ILIPOISHIA.......
"Huyu ni binti yangu, siku ya leo nataka ufanye nae mapenzi kabla hujaondoka, hapo alipo ana miaka zaidi ya hamsini wala hamjui mwanaume, hivyo basi nataka wewe ndio uwe wa kwanza kwake.." Alisema hivyo Ajuza huyo, na safari hii sauti yake ilikuwa ikijirudia mara mbili mbili kama mwangwi huku macho yake nayo yakibadilika rangi..
ENDELEA NAYO......
Bingo aliogopa suala hilo, kwani alishaambiwa kuwa hatakiwi kufanya mapenzi na mtu yoyote ndani ya safari yake, hivyo aliona hakuna njia nyingine zaidi ya kutimua mbio. Bingo alikimbia na muda huo nyuma yake ilionekana mikono ya wafu ikichomoza ardhini kwa sauti juu kabisa vicheko vilisikika, na punde si punde juu ya ardhi lilionekana kundi la wafu likimkimbiza Bingo.
Hali ambayo ilimpelekea kijana huyo kukaza mwendo ingawa mwishowe alikubali matokeo baada mbele yake kuonekana kundi lingine, ghafla kulia na kushoto nako makundi mengine. Sasa Bingo akajikuta yupo katikati.. Hofu dhofu lihali ilimganda Bingo, akaamini tayari mwisho wa safari yake umewadia lakini wakati akiwaza hilo, mara ghafla alitokea msichana mrembo akiwa na upanga mrefu mkali, msichana huyo alimtazama kwanza Bingo akaachia tabasamu kisha mara moja akaanza kazi ya kuwashambulia wale wafu. Ilikuwa shughuli pevu ila mwishowe mwanadada huyo aliwamaliza ambapo hapo ndipo alijitokeza yule Ajuza aliyemsaidia Bingo.. Ajuza huyo naye alikuwa na upanga mkali vile vile ajabu ni ule upanga ambao Bingo alikabidhiwa na mzee Ndelo kabla hajaanza safari ya Tropea.
Alistaajabu sana Bingo wakati huo akiwa pembeni akiacha uwanja uchafuliwe na binti huyo aliyepania kumuokoa kwa kuteketeza kundi lile la wafu lililokuwa likimfuata lakini wakati Bingo akiwa na hali hiyo ya taharuki, yule msichana alimgeukia kwanza kisha akaachia tabasamu.
"Khaa Roya?.." Alijisemea Bingo baada kugundua kuwa yule msichana ni Roya, binti ambaye alikuwa akimtokea mara kwa mara na kumuasa juu ya habari ya kufika Tropea.. Punde si punde Ajuza alirusha upanga wake kuelekea pale aliposimama Roya, ambapo naye kwa umakini kabisa alipotea akaibukia sehemu nyingine.
"Hahaha hahahah" Ajuza aliangua kicheko kisha akajitoa mara nne, yaani nafsi nne na kila nafsi ilikuwa na silaha yake. Bingo alishangaa sana, bado alitulia pembeni huku akishuhudia mpambano mkali baina ya Roya na Ajuza. Wote walionekana sio binadamu wa kawaida ingawa Roya alionyesha kuwa na baadhi ya vitu ambavyo vilifanana na vya Binadamu. Basi patashika nguo kuchanika iliendelea mahali hapo, Roya alionyesha umahiri wa kuzikabili hizo nafsi za Ajuza, hivyo moja baada ya nyengine aliteketeza mpaka pale alipobaki Ajuza mwenyewe. Mbinu hiyo ikawa imegonga mwamba..
"haaa! Kweli hii ni hatari" Alirudia kujisemea Bingo akistaajabishwa na huo mpambano. Na kipindi anashangaa ghafla upanga aliokuwa akiutumia Ajuza ulitua mbele yake, manusura umjeruhi ni baada Roya kuupangua ambapo uliweza kumtoka kiganjani moja kwa moja ukadondokea mahali aliposimama kijana Bingo. Hapo sasa Bingo akapata kuuona vizuri kabisa upanga huo, haukuwa mwingine ni ule ule aliopewa na mzee Ndelo. Muda huo huo Ajuza akawa anajitahidi kumkabili Roya ili aufuate upanga huo. Na hapo Roya akamwambia Bingo auchukue huo upanga na kisha aondoke mahala hapo.
"Bingo chukua panga ukimbie.." Alisema Roya kwa sauti ya juu kabisa huku ikijirudia mara mbili mbili.
Bingo baada kusikia maneno hayo kidogo aliogopa, lakini mwishowe akaona heri lawama kuliko fedheha. Liwalo na liwe, hima aliuchukua upanga huo akaurejesha kwenye kala lake. Ukakaa sawa kisha mara moja akatimua mbio huku nyuma akiacha Roya akipigana na yule Ajuza wa ajabu.
Ila kabla Bingo hajafika mbali.. Alisimama kwanza, machale yakamcheza akahofia usalama wa Roya. Hivyo aligeuka nyuma ajabu kwa mbali akapata kuona makundi mengine ya wafu yakielekea kwenye mpambano. Pumzi ndefu alishusha Bingo wakati huo akijiuliza.
"Mmh Naam! Huu ni muda wa mimi kuonyesha msaada wangu kwa Roya kwa kuwa amenisaidia kuupata upanga wangu, basi sina budi kuutumia upanga huu.. Lakini nitaweza kukabiliana na hawa wafu?.. Ngoja niende liwalo na liwe kama kufa nitakufa tu" Maneno ya kijasiri aliyanena Bingo ndani ya nafsi yake kisha akachomoa upanga wake akaushika kwa nguvu zake zote. Kwa mara nyingine tena alishusha pumzi halafu akatimua mbio kwenda kumsaidia Roya. Vurumai la maana lilizuka mahali hapo, Bingo alitembeza dozi kwa umaridadi wa hatari mpaka akashinda huku Ajuza naye aliamua kupotea kimazingara.
"Pole sana Roya" Bingo alimwambia Roya huku Roya akionekana kuwa hoi bin taabani lakini Roya hakusema chochote alikaa kimya kwanza ingawa baada ya dakika kadhaa kupita alijibu.
"Usijali.. Ila Bingo bado unasafari ya kuingia mji wa wafu.. Hebu fumba macho.." Bingo alifumba. Muda mchache baadae akaambiwa afumbue ambapo hakuweza kumuona Roya.
"Royaaa.. Royaaa.. Royaaaaaa" Bingo akipasa sauti ya kumuita Roya huku akigeuka kila upande na hata asimuone. Na pindi yupo kwenye hali hiyo ya mshangao mbele yake alitokea mzee Ndelo.. Mzee huyo akamwambia kijana Bingo.
"Unajua unafanya sana mzaha kwenye safari hii, sifikirii kama utaweza kufaulu huu mtihani kwa sababu unaenda na kurudi nyuma. Bingo kuwa makini na safari yako, hebu achana na huo upanga ulionao sababu utakufanya ukutane na wingi wa maadui ambao watakufanya safari uione chungu.. "
" Mzee wangu! Unamaana gani sasa? Wewe si ndio uliyenipa upanga huu?.." Alistaajabu Bingo.
"Ahahaha hah hahahah.. Hahahah hahaha ah "Mzee Ndelo aliangua kicheko kisha akaongeza kusema"
Hebu nikabidhi huo upanga halafu nikuonyeshe njia nyepesi ya kukufikisha Tropea.. "
"Mmmh!.. " Aliguna Bingo wakati huo akimtilia shaka mzee Ndelo. Baada kukumbuka namna upanga ulivyomsaidia akahisi kuwa huwenda ukawa mwisho wa maisha yake.
"Hapana hii ni silaha yangu na wewe sio mzee Ndelo.. Hujanipata kwa mtindo huo" Kwisha kusema hivyo aliondoka zake ilihali huku nyuma mzee Ndelo aligeuka akawa yule yule Ajuza aliyekuwa akipigana na Roya hapo awali. Ajuza huyo aliamua kutumia njia hiyo akiamini kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kijana Bingo kumuamini akamkabidhi upanga huo. Hapo alipotea. Bingo alipogeuka nyuma hakumwona hivyo aliamua kutimua njia kwa kutumia ramani yake.
********
Millander, hapo nikawa nimefaulu huo mtihani yaani kiasi kwamba endapo ningemkabidhi upanga yule Ajuza aliyechukua taswira ya mzee Ndelo. Bingo ningekwisha. Basi nilitimua mbio kwa kufuata ramani, ila pindi safari inaendelea mbele yangu nilimuona mama mjamzito akiwa kando ya njia. Mama huyo uchungu ulikuwa umemshika kwahiyo alikuwa akigaagaa huku na kule wakati huo anapiga kelele akihitaji msaada. Sasa basi mimi pasipo kufikiria ama kujiuliza mama huyo kafikaje mahala hapo, haraka sana nikataka kumgusa ili nimuulize maswala kadhaa ikiwezekana niweze kumsaidia.
"Mmh kumsaidia? Sasa ungemsaidiaje wakati wewe sio doctor?.." Aliuliza Millander mkewe Bingo.
"Ndio hapo sasa maajabu hayo, tulia nikusimulie ili hata siku nyingine usinishangae pindi nitakapo toka nyakati za usiku huku nikirudi nanukia ubani ilihali sehemu mbali mbali za mwili wangu zilionekana damu. Tropea mamaa Tropea hiyo.. Oohoo hatari sio mchezo nakwambia " Bingo alijibu huku akitia utani kidogo. Millander alionyesha utulivu, na hapo Bingo akapata wasaa wa kuendelea kusimulia. Basi kabla sijamgusa, na mie niliguswa mgongoni nilishtuka haraka sana nikageuka kumtazama mtu huyo aliyenigusa, cha ajabu mtu huyo na yule mama mjamzito walifanana kila kitu. Nilishangaa sana, niliporudisha macho yangu kumtazama yule mama aliyekuwa anagagaa chini ajabu sikumuona, yule naye aliyenigusa alipotea.
******
Bingo alipagawa akatoka mbio, alikimbia sana mbele zaidi aliona njia tatu. Njia moja ilielekea kulia na nyingine ilielekea kushoto vile vile njia ya tatu ilinyooka. Hapo sasa akachomoa ramani ili impe muongozo. Ramani ikamuonyesha kuwa anatakiwa anyooshe, jambo ambalo lilimfanya kijana Bingo kuachia tabasamu kisha akaendelea na safari. Alitembea umbali mrefu sana pasipo kubuguziwa na mauzauza yoyote, hali ambayo ilimfurahisha sana. Hatimaye anapata kuona ngome iliyojengwa kwa dhahabu huku ngome hiyo ikiwa imepambwa nembo mbali mbali za kuzimu, juu ya ngome hiyo kuna ubao uliandikwa maneno ya kuitambulisha ngome hiyo, hivyo Bingo aliinua uso wake ili ayasome maandishi hayo yaliyoandikwa kwenye huo ubao ili ajue kama yameandikwa Tropea ama la! Lakini kabla hajaanza kusoma, ghafla aliguswa bega, hima aligeuka akakutana uso kwa uso na mtu aliyemfahamu, mwanakijiji mwenzake ambaye alifariki miaka kadhaa iliyopita. Kifo chake kikisababishwa na ajali ya gari.
"Habari yako Bingo, vipi mama na baba yangu wazima? Vipi mke wangu na mwanangu! .." Alisema mtu huyo jambo ambalo lilipelekea Bingo kuacha kutazama bango lile ambalo lilikuwa kwenye ngome ile, alitaharuki.
Akajiuliza ndani ya moyo wake "Inamaana Michael hajafa au macho yangu?.."
"Huna budi kujiuliza maswali mengi Bingo, kwanza kabisa karibu Tropea, nafikiri uwepo wako huku utaweza kuleta manufaa kwenye ngome ya baba yako.." Aliongea mtu huyo, mtu ambaye Bingo alimfahamu fika sababu alikuwa mmoja ya wanakijiji mwenzake, ila alifariki kwa ajali ya kugongwa na gari.
Maneno hayo yalimshtua Bingo, na hapo ndipo alipoinua macho yake kutazama juu kwenye ngome ambapo lilionekana bango. Bango hilo liliandikwa kwa lugha ya ajabu sana, lugha ambayo ilimuwea ngumu Bingo kufahamu kilicho andikwa.
"Pale juu pameandikwaje?.." Bingo alimuuliza yule mtu aliyeitwa Michael. Michael aliangua kicheko kisha akajibu "Karibu Tropea.. Bingo huu ndio mlango wa kuingia Tropea, mji uishio wafu, sisi huku ni watumwa.. Kuwa makini sana Bingo, sababu tayari mji huu umechafuka sana shauri ya pande mbili tofauti kuzozana..." Aliongea Michael kwa kirefu zaidi.
Pumzi ndefu alishusha Bingo, hata asiamini kama kweli kafika mji huo aliotakiwa kufika na wakati yupo katika hali hiyo ya taharuki mara ghafla Michael alipotea, na punde si punde wakatokea watu wawili waliovaa makoti meusi huku nyuso zao zilionekana kutisha kutokana na namna walivyofanana, walikuwa warefu kuliko binadamu yoyote duniani, miili yao mikubwa. Macho yao yalifanana fika na macho ya nyoka ilihali midomo yao nayo ikiwa ya kawaida kama ilivyo ya binadamu kasoro rangi ya ngozi yao ambayo kwenye nyuso walionekana kuwa na rangi nyekundu.
"Bingo..!.." Moja ya watu hao wawili alipasa sauti kumuita Bingo. Bingo akaitika.
"Karibu sana Tropea.." Mtu wa pili alisema kisha wote kwa pamoja wakainamisha nyuso zao wakitii heshima kwa kijana huyo ni heshima ambayo ilimshangaza Bingo, jambo hilo lilimfanya sasa roho yake kuwa na imani akiamini kuwa tayari yupo katika lango la kuingilia Tropea. Muda mchache baadae lango la ngome hiyo ulifunguka kisha mmoja akaongoza kuingia ndani akifuatia na mwenzake ambaye naye alimtaka Bingo amfuate nyuma. Bingo alifanya kama alivyoambiwa lakini kabla hajaingia ndani.. Nyuma yake alitokea mzee Ndelo. Mzee huyo alikohoa kidogo kisha akamuita Bingo.
"Bingooo!.." Bingo alishtuka kusikia sauti hiyo, haraka sana akageuka akakutana na uso wa mzee huyo ambaye alimpa njia ya kuelekea Tropea. Mzee Ndelo akiwa na tabasamu bashasha alimnyooshea Bingo kidole gumba akimanisha kuwa mambo sio mabaya, ambapo Bingo naye tabasamu hilo alilijibu hivyo hivyo kisha naye akamnyooshea kidole kama alivyofanya Ndelo. Lango likafungwa, Bingo akatokomea na watu hao. Ajabu alipata kuona majengo marefu kwa mafupi, mikubwa kwa kidogo. Na jambo ambalo lilimshangaza zaidi Bingo ni baada kuona maisha ya Tropea hayajapishana sana na maisha ya ulimwenguni. Watu waliendelea kufanya shughuli zao kama kawaida, watembea kwa miguu walionekana wakitembea ilihali vile vile waendesha magari waliyaendesha magari yao kwa kasi. Hali ya hewa ya mji huo ilikuwa hafifu mfano wa hali ya hewa ya duniani pindi jua lizibapwo na mawingu mzito ya mvua. Mbali na hayo yote, lakini pia watu wa Tropea hubadilika kutokana na siku. Jumatano, ijumaa pamoja na jumapili. Hizo ndizo siku ambazo watu wa huo mji hubadilika kuwa wafu ambapo hapo ndipo huchaguliwa baadhi ya watu hutumwa duniani kufanya mauaji kwani siku hiyo ndio siku ambayo Tropea hutakiwa damu ili kupata chakula ambacho ndicho huwafanya watu hao kuishi. Watu waishio ndani ya Tropea hutegemea nyama za binadamu ikiwa kinywaji nacho hutumia damu.
"Bingo.."
"Naam! Naona umekipenda kitabu hicho lakini pia unaonekana kukiogopa na yote sababu ya mambo yaliyoandikwa humo ndani.." Aliongea mtu mmoja kati ya wale wawili waliompokea Bingo. Mtu huyo alikuwa kando ya Bingo, mmoja alisimama kulia na mwingine alisimama kushoto. Ni kitabu kikubwa alichokabidhiwa Bingo mara baada kuingizwa ndani ya chumba ambacho ndani yake zilisikika sauti za watu wanaolalama na wengine kupiga kelele kuomba msaada. Hivyo Bingo baada kusoma baadhi ya mambo yaliyoandikwa katika kitabu hicho, pumzi ndefu alishusha ilihali muda huo huo ndani ya chumba hicho aliingia mwanadada ambaye alionekana kuvaa gauni refu huku miguu yake ikiwa na kwato za ng'ombe. Dada huyo mkononi alishika plet moja ya iliyojaza sahani na bakuli. Alitembea kwa madaha kuelekea mahali aliposimama Bingo, ambapo mara baada kumkaribia alikichukuwa kitabu hicho ambacho alikuwa akikisoma kisha akamsogezea plet hiyo ambayo ilionekana kuwa na sahani pia na bakuli iliyojaza vyakula.
"Karibu mwana Abd. Chakula hiki ni mahususi kwa ajili yako.." Aliongea dada huyo halafu akapotea.
Ukweli muda huo tumbo la Bingo lilihisi njaa kali mno, kwahiyo haraka sana alipitisha stick ndani ya bakuli ili aanze kula.. Ajabu alipouvuruga mchuzi uliokuwemo katika bakuli hilo, aliona macho ya binadamu pamoja na ulimi.. Ilihali muda huo mchuzi wa mboga hiyo ulitoa harufu mbaya sana..
"Nini hii?.. Aliuliza Bingo. Wale watu wawili ambao muda wote walikuwa wamesimama walitazamana kisha mmoja akasema kwa sauti nzito
"Bingooo mwana wa Abd.. Unakazi ngumu iliyopo mbele yako, hupaswi kuuliza zaidi ya kula ili uanze kufanya kile kilichokuleta ndani ya mji huu.. " Maneno hayo yalisikika kwa ukali kitendo ambacho kilimuogopesha sana Bingo, na hivyo hakuwa na namna alikula japo kwa tabu sana.
Muda mchache baadae, Bingo akaingia mtaani sasa mjini Tropea kuangalia manzari ya mji ikiwa wale watu wawili tayari wameshapotea kwani shughuli yao ilikuwa imeshamalizika. Shughuli ya kumpokea Bingo na kisha kumsimamia katika suala zima la chakula lakini kitendo ambacho kilimshangaza Bingo ni pale kila alipokuwa akipita watu walimsujudia, si mkubwa wala mtoto. Wote heshima walimpa.
Hatimaye kwenye tembea tembea yake kwa mara nyingine tena anakutakana na Michael, kwa sauti ya juu Michael akamwambia Bingo "Bingo, naona tayari upo mtaani.. Heshima yako mkubwa.."
"Michael, hebu subiri kwanza, hivi mbona kila ninapo pita watu wanainisujudia?.." Aliuliza Bingo kwa taharuki baada kuonana na Michael mtu ambaye anaishi kwenye ulimwengu wa kiroho ilihali duniani akihesabika kuwa ameshafariki.
Michael baada kuyasikia maneno hayo ya Bingo alicheka sana, sauti ya cheko lake lilijirudia mara mbili mbili. Alipolikatisha akamjibu "Bingo wewe ni mtu mkubwa sana hapa Tropea, muhimu kumbuka ulichofuata huku ili uweze kurudi salama..."
"Unamaana gani?.." Alihoji Bingo.
Michael akajibu "Kwanza kabisa wewe kula nyama ya mtoto mchanga mwenye sekunde kadhaa tangu azaliwe hiyo ni heshima kubwa sana kwako, sababu chakula hicho huliwa na viongozi wakubwa wa mji huu..."
"Khaa? Michael unataka kuniambia kuwa nimekua nyama ya binadamu?"
"Ndio Bingo.."
"Doh!.. Kwahiyo huku Tropea mnazaliana?.."
"Hapana, kwanza fahamu huu mji ulipotea karne ya nane. Mji ambao ulifukiwa baada kutokea tetemeko kubwa la ardhi. Mengi nitakueleza Bingo, sababu kila kitu nakifahamu juu ya mji huu, nitakueleza namna watoto tunavyowaiba hospitalini, lakini pia nitakueleza ajali tunazo sababisha majini angani na nchi kavu. Hata meli kubwa kuliko zote duniani iliyowahi kuzama akapona mtu mmoja. Sisi ndio chanzo.. "
"Meli gani?... " Aliuliza Bingo kwa mishangao wa hali ya juu. Michael aliangua kicheko kisha akajibu..
USIKOSE MUENDELEZO WA KIGONGO HIKI TROPEA.. Tusubiri kesho atueleze Mbinu wanayotumia na ajali wanazo sababisha.. Hivi Uliwahi kutokewa na ile hali ya kufika sehemu ambayo haujawahi kufika na ndio mara yako ya kwanza? Lakini kwa mbali unakumbuka kuwa sehemu hiyo uliwahi kufika ila hukumbuki ilikuwa lini?
Tags:
RIWAYA