TAFADHALI MAMA USIWAUE WATOTO WANGU 30 MWISHOOOOO


Jioni ya siku hiyo mchungaji Aaron hakurudi tena nyumbani kwake alipangishiwa chumba katika hoteli waliyofikia Patrick, Nancy na mama yao, usiku waliongea mambo mengi yaliyopita katika miaka yote ambayo hawakuwa pamoja! Mchungaji hakuamini kama kweli alikuwa amekutana na familia ile tena.
“Niliwahi kwenda Tanzania wakati fulani nikaelezwa kuwa ulikufa baada ya kupewa sumu gerezani kumbe haikuwa kweli?”
“Aliyekufa ni rafiki yangu alikula chakula chenye sumu kabla ya kukifikisha kwangu! Watu wote hata watoto wangu walielewa mimi nilikufa!”
“Aisee! Kwahiyo kifungo ulimaliza?”
“Nilimaliza na Nancy aliyekuwa ameolewa Uingereza alinichukua kwenda kwake ambako nilikutana tena na Patrick aliyeondoka akiamini mimi na Nancy tulikuwa marehemu!” Alisema Anne na kuendelea kufafanua zaidi baada ya mchungaji kuonekana hakuelewa.
Siku iliyofuata mkutano uliendelea na watu walizidi kuokolewa na kuponywa magonjwa yao, sifa za Patrick zilizidi kusambaa nchini Kenya, alipomaliza mkutano wa wiki moja mjini Nairobi alialikwa tena Kisumu na baadaye Kisii! Hawakuona tena sababu ya kurudi Nairobi waliamua kupanda basi hadi Musoma ambako pia walifanya mkutano mkubwa kwa muda wa wiki mbili.
Kutoka Musoma walihubiri mjini Mwanza, mji uliowakumbusha mengi kuhusu maisha yao, ndipo mahali walipozaliwa na kukulia! Baadhi ya watu waliwakumbuka Patrick na Nancy.
Wakiwa mjini humo walipata nafasi ya kutembelea makaburi ya kaka zao waliofariki na kaburi la baba yao Huggins! Walipoiona nyumba waliyoishi watu walilia machozi, historia yao ilikuwa ya maumivu makubwa mno.
“Hakuna haja ya kuhuzunika sana kwani tayari tunaye Yesu Kristo! Na tumeokolewa tunachohitaji ni kufurahi kila siku!” Patrick alisema wakati akijaribu kuwasihi mama na dada yangu wanyamaze kulia, yote hayo yalitokea wakati wakitembea kutoka makaburini.
*****
Baada ya kuhubiri mjini Mwanza waliendelea na safari yao hadi Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Morogoro na hatimaye kuingia jijini Dar es Salaam, wote walifurahi kuingia tena Dar es Salaam ambako mkutano mkubwa sana wa wiki moja uliendelea katika viwanja vya Jangwani, waumini wa madhehebu mbalimbali walihudhuria kujifunza neno la Mungu na wagonjwa waliombewa.
Mara ya kwanza watu waliposikia habari za mhubiri wa kimataifa Patrick Heinz hawakufikiri alikuwa ni Patrick mtoto waliyemfahamu, aliyetambulishwa kwao na Mwinjilisti Heinz kama msaidizi walipokutana Dar es Salaam kwa mara ya kwanza miaka mingi kabla!
Siku ya kwanza ya mkutano huo watu wote walishangaa kumwona Patrick akiwa jukwaani akitenda miujiza katika jina la Yesu!Sura ilikuwa ni ileile ingawa mwili wake uliongezeka ukubwa na unene kwani alipoondoka Tanzania alikuwa mtoto mdogo.
Mamia ya watu walihudhuria mikutano yake, kwenye viwanja vya jangwani wengi waliokolewa na wenye magonjwa waliponywa! Waliopotea walirejewa na imani zao! Kwa watu wengi waliozoea wahubiri wa kizungu ilikuwa si rahisi kuamini Patrick alikuwa Mtanzania.
“Ndugu zangu Mungu ni mwema sana!”
“Ameeeeeeeeeeni!”
“Wangapi kati yenu wanakumbuka niliposimama katika jukwaa hili hili miaka mingi iliyopita nikiwa na Mwinjilisti Heinz?” Patrick aliuliza mkutanoni na mikono mingi ilionekana hewani kuonyesha kuwa walimkumbuka.
“Sasa nitawapa ushuhuda wangu mpo tayari?”
“Ndiyooooo!”
“Bwana alinichagua mimi kuwa mtumishi wake na ninapenda kusema kuwa zipimeni kila roho zinazokuja kwenu, Mwinjilisti wa kimataifa Heinz hakuwa mtumishi wa Mungu kama mlivyofikiri bali alikuwa Mafia na muuzaji wa madawa, alitumia mgongo wa dini kusafirisha madawa yake, alifanya miujiza kwa kuwanusisha watu madawa ya kulevya! Tukiwa safarini pamoja nilimgundua na nikamwomba Mungu awaokoe watu wake na akakutana na mkono wa Mungu na kufa! Haleluyaaa!”
“Ameeni!”
“Ni wangapi walipatwa na miujiza ya Mwinjilisti Heinz kati yenu, kama wapo wapite mbele upesi!” Alisema Patrick na ghafla vijana kama ishirini hivi wenye afya mbaya walianza kutembea kuelekea jukwaani walionekana kama wendawazimu.
“Waacheni wapande huku juu ninahitaji kuongea nao!”
Vijana wale walipanda jukwaani, wengi walikuwa wakilia machozi, walikuwa wamekonda na walivaa nguo chafu zilizonuka Patrick alijua wazi halikuwa kosa lao.
“Hebu wewe nieleze tangu wakati huo unaaishije?”
“Siwezi kuishi bila kuvuta unga mtumishi wa Mungu, kila siku ni lazima nivute unga wa shilingi 8,000! Nisipovuta huwa mgonjwa kabisa na wenzangu wawili waliokuwa wacha Mungu wazuri na tulisali nao kanisa moja walijikuta wanaacha imani na kuwa wezi ili wapate pesa ya kununulia madawa wengi walichomwa moto na wananchi wenye hasira na kufa!”
“Je unampenda Yesu bado?”
“Ndiyo maana nipo hapa nisaidie mtumishi wa Mungu ili niepukane na madawa sipendi kuwa hivi!” Aliendelea kusema msichana huyo aliyeonekana kuathirika na madawa kuliko wengine.
Patrick aliendelea kuwauliza mmoja baada ya mwingine na maelezo yao yalifanana! Roho ilimuuma sana akawaomba wapige magoti na kuanza kuwaombea akishirikiana na wachungaji wengine waliokuwepo mkutanoni baada ya maombi wote walisimama kila mmoja akiahidi kuchukia dawa na walionekana wenye nguvu!
“Najua wapo wengi wa aina hii kati yenu na si ajabu wameshindwa kujitokeza mbele, mkono wa bwana utawagusa na kwa sababu sasa hivi tutaanzisha kanisa hapa Dar es Salaam nitawaomba muwe mnahudhuria kanisani nina imani mtafunguliwa kwa sababu Mungu anaweza kuponya!” Alisema Patrick akiagana na vijana hao.
******
Alihubiri wiki zote mbili watu walizidi kubadilika, siku ya mwisho wa mkutano wake aliamua kutoa ushuhuda wa maisha yake mwenyewe, aliongea juu ya shida alizozipata maishani, mateso ya mama yake na alivyonusurika na kifo cha sumu katika chakula, watu walisikitika sana kwani wengi hawakutegemea historia yake ingekuwa hivyo!
Karibu watu wote uwanjani walilia machozi wakati Patrick akiwasimulia usiku yeye na dada yake walipokuwa makaburini na jinsi alivyopotezana na familia yake akiamini walikufa mpaka walivyokutana tena nchini Uingereza akijua duniani alikuwa peke yake.
“Kwa kweli Mungu ni mwema sana ndugu zangu kwani leo hii amemponya mama yangu na ugonjwa wa hedhi isiyokatika na amenifanya mimi kuwa mtumishi wake! Haleluya!”
Jioni ya siku hiyo walirejea hotelini ambako Nancy aliongea kitu ambacho hakuna mtu kati yao alikitegemea
“Hivi mnawakumbuka anti suzanne na mumewe Anorld?”
“Ndiyo ninawakumbuka!” Alijibu Patrick.
“Unajua sisi tumeokoka hata kama walitaka kumuua mama yetu, ni vyema tuwasamahe ili tuwe wakamilifu, nina uhakika bado wapo gerezani kwanini tusiwafuate gerezani tukawaombe kama kuna kitu tulichowakosea?” Aliuliza Nancy.
“Mimi sina matatizo, au vipi wewe mama?” Patrick alimuuliza mama yake.
“Haina tatizo ninahitaji kuonana na Suzanne ili niongee nae juu ya suala hili!”
“Ulishasamehe au bado?”
“Nilisamehe miaka mingi iliyopita wala sina kumbukumbu tena!” Alijibu Anne
“Basi kesho twende gerezani nimesikia walihamishiwa gereza la Keko!”
Fikra juu ya Anorld na Suzanne ziliwafanya wote wasikitike sana Anne hakutaka kuyapa nafasi yaliyopita ili mradi alikuwa na watoto wake na maisha yake hayakuwa na machozi tena!
Kesho yake asubuhi walidamka na kukodisha gari lililowapelekea hadi gerezani Keko! Walifika gerezani saa mbili kamili na kuomba kuonana na Anorld pamoja na mkewe Suzanne!
“Asubuhi yote hii nyie ni nani zao?’
“Mimi ni binadamu yake na Suzanne na hawa ni watoto wangu Patrick na Nancy!”
“Subirini kwanza nikawaangalie, lakini sijui... unajua hapa gerezani kuna kipindupindu na jana tu wote wawili walikuwa wagonjwa taabani sijui hali zao zikoje?”
“Mungu wangu! Kipindupindu watapona kweli?”
“Sijui nisubirini kwanza!”
Afande aliondoka na kuwaacha wakiwa katika wasiwasi mkubwa sana, hawakuelewa angerudi na jibu gani kutoka ndani ya gereza, walihisi hawakuwa tayari kupambana na jibu la Anorld na Suzanne kuwa wafu!
Mpaka dakika kumi hivi baadaye askari jela alikuwa bado hajarejea, wasiwasi wao ulizidi kupanda lakini sekunde chache baadaye walimwona akijitokeza na kuwafuata waliposimama.
“Kwa kweli sijui kama mnaweza kuwaona hali zao ni mbaya sana! Ila nilipowatajia majina yenu wamefurahi hata wao wanataka kuwaona lakini haiwezekani, Anorld amenipa maagizo na kaandika barua hii muisome na labda mjaribu kuja kesho mnaweza kukuta hali zao ni nzuri kidogo angalau mkaongea nao maneno machache!”Alisema askari huyo na kumkabidhi Patrick barua.
Bila kuchelewa Patrick alifungua barua hiyo na kuanza kuisoma, mistari mitano ya mwanzo ilimfanya aanze kulia, hakuimaliza barua hiyo na kumkabidhi Anne. Alipiga magoti chini na kuanza kumwomba Mungu afungulie miujiza juu ya Anorld na Suzanne.
Anne aliipokea barua hiyo nae alianza kuisoma alishindwa kuvumilia na kuanza kulia machozi na kuungana na mwanae Patrick kupiga magoti na kuanza kusali nje ya gereza, aliiweka barua hiyo chini na Nancy akaiokota na kuanza kuisoma taratibu huku akibubujikwa na machozi.
“Anne mimi ni Anorld, naumwa sana na sitegemei kupona! Niliugua kipindupindu tangu juzi, hata nduguyo Suzanne pia anaumwa ugonjwa huohuo najua wazi tutakufa kwa sababu hapa gerezani hakuna dawa wala maji ya kutuongezea, ninaharisha na kutapika isivyo kawaida! Siku zote nimekuwa nikitamani kukutana na wewe ili nikuombe msamaha hatimaye Mungu ametukutanisha katika dakika za mwisho za maisha yetu! Anne naomba uyasikilize maneno yetu yafuatayo.
NI KWELI TULITAKA KUKUUA! Na sababu ya kufanya hivyo ilikuwa ni kutaka kukunyang’anya watoto wako wazuri Patrick na Nancy! Lakini haikuwa mipango ya Mungu akafa mtu tuliyemtuma aje kukuua! Kikubwa ninachosema ni kwamba tusamehe sana Anne, yote yalitokea sababu ya shetani, tusamehe mimi na mke wangu kabla hatujafa! Hatutaki kufa kabla ya kutubu dhambi hii kwako hatuwezi kusamehewa hata mbinguni.
Ahsante.
Niombee msamahe hata kwa wanao ni mimi
Anorld.
Nancy alipomaliza kuisoma barua hiyo alishindwa kuvumilia alilia kwa nguvu na kupiga magoti chini na kuungana na mama na kaka yake wote waliwaombea Anorld na mke wake ili wapone kwa uwezo wa Mungu! Askari jela alibaki akishangaa.
“Kipindupindu kweli kitaponyeshwa na maombi?”“Dada yangu Mungu hashindwa kitu!” Alijibu Patrick baada ya kusali.
Kabla hawajaondoka gerezani walishuhudia gari lililoandikwa ‘Wizara ya Afya’ ubavuni likiwa na maboksi mengi nyuma liliingia gerezani kila mtu alihisi yalikuwa ni madawa ya kipindupindu.
******
Waliporudi asubuhi siku iliyofuata walishangaa kupewa taarifa kuwa hali za Anorld na Suzanne zilikuwa zikiendelea vizuri lakini hawakuruhusiwa kuonana nao mpaka baada ya siku mbili ndipo walikutana nao! Anorld na Suzanne walikuwa wamekonda mno na miili yao ilijaa upele na ukurutu, walipomwona Anne walipiga magoti na kumshika miguu wakimwomba msamaha.
Anne alikataa na kuwaomba wanyanyuke sakafuni nao walifanya hivyo bila kuchelewa, waliongea mengi akiwahakikisha kuwa msamaha alioutoa ulikuwa wa kweli.
Walimueleza wazi kuwa kwa kosa lao walihukumiwa kifungo cha maisha lakini wakili wao alikata rufaa wakawa wamefungwa miaka 15 gerezani kila mmoja na wakati huo walikuwa wamebakiza mika mitatu tu mbele yao.
“Hata sisi tulishampokea Kristo tulihubiriwa hapahapa gerezani!” Alisema Anorld.
“Kweli?” Patrick aliuliza.
“Ndiyo!” Aliitikia Suzanne.
“Basi Mungu amewageuza kama alivyomgeuza mtume Paulo!”
“Ni kweli!”
******
Patrick alijenga kanisa kubwa sana maeneo ya Mwenge jijini Dar es Salaam ambako katika muda mfupi lilipata waumini wengi kupita kiasi, kwa pesa walizokuwa nazo alinunua nyumba tatu nzuri maeneo ya Mikocheni moja alimpa mama yake nyingine dada yake na nyingine akaishi yeye mwenyewe, maisha yao yalikuwa mazuri hatimaye, baada ya mateso ya muda mrefu.
Huduma yake ilikuwa kwa kasi kubwa zaidi nchini Tanzania ikabidi amuagize Mwinjilisti Aaron kutoka Nairobi aje kumsaidia kazi ya Mungu, mchungaji hakuwa na kipingamizi alirejea Dar es Salaam, Patrick alimnunulia nyumba maeneo ya Kijitonyama na kazi ya Mungu iliendelea kukua zaidi na zaidi, walifungua matawi karibu kila sehemu nchini Tanzania, kanisa lilijukana kila mahali na waumini walijiunga kila siku iliyokwenda kwa Mungu.
Miaka mitatu baadaye Anorld na Suzanne walitolewa gerezani na hawakuwa na mahali pa kwenda sababu mali zao zote walishauza katika kuishughulikia kesi yao, ilibidi waende nyumbani kwa Patrick ingawa bado walikuwa na hofu ya kupokelewa, walishangazwa na mapokezi waliyopewa! Patrick aliamua kuishi nao nyumbani kwake, maisha yalikuwa ya raha mustarehe kama vile hapakuwahi kutokea kitu kibaya kati yao.
**************
Maongezi mazito:
“Kijana mimi na mama yako tumekuita!”
“Ndiyo mchungaji!”
“Kuna kitu tunataka kukueleza na sijui kama utatuelewa lakini kwa sababu sisi ni watu wazima ni bora tukaweka mambo yetu wazi ingawa wewe ni mtoto kwetu!”
“Kwa vipi mtumishi wa Mungu?”
Mchungaji Aaron hakujibu kitu chochote Ikabidi Patrick amgeukie mama yake na kumuuliza.
“Eti mama kuna nini mbona mnanistisha?” Alisema patrick akicheka hakutegemea kitu cha kumsikitisha.
“Muulize vizuri mchungaji atakueleza!”
“Mimi na mama yako tuna mpango mzito wa kuishi pamoja sababu sisi sote ni wapekwe!” Alisema mchungaji kabla hajaulizwa.
Badala ya kusikitika Patrick alinyanyuka kwa furaha na kunyanyua mikono yake juu akitamka neno “Haleluya!” Alimshukuru Mungu kwa habari aliyopewa na aliwaomba wote wapige magoti na kumshukuru Mungu kwa mpango wake.
Miezi mitatu baadaye harusi kubwa ya kufana ilifungwa kati ya mchungaji Aaron na Anne mama yao Patrick na Nancy na aliyefungisha ndoa hiyo hakuwa mwingine bali Patrick mwenyewe.
“Kweli tumepitia mabonde na milima!” Alisema Patrick jioni ya siku hiyo wakila chakula pamoja kwa furaha.
“Ni kweli mwanangu hatimaye machozi yamekauka usoni kwetu bwana ametupumzisha!”
“Jina la bwana lihimidiwe!” Nancy alisema.
“Milele na milele !” Aliitikia mchungaji Aaron.
MWISHO.
Nawashukuru sana kwa kuwa nami kuanzia mwanzo wa hadithi hii mpaka siku ya leo ambapo hadithi yetu imefikia mwisho. Nashukuru sana kwa ushauri ambao mmeweza kunipa, kama mwandishi ambaye ninatamani kuwa juu zaidi ya hapa nilipo, hakika nitafuata ushauri wenu ambao kwangu utakuwa ukiniongoza na kunipeleka juu zaidi na kunifanya kuwa bora.
Mwisho wa simulizi hii ambayo imekuwa ikikuburudisha, kukufundisha ndiyo mwanzo wa hadithi yangu nyingine, kuwa nami na nina uhakika utaendelea kuburudika na kujifunza mengi. 

Post a Comment

Previous Post Next Post