yakiendelea.
Dakika kama arobaini na tano hivi baadae hali ilitulia kukawa na ukimya wa ajabu, alisikia kitu kama mizigo ikiburuzwa juu ya ardhi na watu ikivutwa na watu waliokuwa wakinong’ona .
“Tumewamaliza na kama Anorld asingenyoosha mikono juu naye tungemmaliza pia!” Nancy aliwasikia watu hao wakiongea.
******
Mapigano kati ya polisi na majambazi aliokuwa nao Anorld yalikuwa makali kupita kiasi, majambazi wote isipokuwa Anorld walipigwa risasi na kufa papo hapo, kilichomuokoa Anorld ni kujisalimisha mbele ya polisi, maiti za majambazi aliokuwa nao zilichukuliwa na polisi kupelekwa chumba cha maiti cha Bugando ambako ziihifadhiwa .
Hakuna askari hata mmoja aliyepoteza maisha yake katika mapambano hayo, maaskari waliuona huo kama ushindi mkubwa na hakuna askari hata mmoja aliyekumbuka kuwepo kwa watu wengine zaidi ya majambazi katika makaburi hayo, wote walisahau kuwa majambazi waliwafuata Patrick na Nancy.
*****
Asubuhi kulipokucha taarifa za kuuawa kwa Anorld zilishasambaa mji mzima wa Mwanza, redio na televisheni zilitangaza juu ya mauaji hayo yaliyounganishwa na mauaji yaliyotokea gerezani Butimba ambayo Anorld alihusishwa nayo moja kwa moja!
Majira ya saa mbili hivi asubuhi Nancy kwa msaada mzizi uliokuwemo ndani ya shimo hilo alifanikiwa kutoka hadi nje, alishangazwa na hali iliyokuwepo juu, nyasi zililala na damu ilitapakaa sehemu mbalimbali katika nyasi.
Kitu cha kwanza alichofanya Nancy baada ya kusimama juu ya ardhi ni kwenda moja kwa moja hadi mahali alipouacha mwili wa kaka yake ukiwa umelala. Hakuyaamini macho yake alipokuta mwili huo haupo! Alianguka chini na kuanza kulia alijua majambazi waliuchukua na kuondoka nao, ilikuwa huzuni kubwa kwa Nancy.
*****
Milio mengi ya risasi iliyotawala makaburini ndiyo iliyomzindua Patrick kutoka katika hali ya kuzimia aliyoipata sababu ya hofu! Kwanza hakukumbuka mahali alipokuwa lakini muda mfupi baadae fahamu zake zilimrejea akamkumbuka kila kitu kilichotokea na pia dada yake Nancy!
Aliangaza huku na kule lakini hakumwona dada yake mahali popote, kwa jinsi risasi zilivyolitawala anga Patrick alijua kwa vyovyote majambazi walishamuua! Naye alianza kulia akimlilia dada yake.
Hali ilipozidi kuwa mbaya zaidi makaburini aliamua kuokoa maisha yake bila kujali kitu gani kingempata, alinyanyuka na kuanza kukimbia mbio kuelekea kwenye nyasi ndefu zaidi, alifanikiwa kutokomea bila kuonekana mbele aliendelea kutembea kwenda mbali zaidi.
Alitembea usiku mzima kulipokucha alikuwa barabarani eneo la Usagara, njia panda ya kwenda Bukumbi! Mwili wake wote ulikuwa ukimwasha kwa sababu ya kupita kwenye nyasi zilizowasha! Mawazo yake yote yalikuwa kwa dada yake Nancy! Mpaka wakati huo hakuelewa alikokuwa na kama alikuwa hai au alikuwa amekufa!
“Jamani Nancy dada yangu umekufa kweli?” Patrick aliongea peke yake huku akilia.
Alijiona mtu asiye na thamani yoyote duniani bila dada yake! Hakuwa na mama, baba wala mtu yeyote aliyemfahamu kama ndugu, mtu pekee aliyemtegemea alikuwa Anti Suzanne lakini nae tayari alishawasaliti na kuamua kumuua mama yao na sasa alikuwa akitaka kuwaua wao.
“Naondoka sirudi tena Mwanza hata shule kusoma tena sitaki mie! Nitakwenda mahali popote hata kama nikifa hukohuko sawa!” Alisema Patrick kwa uchungu.
Siku hiyo nzima alishinda hapo hapo Usagara akifikiria akifikiria mahali pa kwenda tena bila kuwa na pesa yoyote mfukoni mwake, mchana aliosha vyombo kwa mama ntilie na kupewa ukoko akala! Watu wengi waliomuona walishangaa ni kwa nini alikuwa akilia muda wote, walipomuuliza hakuwa tayari kueleza kila kitu kwa kila mtu! Lakini alifanya hivyo kwa mzee mmoja wa Kisomali aliyemkuta ndani ya Hoteli iliyoitwa Bismillah, mzee huyo alimnunulia Patrick chakula cha usiku baada ya kumwona akilia nje ya hoteli hiyo.
“Kwa hiyo lengo lako ni kuondoka mkoa wa Mwanza siyo?”
“Ndiyo, nisipoondoka wataniua!”
“Unataka kwenda wapi?”
“Mimi?”
“Ndiyo”
“Nataka kwenda Dar es Salaam! Nataka nipotee kabisa sitaki kubaki Mwanza, sitaki kuona vitu vitakavyonikumbusha mama na ndugu zangu hasa dada yangu Nancy nilimpenda mno!”
“Mimi ni dereva wa lile gari aina ya Fiat pale nje ninasafiri kwenda Dar es Salaam, leo ninalala hapa kesho alfajiri naendelea na safari yangu, nitakusaidia kufika huko Dar es Salaam, lakini una ndugu yeyote katika jiji hilo?”
“Yupo shangazi yangu!” Patrick alimdanganya ili yule mzee azidi kumwamini zaidi.
Mzee yule ambaye baadae Patrick aligundua aliitwa Bashir alimchukulia chumba katika hoteli aliyopanga yeye akalala, alfajiri saa 11 siku iliyofuata alimwamsha tayari kwa safari kuelekea Dar es Salaam iliyotegemewa kuwachukua karibu siku nne.
Siku hiyo hiyo jioni walifika Nzega walichukuwa vyumba na kulala tayari kwa safari tena siku iliyofuata! Mawazo na akili yote ya Patrick ilikuwa kwa dada yake Nancy! Hakuwa na uhakika kama alikuwa hai mpaka wakati huo, safari yote hadi Nzega aliimaliza akilia.
Dereva na utingo walijaribu kila waliloweza kumfariji lakini haikuwezekana , alinyamaza dakika thelathini na kulia masaa mawili na kila alivyolia alilitaja jina la Nancy!
******
Pamoja na Anne kulia machozi akiomba abaki gerezani Butimba kumalizia kifungo chake, alishindwa kumshawishi mkuu wa gereza kukubaliana naye hivyo jioni ya siku iliyofuata alipakiwa ndani ya treni la abiria kutoka Mwanza kuelekea Dar es Salaam.
Muda wote alilia watoto wake, alishindwa kuelewa angewaona vipi maishani mwake, alikuwa na uhakika kabisa kuwa halikuwa jambo rahisi kwa watoto wake kupata nauli za kuwafikisha Dar es Salaam, moyo wake uliumia sana.
Aliondoka gereza la Butimba bila kuelewa ni kitu gani hasa kilichompelekea rafiki yake Zena kujiua kwa kujidunga sindano, hakuwa na ufahamu wowote juu ya kuhusika kwa ndugu yake Suzanne na mume wake Anorld katika jambo hilo na hakujua ni yeye aliyetakiwa kufa badala ya Zena !
Aliendelea kulia akililia watoto wake pamoja na rafiki yake Zena.
Nasikitikia sana uamuzi wa wa Zena kujiua, nilikaa nae muda mfupi sana nikamzoea!” Aliwaza Anne akiwa ndani ya treni akilindwa na maaskari jela watatu.
Miongoni mwa watu waliopanda treni ya abiria siku hiyo ni Nancy tena bila tiketi, alikuwa ameamua kutoroka ili kuokoa maisha yake, alikuwa na uhakika asilimia mia moja kuwa kama angeendelea kukaa Mwanza ni lazima angeuawa kama alivyokuwa imepangwa! Akiwa ndani ya treni daraja la tatu alijificha chini ya kiti ili asionekane.
Je, nini kitatokea?
Je, Anne na Patrick watakutana?
Na nini kitatokea ndani ya treni?
HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 21
MTUNZI: ERIC JAMES SHIGONGO
Tofauti na wengi walivyoamini baada ya vyombo vya habari kutangaza kuwa Anorld alikufa katika mapigano makali kati ya majambazi na polisi makaburini, Anorld alikuwa hai na kutiwa nguvuni na polisi na yeye na mke wake Suzanne walifikishwa mahakamani wakishitakiwa kwa makosa ya mauaji ya Zena ndani ya gereza kwa kumpa chakula chenye sumu na pia mauaji ya watu wengine waliouwawa makaburini.
Watu wengi waliomfahamu Anorld walisikitika sana kusikia Anorld alishiriki katika kitendo hicho na wengi hawakuamini, Anorld aliaminiwa sana na watu kwa sababu ya utoaji wake wa misaada kwa wasiojiweza.
Mahakamani hawakutakiwa kujibu kitu chochote na walipelekwa mahabusu gerezani Butimba.
Suzanne alifika gerezani akilia na kichwani mwake alifikiria kitu kimoja tu nacho ni kumuomba Anne msamaha kwa mabaya yote aliyoyafanya! Alijua wazi kitendo cha kuamua kumuua ili awachukue watoto wake hakikuwa chema na alijua bila Mungu kuepusha Anne angekuwa marehemu!
Tayari mambo yalishawaharibikia Anorld na mke wake, yote hayo sababu ya tamaa ya kupata watoto! Wakiwa ndani ya gari la kuelekea gerezani wakiangaliana na hawakusema lolote, kila mtu alimuonea aibu na huruma mwenzake.
Walipofika gerezani kila mmoja alishuka na kuongozwa kuelekea gerezani, Anorld alipelekwa upande wa wanaume na Suzanne alipelekwa upande wa wanawake.
Kitu cha kwanza alichokifanya Anne baada ya kuingia gerezani ni kuanza kumtafuta Anne, alikuwa akijuta moyoni mwake kwa kitu alichokifanya! Aliulizia kwa muda mrefu bila kufanikiwa kumpata. Jioni ya siku hiyo hiyo alikutana na mama mmoja na kumuulizia yeye alionekana kumfahamu Anne vizuri!
“Si yule rafiki yake na marehemu Zena?”
“Ndiyo!”
“Amehamishiwa gereza la Segerea Dar es Salaam na aliondoka jana tu hapa gerezani”
“Eh ungu wangu eh! Nitamwona wapi Anne? Sitaki kufa bila kumuona ninajua nitafungwa lakini kabla ya hilo nataka kwanza nikutane na Anne!” Alisema Suzanne huku akilia.
“Kwani kuna nini?” Mama aliuliza.
“Nimemkosea sana!”
“Umemkosea nini?”
“Mama hayo tuyaache ila ahsante sana kwa kunisaidia” Alisema Anne na kuanza kuondoka sehemu hiyo huku akilia na kumwacha mama huyo akishangaa!
Siku hiyo pia kama siku mbili zilizopita alilala safarini, aliumwa na kunguni na kupigwa na baridi kali! Suzanne aliumia sana moyoni na kujutia uamuzi ambao yeye na mume wake waliufikia.
“Pesa tulikuwa nayo tungeweza hata kuzaa watoto wa kwenye chupa! Sasa maisha yetu yameishia gerezani hata Patrick na Nancy wenyewe hatukuwapata!”
****************************
Lori aina ya Fiat lililoendeshwa na dereva Kisomali lilikuwa likiingia mjini Dodoma, Patrick akiwa amechoka hoi bin taban, ilikuwa ni mara ya kwanza kwake kusafiri safari ndefu kiasi hicho, njiani alishalia machozi mengi yakakauka na hatimaye kuyaona yote yaliyotokea kuwa ni sehemu ya maisha!
Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuingia Dodoma usiku huo, alishangazwa na wingi wa taa alizozifananisha kabisa na mji wa Mwanza aliotoka! Zilimkumbusha mengi kuhusu nyumbani, zilimkumbusha marehemu mama yake, zilimkumbusha mengi kuhusu Mchungaji Aron na mke wake na Patrick alijua bila wao kuondoka kwenda Nairobi kisha yeye na dada yake kuhamia nyumbani kwa Suzanne yaliyotokea yasingetokea!
Patrick alikuwa ameyaacha maisha yake yote nyuma yake, alikuwa akienda katika nchi ya ugeni ambako hakumjua mtu yeyote, hofu ilimuingia moyoni kila alipolifikiria jiji la Dar es Salaam na sifa alizopewa juu yake! Madawa ya kulevya, machangudoa, vibaka, majambazi kwa upande mwingine aliamini alikokuwa amekwenda alikuwa anafuata matatizo kama si kifo chake mwenyewe.
Siku hiyo walilala Dodoma kama ilivyokuwa kawaida yake hakuacha kusali kabla ya kulala, dereva aliwaacha yeye na Tingo na kwenda kulala hotelini ingawa alilala kwa tabu kubwa alipata usingizi na katika usingizi wake siku hiyo aliota ndoto aliyomrejeshea faraja zake, katika ndoto hiyo alikuwa na mama yake pamoja na dada yake Nancy lakini hawakuwa watoto tena, mama yao alikuwa mzee sana na Nancy alikuwa mwanamke tajiri na yeye Patrick alikuwa mtumishi wa Mungu!
Alifurahi sana lakini alipozinduka na kukuta ilikuwa ni ndoto aliumia na kujikuta akilia machozi.
Hakulala tena mpaka asubuhi akilia na dereva alipokuja saa kumi na mbili asubuhi, waliendelea na safari yao kuelekea Dar es Salaam.
“Hivi kutoka hapa mpaka Dar es Salaam ni kama kilometa ngapi?”
“Ni kama kilometa 450 hivi, tumebakiza miji ya Morogoro, Mlandizi, Chalinze, Kibaha na Dar es Salaam yenyewe, leo hii hii saa mbili ama saa tatu usiku tutakuwa tayari tupo Dar!”
“Mtakaa muda gani Dar es Salaam?”
“Hatukai sana tukifika tutateremsha mzigo huu na kupakia mwingine kwenda Congo Braziville!”
Jibu hilo lilimtisha sana Patrick aliyetegemea dereva na utingo wangebaki Dar es Salaam angalau kwa siku kadhaa wakati akijaribu kutafuta utaratibu wowote wa kuishi! Lakini yote hayo alimwachia Mungu.
“Si ulisema kuna shangazi yako Dar?”
“Ndiyo!”
“Una namba zake za simu ili tukifika tumpigie aje kukuchukua?”
“Namba zake?”
“Ndiyo!”
“Hapa sina ila nikizifikiria vizuri naweza kuzikumbuka!” Alisema Patrick na kujifanya kufumba macho kama mtu aliyekuwa akikumbuka kitu fulani wakati hakuwa na namba yoyote ya kukumbuka wala huyo shangazi yake pia hakuwepo!
“Aisee mzee sikumbuki kabisa!”
“Sasa utafanyaje maana sisi tunaweza kuondoka usiku wa leo hii hii kwenda Congo!”
“Hiyo usijali mtaniacha tu hapo hapo Dar es Salaam nitajua la kufanya ili asubuhi niende kutafuta shangazi yangu!”
“Anafanya kazi wapi?”
“Anafanyakazi uhimbili hospitali” Patrick alitaja jina lililokuwa karibu yake.
*****************************
Tatizo la Anne kutokwa na hedhi kila siku lilikuwa bado linaendelea na yeye kama mfungwa hakuweza kujitunza vizuri, ndani ya behewa alilokaa hapakukalika abiria wote waliokuwa katika viti vya karibu na kiti alichokikalia Anne walivikimbia viti vyao! Hali ya hewa iliwashinda maafande wa magereza tu ndiyo walibaki walishindwa kuondoka kwa sababu ilikuwa kazi yao lakini hata kwao pia yalikuwa mateso.
Anne alikaa kwenye kiti chake akilia machozi ya uchungu wa mateso aliyokuwa akiyapata, pia aliwalilia watoto wake na hakujua angekutana nao vipi! Mikono yake ilifungwa pingu! Aliyafikiria maisha yake tangu utotoni na kugundua yalijaa maumivu na machozi, hakuwahi kupata furaha yoyote katika maisha yake!
Mume wake alikufa! Watoto wake wawili nao pia na bado mapacha wake Patrick na Nancy aliobakiza pia alikuwa ametenganishwa nao na alikuwa akisota kifungoni na ugonjwa wa ajabu uliomfanya atengwe na watu kwa sababu ya harufu aliyotoa! Alimlaumu mama yake kwa yote haya na muzimu wa uchawi aliokuwa nao!
“Kweli mama alistahili kufa! Ni heri nilimuua!” Aliwaza Anne huku akilia.
Wakati akiwaza hayo tayari treni ilikuwa ikiingia stesheni ya Saranda, watu wengi waliteremka na kwenda chini kununua pilau na wali na vyakula vingine vilivyouzwa stesheni hapo! Anne alibaki ndani ya treni akilalamika njaa, askari aliteremka na kwenda chini kununua chakula kwa ajili ya Anne!
Aliporudi askari alikuwa na sahani ya pilau na glasi ya maziwa, walimfungua na kuzifunga miguuni kisha akamkabidhi sahani ya chakula alikifakamia chakula hicho na kukila kwa fujo.
“Wamepika pilau nzuri sana hawa watu! Utafikiri ya nyumbani!” Alisema Anne na baada ya kumaliza kula alichukua glasi ya maziwa na kuimimina mdomoni na akajisikia vizuri, ni mara ya kwanza alikunywa maziwa katika muda wa miaka karibu kumi na tatu aliyokaa gerezani.
*****************************
Nancy chini ya kiti:
Kwa siku mbili mfululizo Nancy alijificha chini ya kiti cha treni akiogopa kugunduliwa na wakaguzi wa tiketi kwa sababu hakuwa nayo, hakuna mtu aliyegundua kulikuwa na mtu chini ya kiti, hata abiria waliokikalia kiti hawakugundua kuwa kulikuwa na mtu chini ya kiti chao, Nancy alijibana vizuri katikati ya maboksi mawili na kulala kimya!
Njaa ilimsumbua kupita kiasi lakini hakuwa na la kufanya ilibidi avumilie, alikuwa amedhamiria kujificha chini ya kiti hicho mpaka treni ifike Dar es Salaam! Hakuwahi kufikiria Dar es Salaam ilikuwa ni umbali mrefu kiasi gani kwa treni, alikuwa amesafiri kwa muda mrefu sana lakini bado hawakufika, mwisho alichoshwa na maumivu ya njaa kali aliyokuwa nayo!
Mpaka treni lilipofika stesheni ya Saranda, Nancy alikuwa akilia kwa njaa kali chini ya kiti na alishindwa kuvumilia zaidi hasa alipoanza kusikia harufu ya wali kutoka kwa abiria wengine! Aliamua kujitokeza na kupambana na sura za watu mbalimbali waliomwangalia na kumshangaa!
“Wewe binti umekaa hapo chini ya kiti tangu saa ngapi mbona hatujakuona?”
“Tangu mwanzo wa safari!”
“Mh! Kwanini lakini? Una matatizo gani?”
“Nina njaa! Nisaidieni chakula kwanza!” Nancy alisema bila woga.
“Chakula? Mbona nimemaliza hebu njoo huku!” Mama yule alijibu huku akiondoka na Nancy.
Walishuka hadi chini ambako mama huyo alimnunulia Nancy chakula akaanza kula, kasi yake ya kula ilimshangaza sana, alionekana kuwa na njaa kali kupita kiasi.
Kabla hata Nancy hajamaliza chakula chake vizuri katika sahani, treni lilipiga honi.
“Malizieni tu hiyo ni honi ya kwanza!”
“Kweli?” mama aliyemnunulia Nancy chakula aliuliza.
“Ndiyo” Mama muuza aliitikia.
Baadae treni ilianza kusogea mbele taratibu na Nancy aliendelea kula chakula na hiyo ilikuwa ni sahani ya pili ! Baada ya chakula wote wawili walipanda ndani ya treni kwa haraka kabla halijazidisha mwendo.
“Lo kumbe walikuwa wanatudanganya!” Alisema mama yule wakati wakikaa vitini, Nancy alianza kujikunja ili aingie tena chini ya kiti!
“Hapana kaa tu hapa juu ili unieleze wewe ni nani na umetoka wapi?”
“Sina tiketi nitakamatwa!”
“Wee kaa tu usiwe na shaka, wakikukamata sisi tutalipa!”
Nancy alikaa kitini na kuanza kumsimulia mama huyo kila kitu kilichotokea maishani mwake, alimweleza ni kwanini alikuwa akisafiri kwenda Dar es Salaam, mama yule alisikitika sana na machozi yalimtoka bila kutegemea, hakudhani Nancy angekuwa na matatizo makubwa kiasi hicho! Kila mtu aliyesikia habari hiyo alisikitika.
“Hiyo habari niliisoma magazetini na ilidaiwa wewe na kaka yako mlikuwa mmekufa!”
“Hapana mimi sikufa ila kaka yangu ndiye amefariki dunia!”
“Pole sana”
“Ahsante!”
“Usiwe na shaka tutakusaidia tutafika Dar es salaam mimi na mume wangu tunafanyakazi chuo kikuu cha Dar es Salaam tunatoka nyumbani Bukoba, huko ndiko nyumbani kwetu na hawa wawili ni watoto wetu Lilian na Rugarabamu” Alisema mama huyo na kumtambulisha Nancy kwa mume wake!
**********************************
Usiku wa saa sita treni lilingia Kilosa mkoani Morogoro, lakini hali ya Nancy haikuwa nzuri, tumbo lake lilikuwa linauma sana na hakuwa yeye tu aliyeumwa na tumbo ni pamoja na mama aliyemnunulia chakula na watoto wake pia waliumwa sana na matumbo, kila mtu alikitilia shaka chakula walichokula!
Kabla hawajaondoka Kilosa wote walianza kuharisha na baadae kutapika! Waliharisha maji meupe sana kama maji ya mchele na kuchafua behewa! Minong’ono kuwa walikuwa na kipindupindu ilianza kujitokeza, taarifa zilitolewa kwa kiongozi wa treni na Nancy, mama Isabela, Rugarabamu na mume wake walichukuliwa na kupelekwa zahanati iliyomo ndani ya treni ambako daktari alithibitisha kuwa wote walikuwa na kipindupindu!
Hakuwa na maji ya kutosha kuwawekea katika mishipa yao, aliwawekea chupa moja moja lakini haikusaidia kitu hali zao zilizidi kudhoofika, waliharisha na kutapika maji mengi mno! Watoto wa yule mama katika muda wa masaa mawili wakawa hawawezi hata kuongea.
Wakati wanaingia Morogoro watoto wote wawili wa mama yule walishafariki na hali ya Nancy ilikuwa mbaya mno! Walikimbizwa haraka hospitali ya mkoa wa Morogoro ambako walilazwa na kutundikiwa dripu za maji ili kuyarejesha maji yote yaliyopotea na walipewa madawa aina ya tetracycline!
Hali ya Nancy ilikuwa mbaya mno na hakuna mtu aliyekuwa na matumaini kuwa angepona kwa hali aliyokuwa nayo.
Alilazwa kitanda cha kwanza kabisa katika chumba alichopewa na mama Isabela na mume wake waliwekwa chumba cha pili, ingawa hali yake ilikuwa mbaya sana Isabela akiwa katika chumba hicho alimwona mgonjwa mwingine akiingizwa yeye naye hali yake ilikuwa mbaya mno na pamoja na kuwa hoi mgonjwa huyo alikuwa na pingu mkononi na nyuma yake walikuwepo maaskari magereza watatu.
“Huyu ni nani?” Muuguzi aliuliza.
“Ni mfungwa amehamishwa gereza la Segerea kutoka Butimba baada ya kutoka Kilosa ghafla alianza kuharisha nafikiri ni chakula alichokula Saranda!” Alijibu askari magereza mmoja.
Macho ya Nancy yalikuwa yamelegea na midomo ilikuwa mizito kupita kiasi, giza lilishaanza kuyaingilia macho yake, alijua huo ndio ulikuwa mwisho wake, lakini aliposikia kwa mbali maneno ya askari Magereza juu ya mgonjwa aliyeingizwa ndani ya chumba alijitahidi kufumbua macho yake ili amuone mgonjwa mwenzake! Hakuyaamini macho yake alipokuta ni mama yake na kujikuta akitamka kwa shida.
“Ma....ma!” Aliita kwa taabu kama mara tatu lakini alizidi kuishiwa nguvu na kulegea, hakusema neno tena.
Anne alisikia sauti ikiita mama, ingawa haikusikika vizuri lakini sauti hiyo aliifananisha na sauti aliyozoea kuisikia kabla, ilifanana na ya Nancy! Ingawa hakuwa na uhakika sana wa jambo hilo Anne aligeuza macho yake na kuangalia pembeni, alimwona mwanae Nancy katika hali mbaya.
“Ja...ma...ni mwa...na...ngu!” Alisema Anne kwa shida na kunyoosha mkono wake, Nancy nae alinyoosha wa kwake mpaka wakashikana waliamini huo ulikuwa ndiyo mwisho wao baada ya hapo walianza kuharisha mfululizo bila kusitisha!
“Patr..ic...yupo wa...pi!?” Aliuliza Anne kwa shida huku akiendelea kuharisha.
“Ali...ku...fa!”
Ingawa alikuwa mgonjwa taabani aliposikia Patrick alikufa Anne alimwaga machozi! Lakini alishukuru Mungu kukutana na mwanae angalau mmoja.
Je, nini kitaendelea?
Nini kitampata Patrick jijini?
Je, Nancy na mama yake watapona au ndiyo mwanzo wa Patrick kuwa peke yae duniani?
Tags:
RIWAYA