SEHEMU YA 26
Kauli ya Madame ilimstua sana Shaymaa na kujikuta akitetemeka akiona dhairi shairi kuwa anaenda kuumbuka.
Kabla Kijana wa Madame hajaenda kufungua kabati walistuka baada ya kusikia mlango unagongwa “Rayuu kipenzi changu” Mzee Mustapha aliita na kufungua mlango kabla hata Shaymaa hajaitika.
“Mungu wangu!” Mzee Mustapha alistuka baada ya kumuona Shaymaa akiwa amepiga magoti huku machozi yakiwa yanamtoka
“Kuna nini kimemkuta Binti yangu? Kwanini amekupigia magoti ulikuwa unamfanya nini? Asia tafadhali usijaribu kumgusa Rayuu wangu. Na wewe kijana unafanya nini humu? Hebu toka haraka” Mzee Mustapha alifoka na kumtimua yule kijana wa Madame
“Kwanini unakuwa hivi lakini? Unapokuta watu wametulia sehemu unapaswa kuuliza kwanza kabla ya kuanza kufoka. Shaymaa aliumwa kichwa ghafla Mimi na kijana wangu yule tulifika kumsaidia” Madame aliongopa huku akimtazama macho makali Shaymaa
Kitendo cha kusikia Shaymaa alikuwa anaumwa ghafla kilimchanganya zaidi Mzee Mustapha aliyekuwa anamuuliza maswali mfululizo Shaymaa “Nini tatizo? Kwanini unawaza sana mpaka unaumwa Mwanangu? Hebu niambie ni kweli unaumwa?”
Shaymaa alimtazama Madame ambae nae alimtazama kwa macho makali, kama Mtu aliyesema kwa macho ole wako uzungumze ukweli utajuta nitakachokufanya.
“ni kweli naumwa Baba, tafadhali naomba mniache kwa dakika kadhaa nipumzike”
Shaymaa aliongea na kuzidi kumchanganya Mzee Mustapha baada ya kumsikia Shaymaa amekiri kwa kinywa chake kuwa alikuwa ni Mgonjwa “Hapana tunapaswa kwenda hospital” Mzee Mustapha aliongea huku akiwa anampima joto lake la mwili.
“Sawa Baba naomba mnipishe nibadili nguo kwanza” Shaymaa aliona hiyo ndio njia pekee ambayo anapaswa kuitumia ili kumuokoa Liyuna.
“Nikiwa kama Mama yako, napaswa kukuchagulia nguo Mwanangu kipenzi. Mustapha naomba utupishe Mtoto avae” Madame aliongea huku akiwa anatabasam akimtazama Shaymaa akimaanisha kuwa ni lazima atajua tu Liyuna yupo ndani au lah!
******
Irina aliongea mambo mengi ya uongo kuhusu Shaymaa kiasi ambacho Hakeem alitokea kumchukia sana Shaymaa kutokana na sumu aliyokuwa akilishwa na Irina. {Hapo unajifunza usipende sana kuamini vitu vya kuambiwa, penda sana kuthibitisha Mwenyewe kuliko kuchukua maamuzi kwa maneno ya kuambiwa}
“Kumbe ndio mana amefika pale akaanza kunitolea macho Mimi ili nimuoe!! Ukimtazama alivyo unaweza kuhisi ni Mwanamke bora kumbe wapi? Hawezi kunipata na hatofanikiwa katika upuuzi wake hata mara moja”
Hakeem alionekana kuamini habari za uongo ambazo aliongea Irina kuhusu Shaymaa “Mimi nakwambia unapaswa umfanye aumie, la sivyo atakuumiza wewe na Familia yako kama vile alivyomuumiza Mume wangu”
Irina alipigilia msumari wa moto kusisitiza ili Shaymaa afukuzwe kwa kina Hakeem na azidi kutanga na Dunia. Furaha yake ilikuwa ni kumuona Shaymaa akipata tabu tu na si vinginevyo
“Alafu kuna kitu nimekumbuka, nilikuwa naomba msaada wako kama hautojali” Hakeem aliongea na Irina alikaa sawa kumsikiliza “Nilikuwa nataka ukae na Mpenzi wangu kwa siku kadhaa”
Hakeem aliongea na kitendo cha kusema ana Mpenzi kilimchanganya kidogo Irina na hakutegemea kama Hakeem angekuwa na Mwanamke “Nilitaka kushangaa, Mwanaume Mtanashati kama wewe unakosaje kuwa na Mwanamke? Ama kweli ni ngumu kumkuta Mwanaume bora akiwa mtaani anatangatanga” Irina aliongea huku akiwa anaonekana kukata tamaa “Mimi nafikiri hata Mwanamke bora uwezi kumkuta mtaani akiwa anatangatanga labda hawe ameumizwa na akate tamaa ya kupenda” Hakeem alichagiza na wote walifurahi
“Sasa kwanini nikae na Mpenzi wako badala Mfunge ndoa?” Irina alimuuliza huku akionekana kutopendezwa na kitendo cha Hakeem kuwa na Mpenzi
Hakeem alimsimulia kila kitu Irina kuhusu Liyuna na Irina alimuelewa na kumwambia kuwa yupo tayari kumsaidia.
“Asante sana itabidi nimpigie ili nipange mipango ya kumtorosha pasipo Mtu yoyote kutambua jambo hilo. Nilitamani kumpangia nyumba ila kutokana na hali yake nahitaji hawe katika hali ya uangalizi zaidi”
Hakeem aliongea huku akichukua simu yake na kutafuta namba ya Liyuna
*******
Mzee Mustapha alimtazama Shaymaa na kugundua kuwa hajafuraishwa na kitendo cha Madame kutaka kubaki chumbani ili amchagulie nguo ya kuvaa Shaymaa
“Shaymaa ana uhuru wa kuchagua nguo aitakayo tafdahali hebu mpe uhuru Mtoto bwana” Mzee Mustapha alimshika mkono mkewe ili watoke nje na hapo Madame hakuwa na mbinu nyingine. Ile wanatoka tu simu ya Liyuna ilikuwa inaita Shaymaa aliichukua na kuipokea “Utanipigia baadae tafadhali”
Madame aligeuka na kumtazama Shaymaa na kuhisi kitu kisha akatulia, lakini hakutaka kuongea chochote badala yake walitoka nje na Mumewe.
Shaymaa aliufunga mlango kwa ndani kisha alimfungulia Liyuna aliyekuwa tayari ameshaanza kuishiwa pumzi
“Madame ameshajua kila kitu kama hupo humu chumbani hivyo kivyovyote atahitaji kuthibitisha kama kweli hupo humu au lah”
Shaymaa alimwambia Liyuna aliyekuwa anaogopa huku akimuomba Shaymaa amsaidie “Wala usijali nitajitahidi kadri ya uwezo wangu ila cha msingi unapaswa kuwa Jasiri tu” Shaymaa aliongea na kuonekana akitafakari na kutafuta wapi anaweza kumtoroshea Liyuna “Asante sana, umekubali kupigwa kwa ajili yangu akika nimejifunza kitu kutoka kwako” Liyuna alimwambia Shaymaa ambae alimsihi anyamaze “Wala upaswi kunishukuru, Mungu hakufanya makosa kukusukuma uje kwangu nikusaidi. Hakika alijua fika kuwa Mimi ni Mtu sahihi” Shaymaa aliongea na kumfanya Liyuna ashushe pumzi na kumtazama akishindwa kummaliza
*****
Kitendo cha Shaymaa kupokea simu ya Hakeem kilimchanganya kidogo Hakeem na aliweza kutambua kuwa aliyekuwa amepokea simu ya Mpenzi wake ni Shaymaa na siyo Liyuna. Alipiga tena na simu ilikuwa haipatikani “shaymaa amepokea simu ya mpenzi wangu na kuniambia nitampigia baadae, na sasa napiga namba ya Liyuna naambiwa haipatikani Sasa sijui kutakuwa na nini?”
Hakeem aliongea na kumshangaza Irina na hakutaka kumpa nafasi kwani alitumia tena fursa hiyo kumkandamiza Shaymaa “Kama Mpenzi wako ameungana na Shaymaa basi kaa ukijua kuwa atakuwa amekwisha kwani Shaymaa atatumia nafasi hiyo kumrubuni ili kuwatapeli zaidi”
Hakeem alichukia zaidi baada ya kusikia maneno hayo na kujikuta akipiga meza kwa hasira “Tunaweza kwenda wote nyumbani kwetu?” Hakeem aliuliza na hilo ndio swali ambalo Irina alikuwa kama analisubiria
“Sawa hakuna shida mpenzi ni wewe tu” Irina aliongea na Hakeem alimwambia kuwa anahisi kuna hatari inamkuta Liyuna hivyo kama inawezekana wafanye haraka.
Walikubaliana watumie gari ya Hakeem, waliingia kwenye gari na kabla hawajafanya chochote, kioo cha upande wa Irina mtu aligonga kwa mkono akiitaji afunguliwe na alipomtazama hakuwa mwengine alikuwa ni Jack
“Unatamani kuwa na kila Kijana Mtanashati katika Mji huu? Hivi haujui ni jinsi gani nampenda Hakeem?” jack alimuuliza Rafiki yake baada ya kutoka pembeni kwenda kuzungumza
“Hapana Jack, Mimi wala sina nia na Hakeem wako, ila Shaymaa yupo kwenye jumba la kina Hakeem na analazimisha kuolewa na Hakeem ndio nachochea utambi ili atimuliwe. Nafanya yote haya kwa ajili yako ili kukutengenezea njia ya kumpata Hakeem”
Irina alimwambia Jack kisha alimsimulia kila kitu kuhusu hakeem kuwa Baba yake tajiri mpaka Hakeem alivyomuomba kuishi na Mwanamke wake ambae Mama yake hamtaki
Maongezi yalikatishwa na honi iliyopigwa na Hakeem baada ya kuona wanachelewa “Twende wote basi na Mimi nikapaone ukweni” Jack aliongea na wote walifurahi “Twende tukaongee nae hawezi kukataa kitu mbele yako”
“Hakeem tunaweza kwenda na Jack?” Irina aliuliza na Hakeem hakuwa na kipingamizi na waliingia kwenye gari ya Hakeem na kuelekea nyumbani kwa kina Hakeem.
Walijuta kupanda gari ya Hakeem kwa huo Mwendo aliokuwa anatembea “PUnguza Mwendo Mpenzi” Jack aliongea akijipendekeza huku akiwa anamfinya Irina “Mbona hapa naendesha kistaarabu kwa ajili yenu” Hakeem alijibu na kukanyaga mafuta zaidi huku Jack na Irina wakipaza sauti
******
Baada ya kuwaza na kuwazua atimaye Shaymaa aliweza kupata jibu. Haraka alikimbilia bafuni na kufungua dirisha la bafuni na kuona ukingo ambao Mtu anaweza kusimama bila tabu yoyote.
“Utatoka kupitia dirisha la bafuni na utajibanza kwenye ukingo wa ukuta huo, akikisha unakaa huko hata nusu saa kwani muda mfupi baada ya Mimi na Mzee kuondoka ni lazima Madame atakuja kukagua humu kama hupo au lah!!”
Shaymaa aliongea kwa tahadhali ili Madame hasije kumsikia kwani alihisi atakuwa yupo nje ya mlango akimsubiri
Liyuna alifanya kama ambavyo Shaymaa alimuagiza kisha shaymaa alirejesha kioo vyema na kuacha nafasi ambayo Liyuna akitaka kurudi ndani hawe na uwezo wa kufungua dirisha
Baada ya hapo Shaymaa alioga na kujiandaa haraka na kufungua mlango na kweli alimkuta Mzee Mustapha na Madame wakiwa nje wakimsubiri
Shaymaa kwakuwa aliambiwa kuwa anaumwa na yeye aliona ni bora aigize kuwa anaumwa. Alijifanya kutetemeka kiasi ambacho hata Mzee alimuonea huruma na kuagiza watu wamsaidie kutoka “Subiri kwanza Mtoto anasikia baridi”
Madame alitumia Mwanya huo ili aingie tu chumbani kwenda kuakikisha kama Liyuna yupo chumbani au lah!! Shaymaa alistuka na kumtazama “Mama hapana tu wala usijali” Shaymaa alijaribu kumtuliza lakini wapi Madame alikuwa amedhamiria na alionesha upendo wa unafki mbele ya Mzee “Siwezi kukuona Mwanangu unapelekwa hospital ukiwa hivyo. Nguo uliyovaa inakufanya uhisi baridi unapaswa kupata jacket” Madame alimjibu na kuingia chumbani
Alifika mpaka chumbani na cha kwanza tu alifungua kabati na kutazama lakini hakumuona Liyuna na kujikuta akisonya kwa hasira. Aliingia bafuni kutazama ilikuwa ni bure, alirudi na kutazama ilikuwa ni bure
“Jacket hakuna?” Mzee Mustapha aliuliza kwa sauti yake kavu iliyokuwa na mikwaruzo “Nimeshapata” Madame alijibu na kutoka na Jacket na kumvisha Shaymaa
“Tafadhali muaishe Mwanangu hospital” Madame aliongea huku akiwatazama kwa zamu Mzee Mustapha na Shaymaa
******
Shaymaa akiwa ameshikwa na Wasaidizi akitolewa ndani ili apakizwe kwenye gari Hakeem nae alikuwa amefunguliwa geti na kuingia ndani na kugesha gari yake kwa kasi kiasi ambacho aliwastua wote waliokuwa pale
“Baba subiriiii!!” Alipaza sauti na wote walisimama wakisubiri kuona Hakeem anataka kufanya nini.
Wakati huo huo Irina na Jack waliteremka kutoka kwenye gari huku wakiwa wamemkazia macho Shaymaa ambae alipatwa na Mstuko baada ya kumuona Irina amekuja katika jumba hilo la Mzee Mustapha
“Mnafki Mkubwa wewe!! Hivi unafikiri unaweza kukimbia kimvuli chako milele?” Hakeem alimtazama Shaymaa na kumuuliza Huku Irina na Jack wakimtazama kwa kejeli ……………………
NINI KITAENDELEA? IRINA NA JACK WATAFANYA NINI MBELE YA MZEE MUSTAPHA? VIPI KUHUSU LIYUNA ATAFANIKIWA KUTOROKA? SEHEMU YA 27 ITAKUWA NA MAJIBU. KUMBUKA KUWA TUMEBAKIZA EPISODE 3 KUMALIZA MSIMU WA KWANZA WA MAUMIVU YA NDOA
MAUMIVU YA NDOA
SEHEMU YA 27
MTUNZI: Abdulkarim Dee
Shaymaa Alimtazama Hakeem, kisha aliwatazama kina Irina na kushusha pumzi pasipo kuongea chochote
“Unajisikia aibu baada ya kuona nimegundua ukweli wako?” Hakeem alimuuliza na Shaymaa alishindwa kujizuia na kujikuta akimuuliza swali “ukweli gani ambao wewe unaujua kuhusu Mimi?” “Ulidhani unaweza kuficha uongo wako milele? Baba huyu Binti ni Jambazi ambae anatumia Mwili wake kuwalaghai Wanaume kisha anawaibia”
Hakeem aliongea kwa hasira huku akiwa amemtolea macho Shaymaa aliyeonekana kustushwa na kauli hiyo ya kuitwa Changudoa anaetumia Mwili wake kuwalaghai Wanaume. Mzee Mustapha alionekana kustuka na kumtazama kwa makini Hakeem kabla ya kugeuka na kumtazama Shaymaa ambae pia alimtazama na kujikuta akikosa cha kuongea
******
Baada ya kuona Shaymaa na Mzee Mustapha wameondoka. Madame hakujua kama walikuwa hapo nje wanaongea na Hakeem aliyekuwa amerejea akiwa na Irina na Jack.
Alifungua chumba cha Shaymaa na kuingia kwenda kuchunguza kama kweli Liyuna hakuwepo chumbani au kuna mchezo alijaribu kucheza yeye na Shaymaa. Alifika na kuufungua mlango kwa tahadhaari na kuufunga taratibu.
Liyuna akiwa kwenye kingo ya ukuta aliweza kuusikia mlango ukifunguliwa na kufungwa na alijua fika atakuwa ni Madame ndie aliyekuwa ameingia
“Liyunaa!!” Madame aliita huku akiwa anaangaza kila upande “Huna haja ya kujificha Mkwe wangu kipenzi hebu njoo tuongee” Madame alimuita na kuongea kwa upendo akijifanya kama anampenda kweli.
Liyuna akiwa amejificha aliweza kumsikia Madame na kujikuta akiziba Mdomo akihofia hasije kusikika
“Mwanangu kipenzi, wala hupaswi kuwa na hofu ukiwa katika tumbo la Mama yako, tunaye Mungu wetu aliye hai ndio tunamtegemea kwa kila jambo”
Masikini Liyuna aliongea moyoni huku akiwa ameshika tumbo lake akiamini kwa kufanya hivyo kutamfanya kijana wake aliyekuwa tumboni kutokuwa na hofu yoyote kuhusu kifo chao.
Madame aliita na kumtafuta kila kona lakini hakuweza kumuona Liyuna, baadae aliingia bafuni na kuangaza kila upande.
“Liyunaaaa!! Najua kama bado hupo humu wala usijali wewe jitokeze tu Binti yangu”
Madame aliongea na Liyuna alizidi kuogopa na kutetemeka na kutamani hata kujirusha ili afe kuliko kuingia katika mikono ya Mama yake Hakeem
Baada ya kuona kimya Madame alisonya na kuchukia Mwenyewe “Liyuna najua umetoroka nitakukamata kwa mikono yangu tu wala huwezi kufika ppote nitakukamata haraka sana”
Aliongea na kutoka kwa hasira na kuubamiza mlango. Liyuna alishusha pumzi na kujikuta akitabasam baada ya kusikia Madame ametoka nje. Alifungua kioo taratibu na kurudi bafuni kisha akarejesha kioo kama kilivyokuwa na kurudi chumbani kwa taadhari
Ghala alistuka baada ya kusikia anapigiwa makofi. Hakuwa Mwengine bali alikuwa ni Madame ndie aliyekuwa anampigia makofi.
Ilikuaje mpaka Madame akabaki chumbani wakati Liyuna alimsikia kama ameufungua mlango na akatoka nje?
Madame alipoingia bafuni aliona dirisha la kioo halikufungwa vizuri na alipotazama kwenye sink aliona harama ya mguu imekanyaga hapo hivyo alijua tu Liyuna anaweza kuwa amejificha hapo
Alijifanya kuchukia kumpa ishara Liyuna ili atambue kuwa anatoka nje kisha akaondoka, alifika mpaka mlangoni na kuufungua mlango na kuubamiza kisha yeye akabaki ndani na kujibanza kwenye kabati.
Liyuna alivyosikia mlango umebamizwa alijua bila shaka Madame atakuwa ametoka nje, kumbe wapi alijikuta anaingia mtegoni bila kutarajia
“Tafadhali naomba usiniuwe, Nina Mtoto wa mwanao kwenye tumbo langu” Liyuna aliongea na Madame alimnyamazisha asiendelee kuongea kisha akachukua simu yake na kuipiga namba fulani na kumwambia Mtu kuwa unaweza kuja. Baada ya kuongea hivyo taratibbu alikuwa akipiga hatua akijongea alipo Liyuna huku Liyuna akiwa anatetemeka kwa uoga
“Hiyo damu iliyo tumboni mwako ndio Damu ambayo inakufanya wewe utoweke katika ulimwengu huu. Lakini una dakika kadhaa za kukomboa maisha yako endapo utafanikiwa kujibu maswali yangu ipasavyo”
Madame aliongea huku akiwa anatabasam kabla ya kubadlisha tabasam lake na kumtazama kwa jicho fulani lenye kumaanisha “Unayajua maua pori?” Madame alimuuliza huku akimtazama. Liyuna alimjibu kwa kuitikia na kichwa akimaanisha kuwa anayajua huku wakati huo machozi yakimtoka na akiwa anaogopa akijua tayari amekwisha
“Mwaanamke wa shoka siku zote huwa halii pindi anapokuwa katika wakati mgumu, bali utabasam na kupambana wakati wote. Huwezi kumpata Mwanangu kama huwezi kuwa Jasiri. Hebu niambie unavyozani maua pori yanapaswa kuota wapi?” “yanapaswa kuota porini” Liyuna alijikaza na Madame alimpigia makofi “Safi sana umepatia swali la kwanza na umejitengenezea mazingira mazuri ya kuokoa maisha yako. Maua Pori yanapoota nyumbani na kuchanganyika na Maua mengine ya kawaida, unadhani nini kinapaswa kifanyike?”
Madame aliuliza na safari hii Liyuna alitafakari kidogo kabla ya kujibu swali hilo “Yanapaswa kung’olewa ili kuyaacha maua alisi yastawi vyema” Liyuna alijibu na Madame alimpigia makofi tena na kuonekana kufuraishwa na jibu hilo
“Sasa wewe una tofauti gani na maua pori? Unapaswa ung’olewe ili Sisi ambao ni Maua alisi tustawi vyema kabisa”
Madame aliongea na kumfanya Liyuna aishiwe nguvu zaidi na kujikuta akianguka na kufikia magoti. Madame alimtazama na kusikitika akijifanya kumuonea huruma kisha akamsimulia hadithi kuhusu yeye
“Miaka kadhaa iliyopita nilikuwa kijakazi kama wewe ulivyo Kijakazi katika Jumba hili la Mzee Mustapha. Binafsi nilitokea kumpenda sana Boss wangu lakini kwa bahati mbaya Boss alitokea sana kumpenda Rafiki yangu”
Madame aliendelea kumsimulia jinsi alivyopambana kuweza kumpata Boss wake lakini ilikuwa ngumu kwani Boss wake hakuwahi kumpeda kimapenzi kama ambavyo alivyompenda rafiki yake “Rafiki yangu alipewa Mimba na kutoroshwa kwa siri katika jumba hili na Mimi ndie niliyekuwa nikimsaidia kwa kila kitu. Lakini Baadae niliweza kumsaliti Rafiki yangu, nilimuua kwa maslahi yangu binafsi. Nilifanya yote kwa faida yangu Mimi na Mtoto wangu ambae ndio wewe unaempenda. Sasa siwezi kukubali kuona Mwanagu anakuja kuzaa na Kijakazi masikini kama wewe ikiwa bado nina malengo yangu”
Madame aliongea na muda huo yule kijana aliweza kuingia na Liyuna alipomuona yule kijana alimuwahi Madame na kumkunja koti lake huku akijaribu kupiga kelele ila yule kijana alimuwahi na kumziba mdomo kwa kutumia kitambaa kilichokuwa na madawa huku akiwa anamvuta amuachie Madame
Liyuna alikuwa anakukuruka huku akiwa bado ameshikilia koti la Madame ipasavyo na Kijana alitumia nguvu kumvuta mpaka Liyuna aliondoka na kishikizo cha koti la Madame pasipo Madame kujua
******
“Shaymaa alimtazama Hakeem kisha akajikuta tu anafurahi “Kwa bahati mbaya sana uongo huwa unakubalika kwa haraka zaidi ila cha ajabu huwa haudumu, ila ukweli huwa unachelewa kukubalika na unapokubalika huwa unadumu. Ndio maana wengi wetu huwa tunakuja kuwatambua Watu wakweli pale ambapo tunapokuwa tumewapoteza. Sina cha kukujibu chochote kati ya hayo uliyoongea, ila si unakumbuka kama nilipokea simu yako ambayo haukuwa umenipigia Mimi?”
Shaymaa alimaliza kwa kumuuliza kisha alijongea na kumsogelea sikioni na kumnong’oneza kitu Hakeem aliyeonekana kustuka na kumtazama “Unasemaje wewe? Yani Liyunaaa … anaaaa??” Hakeem alistuka na kushindwa kuongea na kujikuta akikurupuka mbio kukimbilia ndani
Mzee Mustapha alimtazama Hakeem na kujikuta akishangaa “Rayuu kuna nini kinaendelea Mwanangu baina yako na Mwenzio?” Alimuuliza swali ambalo Irina na Jack walishangaa kumuona Mzee Mustapha anamuita Shaymaa Rayuu, tena kwa kumuita Binti yake
“Baba naomba unipeleke hospital naijisikia vibaya” Shaymaa alijibu na haraka alipakizwa kwenye gari ya Baba yake kwa kusaidiwa na Wafanya kazi huku akiwatazama kina Irina walivyokuwa wameduwaa baada ya kumuona Shaymaa akipewa usaidizi wa namna hiyo
******
Hakeem alikimbia akiwa anapandisha Juu huku akwa anahema na kukumbuka maneno ya Shaymaa “Mpenzi wako anataka kuuwawa. Nenda chumbani kwangu, fungua dirisha la bafuni utamkuta kwenye ukingo wa ukuta, fanya haraka anahitaji msaada”
Hakeem alikumbuka kauli ambayo Shaymaa alimwambia sikioni na kujikuta akipata nguvu zaidi ya kukimbia.
Alifika kwenye chumba cha Shaymaa na alifungua mlango kwa nguvu pasipo kubisha hodi na alipatwa na mstuko wa ghafla na kuishia kuduwaa ………………
NINI KITAENDELEA? USIKOSE SEHEMU YA 28.
MAUMIVU YA NDOA
SEHEMU YA 28
MTUNZI: Abdulkarim Dee
Ilikuwa ni habari ambayo iliweza kumstua sana Hakeem hivyo aliweza kutoka mbio na kuwahi chumbani kwa Shaymaa kuona kama anaweza kujaribu kumuokoa Mpenzi wake
Alifika na kujaribu kufungua mlango ambao ulionekana kuwa ulikuwa umeegeshwa. Alifungua mlango na kupatwa na mstuko baada ya kuona chumbani kwa Shaymaa vitu vikiwa vimevulugika utafikiri Watu walikuwa wanagombana.
Hofu ilitanda na moyo ulshikwa na wasiwasi akiamini kuwa uenda kuna jambo baya litakuwa limemfika Liyuna.
Aliingia taratibu chumbani huku akiwa na taadhari huku akijaribu kumuita Liyuna. Alifika mpaka kule ambapo Shaymaa alimuelekeza lakini wapi hakuweza kumkuta Liyuna.
Hakeem alizidi kuchanganyikiwa na kupekua kila mahara huku akimuita Mpenzi wake lakini wapi Liyuna hakuwemo katika chumba hicho “Inamaana yule Mpuuzi amecheza na akili yangu?” Hakeem alijiuliza mwenyewe huku akitafakari maneno ya Shaymaa na kujiuliza kwanini Shaymaa aliamua kuongea maneno kama yale
“Inamaana ile ilikuwa ni mbinu ya kunitoa pale kwa Mzee? Kama hausiki kwanini alipokea simu ya Liyuna? Inamaana alikuwa na Liyuna wakati napiga simu?”
Hakeem hakuweza kupata jibu sahihi kuhusu Shaymaa na kadri alivyokuwa anatafakari ndivyo alivyomtilia shaka zaidi Shaymaa
Aliamua kutoka nje na wakati anapiga hatua kuelekea nje, alisita baada ya kuona kitu aligeuka na kutazama
Aliona kitu kama simu, alisogea na kufunua shuka ni kweli ilikuwa simu. Aliitazama simu na kujikuta anakumbuka kitu
“Sina kitu kikubwa cha kukupa katika sherehe yako hii ya kuzaliwa zaidi ya viatu”
Hakeem alimwambia Liyuna na kumpa viatu ambavyo vilionekana kuwa chakavu na kumfanya atabasam “Ujavipenda?” Hakeem alimuluuliza na Liyuna alijibu kuwa amevipenda huku akiwa anafurahi.
“Ingiza mkono kwenye hivyo viatu” Hakeem alimwambia na Liyuna alimtazama na kuingiza huku akiwa na Shauku akitaka kujua kuna nini? Aliingiza mkono na kutoa simu. Liyuna alifurahi na kumkumbatia Hakeem “Nafikiri hii itakusaidia kuwasiliana na Mimi”
Baada ya kuongea hivyo Hakeem alitoka kwenye mawazo na kuiwasha simu ya Liyuna, alishangaa baada kuona simu ya Liyuna ilikuwa imejaa chaji “Inamaana Shaymaa aliizima hii simu ya Mpenzi wangu muda mfupi tu baada ya Mimi kumpigia?” Hakeem aliongea mwenyewe na kuonekana kuwa na mashaka na Shaymaa “Bila shaka Shaymaa atakuwa anajua kila kitu kuhusu Liyuna wangu? Kwa nini alipokea simu yake kisha akaizima?”
Hasira zilimpanda Hakeem na kuamua kutoka nje haraka kumuwahi Shaymaa ili ajibu maswali yake aliyokuwa anajiuliza muda mfupi baada ya kuokota simu ya Mpenzi wake chumbani kwake
“Yupo wapi yule mpuuzi nauliza ypo wapi?” Hakeem alitoka na kuwauliza kwa hasira Irina na Jack waliokuwa wanamsubiri
Irina na Jack walitazamana na Jack alikuwa wa kwanza kujibu “Ameondoka na Baba yake” “Hapana usiseme hivyo, yule hawezi kuwa ndugu yangu. Nitamfanya kitu kibaya endapo nitagundua amemfanya kitu kibaya Liyuna wangu”
Hakeem alijibu kwa hasira huku Madame akiwa amejibanza sehemu kusikiliza “Inamaana Shaymaa ameshatoboa siri hii kwa Hakeem si ndio? Pole sana Shaymaa mana nilikuambia usijaribu kuingia kwenye hii vita, nitakufanya kitu kibaya sana”
Madame aliongea mwenyewe huku akimtazama Hakeem na watu wake wakiingia kwenye gari na kutoka kwa kasi kama kuna kitu walikuwa wanawahi
******
Safari ya kuelekea hospital ilikuwa inasonga mbele huku ukimya ukiwa umetawala na Mzee Mustapha akionekana kuguswa na kauli za Hakeem ambazo alimwambia Shaymaa mbele yake
“Shaymaa” Mzee Mustapha alimuita Binti yake na Shaymaa aligeuka na kuitika kwa upole zaidi “Unaweza kuniambia ukweli?”
Mzee Mustpaha aliongea na safari hii swali lake lilionesha kumshangaza kidogo Shaymaa “Ukweli hupi huo Baba?”
Shaymaa alijibu na Mzee Mustapha alitaka kujua kama yeye na Hakeem walikuwa wakifahamiana hapo kabla au lah? Lakini pia alikuwa anataka kujua nini kilikuwa kinaendelea wakati alipomkuta Madame yupo chumbani kwake na yeye amepigia magoti Madame huku akionekana kuwa analia.
“Nikweli nilikuwa naumwa Baba” Shaymaa alistuka na kuogopa na kujikuta akishindwa kusema ukweli
“Macho yako yanaonesha dhairi kuna jambo unajaribu kunidanganya huku ukionekana kuwa wewe siyo bingwa wa mambo hayo. Nafikiri ni ngumu kumkuta mgonjwa akiwa amepigishwa magoti huku akiwa analia. Nilifika pale dakika kadhaa nyuma kabla ya kubisha hodi, najua kuwa huna unachoumwa Binti yangu. Hii ndio nafasi yako, tafadhali naomba uitumie vyema”
Mzee Mustapha aliongea na kumfanya Shaymaa hakose cha kujibu na kujikuta akitetemeka na kuwa na hofu. Aliogopa kusema ukweli kwa sababu alihofia maisha yake.
“Baba samahani tunaweza kuzungumza Mimi na Wewe Binafsi” Shaymaa alifikiria na kuongea na Mzee Mustapha alionekana kutabasam kidogo “Bila shaka tunaweza, lakini vipi kuhusu hali yako inakuruhusu?” Mzee Mustapha alimuuliza na Shaymaa alimtoa hofu na kumwambia kuwa haumwi
Walitafuta sehemu moja tulivu na kukaa walau kupata juice ili wazungumze kwa kina.
*****
“Unajua bado sijapata majibu kuhusu wewe? Hiyo gari umevutiwa nayo au lah?’ Madame alikuwa chumbani kwake akiongea kupitia simu na Mwanae “Mama niache kwanza kuna kazi maalum ambayo nahitaji kuikamilisha. Yani nyie mmempokea jambazi alafu hamjui kitu”
Hakeem aliongea na Madame alionekana kustuka kutokana na kauli ya Mwanae na kumtaka kumjua huyo Jambazi.
Hakeem alimueleza kila kitu Mama yake kuhusu Shaymaa kama vile ambavyo yeye alivyodanganywa na Irina na Madame alijifanya kushangaa huku uso wake ukiwa umetawaliwa na furaha.
“Shaymaa ameingiza Mtu ambae amemteka Liyuna na sijui ana mpango gani na jambo ambalo anataka kulifanya kupitia Liyuna, hivyo naomba uniache kwanza nitakujuza”
Hakeem aliongea na kukata simu huku Madame akionekana akifurahi zaidi “Ukiona panafuka moshi basi kaa ukijua kuwa moto unakaribia kuwaka” Madame aliongea mwenyewe na kuzidi kufurahi kabla ya kunyamaza baada ya kusikia Mtu akibisha hodi
“Kila kitu kimeenda sawa?” Madame alimuuliza Kijana wake baada ya kumkaribisha ndani kwake. “Nimeshafua nguo ila tatizo nimekosa kwa kumwaga mapovu baada ya kufua zile nguo” Yule kijana aliongea na kumfanya Madame afurahi baada ya kuskia nguo zimefuliwa.
“Lazima tumuoneshe kuwa yeye ni mchafu na hastahili kuishi hapa, Nenda kamwage mapovu kwenye chumba cha Shaymaa”
Madame alimpa maagizo na yule kija alionekana kutihi kama ambavyo madame alivomuagiza na madame alionekana kufurahia kile ambacho kimetokea na kuona mipango yake imeenda kama ambavyo alivyokuwa amepanga. Alichukua simu ya mezani na kupiga sehemu
“Othman kahawa tafadhali” Alionekana akiomba kahawa kutoka kwa mpishi Mkuu huku akisubiri matokeo kwa kile ambacho amekitengeneza na kuamini kitampa matokeo kwa muda mfupi zaidi.
*****
Mzee Mustapha alimtazama Shaymaa pindi alivyokuwa anakunywa juice na kujikuta akitabasam mwenyewe “Shaymaa wewe ni Rayuu uliyerudi kivingine kabisa. Ndio maana napenda sana kukuita Rayuu kwa maana mnafanana sana na Binti yangu, tofauti yako na Binti yangu ni wewe mpole na mkarim lakini Rayuu alikuwa ni mkrofi hasiyejua kuishi vyema na watu ila nilimpenda sana”
Mzee Mustapha alimwambia Shaymaa ambae alionekana kufuraishwa na kauli hiyo aliyoisikia. “Baba Mimi ni Mwanao, alafu Mungu amenileta kwako kuja kuokoa maisha yako”
Shaymaa aliongea kwa utulivu huku Mzee Mustapha akiwa makini kumsikiliza “Nilikuwa naomba nikuulize maswali kadhaa kama hautojali” “Kuwa huru Mwanangu nipo kwa ajili yako”
Mzee Mustapha aliongea na kumfanya Shaymaa atafakari kidogo kabla ya kumuuliza “Unaweza kuniambia kuhusu Hakeem na Rayuu ni Mama Mmoja au lah!”
Lilikuwa ni swali gumu kidogo kuweza kujibu lakini Mzee alijikaza na kumjibu kama Mwanaume “Rayuu na Hakeem ni Mama tofauti ila wote ni watoto wangu” Mzee alijibu na Shaymaa alijkuta akipata ukakasi kidogo kuhusu jibu la Mzee kwani kwa taharifa ambazo alipewa na Liyuna kuwa Hakeem si Mtoto wa Mzee Mustapha
“Baba, nimejitolea maisha yangu kwa ajili yako. Hata kama nitakuja kufa nitaakikisha nakufa nikiwa nimekuacha salama” Shaymaa aliongea na kumstua Mzee kutokana na kauli yake “kwanini unasema hivyo tena?”
“Mkeo si Mtu mzuri kwako, anaandaa mipango maalum ya kukuua, kila siku unapewa chai maalum ambayo itaondoa uhai wako baada ya siku 90 hivyo naomba kuanzia sasa uweke sheria maalum ya kutaka chakula chako niandae Mimi. Na ningependa haya tuliyoyaongea usimwambie Mtu mwengine yoyote mapaka pale nitakapopata ushahidi zaidi. Pia anza kufanya uchunguzi binafsi utagundua kitu”
Shaymaa aliongea na kumstua Mzee ambae alionekana kustushwa na taharifa hiyo “Inamaana ile chai ninayoandaliwa ili kutibu tatizo langu la upumuaji ndio chai ambayo inatengenezwa kuchukua uhai wangu?” Mzee Mustapha aliongea na Shaymaa alimjibu ndio.
Shaymaa alimwambia Mzee kila kitu kuhusu ndoa yake mpaka jinsi Irina alivyoweza kumchukua Mumewe na yeye kwenda kuishi kwa shangazi yake.
Alimwambia mateso aliyokuwa anakutana nayo kwa shangazi mpaka pale ambapo aliamua kwenda kujiua na kwa bahati aliweza kuokolewa na Mzee Mustapha.
“Mmoja kati ya wale Mabinti ambao alikuja nao Hakeem ndie aliyenichukulia Mume wangu hivyo anatumia fursa hiyo kunichafua kwa Hakeem. Nahisi furaha yake ni kuniona naumia zaidi”
Mzee Mustapha alimuelewa sana Shaymaa na kuomba msaada wake wa kumnasua katika lindi hilo “Nipo tayari kwa ajili yako lakini nilikuwa naomba niende nikaione familia yangu, najua itakuwa na hofu dhidi yangu kutokana na barua ya mwisho niliyokuwa nimeiandika” Shaymaa aliongea na Mzee Mustapha hakuwa na pingamizi na walikubaliana waende pamoja nyumbani kwa kina Shaymaa ili Mzee akajitambulishe kama yeye ndie Mtu anaeishi nae kwa sasa
*****
Hali ya Mjomba ilikuwa inaanza kutengemaa na alikuwa ameanza kufanya mazoezi mepesi kwa msaada wa Mke wake.
Akiwa amekaa kibarazani kwake akisikiliza redio na kupata habari za Nchi zinavyoenda hususani Msiba wa aliyekuwa Rais kipenzi cha Watanzania. Ghafla gari mbili za kifahari ziliingia na kupaki.
Shangazi ndie aliyekuwa wa kwanza kupata mstuko baada ya Kumuona Shaymaa akishuka “Shaymaa!!!” Shangazi aliuliza na kujikuta akishangaa.
Mjomba alistuka na kupata nguvu za ajabu baada ya kusikia jina la Binti yake lakini ghafla alipatwa na Mstuko zaidi baada ya kumuona Mzee Mustapha.
Mjomba alistuka na kutetemeka na kuita jina la Mustapha? Mzee Mustapha nae alishangazwa na kumuita “Majaliwa?” Shaymaa alijikuta akishangazwa na kuuliza “Inamaana Mjomba na Baba Mnajuana?” seas
NINI KITAENDELEA? MAPOVU GANI WALIYOENDA KUMWAGA CHUMBANI KWA SHAYMAA? VIPI KUHUSU MZEE MUSTAPHA NA MJOMBA? EPISODE YA 29 ITAKUWA NA MAJIBU
MAUMIVU YA NDOA
SEHEMU YA 29
MTUNZI: Abdulkarim Dee
Ilikuwa ni ngumu kujibu swali la Shaymaa kwani kila mmoja alijikuta akipatwa na kigugumizi kabla ya wote kujikuta wakijibu kwa pamoja “Tufahamiana!!”
Shaymaa alishusha pumzi na kuziachia kwa mkupuo kabla ya kupiga goti kumuangukia Mjomba kwa kile ambacho alitka kukifanya, cha kuondoa uhai wake
Mjomba alimkumbatia Binti yake huku machozi ya furaha yakiwa yanamtoka ila alijisikia udhuni sana baada ya kumuona Shaymaa amekuja nyumbani akiwa na Mzee Mustapha.
“Mustapha naomba uondoke nyumbani kwangu” Mjomba aliongea kwa upole lakini alimaanisha kile alichokizungumza na kumfanya Shaymaa amshangae Mjomba wake “Mjombaaa!! Mzee Mustapha hausiki lolote kwa upotevu wangu, nafikiri familia inapaswa kumshukuru zaidi kuliko kumfedheesha”
“Shaymaa hujui lolote na upaswi kongea” Mzee Majaliwa aliongea huku akimsogelea Mzee Mustapha huku akiwa anachapia mguu na mkono wake mmoja ukiwa umepooza kabisa na hapo Shaymaa alipatwa na mshangao baada ya kumuona Mjomba yupo katika hali ile
“Shangazi imekuaje tena? Mbona Mjomba yupo hivi? Nini kimemkuta?” Shaymaa alimuuliza Shangazi ambae hakutaka kumficha “Unashangaa nini wakati wewe ndio umesababisha? Umjomba wako alipatwa na mstuko baada ya kusoma barua uliyokuwa umeiandika hivyo ushukuru Mungu kumkuta yupo hivi la sivyo ungekuta ameshafariki”
Shangazi aliongea na kumfanya Shaymaa astuke na kuanza kuhisi kwanini Mjomba anamtimua Mzee Mustapha alihisi labda Mjomba anafanya yote kwa sababu anahisi labda Mzee Mustapha atakuwa alikuwa anamtumia kingono Shaymaa.
Alisogea mpaka mbele ya Mjomba na kujaribu kumsihi asifanye chochote kabla ya kumpa nafasi ya kumsikiliza “Mjomba tafadhali usimuumize Mzee Mustapha, ana Binti yake kama Mimi ambae ameshafariki siku nyingi, Binti yake alifanana na Mimi kila kitu hivyo siku zote nilizoishi kwake alikuwa akinipenda na kunijali kama Binti yake wa kunizaa kwani alikuwa anapoza machungu ya Binti yake kila anionapo Mimi. Kama utamfukuza na kumfanya aniache hapa, utamfanya Mzee Mustapha aishi kwa shida sana”
Shaymaa alijielezea huku kiwa amemkinga mjomba asimfukuze Mzee Mustapha nyumbani kwao, tena aliona ikiwezekana apewe nafasi ya kusikilizwa na kushukuriwa kwa kuishi nae vyema.
“Mustapha inamaana Shaynaa wako amekufa? Kwanini lakini umejua kama na sisi tuna Shaymaa wetu? Kwanini ulijua wewe”
Mzee Majaliwa aliongea kwa ukali na kumshangaza Shaymaa na Mustapha mwenyewe “Mjomba mbona unanichanganya? Kuna nini baina yenu? Kwani kuna Shaymaa Mwengine zaidi yangu?” Shaymaa aliongea na kumfanya Mzee Majaliwa azidi kuchanganyikiwa
“Rayuu wangu alishakufa mwaka mmoja uliopita, lakini kwanini hamkuniambia ukweli kama Rayuu alikuwa na Mwenzie?”
Ulikuwa ni ubishi baina ya Mzee Majaliwa na Mzee Mustapha kila Mmoja akimtupia lawama Mwenzie akimuona ni Mtu mwenye makosa
“Inatosha Mjomba, kama hamtaki kutuweka wazi nini mnachogombana basi Mimi naondoka zangu na sihitaji Mtu yoyote anifuatilie”
Shaymaa aliongea kwa hasira na wote walijikuta wakimsihii hasifanya maamuzi hayo magumu.
*******
Katika moja ya jengo kubwa lililokuwa katikati ya Jiji la dar es salaam kulikuwa na hospital ya BJ.
Jioni hiyo Abdul alikuwa ameruhusiwa kurejea nyumbani na kwa bahati mbaya Mkewe alikuwa hakuja kabisa kuja kumjulia hali “Nahitaji unipeleke nyumbani kwakina Shaymaa” Abdul alimwambia Amina Baada ya kuingia kwenye gari ya Mwanamke huyo ambae alikuwa ni msaidizi wake ofisini kwake
“lakini si unakumbuka kama ulinitumia vibaya kuvunja ndoa yenu? Shaymaa akiniona atanihisi vibaya mana nilienda kwake kama Rafiki itakuaje akijua kama Mimi na wewe tunajuana?”
Amina aliongea kwa upole akimwambia Boss wake ambae alionekana kuguswa na kauli hiyo ya Amina “Najisikia vibaya sana kuona nimekushirikisha kwenye dhambi hii. Kiukweli Mimi napaswa kuwa na makosa kwa sababu sikupaswa kukufanya huwe sehemu ya kuivunja ndoa yangu”
Abdul aliongea huku chozi la kiume likimtoka na kuchukua kitambaa na kujifuta “Hata hivyo usijali wewe twende tu kwa maana Shaymaa hayupo tena katika ulimwengu huu”
Abdul alimwambia kila kitu kuhusu mazingira ya kifo cha shaymaa na Amina alionekana kuguswa sana na kifo cha Shaymaa “Namkumbuka sana yule Dada. Sema basi tu ni ngumu sana kumchagulia Mtu Mke ila kama ningekuwa na uwezo wa kukuchagulia mke, basi Shaymaa kwako alikuwa ni Lulu ulipaswa kuilinda”
Maneno ya Amina yalimgusa sana na Abdul alimwambia kila kitu jinsi Shaymaa alivyokuwa na sifa zote za kuwa Mke wa Mtu. Alimueleza jinsi alivyokuwa anamsubiri mpaka usiku wa manane ili wapate chakula pamoja ila yeye hakuwahi kutambua upendo wake kwake na aliona kama karaha kwa upendo ambao Shaymaa alikuwa anauonesha kwake.
“Je ni kweli Shaymaa Aliwahi kutembea na Mshenga wenu?” Amina alimuuliza na Abdul alisikitika zaidi kuona alitumia mbinu Chafu kumuacha Mkewe kwani hakuwa nasabu muhimu ya kumuacha “Shaymaa hakuwahi kunisaliti kwenye ndoa na wala hakuwahi kufikiri kufanya hivyo. Leo ndio nimeamini pindi Mwanamke anapoamua kukupenda basi huwa anakupenda kutoka moyoni na pindi Mwanamke anapoamua kukudanganya anakupenda anaweza kutumia kila mbinu kukudanganya ila leo nakiri kuwa nilikosea kumuacha Shaymaa na kumuoa Irina”
Abdul liongea kwa kinywa chake mwenyewe huku Amina akiwa pembeni akimsikiliza na kikubwa alichoweza kumshauri ni kumuombea sana Shaymaa. Pia alimsihi kutomuacha Irina na itakapobidi basi amuelekeze “Kosea yote katika maisha ila usikosee kuoa kwa maana kosa moja utakalolifanya linaweza kuja kugharim maisha yako yote”
Amina aliongea na kumuuliza wanaenda kufanya nini kwa kina Shaymaa na Abdul alimjibu kuwa anaenda kutoa pole kwa kuondokewa na mpendwa wao
Amina aliwasha gari na kuelekea kwa kina Shaymaa sehemu ambayo alikuwa akimpeleka Boss wake kwenda kutoa pole huku yeye mwenyewe akiwa hana hofu kwani Mwanamke ambae alitumika kuvunja ndoa yake huku yeye akiwa ameenda kama rafiki akiamini kuwa amekufa
********
Hakuna kitu kikubwa katika maisha ya ndoa kama neno samahani haswa pale unapotambua kwa kiasi fulani umemkosea mwenzi wako. Unapotamka samahani unakuwa kama ni Mtu ambae umechukua ufutio na kufuta makosa yaliyokuwa yameandikwa ndani ya moyo na hapo unauruhusu moyo kuanza kupokea mapya
Ila usitumie samahani kama kifichio cha makosa yako kwani hakuna kitu kibaya kama Mtu anakusamehe alafu unarudia upya kufanya kosa lile lile ambalo ulitoka kuomba msamaha
“Nisamehe sana Feisal” Pili liongea kwa mara nyingine akimwambia Mumewe huku akiwa anamaanisha kweli alikuwa akimkosea sana Mumewe “nilipokuoa wewe, sikuwahi kukuoa nikiamini kuwa wewe ni Mkamilifu. Hata kama nawe ulifunga ndoa name ukiamini hivyo utakuwa umenikosea sana. Nilikuoa kwa kuamini kuwa mapungufu yako yanavumilika kama wewe jinsi unavyoweza kuvumilia mapungufu yangu kwani hakuna mkamilifu baina yetu”
Feisal aliongea na kumpa mfuko uliokuwa na zawadi na kumwambia kuwa hiyo ni zawadi yako, tokea Baba ameumwa ujaonekana ukienda kumtembelea. Hipo tofauti kidogo kwani leo nataka huwe kama Mama Africa” Feisal aliongea na kumfanya Pili hawe na Shauku ya kutaka kujua ni nguo gani ambayo Mumewe alikuwa amemletea
Ilikuwa ni gauni fulani iliyoshonwa kupitia kitenge huku ikiwa imenakshiwa kwa kitambaa fulani cha asili na kulifanya gauni hilo kuwa zuri zaidi.
Pili alichukua na kuvaa gauni hilo na kupendeza ipasavyo “Umewezaje kutambua vipimo vyangu?” Pili aliongea baada ya kuvaa na kuona utafikiri ameenda kupima mwenyewe
“Nimeenda kushona kwa fundi wako ila kitambaa nilienda kutafuta mwenyewe” Feisal aliongea na wote walifurahi na kutazamana “Asante sana Mume wangu” Pili aliongea huku akijisikia raha isiyokifani
Zawadi ina maana kubwa sana kwenye mapenzi, jifunze kuanzia leo kumpa zawadi mpenzi wako hata kama ni ndogo ila wewe Mpe zawadi alafu mtazame usoni utakuja kunishukuru.
Feisal na Mkewe walimuaga Mzee Juma kuwa wanaenda kumtembelea Mgonjwa na Mzee juma alisisitiza kuwa lazima warejee nyumbani kwani alikuwa na mazungumzo nao na Feisal alimtoa hofu mzee n kumuahidi kuwa watarejea
*****
Kitika chumba cha Shaymaa Sabrah aliingia kwenda kufanya usafi kama ilivyo kawaida yake.
Alishangazwa na mazingira yalivyo katika chumba icho na mara kadhaa alijikuta akiwa na hofu.
“kwanini naogopa?” Sabrah alijiuliza mwenyewe na kukosa jibu na wakati anafanya usafi aliuona mkoba na kupatwa na mstuko wa hali ya juu na hapo hapo aliweza kukumbuka jambo
“Nakupenda sana Rafiki yangu, najua tunatenganishwa kwa sababu ya upendo wangu kwa Hakeem ila hipo siku tutakuja kuonana tu” Liyuna alimwambia na kumfanya Sabrah abubujikwe na machozi “Huu utakusaidia, naupenda sana ila Bibi aliwahi niambia njia nyepesi ya kudumisha upendo kwa rafiki yako ni kumpa kitu chochote cha thamani unachokipenda” Sabrah alimwambia Rafiki yake na Liyuna aliupokea na kumshukuru na hapo hapo alianza kuweka vitu vyake.
Sabra alitoka kwenye kumbukumbu na kujikuta akiukagua ule mkoba na kukuta vile vitu ambavyo Liyuna aliviweka vyote vilikuwemo
“Inamaana huu aliusahau au bado yupo humu amejificha” Sabrah aliongea Mwenyewe na kuanza kumuita Rafiki yake lakini wapi ukimya ulitawala.
Kadri alivozidi kumuita ndivyo alivyozidi kujikuta akiingiwa na hofu na kuzidi kutetemeka.
Alianza kukagua kila eneo kama Liyuna yupo humo na alipochungulia uvunguni kwa maajabu alimuona Liyuna amelala. Mwanzo alimuita kawaida ila baadae alipojaribu kumgusa aligundua kuwa Liyuna ameuwawa
Yowe la uoga lilisikika na watu wote walikimbilia ili kujua kuna nini kimetokea “liyuna amekufa Shaymaa amemuaa Liyuna Shaymaa amemuua Liyuna”
Sabrah alimwambia Madame huku akiwa anaogopa na Madame alipoiona Maiti ya Liyuna alijikuta akipatwa na mstuko wa hali ya juu “Wewe imekuaje tena yani Shay maaa ame……? Nakataa Shaymaa hawezi kufanya hivi mnamsingizia Binti yangu” Madame aliongea na kupatwa na mstuko wa hali ya juu.
“Ni kweli Madame Shaymaa amemuua Liyuna alimwambia siku moja kabla, Liyuna alishaniambia kuwa Shaymaa amemtishia maisha”
Sabrah aliongea na kuwastua Watu wote waliokuwa pale
******
Kikao cha dharula kilifanyika ili kuondoa utata ambao ulikuwa umejitokeza.
“Mimi binafsi ndio napaswa kulaumiwa kwa kila kitu, ila Sakina hakuwa na makosa yoyote wala sipendi nimseme vibaya” Mzee Majaliwa aliongea na kila mmoja alikuwa makini kumsikiliza.
“Najisikia aibu sana kutamka hiki ninachotaka kutamka ila samahani sana Shaymaa na samahani sana Mustapha ila kiukweli Sakina hakujifungua Mtoto Mmoja kama ambavyo ulivyokuwa ukitambua. Mara ya Mwisho wakati anakufa, alinisihi hata siku moja nisije kukwambia siri hii kwa usalama wa Binti yake. Ila Shaymaaa alikuwa na pacha wake ambae ni Doto wake ambae sisi tulimtambua kama Shaynaa kabla ya familia yako kuja kumchuka na kwenda kumbadili jina na mkamuita mtakalo ila Kiukweli huyu pia ni Binti yako.
Mzee majaliwa aliongea na kuwastua wote waliokuwa pale huku Mzee Mustapha akiinua mikono juu na kumshukuru Mungu huku akiwa anabubujikwa machozi ya furaha.
Shaymaa alikuwa amepigwa na butwaa hasijue nini cha kusema ghafla msaidizi wa Mzee Mustapha alimletea simu Mzee Mustapha
“Shaymaa anatuhumiwa kufanya mauaji ya Mfanyakazi wetu anayeitwa Liyuna na kumficha uvunguni mwa kitanda, hivyo popote alipo naomba huwe nae makini hasije kutoroka ili akamatwe na polisi na akajibu mashtaka yake”
Madame alimwambia Mumewe na kumfanya Mzee Mustapha apatwe na mstuko mpaka simu ilimponyoka kutoka katika mkono wake
WEWE UNAFIKIRI NINI KINAENDA KUTOKEA? ESIKOSE EPISODE YA MWISHO YA MSIMU WA KWANZA WA SIMULIZI HII
MAUMIVU YA NDOA
S2: EP 30
MTUNZI: Abdulkarim Dee
ILIPOISHIA ……………
Taratibu yule Daktari fake alijichkesha na kuokota ile sindano “Mzee Mustapha, nasikitika kukwambia kuwa wewe unapaswa kufa” Aliongea na kumsogelea ili amchome sindano.
Alistushwa na pigo zito kutoka kwa Othman aliyekuwa amejificha kwenye wodi hiyo na kumdhibiti ipasavyo
ENDELEA ………………
Yupo wapi Mtu aliyewahi kusema Damu ni nzito kuliko maji?
Baada ya Madame kuweza kumparamia na gari Mtoto wake na kumuumiza vibaya, Feisal hakujali kama ndugu yake alikuwa amedhamiria kumdhuru na bastola, badala yake alifanikiwa kumbeba ndugu yake na kumkimbiza hospital huku Madame akiwa analia kama Mtoto Mdogo akimtaka kipenzi chake asife
******
Ulikuwa ni mtego wa aina yake ambao alikuwa ametegewa Dokta Joel na kufanikiwa kunaswa na hakutegemea wala kufikiri kama angeweza kukamatwa kirahisi kwa namna hiyo
“Kila kitu kimearibika Madame” Kennedy alimwambia Madame huku akiwa anahema juu juu “Kivipi?” Mustapha alikuwa ni Mzima, wewe ukumtazama, alikuwa amejifanyisha tu” Kennedy alijibu na kumstua Madame ambae hakutegemea kusikia kauli hiyo kutoka kwa kijana wake na kabla ajaongea chochote ili kujua nini kilikuwa kimetokea, Mustapha alikuja walipokuwa akiwa ameambatana na maaskari kdhaa “Unafanya nini muda huu hapa hospital?” Mustapha alitazama saa yake na kumuuliza Mkewe
Lilikuwa swali zuri kwa upande wa Madame kwani aliweza kushusha pumzi na kuongea kwa kujiamini akiona hiyo ndio ilikuwa nafasi ya kufanya maigizo yake kwa upande wa Mumewe ili kukwepa aibu ya kutaka kumuua Mumewe
“Hali ya Mwanao Hakeem ni mbaya sana, nimemgonga na gari pasipo kujua na hivi tunavyoongea, anafanyiwa operation ya mguu” Madame aliongea na kujifanya kachanganyikiwa. Ukweli ni kwamba alikuwa amechanganyikiwa lakini alikwa akijiongeza zaidi ili kupoteza maboya asijulikane kama yupo nyuma ya mpango mzima juu ya kutaka kumuua Mumewe
“Wala usitumie nguvu kuweza kunidanganya kwani najua kila kitu kama Hakeem si Mtoto wangu wa kumzaa na wewe ulikuwa na mpango wa kuniuwa Mimi” Mustapha aliongea na kumstua Madame ambae hakutegemea kama Mumewe anaweza kuijua siri hii kirahisi sana na kama isingekuwa umahiri wa Kennedy katika kumdaka, basi angeweza hata kwenda chini kama mzigo
“Katika maisha yangu, kupitia biashara zangu zimenisaidia na kujikuta nikipata mafanikio makubwa sana, na hii ilitokana na mimi kuwa mtumiaji mzuri sana wa muda. Sikuwahi kuthubutu hata kidogo kupoteza angalau dakika moja pasipo kufanya jambo la maana. Ila katika yote hayo bado nabaki kuwa ni mmoja kati ya wanaume wapumbavu ambao waliwahi kukosea katika swala zima la kuchagua Mwanamke ambae nilipaswa kumuoa”
Mzee Mustapha alipiga hatua na kuongea huku Watu wote wakiwa makini kumsikiliza na hapo aliweza kuadisia ilikuaje mpaka akagundua uovu wote wa Mke wake
SIKU KADHAA NYUMA
Usiku Mmoja Mzee Mustapha aliamka na kupatwa na mstuko baada ya kutomuona Mkewe kitandani.
Alipatwa na hofu kubwa sana na alihisi labda kutakuwa na jambo baya ambalo Binti yake atakuwa anafanyiwa na Mama huyu ambae Mzee Mustapha alikuwa ameshaanza kumtilia mashaka
Mzee Mustapha aliamka haraka kwenda chumbani kwa Binti yake kuona kama kutakuwa na jambo baya ambalo litakuwa limemkuta Binti yake
Haraka alitoka na kuelekea chumbani kwa Shaymaa na kujaribu kumgongea mlango ili kujua kama yupo salama au lah.
Sauti ya mlango kugongwa ilimstua Shaymaa na kujikuta akipata hofu Zaidi na kujikunyata kama kifaranga kilichokuwa kimakosa Mama.
“Shaymaaaa!!” Sauti ya Mzee Mustapha ilisikika na kumpa faraja Shaymaa ambae alitoka na kwenda kufungua mlango huku akiwa Analia.
“Baba Mimi naogopa” Shaymaa alimwambia Baba yake huku akiwa amemkumbatia kwa nguvu.
Baada ya hapo waliongea mambo mengi na Shaymaa alimueleza hofu yake huku akiwa amekataa kuwa Mkurugenzi Mpya wa kampuni.
Baada ya kuongea mambo yao, Mustapha alimtakia usiku mwema Shaymaa na kuondoka zake na wakati anatoka chumbani kwa Shaymaa, ghafla alikamatwa na kutekwa nyara
“Samahani sana Mzee wangu kwa hiki nilichokifanya” Alikuwa ni Othman ndie aliyekuwa amemshikia bunduki Boss wake kitu ambacho kilimstua na kumuogopesha Mustapha
“Wewe Othman unawezaje kuthubutu kufanya hivyo” Mustapha alimuuliza Othman huku akiwa anatetemeka akihisi labda Othman atakuwa anashirikiana na majambazi
“Napaswa kufanya hivi kwa sababu ya usalama Wako, jina langu naitwa Mr Daniel Mdimu na nipo hapa nyumbani kwako ili kutekeleza majukumu maalumu ikiwemo na kulinda usalama wako pale inapopibidi
Othaman aliendelea kujitambulisha zaidi kisha akamuomba washirikiane katika kutafuta ushahidi “Mkeo ndie muhusika wa kila kitu juu yako, Asia alikuulia Mwanao pamoja na Mama yake Shaymaa hivyo nataka msaada wako katika kukamilisha ushahidi wake”
Othman aliongea na kumshawishi Mustapha ambae alikubali kufungwa kinasa sauti na kuvamia maongezi ya Madame na Hakeem “Akikisha unaanzisha unajifanya kupatwa na mstuko na kupoteza fahamu bila shaka hapo unaweza kusikia mengi zaidi”
“Kwanini Umemuua Liyuna” Hakeem alibadilika na kumsogelea Mama yake huku akiwa na hasira akitetemeka mikono “Hakeem? Inamaana simulizi yangu yote niliyokusimulia umeshindwa kuelewa kuwa wewe ndio chanzo cha kuvuluga maisha yangu na kunipa moyo ambao nilikuwa sina?”
Madame aliongea na kabla Hakeem hajajibu kitu walisikia mlango umefunguliwa ghafla na Mzee Mustapha akiwa anahema juu juu huku akiwa anamtazama jicho kali Madame “Honey vipi mbona ghafla?” Madame aliongea huku akiwa anajistukia “Nimejua kila kitu kuhusu wewe Asia na leo utanieleza ukweli wako wote”
Mzee Mustapha aliongea kwa hasira huku akiwa anatetemeka midomo na macho yake yote yakiwa kwa Madame
“Honey bwana mbona unanichekesha” Madame alijaribu kujichekesha ili kumtoa Mustapha katika reli na kujifanya kama alikuwa anaongea kitu cha kawaida na Mwanae
Baada ya hapo walijikuta wakipishana Kiswahili na Mzee Mustapha alifanya hivyo kusudi ilia pate kujifanya amepatwa na mstuko nakupoteza fahamu.
Kabla hajapata nafasi ya kujifanya amepatwa na mstuko alistuka amepigwa ngumi na Hakeem na kujikuta akipoteza fahamu kweli tofauti na wao walivyotaka kuigiza
“Hakeem umemuua Baba yako?” Madame aliongea kwa hofu huku akiwa anamtazama Mzee Mustapha aliyekuwa amepoteza fahamu lakini kile kinasa sauti kilikuwa kinachukua kila kitu kilichokuwa kinaendelea
“Unaogopa nini? Wewe si ulitaka kumuua? Nimekusaidia kutenda dhambi uliyotaka kutenda”
Hakeem aliongea na kumfuraisha Mama yake ambae sasa aliona Mwanae amemsaidia kufanya jambo ambalo alitamani kulifanya kwa siku nyingi.
“Lakini ni bora afe tu kwa sababu akiendelea kubaki, siku moja atakuja kugundua kuwa wewe siyo Mtoto wake wa kukuzaa na hii itakufanya ukose nafasi ya kuwa mrithi wake”
Madame aliongea na baada ya hapo walipanga mipango jinsi ya kumbeba na kumuingiza chumbani kwake huku Madame akipanga kutoa maelezo kuwa Mzee Mustapha alikuwa amepatwa na mstuko.
Walifanya kama wlivyokubaliana na Madame alimtaka Kijana wake aondoke eneo hilo ili asije kustukiwa kama ni yeye ndie aliyekuwa muhusika na mauaji ya Mzee Mustapha kwani alijua anaweza hasiwe mzuri katika kutoa maelezo
*****
Asubuhi na mapema Shaymaa alikuwa wa kwanza kwenda kugonga mlango ili amsalimie Baba yake lakini Madame alimjibu ovyo na wakati huu Mzee Mustapha alikuwa ameshapata fahamu ila aliendlea kujifanyisha kuwa amepoteza fahamu.
Madame alipiga simu ya dharula hospital ili gari ya wagonjwa ije kumbeba Mzee Mustapha, kumbe wakati huo Othman kupitia hidara yake aliyokuwa anafanyia kazi walikuwa wameshajiandaa na kutoka na gari ya wagonjwa huku wale waliokuja kumchukua Mzee Mustapha wakiwa ni Maaskari
Mzee Mustapha hakupelekwa hospital moja kwa moja na alipelekwa kwenye kituo chao maalum na hapo Othman aliweza kumpigia simu Abdul ambae alikuja baada ya kupewa taharifa tata huku akiwa na hofu ya kunaswa kwa mawasiliano yake.
Wakati huo walikuwa wamenasa mawasiliano ya Madame na Kennedy na waliweza kugundua kila kitu kama Madame kaanda mipango ya kutaka kwenda kumchoma sindano ya sumu Mumewe hivyo waliandaa mpango kabambe wa kuweza kuwanasa wahusika mpaka hapo walipokuwa wamefanikiwa ………………
NINI KITAENDELEA USIKOSE EPISODE YA 31
Tags:
RIWAYA