“MIMI SI MALAIKA, MIMI NI MAMA…”

Baba mmoja alikua akijaribu kuwanunua watoto wake ili wampende yeye zaidi kuliko wanavyompenda Mama yao, kila siku aliwaletea zawadi za gharama, walipokosea aliwasifia na Mama yao alipojaribu kuwaadhibu alikua mkali na kumuambia awaache watoto wake na kama amechoka namna ambavyo anawalea basi aondoke kwake.

Mama alikua akiumia, kila siku akilia, watoto walimdharau, hawakumsikiliza na kila mara walikua wakimtukana na alipoongea Baba yao aliwakingia kifua. Walimuona hana msaada na kila siku watoto waliomba Mungu Mama yao aondoke au hata apate ajali afie mbali ili wabaki na Baba yao.

Siku moja dua zao zilisikika, Mama yao alipata ajali mbaya ya Gari, alilazwa Hospitalini akiwa hajitambui. Wakiwa na furaha waliomba afe kabisaaa kwani yeye alikua ni mnoko sana na wangekua na furaha kuishi na Baba yao tu. Siku ya kwanza ilienda vizuri, lakini wiki moja baada ya Mama yao kulazwa Hospitalini mambo yalibadilika.

Watoto waliamka asubuhi hakuna chai, Dada wakazi alikua hawezi kupika kama Mama yao, Baba yao alikua naye akisubiri chai na hakuiona. Walienda shuleni na njaa, waliporudi Mama hakuepo, chakula kilichopikwa na Dada wakazi hakikua kizuri, Dada alikua na kazi nyingi hivyo nguo zao hazikufuliwa. Walimfokea na baada ya kuona kelele Dada wa kazi aliondoka.

Wakiwa hawana mfanyakazi wakidhani baba yao atatosha, mambo yalianza kua magumu, nyumba ilikua chafu, hakuna mtu wa kupika kila siku ikawa ni kula Hotelini. Baba naye kazi zilikua nyingi Ofisini, akirudi nyumbani kachoka, watoto wanalia njaa, wanalalmika nguo hazijafuliwa, wanalalamika wamechoka kula Hotelini, malalamiko yalikua mengi.

Kelele za watoto zilimpa Baba hasira, akawa anakasirika na kuwatukana akiwalazimisha kufanya kazi za nyumbani na hata kuwapiga walipomjibu jeuri kama walivyokua wakimjibu Mama yao. Watoto walianza kumchukia, hawakuona tena faida ya pesa zake, Baba naye alianza kuwachukia watoto wake, aliwaona kama hawana shukurani, visirani wamedekezwa.

Hakutamani hata kurudi nyumbani kukutana na kelele za watoto ambao walikua hawajui hata kupika chai kwakua alimkataza mkewe kuwapa kazi. Kila siku alikua akiomba Mungu mkewe apone arudi aanze kulea watoto wake, watoto nao walianza kusali kumuomba Mungu Mama yao apone ili arudi nao wawe na furaha tena, walimmiss sana na dua zilibadilika.

Walikua hawaendi Hospitalini lakini walianza kwenda, kumpelekea zawadi na kulia katika kitanda chake. Mama yao alipopona walianza kumuomba msamaha na kumuahidi watabadilika kwani sasa wanamchukia Baba yao. Baba naye alimuomba msamaha mkewe kwa kujaribu kumgombanisha na wanae, alimuambia sikua nikijua taabu unazozipata kama Mama.

Nimeamini kua pesa haziwezi kulea watoto kwani ulipoumwa pesa bado nilikua nazo lakini nilitamani hata kuwauza kuliko kukaa nao ndani kwa siku moja. Sijui unafanya nini kila siku mpaka nyumba inakua na amani lakini nashukuru kazi unayoifanya kwani siiwezi hata kwa dakika moja, nisamehe mke wangu nisamehe sasa nitakuacha uwe Mama sitaki tena wanipende! 

Wewe ni Malaika Mke wangu sijui unawezaje yote haya?” Mkewe alitabasamu kisha akamuangalia mumewe na kumuambia “Mimi si Malaika, Mimi ni Mama…”

#SHARE KAMA UMEJIFUNZA KITU 

Post a Comment

Previous Post Next Post