PENZI LISILO SAHAULIKA 05---06❤


   ZANZIBAR 

"Ben ni rafiki yangu tumemaliza nae chuo na tumekuwa tukisaidiana na kushirikiana katika mambo mengi sana na ndio maana baada ya Mimi kusikia amepatwa na hii dhoruba nikaona ni bora nije nimsaidie". Aliongea Adera."Sawa tutamtoa ila siku nyingine mwambie aache kabisa tabia za wizi bali ajitume katika kufanya kazi kwa bidii". Aliongea afande na muda huo huo akamuagiza yule Afande mwingine aende akamlete Ben ndani ya kile chumba kilichokuwa kimegubikwa na giza.Baada ya yule Afande kuelekea humo zilipita dakika kama tano hivi akawa amekuja mbele ya yule mkuu wake akiwa amemshikilia Ben.Sasa Adera alipoyaangaza tu macho yake na kumuona Ben,mapigo ya moyo wake yalianza kuongezeka maradufu ikabakia kidogo tu ashindwe kujizuia ila akajikaza ili asije kuumbuka mbele ya wale maafande na kuifichua Siri aliyokuwa ameificha moyoni mwake."Nipe namba ya M-PESA Afande hiyo pesa niitume muda huu huu".Alisema Adera na kumfanya Afande yule mwenye kitambi aanze kutumbua macho kana kwamba haelewi chochote kutoka kwa binti huyo mrembo."Una...una... Unasema?" Aliuliza kwa sauti ya kigugumizi."Nipe namba ya M-PESA mnayoitumia Officially ili niwatumie hiyo pesa muda huu huu". Alijibu Adera kwa sauti ya juu kidogo huku macho yake mawili yakiwa yanamtazama Ben,kwa muda huo tayari mishale ya saa mbili ilikuwa imeshaingia ila hilo Adera akilini mwake wala halikumpa shida maana moyo wake ulikuwa umeshafarijika vya kutosha tu baada ya kumuona Ben .Afande alimpa ile namba na muda huo huo bila kupepesa macho Adera aliituma ile pesa wakawa wamemalizana."Adera ila huyo siyo mpenzi wako kweli ?" Aliuliza Afande kitambi huku akimkazia macho kijana Ben."Afande si nimeshakwambia kwamba huyu ni rafiki yangu ina maana hukunielewa?". Aliuliza Adera muda huo huo akimsogelea Ben ."Sawa nimekuelewa".Baada ya Afande kumjibu tu,hapo hapo Adera akamshika mkono Ben wakawa wanaondoka pale kituoni.....walipoziacha hatua tatu mbele mara Afande akamuita Adera ."Adera sitaki huyo kijana awe mpenzi wako Sawa?" Aliuliza Afande kwa sauti asiyoitarajia na kwa matamko asiyoyatarajia lakini Adera akampa ishara ya mkono na kuendelea kuzipiga hatua na Ben wake,walinyoosha kushoto baadae kulia kisha wakafika sehemu yenye mwangaza wakasimama hapo."Ben pole sana Kaka yangu ,Hawajakuumiza kweli wale?" Aliuliza Adera huku akimshika begani Ben aliyekuwa amevaa shati lililotoboka begani hapo hapo."Hapana hawajanifanya chochote sema tu mpaka hapa nilipo bado sijajua kosa langu lilikuwa ni lipi mpaka wakanikamata ila yote kwa yote dada Adera ubarikiwe kwa wema wako dada angu maana umeonyesha moyo wa kipekee sana sijawahi ona tangu nizaliwe". Aliongea Ben kwa sauti ya huruma sana sauti ambayo iliweza kumsisimua Adera na kumsababisha chozi lianze kumtoka machoni mwake,kwa vile Ben hakuwa akimuangalia kwa makini usoni zaidi ya kumuangalia kwa lasha lasha hilo hakuweza kulitambua hata kidogo.Kwa kuzuga ili Ben asigundue ,Adera alinyooosha mkono wake wa kushoto akaupandisha kichwani mwake akawa anajifanya kama anajikuna baadae kufumba na kufumbua yale machozi akayafuta fasta ,sasa pamoja na kwamba alifanya hivyo ila tayari Ben alikuwa ameshamgundua."Adera mbona naona kama unalia au macho yako yanauma?" Aliuliza Ben."Akaa!! Mi silii Ben". Aliongea Adera kwa sauti ya kudeka."Ben tuendelee kutembea sasa".Alisema Adera wakaondoka pale wakawa wanatembea haraka haraka,,,dakika kumi na tano baadae wakafika hadi nyumbani kule alipokuwa akiishi Ben."Usiku mwema Kaka yangu Ben,ila kama hautojali naomba unisaidie namba yako ya simu na itapendeza zaidi iwapo utanipa ile yenye WhatsApp si unatumia WhatsApp Kaka Ben?" Aliongea Adera huku akiinyonga nyonga shingo yake na wakati mwingine kuving'ata ng'ata vidole vyake."Ndio WhatsApp natumia dada angu,namba yangu ni 0756411314 hiyo ndiyo namba yangu ".Alimtajia Adera nae akaiandika na kisha kuisave vizuri."Haya Ben Usiku mwema na Mungu akulinde na akupe njonzi njema uote ndoto njema Kaka angu kipenzi". Aliongea Adera baadae wakaagana Adera akawa anaondoka ,alianza kutembea huku akigeuka geuka kumtazama Ben ambaye nae alikuwa akimtazama.Adera alitokea kumpenda sana kijana huyo na alitamani awe mume wake kabisa ila hakujua ataanza vipi kumueleza Ben kwamba anampenda maana Ben mwenyewe mbali na kwamba alikuwa ni kijana mcheshi lakini pia alikuwa kijana mwenye heshima zake na msimamo wake,,,Adera alikuwa akimchukulia kama dada yake na ndani ya moyo wake wala hakuwa akimtamani binti huyo pamoja na urembo wake....kitu pekee alikuwa akimheshimu sana Adera na hakuwaza hata siku moja kuja kumtongoza au kumtamkia neno lolote lile linalohusiana na mapenzi.Sasa hicho ndicho kilichokuwa kikimuumiza sana Adera na kumfanya awe anawaza hata visivyowazika ili mradi tu Ben awe wake wa kufa na kuzikana.

  Upande mwingine alionekana mama Adera akiwa amemkaba shingoni yule mlinzi wake wa getini huku akimfokea sana na wakati mwingine kumzaba zaba vibao vya usoni na alikuwa akihema kwa hasira mithili ya mtu anayetaka kupasuka."We mbwa....mbwa koko wewe nikikuachia hapa naomba nisikuone ukiendelea kuning'iniza kengere zako mbwa we,nilikuambia nini na umefanya nini??".Kwa hasira mama Adera aliyaongea hayo."Mimi sina kosa mama utanionea bure tu,binti yako haya yote nilimuambia ila kwa kiburi chake hakunielewa kabisa,sasa kama umeamua hivyo Sawa mimi nipo tayari". Aliongea mlinzi kwa sauti ya kutetemeka."Mpumbavu mkubwa wewe,jibaba zima ushindwe na yule binti? Au wewe ndo umemtanguliza gesti mwanangu ili Usiku wa manane ukazini nae eti ,sasa siyo tu nitakufukuza kazi na kukuacha uende salama bali nitajua cha kufanya". Aliongea mama Adera na hapo hapo akamuachia yule mlinzi na yeye akawa ameelekea ndani haraka ,sasa alipotoka humo tayari alikuwa ameficha bastora ndani ya kanga yake akawa anamsogelea mlinzi yule."Simama,geuka nyuma kama ulivyo kisha nenda sikutaki humu ndani".Alisema mama Adera na mlinzi akawa amesimama....Sasa alipogeuka tu nyuma,kabla hata hajaanza kutembea mama Adera aliichomoa haraka bastora yake akamfyatulia risasi tano za kisogoni mlinzi,damu iliyochanganyikana na ubongo ikaruka hewani mlinzi akakoroma mara Moja tu akadondoka mazima chini na kupoteza maisha hapo hapo.Jimmy sauti ya mlio wa zile risasi aliisikia na akawa anatimua mbio kuja pale getini akitokea ndani ya jumba lile."Mama....mama!! Nini hikiiii!!!!! Ina maana umeuwa siyooo??" Aliuliza Jimmy mfanyakazi huyo wa ndani huku akiwa amepaniki."Ndio nimemuua na kwa hili naomba unyamaze kimya usimuambie mtu yeyote yule,endapo utashindwa kufanya hivyo kaa ukijua hata wewe kaburi litakuita,haya tokaa hapaaa".Jimmy alifukuzwa kama mbwa nae kwa kuyahofia maisha yake aliondoka pale huku akiwa amejawa na uwoga wa hali ya juu,,Baada ya Jimmy kuondoka ,mama yule mwenye roho ya kigaidi aliusogelea mwili wa marehemu mlinzi akawa anauvuta pembeni.....baada ya kuhakikisha ameusogeza pazuri aliifuata gari yake ya wazi aina ya Toyota akapanda ndani ya gari hiyo akaiwasha na kuisogeza ubavuni mwa ule mwili .Haraka haraka alishuka humo akaubeba mwili ule ndani ya gari kisha nae akapanda na kuiondoa fasta kwenda kuutupilia mbali.

********************

Dakika chache baada ya mama Adera kuondoka....Adera alifika pale getini na akashangaa sana kuuukuta mlango wa geti lile ukiwa wazi,aliangaza kulia kisha kushoto akaona hakuna mtu.Moja kwa Moja akaingia ndani na kuanza kuita "We mlinzi....mlinzi..... mlinzi weee!!" Aliita lakini akawa anapokelewa na mwangwi tu wa sauti yake,sasa akiwa anatembea kwa mwendo wa taratibu mara alijikuta akishtuka sana baada ya kuona damu ikiwa imetapakaa mbele yake.Macho ya uwoga yalimtoka ."Mamaaaaaa!! Mamaaaaaa!!" Adera alianza kupiga mayowe huku akikimbilia ndani ya jumba lao,,,Baada ya kufika tu humo alindondoka chini akawa amepoteza fahamu.Alikuja kuzinduka na kumkuta mama yake amekaa karibu nae huku akiwa amekunja ndita usoni."Adera naomba unijibu maswali mawili tu...moja ulikuwa wapi na pili ulikuwa kwa nani hadi muda huu !!" Aliongea mama yake huku akiwa hana utani kabisa."Nilikuwa kwa rafiki yangu" alijibu Adera kwa jibu la mkato huku akiwa hamtazami kabisa mama yake."Ulikuwa kwa rafiki yako? We binti naona sasa umeshaanza kuwa jeuri,kwa akili yako finyu unadhani huo ni uwongo wa kunidanganya mimi bi Marry? Wewe umeshaanza kuwa changudoa...Sasa nitakunyoosha na utanyooka,,Unadhani ni nani aliyesababisha hadi baba yako afe!!! Nadhani jibu utalipata baadae ". Aliongea mama Adera kisha akasimama juu,,macho yalimtoka Adera akawa anatetemeka na kutokwa na jasho mwili mzima.

INAENDELEA.............? 

           SEHEMU YA 6.

          Adera hakuamini kabisa baada ya kuyasikia maneno kama yale kutoka kinywani mwa mama yake,hakutarajia kama mamaye angepata ujasiri wa kuongea vile tena mbele yake bila ya uwoga wowote ule.Tangu marehemu baba yake afariki dunia yapata miaka kumi sasa hakujua baba yake alifariki kwa ugonjwa gani.....Kila akijaribu kukumbukia kifo cha baba yake tena mbele ya macho yake hapo alianza kuelewa picha halisi,,hii ilitokana na kwamba babaye hakufa kifo cha kawaida."Mama ina maana kumbe wewe ndiye uliyemuua babaa?" Aliuliza Adera huku machozi yakianza kumlenga lenga."Unauliza jibu,nasema unauliza jibuu?? Huo ndio ukweli maana Mimi huwa sipendagi ujinga.Labda nikuambie tu ukweli,baba yako nilimuua mimi mwenyewe baada ya kumuona anatabia za kipumbavu zisizofundishika ,baba yako alikuwa na nyodo sana harafu alikuwa akijiona yeye ndiye yeye wengine mapaka!! Sasa kutokunisikiliza kwake na kujiona yeye ndo kichwa niliapa kumkomesha ,na nikamkomesha kweli maana sumu ya panya niliyomlisha kwenye chakula ilitosha kabisa kumpeleka kaburini". Aliongea mama yake kwa kujiamini sana."Mama kumbe wewe ni kama shetani!! Ulimuua babaa??" Adera alishindwa kujizuia akawa analia kabisa ."Tena haya niliyokuambia naomba uyaache hapa hapa,siku ukijichanganya ukamwambia mtu yeyote yule haki ya nani nitakuuwa".Alipoyazungumza hayo,Adera alinyanyuka kwa hasira akaelekea chumbani kwake kwenda kulala maana kichwa chake kilikuwa kimeshavurugwa....Usiku huo hata hamu ya kula ilikatika akawa anawaza namna ya kufanya ili mama yake ayalipe aliyoyafanya.Tukiachana na hayo turudi kwa Steve.......Usiku ule ule Steve kwa upande wake aliwakusanya vijana wake wote akaandaa gari mbili ambazo walizitumia kwenda hadi nyumbani kwa Afande Kitambi kufuata pesa.Safari yao haikuchukua muda sana kwani walitumia kama dakika kumi tu wakawa wamefika huko na kumkuta Afande akimalizia kushuka ndani ya gari yake maana nae kwa muda huo ndo alikuwa akitoka kazini,Steve bila kupoteza muda alishuka ndani ya gari na vijana wake wakasimama kwa kupanga mstari mmoja."Steve mbona umekuja hapa mida kama hii kuna nini?" Aliuliza Afande baada ya kusimama mbele ya gari yake."Jemedari hachagui muda wa kuingia vitani....by the way hapa hatujaja kukaa sana,vipi ule mzigo yule msenge aliutoa!! Maana nimesikia tayari mmeshamuachia na yupo uraiani". Aliongea Steve huku akimtazama Afande kwa macho makali."Ule mzigo ninao ila sasa kwa namna ambavyo ulipatikana mpaka hapa siamini kabisa". Aliongea Afande."Huamini nini Afande ina maana Ben hizo pesa alizipata kwa njia za kimiujiza au?" Aliuliza Steve."Hapana si kwamba alizipata kwa njia za kimiujiza bali yule aliyezitoa sikutarajia kabisa kama angeweza kufanya hivyo". Aliongea Afande Kitambi huku akijikuna kichwani."Ni nani huyo ambaye alizitoa hizo pesa mpaka Ben akafunguliwa?" Aliuliza Steve."Ni binti mmoja kutoka familia ya marehemu mfanyabiashara Mr Gambo anaitwa Adera,,,pale alikuja huku akionekana kama amechanganyikiwa sana akazitoa pesa hizo muda huo huo". Aliongea Afande."What?? What?? Adera huyu ninaye mfahamu au ni Adera mwingine?" Aliuliza Mr Steve."Ndo huyo huyo".Alijibu Afande."Okey Afande niachie mimi hilo jambo maana Mimi siwezi kuona au kushuhudia kwa macho yangu ,Adera akienda na Ben,,,Adera lazima awe wangu kivyovyote vile". Aliongea Steve."Usifanye hivyo Mr Steve....Usifanye hivyooo!! Yule binti pamoja na kufanya hivyo alisema Ben si mpenzi wake bali ni rafiki yake tu wa kawaida na walisoma wote na kumaliza wote chuo". Aliongea Afande."Chuo? Ben ni lini alimaliza chuo wakati fomu four tu alipata bonge la sifuri....Afande huo ni uwongo,Ben namfahamu vilivyo!! Huo ni uwongo Hawa wanayao.Sasa tusipoteze muda sana hizo pesa naziomba zote isibakie hata senti moja,hilo la Ben niachie mimi soon nitalimaliza".Baada ya Steve kuyazungumza hayo Afande alimkabidhi zile pesa na kisha wakaagana ,Steve na vijana wake wakaondoka na kurejea tena kwenye ngome yao.

Baada ya kufika ngomeni hawakuwa na cha kupoteza kabisa,,,Walisimama nje ya ngome hiyo kisha Steve akamshika bega kijana wake gaidi mmoja hivi aliyekuwa akimuamini sana."Mr Mluto nadhani hapa picha ndo linaanza sasa na mshindi lazima apatikane,sasa hapa cha kufanya ni hiki....hizi milioni kumi tulizozifuata kwa Afande Kitambi tunazichange angani kwa namna hii,tutazipeleka kwa Mr Ben na tutampa ili ziwe mtego usioteguka.Mr Mluto hii kazi nakupa wewe,kesho mapema sana utazipeleka pesa hizo kwa Mr Ben". Aliongea Steve kisha wakatoka pale na kurejea tena ndani ya ngome yao kwa ajili ya kuusindikiza Usiku huo.Masaa ya Usiku yalianza kuyoyoma mithili ya maji yaliyo ndani ya mkondo wake hatimaye kukapambazuka.Asubuhi na mapema baada ya kupambazuka,Mr Mluto akiwa rafu na appearance ya kijambazi alivaa koti refu jeusi na viatu vikubwa akachukua zile pesa akaondoka ngomeni na kwenda moja kwa moja hadi kibandani kwa Mr Ben.

**************

Alifika huko akamkuta Ben akimalizia kutoa mizigo yake kutoka ndani ya jengo moja liliokuwa kunako upande wa kulia,Kimya kimya Mluto alifika akasimama mbele ya kibanda cha Ben.....alisimama hapo kwa dakika kadhaa kisha akajikohoza."Habari za asubuhi Mr Ben?" Alisalimia Gaidi Mluto huku akimkazia macho."Safi tu,kwema?" Aliitikia Ben nae akamsabahi."Aisee tuna mshukuru Maulana maana tumeamka salama.Sasa Mr Ben hapa sijaja kukaa sana,nimekuja kwa ajili ya jambo moja tu". Aliongea Gaidi Mluto huku akimsogelea zaidi Ben na kisha wakaenda kukaa juu ya benchi moja hivi lililokuwepo ndani ya kibanda chake."Mr Ben mimi kwa jina naitwa Mr Mluto ni jamaa wa karibu sana na rafiki yako Mr Steve,sasa amenituma nikuletee huu mzigo".Alisema Gaidi Mluto huku akichomoa Rambo moja iliyokuwa imetuna vya kutosha."Mr Ben kwa kutambua umhimu wako katika maisha yake,Mr Steve ameamua kukupa kiasi cha shilingi milioni kumi ili angarau ziweze kukusaidia katika masuala yako ya kibiashara,,, Tafadhari zipokee". Aliongea Gaidi Mluto huku akimkabidhi Ben mzigo ule,kwa muda huo Ben Meno yake thelasini na mbili yalikuwa nje bila ya kujua ni kipi kitakuja kumtokea hapo mbeleni,mwenyewe alijua ni upendo tu kutoka kwa rafiki yake Steve kumbe siyo."Sijui nisemeje tu maana kwa furaha hii niliyonayo nimeishiwa maneno kabisa.Naomba umpelekee shukurani zangu za dhati Mr Steve na Mungu ambariki kwa wema wake maana Mimi sina cha kumpa".Wakati anayaongea hayo Ben,Kwa muda huo Gaidi Mluto alikuwa ameshasimama na hakuongea chochote zaidi ya kutikisa kichwa chake na kuondoka.Gaidi Mluto alitembea haraka kama umbali wa mita kumi na tano akasimama na kuanza kumtazama Ben kwa dakika kadhaa,jamaa akajishika puani na kuondoka zake.

Muda mchache tu baada ya kuondoka Gaidi Mluto kwa mbali alionekana Adera akija huku akiving'ata ng'ata vidole vyake,alitembea taratibu mpaka akakifikia kibanda cha Ben."Adera karibuu!!" Aliongea Ben."Asante Kaka Ben nimeshakaribia tayari".Adera aliongea huku akijipenyeza ili aingia hadi ndani ya kibanda."Vipi leo nikuwekee kilo ngapi za mchele dada angu?" Aliuliza Ben."Hapana Ben leo wala sijaja kununua mchele bali leo nimekuja tu kukusalimia na kupiga story za hapa na pale na wewe " Aliongea Adera kwa sauti ya upole."Kumbe!! Haina shida dada angu".Adera na Ben walikaa kwenye lile benchi wakawa wanapiga story."Yaani Ben mimi huwa nafarijika sana kupiga story na wewe ,yaani natamani hata masaa yasiende haraka ili tu niendelee kuinjoy....Kaka Ben unaweza kuniruhusu leo nije nipike nyumbani kwako?" Aliuliza Adera huku akimtazama Ben kwa macho yaliyolegea sana."Sasa dada Adera utaweza kweli?" Aliuliza Ben."Niamini Ben nitaweza maana nitafurahi sana endapo nitaruhusiwa na wewe kukupikia chakula hicho". Aliongea Adera."Sawa mimi nimekubali.....ila.? Kabla hajamalizia sentensi yake mara nyuma ya kibanda kukasikika sauti ya kikohozi.

ITAENDELEA................................... 

Post a Comment

Previous Post Next Post