TROPEA - Mji wa wafu SEHEMU YA 06

ILIPOISHIA....... 

"Unamanisha nikapigane naye?.." Alihoji Bingo kwa taharuki kubwa. 

"Ndio. Na sio kupigana naye tu, bali unatakiwa kushinda ili safari yako ya kwenda Tropea iweze kuendelea.." Alijibiwa Bingo, maneno ambayo yalimshangaza wakati huo akijiuliza atakabiliana vipi na Jitu hilo kubwa la ajabu hali ya kuwa hana silaha yake! 

ENDELEA NAYO..... 

Bingo alishtuka sana baada kuambiwa apigane na lile Jitu la ajabu, akawaza ni namna gani ataweza kulimudu pasipokuwa na upanga wake. Pumzi ndefu alishusha kisha akafunga zipu ya koti lake ambayo hapo awali alikuwa ameifungua upande wa kifuani, ilihali muda huo shangwe ziliendelea kuripuka katika ulingo ule, watu wale wa ajabu walikuwa wakilishangilia lile Jitu ambalo lilionyesha kuwa na uchu wa kupambana. Hapo sasa Bingo alishuka kwenye ngazi inayoelekea ulingoni, punde si punde alifika kitendo ambacho kilionyesha kama kituko katika ulingo huo. Vicheko mbali mbali vilisikika wakimcheka Bingo, bila shaka walionekana kumdharau kijana huyo kutokana na umbile lake lilivyo dogo wakati huo akitegemea kupigana na Jitu lenye miraba minne, ngoma ilitumbuizwa kuashiria pambano kuanza, ndipo hapo patashika lilipoanza. Jitu lile lilirusha upanga wake kwa nguvu na umakini wa hali ya juu lakini Bingo alichokuwa akikifanya ni kukwepa kwa kuruka kwenye uzio wa nyavu zile za chuma huku akipata upenyo anarusha mateke kadha wa kadha, mateke ambayo si chochote si lolote kwa hilo Jitu. 
Mwendo ukawa huo huo, hatimae mzunguko wa kwanza ukafikia tamati, bila mshindi kupatikana. 
"Bingo unatakiwa kukaza buti, sababu sheria ya huu ulingo hamutakiwi kutoka wote mkiwa hai lazima mmoja afe ndipo apatikane bingwa, hivyo pambana kwa nguvu zote kijana sawa sawa?.." Alisisitiza mmoja ya wale watu waliomtuma Bingo kupigana. 

Jamaa huyo aliongea kwa sauti ya juu sana sababu ya fujo zilizokuwa zikiendelea mle ndani Bingo alikubali kwa kutikisa kichwa kisha ngoma kwa mara nyingine tena ikalia kuashiria kwamba mzunguko wa pili unatarajia kuanza, kama ilivyo ada kwa watazamaji waliweza kushangiria kwa nguvu zote, muda huo huo Jitu lile lilikuwa tayari lipo katikati ya ulingo, safari hiyo halikuwa na upanga bali mkononi mwake lilishika rungu lenye misumari, punde mpambano ukaendelea, hatari kwa kijana Bingo, lile Jitu lilitembeza rungu lake kwa ustadi wa hali ya juu kiasi kwamba Bingo akizubaa basi habari yake itakuwa imekomea hapo lakini Bingo aliweza kukwepa, ila mwishowe alijihisi kuchoka kwani ikumbukwe alikuwa akipigana na mtu wa ajabu yaani sio mtu ambaye wa kawaida. 
Hivyo hali hiyo ilimpelekea Bingo kuishiwa nguvu, hatimaye alianguka chini kitendo ambacho kilifanya lile Jitu kucheka sana wakati huo likinyanyua juu rungu lake ili limalize mchezo, pale alipo angukia Bingo kumbukumbu zake zikarudi nyuma, akakumbuka kuwa hapo alipo yeye ni nafsi ingawa yupo katika hali ya kibinadamu kwahivyo sio mfu wala sio kiumbe cha ajabu kama ilivyo hao aliowakuta katika kitongoji hicho, mwili wake upo duniani na pia unafanyiwa maandalizi ya kuzikwa ingawa mzee Ndelo alimwambia kuwa atafanya juu chini ili kuhakikisha mwili huo hauzikwi mpaka pale atakapo rejea kutoka Tropea. Pia mbali na hayo, Bingo alikumbuka kuwa bado anakazi ngumu na nzito ya kuhakikisha anakanyaga mji wa wafu ili kuikomboa ngome ya baba yake, zoezi ambalo litampelekea kupata dawa ya kumponyesha mama yake, hivyo basi ni wajibu wake kupigana ipasavyo ili safari yake iweze kuwa safari ya matumaini. Matukio hayo Bingo aliyakumbuka kwa haraka haraka ndani ya kichwa chake, ghafla akafumbua macho yake akajihisi kupata nguvu ilihali muda huo huo lile Jitu tayari lilikuwa limeshanyanyua rungu juu likingojea nusu sekunde tu limalize mchezo, kweli punde tu kwa nguvu lilishusha rungu hilo ambapo Bingo aligaagaa pembeni, rungu hilo likawa limepiga sakafu, kitendo ambacho lilipelekea sakafu kupasuka na punde si punde tetemeko la ajabu lilizuka, kwenye upenyo wa nyufa, Bingo alibahatika kupenya ambapo alidondokea kwenye tope. Muda huo sasa bado baadhi ya majengo yaliendelea kubomoka huku vifo navyo vikiendelea kuzuka. 

               **********
Hapo sasa mke wangu Millander nikawa nimepotezana na wale watu ambao walinitaka nifanye kile wanacho kitaka. Niliendelea kukaa kwenye lile tope ambalo liliishia usawa wa kiuno changu, na jambo ambalo nilikuwa nalo makini ni kuilinda ramani ya kunifikisha mji ule wa wafu lakini wakati nipo ndani ya tope hizo mara ghafla nikawekwa chini ya ulinzi na watu wengine tofauti na wale niliokuwa nao hapo mwanzo kuacha wale binadamu wenzangu. Watu hao walikuwa na mapembe, miguu mikubwa ingawa kimaumbile ni wafupi sana. Ajabu masikio yao yalikuwa marefu sana, walikuwa wanne basi walinitoa kwenye tope zile wakanipeleka kwa mkuu wao ambaye naye alifanana nao kila kitu lakini pia lugha waliyoongea sikuweza kuielewa ila tu jambo la kwanza walinivua koti langu halafu wakanipeleka kwenye chumba mahususi ambacho ndani palikuwa na giza nene. Daah! Millander we acha tu, nilipagawa sana sababu koti walibaki nalo halafu kwenye mfuko wa koti lile kuna ramani yangu ambayo itanifikisha Tropea. Niliwaza nitafikaje sasa kwenye ule mji wa wafu? Mungu si Athumani, muda mchache baadaye nilitolewa ndani ya kile chumba, nikapelekwa kwenye mbuga kubwa sana mfano wa jangwa. Nilishangaa sana sababu eneo hilo lipo tofauti kabisa na lile la mwanzo lakini yote kwa yote sikutaka kujaji saana kwa sababu nilijua kwanza sipo duniani kwahiyo mambo hayo inabidi tu niyachukulie kawaida, hivyo pumzi ndefu nilishusha baada kumaliza kuvaa koti langu, punde mwanadada mmoja hivi alinisogelea halafu akaniambia.  
"Unaona hii mbuga! Unatakiwa ukimbie kwa namna uwezavyo, huu ni mchezo mwepesi sana unatakiwa kushinda ili utetee uhai wako" Sauti hiyo ya huyo mwanadada ilipenya vyema masikioni mwangu lakini si kama nilikuwa nasikia sauti ya kike bali sauti niliyokuwa nasikia ilikuwa ya kiume, nene na nzito. 

"Enhee ikawaje sasa maana daah! Mtihani kweli kweli.." Alihoji Millander. Hapo Bingo alishusha pumzi kwanza kisha akaendelea kusimulia.
 
              *********
Firimbi ilipigwa, hapo Bingo akaanza kutimua mbio, ajabu nyuma yake jangwa lile lilikuwa likimomonyoka. Bingo aliposimama aligeuka nyuma, alishtuka kuona jangwa likimomonyoka huku moto nao ukizuka katika shimo hilo, hapo sasa Bingo akaendelea na safari yake ya kukimbia kwa kasi ya ajabu, lakini siku zote mbio za sakafuni huishia ukingoni.. Ndivyo ilivyokuwa kwa kijana Bingo, kwani baada kukimbia kwa muda mrefu hatimaye mbele yake njia mbili tofauti. Njia moja ilielekea kulia na nyingine ilielekea kushoto. Hivyo basi Bingo akaona hapo ndipo pa kuongozwa na ramani lakini alipoingiza mkono mfukoni hakuikuta ramani yake.

"Ramani yangu imepotelea wapi?.." Alijiuliza kijana Bingo baada kujikuta ramani haiko kwenye himaya yake. Muda huo lile jangwa liliendelea kumomonyoka kuelekea pale aliposimama Bingo hali ya kuwa naye akishindwa kuchagua njia ya kwenda sababu palikuwa na njia mbili. Njia moja ilielekea kulia na nyingine ilielekea kushoto, hivyo akawaza endapo kama ramani angelikuwa nayo basi ingemuwea rahisi sana kuamua pakwenda.
"Hapa liwalo na liwe" Alijisemea Bingo ndani ya nafsi yake kisha akatimua mbio kuelekea njia ya kulia, njia ambayo mbele zaidi ilitokomea kwenye msitu mzito wenye miti iliyosheheni miba, wadudu wakali pasipo kusahau wanyama mbali mbali wa mwitu. Hapo sasa Bingo alishusha pumzi ndefu, akakaa kwanza chini wakati huo akitafakari namna ya kufika Tropea ilhali akiwa hana ramani ambayo ingempa muongozo lakini wakati yupo chini mara ghafla aliguswa bega, ambapo alishtuka sana akatoka kwenye dimbwi la mawazo akamgeukia mtu huyo aliyemgusa. Ni mtoto mdogo, mwenye umri wa miaka kumi na mbili, mtoto huyo alimshika Bingo mkono kisha akamvuta pasipo kusema naye neno lolote.

Wawili hao waliambaa msitu kwa msitu mpaka kwenye kilele cha mlima, ambako huko Bingo alipata kuona mto mkubwa mbele yake, na katika mto huo ilionekana boti ndogo ikiwa na watu ndani yake. Bingo aliitazama boti ile kwa dakika kadhaa kisha akarudisha uso wake kumtazama yule bwana mdogo aliyemleta kwenye kilele hicho cha mlima, hapo sasa huyo mtoto alimuonyesha Bingo kiganja chake, ambapo Bingo akapata kuwaona wale watu waliomo ndani ya boti huku mmoja wao akiwa makini kuitazama ramani ya kuelekea Tropea..

"Alaah! Kumbe ramani walibaki nayo pindi waliponivua koti langu? Hapa hakuna kuogopa tena liwalo na liwe" Alijikuta akijisemea hayo Bingo ndani ya nafsi yake mara baada kugundua kuwa ramani ilibaki kwa wale watu waliomuamuru akimbie kwenye jangwa lakini nao vile vile hawakuwa watu wa kawaida. 

"Hahaha hahahaha" Aliangua kicheko bwana mdogo huyo kisha akapotea, Bingo alishtuka ila hakuona haja ya kupoteza muda, haraka sana alishuka kwenye kilele kile cha mlima, kwa kasi ya ajabu akaifuata ile boti ili apate kuichukua ramani yake.

Haikuwa kazi nyepesi lakini mwishowe alipata kufika kwenye huo mto ambapo boti hiyo ilikuwa imesimama huku ndani sherehe mbali mbali iliendelea, hapo sasa Bingo akaizunguka boti, akapita nyuma moja kwa moja akazama mpaka ndani ambapo aliliona sanduku la dhahabu likiwa wazi, na ndani ya sanduku hilo ilikuwemo ramani yake.  

Hakika pumzi ndefu alishusha kijana kisha pasipo kupoteza muda alichukuwa ramani yake akatoka ndani ya boti hilo huku akiwatazama jicho upande watu wale waliokuwa wakisherehekea lakini kabla Bingo hajatoka kabisa, alijigonga kwenye uzio wa boti, kitendo ambacho mkuu wa msafara aliweza kupaza sauti akiwataka watu wake wakae kimya.. 

Muda huo huo Bingo alijitupa ndani ya maji na kisha kuanza kuogelea, watu hao walipomuona, mmoja wao aliingia chumba kile kilicho kuwa na ramani, alishtuka baada kuikosa, akajua dhahiri imechukuliwa na yule mtu aliyeonekana ndani ya maji ambaye ndio Bingo.

Hivyo haraka sana akarudi kwa mkuu wake akamueleza hali halisi. Mkuu huyo akiwa na wingi wa hasira alichomoa upanga wake akamfyekelea kibaraka wake halafu amri ikatoka kwa watu wengine waliosalia, punde si punde walijitupa ndani ya maji hali ya kuwa muda huo Bingo alizidi kuogelea kuufuata mto maji yanako elekea ili apate wepesi wa kuwakimbia wale watu.

Bingo aliogelea kwa nguvu zake zote huku nyuma akifuatiwa na wingi wa maadui, hatimaye alifika kwenye mporomoko mkubwa wa maji, hakuona haja ya kuogopa alijitosa mzima mzima ilihali watu wale waliokuwa wakimfukuza waliogopa kujitosa katika mporomoko huo lakini nguvu ya maji iliweza kuwavuta wakajikuta nao wakiungana na Bingo ndani ya mporomoko huo, vile vile boti nayo ilivutwa hali iliyopelekea Mkuu wa msafara pamoja na vibaraka wake wakateketea ndani namna hiyo ikiwa muda huo Bingo yeye alipoteza fahamu akasombwa na maji ingawa alikwama kwenye mti ambao uliangukia mtoni. 

Pembezo mwa mto huo alionekana Ajuza akipita pita huku akichimba mizizi ya miti, muda huo Bingo alifumbua macho yake akapata kumuona Ajuza huyo. Bingo alitamani sana kumuomba msaada bibi huyo lakini alishindwa sababu hakuwa na sauti wala nguvu ya kujinyanyua pale alipokwama ila mwishowe Ajuza alimuona, hivyo alimfuata akamsaidia kumtoa mahala pale. Ajuza huyo alimpeleka Bingo nyumbani kwake, ambapo huko alimpa dawa mbali mbali zilizo weza kumtibu majeraha na jambo ambalo lilimfurahisha Bingo ni baada Ajuza huyo kuongea lugha ambayo aliielewa.. 

"Pole sana, utapona tu" Alisema Ajuza huyo kwa sauti ya upole Bingo akajibu "Asante sana..! Lakini kuna jambo nataka nikuulize tafadhali.." Aliongeza kusema Bingo. 

"Lipi hilo?.." 

"Hapa ni wapi.." 

"Hapa ni Ambatapra" 

"Ambatapra na Tropea kuna umbali sana?.." 

"Ndio ingawa sio sana, ramani yako ndiyo itakufanya upaone karibu" 

"Unamaana gani?.." Alihoji Bingo, muda huo akijinyanyua kitandani. 

"Maana yangu ni kwamba kama usingekuwa na ramani basi ungefuata mto huu moja kwa moja ungekufikisha Tropea lakini vile vile kwa njia ya mto kwako ingekuwea vigumu sana kukanyaga mji ule sababu kabla hujaingia Tropea kuna ulinzi mkali sana kutokana na hali iliyopo sasa.. "

" Laah! Sawa Asante kwa majibu yako lakini mbali na haya mazungumzo bado nina swali lingine.. "

"Lipi tena?.. "

"Nataka kujua watu mnao ishi huku mmefikaje fikaje?"
 
"Acha maswali yako ya kipuuzi.." Aliwaka Ajuza baada Bingo kumuuliza hilo swali, ni swali ambalo lilimchukiza sana, hapo alinyanyuka akatoka ndani ya chumba hicho alichomlaza Bingo wakati huo Bingo akijutia kuhoji hilo swali.. 

"Nafikiri hali yako imeimarika vyema, sasa unaweza kuendelea na safari yako lakini kabla hujaanza safari, kuna kitu nataka kutoka kwako.." Alisikika akisema Ajuza, mara baada hali ya Bingo kuonekana imekaa sawa. 

"Asante kwa msaada wako,.. Enhe niambie kitu hicho.." Alijibu Bingo huku akimkodolea macho Ajuza.

Kabla Ajuza hajaongeza neno lolote, ghafla katika chumba ambacho mlango wake ulionekana kujazwa na kutu, alitokea binti mlemavu wa mgongo binti huyo alitembea akiwa ameinama ilihali sehemu mbali mbali za mwili wake zilikuwa zikitoa funza na harufu mbaya nayo ikimtoka. 

"Laah!.." Alitaharuki Bingo wakati huo kinywa chake kikiwa kimejaa mate, kichefuchefu nacho kisimuwee mbali. 

Hapo Ajuza alimtazama Bint huyo kisha akarudisha uso wake kumtazama Bingo halafu akamwambia 

"Huyu ni binti yangu, siku ya leo nataka ufanye nae mapenzi kabla hujaondoka, hapo alipo ana miaka zaidi ya hamsini wala hamjui mwanaume, hivyo basi nataka wewe ndio uwe wa kwanza kwake.." Alisema hivyo Ajuza huyo, na safari hii sauti yake ilikuwa ikijirudia mara mbili mbili kama mwangwi huku macho yake nayo yakibadilika rangi..

KABLA YA KUANZA SAFARI, KATIKA MASHARTI ALIYOPEWA NA MZEE NDELO NI KUWA ASIJE AKAFANYA MAPENZI, TUKUTANE KESHO TUJUE ALISALIMIKA VIPI? 

Post a Comment

Previous Post Next Post