TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 22----23----24


Global outreach Mission lilikuwa ni shirika la kidini lililohubiri dini Duniani kote na liliongozwa na Mwijilisti wa Kimataifa Karl Heinz Schroden, Mjerumani mwenye mwenye umri usiopungua miaka hamsini hivi!
Mwinjilisti huyu alizunguka dunia nzima akihubiri Injili, na kazi yake watu wengi waliokoka na kumrejea Mungu! Lengo lake lilikuwa ni kuwafikia watu milioni 200 katika muda wa miaka thelathini. Alikuwa amefanya kazi hiyo kwa miaka karibu ishirini bila kurudi nyumbani kwao Ujerumani.
Heinz hakuwa na mke wala mtoto wala familia iliyomtegemea, kwa sababu hiyo aliamua kutumia kila alichokuwa nacho kuikamilisha kazi ya Mungu kabla ya kulala mauti.
Watu wengi walidai Mwinjilisti Heinz alikuwa na kasoro kimaumbile ndiyo maana aliweza kuifanya kazi hiyo kwa muda mrefu bila kukumbwa na kashfa yoyote! Yeye Heinz alilikanusha sana jambo hilo kwa kudai aliitwa na Bwana kwa ajili ya kazi ya Mungu na ni yeye Mungu aliyemwezesha kufanya yote aliyoyafanya.
Shirika lake lilikuwa kwa kasi ya ajabu, katika miaka mitano ya kuwepo kwake lilikua na kuwa shirika kubwa la Kidini kuliko mashirika mengine ya dini duniani! Mikutano aliyofanya ilijaza maelfu kwa maelfu ya watu na hapakuwa na utaratibu wa kukusanya sadaka bali ni yeye aliyegawa nguo na msaada kwa wasiojiweza waliofika mkutanoni.
Heinz alifungua Makanisa katika kila nchi aliyokwenda, nayo pia yalikua kwa kasi kubwa! Alimiliki ndege tatu, magari ambayo hata yeye hakujua idadi yake, meli za kusafiria, kifupi Heinz alikuwa Mwinjilisti tajiri kuliko wafanyabiashara wengi na watu walishindwa kuelewa alipata wapi utajiri huo.
Mwinjilisti Heinz aliingia Tanzania akitokea Kenya baada ya kuhubiri katika nchi za Msumbiji,Zambia, Zimbabwe, Botswana na Afrika ya Kusini, matangazo ya kuingia kwake Tanzania yalianza miezi mitatu kabla, Redio na vituo mbalimbali vya televisheni vilijipatia mamilioni ya shilingi kwa matangazo yake peke yake!
Vituo vingine vilifikiria hata kubadili vipindi vya taarifa za habari ili kutangaza matangazo ya Mwinjilisti Heinz kwa sababu yalilipiwa pesa nyingi zaidi.
Msafara alioingia nao nchini kupitia Namanga uliwashangaza watu wengi, alikuwa na magari aina ya Scania ya tani ishirini yasiyopungua thelathini ambayo yalibeba mizigo yake, alikuwa na magari mengine madogo ishirini yaliyobeba wafanyakazi wa shirika lake na waimbaji wa Kwaya mbalimbali alizotembea nazo kila alikokwenda duniani.
Hiyo peke yake ilikuwa haitoshi kwani ndege mbili zilimfuata katika kila nchi aliyoingia zikileta mizigo yake mingine, mizigo hiyo iliyodaiwa kuwa misaada iliteremshwa usiku na kwa uangalizi na usiri mkubwa! Hakuna mtu hata mmoja katika watu waliosafiri nao aliyebahatika kujua mizigo hiyo ilikuwa nini na mara nyingi usiku huohuo baada ya kupakuliwa ilipakiwa ndani ya magari madogomadogo na kupelekwa kusikojulikana.
Kila Mwinjilisti alipoulizwa jibu lake lilikuwa moja kuwa “Ilikuwa misaada kwa wenye shida!” ambalo lilitosha kuwafanya wafuasi wake waamini na kutohoji tena.
Siku alipoingia Arusha na msafara wake hoteli zilikodiwa na shirika lake, wageni walioingia Arusha siku hiyo walilala stendi za mabasi na wengine walilazimika kwenda kulala mjini Moshi! Sifa za Mwinjilisti Heinz zilisambaa Arusha nzima katika muda wa masaa mawili!
Alifanya mikutano kwa wiki nzima mjini Arusha akaondoka na kuelekea Moshi ambako alifanya tena mkutano kwa wiki nzima na baadaye kuingia Dar es Salaam, katika mikutano yake watu walipokea miujiza ya ajabu na aliwashangaza watu kwa uwezo wake wa kuwagusa puani kwa mikono yake wakaanguka chini na kupoteza fahamu na kusikia raha ya ajabu mioyoni mwao.
Kilichowashangaza wengi baada ya baada ya kuguswa puani siku iliyofuata walitaka kuguswa tena na walipoguswa walisikia raha ileile kama waliyosikia siku moja kabla hatimaye wengi wakawa hawawezi chochote mpaka wameguswa puani na Mwinjilisti Heinz! Wengi waliamini hiyo ilikuwa nguvu ya Roho Mtakatifu!
Ni siku hiyohiyo aliyoingia Dar es Salaam ndiyo pia Patrick aliingia ndani ya jiji hilo la maraha akitokea Bara, gari alilokuja nalo kwa msaada wa dereva wa Kisomali liliteremsha mizigo usiku huohuo likapakia mizigo mingine na kuondoka kuelekea Kongo kupitia Tunduma! Patrick alisikitika sana lakini alimshukuru sana dereva wa gari hilo kwa msaada wake!
Ingawa alikuwa mgeni jijini usiku wa siku hiyo Patrick alilazimika kutembea hadi ufukweni ambako alilala ndani ya mtumbwi mbovu huku akiumwa na mbu na kupigwa na baridi kali! Usiku mzima Patrick hakupata usingizi akijaribu kuyafikiria maisha yake tangu utotoni na mateso aliyoyapata!
Alipomkumbuka mama yake Anne pamoja na dada yake Nancy alishindwa kujizuia na kujikuta akilia machozi! Mpaka wakati huo Patrick hakujua kuwa aliyekufa gerezani hakuwa mama yake bali Zena, aliamini mama na dada yake hawakuwa hai na alikuwa peke yake duniani!
Mawazo hayo yalimfanya Patrick aumie sana moyoni mwake na kuona alikuwa ni mtu asiye na thamani duniani, aliichukia Tanzania na kuwaona watu wote hawafai.
“Hakuna ninaloweza kufanya hapa duniani zaidi ya kumfuata Yesu Kristo peke yake! Ni yeye ndiye anayeweza kuwa mfariji na rafiki yangu wa kweli, sina mwingine wa kurejesha furaha yangu isipokuwa yeye!’ Aliwaza Patrick huku akilia.
*****
Asubuhi ya kwanza jijini
Dar es Salaam:
Kulipokucha asubuhi Patrick alitoka ndani ya mtumbwi mchafu aliolala na kuamua kuingia mitaani kutafuta lolote! Ilikuwa ni mara ya kwanza kwake kuwa katika mji mkubwa kama Dar es Salaam alishangaa karibu kila kitu alichokiona hasa maghorofa marefu yaliyokuwepo maeneo ya posta!
Hakujua mtu yeyote ndani ya jiji hilo na hakujua aanzie wapi kwa sababu kila sehemu zilifanana! Asubuhi hakuwa na uhakika wa kufungua kinywa chake lakini bado aliamini asingeweza kufa katika nchi ambayo watu walikula na kusaza, alijua lazima ilikuwepo njia ya yeye kuishi ambayo Mungu pekee aliijua!
Ilipofika saa saba ya mchana alikuwa maeneo ya Kariakoo, kila kitu kilishamchanganya hakuelewa ni wapi kulikuwa Mashariki,Magharibi, Kaskazini wala Kusini! Hakuelewa alikokuwa akitoka wala alikokuwa akielekea! Alikwenda tu kama kitu kilichosukumwa na upepo.
Baada ya kuzunguka sana ghalfa alijikuta amesimama kwenye mnara wa askari, Patrick aliiangalia sanamu ya askari yule kwa muda mrefu na hakuona taabu wala aibu kwa jinsi watu ndani ya magari yaliyopita kwenye mzunguko wa mnara huo walivyomshangaa kwani aliamini alikuwa akijaribu kulizoea jiji la Dar es Salaam taratibu!
Huku njaa ikimuuma alipotoka kwenye mnara wa askari alinyoosha moja kwa moja kupitia barabara za Azikiwe na Maktaba na kujikuta kwenye makutano ya barabara ya Maktaba na Bibi Titi, kwa muda aliyashangaa mataa ya kuongozea magari yaliyokuwepo katika makutano ya barabara hizo lakini baadaye alikata kushoto na kuelekea Akiba!
Alipofika kwenye makutano ya barabara ya Bibi Titi na Morogoro alisimama chini ya mti mkubwa nje ya chuo cha Ufundi Dar es Salaam na kuanza kuwaza ni wapi angepata chakula cha mchana huo kwani njaa ilikuwa ikimsumbua kupita kiasi!
“Nitajikaza sababu mimi ni mwanaume isitoshe riziki ya mbwa ipo miguuni mwake!” Patrick alijisemea moyoni na kusonga mbele kufuata barabara ya Morogoro akielekea kituo cha mabasi cha Faya!
“Hivi hapa ndipo kwenye ofisi ya umoja wa vijana? Hapa kumbe ndipo zilipo ofisi za Nchimbi? Nikishindwa kabisa nitamtafuta hata yeye anisaidie hela ya kula! Ingawa hanifahamu, nitajieleza kwake nafikiri hataninyima hata mia mbili!” Patrick alijisemea moyoni mwake wakati akilipita jengo la Umoja wa vijana kulia kwake.
Alipofika kituo cha Faya alikuta watu wengi wakisubiri usafiri wa daladala kuwarudisha majumbani kwao!
“Haya, Sinza, Sinza! Sinza wahi gari!” Mpiga debe alipiga kelele kuwaita abiria wakati gari lake likiegeshwa.
“Ndiyo niliwahi kusikia hapa Dar es Salaam kuna Sinza tena na yule mwanamuziki Remmy anakaa hukohuko!” Aliwaza Patrick na hakusimama kituoni hapo alizidi kusonga mbele na kuzipita taa za kuongozea magari za Faya.
Mbele alishangaa kuona makundi makubwa ya watu wakitembea kwa miguu kuelekea bondeni wengi wakiwa akinamama na watoto!
“Masikini sijui hawa wamekosa nauli?” Aliwaza Patrick lakini alipowaangalia mikononi mwao aliwaona wakiwa na Biblia.
“Nafikiri wanakwenda kanisani, lakini leo mbona siyo Jumapili?” Alijiuliza Patrick.
Ghafla mawazo yake hayo yaliingiliwa na sauti ya kipaza sauti kikiongea kwa sauti ya juu! Alisikia sauti za watu wakiimba nyimbo za kumsifu Mungu!
“Njoo kwa Kristo, Kristo anaokoa!” Patrick aliyasikia maneno hayo ndani ya wimbo ulioimbwa.
“Namshukuru Mungu hiki ndicho kitu nilichokuwa nakitaka!” Patrick alisema na bila hata kusita alianza kuwafuata watu waliotembea katika makundi kuelekea bondeni.
“Karibuni katika viwanja vya Jangwani mmsikilize mtumishi wa Mungu Karl Heinz kutoka Ujerumani, leo yupo hapa! Njooni nyote mpokee uponyaji yaleteni matatizo yenu yote kwa Bwana!” Sauti ilisikika kwenye kipaza sauti.
Bila hata kutegemea Patrick alisikia furaha ya ajabu moyoni mwake alitembea na kujichanganya katikati ya watu na kusogea mbele zaidi ingawa ilikuwa ni kwa taabu kubwa! Aliimba nyimbo za mapambio na kurukaruka pamoja nao.Siku hiyo alijisikia kuutua mzigo uliokuwa kifuani mwake.
Baadaye Mwinjilisti Karl Heinz alisimama na kulihubiri neno la Mungu, karibu kila alichokiongea katika mahubiri yake kiliyagusa maisha ya Patrick moja kwa moja na alipoongea juu ya kifo na mauti Patrick alijikuta akiwakumbuka mama na dada yake.
Patrick alipiga magoti chini na kusali huku akilia machozi, akiwaombea mama na dada yake kwa Mungu ili awaweke mahali pema mpaka siku ambayo angekutana nao tena!
Ilikuwa ni huzuni kubwa sana kwa Patrick lakini alipokumbuka kuwa tayari alikuwa ndani ya Kristo alijisikia amani na furaha ikirejea kubwa moyoni mwake.
Mkutano ulipokwisha Patrick alisikia msukumo wa kutaka kumwona Mwinjilisti Karl Heinz, ingawa alijua ilikuwa kazi ngumu lakini aliamini kama angefanikiwa ni lazima angemwonyesha ni kwa jinsi gani angeweza kuwa mtumishi wa Mungu jambo alilotamani kulifanya!
“Nitamwona tu!” Alisema Patrick na kuanza kujongea mbele kuzunguka nyuma ya jukwaa ambako alikutana na mmoja wa shemasi waliohudumia katika mkutano huo.
“Bwana asifiwe mpendwa?” Patrick alimsalimia shemasi huyo.
“Ameeeni! hujambo mpendwa?”
“Sijambo!”
“Unauonaje mkutano huu?”
“Kwa kweli nimebarikiwa sana na ninatamani kuonana na mtumishi wa Mungu Heinz kwani ameyagusa sana maisha yangu!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Basi subiri, ingawa najua ni shida sana kumwona, hivi sasa bado anafanya maombi kwa wagonjwa!”
“Una kalamu na karatasi hapo mpendwa?” Partick aliuliza.
“Ndiyo!”
Shemasi alinyoosha mkono na kumpatia Patrick kalamu na karatasi pamoja na Biblia kugandamizia, akaanza kuandika ujumbe wa Kiingereza kwa mwinjilisti Karl Heinz.
“Ninaitwa Patrick Huggins, ni kijana mdogo na Mungu amesema na mimi jambo ambalo ni muhimu sana niongee na wewe!
Ni mimi.
Patrick
Patrick alimaliza kuandika barua hiyo na kumkabidhi shemasi.
“Tafadhali mpendwa mkabidhi tu barua hiyo mimi nasubiri huku nyuma!”
“Sawa!”
Shemasi aliondoka kwenda jukwaani ambako aliikabidhi barua hiyo kwa mchungaji mwenyeji wa mkutano ambaye alikaa nayo mkononi akisubiri Mwinjilisti Heinz amalize kuombea wagonjwa ndipo akamkabidhi barua akaanza kuisoma!
“Where is this boy?”(Mvulana huyu yupo wapi?)
“Behind the Platform!”(Nyuma ya jukwaa)
“Bring him forward I want to talk to him!”(Mleteni mbele, nataka kuongea naye)
Mchungaji mwenyeji aliteremka akikimbia na kwenda nyuma ya jukwaa kumwangalia Patrick.
“Wewe ndiyo Patrick?”
“Ndiyo!”
“Tafadhali njoo mtumishi wa Mungu anataka kuongea na wewe!”
Patrick hakuamini ingekuwa rahisi kiasi hicho kuonana na mhubiri mkubwa kama Kart Heinz.
Patrick alipandishwa jukwaani na kupewa kiti akakaa na kusubiri Mwijilisti Karl Heinz amalize kuhubiri, njaa yote aliyokuwa nayo Patrick iliyeyuka alijisikia kushiba bila kujua chakula kilitokea wapi!
“Are you Patrick?”(Wewe ni Patrick?) Mtumishi wa mungu Kart Heinz alimuuliza Patrick alipomfikia.
“Yes I’m, I cant believe I’m talking to the great servant of God!”(Ndiyo ni mimi na siamini kama ninaongea na wewe mtumishi wa Mungu!)
“ Can we talk here?Or you need more Privacy?”(Unataka tuongee hapa au unahitaji faragha zaidi?)
“I need to talk to you alone!”(Nataka kuongea na wewe peke yako)
“Sure!”(Hakika?)
“Yes!”Ndiyo)
“Then come inside with me!”(Basi nifuate ndani) Kart Heinz alimwambia Patrick na wote wawili waliteremka jukwaani na kwenda moja kwa moja ndani ya hema moja lililokuwa na kila kitu kilifanya liitwe ofisi.
“This is my temporally office!”(Hii ni ofisi yangu ya muda)
“Oh it is very nice office!”(Oh! Ni ofisi nzuri)
“Sure?Thanks God!(Hakika? Ninamshukuru Mungu)
Baada ya kujitambulisha kwa Mwijilisti Patrick alianza kumsimulia kila kitu kilichotokea maishani mwake, kufiwa na wazazi wake ndugu zake na baadaye dada yake mpendwa Nancy! Na alieleza nia yake ya kutaka kumtumikia Mungu na kuokoa roho za watu wengi waliopotea, alimwomba Mwijilisti Heinz amsaidie kutimiza ndoto yake.
“I’m very poor, but I always wanted to be an Evangelist and save people’s lives! Please help me!”(Mimi ni masikini lakini siku zote nimetaka kuwa Mwijilisti nihubiri neno la Mungu na kuokoa maisha ya waliopotea, tafadhali nisaidie kutimiza ndoto hiyo) Alisema Patrick Mwijilisti Kart Heinz alitokwa na machozi.
“So you are an orphan?”(Kwa hiyo wewe ni yatima?)
“In the world I’m an orphan, but in Heaven I’m not because I have Jesus Christ!”(Hapa duniani mimi kweli ni yatima lakini mbinguni mimi si yatima kwa sababu ninaye Yesu Kristo)
“So where do you stay in the city?”(kwa hiyo hapa jijini unaishi wapi?)
“I have no where to stay! I arrived yesterday and slept at the beach in a decaying boat!”(Sina mahali pa kuishi hapa jijini, niliingia jijini jana na nililala ufukweni kwenye moja ya boti inayooza)
Mwijilisti Karl Heinz alichukua kitambaa chake na kufuta machozi yaliyokuwa yakimtoka na kulowanisha usoni, alikuwa ameumizwa sana na habari ya Patrick! Aliguswa sana na kujisikia kumsaidia Patrick.
“Patrick I will help you fulfil you dream! will make sure you have a Passiport,and will be travelling with you wherever I go” (Patrick nitakusaidia kutimiza ndoto zako, nitashughulikia hati yako ya kusafiria na tangu sasa nitasafiri na wewe kila ninakokwenda)
“Thanks! Thanks!Thanks!”(Ahsante! Ahsante! Ahsante!) Patrick alisema huku akilia kwa furaha.
*****
Anne, Nancy hospitalini:
Hali za wagonjwa zilikuwa bado mbaya,Anne na Nancy walikuwa bado wakiharisha na kutapika sababu ya kipindupindu! Dawa za kutibu ugonjwa huo zilikuwa zimekwisha hospitali ya Mkoa wa Morogoro na ziliagizwa kutoka jijini Dar es Salaam na kuwaacha Anne na Nancy katika hali mbaya na bila dawa, walilala vitanda jirani mikono yao ikiwa imeshikana na kung’ang’aniana! Hakuna aliyeongea kati yao wote walijua kifo chao kilikuwa kimefika.
Je kweli Anne na mwanae wataokoka?
Nini siri kubwa iliyopo katika kazi ya Mwinjilisti Karl Heinz?
Je, nini kitampata Patrick?
Je, ipo siku familia hii itakutana?


HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 23
MTUNZI: ERIC JAMES SHIGONGO
Ngozi zao zilikuwa nyembamba na zilichukua muda mrefu sana kurudi zilipominywa wauguzi, nyama zao zilikakamaa mwilini kupita kiasi.
“Wapo dehydrated mno na sijui tutaokoaje maisha yao sababu kila tunapowapatia ORS wanatapika!” Alisema muuguzi akimwambia mwenzake aliyekuwa jirani alimaanisha kila walipowapa maji ya chumvi walitapika.
“Waliofuata dripu Dar es Salaam nao wamechelewa mno sijui kifanyike kitu gani kuokoa maisha ya wagonjwa hawa!”
“Tunahitaji dripu zenye sodium chloride ziingie katika mishipa yao hapo watapona kama wangekuwa na pesa tungekwenda kuwanunulia kwenye duka la dawa wakati tukisubiri dawa zetu zifike bila hivyo watakufa tu!” Muuguzi mwingine alijibu.
“Kwani wale wenzao wawili mtu na mke wake wako wapi?”
“Si unaamanisha yule mama aliyekuwa akiongea kihaya?”
“Ndiyo!”
“Amefariki muda mfupi uliopita!”
“Kwa hiyo wote wamefariki maana watoto wao pia walifariki hapahapa hospitalini muda mfupi baada ya kufika!”
Nancy aliyasikia maongezi hayo ya wauguzi kwa mbali sana, mwili wake haukuwa na nguvu kabisa na macho yake yalifunikwa na giza nene, kitu pekee alichokikumbuka kilikuwa ni mkono wake wa kushoto uliokuwa umekamatana na mkono wa mama yake wote walikuwa katika hali ya kufa!
Mwili wa Nancy ulikuwa umelegea kupita kiasi, alishindwa hata kujigeuza kitandani akisubiri dakika yake ya mwisho ifike! Aliamini hapakuwa na njia ya kuyaokoa maisha yake na mama yake hasa aliposikia kuwa mama Rugarabamu na mumewe tayari nao walishafariki dunia!
Alitamani sana kupona ili ajue ni kitu gani kilitokea mpaka mama yake akawa hai wakati hata kaburi lake waliliona, lakini haikuwepo tena nafasi ya kulijua jambo hilo kwani alitakiwa kufa wakati wowote
“Mimi na mama tunamfuata Patrick, familia yetu yote imekwisha duniani!” Aliwaza Nancy.
*****
Mafia Drug Traffikers:
Lilikuwa kundi maarufu la uuzaji wa madawa ya kulevya na mauaji duniani, lilianzishwa miaka ya 1900 huko Mirano, Italia. Lilikuwa na matawi sehemu nyingi sana duniani ikiwemo Ujerumani, Uingereza, Marekani, Nigeria, Tunisia, Brazil, Chile na katika nchi hizo walichaguliwa wawakilishi walioitwa Presdento! Ni hao ndio waliohakikisha madawa yanaingia katika nchi zao na kuyasambaza kisirisiri bila mtu yoyote kugundua, Mapresdento wa nchi nyingine walikuwa ni viongozi kama Mawaziri, Makatibu wakuu na hata Maraisi wa nchi zao.
Biashara ya madawa ya kulevya ilikuwa ni biashara haramu iliyopigwa vita karibu kila pembe ya dunia, katika nchi za Kiarabu watu wote waliofanya biashara hiyo walipigwa risasi ama kuchinjwa hadharani walipokamatwa lakini pamoja na hali hiyo watu hawakuacha kuifanya biashara hiyo ingawa kila siku walikamatwa na kupigwa risasi hiyo yote ilikuwa ni kazi ya kundi la Mafia drug Traffikers.
Heinz Luminie, Berlin 1947
Heinz Luminie alikuwa Presdento wa Mafia nchini Ujerumani, baada ya njia nyingi za kusafirishia madawa kugundulika na wafuasi wengi kukamatwa, kufungwa na wengine kuuawa Heinz alibuni mpango wa kuyasafirisha madawa haya kupitia mkondo wa kofia ya dini! Alielewa mizigo ya Wamisionari haikukaguliwa bandarini au katika viwanja vya ndege na wala haikutozwa ushuru.
Ulikuwa ni mpango wa muda mrefu sana kuutekeleza lakini ilikuwa ni lazima afanyike baada ya miaka mingi. Heinz alikuwa baba wa watoto wawili wa kike na mwingine wa kiume, wa kike aliitwa Patricia na wa kiume aliitwa Karl ni huyo ndiye aliyetegemewa kuja kuwa mrithi wa maliz zote za Heinz Luminie.
“Nitahakikisha siku moja Karl anakuwa mfanyabiashara wa madawa kwa kupitia kofia ya dini!” Aliwaeleza wanachama wa Mafia katika mikutano yao.
“Utalifanyaje hilo?”
“Nitamlea katika mzingira ya kidini, nitampeleka katika shule za Biblia ili aje kuwa mhubiri maarufu duniani ni yeye atayesafirisha mizigo yetu yote kokote duniani na hakuna mtu atakayegundua jambo hilo!” Aliongea kwa uhakika Heinz.
“Inawezekana fanya basi!”
****
Katika umri wa miaka 12 tu Karl alipelekwa katika chuo cha Berlin Theological Institute kusomea mambo ya dini, yote hayo yalifanyika kumwandaa kuja kuwa mwinjilisti wa kimataifa. Karl aliwashangaza walimu wake kwa uwezo aliokuwa nao darasani, alisoma kwa bidii kubwa na kufanya vizuri sana katika masomo yake yote.
Pamoja na hayo Karl hakupenda kuwa Mwinjilisti, katika maisha yake alitaka sana kuwa Mwanasheria au daktari lakini sababu baba yake alimlazimisha kusoma masomo ya Uinjilisti hakuwa na la kufanya zaidi ya kukubali na kila siku aliyakumbuka maneno ya baba yake.
“Unasoma Uinjilisti si kuwa Mwinjilisti bali kutimiza kazi fulani ambayo nitakuja kukupatia baadaye maishani, kazi ambayo siku zote itakufanya kuwa tajiri kuliko binadamu yeyote!”
“Sawa baba lakini kazi gani hiyo?”
“Siwezi kukuambia sasa hivi soma kwanza na ni lazima uifanye vinginevyo utauawa!”
“Nitauawa? Kazi gani hiyo baba mimi napaswa kuifahamu!”
“Haiwezekani kuifahamu sasa hivi!”
Maongezi hayo kila siku yalimsumbua Karl akilini mwake na kwa sababu ya kuogopa kuuawa alisoma kwa bidii.
****
Akiwa na umri wa miaka 23 Karl alifanikiwa kumaliza masomo yake ya teolojia na kupata digrii zake tatu, jina lake likabadilika akawa Dr Karl Heinz!
Ilikuwa ni furaha kubwa mno kwa baba yake, alijua mtoto wake kumaliza masomo hayo kulimaanisha kazi yake kukamilika, alikuwa na uhakika dawa za kulevya aina ya Cocaine, Heroine na Mandrax ambazo kundi la Mafia lilisambaza zingefika mbali sana duniani bila mtu kukamatwa au kutiliwa mashaka na hivyo wangetajirika kupita kiasi.
****
Ulikuwa ni wakati wa kiangazi katika jiji la Berlin, jua la kawaida lilitawala angani na kuufanya mji kutokuwa na baridi hata kidogo, hali hiyo ilimfurahisha karibu kila mkazi wa jiji hilo lenye baridi. Jioni hiyo Karl alikaa na baba yake ndani ya chumba kidogo chenye mwanga duni, walikuwa wawili tu ndani ya chumba hicho! Dada yake Patricia alikuwa shuleni na mama yake alishafariki miaka kumi kabla ya siku hiyo kwa kuzama na boti baharini alikokwenda kuogelea wakati wa Sikukuu ya pasaka.
Mzee Heinz alimwita mtoto wake ili kumweleza ni kwanini alimlazimisha kwenda kusomea Uinjilisti! Karl pia alikuwa na nia sana ya kulifahamu jambo hilo kwani kwa muda mrefu alimuuliza baba yake lakini hakupewa jibu hiyo ilikuwa siku aliyoisubiri kwa hamu kubwa!
“Mwanangu Karl!” Alianza mzee Heinz na maongezi yao yalifanyika katika lugha Kijerumani.
“Ndiyo baba!”
“Leo nataka nikueleze kitu ambacho hukuwahi kukisikia na kama ulishakisikia basi haukuwa na uhakika, nataka nikueleze ni kwanini niliamua usomee Uinjilisti!!”
“Nakusikia baba!” Karl Aliendelea kumwitikia baba yake.
“Tafadhali niahidi kuwa siri nitayaokueleza hapa hautaisema mahali popote!”
“Nakuahidi baba!”
”Mwanangu mimi ni mwanachama wa Mafia na biashara yangu ni madawa ya kulevya!”
Moyo wa Karl ulipasuka paa na mapigo kubadilika, alianza kuhisi jasho likimtoka kwani hakuwahi hata siku moja kufikiri kuwa baba yake aliyeonekana mpenda dini angeweza kuwa mwanachama wa kundi hilo hatari la wauaji.
“Baba unasema kweli?”
“Ndiyo mwanangu na hutakiwi kusema kwa mtu yoyote ukisema tu utauawa wanachama wenzangu watakunywa damu yako!”
“Ndiyo nimekusikia baba sasa ni kwanini ulinipeleka kusoma Uinjilisti?”
“Nilitaka uje kufanya hii kazi ninayoifanya!”
‘Kazi ya kuuza madawa?”
“Ndiyo!”
“Siwezi baba mimi sasa namfahamu Mungu siwezi kufanya biashara hiyo!”
“Karl!Karl! Karl! Unakaidi maagizo yangu?” Alisema mzee Heinz akiwa amepandisha hasira yake kupita kiasi.
“Siyo hivyo baba nasema ukweli wangu!”
Hapakuwa na maelewano kati yao na walitoka chumbani bila kufikia muafaka. Jioni ya siku iliyofuata Karl akitembea mjini alikamatwa na watu wasiojulikana akafungwa kitambaa machoni na kupelekwa mahali kusikojulikana ambako alipewa mateso ya kutikiswa na umeme kwa usiku mzima na kulipokucha asubuhi baba yake alifika na kuongea naye tena, Karl alikubali kuifanya kazi hiyo.
Wiki mbili baadaye shirika la Global Outreach Mission lilianzishwa nchini Ujerumani, mwinjilisti kijana Karl Heinz mwenye umri wa miaka 23 akawa kiongozi wake, kwa siri kubwa shirika hilo lilifadhiliwa kila kitu na kundi la mafia! Lengo la kundi hili kwa nje lilikuwa ni kuzunguka dunia nzima kuhubiri dini lakini kwa ndani lilikuwa shirika la kusambaza madawa ya kulevya duniani.
Ratiba za safari za shirika hilo zilipangwa na kundi la Mafia, Karl Heinz alisafiri kwenda katika nchi ambazo Mafia walitaka kupeleka madawa yao. Hakuipenda kazi hiyo lakini ilibidi aifanye kwa sababu aliogopa kuuawa! Alifundishwa jinsi ya kuushika unga wa Cocaine katika mikono na kuwagusa watu puani wakati wa maombi ili walewe madawa na kuamini alikuwa na miujiza ya Mungu.
Alifundishwa pia kuchukua kitambaa na kukipaka unga wa dawa aina ya Heroine kalina alipompiga mtu na kitambaa hicho usoni alilewa na kuanguka chini na aliponyanyuka alikuwa na furaha isiyo kifani sababu ya madawa hayo kulevya.
Mambo hayo yalimpa sifa kubwa Mwinjilisti kijana Dr.Karl Heinz na kufahamika dunia nzima, kila alikokwenda kuhubiri maelfu ya watu walikusanyika kumsikiliza, katika kila nchi aliyokwenda ilikuwa ni lazima ndege mbili za madawa ya kulevya zimfuate na kushusha mizigo usiku, hakuna mtu aliyetilia mashaka wala kufuatiliwa wengi waliamii ilikuwa ni misaada aliyogawa kwa wasiojiweza.
Karl Heinz aliheshimiwa mpaka na viongozi wa serikali katika nchi nyingi duniani, alikaribishwa Ikulu katika kila nchi aliyokwenda na kula chakula na Marais, aliwapa viongozi wa Afrika pesa nyingi kwa ajili ya maendeleo lakini hakuna mtu aliyeijua siri ya utajiri wake.
Kilichowashangaza watu waliosafiri naye ni kitendo cha kila mtu aliyeteuliwa kuwa msaidizi wake kuchanganyikiwa na kuwa mwehu baada ya kufanya kazi kwa kipindi kirefu na baadaye kukutwa amekufa! Hapakuwepo na maelezo ya kutosha kuhusu vifo vyao, wasaidizi karibu wanne walishakufa kwa mtindo huohuo na Patrick ndiye msaidizi wake wa tano!
Siri ya vifo hivyo vya wasaidizi hao hakuna aliyeielewa isipokuwa Mwinjilisti Karl Heinz mwenyewe, ukweli ni kwamba aliwaua baada ya kuigundua siri yake ya madawa na kuanza kuhoji! Aliwapulizia dawa aina ya Pedraxone iliyowachaganya akili na kuwatia wehu na baada ya hapo aliwatilia sumu katika chakula na kuwaua! Karl Heinz hakutaka hata siku moja siri yake igundulike.
*****
“Nimefurahi sana kukutana na wewe mtumishi wa Mungu!” Alisema Patrick huku akitabasamu na alisema hayo kwa kutokujua ubaya wa Dr Karl Heinz, alikuwa mnyama na mkatili lakini dunia haikuelewa na haikuwa rahisi hata siku moja kulifahamu jambo hilo kwa sababu Mwinjilisti Karl alijificha chini ya mwavuli wa dini!
“Unaweza kutunza siri lakini kijana?”
“Naweza mtumishi wa Mungu!”
“Tafadhali kumbuka hutakiwi kusema chochote cha ajabu utakachokiona sawa?”
“Sawa mtumishi wa Mungu!” Aliitikia Patrick.
*****
Wodini:
“Blandina hivi hauna pesa kidogo tukanunue angalau chupa kadhaa za dripu wakati tunasubiri dawa zetu zifike?” Muuguzi alimuuliza mwenzake.
“Ninayo shingili 5000 na tunaweza kuitumia tu!”
“Basi acha mimi nikaongee na daktari ili tununue maji kwenye duka la dawa vinginevyo hata hawa nao watakufa!’
Baada ya kusema maneno hayo muuguzi alitoka mbio kuelekea ofisini kwa daktari lakini kabla hajafika alikutana na wauguzi wengine wakikimbia kuelekea katika chumba alichotoka muuguzi huyo.
“Vipi hali za wagonjwa?”
“Ni mbaya sana sista, nilikuwa nakwenda kumwomba daktari tukanunue angalau maji ya dripu kwenye duka la dawa!”
‘Hapana twende tu wodini dawa zimeshakuja!”
Walisaidiana na kuanza kutembea kwa haraka kurudi tena wodini ambako walimkuta Nancy na Anne katika hali mbaya kupita kiasi, walitundika chupa za maji na kuzichomeka katika mshipa yao ya damu zikaanza kutiririka kwa kasi kubwa ili kufifia maji yaliyopotea miilini mwao.
Kila chupa ilipoisha ilibadilishwa na dawa walizopewa kwa mdomo na kuzitapika zilianza kupitishwa katika mishipa ya damu, kwa masaa arobaini na nane ya kutumia maji na dawa hali zao zilianza kubadilika na kuwa nzuri, ngozi zao zilianza kupendeza na kujaa badala ya kusinyaa! Fahamu zilianza kuwarejea akilini.
Siku ya tatu Nancy alipopata nguvu vizuri alijigeuza na kuagalia upande wa pili wa kitanda chake, alikutanisha macho na sura ya mama yake akimwangalia na kutabasamu!”
“Nancy mwanangu!”
“Naam mama!”
“Tumenusurika na kifo kwa uwezo wa Mungu!”
“Kweli mama, wenzetu wote wamekufa!”
“Umejuaje?”
“Nilisikia kwa mbali manesi wakiongea!”
Hawakuweza kuongea sana siku hiyo sababu miili yao haikuwa na nguvu za kutosha lakini siku ya tano wakiwa wodini walikuwa wazima kabisa, hawakuharisha wala kutapika tena, kila mtu hospitali alishangazwa na muujiza uliotokea.
*****
Mama ilikuwaje ukawa mzima wakati hata kaburi lako tuliliona nani alikufa?”
“ Sikufa mimi alikufa rafiki yangu Zena, alijichoma sindano ya sumu!”
Pamoja na kuwa Anne kufurahi sana kutana na Nancy, bado alitaka kufahamu ni wapi alikokuwa mtoto wake wa kiume Patrick, alipojibiwa kuwa Patrick alikufa, alidondosha machozi ya huzuni.
******
Siku ya sita maaskari wa magereza walimfunga Anne pingu zake mikononi na safari ya kuelekea gereza la Segerea iliendelea, Nancy ilibidi aungane nao katika safari moja. Walipoingia Dar es Salaam Anne alipelekewa moja kwa moja gerezani Segerea, ambako alipokelewa kama mfungwa lakini kote huko Nancy alifuata kwa nyuma.
“Mwanangu Nancy utakwenda wapi sasa?”
“Sitaki kuondoka nataka nikae na wewe mama!” Alisema Nancy huku akilia machozi.
“Huwezi kukaa na wewe mimi gerezani mwanangu!” Alijibu Anne na kuanza kuvutwa na maaskari kuingizwa gerezani.
“Mama!Mama! Mama!” Aliita Nancy.
Nancy alikaa chini na kuanza kulia hakujua aende wapi baada ya kutoka gerezani, alitembea hadi barabarani ambako alisimama na kuanza kulia machozi, njaa ilimuuma kupita kiasi na hakujua angepata wapi chakula cha mchana huo.
Ghafla aliona gari dogo aina ya Pickup likija mbele yake, Nancy alisogea hadi katikati ya barabara na kuanza kulisimamisha,gari hilo.
“Shikamoo dada!” Nancy alimwamkia mwanamke aliyekuwa akiendesha gari hilo liliposimama na baadaye alimwamkia mwanaume aliyekaa upande wake wa kushoto!
“Naomba shilingi mia nikale nina njaa dada!”
“Baba Teddy una mia tano hapo?” Mama huyo alimuuliza mwanaume aliyeonekana kuwa mumewe aliyekaa pembeni akisoma gazeti la Amani.
“Sina darling nina kubwakubwa tu!”
“Ingia kwenye gari twende pale mbele ukale hotelini!” Mama yule alisema na Nancy alianza kupanda nyuma ya gari hilo.
“Hapana njoo ukae huku mbele!” alisema mwanaume huyo na kufungua mlango, Nancy akaingia na kukaa katikati yao.
“Mimi naitwa mama Teddy na huyu ni mume wangu anaitwa Kidubo wewe unaitwa nani binti!”
“Ninaitwa Nancy!”
“Jina zuri sana unakaa wapi hapa Segerea?”
“Mimi ni mgeni!”
“Mgeni kutokea wapi?”
Alipoulizwa swali hilo Nancy alianza kulia machozi na baadaye kusimulia kila kitu kilichotokea katika maisha yake, hakusahau kueleza juu ya mama yake aliyeingia siku hiyo hiyo gerezani Segerea.
“Pole sana, je umeokoka?”
“Hapana ila natamani sana kuwa hivyo!”
“Twende basi ukale tutakusubiri twende kwenye mkutano wa dini, kuna mhubiri mmoja anaitwa Karl Heinz kutoka Ujerumani anahubiri vizuri na tukitoka huko tutakuja nyumbani kwetu utaishi na sisi sawa?”
“Sawa dada!”
Walimpeleka hotelini akala na baadaye wakaondoka kwenda jangwani kwenye mkutano, watu walikuwa wengi sana siku hiyo kwa sababu ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya mkutano! Mama Teddy, Kidubo na Nancy walisimama nyuma kabisa na haikuwepo nafasi ya kusogea mbele zaidi! Walianza kusikiliza mkutano hadi mwisho mambo yote yalioongelewa katika mkutano huo yalimgusa Nancy na alilia karibu muda wote wa mahubiri hayo.
“We have only three minutes to be in Dar es Salam, let me introduce to you my new tour assistant, I met this boy here yesterday and I’m going to be travelling with him wherever I go, his name is Patrick!”(Tuna dakika tatu tu za kuwa hapa Dar es Salaam, acha nimtambulishe kwenu msaidizi wangu mpya wa safari, ni kijana niliyekutana naye hapa jana na nitasafiri naye kila niendako jina lake anaitwa Patrick!)
Patrick alipunga mkono wake hewani na sekunde chache baadaye wote walianza kuteremka jukwaani na kuingia katika magari tayari kwa safari ya kuelekea Zambia.
Nancy aliposikia jina Patrick alishtuka na kuacha kulia, alipoangalia mbele yake jukwaani, hakuamini macho yake alipomwona Patrick akipunga mkono hewani.
“PATRIIIIIIIICK!” Alipiga kelele na kuchomoka akaanza kukimbia kwenda mbele akipita katikati ya watu lakini alipofika kwa Anne magari tayari yalishaanza kuondoka, alipaza sauti akiita jina la Patrick huku akiyakimbiza magari hayo!
Je nini kitaendelea?
Je, Nancy atafanikiwa kumpata kaka yake?
Na je nini kitampata Patrick kwa Mwinjilisti karl?
Fuatilia Siku ya Jumapili mahali hapa.
Usisahau kushare na kuwakumbusha marafiki zako kuhusu hadithi zinazopatikana katika app hii ya kipekee. 


HADITHI: TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 24
MTUNZI: ERIC JAMES SHIGONGO
“Patrick! Patrick! Patrick!” Nancy aliendelea kuita huku akiukimbiza msururu wa magari ulizidi kusogea mbele kuingia barabara ya Morogoro kutoka viwanja vya Jangwani, alilipita kila gari akiita jina la kaka yake lakini hakuitikiwa! Nancy alichanganyikiwa na kushindwa kuelewa ni wapi Patrick alikokuwa.
“Dada vipi mbona unahangaika?”
“Mimi?”
“Ndiyo!”
“Namtafuta kaka yangu Patrick!”
“Patrick gani?”
“Aliyetangazwa jukwaani kama msaidizi wa Mwinjilisti Heinz! Nimepotezana naye siku nyingi na niliamini alishakufa!”
“Unamwongelea kijana aliyetambulishwa na Mwinjilisti?”
“Ndiyo!”
“Njoo nikuonyesha gari alilipanda!” Kijana huyo alimshika Nancy mkono na kuanza kumvuta kuelekea mbele ulikoelekea msafara wa magari.
Walipokaribia mwanzo wa msafara huo, kijana alijishika kichwani na kuonyesha masikitiko makubwa huku akimwangalia Nancy usoni.
“Nini?” Nancy aliuliza.
“Gari lenyewe ndiyo lile linaloingia barabarani!” Alisema kijana huyo baada ya kuliona gari aina ya Landcruiser Vx likiingia barabara ya Morogoro na kuongeza kasi.
“Una uhakika Patrick kapanda gari hilo kaka?”
“Ndiyo na si yeye tu bali hata mtumishi wa Mungu Heinz!”
“Kweli?”Nancy aliuliza tena.
“Ndiyo!”
“Asilimia mia moja?”
“Ahsante kaka kwa msaada wako Mungu akubariki sana!”
Alisema Nancy na kuondoka mbio akikimbia kwenda mbele, hakufuata barabara ya lami bali alikimbilia bondeni kwenye nyasi akijaribu kuliwahi gari ambalo Patrick alidaiwa kupanda. Mwisho wa bonde aliingia barabarani na kuyaona magari yote yamesimama na alipoangalia mbele yake aliona taa nyekundu zikiwaka!
“Hizi nafikiri ndio taa za kuzuia magari ambazo huwa nazisikia, lazima gari lililombeba Patrick litakuwa miongoni mwa gari haya !” Aliwaza Nancy na kuanza kupepesa macho yake kuangalia magari yote yaliyokuwa katika mstari yakisubiri taa ziruhusu.
Ghafla aliliona gari alililoonyeshwa likiwa kama hatua thelathini hivi kutoka mahali aliposimama! Furaha kubwa ilijaa moyoni mwake akawa na uhakika wa kumpata kaka yake Patrick.Watu waliokuwa ndani ya magari mengine walimwona kama mtu aliyechanganyikiwa, Nancy hakujali wala kuona aibu aliendelea kuliita jina la nduguye huku akikimbia kulielekea gari!
Alipokaribia gari hilo alizisoma namba zake na kuona ndio lenyewe, akawa na uhakika zaidi ya kumpata pacha wake! Akaongeza mbio zaidi lakini hatua kama tatu hivi kabla hajaligusa gari hilo taa nyekundu zilibadilika na kuwa kijani magari yote yakaanza kuondoka kwa kasi.
“Patrick! Patrick! Patrick! Mimi dada yako niko hapa!” Alipaza sauti Nancy lakini sauti yake yake haikusikika sababu gari hilo lilifungwa vioo vyote!
Nguvu zilimwishia Nancy miguuni na kwa sababu ya kukimbia sana alijisikia mvurugiko wa tumbo na kuanza kutapika! Hakutaka kupoteza muda aliendelea kukimbia huku akitapika kuufuata msururu wa magari uliokuwa ukienda kwa kasi kubwa.
“KUUUUUUUUUU!” Ulikuwa ni mlio wa magari yaliyogonana ghafla.
“Wee mshamba utaua watu!” Kelele zilisikika kutoka ndani ya magari yaliyokuwa jirani na eneo hilo, Nancy alikuwa amekatisha barabara ghafla akikimbia, kidogo tu agongwe vibaya kama dereva asingemkwepa! Lakini katika kufanya hivyo gari lake lilikutana uso kwa uso na daladala lililokuwa likitoka upande wa pili!
Kwa hofu ya kupigwa Nancy hakusimama alizidi kukimbia mbio kwenda mbele zaidi, dereva wa daladala alichomoka kwenye usukani na kuanza kumkimbiza, hasira kali ilimshika sababu ya kuharibiwa gari lake kwa uzembe wa Nancy, hatua chache tu mbele alimtia Nancy mkononi na kuanza kumzaba vibao usoni.
“Nisamehe kaka ....mimi ni mgeni hapa mjini!” Alisema Nancy huku machozi yakimtoka.
“Ukiwa mgeni ndiyo ukatishe barabara vibaya kiasi hicho, ungekufa wewe!”
“Ahsante kwa kuokoa maisha yangu kaka, nisamehe na Mungu atakulipia gari lako!”
Dereva alimmshushia Nancy ngumi mzito usoni, iliyomfanya avimbe juu ya jicho lake, alinguka chini na kusikia kizunguzungu lakini sababu alikuwa akilikimbiza gari lililombeba Patrick alijitahidi na kunyanyuka ardhini akiwa na maumivu yake na kuendelea mbele! Watu ndani ya magari walimcheka na kumzomea, roho yake iliuma lakini hakuwa na la kufanya.
Mbele kidogo alikuta magari yote yakiwa yamesimam kama ilivyokuwa nyuma na alipotupa macho yake mbele aliyaona mataa mengine yakiwaka kwa rangi nyekundu! Alijua gari lililombeba Patrick lilikuwa miongoni mwa magari hayo, Nancy aliongeza mbio jicho lake lilimuuma lakini hakujali, alipotupa macho mbele zaidi aliliona gari lililombeba l Patrick likiwa mbele ya magari yote, akaongeza mwendo zaidi lakini kabla hajalifikia taa za kijani ziliwaka na kuyaruhusu magari kuendelea na safari.
Aliendelea kuliita jina la Patrick wakati akikimbiza gari hilo, almanusura agongwe na lori lililobeba mchanga! Roho ya Nancy ilizidi kuuma akajikuta akilia machozi zaidi.
Hakukata tamaa alizidi kulifukuza gari hilo kwa nyuma, alikuwa amechoka kukimbia lakini aliendelea kwani alipania mno kukutana na kaka yake na pacha wake Patrick na alitaka kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa anazuia safari yake ya kwenda nchi za nje na Mwinjilisti Heinz ! Alijua wazi Patrick alichukua uamuzi huo baada ya kuona hakuwa na ndugu tena Tanzania.
Mbele kidogo kwenye mataa ya Lumumba na barabara ya Morogoro Nancy aliyaona magari yakisimama, alikimbia zaidi lakini hakuyawahi kwani kabla hajayafikia taa ziliruhusu na magari yakaanza kuondoka kwa kasi, Nancy alichoka na kuamua kutembea taratibu hadi kwenye makutano ya barabara za Morogoro na bibi Titi ambako aliyaona magari hayo yakikata kushoto kwa mwendo wa kasi.
Hakuweza kukimbia zaidi ikabidi atembee taratibu, mbele aliingia barabara ya Bibi Titi Mohamed, giza lilishanzaa kuingia na taa ziliwaka kila mahali, kwa msaada wa taa alifanikiwa kusoma mabango ya ofisi mbalimbali kushoto kwake, aliona bango la ofisi za Tritel na mbele kidogo kwenye mataa ya Bibi Titi na barabara ya Azikiwe aliona bango jingine lililosomeka “Maktaba ya Taifa”!
“Sasa sijui magari hayo yaliekea upande gani? Sijui yalinyoosha au yalikata kulia?” Alijiuliza Nancy baada ya kuchanganikiwa juu ya upande yalikoelekea magari ya msafara wa mwinjilisti Heinz! Baada ya kufikiri kwa muda hatimaye aliamua kukata kulia kuingia barabara ya maktaba na kunyoosha moja kwa moja hadi Posta mpya lakini hakuona dalili yoyote ya kuliona tena gari lililombeba Patrick wala magari mengine ya msafara wa Mwinjilisti Heinz!
****************
Alipofika maeneo ya Posta alishangazwa na umati wa watu wengi wakisubiri magari ya kuwarudisha majumbani kwao, alizunguka hapo kwa muda bila kuelewa aelekee wapi au amuulize nani! Ghafla alipomwona msichana mmoja akipita jirani yake, msichana huyo alikuwa na biblia mkononi mwake, Nancy alijua huo ndio ulikuwa msaada pekee kwake wakati huo alimkimbilia na kumshika bega!
“Dada yangu samahani sana kwanza shikamoo!”
“Marahaba mdogo wangu, vipi mbona unalia?’
“Mimi?”
“Ndiyo!”
“Ninamtafuta kaka yangu!”
“Wewe ni mgeni hapa?”
“Ndiyo!”
“Unatoka wapi?”
“Mwanza!”
“Huyo kaka yako anafanya kazi wapi?”
“Hafanyi kazi ila yupo na Mwinjilisti Heinz aliyekuwa akihubiri kwenye viwanja vya!……….vya!……..vya! Vya Jangwani!”
“Aha! Yule kafikia hoteli ya Sheraton!”
“Ipo wapi hiyo dada?”
“Pitia hapa!” Alimwonyesha barabara iliyoshuka chini kupitia makao makuu ya wizara ya mambo ya ndani na makao makuu ya posta nchini Tanzania!
“Sawa!”
“Pale mbele utakutana na barabara nyingine inayokatisha, hiyo ni mtaa wa Ohio! Hapo kata kushoto mbele utaona jumba refu mkono wa kulia si unajua kusoma?”
“Ndiyo!”
“Basi hapo utaona bango lililoandikwa Sheraton, kuna magari mengi sana utayakuta, ukifika ulizia tu watakuonyesha chumba cha huyo Mwinjilisti!”
“Ahsante sana dada yangu sina namna ya kukushukuru!” Alisema Nancy na kuanza kuondoka eneo hilo mbele kidogo aliona kibao kilichoandikwa ‘Ohio street’ alikata kushoto kama alivyoelekezwa na kusonga mbele, aliliona ghorofa refu zaidi mkono wake wa kulia na kukata kona kuingia hotelini hapo.
Alishangazwa na uzuri wa hoteli hiyo na kwa jinsi alivyovaa nguo chafu alihisi asingeruhusiwa kabisa kuingia ndani ya hoteli hiyo, alijipa moyo na kusonga mbele!
“Mimi sijali hata kidogo ili mradi tu nimwone Patrick!” Alijisemea Nancy akielekea geti la hoteli hiyo.
Tayari ilishatimua saa tatu ya usiku, Nancy alitembea bila kujiamini alipolifikia lango la kuingilia hotelini askari wa ulinzi alimsimamisha.
“wee changu unakwenda wapi?”
“Mh! Unasemaje kaka yangu?”
“Nakuuliza unakwenda wapi saa hizi?”
“Humu hotelini!”
“Hapana! Utawala wa hoteli umezuia kabisa nyinyi msiingie humu ndani wateja wenu wawakute hukohuko mtaani!” Alisema askari na kuanza kumsukuma Nancy kumtoa nje ya hoteli hiyo.
“Kaka sikuelewi?”
“Kama hunielewi basi shauri yako kafanyie umalaya wako nje!”
“Umalaya? Kwa umri huu mdogo niwe malaya, tafadhali nisikilize kaka yangu nikusimulie shida yangu!”
“Hakuna! Sitakii! Toka nje!” Alisema askari huyo akimsukuma Nancy kumtoa nje na kulifunga lango nyuma yake.
Nje Nancy aliendelea kulia akiligonga lango hilo, ilikuwa si rahisi kuamini kuwa kaka yake na pacha wake Patrick alikuwa ndani ya hoteli hiyo lakini alizuiliwa kumwona, alilia kwa uchungu na kuendelea kuligonga lango!
“Nifungulieni jamani! Nifungulieni, nimwone kaka yangu!”
“Kaka yako gani malaya wewe, toka hapa na nikitoka huko nje utanitambua!”
Nancy hakusikia onyo hilo la askari aliendelea kulia akibisha hodi mlangoni, mlinzi alitafsiri hiyo kama dharau na kuamua kutoka hadi nje ambako alimkuta Nancy na kumbeba juu juu hadi barabarani ambako alimbwaga chini na kurudi ndani ya hoteli.
Muda mfupi akiwa chini kundi la wasichana waliovaa nguo fupi na wengine wakiwa na chupi peke yake walimvamia, Nancy alitetemeka akifikiri labda wasichana wale walikuwa wachawi!
“Mdogo wetu vipi, umetoa huduma wamekudhulumu nini? Maana hapa kuna wazungu wadhulumati ile mbaya!”
Nancy alizidi kuwaangalia kwa mshangao hakuelewa kitu walichokua wakimweleza, aliendelea kulia machozi, kabla hajawaeleza kilichotokea walishtukia magari mawili aina ya Landrover yakiegesha pembeni yao, wasichana wengine wote walitimukia porini na kuwaacha Nancy na msichana mwingine mmoja ambao walijikuta mikononi mwa polisi, walifungwa pingu na kutupwa nyuma ya gari ambako walikutana na askari mwenye virungu, aliyekitumia vizuri kirungu chake juu ya vichwa vyao! Nancy alilia kupita kiasi.
“Nyie malaya tumeshawaeleza msikae mtaa huu wanapita viongozi hamsikii siyo?” Askari alisema huku akiendelea kuwagonga na virungu vichwani, kama wewe mtoto mdogo kabisa unafanya umalaya.
“Mimi siyo……!” Nancy alijaribu kujieleza lakini kabla sentensi yake haijafikia mwisho kirungu kilitua juu ya pua yake na damu zilianza kutoka puani.
“Kimya! Funga domo lako changu wee unafikiri mimi nataka mapenzi hapa?” Alifoka askari huyo.
Kwa upande wake Nancy aliamini kama angepewa nafasi ya kujieleza askari huyu angeweza kumwachia huru lakini nafasi hiyo haikuwepo.
Walipofikishwa kituoni walitupwa mahabusu bila hata kutoa maelezo, kila mtu aliwaita malaya wazururaji, majina hayo yalimuuma sana Nancy ukizingatia katika maisha yake hakuwahi hata mara moja kukutana na mwanaume kimapenzi.
“Ninaitwa Lwina! Sijui mwenzangu unaitwa nani?” Changudoa waliyekamatwa nae alimuuliza, Nancy hakujibu aliendelea kulia machozi ya uchungu mambo yalikuwa yakitokea katika maisha yake yalimsikitisha kupita kiasi, hata siku moja katika maisha yake hakuwahi kufikiria kuwa angeweza kuitwa malaya!
“Unaitwa nani?”msichana yule aliuliza tena.
“Mimi naitwa N….a..n…cy!” Alijibu huku akilia machozi.
“Jina lako zuri sana wewe huwa unasimama kiwanja gani? Sababu kiwanja cha Ohio ndio kwanza nimekuona leo? Huwa upo Kinondoni au Las Vegas nini?”
“Hapana!”
“Oysterbay?”
“Viwanja vya nini dada?”
************
Kidubo na mke wake mama Teddy walimtafuta Nancy kwenye mkutano bila mafanikio, walishaamua kuishi naye nyumbani kwao mpaka mama yake amalize kifungo cha miaka mitano, walijua Nancy alikuwa na matatizo na alihitaji msaada mkubwa na waliamini msaada huu ulikuwa mikononi mwao.
Watu wote kwenye mkutano walisambaa bila Nancy kuonekana, ndipo walipoamua kuzunguka huku na kule jijini wakimtafuta bila mafanikio mwisho walikata tamaa na kuamua kuondoka kurejea nyumbani kwao Segerea.
“Si ajabu amekutana na kaka yake na kuamua kuondoka naye!” Kidubo alimwambia mke wake.
“Inawezekana!” Mkewe aliitikia.
“Basi tena Mungu anajua!”
Walirejea nyumbani wakiwa na masikitiko makubwa mno kumpoteza Nancy Moyoni mwao walishampenda sana Nancy na walitaka kumsaidia!
****************
Mpaka usiku wa manane ndani ya hoteli ya Sheraton wakiwa wamelala chumba kimoja na Mwinjilisti Heinz, Patrick alikuwa bado hajapata usingizi akiyafikiria maisha yake! Hakuamini yote yaliyomtokea katika maisha yake, kukutana na mzungu na kukubali kumsaidia hakikuwa kitu alichowahi kukifikiria maishani mwake.
Pamoja na mawazo hayo yote bado aliendelea kuwafikiria mama na dada yake Nancy ambao aliamini walikuwa wafu! Hakuwa na taarifa yoyote kuwa usiku huo Nancy alishakuja hadi nje ya hoteli ya Sheraton akimtafuta! Mawazo juu ya mama na dada yake yalimfanya atokwe na machozi.
Ghafla alishtukia akimwona Mwinjilisti Heinz akinyanyuka kitandani kwake na kwenda kwenye moja ya masanduku yake na kulifungua akatoa kitu kama bomba la sindano na chupa ya dawa fulani! Alitupa macho yake kuangalia kwenye kitanda cha Patrick, Patrick aliamua kujifanya amelala ili ajue ni kitu gani kilichotaka kutokea, Mwinjilisti alisogea hadi karibu kabisa na kitanda cha Patrick na kumchunguza usoni.
“He is fully asleep!”(amelala fofofo)Mwinjilisti alisema peke yake na kuondoka.
Patrick alishuhudia kila kitu kutoka kwenye kona ya jicho lake la kushoto alimwona Mwinjilisti akihangaika kujifunga na mpira wa plastiki na kujipigapiga, alionekana kama mtu aliyekuwa akitafuta mishipa wa damu mikononi mwake. Alionekana kutofanikiwa ndipo alipochukua mpira huo na kuufunga sehemu za siri kwenye uume wake! Kwa macho yake yote mawili Patrick alishuhudia Mwinjilisti akichoma sindano ndani ya uume wake! Alilegea na kuanza kulala hapohapo sakafuni.
Patrick aliogopa na kunyanyuka kitandani kwake kumkimbilia Mwinjilisti, akidhani labda madawa aliyojichoma yalimzidi.
“Mtumishi! Mtumishi! Mtumishi wa Mungu Heinz!” Patrick aliita lakini Mwinjilisti hakuitikia aliendelea kukoroma na kudondosha udelele mdomoni kwake.
Patrick alimnyanyua na kumpandisha Mwinjilisti kitandani huku akitetemeka, alifikiria kupiga simu mapokezi ili waje wampe msaada!
Patrick ameshuhudia mambo ya Mwinjilisti Heinz ambayo ni siri kubwa na Mwinjilisti humuua mtu yeyote agunduaye siri hiyo!
Je nini kitampata Patrick?
Nancy yupo mahabusu akidhaniwa ni changudoa!
Je nini kinafuata?
Sasa unaweza kushare hadithi hii ili marafiki zako waweze kuisoma zaidi.

Post a Comment

Previous Post Next Post