TROPEA - Mji wa wafu. SEHEMU YA 10



ILIPOISHIA....... 

Kabla hajapata jibu ghafla alitokea mzee Ndelo. Mzee huyo akiwa ndani ya mavazi meupe alimsogelea Bingo kisha akasema. 
"Bingo unatambua kuwa muda mrefu upo Tropea? Hivi unajua kuwa mwili wako... 

ENDELEA NAYO...... 

"Bingo unatambua kuwa muda mrefu upo Tropea? Hivi unajua kuwa mwili wako mpaka sasa unaleta utata kijijini na kushangaza watu?..". Bingo alistushwa na maneno hayo aliyoyaongea mzee Ndelo. Akiwa na hofu dhofu lihali kijana Bingo akamuuliza mzee huyo "Unamaana gani mzee?.." mzee Ndelo alishusha pumzi ndefu kwanza kisha akajibu "Jambo la kwanza utambue umemaliza miezi miwili sasa huku lakini pia..." Kabla Ndelo hajaendelea kuongea Bingo alimkatisha kwa kusema "Miezi miwili? Akha! Tafadhali mzee wangu usitake kuniambia kuwa tayari mwili wangu UMEZIKWA, katu sitofurahia maisha ya Tropea, nahitaji kurudi duniani ikiwezekana hata sasa tuondoke wote.."
"Bingo.." Aliita mzee Ndelo, punde akasema. 
"Ni ngumu sana mimi kuondoka na wewe? Lakini pia usiwe na hofu juu ya mwili wako kwa sababu tayari kuna imani nimewaingizia wanakijiji. Kijiji chote nimekitangazia kuwa wewe bado hujafa na si muda mrefu utarejea katika maisha ya kawaida. Hebu tazama ukutani.. "Alisema hivyo mzee Ndelo halafu akanyoosha kidole chake ukutani, ukatokea moto mwembamba kwenye kidole chake, moto wenye rangi ya blue. Punde pale ukutani palipogota moto huo ilionekana TV.. Tv ambayo ilionyesha namna mzee Ndelo alivyofanikiwa kuwatuliza wanakijiji ambao ambao tayari walitaka kumzika Bingo. Hapo ndipo Bingo alipotupa macho yake kwenye ukuta ili atazame namna ilivyokuwa. 

                     ******
"Katu hatuwezi kuamini suala hili, mtu alishakufa amekufa kamwe hawezi kurudi tena duniani. Hapa lazima Bingo azikwe" Sauti ya mmoja ya wanakijiji. Alisikika akiongea maneno hayo kwa sauti ya juu kabisa baada kuona mzee Ndelo katia mkazo juu ya suala la mwili wa Bingo kuzikwa. Wanakijiji baadhi walimuunga mkono mzee huyo ingawa wengine walikubaliana na mzee Ndelo kwani walijua dhahili shahili mzee huyo anajihusisha na mambo ya jadi. Ndelo akajitokeza akasema. 
"Ni nani anaweza kutuambia kuwa umauti wa Bingo umesababishwa na nini? Je, Bingo aliumwa? Aidha aliuliwa?. Nasema hivi Bingo karogwa na huwenda aliyemroga ni huyu huyu mzee anayeshinikiza kuwa azikwe, kwa sababu anaamini endapo kama leo hii Bingo atazikwa basi zoezi lake atakuwa amelikamilisha. Nasema hivi Bingo hatozikwa, na mchawi wa hiki kijiji nitamuumbua hadharani jua la utosi.. " Mzee Ndelo maneno hayo aliyasema kwa kujiamini kabisa, hapo sasa msibani ndipo minong'ono ilipoanza kusikika, kila mmoja alizungumza lake.

"We mzee Ndelo wewe?!..hivi kweli wewe wa kuniita mchawi mimi?.. " Yule mzee aliyekuwa akisisitiza Bingo azikwe alisema kwa hasira kali.   

Mzee Ndelo akajibu "Naam! Tena narudia kusema wewe ndio ni mchawi, na Bingo atapona halafu sasa nitakuumbua hadharani jua la utosi.. ". Hayo maneno ya mzee Ndelo yalizidi kumchukiza huyo mzee, ambapo ndipo alipoamua kumsogelea kwa dhumuni la kupigana lakini kabla wazee hao hawajafikia muafaka waliamuliwa, ogomvi huo ukawa umetoweka.      

Baada ya siku mbili kupita, bado Bingo alionekana ndani ya jeneza pasipo kurudi duniani kama alivyokuwa akieleza mzee Ndelo. Suala hilo liliwafanya wanakijiji kuingiwa na hofu mioyoni mwao, hivyo haraka sana mwenyekiti wa kijiji akamuita Ndelo ili alete majibu muafaka juu ya mwili wa marehemu. 

"Katika vitu ambavyo serikali yako haiamini ni ushirikina, mzee unataka kutuletea matatizo hapa kijijini. Hivyo basi nia na dhumuni ya kukuita hapa, nataka ule mwili ukazikwe la sivyo utakifanya kijiji hiki kuchafuliwa. Sasa iweje mtu mmoja utie doa kijiji chenye mamia ya watu?.." Alisema Mwenyekiti wa kijiji, maneno hayo aliyokuwa akiongea kwa msisitizo alikuwa akimwambia mzee Ndelo. Ndelo alicheka kwanza kisha akajibu. 
"Mwenyekiti, jambo hili wala lisikupe shida, mimi ndio najua ukweli wa yule kijana. Bingo bado hajafa, yupo hai kabisa ila huko aliko ndio nafanya mpango wa kuonana na watalamu wa masuala haya ya giza ili waweze kumtoa, hebu mzee mwenzangu fikiria kwanza, mama Bingo ataishi maisha gani pasipo mwanae? Nakuomba kuwa mtulivu". Ndelo na mwenyekiti walikubaliana hivyo, ila siku kadhaa mbele wanakijiji waliona Ndelo hana ubinadamu, na hapo ndipo walipoamua kuandamana mpaka nyumbani kwa mwenyekiti kuomba kibali cha kufanya jambo lolote juu ya mzee Ndelo. 

" Mwenyekiti... Mwenyekiti, sisi wanakijiji ndio tuliokuweka hapa na vile vile sisi ndio tutakao kuondoa.." mwanakijiji mmoja alisema kwa hasira huku akiwa na shoka begani. Mwenyekiti aliogopa ujio huo wa silaha, akiwa na hofu akasema. "Jamani mbona hivyo sasa? Mnakuja namna hiyo sio vizuri ndugu zangu!.. Haya niambieni kosa langu nini?.." 

"Usibane sauti kama mama mjamzito aliyeshikwa na uchungu wa mimba, sisi tunachotaka utupe kibali chako tukamfanye chochote mzee Ndelo, haiwezekani maiti imalize wiki ikiwa bado haijazikwa kwa Mila na tamaduni zetu hiyo sio haki ya marehemu.."

"Ndugu zangu si nyinyi mlikuwa mnamuunga mkono Ndelo au?.." Aliuliza Mwenyekiti. 

"Kaaa kimya. Mpumbavu wewe, tunachotaka sisi ni kibali chako tu na sio maneno yako ya kubwabwaja" 

"Sawa nendeni nimewaruhusu" Alijibu mwenyekiti. Fujo ilizuka mahala hapo, wanakijiji hao walishangiria sana. Muda huo ilikuwa yapata saa kumi na moja ya jioni, hivyo kikao cha muda mfupi kwa vijana nguvu kazi kilikaa na kuanza kujadili namna gani ya kupora jeneza na kisha kumuadabisha mzee Ndelo ikiwezekana kumuua kabisa. 

"Hakuna mtu asiyemjua huyu mzee, ukweli mzee ni moto wa kuotea mbali. Ukienda kichwa kichwa anakupoteza" 

"Enhee kwahiyo tufanyeje sasa jamani? Na wakati huo mkumbuke anashinda pale kulilinda jeneza na analala pale pale.." 

"Sikilizeni vijana, kwa kuwa suala hili tumeamua kulivalia njuga basi hakuna haja ya kuhofia wala kuogopa. Twendeni Twendeni tukamnyooshe kisha Bingo azikwe" Wanakijiji hao, vijana shupavu walipokubalina hivyo waligongeana mikono kisha wakaondoka mahali hapo kusubiri giza litakapo ingia ndipo wakatimize azma yao lakini walipotoka tu hapo mzee Ndelo akatokea, alicheka sana halafu akajisemea. 
"Pumbavu sana nyinyi, mlipolalia ndipo nilipoamkia, kajipangeni". 
      
                     *********
Tv hiyo ikawa imepotea, Bingo Alistaajabu sana mambo hayo aliyoyashuhudia. Punde mzee Ndelo akasema. 
"Baada vijana hao kuamua mambo hayo, kuna dawa niliupaka mwili wako, dawa ambayo ni kiini macho ya kuwafanya watu kuamini kuwa muda wowote utafumbua macho kwa sababu ulikuwa ukihema ingawa dhahili shahili haukuwa unahema. Hivyo ilibidi nizidi kutangaza kuwa bado hujafa na muda wowote utaziduka ila sasa kijana wangu Bingo. Hii dawa inamadhara tena makubwa sana endapo kama utachelewa kuuvaa mwili wako.. Fanya ujuavyo, ndani ya siku tano uwe tayari umeuvaa mwili wako la sivyo habari yako itakuwa imekomea hapo" Mzee Ndelo alipokwisha kusema hayo alipotea. 
Akabaki Bingo akiwa na wingi wa taharuki, na ndani ya kichwa chake akajiuliza. 
"Siku tano? Mmh yani muda mchache tu niliokaa huku naambiwa nimekaa miezi miwili, je siku tano itakuaje sasa?

Jambo hilo lilimtia hofu Bingo, suala la kurudi duniani lilimfanya aumize kichwa akiwaza namna gani ataondoka ndani ya mji huo uishio wafu lakini wakati yupo katika tafakari hiyo, mara ghafla ndani ya chumba hicho alitokea Yuli. Bonge la mtu. Jibaba lenye miraba minne. 
"Habari yako Bingo, awali uongozi wa Tropea ulipanga kukukabidhi mji huu, kitendo ambacho kipo kinyume sana na ingekuwa ubaguzi mkubwa sana kwa sababu mie ndio ninayefaa kumiliki hii ngome na wafu waliomo. Lakini pia nisingetaka kukuacha hivi hivi kijana, kwa sababu wewe ni jamii ya Abby hivyo nitakupa wadhifa fulani hapa hapa ili uendelee kufurahi maisha ya huku " Alisema Yuli. Maneno hayo alikuwa akimwambia Bingo.

"Kwahiyo unataka kusema kwamba Tropea inaweza kutawaliwa na watu wawili?"

" Mmh! Unamaana gani? Mimi ndio kiongozi kwa sasa. Namanisha kuwa Abatish nimeshampoteza na kuanzia sasa mimi ndio Sultan mkuu, hivyo basi uwezo wako wa kupambana umenifanya nikupe wadhifa katika mji huu ila endapo kama hutakubaliana na hitaji langu basi utakosa vyote, duniani hutorudi na vile vile Tropea hutoishi " Yuli alisisitiza. 

Hapo Bingo akaingiwa na hofu zaidi lakini baadae akaona hamna njia nyingine bali ni kukubali cheo hicho ingawa moyoni akiwa na nadhiri ya kufanya mapinduzi. 

" Yuli.. Nipo tayari kwa hilo." 
Alikubali Bingo. 
Yuli alicheka sana, ndipo akapeana mkono na kijana Bingo wote wakawa kitu kimoja. 

Nje, kengele kubwa ya mji wa Tropea iligongwa kisha mtangazaji akawataka wafu wote ndani ya mji huo watulie.
"Wafuasi wote katika mji huu wa Tropea, kuna taarifa ya mpya ambayo imejitokeza. Nayo ni kuhusu mapinduzi. Tropea kuanzia sasa itakuwa chini ya Yuli kwa sababu aliyekuwa kiongozi hapo awali Sultan Abatish kaachia ngazi. Hivyo basi hatutegemei kuona mfu akienda kinyume na sheria na taratibu ya Tropea, maisha yataendelea kama kawaida lakini mbali na hayo, jeshi mnatakiwa sinagogi ili mpewe utaratibu mpya jinsi ya kulinda mipaka ya mji wetu ". Mtoa taarifa aliongea maneno hayo, taharuki ikazuka Tropea kila mmoja akishangazwa na maamuzi hayo lakini wakati taarifa hiyo ikienea Tropea, hatimaye taarifa hiyo ikafika kwenye ngome ya Sultan Starlon. Ajabu shangwe zilizuka, kiongozi mkuu akaita jeshi lake ndani ya sinagogi na kisha akaanza kuzungumza nao jambo ingawa habari kuu ambayo iliwafurahisha ni juu ya kijana Yuli kuuchukua mji wa wafu.

"Nafikiri kila kitu kinaenda sawa, Abenego, Joyka, Bluyner. Nyie ni watu wangu wa nguvu. Huu ndio wakati wa kukamilisha azma yetu ili Tropea iwe chini yetu. Anzeni kuwanoa vijana kujiandaa kwa ajili ya mapambano.." Alisema mkuu huyo aitwae Rauu. 

"Hilo shaka andoa, tutapigana mpaka tone la mwisho, mji ule kwa vyovyote vile lazima uwe chini ya Sultan Starlon.." Aliongea Joyka. Jitu ambalo lilionekana la ajabu sana. 

"Safi sana. Je, Joyka unaniahidi nini?.." Rauu alihoji huku akimtazama Joyka. Joyka akacheka kidogo kisha akajibu. 
"Hapa ni kipigo tu hakuna namna" 

"Ahahah aah hahahah" Wote kwa pamoja waliangua kicheko wakati huo wakigongeana mikono. 

Kwengineko mambo sio mambo, Tropea Bingo anapata kukutana na Roya faragha, hapo ndipo Bingo alipomueleza Roya juu ya uamuzi wa kijana Yuli aliochukuwa. Ukweli Roya hakufurahishwa na kitendo cha Yuli kwani alijua Yuli ni kiumbe mwenye roho mbaya sana, hivyo sio ajabu akaanza kuuharibu mji huo.

"Roya! Hivi kwanini Yuli ameamua kuchukuwa uamuzi wa kumuondoa Abatish?.." Bingo alimuuliza Roya, muda huo walikuwa wawili katika moja ya chumba ndani ya sinagogi. 
"Je, upo tayari na sisi tupindue meza?.." Aliongeza kuhoji Bingo ikiwa Roya bado akionekana kutafakari kitu ndani ya moyo wake hali iliyopelekea kukaa kimya. Lakini punde baada kusikia swali hilo la pili alilouliza Bingo.. Aligeuka kisha akasema. 
"Bingo katika hili nipo tayari, Yuli hafai hata kidogo ila naomba uniahidi utakuwa tayari kushika nafasi ya mzee wako?.." 

"Ndio Roya ila kuna kitu nataka kufahamu kidogo maana kinanishangaza sana!.." 

"Aah Bingo kitu gani hicho?.." Alihoji Roya huku akiwa na wingi wa tabasamu baada kusikia Bingo kukubali kusalia Tropea. 

Bingo akasema "Hivi masaa ya huku na duniani yapo sawa kweli?.." 

"Hahahah hahahah.. Bingo Bingo tofauti kabisa. Masaa ya huku yanaenda kasi sana mbali na duniani.." Alijibu Roya. 

"Mmh! Kwahiyo siku tano duniani ni sawa na siku ngapi huku?.." 

"masaa sita tu.." Alisema Roya. 

Bingo alishtuka sana. Mshtuko ambao ulimfanya Roya kumuhoji. 
"Mbona unashtuka?.." Bingo kabla hajamjibu Roya, ghafla fujo zilisikika nje, mayowe ya hapa na pale yalitamalaki. Haraka sana Roya alikwenda dirishani kuchungulia ili ajue kinajiri nini? Alistaajabu sana kuona umati wa wanajeshi kutoka ngome ya Starlon ikiwa imevamia. 

NAAM SIKU 5 NI SAWA NA MASAA SITA NA HUKU JESHI LA STARLON LIMEVAMIA. TUKUTANE KESHO SEHEMU YA MWISHO ILI TUJUE BINGO ALITOKAJE TOKAJE NDANI YA TROPEA. 

Post a Comment

Previous Post Next Post