TROPEA - Mji wa wafu. SEHEMU YA 09



ILIPOISHIA....... 

"Inamaana kuwa huu ulikuwa mtego?.." Alijiuliza kijana Bingo ndani ya akili yake. "Laah! Hapana sasa inatakiwa kubadilisha maamuzi... Lazima nirudi duniani.." Aliongeza kujisemea hivyo Bingo wakati huo huo akiingiza mkono mfukoni kuchukua ramani yake ili ajihakikishie safari yake ya kurudi duniani. Lakini ajabu alipoitoa ramani hiyo aliona hakuna mahali palipochorwa zaidi ya karatasi kuonekana tupu.

ENDELEA NAYO......... 

Bingo alishangaa sana baada kuona mchoro wa ramani umetoweka kimiujiza, akawaza ni vipi atafanikiwa kuondoka hapo Tropea kwenye mji huo wa wafu pasipokuwa na ramani yake. Lakini wakati anatafakari suala hilo ghafla aliwekwa chini ya ulinzi akafungwa minyororo miguu mwake kisha akapelekwa kwenye chumba mahususi chumba ambacho muda wote kilikuwa kimya huku kikinukia marashi ya udi na ubani. Bingo aliwekwa humo. Punde Roya akatokea humo ndani, akaangua kicheko kisha akasema. 
"Bingo maisha ya huku raha sana, nakushangaa unang'ang'ana kurudi duniani, wakati duniani ni sehemu iliyojaza shida za kila aina. Huku Tropea hakuna kuumwa wala hatuna shida ya utajiri sababu kila kitu kipo. Na endapo kama utakubali kuishi huku basi mali zote za Tropea zitakuwa chini yako... "

"Roya, kwanza siamini kama ni wewe ambaye umeniingiza mkenge, haya hayakuwa makubaliano yetu. Sasa iweje niishi huku?" 
Alijibu Bingo huku akiwa amemkazia sura mwanadada huyo aitwae Roya. 

"Ahahah ah hahaha ha " Roya alicheka kisha akaongeza kusema. 
"Pole sana ila huu ndio ulikuwa mpango wetu, uwezo wa wewe kuja huku bila kupata misukosuko ungewezekana ila tuliamua upite njia ya misukosuko ili kupima uwezo wako na ndio maana tulikupa ramani ili ikupitishe huko tulipopataka sisi. Kweli hatimaye ukavuka vigingi, kwa maana hiyo wewe ni kidume na unafaa kuongoza jeshi la Tropea ambalo lipo katika kampeni kubwa ya kuimalisha ngome yake"

"Sipo tayari.. Nasema sipo tayari ni bora mniue kuliko kuendelea kuishi huku" Alifoka Bingo, muda huo mlango wa chumba hicho ulifunguka, akaingia mzee wa makamo ambaye ulionekana kutisha kwa muonekano wake. Mzee huyo alikuwa na vichwa viwili. Kichwa kimoja cha kawaida na kingine kilikuwa upande wa bega la kulia. Macho yalishabiana vyema na macho ya nyoka hali ya kuwa upande mmoja wa mwili wake ilionekana mifupa ya mbavu iking'aa mithili ya dhahabu. Mzee huyo alikuwa ameketi kwenye kiti maalumu chenye magurudumu. 
"Bingo mwanangu" Mzee huyo aliongea. Sauti yake ilikuwa nzito sana, sauti ambayo ilimfanya Bingo kushtuka ingawa alitulia na kisha kumsikiliza ili ajue kipi kitajiri hapo. 

"Safi sana kwa kutii agizo la baba yako, nadhani tayari vita hii imekuwa rahisi kwangu kwa sababu taarifa zako nimezipata zamani sana tangu siku ile uianze safari ya Tropea.. Bingo wewe ndio mwanangu ninaye kukubali na ndio maana nimepanga kukukabidhi Tropea ili uiongoze.. "

"Sipo tayari.. " Alijibu Bingo. Jibu hilo lilimshangaza Sultan Abatish, ndipo akamuuliza. 
"Unamaana gani?" Bingo hajajibu, ambapo hapo ndipo Sultan Abatish alipoamua kupotea lakini licha ya kutoweka, ilisikika sauti yake ikisema. 
"Hapa ndio Tropea, kuingia ni rahisi ila kutoka ni vigumu.. Bingo wewe ndio mrithi wa mji huu, ondoa fikra za kurudi duniani. Haha hahaha hahaha" ilimaliza kwa kicheko sauti hiyo.   

Hali hiyo ilimfanya Bingo kuwa na hofu dhofu lihali, mawazo chungu nzima yalitawala kichwa chake. Akiangalia ramani imetoweka, lakini pia maneno aliyoambiwa kuwa kuingia Tropea rahisi kuliko kutoka, nayo vile vile yalimtisha sana kwa sababu alipata tabu wakati wa kuja, tabu ambayo haikuwa rahisi kuivuka. 
"Inamaana kwamba kurudi ndio kuna shida zaidi ya zile nilizopata?.." Alijiuliza Bingo. Ila wakati suala hilo likiendelea kupasua kichwa, upande wa pili. Ngome ya Sultan Abatish inapokea taarifa kutoka kwenye ngome ya Sultan Starlon. Taarifa hiyo ilieleza kuwa unahitajika mpambano wa wafuasi kwa wafuasi. 

"Hili suala kwa upande wetu ni gumu sana, hatuwezi kulikubali kwa sababu bado Bingo hajakaa kwenye mstari ulio nyooka, hivyo mara moja taarifa hii ipuuzwe.." Aliongea kiongozi msaidizi wa ngome ya Abdy iliyopo chini ya Sultan Abatish.

Hivyo kibaraka mmoja akaagizwa kupeleka jibu, alichukuwa farasi wake kisha safari ya kuelekea kwenye ngome ya Sultan Starlon ikaanza. Ngome hiyo ilijaza watu katili sana, kwani kibaraka huyo kutoka ngome ya Abatish hakuweza kurudi aliuliwa huko huko na kisha kugeuzwa kitoweo. Walikula na kufurahi,.. Kiongozi wao alisikika akisema. 
"Ndio maana ngome ile naitamani sana, tazama chakula cha huyu mtu kilivyokuwa kitamu..." 

"Ahahaha hahaha ah.." Wote walicheka kisha shughuli ya kuendelea kupata chakula ikaendelea. 

Upande wa pili, kiongozi msaidizi ndani ya ngome iliyopo chini ya Sultan Abatish, ghafla akaingiwa na hofu juu ya kibaraka wake aliyemuagiza kwa Starlon. Na hivyo hakutaka kuzihukumu mapema hisia zake, ndipo alipoamua kuchukuwa jukumu la kumfuatilia yeye mwenyewe katika ngome ile. Alipofika alikuta lango lipo wazi,,aliingia bila wasi wasi wowote. 
"Ni kipi ulicho sahau, au na wewe unataka kugeuzwa chakula siku hii ya leo?.." Mmoja ya wafuasi waliopo ndani ya hiyo ngome alisikika akisema hivyo. Jamaa huyo, kiongozi msaidizi wa ngome ya Sultan Abatish ambaye aliitwa Yuli alicheka kisha akajibu. 
"Hiyo itakuwa ni hadithi. Kwahiyo wataka kuniambia kuwa mtu wangu kageuzwa kitoweo?.." 

"Ahahaha hahahah" Mfuasi huyo alicheka sana halafu akamwambia. 
"Hilo ndilo jibu.. Kajipange upya, na tena kawambie wenzako, wakati wowote wategemee gharika kubwa.." 

"Karibuni sana.." Yuli alijibu kisha akampindua farasi wake, safari ya kurudi kwenye ngome yao ikaanzia hapo. 

Alipofika alionekana ni mtu mwenye hasira mno, hivyo ikabidi akaongee na Sultan Abatish kwa dhumuni la kumwambia kile kilichojiri mara baada kukataliwa takwa waliloleta maadui zao. Habari ya kuuwawa mfuasi wake kiukweli ilimuumiza sana Abatish, na hapo akaita askari wake baadhi, askari ambao waliongozwa na mwanadada Roya. 

"Roya.. Tayari bwana Starlon ameanza kuchochea moto. Hivyo basi nawapa kazi moja, fanyeni juu chini Bingo akubali matakwa yangu, iwe kwa kipigo aidha kwa vyovyote vile ilimradi asalie Tropea. Baada ya hapo sasa mapambano yaanze" 

"Sultan Abatish, unadhani bila huyo Bingo vita hii hatuiwezi?.." Aliuliza Yuli kiongozi msaidizi katika ngome hiyo.. Abatish hakumjibu swali hilo zaidi alipotea maeneo hayo..ilihali muda huo huo Roya na jeshi lake walielekea kwenye kile chumba alichohifadhiwa Bingo, ajabu walipoingia hawakumkuta.. Roya na wenzake walishtuka, hima wakatoka ndani ya chumba hicho, moja kwa moja walielekea mahali ilipo kengele ya kutoa taarifa..

Punde kengele hiyo yenye sauti kali yenye uzito wake ililia kisha Roya akasema "Bingo katoweka, haraka sana lango la Tropea lifungwe na kila askari afanye jitihada za kumtafuta.. Asirudi duniani..". Aliongea hivyo Roya kwa sauti ya juu.. 

Hapo sasa ndipo Tropea ilipochafuka, makaburi yalipasuka wafu wakazidi kutokea, viumbe wa ajabu nao walionekana katika mji huo.

Sultan Abatish ilipomfikia habari hiyo ya kwamba Bingo haonekani, alitaharuki sana. Haraka akamuita Yuli ili aweze kusaidia harakati hiyo ya kumsaka Bingo popote pale alipo huku akiamini kuwa kijana huyo bado hajaondoka Tropea.
"Yuli.. Nahitaji Bingo aonekane, ukishamleta mbele yangu nitakupa asilimia stini ya uongozi wako" Alisema Sultan Abatish.

Yuli alicheka kwanza halafu akajibu "Sidhani kama bado unamawazo mgando ya kuendelea kunidanganya. Miaka mingapi imepita na ahadi zako zisizo tekekelezwa? Baba mimi ni mwanao lakini namna tunavyoishi ni kama vile mimi ni kibaraka wako. Leo hii mtoto wa juzi Bingo unamlazimisha kumpatia madaraka ambayo yeye hana mpango nayo. Sasa basi nasema hivi sipo tayari kumtafuta Bingo.." Yuli alipokwisha kusema hayo alipotea.

Yuli naye ni mmoja wa familia ya Sultan Abatish, kijana huyo hakufurahishwa na namna baba yake anavyomwamini Bingo kuliko yeye. Kwa maana hiyo alilazimika kukaidi matakwa ya baba yake ilihali pole pole ndani ya moyo wake akiwa na nadhiri dhidi ya mji huo wa Tropea. Jambo la kwanza alimuita Roya, ambapo Roya nae alitii wito. Ni ndani ya chumba maalumu, chumba ambacho wawili hao waliweza kuteta. 

"Ndio Yuli umeniita, nami nimetii wito?.." Aliongea Roya. 

"Roya, nahitaji msaada wako kama upo tayari kunisaidia" 

"Masaada gani huo Yuli? Na je, hujui kuwa muda huu tupo katika harakati za kumtafuta Bingo?.." 

"Ahahah ah hahahah.." Yuli aliangua kicheko, Roya alimshangaa sana ilihali muda huo huo Yuli akaongeza kusema. 
"Achana na suala hilo la Bingo, hebu fanya kama unalisahau kwa muda..." 

"Haya zungumza.." 

"Vizuri sana kwa kunipa nafasi... Roya kuna siri nzito sana imejificha ambayo wewe usingeweza kuijua pasipo mimi kukwambia. Bingo na Abatish wana agenda nzito sana juu ya mjini huu wa Tropea, na ndio maana Sultan anamuhitaji Bingo kwa udi na uvumba ili amrithishe mji huu. Amini kwamba Roya, Bingo sio mfu kama tulivyo sisi. Bingo anauwezo wa kurudi duniani akaishi maisha mengine tofauti na sisi lakini pia mbali na hilo, Starlon anaitamani hii ngome, hivyo sioni sababu ya mtu kama Bingo ambaye sio jamii yetu atuongoze sisi. Ngome hii itapotea zaidi na zaidi." 
Alisema Yuli huku akiwa amempa mgongo Roya. 

" Kwahiyo?.. " Alihoji Roya kwa taharuki ya hali ya juu. Hapo Yuli alimgeukia kisha akamwambia. 
"Mapinduzi yanahitajika, uamuzi nitakao chukua ni mgumu sana kwa kuwa nimeona kuna ubaguzi unaoendelea kimya kimya.. "

"Yuli uamuzi gani huo?.. "

"Abatish nitamuua kwa mikono yangu kisha siku kadhaa mbele nitajitangaza kuwa mliki wa Tropea, na vile vile nitaanda jeshi nguvu kazi la kupambana na jeshi la Sultan Starlon.. Ahahah hahahah.. " Yuli alijibu hivyo huku akimaliza kwa kicheko.

Maneno ya Yuli yalimshtua sana Roya, ghafla akajikuta akiingiwa na hofu juu ya Yuli, uamuzi huo ulimtisha sana. Lakini wakati Roya akiwa na hofu, Yuli aliongeza kusema" Bingo yupo katika mikono yangu.. Kwahiyo mpango huu nilioanzisha utaenda sawa kabisa."
Hapo Roya alishusha pumzi baada kusikia Bingo bado yupo ndani ya mji huo wa Tropea.. 

"Wapi alipo Bingo?.. "Roya alimuuliza Yuli, lakini Yuli alikataa kumuonyesha akidai kuwa mpaka pale atakapo kamilisha mpango wake ndipo atakapo muelekeza mahali alipo. Vile vile Yuli alihitaji kujua kama Roya yupo tayari kuungana naye katika harakati hizo za kufanya mapinduzi. Jambo hilo kwa Roya lilikuwa gumu sana ila akahofia huwenda akawa rehani endapo kama atapingana na matakwa ya Yuli mtoto wa kwanza wa Sultan Abatish ingawa moyoni Roya alitamani sana Bingo ndio achukue nafasi hiyo. 
"Nipo tayari.." Alijibu Roya. Jibu ambalo lilimfurahisha mno Yuli na hapo ndipo ulipofanyika mpango wa kuwatuliza wafu pamoja na kuwarudisha jeshi ambalo tayari lilikuwa likihangaika kumtafuta Bingo.  

Wakati huo ghasia hiyo inatulizwa, upande wa pili kijana Bingo alikuwa ndani ya chumba kile ambacho mara ya kwanza alipata kulia chakula ambacho kilikuwa ni nyama ya mtoto mchanga. Bingo akiwa ndani ya chumba hicho, aliwaza atatoka vipi ndani ya Tropea ili arudi duniani kuvaa mwili wake kabla haujazikwa sababu endapo kama mwili wake utazikwa basi habari zake zitakuwa zimeishia hapo, hata afanyeje Tropea hatotoka tena lakini pia mbali na suala hilo la mbinu ya kuchoropoka Tropea, vile vile Bingo alijiuliza siku ngapi amemaliza Tropea. Kabla hajapata jibu ghafla alitokea mzee Ndelo. Mzee huyo akiwa ndani ya mavazi meupe alimsogelea Bingo kisha akasema. 
"Bingo unatambua kuwa muda mrefu upo Tropea? Hivi unajua kuwa mwili wako..... 

KIPI KILIJIRI HAPO? JE, MWILI UMEZIKWA? AMA NAMNA GANI VIPI? TUKUTANE SEHEMU IJAYO. 

Post a Comment

Previous Post Next Post