TROPEA - Mji wa wafu. SEHEMU YA 11 (Final)

ILIPOISHIA....... 

Haraka sana Roya alikwenda dirishani kuchungulia ili ajue kinajiri nini? Alistaajabu sana kuona umati wa wanajeshi kutoka ngome ya Starlon ikiwa imevamia.

ENDELEA NAYO......... 

"Bingo kaa tayari kazi imeanza.." Aliongea Roya akimuasa Bingo, na hivyo kijana huyo hakutaka kupoteza muda, hima alivaa vyema koti lake, upanga begani tayari kwa niaba ya kulikabili jeshi hilo ambalo lilijaza watu wa ajabu ajabu. Wapo waliokuwemo wenye macho makubwa na masikio marefu, lakini pia wapo waliokuwemo wenye jicho moja huku ngozi zao zikiwa zimeshabiana na ngozi za nyoka. Ndimi za watu hao ni hatari sana kwa maisha.

"Bingo yakupasa kuwa makini" Roya aliongeza kumwambia Bingo hali yakuwa jeshi la Tropea ambalo kwa muda huo lilikuwa chini ya Yuli lilikuwa limeshalivaa jeshi la Starlon linalo ongozwa na Rauu. Patashika nguo kuchanika Tropea mji wa wafu,.. Hakika wafu walivyekwa vyekwa, jeshi la Yuli liliteketea.

Baadae kidogo Bingo alitua chini kutoka juu kwenye majengo mrefu.. Vumbi ilitimka wakati huo koti lake likipepea nyuma. 

"Wewe ni nani?.." Rauu Aliuliza. 

"Bila shaka salamu zangu mmeshazipata. Mimi ndio Bingo mwana wa Abatish. Nimekuja Tropea kuharibu mipango yenu ya kuuteka mji huu, huu mji utabaki chini ya Batish miaka yote.." Alijibu Bingo. 

"Ahahaha ha hahahah.." Rauu alicheka sana kisha akamwambia Bingo. 
"Ni vigumu nafsi kushindana na mfu..." kwisha kusema hivyo, akaruhusu jeshi limshambulie Bingo. Bingo kwa nguvu zote akajinyanyua juu, punde akashuka.. Kitendo hicho kiliweza kutimua vumbi nyingine kwa mara nyingine tena, katikati ya vumbi hiyo Bingo akaanza kuwashambulia. Muda mchache jeshi lote la Rauu liliteketea, hapo Rauu akajikuta akibaki peke yake.. Alishangaa sana asiamini kama kweli Bingo anauwezo namna hiyo. Ila baadae akaona sio vizuri kama hatodhihirisha ubora wake mbele ya Bingo hatakama anaonekana ni mtu mwenye uwezo mkubwa. Hivyo basi Rauu alinyoosha mkono juu, ukatokea upanga kwenye mkono wake, wakati huo huo kwa mbali kabisa kwenye jengo ndefu ilisikika sauti ikimtaja Bingo. Bingo akainua macho yake kutazama kule ilipotokea sauti hiyo akapata kuona mtoto mdogo mwenye umri usiozidi miaka mitano. Mtoto huyo akamtupia Bingo upanga kisha akapotea. 

Hapo sasa wawili hao kila mmoja akawa na silaha mkononi mwake. Shangwe zilizuka za kumshangiria Bingo. 
"Bingooo.. Bingoooo.. Bingoooo Bingooo". Muda huo huo pambano likaendelea. Na wakati mpambano huo unaendelea, upande wa pili Roya alionekana ndani ya chumba alichokuwa akitumia Batish. Roya alikuwa na haraka sana kutafuta kitu kwani alifungua kila sanduku. Alifungua hili akaliacha, akafungua lile akaliacha lakini mwishowe kitu alichokuwa anakitafuta alikipata, nacho sio kingine bali ni ramani ya kurudi Duniani. Hima aliihifadhi kwenye mfuko wa koti lake kisha akaendelea kusaka kitu kingine. Safari hiyo alitafuta pete ya miujiza na ufunguo wa Tropea. Navyo alivipata, na hivyo aliondoka ndani ya chumba hicho, lakini sasa kabla hajatoka, Yuli aliingia chumbani humo. Alicheka sana kisha akasema. 
"Roya, hatimaye unanisaliti. Si ndio? Hahahah. Hahahah. Nasema hivi umechelewa, kwa usalama wako nipe kila kitu ulicho chukuwa humu ndani.." Alifoka Yuli. 

Roya kamuuliza "Kitu gani?.."
 
"Hujui? Sasa ngoja nikunyooshe" Alijibu Yuli na mara moja akaanza kumshambulia Roya kwa mateke na ngumi, ila Roya alionekana kuwa makini sana kukwepa wakati huo akijaribu kumkimbia Yuli ambaye nae alionyesha umahiri wa kumdhibiti. 

Nje mambo bado yalikuwa sio mambo baina ya Bingo na Rauu.. Hao mabwana walionyeshana umwamba mbele ya umati wa wafu ingawa Bingo aliweza kutawala vyema pambano. Na wakati mpambano huo ukiendelea kupamba moto, ghafla Roya aliingilia kati huku nyuma akifuatwa na Yuli lakini kabla Yuli hajamfikia, Michael aliingilia kati, muda huo sasa wafu walimvamia Rauu na kisha kumshambulia. Bingo akamaliza mchezo kwa urahisi kabisa.. Roya alimkumbatia Bingo, akamkabidhi funguo na Pete pia ramani kisha akamwambia. 
"Bingo naimani ipo siku tutakutana kwa mara nyingine tena ila kwa sasa kimbia. Tropea haifai tena.. Funguo hii hakikisha uki..." Kabla Roya hajamaliza kusema alichotoka kuongea, alichomwa upanga na mtu wa kuitwa Yuli. Muda huo huo Michael tayari alionekana akiwa chini mwili wake ukiwaka moto. 

"Bingo kimbia.. Kimbia niache mimi. " Roya alipaza sauti akisema hivyo baada kuona Bingo amemng'ang'ania. Muda mchache makaburi yalipasuka, mikono ya wafu ilionekana na punde tu wafu waliandamana kumfuata Bingo." Bado nusu saa Bingo.. Na mwili wako tayari upo katika maandalizi ya mwisho ili uzikwe.." Sauti hiyo ilikuwa ya mzee Ndelo, sauti hiyo Bingo aliisikia kwa mbali sana huku akitimua mbio ilihali jopo la wafu likimfuata nyuma. Bingo alikimbia sana, alibahatika kulipita lango lakini baada ya lango hilo la Tropea lilionekana giza hakuna pa kwenda njia imefikia kikomo. Pumzi ndefu alishusha kijana Bingo, akitazama nyuma aliona kundi kubwa la wafu likimfuata nyuma huku likiongozwa na Yuli, hofu ikazidi kumjaa hasa baada kuona njia imefika mwisho ilihali ananusu saa tu ya kuendelea kusalia Tropea kwani mwili wake upo katika maandalizi ya mwisho ili uzikwe.

"Niende wapi?.." Bingo alijiuliza baada kuona njia imefika ukingoni hali ya kuwa huku nyuma kundi la wafu likiongozwa na Yuli likizidi kumfuata. Akili ya ghafla ikamjia Bingo, akili hiyo ikamtuma kuwa afunge lango hilo la Tropea kabla wafu hao hawajamkaribia.

Uamuzi huo Bingo aliuona unafaa sana, bila kupoteza muda aliusogelea mlango huo kisha akaufunga na kufuli halafu akajitosa kwenye lile giza lililokuwa mbele yake. Mayowe yalisikika.. Bingo akilalama huku akizidi kutokomea kwenye giza lile nene lakini muda mchache baadae alipoteza fahamu, ila punde fahamu zilimrudi na hapo ndipo alipokohoa ndani ya jeneza kisha akajinyanyua akaketi huku akiwatazama watu waliokuwa kando ya jeneza.  

Taharuki inazuka, watu waliokuwepo hapo walikimbia baada kuona Bingo kafufuka, na wale wenye roho ngumu waliishia kustaajabu tu ilihali mboni za macho yao hata zisiamini kama kweli marehemu kafufuka.

"Bingo habari yako.." Alisikika akisema mmoja ya wanakijiji. Mwanakijiji huyo alimsalimu Bingo ambaye muda huo alionekana kutofahamu kinacho endelea, hali iliyomfanya asimjibu mtu huyo.
 
"Tulieni kwanza fahamu zimrejee vizuri" Alisema mzee Ndelo wakati huo huo akamsogelea Bingo, akachuchumaa kisha akamwambia. 
"Hongera sana kwa kurejea duniani muda muafaka, hakika wewe ni shupavu kwa sababu ilikuwa imebaki dakika moja tu kati ya zile dakika thalathini (nusu saa) nilizokwambia.." Ndelo alipokwisha kusema hivyo aliinuka akachukua kibuyu chake chenye dawa za asili, akamnyunyizia Bingo mulemule ndani ya jeneza. Muda wa dakika sita Bingo alirejea katika kumbukumbu zake sasa, na hivyo mzee Ndelo akaruhusu kila mwanakijiji kumsalimia kijana huyo pasipo kumuogopa wakati huo huo baadhi ya vijana walionekana wakilifukia kaburi kwani aliyetajiwa kuzikwa kafufuka.
  
"Pole sana Bingo.." 

"Pole sana kijana mwenzetu kwa mtihani.." 

"Pole sana Bingo wangu kwa jambo hili jamani" 

"Bingo, pole Sana kwa kweli".

Hizo zilikuwa pole za baadhi ya wanakijiji waliokuwa wakimpa pole Bingo. Walikuwa vijana kwa wazee, wamama kwa wababa. Wote kwa pamoja walimsabahi Bingo ingawa hawakujua kama kijana huyo alielekea Tropea mji uishio wafu. 

Mambo ndivyo yalivyokuwa, ila ghafla furaha ya Bingo ilizidi mara mbili ya hapo awali baada kumona mama yake kipenzi akiwa na wingi wa afya. Mama Bingo alijikuta akidondosha machozi kwa furaha. Alisema "Bingo mwanangu, awali ya yote naomba unisamehe mwanangu, najua umeteseka kwa sana kwa sababu yangu, umeishi maisha ya tabu kwa sababu yangu lakini nilifanya hivyo nikiamini kwamba nitaimarisha ndoa yangu, ingawa mawazo yangu hayakwenda kama nilivyo tarajia. Maradhi yaliyokuwa yameniandama kwa kipindi kirefu yalimfanya baba yako kunitelekeza akaoa mwanamke mwingine na hata pia akaamua kuhama kijiji pasipo kunijali hata kwa salamu.." 

Maneno hayo mama Bingo aliyaongea kwa uchungu mkubwa huku machozi yakimtiririka. Bingo alishusha pumzi ndefu kisha akasema. 
"Hilo ondoa shaka mama, kila kitu nakifahamu, kwanza nafurahi kukuta ni mzima kabisa hayo mengine tufanye yamepita.. "

                       *********
Kijiji kuzima kinapata kujua kuwa Bingo kafufuka, jambo hili linampa heshima mzee Ndelo kwa kufanikisha kumrudisha kijana Bingo. 
Jioni moja Bingo alikutana na mzee Ndelo, wawili hao waliweza kuteta mambo mengi sana, lakini katika mazungumzo yao walizama sana kuhusu safari ya ajabu ambayo ilimtokea Bingo. 
"Ndio bwana pole na hongera pia kwa safari ndefu" Alisema mzee Ndelo huku akiwa na wingi wa tabasamu. 

"Daah! Asante sana lakini mzee safari ilikuwa ngumu mno ingawa namshukuru Mungu nimerejea salama. Na moja ya vitu nilivyorudi navyo ni funguo wa huko pia na pete, vile vile nimerudi na ramani. Vitu hivi vyote alinipatia Roya.." 

"Loh! Bingo? Kweli wewe ni noma. Pete hii sio ya kawaida kijana, na hii ndio Pete ambayo ilikuwa ikitafutwa na watu wengi sana ingawa wengi walioifuata walipotelea huko huko." 

"Kwahiyo mzee naweza kusema sisi umasikini basi tena?.." 

"Ndio maana yake!.." Alijibu mzee Ndelo. Wote kwa pamoja walifurahi sana. 

Usiku wa siku hiyo hiyo Bingo akiwa usingizini, kwa njia ya ndoto alikuja Roya. Roya akamuomba Bingo atupe ufungo huo aliotoka nao Tropea kisha akamwambia. 
"Bingo tayari upo duniani, hivyo huna budi kuichana ramani hiyo lakini pia pete niliyokupatia unaweza kuomba kitu chochote na ikakupatia. Tropea imefunikwa na majivu ya moto, mji umeyeyuka. Ila mbali na hiyo Bingo, bado kuna laana inakuja nyuma yako, nayo itakufanya uishi kwa shida sana hapa duniani" Roya aliongea.
 
"Laana? Laana ipi tena Roya? Kwanini iwe hivyo?.." Bingo aliuliza huku akiwa na wasiwasi. 

Roya alikaa kimya kidogo halafu akasema.
"Hilo lisikutishe, mimi sio binadamu ingawa nilitamani kuishi na wewe ikiwezekana tujenge familia kwa sababu nakupenda sana lakini kwa kuwa hili limeshindikana basi nitakusaidia kwa lingine ikiwa kama upendo wangu kwako..." Bingo alitaharuki moyoni mwake. Hapo akahoji kwa mara nyingine tena.
"Utanisaidiaje Roya?"  

Roya akajibu. "Ili uiepuke laana iliyokuwa ikija nyuma yako, ingekulazimu ufe moja kwa moja, ila kwa sasa nitazikwa mimi kwenye kaburi lako ingawa nitahitaji msaada wako, nao sio mwingine ni msaada wa damu.. Bingo fanya ujuavyo, kila siku usiku wa manane vaa nguo nyeusi kisha njoo kwenye kaburi langu, jichanje damu idondokee kwenye kaburi na hapo nitapunguziwa adabu juu ya kile nilichofanya Tropea. Damu yako kwangu ya thamani Bingo tafadhali usisite kufanya hivyo." 

Maneno hayo Roya aliongea huku akilia kwa uchungu. Bingo alisikitika sana, maneno ya Roya yalimuumiza vilivyo. Na mwishowe akasema. 
"Nipo tayari kwa hilo Roya. Na pia nakupenda kama unavyonipenda wewe."

"Nashukuru sana." Roya kwisha kusema hivyo alipotea ambapo muda huo huo Bingo naye alizinduka kutoka usingizini.   

Kweli kijana huyo alifanya kama alivyoagizwa, lakini pia aliomba utajiri..kufumba na kufumbua Pete ikampatia nyumba nzuri kuliko zote kijijini, hakuweza kumsahau mzee Ndelo, mzee cha pombe ambaye alikuwa na umasikini wa kutupwa. Naye alitajirika vya kutosha. Kijiji kikajawa na neema, Bingo alitoa msaada mbali mbali kwa wasio jiweza hata waliopungukiwa. 
       
                           *******
Hivyo ndivyo ilivyo mke wangu, nadhani umepata maana kamili ya mimi kutoka hapa usiku wa saa nane kisha baadae nikirudi nanukia ubani na udi. Namuenzi Roya kwa sababu nisipofanya hivyo kuna hatari ya mimi kupata matatizo. Alisema Bingo akimwambia mkewe wa kuitwa Millander.

Millander hapo awali alikuwa na wasiwasi kuhusu mumewe baada kuona kila siku usiku Bingo huamka huondoka akirudi huwa na damu sehemu mbal mbali ya mwili wake hali ya kuwa hunukia ubani na udi. Na ndio maana siku hiyo akaamuwa kumwambia Bingo. 
"Bingo mume wangu, tayari tumefikisha miezi takribani mitatu sasa tangu mimi na wewe tufunge pingu za maisha. Ukweli nafurahia sana uwepo wako katika maisha yangu na najivunia kuwa na mwanaume mzuri mkamilifu vile vile muaminifu, ukweli uko sawa kwangu lakini licha ya kwamba maisha yetu ya ndoa kuwa yenye furaha na amani ila kuna suala moja huwa linanitatiza akilini mwangu na nashindwa kulielewe, hivyo natumaini leo utanipa uvumbuzi ili niweze kulielewe. Bingo nakupenda sana mume wangu tena zaidi ya sana, kwahiyo nakuomba unambie ukweli usinifiche mimi ni mkeo". Hitaji hilo la Millander kutaka kujua ukweli ndio lililomfanya Bingo kumsimulia safari ngumu iliyompeleka TROPEA - mji wa wafu.  

Hakika ilikuwa ni simulizi tata iliyomshangaza Millander. 
"Pole sana mume wangu, nadhani Pete yenyewe ndio hiyo mkono mwako!.." Millander alisema. 

"Ndio mke wangu ila hapa ilipo imeshapoteza uwezo wake kwahiyo naivaa tu ikiwa kama kumbukumbu ya kutoka Tropea." Alijibu Bingo kisha akacheka. . Millander aliachia tabasamu pana huku akimkumbatia mume wake mpenzi kwa kuwa na moyo wa kijasiri. 
        
          ... ↘️M W I S H O↙️...

ASANTENI KWA KUA PAMOJA KWENYE SIMULIZI HII, MWANZO MPAKA TUNAHITIMISHA LEO ILA UKUMBUKE HII NI RIWAYA YA KUFIKIRIKA 🤣🤣🤣🤣 

Post a Comment

Previous Post Next Post