ILIPOISHIA.......
Akakumbuka pia na maneno yale aliyoambiwa na yule Ajuza wa ajabu kwenye ndoto mara baada kumuelezea habari kuhusu upatikanaji wa dawa itakayo mfanya mama yake kupona.
"Dawa ipo Tropea! Mji uishio wafu itakulazimu ufe ili kufika huko"
ENDELEA NAYO.....
Punde usingizi ulimpotea kijana Bingo, ndoto hiyo aliyoota kwa mara nyingine tena ilimuogopesha. Akajikuta anashindwa kuelewa afuate kipi, na ninani mkweli kwa maana Ajuza yule wa ajabu alimwambia afuate dawa Tropea hali ya kuwa mtu yule aleyemtokea ndotoni alimwambia aende Tropea kuokoa ngome ya Abdy, ngome ambayo mtoto wa Sultan Starlon anataka kujimilikisha zote. Ngome ya baba yake ambayo ni Buda, lakini pia ngome ya Sultan Abatish. Abatish aliona tayari anakwenda kupoteza umwamba wake katika mji huo, nguvu za kupigana zilikuwa zimeshamtupa mkono kwa sababu uzee ulikuwa umeshashika kasi katika mwili wake na ndio sababu ya kutuma watu wake waje duniani kuitafuta damu yake ili akakomboe ngome hiyo ili Zama zisipotee. Pumzi ndefu alishusha kijana Bingo, katu usingizi haukuweza kumjia kwa haraka zaidi ya kutafakari mara mbili mbili safari hiyo ya Tropea. Lakini baadaye kidogo alijilaza kitandani kwa mara nyingine tena na punde si punde usingizi uliweza kumpitia.
Kesho yake asubuhi Bingo alifanya shughuli zake kama afanyavyo kila siku kabla ya kwenda kwenye mihangaiko, baada kuhakikisha kila kitu kipo sawa alifunga safari kuelekea nyumbani kwa mzee Ndelo. Mzee ambaye alionyesha anavitu vingi sana anavyovifahamu mama yake lakini pia Bingo alihisi kuwa mzee huyo anaweza kumpa mambo mawili na matatu yanayohusu Tropea.
"Habari mzee" Alisema Bingo mara baada kufika nyumbani kwa mzee Ndelo. Muda huo alimkuta mzee huyo akilisha mifugo yake. Ndelo aliposikia sauti hiyo aligeuka nyuma akawa amekutana uso kwa uso na kijana Bingo, ajabu kilichomshangaza mzee Ndelo ni kumuona Bingo akiwa emedhoofu ilihali uso wake ukionyesha kuwa ni mtu mwenye matatizo chungu nzima.
"Aah Bingo?.." Aliachia tabasamu mzee Ndelo kisha akaongeza kusema "Karibu sana"
"Asante sana babu, lakini ujio wangu huu unajambo.."
"Ni kweli hata mimi nafahamu hilo lakini subiri nimalize shughuli yangu hii kisha tuketi ili tuweze kuongea kwa kina zaidi"
"Sawa"
Baada ya shughuli nzima kukamlika hatimaye Bingo na mzee Ndelo waliketi chini, wakaanza kuteta mambo mbali mbali hasa kuhusu mji wa Tropea ambapo Bingo alianza kwa kumueleza Ndelo juu ya ndoto za ajabu anazoota.
"Pole sana kijana, lakini ukweli utabaki kuwa huo. Ni siri nzito uliyonayo Bingo na nilitegemea hapo baadaye itakuja kukusumbua tangu pale mama yako akosee masharti aliyopewa Tropea.." alisema Ndelo.
Bingo alishtuka kwa taharuki ya hali ya juu akauliza "Unamaana gani mzee?.." Ndelo aliangua kicheko kidogo halafu akajibu
"Nitakwambia Bingo, lakini pindi utakapo jua huu ukweli haraka sana fanya mamuuzi yaliyo sahihi. Bingo, tazama kwenye bega lako" Bingo alitazama, aliiona alama kwenye bega lake. Bado alionyesha kutokuwa na sitofahamu na hivyo alirudia kuhoji
"Hii ni nini?"
Ndelo akasema
"Huu ni muhuri kutoka Tropea, katu chata hii haitoweza kufutika sababu wewe ni mtoto kutoka ngome ya Abdy.."
Alipokwisha kusema hivyo alimsimulia moja kwa moja na kisa kile kilichomkuta mama yake mpaka kufika hali hiyo, kwa mara nyingine tena Bingo akaisikia simulizi hiyo ukiachilia mbali ile aliyosikia mwanzo akiwa mafichoni.
Hakika ilimshtua sana Bingo, hofu ilimjaa huku maswali kibao akijiuliza kichwani mwake.
"Kwahiyo nifanye nini sasa mzee wangu, sababu ndoto hizi zinanikosesha amani kabisa, sipati usingizi, na hata nikipata silali kwa muda unaotakiwa. Nisaidie tafadhali" Akionekana kuwa na majonzi usoni mwake alisema maneno hayo kijana Bingo.
Hapo mzee Ndelo alikaa kimya, lakini punde si punde akasema
"Njia pekee ya wewe kuepuka mauza uza haya ni kujitoa muhanga wa kuelekea Tropea basi. Eeh tofauti na hivyo utaendelea kusumbuliwa na mwisho wa siku utaangukia pabaya" Alisema mzee Ndelo.
Hapo Bingo alikaa kimya katu hakutaka kuongeza neno lolote zaidi ya kujiinamia huku akitafakari safari hiyo nzito ya kuelekea mji wa wafu kwenda kuikomboa ngome ya baba yake lakini vile vile kwa dhumuni la kufuata dawa ya kumtibia mama yake.
Mwisho wa yote Bingo alinyanyuka akaondoka zake kichwa chini mikono nyuma akirejea nyumbani, lakini kabla hajafika mbali mzee Ndelo alipaza sauti kumuita Bingo. Bingo aliposikia sauti ya mzee huyo aligeuka nyuma kumtazama. Mzee Ndelo akasema.
"Nenda Tropea kijana" Kwisha kusema hivyo mzee huyo alizama ndani huku akimuacha Bingo akiambaa na njia ya kuelekea nyumbani kwao.
Akiwa njiani bado akili yake aliipa mzigo mzito sana wa kuifikiria safari ya Tropea, kijana aliona shida kuu si kufika huko bali ugumu upo katika njia ya kufika huko. Njia ngumu sana, ni njia ambayo ilimuogopesha Bingo.
"Nife? Mmh mbona kibarua kizito?.." Alijikuta akijisemea hivyo Bingo mara baada kutafakari kwa kina safari hiyo wakati huo akiwa njiani akirudi nyumbani.
Ajabu alipokwisha kujisemea hivyo ilisikika sauti nyuma yake ikiangua kicheko
"Ahahah ah hahaha" Bingo alishtuka, haraka sana akageuka. Akakutana uso kwa uso na mama yake.
"Khaa mama?.." Alitaharuki Bingo huku akirudi nyuma kwa woga.
Wakati huo huo mama yake alisema
"Bingo mwanangu kwanini hutaki kwenda kuikomboa ngome ya baba yako ambayo ipo shakani? Ama kwanini hutaki kufuata dawa ili mama yako nipone? Bingo mwanangu Bingo tafadhali nenda Tropea" Alisema mama Bingo, Bingo alishtuka, asiamini kile akionacho.
Kwa sauti ya mshangao akasema "Mamaaa? Ni wewe?.."
"Ahahahahaha hah hah" Aliangua kicheko mama Bingo kisha akapotea.
Hapo sasa Bingo alitimua mbio huku akipiga mayowe. Alipofika ndani alifungua mlango kwa nguvu moja kwa moja mpaka chumbani kwake, huko akapata kukaa na kutuliza hofu. Na wakati yupo katika hali hiyo ya hofu, punde alimsikia mama yake akikoroma chumbani kwake.
Hapo Bingo alisimama akiwa ameshika kiuno, mwili nao ukiwa umechoka dhofulihali huku akijiuliza juu ya yule mtu aliyechukua taswira ya mama yake na kisha kumuelezea maneno yale.
Mwishowe alishusha pumzi ndefu kisha akazipiga hatua kuingia chumbani kwa mama yake ambapo alimkuta akihema kwa nguvu, jasho nalo lilimtoka kwa wingi. Bingo aliogopa alitoka ndani mbio akaelekea nyumbani kwa mzee Ndelo kuomba msaada.
"Babu mama hali yake ni mbaya sana, tafadhali twende ukanisaidie. Nampenda sana mama yangu" Alisema Bingo kiasi kwa sauti ya juu juu. Mzee Ndelo akajibu "Sawa tangulia nakuja"
"Usikose mzee wangu nipo chini ya miguu yako" Alisisitiza Bingo. Mzee Ndelo aliahidi kufika bila kukosa.
Ujio wa mzee huyo alifanya kila jitihada walau kupoza hali ile iliyokuwa imemuibukia mama Bingo, hivyo baada kuwa sawa mzee Ndelo alimuita Bingo nje. Bingo alitii wito, na hapo ndipo Ndelo alipomwambia "Bingo, hii hali inaweza kumuondoa dunia mama yako siku yoyote ile endapo kama hutokubali matakwa ya kutakiwa Kufika Tropea. Kijana piga moyo konde, wewe ni mwanaume nenda Tropea, lakini pia nakuhakikishia kuwa kuna mafuta utayapaka mwilini mwako, hayo yatakusaidia pindi utakapo wasili mji ule wa wafu.. "
" Mafuta? Mafuta gani hayo?.. " Alihoji Bingo. Mzee Ndelo akaongeza kusema. 'Niambie kwanza upo tayari?."
Alikaa kimya kidogo kijana Bingo ila mwishowe alijibu" Ndio nipo tayari.. " Hakika jibu hilo lilimfanya mzee Ndelo kuachia tabasamu bashasha kisha akasema kwa sauti ya upole. "Bingo, nakuhakikishia utaenda salama, na utarudi salama pia. Vile vile nakuasa ukirudi kutoka Tropea, basi hautoishi maisha haya. Tropea huu ni mji wa wafu lakini pia unamali nyingi sana. Muhimu usivunje masharti ya huko. Bingo kijana shupavu kesho Tropea.
*******************
Jioni sana, yapata saa moja kasoro robo. Kijana BINGO kwa mara nyingine tena anakutakana na mzee Ndelo katika mapanda njia.
"Bingo.."
"Naam! Mzee"
"Kwanza napenda kukupa hongera ya kukubali takwa hili la kuelekea Tropea, vile vile ukiachilia mbali hongera hiyo nataka nikuthibitishie kuwa tupo pamoja katika safari yako hii ngumu. Hivyo basi chukuwa mafuta haya, jipake mwilini kabla hujalala, pia chukuwa maji haya ambayo nayo utakunywa mara tatu, yaani bunda la kwanza bunda la pili mpaka la tatu. Hii ni safari ngumu sana kwako Bingo lakini hupaswi kuogopa kwa sababu woga wako utaweza kukugharimu, yapaswa kupiga moyo konde. "
"Huko maisha utakayo ishi katu usithubutu kufanya mapenzi na mwanamke yoyote yule, wala usikatae chakula utakacho letewa. Pia Bingo kuwa makini, pindi utakapo muona mtu yoyote uliyewahi kumuona hapa Duniani usimpaparikie kujifanya unamfahamu. Kuwa mtu tofauti kabisa na watu utakao wakuta huko ingawa najua kwa vyovyote vile lazima utahusudiwa ukiwa kama mtoto wa Sultan" Aliongeza kusema mzee Ndelo wakati huo Bingo akiwa ameshikilia vitu vile aliyopewa ambavyo ni mafuta na maji maalumu aliyoyatengeneza mzee huyo ambaye ni mganga wa jadi.
"Sawa nimekuelewa, na napenda kukuahidi kuwa nitafanya kama ulivyo nielekeze" Alisema Bingo.
"Sawa safari njema kijana"
"Ammh vipi Kuhusu mama yangu? Ni nani atamuhudumia?" Kabla Bingo hajaondoka alimuuliza swali hilo mzee Ndelo. Mzee huyo alijibu kuwa atamsaidia bila tabu yoyote. alifurahi sana Bingo kisha akarejea nyumbani huku akili yake ikifikiria safari ya Tropea. Alipofika nyumbani alimkuta bibi yake mzaa mama amekuja nyumbani, ujio huo ulimfurahisha sana Bingo kwani alijua tayari kapitakana mtu wa kumlea vilivyo mama yake kwa kipindi hicho atakachokuwa yupo mji wa wafu.
"Karibu sana bibi, habari za siku nyingi" Alisema Bingo akimsabahi bibi yake.
"Ni nzuri, ingawa nimepotea njia mara nyingi ila hatimaye leo nimefika, umekuwa mkubwa Bingo" Alijibu bibi huyo huku akitupia na utani kidogo, utani ambao ulimpelekea Bingo kuangua kicheko.
Baada miaka gedegede kupita hatimaye bibi huyo anakuja kumuona mwanaye ambaye ni mama yake Bingo. Alikuwa ni mzee sana, alipata tabu sana kutembea lakini siku hiyo alidhamiria kufika pasipo kukosa.
"Naam! Safari hii sasa inaonekana itakuwa ya neema kwangu.. Tayari kapatikana mtu wa kubaki na mama yangu. Najua hawezi kupata shida pindi bibi atakaposhirikiana na mzee Ndelo. Mungu nitie nguvu" Alijisemea Bingo, muda huo tayari ulikuwa muda wa kulala.
Muda muafaka ulipo wadia akafanya kama mzee Ndelo alivyomwambia.
Mara baada kujipaka mafuta yale, ghafla mwili wake ukaanza kumuwasha. Akajikuna kila sehemu ya mwili wake mpaka akajikuta akihisi kuwa huwenda mzee Ndelo kamuingiza mkenge lakini baadaye kidogo hali hiyo ikampotea ila mwili wake ulionekana kuvimba manundu kila mahala. Kitendo ambacho kikamfanya kuhofia kuinywa ile dawa, ingawa baadaye akakata kauli akajitoa ufahamu akainywa.
Baada ya hapo hakuona kilicho endeelea, yaani akawa ameamka kutoka kitandani, tayari palikuwa pamekucha. Akakurupuka akavaa nguo zake haraka haraka kisha akazipiga hatua kuelekea chumbani kwa mama kumjulia hali, ajabu sebuleni akakutana na jopo la kina mama wakionyesha nyuso za huzuni sambamba na kuangua vilio. Kitendo hicho kikamshtua Bingo, kwa taharuki wasiwasi nao ukimjaa tele akihisi kuwa mama yake ameaga Dunia, lakini ghafla wasiwasi huo ukapotea, hofu zaidi ikamjaa baada wale wakina mama kumtomtizama licha ya kwamba alikatiza katikati yao, mbali na hilo, hata alipo simama mlangoni kuna mzee mmoja alifika eneo hilo alilosimama alipo msalimia hakuitikia na vile vile alionekana kuwa bize na wala asijishughulishe na salamu ya Bingo.
Hapo Bingo akaamuwa kutoka ndani kabisa, nje akaona jeneza, akastaajabu sana akalisogelea jeneza hilo kwa dhumuni la kutaka kujua ndani ya jeneza hilo kuna mwili wa nani. Lahaulla. Kijana Bingo akakuta ndani ya jeneza hilo kuna mwili wake.
********
Baada kuona mwili wake ndani ya jeneza alizidi kuogopa, lakini punde tu mzee Ndelo alionekana mbele yake. Mzee huyo alikuwa ameshika koti kubwa jeusi lenye kofia yake, vile vile alikuwa na upanga mkubwa kiasi.
"Bingo.." Mzee Ndelo alipasa sauti kumuita Bingo. Bingo akaitika kwa sauti ya woga.
"Usiwe na hofu juu ya haya maombolezo, japo huu ni msiba wako lakini usiwe na tabu yoyote kwani hapo ulipo tayari upo katika mazingira ya kwenda Tropea. Wewe ni nafsi na ule kwenye jeneza ni mwili wako" Alisema mzee Ndelo.
"Mzee unamaana gani sasa? Mbona kama sikuelewi?.." Aliuliza Bingo kwa mashaka.
"Ahahahah hahahhaa" Aliangua kicheko mzee huyo, punde akasema
"Ndio. Kwa sasa huwezi kunielewa ila utakapo toka Tropea nafikiri utanielewa. Mwili huu nitahakikisha hauzikwi, nitajua kipi cha kufanya ilimradi mwili wako uendelee kuwepo Duniani. Ukisharudi kutoka Tropea, utauvaa na maisha kama kawaida yataendelea"
"Je, unataka kuniambia kwamba kuna madhara endapo kama mwili wangu utazikwa?.." Kwa mara nyingine tena Bingo aliuliza.
"Madhara yapo"
"Ni yapi hayo"
"Ni mwanzo na mwisho wa maisha yako" Alijibu Mzee Ndelo, ni jibu ambalo lilimshtua Bingo ilihali muda huo huo mzee huyo aliweza kumkumbusha kijana mambo kadhaa ambayo hatakiwi kuyafanya pindi atakapo kanyaga ardhi ya mji wa wafu.
"Bingo, na kukumbushia kwa mara nyingine tena na tena. Tropea huu ni mji wenye mitego ya kila aina, unavishawishi vya hapa na pale ambavyo usipokuwa navyo makini utajikuta unaishia huko huko. Hivyo basi unachotakiwa kufanya ni kuwa makini, acha tamaa ya wanawake. Usikatae chakula wala kinywaji haijalishi vyakula hivyo ni vya aina gani, aidha vinywaji hivyo ni vyaina gani. We kula, we kunywa tu ili usije ukaonekana tofauti sana na watu wa kule. Ni hayo tu mengine utayajulia huko kwani inavyosemekana ule mji kila baada ya miaka miwili hubadilishwa tamaduni ya namna ya kuishi... "
"Asante sana babu, hakika sitokuangusha. Nitafika kwenye ngome nitafanya kile kinachotakiwa mpaka pale nitakapo rejea Ulimwenguni. Ila muhimu tu. Utunze mwili wang."
Mzee Ndelo aliposikia maneno hayo ya Bingo aliachia tabasamu pana kisha akilikunjua koti lile jeusi akamvisha Bingo sambamba na kumkabidhi na upanga. Upanga hatari zaidi.
"Upanga huu ni mahususi kwa kuutumia pindi utakapo kabiliwa na maadui wabaya, najua itakuwa moja ya changamoto kubwa kwako ila pambana usikubali kushindwa kirahisi" Aliongezea kusema mzee Ndelo.
Bingo aliukamata upanga huo kikamilifu, upanga ambao ulionekana kumeremeta vilivyo. Punde mzee Ndelo alinyoosha mkono juu kisha akashusha, ikatokea wingu jeusi la ajabu likamfunika usoni Bingo, baada ya dakika kadhaa wingu hilo lilitoweka usoni mwa Bingo, na hapo alijikuta yupo katika msitu mnene, msitu tulivu pasipo kusikika sauti ya ndege wala mnyama yoyote.
Alishtuka sana Bingo akashindwa sasa aelekee wapi ndani ya msitu ule wa kutisha.
"Ooh Mungu wangu" Akajisemea akianza kwa kushusha pumzi ikiwa muda huo mbele yake aliona watu wanne. Wanaume wenye miili miraba minne. Watu hao walionekana kutisha sana kwa namna walivyoumbika. Kila mmoja alikuwa na masikio makubwa huku macho yao nayo yakishabihiana vyema kabisa na macho ya Simba. Vile vile, kucha zao za vidole zilikuwa ndefu.
Upesi Bingo akarudisha mkono wa kulia nyuma ya mgongo wake akitaka kuchomoa upanga uliokuwa kwenye Kala alilolivaa lakini kabla hajafanya kitendo hicho, ghafla alisikia sauti nzito. Sauti ambayo ilikuwa ikijirudia mara mbili mbili, sauti hiyo ilisema "Bingooo. Kwa hapo ulipo huwezi kukabiliana na hao viumbe tambua hao sio binadamu, hivyo haraka sana kimbia" Aliposikia sauti hiyo alishtuka kisha akainua uso wake kutazama huku na kule.
"Nikimbilie wapi?.."
Kwa woga Bingo aliuliza. Sauti hiyo ya Bingo iliwafanya wale watu kugeuka upende ule aliokuwa amesimama.
Hapo sasa ndipo Bingo alipoogopa zaidi, haraka sana akatimua mbio akipita ndani ya msitu ule huku nyuma wale watu wa ajabu wakimfuata kwa kasi ya kimbunga.
Shughuli ilikuwa pevu kwa kijana Bingo ambaye muda huo yupo katika hali ya nafsi, na kila alipogeuka aliwaona watu wale wakimfuata, hapo sasa purukushani ya maana ikazuka ndani ya msitu huo lakini wale watu baada kukimbia kwa muda mrefu pasipo kufanikiwa hatimaye wakatumia njia ya kuruka kwenye mti mmoja baada ya mwingine mithili ya Kima ilihali Bingo baada kukimbia bila muelekeo hatimaye mbio zake zikaishia ukingoni, mbele alikutana na maporomoko makubwa ya maji huko chini ikionekana miamba mbali mbali ambayo ilimuogopesha. Wakati huo huo wale watu wa ajabu nao walizidi kumfuata kwa hasira
TUNAONA BINGO AMEKUBALI KWENDA MJI WA WAFU. JE, HUKO KUNA MAISHA GANI? NA MASHARTI HAYO ALIYOPEWA ATAWEZA KUYATEKELEZA KAMA ALIVYOAHIDI?
KUFIKA TU AMEANZA KUKUTANA NA MITIHANI.
NA MZEE NDELO ATAWEZA KUULINDA MWILI WA BINGO USIZIKWE?
USIKOSE SEHEMU IJAYO.
Tags:
RIWAYA