TROPEA - Mji wa wafu. SEHEMU YA 08

ILIPOISHIA....... 

"Hapana, kwanza fahamu huu mji ulipotea karne ya nane. Mji ambao ulifukiwa baada kutokea tetemeko kubwa la ardhi. Mengi nitakueleza Bingo, sababu kila kitu nakifahamu juu ya mji huu, nitakueleza namna watoto tunavyowaiba hospitalini, lakini pia nitakueleza ajali tunazo sababisha majini angani na nchi kavu. Hata meli kubwa kuliko zote duniani iliyowahi kuzama akapona mtu mmoja. Sisi ndio chanzo.. "

"Meli gani?... " Aliuliza Bingo kwa mshangao wa hali ya juu. Michael aliangua kicheko kisha akajibu.

ENDELEA NAYO........ 

 "Nifuate huku" Bingo alifanya kama alivyoambiwa. Wawili hao walielekea kwenye moja ya nyumba kubwa. Nyumba ambayo ndani walikuwemo watu wengi sana wakiimba na kucheza.. Michael akamtaka Bingo wakaketi kwenye meza kisha aendelee kumueleza maisha na maajabu mbali mbali yaliyopo kwenye ulimwengu wa pili.  
"Bila shaka unawaona watu hawa" Aliongea Michael. 

"Ndio nimewaona.." Bingo aliitikia. Ambapo hapo ndipo Michael alipoongeza kusema. 
 "Watu hawa ni wale waliopata ajali kwenye iliyokuwa Meli kubwa kuliko zote duniani. Na katika ajali hiyo alipona mtu mmoja tu. Na sababu nzima iliyopelekea Meli ile kupata ajali ni baada kiongozi wa wafu kuingiwa na tamaa ya wingi wa watu wale, akaamini kabisa endapo kama atapiga ndege wawili kwa jiwe moja basi itakuwa moja ya faida kubwa sana na istoshe siku ile ambayo Meli ile ilianza safari ilikuwa siku ya skukuu Tropea.. Si kweli kwamba angeokoka mtu mmoja, la hasha wangeokoka watu zaidi ya elfu ila siku ile mji huu uliamua kuishangaza dunia " Alisema Michael kwa kirefu zaidi, akilini mwake akiifahamu fika Meli hiyo. 

"Naam! Nakuelewa Michael." Aliunga mkono Bingo. 

Michael alicheka sana kisha akasema. "Sasa watu hawa unao waona huku ndani ndio wale waliokuwemo katika Meli ile, labda ngoja nikuulize swali Mr Bingo. Hivi hujawahi kuambiwa na mtu kuwa kuna wakati baharini huonekana mauza uza?.."

"Ndio nishaambiwa mara nyingi tu." Alijibu Bingo. 

" Basi ukae ukijua kuwa kuna wakati roho zinatoka Tropea zinatembea kwenye uso wa dunia iwe baharini ama nchi kavu lakini pia ukae ukijua kuwa Meli ile iliyozama akapona mtu mmoja kuna wakati huonekana ikiendelea na safari yake saa za usiku ingawa kwa macho ya kawaida huwezi kuiona... " Aliongeza kusema Michael.

Ukweli yalikuwa ni maneno ambayo yalimshangaza sana kijana Bingo, hivyo macho yake akayarudisha kutazama kule wanakoonekana watu wale waliokuwepo kwenye Meli ya Titanic. Watu ambao muda wote walikuwa wakiimba na kucheza huku wengine wakila na kunywa. 
Hatimaye wawili hao walitoka ndani ya jengo hilo, wakazipiga hatua kuingia kwenye jengo jingine ambalo nalo ndani lilisheheni watu mbali mbali pamoja na mashine za ajabu ajabu, mashine hizo zilikuwa zikirindima huku sauti za watoto wachanga zikisikika wakilia. 
"Hiki nacho ni kiwanda.." Aliongea Michael. 

"Kiwanda?.. Kinatengeneza nini?.." Bingo alihoji. 

Michael akajibu "Ndio maana nikakwambia kuwa kuna wakati maisha ya huku hushabiana vyema na maisha ya ulimwenguni. Bingo huu ni mji, kwahiyo dhumuni kuu la mji huu ni kuzidi kutia sumu ulimwengu ili magonjwa yazidi mpaka kupelekea kifo.. Kifo pekee ndio njia ya kumfanya mtu afike Tropea.. Ingawa kuna baadhi ya nafsi hurejea duniani, na ndio pale unaposikia kuwa marehemu fulani kaonekana sehemu fulani.."

"Na hawa watoto nao vipi?.."
 
"Hawa wengine hunyofolewa wakiwa tumboni kwa mama zao, na wengine huchukuliwa pindi wanapozaliwa, kuna watu wanatumwa kuzunguka hospital kubwa zote kufanya kazi hii. Kuna baadhi ni madaktari na wengine ni nafsi tu..." Alisema Michael.

Hapo Bingo alishtuka, kwa taharuki ya hali ya juu akamuuliza Michael mara mbili mbili. 
"Michael unataka kusema katika hospital kuna madaktari wa uongo?.. "

"Ahahaha haha " Michael aliangua kicheko kwanza kisha akajibu. 
"Asilimia mia moja kijana na ndio pale mama mjamzito anaweza kujifungua mtoto kisha akaambiwa mtoto bahati mbaya kafariki aidha mtoto anapotea katika mazingira tatanishi. Wakifikishwa huku sasa, wanasagwa kisha baadhi hugeuzwa kitoweo huku na baadhi hupelekwa kwenye maduka ya vyakula Duniani..."

"Na hayo magonjwa nayo husababishwa na nini?.." Alihoji Bingo, lakini kabla Michael hajamwambia. Mara ghafla nje ilisikika shangwe za wafu wakitimua mbio. Jambo ambalo lilimshtua Bingo, hima akamtazama Michael kisha akarudia kumuuliza nini kinacho endelea nje. Michael akamtaka atulie, kisha akasogelea dirisha akapata kumuona mtu wa ajabu akifanya fujo mtaa huo. Ajabu mtu huyo alitishia amani zaidi huku akimtaka Bingo popote pale alipo ajichomoze.. 

"Mbona nasikia jina langu?.." Michael alimgeukia Bingo akamtazama kisha akamjibu "Hii ndio sababu kuu iliyokuleta Tropea Bingo.." Michael alisema wakati huo aking'atuka kwenye dirisha na kuzipiga hatua kumsogelea. Alipomkaribia zaidi akaendelea kusema" Huyu ni mfuasi wa Buda, kundi linalo ongozwa na kijana wa Sultan Starlon. Nadhani baada kusikia mtoto wa jamii ya Abdy, mtoto wa Sultan Abatish tayari yupo katika mji huu, anataka kukumaliza mapema ili mpango wake uweze kutimia... Tambua unakibarua kizito sana Bingo, usimuangushe mzee wako na najua anahamu sana ya kukuona.." Alisema Michael wakati huo huo nje fujo ziliendelea na punde si punde ukatokea ulingo mrefu uliojengwa kwa dakika kadhaa kisha mfuasi huyo wa Starlon akaendelea kupasa sauti yake kumuita Bingo huku akidiriki kutisha kuteketeza wafu wengine na kisha kuwageuza kitoweo. 

"Michael kipi sasa nifanye?.."
 
"Kupigana unaweza?.." 

"Ndio.." 

"Kweli unaweza kuutumia vizuri upanga?.."

"Hilo ondoa shaka kabisa.."
 
"Basi.. Jitokeze, nje tayari kuna ulingo mkubwa ambao upo kwa niaba yako.." Aliongeza kusema Michael kwa sauti ya upole iliyojaa huzuni ndani yake. 

Hapo ndipo Bingo alipovaa stahiki koti lake kisha akafungua mlango akajitokeza kukabiliana na yule mtu ambaye kimuonekano sio mtu wa kawaida... Ajabu fujo za vilio zilitoweka, safari hiyo ikisikika sauti ya kumshangiria Bingo.. 

"Bingo.. Bingoooo.. Bingoooo.. Bingoooo.." Na kadri shangwe hizo zilipokuwa zikisikika ndivyo wafu wengine walivyozidi kuongezeka kumshuhudia kwa mara ya kwanza mtoto wa kiongozi wao bwana Sultan Abatish.. Bingo alishangazwa na shangwe hizo, muda huo akamtazama yule mtu wa ajabu anayetarajia kupigana naye kisha akarudisha uso kumtazama Michael. Michael akamnyooshea dole gumba. Na hapo na hapo wawili hao wakapanda kwenye ulingo.. Ndivyo shangwe zilipozidi, jina la Bingo lisikauke midomoni mwa wale wafu.. "Bingo... Bingoooo Bingoooo.." 

Shangwe zilizosikika zilimfanya Bingo kujawa na mzuka mara mbili ya hapo awali, hivyo haraka sana alichomoa upanga wake kisha akawa tayari kwa mpambano.
"Bingooo.. Bingoooo Bingooo" Bado sauti za wale wafu ziliendelea kumshangiria Bingo. Muda huo huo yule mfuasi wa ngome ya Starlon naye akachomoa upanga wake, na hivyo wote wakawa tayari kwa niaba ya mpambano. Punde mtu huyo alirusha panga lake.. Bingo alikwepa kwa style ya kutembelea magoti, panga hilo likawa limepiga moja ya mbao zilizojenga ulingo. Na kwa namna panga hilo lilivyokuwa na makali ilipelekea mbao hiyo kukatika vipande viwili. Bado patashika ilizuka ulingoni hapo, kijana Bingo alionyesha ushujaa wa kumkwepa vilivyo mtu huyo ambaye kimuonekano alionekana ni hodari sana kuchezea panga.

"Bingo.. Hapa ndio mwisho wako.." Aliongea mtu huyo kwa sauti ya kutisha wakati huo huo akarudia tena kutembeza kichapo ingawa alionyesha sio chochote kwa kijana Bingo. Bingo aliruka samasoti aliruka sarakasi ya kila aina.. Jambo ambalo liliwafanya wafu hao waliokuwa wakishuhudia pambano kuzidisha nguvu ya kushangiria. Michael alionekana kubaki mdomo wazi, na hata asiamini kama kweli ni huyu huyu Bingo anayemfahamu yeye. 
"Laah! Noma sana" Alijisemea Michael huku mikono ikiwa kichwani akikoshwa na uwezo wa Bingo. 

Baada muda wote Bingo kuonekana akikwepa mapigo ya mtu huyo mfuasi wa ngome ya Starlon, hatimaye sasa akaona ni wakati wa yeye naye kuonyesha umwamba mbele ya mtu huyo kwani kwa muda wa takribani dakika thalathini alikuwa akimsoma namna anavyopigana na janja anayotumia. Hapo kwanza Bingo aliangua kicheko "Ahahaha hahahah" Alipokwisha kukatisha kicheko chake akamnyooshea kidole kisha akamwambia "Wewe.. Hebu nisikilize. Jina lango naitwa Bingo. Mimi ni nafsi na sio mfu kwahiyo sijaja Tropea kushangaa majengo yenu sababu kama ni majengo basi hata duniani yapo mengi sana. Nimekuja Tropea kufanya mapinduzi, tazama uma wa wafu hao hapo chini. Wafu hao wanangoja kuona maajabu yangu, hivyo basi nakupiga, nakucharaza kisha nikutume ukamwambie mkubwa wako kuwa, maji yameingia upupu na hivyo sio rahisi kuyaoga.. " Aliongea Bingo huku akionyesha kujiamini asilimia mia moja. Ni majigambo ambayo yalifanya eneo hilo kuripuka shangwe, na mwisho wa shangwe hizo jina la Bingo lilitajwa ilihali likisindikizwa na makofi ambayo yalipigwa sambamba na jina Bingo

Hapo makofi yalisikika, hivyo hivyo ilimradi kumfanya Bingo ajihisi amani. Amani ambayo itampelekea kujiamini, na mwisho wa kujiamini kinachofuata ni ushindi.

" Ahahaha hahahah " Alicheka sana mtu huyo baada kuyasikia maneno ya dharau aliyoyaongea kijana Bingo. Kicheko cha mtu huyo kilisindikizwa na ngurumo nzito ambazo ziliambatana na miale ya radi. Na mara baada ya kuhitimisha kicheko hicho alinyoosha mkono juu, punde katika kiganja chake lilitokea rungu kubwa lenye misumari ilihali muda huo huo nywere zake ziligeuka nyoka. Bingo alishtuka lakini kwa kuwa toka awali alishaonyesha moyo wa kujiamini.. Hivyo hakutishika na mambo hayo, nywere hizo ambazo ziligeuka nyoka alizichukulia ni rasta hali ya kuwa rungu hilo la misumari alichukulia kama fimbo tu. Hapo Bingo alishusha pumzi ndefu kisha akautupa kando upanga wake na mara moja kwa kasi ya ajabu akamvaa huyo mtu. Pambano kwa mara nyingine tena likaendelea, safari hiyo Bingo hakuogapa. Japo huyo mtu mfuasi wa kutoka ngome ya Starlon alionekana kuwategemea nyoka walio kichwani mwake ila bado mipango yake ilishindwa kumpa matokeo chanya, alipigwa kama mbwa mwizi. Bingo baada kuona mtu huyo hana tena Jeuri alichukuwa upanga wake kisha akamsogelea, akafungua kifungo cha koti lake upande wa kifuani, akajichana kwa upanga wake, upanga huo ukiwa unatiririsha damu akamnyooshea mtu huyo kisha akasema "Nakuacha ili upeleke ujumbe huko kwenye ngome yenu, mwambie kuwa Bingo yupo ndani ya Tropea.." 
     
               *********

Hayo yalipopita alionekana Bingo na Michael wakiwa kwenye moja ya ukumbi wakipata chakula baada ya mpambano. 
"Bingo.. Unajua kwa sasa kila sehemu unazungumziwa wewe?.." Aliongea Michael. 

"Hahaha hahahah.. Najua yote sababu ya kile nilicho kifanya ila kwa kuwa tayari nimejitoa muhanga kwenye hili jambo basi nitapambana mpaka hatua ya mwisho.." 

"Safi sana kijana, lakini mbali na upiganaji wako kuna maneno ambayo umeyaongea, hakika ulionyesha ushupavu Bingo. Hongera yako jamaa" Aliongeza kusema Michael, maneno ambayo yalimfurahisha sana Bingo.

Muda huo nje kulikuwa na wafu wengi wakigombea kumuona Bingo. Bingo alishangazwa na jambo hilo lakini muda huo huo ndani humo aliingia Roya huku akionyesha mtu mwenye tabasamu pana. Roya alizipiga hatua kumsogelea Bingo, alipomfikia akamwambia. 
"Tayari upo ndani ya Tropea Bingo, hongera kwa kufanya vizuri kila hatua. Na pia siku ya leo ndiyo siku ambayo unatarajia kwenda kuonana na baba yako. Sultan Abatish" 

"Roya nashukuru sana, ndio nafurahi uwepo wangu huku Tropea kwani najua kurudi kwangu duniani ndio kutampelekea mama yangu kupona.." Alijibu Bingo wakati huo akikunjua miguu yake ambayo alikuwa amekaa style ya nne. Roya alicheka kwanza kisha baadae akajibu. "Bingo hebu acha kunichekesha bwana.. "

Alisimama Bingo kisha akahoji "Uamaana gani Roya, je wataka kuniambia ahadi mliyoniahidi haitotimia?.. "

"Hapana Bingo wala sina maana hiyo, lakini mbona ameshapona? Yaani siku ile uliyoanza safari ndio siku ambayo mama yako alipona maradhi kwa maana hiyo basi wewe ni wa kwetu kamwe hutoweza kurudi duniani " Alisema Roya, safari hiyo akiwa amebadilika asiwe na hata chembe ya asili ya binadamu. Bingo alishtuka, hakuyaamini yale ayasikiayo. Ghafla akajihisi kuishiwa nguvu ilihali kijasho chembamba kikimtoka. Pumzi ndefu alishusha wakati huo akijitazama mwilini, machozi yalimtoka hasa baada kujigundua kuwa hapo alipo ni nafsi ila mwili upo duniani. Na endapo mwili huo utazikwa basi habari yake itakuwa imekomea hapo.  

"Inamaana kuwa huu ulikuwa mtego?.." Alijiuliza kijana Bingo ndani ya akili yake. "Laah! Hapana sasa inatakiwa kubadilisha maamuzi... Lazima nirudi duniani.." Aliongeza kujisemea hivyo Bingo wakati huo huo akiingiza mkono mfukoni kuchukua ramani yake ili ajihakikishie safari yake ya kurudi duniani. Lakini ajabu alipoitoa ramani hiyo aliona hakuna mahali palipochorwa zaidi ya karatasi kuonekana tupu.. 

KIPI KILIJIRI HAPO? JE, BINGO ALIFANYAJE KUREJEA DUNIANI? 

Post a Comment

Previous Post Next Post