TROPEA - Mji wa wafu. SEHEMU YA 05



ILIPOISHIA....... 

Bingo baada kukimbia bila muelekeo hatimaye mbio zake zikaishia ukingoni, mbele alikutana na maporomoko makubwa ya maji huko chini ikionekana miamba mbali mbali ambayo ilimuogopesha. Wakati huo huo wale watu wa ajabu nao walizidi kumfuata kwa hasira. 

ENDELEA NAYO...... 

Bingo alijikuta yupo roho juu, aliutazama ule mporomoko roho ikasita kujitupa lakini alipogeuka nyuma akahofia wale watu na hivyo akapata ujasiri wa kujitosa. Wale watu hawakuweza kubaki kumtazama tu, vile vile nao walijitupa katika mporomoko huo.

Watu hao walipania kumpata Bingo kwa sababu binadamu upande wao ni chakula, tena nyama pendwa kabisa. 

Akiwa na hofu dhofu lihali akaibuka kutoka chini ya maji yaliyokuwa yakishuka kwa kasi, akatema maji yaliyo kuwa kwenye kinywa chake na kisha akaogelea kufuata maji yanako elekea, hatimaye alifanikiwa kufika nchi kavu ambapo alionekana kusafa kwa maumivu huku akiwa ameshika goti wakati huo akihema haraka haraka.  

Lakini wakati yupo katika hali hiyo, ghafla mtu moja aliinuka ndani ya maji. Mtu huyo alipotazama upande ule aliokaa Bingo wakakutana uso kwa uso. Safari hiyo macho ya mtu huyo yalionekana kuwa yenye rangi ya bluu. Bingo alishtuka ilhali mtu huyo akapiga mbizi wakati huo wengine wakizidi kushuka kwenye mporomoko ule. Ujanja huo aliotumia mtu yule aliyezama, Bingo aliushtukia na hivyo akatoka mahali hapo akakimbilia ndani ya msitu mwingine ambao wenyewe ulisheheni viumbe hai. Walikuwemo ndege, wanyama na wadudu pia.

Kwa mwendo wa kawaida alitimuwa mbio akiwakimbia wale watu waliompania, na mara baada kukimbia kwa dakika kadhaa hatimaye aliishiwa nguvu akaanguka chali sambamba na kuhema haraka haraka wakati huo nyuma yake vikisikika vishindo vikisogea mahali alipoangukia, dhahir shahir Bingo alijua ni wale wale watu. Hivyo hofu ilizidi kumjaa jambo ambalo lilimpelekea kupata nguvu za kuendelea na harakati za kuwakimbia watu wale wa ajabu. Punde akaona pango, upesi akajitosa kitendo ambacho kiliwafanya watu wale kupitiliza. 

Hapo alishusha pumzi ndefu, hata asiamini kama kweli watu wale wamepitiliza. Zaidi alipumzika humo humo na punde usingizi ukampitia akalala fofofo, alipozinduka hakujua ni saa ngapi sababu hali ya hewa ya msitu huo ilikuwa tofauti kabisa na hali ya hewa ya kawaida. Muda wote ilikuwa hali ya mawingu, hakuna jua wala mbalamwezi. 

"Inamaana Tropea bado sijafika?.." Kwa mashaka Bingo alijiuliza mara baada ya kuamka, lakini kabla hajapata jibu la swali lake akashtuka kuona karatasi mbele yake. Karatasi hiyo ilikuwa imetapakaa damu. 

"Bingooooo hiyo ni Ramani, ichukue ili ipate kukuongoza " Wakati Bingo anastaajabu kuona karatasi hiyo akasikika sauti ikimwambia maneno hayo. Sauti ya ajabu nzito iliyo sikika mara mbili mbili. Kamwe Bingo hakuweza kukaidi maneno hayo, pole pole alipeleka mkono wake kuichukuwa karatasi hiyo, akaitwaa mkononi akaifungua kuitazama.  

Akashangaa kuona bado hajafika hata robo ya safari yake, kitendo hicho kilimfanya kutoka mule ndani ya pango kwa kutumia Ramani hiyo akaendelea na safari yake. 

Alipokuwa akitembea, ghafla akaguswa bega. Akasimama kisha akageuka nyuma kumtazama ili ajue nani aliyemgusa lakini hakuona mtu yoyote, hakujali aliendelea na safari yake ndani ya msitu huo mnene huku Ramani ikimuongoza vyema. Aliambaa katika msitu huo, alitembea bila kuchoka, ajabu alikuwa hasikii njaa wala kiu. Ila pindi safari hiyo ilipokuwa imekolea punde si punde akasikia ngurumo ya Simba. Ngurumo nzito iliyo pelekea msitu wote kudondosha majani makavu. 

Hapo Bingo akasimama akachomoa upanga wake kisha akatulia kusikiliza wapi inapotokea sauti hiyo. Punde si punde mbele yake akamuona Simba akimjia kwa kasi ya ajabu. Upesi Bingo naye akatimua mbio kumfuata Simba huyo huku akiwa ameshika kikamilifu upanga wake akiwa amenyanyua, tayari kabisa kukabiliana na mnyama Simba. Alipomkaribia akakunja magoti yake kisha akalaza mwili wake ilihali Simba naye akiwa tayari ameruka kwa niaba ya kumkwaruza kifuani lakini mpango wake ukawa umeenda kinyume na tarajio kwa sababu Bingo alionyesha umahiri wa kumkwepa namna hiyo. Vumbi likatimka, kwa mara nyingine Simba huyo akaunguruma kwa hasira, ikiwa muda huo Bingo akihema haraka haraka. Muda mchache baadaye, Simba huyo akarudia kumfuata Bingo, hivyo hivyo Bingo naye akajiandaa vizuri kumdhibiti lakini kabla hajafanya jambo lolote, ghafla akasikia sauti ikisema "Bingo fanya ulichokifuata" Sasa Bingo aliamua kutimua mbio, lakini bado Simba huyo aliendelea kumkimbiza, purukushani ikazuka ila wakati purukushani hiyo inaendelea punde mshare ukapita nyuma yake ukaenda kumchoma Simba kisha vicheko vikasikika. 

Muda huo huo Bingo akasimama, akageuka kumtazama yule Simba, akashangaa kumuona amechomwa mshare lakini pia akashtuka kusikia vicheko. Walio fanya kitendo hicho ni watu jamii ya wale ambao walikuwa wakimkimbiza Bingo, watu hao walikuwa katika mawindo. Walifurahi sana, wakakusanyika pale alipofia Simba, na mara moja shughuli ya kumuandaa ikanza wakati huo Bingo akishuhudia kwa macho yake akiwa amejificha ili asionekane. 

Shughuli nzima ilipokamilika walimteua mtu mmoja abebe mzigo wa nyama, ni kijana mdogo ndio aliyepewa jukumu hilo. Safari ya kurejea kwenye makazi yao ikaanza, na mahali alipokuwa amejificha Bingo ndipo walipopita. Hivyo Bingo akajikuta amekamatwa na hao watu. 
     
                 ********

Ni katika kijiji kidogo kabisa, watu hao walifika. Na ndipo makazi yao na familia zao. Wake waliwapokea waume zao ilihali watoto nao walishangiria urejeo wa wazee wao lakini kituko na jambo la kushangaza ni baada jamii hiyo yenye watu wa ajabu kumuona Bingo. Watu hao walimzunguka huku wakishangaa kwa namna alivyokuwa, mtu mmoja alimgusa ajabu haraka sana alirudisha mkono nyuma wakati huo akilalama maumivu. Hali hiyo iliwashangaza watu hao, ndipo mmoja alimsogelea ili naye amguse. Hivyo hivyo alisafa na maumivu.

Amri ikatoka, ni sauti kubwa na nzito iliyopenya vyema kwenye masikio ya Bingo ingawa hakujua watu hao wanaongea lugha gani zaidi ya kuona watu wanasambaratika akajikuta yupo pake yake katikati ya uwanja. Muda mchache baadaye akamuona Ajuza akijikongoja kuja mahali aliposimama, na kabla hajamkaribia akamuuliza Bingo jina

"Unaitwa nani?.." 

"Naitwa Bingo.." 

"Nani aliyekuleta huku wakati hustahili kukanyaga mahali hapa? Je, ukijitazama ulivyo, unaendana na sisi?.." Alirudia kuhoji Ajuza huyo kwa lugha ambayo Bingo alielewa, ni Ajuza ambaye alionekana kuzeeka sana huku ngozi yake ikiwa mfano wa gamba la nyoka, macho yake nayo yakishabihiana mno na macho ya Simba.  

"Hapo ndipo utaweza kujihami kwa kutumia panga lako" Wakati Bingo anatafakari jibu la kumrudishia Ajuza huyo, mara ghafla akasikia sauti ikimwambia maneno hayo. Hapo Bingo akajua kuna balaa linatarajia kutokea muda wowote, hivyo akawa kamili gado kwa jambo lolote lile. Wakati akijiamini kwa jambo hilo, muda huo huo Ajuza aliyekuwa akimuhoji maswali alitoweka, kufumba na kufumbua akajikuta yupo sehemu tofauti kabisa. Nje ya jengo kubwa, juu ya jengo hilo akaona ubao ulio andikwa SPIRITUAL PRISON (JELA LA KIROHO) 

"Mmmh! Kwani hapa wapi ?.." Alijiuliza Bingo baada kuliona jengo hilo. Lakini kabla hajapata jibu, mlango mkubwa wa jengo hilo ukafunguliwa, nguvu ya ajabu ikamvuta mpaka ndani kisha mlango ukajifunga. Humo ndani Bingo alipata kuona ulingo mkubwa wakati huo watu wakipigana, sio watu wakawaida sababu walionekana kutumia nguvu za kichawi. 

"Hapo Bingo unatakiwa kuwa makini, chini ya ulingo kuna mikuki yenye sumu kali, chunga usidondokee huko lakini pia vile vile mtu utakaye pigana naye hakikisha asikuguse hata kidogo, miili ya watu hawa inasumu kama ilivyo mikuki hiyo. Tambua hiyo ni hatua ya kwanza, bado unasafari ndefu ya kufika Tropea" 

Pindi Bingo amepigwa na bumbuwazi kwa kile alicho kiona ndani ya jengo hilo, akasikia sauti hiyo ikimuasa. Ni sauti ambayo ilimfanya Bingo kushusha pumzi ndefu wakati huo akijiandaa kuchukuwa upanga wake ili akabiliane na mtu atakaye tunukiwa cha ajabu upanga haukuwepo. 

Bingo akashtuka baada kujikuta hana upanga wake, hofu ikamjaa akawaza ni namna gani ataweza kulimudu pambano pasipokuwa na upanga wake. Na wakati yupo katika hali hiyo ya hofu, kule ndani ya ulingo ule uliozungushiwa nyavu za chuma ilihali chini ya ulingo huo pakiwa na utitiri wa simba na chui pasipo kusahau mikuki yenye sumu, mpambano ulikuwa ukiendelea kwa wale watu wa ajabu.

Wote kwa pamoja walikuwa wakitumia panga za kichawi ambazo zilipambwa na nembo mbali mbali za mafuvu. Bingo alishusha pumzi ndefu, bado hofu dhofu lihali ilizidi kutawala moyo wake lakini mwishowe akainamisha uso wake kuzitazama zile ndondi ikiwa moyo wake umesharidhia kukabiliana na changamoto yoyote ile. Shangwe za hapa na pale ziliripuka, mtu yule ambaye alionekana kuutawala vyema ulingo alishangiriwa kwa nguvu zote.  

"Eeh Mungu nisaidie" Alisema Bingo ndani ya nafsi yake baada kuona pambano hilo ni la kukata na shoka, ajabu maneno hayo aliyojisemea yalipelekea ngumi zilizokuwa zikiendelea kusitishwa mara moja na kisha mkuu wa mapigano hayo alimuamuru mpiga ngoma maalumu aliyekuwa akiruhusu mapigano kutuliza ghasia iliyokuwa imetokea. Ndipo ngoma ikapigwa halafu mkuu huyo akaongea maneno ambayo Bingo hakuweza kuyaelewa zaidi ya kujikuta amekamatwa na watu ambao walikuwa binadamu wa kawaida kama alivyo yeye.

Watu hao walimpeleka kwenye chumba maalumu ambacho kilikuwa bucha kwa sababu chumba hicho kilikuwa na ndoano kubwa za kutundikia nyama vile vile kilitapakaa damu mbali mbali huku baadhi ya viungo vya binadamu vikiwaa vimezagaa kila kona.. Bingo alizidi kuogopa wakati huo huo mtu mmoja kati ya wale waliomfikisha ndani ya chumba hicho alimuuliza "Unajua upo wapi hapa?.." 

"Hapana sijui" Alijibu Bingo kwa sauti ya upole iliyojaa woga ndani yake.

"Ahahahahaha hahaha" Watu hao waliangua vicheko, punde mtu wa pili akaongeza kusema "Hapa haupo Duniani, huu ni utawala mwingine na sio utawala wa kiungu muumba mbingu na nchi.. Hivyo basi unapofika maeneo haya hustahili kabisa kumtaja Mungu wako.." 

"Kwanza umefuata nini huku?.." Mtu wa tatu alihoji ilihali muda huo kijana Bingo akionekana kuwa na sitofahamu fahamu juu ya mambo hayo yanayomkabili. 

"Hapa nimepita tu, safari yangu mimi ni kuelekea Tropea.." Alisema Bingo. 

"Tropea?.." Mtu wa nne alitaharuki. 
Kwa kujiamini kabisa Bingo akajibu "Naam!.." Jibu hilo la Bingo liliwafanya wale watu wanne kutazamana wakakonyezana kisha mmoja wao akaongeza kusema. 
"Safari bado unayo ndefu kijana, lakini kutokana na kuvunja taratibu za himaya hii nafikiri safari yako imekomea hapa.." Maneno hayo yalimshtua Bingo, ghafla kijasho chembamba kikaaza kumtoka lakini muda mchache baadaye akauliza. 

"Kwanini sasa ndugu zangu?.." 

"Ukiwa huku hutakiwi kumtaja Mungu, nadhani uliona namna mkuu alivyositisha mapigano sababu yako wewe lakini pia mbali na hilo, umetia hasara baadhi ya rasilimali za huku, kuna baadhi ya vitu vimeteketea kwa moto vile vile umesababisha maafa makubwa..na ndio maana umeletwa katika chumba hiki cha mateso. Utakatwa kiungo kimoja kimoja mpaka unakufa."

"Hapana msinifanyie hivyo, nyinyi ni binadamu wenzangu.. Tafadhalini nisaidieni jamani nipo chini ya miguu yenu " Aliomba msahamaha Bingo sambamba na kupiga magoti chini akiomba msaada kwa watu hao ambao aliona wanaweza kumsaidia juu ya kile alichokosea. 

Watu hao walicheka kwa mara nyingine tena kisha mtu wa pili akamwambia "Usajili lakini utatakiwa kufanya kile tunacho kitaka. Je, upo tayari?.. "

" Ndio nipo tayari ". 

"Ahahah hahaha hahahaha. Vizuri sana kijana, tulikuja na mtu wetu kwa niaba ya kupigania pesa katika kitongoji hiki lakini mtu wetu kauliwa, kwahiyo basi wewe itabidi ushike nafasi yake ili turudi Duniani na mali za kutosha kama yalivyokuwa malengo yetu. Ila chunga sana usirudie kosa.." Aliambiwa hivyo Bingo, naye akashusha pumzi ndefu akasimama akanyoosha mkono kuwapa shukrani watu hao lakini ajabu hao watu walikataa na mmoja akamwambia "Haturuhusiwi kushikana mikono, nyota zetu zipo katikati ya viganja vyetu "

" Sawa naitwa Bingo.." Alisema Bingo.. 

"Vizuri sana karibu ujumuike nasi.. "

                       ********
Bingo akaepuka kifo cha kikatili baada kapata nafasi ya kuungana na wale watu ambao walikuwa binadamu wenzake, lakini moyoni bado alikuwa na hofu sababu alijiuliza atapigana vipi kwenye ulingo hali ya kuwa upanga wake umepotea kimaajabu. 

Na vile vile jambo lingine ambalo lilimpa hofu na kujikuta akiwa na wingi wa woga ni baada kuambiwa kwamba afanye kile watakacho kitaka, hakuwa na namna aliambatana nao, wakatoka ndani ya chumba kile ambacho kilionyesha kweli kweli ni chumba cha mateso, tena mateso yenyewe sio ya kawaida. Ni mateso ya kukatwa viungo mbali mbali vya mwili. 

Waliambatana moja kwa moja mpaka kwenye chumba kingine ambacho huko napo palikuwa na watu wengine, binadamu wa kawaida. Bingo alijikuta akitabasamu wakati huo huo watu hao walimkaribisha kwa bashasha huku kila mmoja akijitambulisha jina lake. 
"Mimi jina langu Bingo" Alisema Bingo baada watu hao kumaliza kujitambulisha kwake. 

Hatimaye siku ile ambayo Bingo anatakiwa kupigana ikawaidia, mashabiki wengi waliujaza ukumbi ule wenye ulingo wa kutisha. Ndondi za ufunguzi ziliendela mahala pale, watu hao ambao hawakuwa binadamu wa kawaida walichapana kama hawana akili vizuri. 

Na pambano lilipoonekana kupamba ubabe na ubishi wa hapa na pale, Bingo alijikuta akiwa roho juu akihofia uhai wake akilinganisha na hali tete aliyomuacha nayo mama yake duniani. Punde ngoma nzito ilipigwa, mpambano wa ufunguzi ukamalizika na hivyo nafasi ifuatayo ni kwaniaba ya Bingo na mpiganaji mwingine ambaye hakumfahamu. Kwa mara nyingine tena ngoma hiyo ilipigwa, ndipo shangwe ziliporipuka, muda mfupi baadaye akajitokeza Jitu kubwa lenye miraba minne, macho ya Jitu hilo yalishabihiana vyema na macho ya Simba huku baadhi ya sehemu ya mwili wake akiwa na magamba ya nyoka.

"Ahahaha hahaha ha!.." Jitu hilo lilicheka, kicheko ambacho kilizua tetemeko fulani, na kila lilipopiga hatua kishindo kizito kilisikika, lilipofika katikati ya ulingo lilinyanyua mkono wake juu, ghafla katika kiganja chake ukatokea upanga mkubwa wenye nembo za ajabu ajabu. Na sasa likasimama kidete kumsubiri mtu anayepigana naye siku hiyo.

"Bingo.." Mtu mmoja ambaye ni binadamu, alimuita Bingo. Bingo akaacha kulitazama Jitu lile la kutisha akamgeukia mtu yule aliyemuita. 
"Kazi kwako sasa..." Mtu yule aliyepasa sauti kumuita aliongea. 

"Unamanisha nikapigane naye?.." Alihoji Bingo kwa taharuki kubwa. 

"Ndio. Na sio kupigana naye tu, bali unatakiwa kushinda ili safari yako ya kwenda Tropea iweze kuendelea.." Alijibiwa Bingo, maneno ambayo yalimshangaza wakati huo akijiuliza atakabiliana vipi na Jitu hilo kubwa la ajabu hali ya kuwa hana silaha yake! 

JE, BINGO ATAFUA DAFU? TUNGOJE SEHEMU IJAYO.. TUMUOMBEE BINGO WETU SABABU BADO ANASAFARI NDEFU SANA. 

Post a Comment

Previous Post Next Post